read

15. Tuifaidi Tawba

Sisi tusiupoteze muhula huu wa TAWBA kutoka mikononi mwetu, na tusije tukaingia makaburini mwetu bila ya kufanya TAWBA, kwani huu ndio mlango wa Rehema. Neema hii ya TAWBA (kurejea katika haki) hubadilisha giza kuwa nuru, baya kuwa jema na vile vile kuuzima moto wa Jahannam. Iwapo utakufa huku umejitwisha mzigo mzito wa madhambi yako, utambue wazi kuwa kaburi ni mahala pabaya sana pa kutokewa adhabu.Lakini iwapo utakwenda huko umeshatubu, basi kaburi ni mahala pazuri kwa waliofanya TAWBA- wingi wa rehema. Shimo lako halitakuwa shimo la mateso, bali litakuwa ni mahala penye rehema!

Pale panapofikia maji, hugeuka kuwa kijani na hali ya uhai hujionyesha, na pale panapotokea machozi, hugeuka rehema. Iwapo mja ataka kumridhisha Mola wake, basi amrejee na kumlilia Mola wake. Yamebahatika yale macho ambayo hulia na kutoa machozi kwa khofu ya Mola na nyoyo nyenyekevu ni zile zilizojiweka chini (zisizo na kiburi, fakhari au maovu). Baada ya dhiki ni faraja. Amefarajika baada ya kufanya TAWBA ndiye mtu aliyebahatika mno!

Mtume Yusufu a.s. alikuwa ni Mtume na vile vile alikuwa ni mwana wa Mtume Yaakub a.s. alikuwa na sifa moja iliyo bora kabisa ambayo ni uvumilivu na saburi ya hali ya juu. Na hii ndiyo sababu alikubalia kuwasamehe kwa uwepesi ndugu zake kwa makosa makubwa kama hayo yaliyokuwa ametendewa nao.

Sisi pia tumwangukie Allah swt kwani atatusamehe madhambi yetu yote,Yeye atazikubalia duaa zetu zote, tuseme:"Ewe Allah swt! nilikuwa sijui, nilipotoka, nilikuwa katika ndoto na nilikuwa nimefungwa kwa minyororo ya matamanio ya nafsi yangu.

"Ewe Allah swt! Mimi nimekuwa nikiasi hukumu zako kwa kipindi kirefu mno, sasa nimeshaamka kutoka ndoto yangu.

Nisamehe harakati zangu zisizokuwa sahihi na kunifutilia makosa yangu yote. Ewe Mola wangu! Nisamehe makosa yangu. Ewe Msamehevu! Nisamehe makosa yangu! Kwani mimi nilikuwa mwovu na mtenda maasi, wakati wewe u Mrehemevu na Msamehevu na Makarimu, naomba msamaha! Niteremshee rehema na baraka zako ili niongoke kutokana na balaa za maasi."