38. Madhambi Ni Giza Wakati Tawba Ni Nuru
Allah swt anatuambia katika Qurani:
Mwenyezi Mungu ni mlinzi wa wale walio amini, yeye huwatoa kutoka giza na kuwaingiza katika nuru.....(2:257)
Imam a.s. anasema: "Kuongozwa kunamfanya mtu atolewe kutoka gizani na kuelekezwa penye maghfrah na ambavyo hatimaye TAWBA kamilifu."
Wale ambao wameshapotoka na ambao wanamfuata Taaghuti (sheitani) hutolewa kutoka nuru na kuingizwa katika giza. Hapa muradi (maanisho) ni wale ambao walikuwa katika nuru ya Islam na wakapendana na kiongozi mwovu na mdhalimu (sheitani) basi hao kwa sababu ya mapenzi hayo pamoja na mwovu wametoka kutoka nuru na kuingia katka giza. Basi hapo ndipo Allah swt anawaahidi kuwaingiza katika Jahannam pamoja na makafiri.
Mtu anapoamua kufanya urafiki wa Mwenyezi Mungu basi utamwona daima akijiweka katika hali ya tahadhari kwani utakachomwambia utaona akikuambia kuwa yeye kwanza atalifikiria na kuona iwapo hakuna uvunjaji wa hukumu za Allah swt na vile vile ataangalia maadili. Kwa hakika katika mambo yako mengi wewe utamwona yeye akikuambia kuwa yeye hataweza kushiriki pamoja nawe katika safari, michezo au hata hafla fulani fulani na hata mikutano kwani sababu atakazokuambia wewe utaona kuwa huyu mtu amezidi mipaka ya ucha Mungu na hapo hautasita kumwambia kuwa 'Bwana, mambo haya unayotaka kufafuata ni ya kale, na dunia siku hizi imeshaendelea, hivyo achana navyo!' Lakini yeye hatatingisika katika uamuzi wake kwani yeye anataka ridhaa ya Allah swt! Na vinginevyo atakushauri wewe uyaache hayo kwani hayana faida kimaadili.
Lakini yule aliyejitakia urafiki wa Sheitani, mambo ni kinyume kabisa na hayo ya juu. Huyu hata bila ya kumwambia chochote utaona akibuni mambo ya kiajabu ajabu, mara hebu twende tukajaribu bangi, pombe, mihadarati, mabibi na maovu ya aina yote. Na wewe iwapo utajaribu kumpinga basi utaona akikulaumu na hatimaye ataweza kukushawishi kwa njia mbalimbali kwani atakuambia,"Basi twende pamoja, lakini wewe usifanye lolote lile" au mara nyingine "Twende lakini utajaribu kidogo tu na iwapo utaona haupendelei kuendelea, basi tutaacha na tutarudi........" Na hapo utaona kweli hebu niende na nitarudi iwapo sitapendezewa, lakini ukifika huko utaona akikugeuka na kukuambia ngojea kidogo tu, sasa hivi tutakwenda hebu jaribu kidogo....
Hii ndiyo tofauti kati ya nuru na giza, urafiki wa Allah swt na sheitani!