Si Uzushi wa Mashia

Katika karatasi zao, mawahabi wamesema: "Waandishi wa ki-Sabai wa Iraq walizua hadithi za urongo, za kikatili na za kutisha, kama vile kunyimwa maji ya kunywa (Hussein na watu wake) na kulazimishwa kupigana, kukatwa vichwa, ambazo haziaminiki wala haziwezi kutegemewa na pia ziko mbali na ukweli."

Majibu yetu: Penye vitabu vya Kiswahili, viwezavyo kupatikana madukani humu humu mwetu, hapana haja ya kutaja vitabu vya lugha nyengine ambavyo wengi wa watu hawana au hawawezi kuvipata au hawaijui lugha iliyoandikiwa vitabu hivyo. Kwa hivyo tuangalie kitabu kiitwacho Maisha ya Sayyidna Hussein (chapa ya 1999) kilichoandikwa na Sheikh Abdalla Saleh Farsy na kuchapishwa na Adam Traders wa Mombasa.

Katika uk. 37 wa kitabu hicho, Sheikh Abdalla ameandika hivi: "Alipowajibu kwa yakini (yaani Imam Hussein a.s.) kuwa hakubali kwenda kuuawa na Ubeydillah na kudhalilishwa, wala kuuawa watu wake na kudhalilishwa, wanaume na wanawake na watoto, waliwazunguka darmadar wasiwe na njia ya kupenya na kukimbia. Wakakosa maji na chakula tangu hapo mwezi nane Mfunguo Nne 61 mpaka mwezi kumi 61; hapo wakaingia kuwapiga baada ya kuwa hawajifai kwa njaa na kiu". Baada ya hayo, akataja orodha ya watu kumi na moja ambao ndio "wa mwanzo kuuawa"; wote wakiwa ni jamaa zake Mtume (s.a.w.w.)!

Na katika uk. 39 wa kitabu hicho hicho, akasema kwamba baada ya kuuliwa hivyo, walipelekwa "kwa shangwe kubwa na ngoma mpaka Al Kufa kwa Liwali. Kila mtu akajitapa mbele ya huyo Liwali 'Mimi nimemuua fulani …. Mimi nimemuua fulani…' na huku wanapewa tuzwa (tunza)". Wakifika huko, Sheikh Abdalla anasema, ikawa "vichwa vimetawanywa chini".

Jee, vichwa hivyo vilitoka vyenyewe miilini mwao au vilikatwa?

Wakasema tena katika hiyo karatasi yao: "Na madai ya Mashia kwamba Hussein alikatwa kichwa chake ni urongo mtupu."

Majibu yetu: ni tumsome tena Sheikh Abdalla Saleh Farsy. Katika uk. 38 wa hicho kitabu chake, shekhe wetu huyo anaeleza kwamba, baada ya kumzingira "kila upande kwa kumpiga kwa mishare, mikuki na panga mpaka akaanguka chini, wakamkata kichwa. Na qawli mashuhuri (ni) kuwa aliyemkata kichwa ni Shimr bin Dhiljawshan…" Kisha akaongeza: "Pesa na kutaka ukubwa kunafanya kazi."

Wala madhalimu hao hawakutosheka tu na kukikata kichwa cha Imam Hussein (a.s). Anavyoeleza Sheikh Abdalla Saleh Farsy (uk. 39) ni kwamba, kilipofika kwa Liwali Ubeydillah, ikawa "anakigonga kichwa cha Al-Hussein kwa kifimbo mkononi kama kwamba anapiga upatu au chapuo." Na kilipofika kwa Mfalme mwenyewe (Yazid bin Muawiya), Sheikh Abdalla anaeleza (uk. 40), alifanya "kama yale aliyoyafanya Liwali wake wa Al Kufa. Akakamata kifimbo akawa anayagonga meno ya Hussein .."

Basi hayo ndiyo aliyoyaandika Sheikh Abdalla Saleh Farsy aliyekuwa Kadhi Mkuu wa Kenya na, kabla ya hapo, Zanzibar. Jee, yeye alikuwa "mwandishi wa ki-Sabai wa Iraq?" Alikuwa Shia? Ni "mrongo"? Hakuwa shekhe mkubwa waliyekuwa wakijifakhiri naye hao "Ahlul-Tawheed", na mpaka leo hujifakhiri naye? Sasa wanasemaje?