4. Yaliyosemwa na Wanazuoni wa Kisunni

Tuanze na Sheikh Abdalla Saleh Farsy. Yeye amesema hivi katika uk.40 wa kitabu chake, Maisha ya Sayyidna Hussein: "Utawala wa Yazid, kama tulivyoona , ulikuwa wa nguvu tu bila ya ridhaa ya watu". Suali ya kuuliza hapa ni: jee, inawezekana utawala wake ukawa ni "wa nguvu", lakini yeye mwenyewe akawa si wa aina hiyo? Jee, kwa mafunzo ya Kiislamu, Amiirul-mu'minin huruhusiwa kutawala watu kwa "nguvu tu bila ya ridhaa" yao?

Maneno kama hayo takriiban yamesemwa na Sheikh Muhammad Abduh. Chini ya maelezo ya Sura 5:36-37, katika uk. 367 wa Juzuu ya Sita ya tafsiri yake ya Qur'ani Tukufu ijulikanayo kwa jina la Tafsiirul Manaar, shekhe huyo amemwita Yazid "kiongozi wa dhulma na ukandamizaji ambaye alitawala mambo ya Waislamu kwa nguvu na makri"! Jee, aliye hivyo huitwa Amiirul-mu'minin ?

Wa tatu ni Allamah Shawkaani katika kitabu chake cha Hadith za Mtume s.a.w.w. kiitwacho Naylul Awtwaar. Katika uk. 362 wa Juzuu ya Sabaa ya kitabu hicho, amemweleza Yazid kuwa: "mlevi, katembo, mvunjaji utukufu wa sharia takatifu"! Huyo ndiye Amiirul-mu'minin kwa mawahabi wetu?

Wa nne ni Abul Hasan Ali bin Muhammad bin Ali at Twabari, mwanachuoni mashuhuri wa Kishaafi'i. Alipoulizwa kuhusu Yazid, kati ya ila alizomtia ni: "alikuwa mlevi wa kutopea (kubobea) ambaye mashairi yake ya (kusifu) ulevi yanajulikana". Hayo yamenukuliwa katika uk. 287 wa Juzuu ya Tatu ya Wafayaatul A'yaan ya Ibn Khalikaan.

Wa tano ni Imam Ibn Hazm, katika uk. 98 wa Juzuu ya Kumi na Moja ya kitabu chake kiitwacho Al Muhallaa, amemtia Yazid bin Muawiya katika kundi la wale "waliosimama kwa lengo la kutaka dunia tu", na akasema kuwa msimamo wake huo ulikuwa "ni ukandamizaji mtupu usiokuwa na udhuru (wa kisharia)". Haya! Mtu wa aina hiyo huwa Amiirul-mu'minin?

Wa sita ni Abul Falaah Abdul Hayy Ibnul Imaad, mwanachuoni mkubwa wa Kihambali, katika uk. 69 wa Juzuu ya Tatu ya kitabu chake mashuhuri kiitwacho Shadharaatudh Dhahab. Katika ukurasa huo amemnukuu Imam Dhahabi, mwanachuoni mwengine mkubwa, kuwa amesema kwamba. Yazid "alikuwa naasiby (mtu anayemchukia Imam Ali a.s), fidhuli, jeuri, anakunywa pombe na kufanya munkar. Aliianzisha dola yake kwa kumuuwa Hussein, na akaimaliza kwa tukio la Harra. Watu wakamchukia, wala hakubarikiwa katika umri wake". Tukio la Harra ni lile shambulizi la Madina tulilolitaja uk. 15 – 16.

Jee, mtu ambaye ameianza dola yake kwa kumuuwa mjukuu wa Bwana Mtume s.a.w.w., na kuimaliza kwa kuushambulia "mji wa Mtume s.a.w.w." (Madina) na kuwaachia mimba za haramu wanawake wasiopungua elfu moja, hufaa kuitwa Amiirul-mu'uminin? Tunawauliza mawahabi wetu: Kwa hujja gani ya Kiislamu?

Wa sabaa ni Ibn Kathir ambaye, kwa kawaida, mawahabi humtegemea mno. Yeye, katika uk. 235 - 236 wa Juzuu ya Nane ya kitabu chake kiitwacho Al Bidaaya Wan Nihaaya, ameyataja "yaliyopokewa" kuhusu Yazid. Kati ya hayo ni "kwamba Yazid alikuwa mashuhuri kwa kupenda muziki na kunywa pombe, kufanya urafiki na watoto wa kiume na wanawake waimbaji; Na hakuna siku ambayo aliamka hakulewa.."!

Na kabla ya hapo, katika uk. 216 wa kitabu hicho hicho na juzuu hiyo tuliyoitaja hapo juu, Ibn Kathir anaeleza ya ujumbe wa "watukufu wa watu wa Madina" uliokwenda kwa Yazid. Anasema: "Waliporejea Madina, walitangaza shutuma zao dhidi ya Yazid na aibu zake. Wakasema, 'Tunatoka kwa mtu asiyekuwa na dini, anayekunywa pombe, ambaye wanawake waimbaji humuimbia na kumpigia muziki…" Pia ametaja yaliyosemwa na kiongozi wa ujumbe huo, Mundhir bin Zubeir, aliporejea Madina baada ya kupitia Basra kwa swahibu yake, Liwali wa huko (Ubeydillah bin Ziyaad), kuwa Yazid "anakunywa pombe na kulewa mpaka akaacha swala"!

Haya! Mambo yakifikia hapo, ni Mwislamu wa aina gani atakayejifakhiri kuwa na Amiirul-mu'minin sampuli ya Yazid?

Mawahabi waliotoa karatasi zao na kumwita Yazid Amiirul-mu'minin bakhti yao hawakuwako zama za Ukhalifa wa Umar bin Abdulaziz. Wangekiona cha mtema kuni! Khalifa huyo, aliyekuwa kabila moja na Yazid, alimpiga mtu aliyemwita Yazid hivyo, viboko ishirini! Kama wataka kuyaona hayo, nawatizame uk. 69 wa Juzuu ya Tatu ya Shadharaatudh Dhahab.