read

6. Mwana Wa Hatim

Kabla kuja kwa Uislamu, waarabu walikuwa na viongozi huru wa kikabila. Watu walikuwa wamezoea utawala wa machifu wao na walikuwa wakiwatii; na kila wakati wakiwalipa ushuru na kodi. Hatim, aliyekuwa mkarimu na mashuhuri kutoka kabila la Tai alikuwa mmoja wa machifu wa kiarabu. Mwanawe ‘Adi alimrithi baba yake baada ya kufariki kwake na kabila lake lilikubali uongozi wake. Alikuwa akiwatoza ushuru kwa kiwango cha robo ya mapato yao kila mwaka.

Uongozi wake ulitukia sawia na zama za Mtume (s.a.w.w). Kabila la Tai lilikuwa likiabudu masanamu, lakini Adi mwenyewe alikuwa mkristo na aliwaficha watu wake dini yake. Watu hao baada ya kuyafahamu mafunzo bora ya kiislamu, walipata faraja ya kuondolewa katika mzigo wa viongozi wao ambao mpaka wakati huo walikuwa wamelazimisha utawala wao juu ya watu.

Kutokana na jambo hili, Adi kama viongozi wengine alikuwa akiutazama Uislamu kama tishio kubwa kwake na alikuwa akificha uadui kwa Mtume (s.a.w.w) lakini uamuzi ulikuwa umeshapita. Watu walikuwa wakiingia katika Uislamu makundi makundi na dini ya Mwenyezi Mungu ilikuwa ikienda mbele siku baada ya siku. Alijua kwamba siku inakuja ambapo Waislamu watakuja kumtafuta yeye pia, na huo ndio utakuwa mwisho wa uongozi wake. Kwa hivyo alimwamrisha mfanyakazi wake maalum, ambaye ni mtumwa, kila siku kuwaweka tayari ngamia wenye nguvu na mbio karibu na kambi yake na kuwa macho.

Siku moja yule mtumwa wake alimjia na kusema “Fanya kila maandalizi unayotaka kufanya kwa sababu waislamu wako karibu sana.” Adi alipandisha familia yake kwenye ngamia na kuchukua vitu vilivyo kuwa na thamani na mzigo ambao angeweza kubeba na kutoroka kwenda Damascus, ambako watu walikuwa wa dini yake. Lakini katika kuchanganyikiwa huko alisahau kumchukua dada yake Saffana pamoja naye na akaachwa huko nyuma.

Waislamu waliwashinda kabila hilo kwenye vita; na baadhi yao wakachukuliwa mateka. Waislamu walimchukua Saffana na mateka wengine na kuwapeleka Madina na kumuelezea Mtume (s.a.w.w) kuhusu kutoroka kwa Adi.

Wafungwa walipewa makao katika kambi yenye ukuta mfupi karibu na msikiti. Siku moja Mtume (s.a.w.w) alipokuwa akienda msikitini alipitia karibu na sehemu ile ya wafungwa. Saffana aliyekuwa mwenye akili na mzungumzaji aliinuka kutoka mahali pake na kusema;

“Baba yangu amefariki na mlezi wangu amejificha, kuwa mkarimu kwangu na Mungu atakuwa mwema kwako!!’’

Mtume (s.a.w.w): “Ni nani mlezi wako?” Saffana: “Adi mwana wa Hatim.”

Mtume: “Yule ambaye amemtoroka Mwenyezi

Mungu na Mtume wake?”

Alipotamka maneno hayo, Mtume (s.a.w.w) aliondoka zake. Siku iliyofuata, Saffana alirudia maneno yale yale, na akajibiwa sawa kama alivyojibiwa siku iliyopita. Maombi yake hayakuwa na mafanikio. Siku ya tatu alipokuwa amepoteza matumaini aliamua kukaa kimya. Lakini kijana mmoja ambaye alikuwa akitembea nyuma ya Mtume (s.a.w.w) alimuashiria kuwa arudie matakwa yake. Akarudia maneno yale yale. Mtume (s.a.w.w) akasema;

“Sawa kabisa, namsubiri mtu muaminifu kutoka kwenye kabila lako. Punde tu mtu kama huyo atakapopatikana basi nitakutuma wewe pamoja na mtu huyo kwenye kabila lenu. Nijulishe ukipata habari za mtu kama huyo atakapokuja hapa Madina.”

Mwanamke huyo aliwauliza watu, ni nani yule kijana ambaye alikuwa nyuma ya Mtume (s.a.w.w) aliyemhimiza kurudia madai yake. Wakasema, alikuwa Ali.

Baada ya muda mfupi Saffana akamjulisha Mtume (s.a.w.w) kuwa kuna watu wa kabila lake wamekuja Madina. Mtume (s.a.w.w) akampa mavazi mapya na pesa za matumizi njiani na ngamia wa kusafiria. Alifuatana nao moja kwa moja hadi kwa nduguye ambaye alikuwa Syria.

Wakati alipomuona nduguye, alimkemea huku akisema; “Uliwachukua mke na watoto wako na kunisahau mimi kumbukumbu ya baba yako!” Adi alimuomba msamaha. Na kwa vile alikuwa ni mwanamke mwenye hekima, Adi alimuomba ushauri kuhusu mpango wake. Alimuuliza: “Ungenishauri nifanye nini kwa kuwa umemuona Muhammad kwa karibu? Nijiunge naye ama nijitenge?”

“Naamini bora ungejiunga naye. Kama yeye ni Nabii wa Mwenyezi Mungu itakuwa ni nyongeza kwenye heshima na uungwana wako. Na kama yeye sio Mtume, anataka tu kuwa kiongozi wa kidunia, tena kwenye sehemu (Madina), ambapo sio mbali na Yemen, hakuna mtu yeyote atakayethubutu kukuvunjia heshima, kwa sababu ya heshima uliyokuwa nayo kwa watu wa Yemen. Vyovyote itakavyokuwa utahakikishiwa heshi- ma yako.”

Adi alivutiwa na wazo hilo. Akaamua kwenda Madina na kuchunguza mwenendo wa Mtume (s.a.w.w) kwa undani. Kama atakuwa Mtume atamfuata sawa na Waislamu wengine. Lakini ikiwa yeye ni mtu mwenye tamaa za kidunia ya uongozi na mali, basi atashirikiana naye hadi kiasi cha kunufaika wote sawa.

Aliingia msikiti wa Madina na kumsalimia Mtume (s.a.w.w). Mtume (s.a.w.w) akampokea kwa heshima inayostahili na kumkaribisha kwake nyumbani.

Walipokuwa wanaelekea nyumbani mama mmoja aliyesawijika alishika nguo ya Mtume (s.a.w.w) na akaanza mazungumzo naye. Muda mrefu ulipita na Mtume (s.a.w.w) alijibu maswali yake kwa upole na subira.

Adi alijiambia moyoni, “Hii ni ishara moja toka kwenye tabia yake kuonyesha kuwa huyu mtu ni Mtume. Watu wenye matamanio ya kidunia hawana tabia na moyo wa kumjibu mama masikini kwa subira kiasi hiki na upole.”

Walipoingia ndani ya nyumba, Adi alikuta kuwa maisha yake yalikuwa ya chini sana na yasiyo na majivuno. Palikuwa na tandiko la kulalia ambalo pia Mtume alikuwa akilitumia kwa kukalia, lakini sasa analitandika ili Adi akalie. Adi alisisitiza kuwa Mtume (s.a.w.w) alikalie lakini Mtume (s.a.w.w) alikataa. Kisha Adi alikalia lile tandiko na Mtume (s.a.w.w) aliketi chini kwenye sakafu. Adi akajiwazia “Hii ni ishara ya pili ya tabia ya huyu mtu. Hii ni tabia ya Mitume siyo ya wafalme.

Mtume (s.a.w.w) alimgeukia na kumuuliza, “Lakini Ukristo haukuwa dini yako wewe?” Adi alijibu, “ndio, kwa nini?” Mtume (s.a.w.w) akasema “Basi ni kwa nini na kwa misingi gani, ulikuwa ukichukuwa robo ya mapato ya watu wako? Hiyo haikatazwi na dini yako ?”

Adi ambaye alikuwa ameficha dini yake hata kwa watu wake wa karibu, alishangaa kusikia maneno haya kutoka kwa Mtume (s.a.w.w). Akanena moyoni, “Hii ni ishara ya tatu kuwa mtu huyu ni Mtume.

Kisha Mtume (s.a.w.w) alisema “Unaona umasikini na udhaifu wa sasa wa Waislamu. Unaona Waislamu leo wanaishi maisha ya dhiki. Wamezungukwa na makundi ya maadui na hawana usalama wa maisha yao na mali zao. Hawana uwezo mikononi mwao. Wallahi wakati utafika karibuni ambapo utajiri huo mkubwa utawafikia na hakutakuwa na masikini miongoni mwao. Wallahi, maadui wao watashindwa na kutakuwa na amani kiasi cha mwanamke kusafiri kutotaka Iraq hadi Hijaz peke yake bila ya mtu kumsumbua. Wallahi, wakati unakaribia yale makasiri meupe ya Babiloni yatakuwa katika mikono ya Waislamu.’’

Adi aliingia katika Uislamu kwa Imani kamili na uaminifu na alibakia kuwa mwaminifu mpaka mwisho wa maisha yake. Aliendelea kuishi kwa miaka kadhaa baada ya Mtume (s.a.w.w). Alikuwa kila mara akikumbuka mazungumzo yake na Mtume (s.a.w.w) wakati walipokutana kwa mara ya kwanza na vile alivyotabiri wakati ule juu ya hali ya baadaye ya Waislamu. Alikuwa ana mazoea ya kusema “Wallahi katika wakati wa uhai wangu nimewaona Waislamu wakishinda na kuteka makasiri meupe ya Babiloni, na kuna amani na utulivu kiasi cha kumwezesha mwanamke kusafiri kutoka Iraq hadi Hijaz bila mtu kumsumbua. Wallahi naamini siku itafika ambapo hakutakuwa na masikini miongoni mwa Waislamu.