read

9. Mwito Wa Kwanza

Habari zilizosikika mara kwa mara kutoka Makka kwa kabila la Bani Ghiffar zilimvutia Abu Dhar, bwana ambaye alikuwa mtu mdadisi. Alikuwa anataka kujua kwa kina maendeleo yale yaliyokuwa Makka, laki- ni habari potofu ambazo alikuwa akipata mara kwa mara kutoka kwa watu binafsi zilikuwa hazimkinaishi.

Jambo la wazi tu alilojua ni kuwa kuna sauti ngeni imezuka kule Makka na wenyeji wake wanafanya juhudi ili kuinyamazisha. Lakini ni sauti gani hiyo mpya, na kwa nini watu wa Makka walikuwa wakiipinga? Haya ndiyo maswali yaliobaki bila ya kujibiwa. Alimueleza nduguye aliyekuwa akien- da Makka, kuwa, “Watu wananiambia kuwa huko Makka ametokea mtu na ameleta habari mpya, na yeye anadai kuwa amefunuliwa habari hizo kuto- ka kwa Mungu. Kwa vile unaelekea Makka, nichunguzie mambo hayo na uniletee habari kamili.”

Siku zikapita huku akimsubiri kaka yake kwa hamu. Aliporudi Abu Dhar alimwambia, ‘‘Nipe habari ya mambo yalivyo huko?”

“Kulingana na udadisi wangu yeye ni mtu ambaye anawaita watu kwenye maadili mema pia ameleta maneno ambayo sio mashairi.”

“Nilikuwa nataka ufanye uchunguzi makini zaidi na wa kina. Hizi habari ulizoleta hazitoshi kwa lengo langu. Afadhali niende mwenyewe kujua ukweli.” Alibeba mkoba wake kisha moja kwa moja alielekea Makka. Alikuwa amedhamiria sana kukutana na yule bwana ambaye ameleta maneno mapya na angepeda kusikia maneno hayo kutoka kwenye kinywa chake mwenyewe. Lakini hakumjua mtu huyo wala hakuona umuhimu wa kuuliza kwa wengine kumhusu.

Hali ya Makka ilikuwa mbaya kwa dhuluma na kuogofya. Bila kudhi- hirisha nia yake kwa mtu yeyote alikuwa akichunguza kila mahali huku akisikiliza mazungumzo ya watu karibu naye akitumaini kupata dalili. Msikiti wa Makka ndio ulikuwa kituo cha habari ya matukio yote. Ndipo alipokwenda na mzigo wake mgongoni. Usiku ulifika lakini hakupata habari yoyote. Aliamua kujinyoosha kidogo. Baadaye kijana fulani alipita karibu na alimuangalia Abu Dhar kwa macho ya kupeleleza na kwenda zake. Kumuangalia kwake kulikuwa na maana kubwa kwake. Aliona huen- da huyo bwana mdogo ndiye angelifaa kumueleza siri yake. Alimfuata lakini alirudi bila kuthubutu kusema naye.

Siku ya pili pia aliketi Msikitini mchana kutwa kwa makini akitafuta kidokezo chochote kile lakini hakufanikiwa.

Usiku ulifika na akajinyoosha mahala pale pale. Kijana yule alikuja tena kwa heshima na akasema: “Wakati haujafika wa wewe kwenda nyumbani kwako na kulala huko?” Baada ya kusema hivyo alimchukua nyumbani kwake. Abu Dhar hakumfunulia siri yake usiku huo, wala bwana mdogo hakumuuliza. Asubuhi Abu Dhar alimuaga na akaenda msikitini kuendelea na uchunguzi wake. Siku hiyo pia ilipita na usiku ukafika na hakuweza kupata chochote kutokana na mazungumzo ya watu. Kijana yule alimjia tena na akaenda naye hadi kwake, lakini wakati huu alizungumza.

“Waweza kuniambia ni kwa nini umekuja katika mji huu?” “Nitakueleza tu kama utaahidi kunisaidia.”

“Nakuahidi nitajaribu kadiri ya uwezo wangu kukusaidia ”

“Ukweli ni kwamba tumekuwa tukisikia kutoka miongoni mwa makabila yetu kwamba kuna bwana amezuka huku Makka na ameleta mazungumzo fulani akidai yametoka kwa Mungu. Nimekuja ili nimuone na nimchunguze. Kwanza nieleze unaamini nini kuhusu yeye? La pili, unaweza kunielekeza kwake?”

Nakuhakikishia kuwa yuko kwenye haki na anayoyasema yanatoka kwa Mwenyezi Mungu. Nitakupeleka kwake asubuhi. Lakini kama ujuavyo hawa watu wakijua, maisha yako na yangu yatakuwa hatarini. Kesho asubuhi nitatembea mbele yako na utanifuata nyuma kwa mbali kidogo, kama nitaona hatari yoyote nitasimama na kuinama chini kama mtu ambaye anamwaga kitu kutoka kwenye chungu, kisha utoroke. Na kama hakuna hatari basi utanifuata popote niendapo.”

Asubuhi iliyofuata kijana huyo ambaye alikuwa si mwingine bali ni Ali alitoka kwenye nyumba yake, na Abu Dhar akamfuata. Bahati nzuri njiani kulikuwa hakuna matatizo yoyote na walifika kwa Mtume (s.a.w.w) kwa salama.

Alifanya uchunguzi makini kuhusiana na tabia ya Mtume (s.a.w.w) na pia kusikiliza aya za Qur’ani. Haukupita muda mrefu akasilimu kwa moyo wake wote. Alichukuwa ahadi kwa Mtume (s.a.w.w) kuwa hatasikiliza lawama yoyote katika njia za Allah maishani mwake na atazungumza kweli ingawa itakuwa chungu kwa upande mwingine.

Mtume (s.a.w.w) alimwambia “Sasa urudi kwa makabila yako na ukawalinganie katika Uislamu hadi utakapopata amri nyingine kutoka kwangu.” Akasema, “Sawa kabisa; lakini kabla sijaondoka katika mji huu nitakwenda mbele ya watu hawa na kutangaza wito wa Uislamu mbele yao wapende wasipende, lolote liwalo.”

Alikwenda moja kwa moja hadi katikati mwa jiji (Msikitini) na akasema kwa sauti mbele ya umati wa Makureshi. “Nashuhudia kuwa hapana mola ila Allah na Muhammad ni mja na Mtume Wake. ”

Waliposikia mwito huo kutoka kwa mtu wasiyemjua, watu wa Makka walimkimbilia upesi na kama Abbas bin Abdul Muttalib asingekuja kumuokoa wangemkatakata vipande vipande. Abbas alisema: “Huyu bwana ni wa kabila la Ghifar, na misafara ya biashara ya maquraishi kati ya Makka na Syria hupitia kwenye ardhi yao. Hamfikirii kwamba mkimuua mmoja wa watu wao hamtakubaliwa kamwe kupita kwenye nchi yao kwa amani?

Abu Dhar aliokolewa kutoka mikononi mwao. Hata hivyo hakuridhika. Alisema, “Kwa mara nyingine nitarudia mwito huu wacha hawa watu wasikie kile ambacho hawataki kukisikia kabisa. Kama wakikisikia mara kwa mara watakizoea.”

Kesho yake alirudia maneno yale yale tena. Wale watu wakamshambulia na Abbas ambaye alikuwepo hapo akamuokoa kutokana na ukatili wao.

Baada ya hapo kulingana na amri ya Mtume (s.a.w.w), alirudi nyumbani na akaanza kulingania Uislamu miongoni mwa kabila lake. Wakati Mtume (s.a.w.w) aliguria Madina, Abu Dhar naye alikwenda na kubaki huko Madina hadi mwisho wa maisha yake. Alikuwa mkweli na mwenye msi- mamo na kutokana na sifa za uadilifu wake alifukuzwa na kuhamishwa wakati wa khalifa Uthman, mwanzoni kwenda Syria na baadaye mahali palipoitwa Rabdha karibu na Madina. Huko alifariki kifo cha upweke. Mtume (s.a.w.w) alikuwa amesema kuhusu yeye:

“Mwenyezi Mungu amrehemu Abu Dhar! ataishi peke yake atakufa peke yake, na Siku ya Kiyama atafufuliwa peke yake.