read

31. Majuto Ya Moyoni Yawe Kwa Ajili Ya Allah Tu

Iwapo mtu atasema kuwa mimi nimekwisha fanya TAWBA na huku moyoni hana majuto yoyote ya madhambi, basi huyo ni MWONGO. Kwani uhakika wa TAWBA ni kujuta kwa madhambi aliyoyatenda mtu. Inawezekana mtu akajuta au kusikitika kwa dhambi alizozitenda na wala majuto yake si kwa ajili ya kutaka kufanya TAWBA na vile vile mtu anaweza kujiepusha na matendo ya madhambi kwa sababu za kidunia tu kama vile anahofia asidhurike kwa hasara za kimwili au heshima yake itapotea kwa kujihusisha navyo au anaogopa asije akafungwa jela. Sasa iwapo yeye atasema 'Astaghfirullah' kwa kutokana na vitisho kama hivyo, basi huyo ni mnaifki na ndiyo maana tunasema kuwa yu-mwongo. Sifa kubwa kabisa ya TAWBA ni kwanza kuacha kutenda madhambi na kufanya majuto na huzuni kwa madhambi yaliyokwisha fanywa hapo awali.

Lakini kwa kuwa kilio chake ni kwa sababu ya khofu ya adhabu au kukosa thawabu za Allah swt basi ni sawa na yule mtu ambaye baada ya kutesa na kudhulumu kupita kiasi na yupo anatafutwa na Serikali kwa kushitakiwa ili akamatwe popote pale alipo na hatimaye kufungwa jela. Sasa anatumia hila kwa kumwendea aliyemdhulumu ili amsamehe huku akilia ili kwamba asije akakamatwa na polisi akahukumiwa. Haya hayakuwa matendo yake yenye nia njema ya kumwomba msamaha wa kweli bali yalikuwa ni baada na kwa khofu ya polisi.

Hivyo huyo mtu akiwa amejaa khofu ya Jahannam anafanya TAWBA - hadaa. Na iwapo angalikuwa na matumaini ya kutoingizwa motoni (Jahannam) basi asingalifanya TAWBA wala asingelisikitika na wala asingejitambua kuwa yeye ni mwenye madhambi. Swala hili lipo wazi na sisi hatuwezi kusema kuwa hiyo ndiyo TAWBA hakiki. TAWBA ya uhakika ni ile ambayo itatoa ushahidi wa nia na matendo yake yaliyo mema na kumfanya mtu akajirekebishe na kufuata njia nyoofu.

Allamah Tusi A.R.na Allamah Hilli A.R. wameelezea katika 'Tajrid al-Kalaam' kwa mukhtasari kuwa, mtu aketi kwa kutulia na kusikitikia madhambi aliyoyatenda dhidi ya hukumu za Allah swt, basi hapo TAWBA yake inaweza kuwa sahihi.Lakini iwapo atafanya TAWBA kwa uoga wa serikali au kwa khofu ya kupoteza heshima yake mbele ya watu, basi TAWBA yake hiyo ni kujihadaa mwenyewe!

Hivyo tumeelewa kuwa TAWBA ni kwa ajili ya Allah swt tu kwani tumemwasi Allah swt na hivyo tunuie kuwa hatutarejea kamwe madhambi na hapo ndipo kweli tutakuwa tumefuata njia ya kufanya TAWBA.

TAWBA inayo mambo mawili, kwanza, kusikitikia na kuhuzunikia matendo maovu tuliyoyatenda, na pili, kunuia na kuazimia kutorejea kutenda madhambi na vile vile kujiepusha nayo.

Mtu atakapoukaribia wakati wake wa mwisho wa kufariki, na iwapo atafanya TAWBA au asipofanya, lakini ataingizwa kaburini tu.Iwapo atafanya TAWBA basi kuna uwezekano wa kupona adhabu za Jahannam, lakini Maulamaa wanapinga TAWBA ya wakati wa mwisho (sababu zake zitatokezea mbeleni). Firauni alitubu wakati wa mwisho wa maisha yake, lakini ilimfaidia nini? Alizama pamoja na wafuasi wake kwa pamoja.Hivyo nasi tusije tukatubu kumbe kutubu kwetu kusitufaidie chochote.