read

7. Ibni Sayyaba

Ibni Sayyaba mkazi wa Kufa alikuwa kijana ambaye baba yake alikuwa amefariki. Msiba wa kifo cha baba yake ukiambatana na umasikini na ukosefu wa kazi ulikuwa unavunja moyo wa mtu mwenye hisia. Siku moja alipokuwa katika nyumba yake alisikia mlango ukibishwa. Alikuwa ni rafiki ya baba yake. Baada ya kumpa pole, alimuuliza,

“Je babako alikuwachia kitu chochote?” “Hapana,” alijibu.

“Basi chukua hizi Dirhamu elfu moja; jaribu kuzifanya kuwa mtaji na faida yake utumie kwa mahitaji yako.

Alipomaliza maneno hayo aliondoka. Kwa furaha aliokuwa nayo Ibni Sayyaba alikwenda kwa mama yake kumuonyesha pesa zile na kumueleza kisa hicho. Siku hiyo hiyo alitumia pesa hizo kununua bidhaa na kufungua duka na kuweka moyo wake hapo. Alifanya maendeleo ya haraka. Muda mfupi baadaye alifahamu kuwa siyo tu aliweza kujimudu kimaisha kutokana na faida bali pia mtaji ulikuwa umeongezeka marudufu. Alifikiria kwenda kuhiji na alimuendea mama yake kwa ushauri. Mama yake alimwambia “Tafadhali, kwanza ungerudisha zile pesa za watu”

Alikwenda kumuona yule rafiki ya baba yake na kumkabidhi zile Dirham elfu moja huku akisema “Tafadhali pokea pesa zako.” Bwana yule alidhani kuwa Ibni Sayyaba anamrejeshea pesa zile zile kwa sababu hazikutosha kufanyia biashara yeyote, kwa hivyo alimwambia: “Kama kiwango hicho cha pesa hakitoshi katika biashara naweza kukiongeza.”

“Mungu wangu mwema, zilitosha. Pesa hizo zimetuletea mafanikio makubwa na kwa kuwa sasa naweza kujimudu vizuri kifedha, nimekuja kurejesha (kulipa) pesa zako, na kukushukuru, haswa wakati ambapo nimeamua kwenda kuhiji.”

Alirudi nyumbani na kufungasha mzigo wake tayari kwa safari ya Makka. Baada ya kutimiza Hija tukufu alielekea Madina na akaenda kumuona

Imam Sadiq (a.s) pamoja na mahujaji wenzake. Kulikuwa na umati mkubwa wa watu katika nyumba ya Imam (a.s). Kwa vile alikuwa mdogo aliamua kuketi mbali mwisho wa umati huo wa watu. Hapo aliwaona watu wakiingia na kutoka; pia alisikia maswali yao yakijibiwa na Imam (a.s). Wakati nyumba ilipokaribia kuwa tupu Imam (a.s) alimuashiria kidole na akasema “Naweza kukusadia vipi?”

“Mimi naitwa Abdul Rahman mwana wa Sayyaba kutoka Kufa (kabila la Bijilli).’’

“Baba yako anaendeleaje?” “Alifariki.”

“Ah! Ah! Mwenyezi Mungu amrehemu, je alikuwachia chochote?” “La, hakuniachia”

“Basi umewezaje kwenda Kuhiji?”

“Baada ya kifo cha baba yangu tulikuwa na shida. Kwa upande mmoja kifo chake na upande mwingine umaskini na ukosefu wa kazi. Yote hayo yalit- ulemea vibaya. Siku moja rafiki ya baba yangu alinipa Dirham elfu moja na kunishauri nifanyie biashara. Nilifuata ushauri wake na kutokana na faida ya hizo pesa ndiyo nimeweza kuja kuhiji.”

Kabla hajamaliza kisa chake Imam (a.s) alisema, “Niambie ulifanya nini kuhusu pesa ya rafiki ya baba yako?” “Nilimrejeshea pesa zake zote kwa mujibu wa ushauri wa mama yangu kabla sijakuja kuhiji.” “Vizuri sana je ungependa nikupe ushauri?”

“Niwe fidia yako; ndio tafadhali”

“Kuwa mkweli na muadilifu. Mtu muaminifu na muadilifu ni mshirika katika utajiri wa wengine.”