33. Tawba Ni Mlango Wa Rehema
TAWBA ni mlango mmoja mtukufu kabisa wa Rehema za Allah swt na TAWBA ni bahati ya watu wenye imani na wapenxi wa Ahli Bayt a.s. Tujue kuwa hakuna dhambi lolote lile lisiloweza kusamehewa, hata TAWBA ya Makafiri au mapagani pia huweza kukubaliwa.
Lakini mapenzi ya Ahli Bayt ya Mtume Mtukufu s.a.w.w. ni sharti mojawapo au sivyo mtu anaweza kukosaukubalio wa TAWBA yake hadi kufari dunia.Kwani mapenzi hayo yapo yameamrishwa na Mwenyezi Mungu katika Qurani Tukufu na vile vile Mtume Mtukufu s.a.w.w. pia ametulazimisha kwa hayo.
Ni lazima vile vile tutambue kuwa TAWBA itakayofanywa katika uhai wa mtu kabla ya kifo chake, ndiyo itakayomfaidi kwani atanuia kuacha maovu kuanzia hapo anapotubu lakini yule mtu anayefanya TAWBA wakati wa mwisho wa pumzi yake hutambua kuwa sasa hanao muda mwingine wa kutubu, hivyo anajaribu kufanya TAWBA ili anusurike, lakini hivyo haitamsaidia kwani anatambua kuwa hana njia nyingine ila ni TAWBA tu na hivyo hana wakati wa kujirekebisha na kuacha maovu kwani mauti imeshaanza kumtoa jasho utosini. Je, mtu kama huyo anaweza kudai kuwa hatarudia kutenda maovu tena? Ambapo katika TAWBA tunanuia kutotenda tena madhambi. Huyo amejihadaa kabisa. Watu kama hawa wapo wanzungumzwa katika Qurani Tukufu:
Na TAWBA (yenye faida) kwa ajili ya wale watendao maovu hadi mauti inapowahudhuria mmoja wao. (4:18)
TAWBA si jina la kulazimishwa, bali ni kutekelezwa kwa ibada zote zilizo za faradhi tulizoziacha, iwapo tunadaiwa fidia, basi tuzilipe na tuache kabisa mambo yote yaliyoharamishwa katika Islam.
Kwa kifupi ni kwamba, iwapo mtu ataathirika kwa masikitiko ya madhambi yake wakati wa kufa, basi haitambuliwi kuwa ni TAWBA. Kwani TAWBA ni kusikitika na kujutia kwa yale mambo yaliyo kinyume na maamrisho ya Allah swt na wala si kusikitika baada ya kuona na kuhisi adhabu.
Imam Zaynul Aabediin a.s. anasema katika Sahifa-i-Sajjadiyyah, kuhusu TAWBA:
"Mlango wa Rehema ulioufungua wewe (Allah swt) kwa ajili ya waja wako unaitwa TAWBA, mlango huo huwa daima upo wazi, sasa hakutakuwapo yeyote na kisingizio mbele yako...."
Allah swt anatuambia katika Qurani:
Basi hoja yaMwenyezi Mungu (pekee) ndiyo amri (6:149)
Kwa yakini kuna ushahidi kamili mbele ya Allah swt, hivyo iwapo mtu atajaribu kujitetea visivyo kwa kusingizia kuwa alipotoshwa na matamanio nafsi yake, basi hapo atajibiwa:"Je, hatukuwawekeeni wazi mlango wa TAWBA? Sasa kwa nini haukufanya TAWBA na kuomba msamaha na rehema za Allah swt.
Bila shaka Rehema na Maghfirah za Mwenyezi Mungu zipo kwa wingi, hivyo inatubidi sisi tufanye TAWBA kamilifu ili maovu yetu yabadilishwe kuwa mema, kama vile Qurani isemavyo:
..Hao (waliotubu) ndio Mwenyezi Mungu atawabadilishia maovu yao kuwa mema. (25:70)
Kwa mujibu wa Aya hiyo juu ya sura al-Furqaan, si kwamba ni madhambi yetu tu ndiyo yatakayo futika bali hata matendo yetu maovu pia yatabadilishwa kuwa mema. Hivyo tujihadhari na jitihada za sheitani ambaye daima huwa akibuni kila aina ya mbinu za kuwapotosha wale walio katika Siraat-i-Mustaqiim.
Katika Sura an-Nahl twaambiwa:
Kisha hakika Mola wako kwa wale wanaotenda ovu (tendo) katika hali ya ujahili (ujinga) na hugeuka (kwa kutubu) baada yake na hujirekebisha, kwa hakika Mola wako ni mwingi wa kusamehe, Mwingi wa kurehemu. (16:119)
Katika tafsiri 'Majmaul Bayaan' na 'Al-Miizan fi Tafsiril Quran' Juzuu ya nne na Juzuu ya ishirini uk. 398 ya Allamah Syad Muhammad Husseyn Tabatabai. Chapa ya pili 1974 Beirut. Ipo riwaya ifuatayo juu ya Istighfaar:
'Baada ya kuteremka kwa Aya 3:135, Sheitani alikuja Makkah na kupiga sauti kubwa mno juu ya mlima Thuwayr, ambayo iliwafanya mashabiki wake wote wakusanyike, nao walipokuja walimwona bwana huyo amezongwa na mushkeli mkubwa sana na hapo hawakusita kumwuliza: "Je umekuwaje na hoja gani ya kutukusanya hapa?"
Akajibu: Imeteremka Aya isemayo kuwa Ummah wa Muhammad utasamehewa kabisa madhambi yake na masharti ya TAWBA yaliyokuwa yamewekewa Ummah yaliyotangulia, yameondolewa kwao. Na iwapo sisi hatukubuni mbinu dhidi yake, basi juhudi zetu zote za kuwapotosha hazitakuwa na athari yoyote kwani wao watakapofanya TAWBA,madhambi yao yatasamehewa yote kwa pamoja na hata kubadilishwa kuwa matendo mema."
Kwa hivyo nimekuiteni hapa ili tutafute mbinu za kukabiliana na swala hili ama sivyo sisi hatutakuwa na kazi yoyote ile."
Kila mmoja wao alitoa mpango wake aliinuka mmoja wa Masheitani, akasema: "Nitafanya hivi na vile......." Lakini hawakukubaliana naye, nao wengine pia walisema walivyokuwa wakiona, nao wote walikwenda wakipingwa mmoja baada ya mwingine.
Na hapo akainuka Waswas - Khannas, naye akasema: "Nitawatia watu katika hatia (madhambi) na papo hapo nitawasahaulisha Istighfaar (TAWBA) na nitawaambia kuwa "Ewe bado unao muda mwingi wa kufanya TAWBA, haraka ya nini? Huu ndio muda wako wa kustarehe na kufaidi umri wako! Siha yako na vile nguvu zako zinakuruhusu ufanye hivyo, hivyo starehe hadi utakapokuwa mzee, utafanya TAWBA kiasi utakacho!"
Kwa hayo, Masheitani wote walifurahi mno na yeye Khannas alikabidhiwa kazi hiyo hadi kufika siku ya Kiyama.
(Tafakari Sura an-Naas, Nambari 114)
Hizi ndizo wasiwasi za Sheitani ambazo huwapotosha watu wengi hasa vijana ambao hudhani kuwa wao bado wanao umri mrefu wakufanyw TAWBA hapo mbeleni. Sisi twachukulia uzee ndio wakati wa kufanya TAWBA, lakini nani anayejua kuwa uzee huo ataufikia au atakufa kabla yake. Je siku hizi hatuoni kuwa wazee ndio waliobakia hai ambapo vijana wamekufa kwa magonjwa kama UKIMWI? Na magonjwa mengine ambayo hayana hata muda wa kuyashughukikia vyema kama homa ya uti wa mgongo, (seven days) n.k. Kwa hivyo fanya lile uliwezalo leo badala ya kungojea kesho, kwani unaweza kuugua vibaya sana na hata kufa! Jambo linlotubidi kujiambia ni : "Sielewi ni lini mauti yangu itanifikia na kunichukua, labda hata sasa hivi ipo mgongoni mwangu ikinichukua, hivyo ni aibu kufika mbele ya Mwenyezi Mungu huku nimejitwisha mzigo mzito wa madhambi bila ya kufaidi fursa ya TAWBA!"
Je, ndugu zangu, Imani yetu haipo hatarini? Labda tukafa mauti isiyo ya Islam na ambapo Allah swt anatuambia tusife ile tukiwa Waislamu!
Quran Tukufu inatuambia katika Sura ar-Ruum:
"Kisha ubaya ndio ulikuwa mwisho wa wale waliotenda uovu, kwa kukadhibisha Aya za Mwenyezi Mungu, na kwa haya walizoea kudhihaki. (30:10)
Vile vile twaambiwa katika Sura Aali Imraan:
Na harakisheni kwa (njia ya kujipatia) Maghfirah kutoka Mola wenu! (3:132)