read

8. Aqiil Kama Mgeni Wa Ali (A.S.)

Aqiil aliwasili kama mgeni katika Nyumba ya Serikali zama za ukhalifa wa nduguye, Ali (a.s). Ali (a.s.) alimuamrisha mwanae mkubwa, Hasan ampe ami yake vazi. Hasan alimpa joho na kilemba. Usiku ulipofika, hali ya anga ilikuwa ya joto. Walikuwa wameketi juu ya paa la nyumba wak- izungumza kwa furaha. Ulikuwa wakati wa chakula cha jioni. Aqiil alijiona kuwa ni mgeni wa mtawala mkuu kabisa wa ulimwengu wa Waislamu, hivyo alitarajia chakula cha kupendeza cha kitajiri. Lakini kwa mshangao wake kilikuwa ni chakula cha kawaida sana. Akauliza; “Hiki ndicho chakula chote?”

Ali (a.s) alimuuliza, “Je hii sio riziki ya Mwenyezi Mungu? Ndani ya moyo wangu namshukuru Mwenyezi Mungu muumba kwa kunipa riziki hii.”

Aqiil alisema “Basi afadhali nikueleze mahitaji yangu haraka ili niondoke. Ninadaiwa, hivyo basi tafadhali amrisha kulipwa kwa madeni yangu hara- ka iwezekanavyo; pia msaidie nduguyo masikini kadiri ya uwezo wako. Ili nirudi kwangu nikiwa nimeondokewa na mzigo”

“Una deni la kiwango gani? “Dirham elfu mia moja”

“Oh! Dirham elfu mia moja! Kiwango kikubwa sana! Samahani ndugu yangu sina kiwango hicho cha pesa za kukupa; lakini subiri hadi wakati wa kulipa mishahara. Nitatoa katika fungu langu na kukupa, ndio ushirikiano na undugu. Kama familia yangu na watoto hawangekuwa na haja ya matu- mizi yao ningekupa fungu langu lote.”

“Unasema nini?!! Yaani nisubiri hadi utakapolipwa mshahara wako? Hazina ya umma iko mikononi mwako na unaniomba nisubiri hadi utakapopata mshahara ndipo unipe kutokana na fungu lako! Unaweza kutoa kiasi upendacho kutoka kwenye hazina ya umma! Basi mbona unani- taka nisubiri hadi siku hiyo? Hata hivyo, fungu lako ni kiasi gani? Hata kama utanipa fungu lako lote utaniondolea kiwango gani cha shida yangu?”

“Nashangaa kusikia mapendekezo yako. Inatuhusu vipi kati yangu na wewe kama kuna pesa kwenye hazina ya Waislamu au la? Sisi ni kama Waislamu wengine. Kwa kweli, wewe ni ndugu yangu na lazima nikusai- die iwezekanavyo, lakini kutokana na pesa zangu binafsi, siyo katika haz- ina ya umma.”

Mabishano yaliendelea na Aqiil akamuomba na kumsisitizia Ali kwa kila njia. Alisisitiza kuwa Ali ampe kutoka kwenye hazina ya waislamu. Sehemu waliokuwa wameketi waliliona soko la mji wa Kufa na wangeweza kuyaona masanduku ya pesa ya wafanyabiashara. Ali (a.s) alisema; “Kama bado unasisitiza na hauko tayari kunisikiliza, basi nina wazo jingine kwa ajili yako. Ukilifuata utalipa madeni yako yote na utabaki na pesa nyingi!”

“Ni wazo lipi hilo?”

“Pale chini kuna masanduku ya pesa. Pindi tu soko litakapofungwa na kukawa hakuna mtu hapo, nenda na uyavunje hayo masanduku na uchukue chochote utakacho.”

“Ni makasha ya akina nani”

“Ni mali ya watu masikini wa soko hili. Wanahifadhi pesa zao humo.” “Ajabu! Unaniambia niibe pesa za watu masikini ambao wamezipata kwa kazi zao ngumu na wamekwenda nyumbani wakaziwacha hapo kwa kumuamini Mwenyezi Mungu?”

“Basi kwa nini unanisisitizia nikufungulie hazina ya serikali? Ni mali ya watu gani? Hii pia ni ya watu hao hao ambao wamelala kwenye nyumba zao bila ya wasiwasi na kwa starehe. Sawa, basi nina wazo lingine, lifuate kama utapenda.”

“Ni wazo gani hilo?”

“Kama uko tayari basi chukua upanga wako na mimi nitachukua wangu. Mji wa zamani wa Hirah hauko mbali na hapa. Kuna wafanyabiashara wakubwa na matajiri, twende huko tumvamie na tumshambulie mmoja wao wakati wa usiku na tumnyang’anye mali nyingi’’

“Ndugu yangu, sikuja hapa kwa wizi na unyang’anyi kwamba ndiyo unishauri mambo hayo. Nakuomba tu uwaamrishe waweka hazina wanipe pesa ambazo ziko chini ya mamlaka yako ili niweze kulipa madeni yangu.”

“Kama tukiiba mali ya mtu mmoja siyo bora zaidi ya kuiba mali ya mamil- ioni ya Waislamu? Ni vipi kwamba kuchukua mali ya mtu mmoja binafsi kwa upanga ni wizi na kunyakua mali ya umma sio wizi?” Unavyochukulia ni kuwa wizi unamaanisha tu kumvamia mtu binafsi na kumnyang’anya mali yake kwa nguvu. Wizi wa aina mbaya zaidi ni ule ambao unanishau- ri na kunisisitizia mimi kuufanya hivi sasa.”