read

45. Sifa Za Wamchao Allah

Ifuatayo ni Hotuba Na. 193 ya Imam Ali ibn Abu Talib a.s. kutoka Nahjul Balagha. (Sharh ya al- Hadid, Vol. 10, uk. 132-162)

Imeripotiwa na Sahaba wake Amir al- Muuminiin Ali ibn Abi Talib a.s. aliyekuwa akiitwa Hammam ibn Shurayh ambaye alikuwa mcha Mungu sana. Alimwambia Imam Ali a.s. "Ewe Amir al-Muuminiin, nielezee sifa za Muttaqiin (Wacha Mungu) kwa hali ambayo kama kwamba ninawaona wao." Imam Ali a.s. alijaribu kusita katika kumjibu na alimwambia, "Ewe Hammam, mwogope Allah swt na utende matendo mema kwa sababu Allah swt anasema katika sura ana-Nahl Aya 128: "Kwa hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wale wanaomcha, na wale wafanyao wema."

Hammam hakuridhika kwa hayo na alimfanya Imam Ali a.s. aseme zaidi. Kwa hayo Amir al-Muuminiin a.s. alianza kwa kumtaja na kumhimidi Allah swt na kumsalia mtume Muhammad s.a.w.w. na hapo alisema:

"Amma baad, Allah swt aliyetukuka, aliyeumba viumbe. Yeye aliviumba bila ya kuwa na mahitajio ya utiifu wao au kusalimika kwao kwa utendaji wa madhambi yao, kwa sababu dhambi afanyalo mtu yeyote haimdhuru yeye na wanaomtii wala haitamfaidia kitu chochote. Yeye amewagawia miongoni mwao riziki zao na amewaweka katika nafasi zao humu duniani.

Hivyo wanaomwogopa Allah swt, hao ni watu wapambanuao, mazungumzo yao yapo mahasusi (bila ya kuongezea au kubabaisha huku na huko) na mavazi yao ni ya heshima na mwendo wao ni wenye haya (nyenyekevu). Wao huwa wanafumba macho yao kwa yale yaliyoharamishwa na Allah swt kwa ajili yao, hutega masikio yao kwa elimu ambayo inamfaidia yeye. Wao huwa daima katika hali ya majaribio (hujitaabisha kwa ajili ya dini) hata kama wao huwa katika hali ya kustarehe. Iwapo kusingekuwa kumepangiwa wakati maalum wa kufariki, basi roho zao zisingekuwa zimebakia katika miili yao hata kwa kufumba na kufumbua macho kwa sababu ya hamu yao ya kutaka malipo yao (jazaa) na kwa khofu ya adhabu za Allah swt zenye kutisha mno.

Ukuu wa Muumba upo moyoni mwao na kwa hivyo, kila kitu kilichobakia huwa ni dogo machoni mwao. Kwao Jannat (peponi au Paradiso) ni kama kwamba wanaiona na kustareheka kwa neema zake. Kwao, Jahannam (motoni au Helo) ni kama kwamba wanaiona wapo wanataabika kwa adhabu zake.

Nyoyo zao zimejaa masikitiko, wamehifadhika na maovu, miili yao ni miembamba, mahitajio yao ni machache, na nyoyo zao zipo safi. Wao wamevumilia shida kwa kitambo kidogo na badala yake wamejipatia starehe za muda mrefu. Hiyo ni biashara iliyorahisishwa na Mola kwa ajili yao. Dunia inawatamani wao, lakini wao hawaitamani kamwe. Dunia iliwateka, lakini wao walijifanya huru kwa malipo. (nafasi zao)

Amma wakati wa usiku wamekuwa wakisimama kwa miguu yao wakisoma sehemu ya Qurani na usomaji wao huwa sahihi kimizania, wakifanyia majuto na masikitiko na kuomba kwa hiyo Qurani, matibabu ya magonjwa yao. Wanapopitia Aya juu ya Shauku (ya peponi) wao huichukua kwa pupa, na nyoyo zao huzigeukia kwa shauku, nao huhisi kama kwamba hivyo vipo mbele ya macho yao.

Nao wanapopitia aya zenye khofu (za Jahannam) wao huzizingatia kwa moyo na kuhisi kama sauti za Jahannam na milio yake yanaingia masikioni mwao. Migongo yao hukunjika, husujudu juu ya vipaji vyao, viganja, magoti na vidole vyake vya miguuni na huomba kwa Allah swt ukovu wao, wakati wa mchana wao huvumilia, wakiwaona waja wa kwelikweli ambao wanamwogopa Allah swt kwa wingi. Iwapo mtu yeyote akiwatazama, watawadhania kuwa wao ni wagonjwa, ambapo wao si wagojwa kama vile wanavyodhaniwa na vile vile husemwa kuwa wamerukwa na akili. Kwa hakika, khofu ya ziada zimewafanya wawe wendawazimu.

Wao hawaridhishwi na matendo yao yaliyo mema kwa uchache, na wala hawachukulii matendo yao makubwa kama ni makubwa. Wao huwa daima wakijilaumu na kuogopea matendo yao. Anapotokea mmoja wao akizungumzwa saidi, yeye husema: 'Mimi ninajielewa vyema kuliko vile wanielewavyo wengine, na Ewe Mola wangu! wanijua zaidi kuliko hata nafsi yangu. Ewe Allah! usinitendee kwa mujibu wa yale wayasemayo, na unifanyie mema zaidi kuliko vile wanifikiriavyo na unisamehe (zile kasoro) wao wasizozijua.'`

Alama yake ya kipekee ni kuwa utamwona yu mwenye nguvu katika Dini, mshupavu na mpole kwa pamoja, imani pamoja na kusadiki, juhudi katika (kutafuta) elimu kwa subira, ukiasi katika utajiri, upendo katika ibada, mwenye kushukuru katika njaa, mstahimilivu na mvumilivu katika hali ngumu, mapenzi katika kutafuta halali, raha katika mwongozo na chuki kwa uroho. Yeye huwa daima akitenda matendo mema lakini bado huwa mwenye woga. Ifikapo jioni huwa na shauku kubwa ya kumshukuru Allah swt. Huupitisha usiku katika khofu na huamka asubuhi katika furaha-khofu ya labda kuupitisha usiku katika hali ya usahaulifu, na furaha kwa neema na baraka alizotunukiwa na Allah swt. Ikiwa nafsi yake itakataa kustahimili kila kisichokipenda, basi naye hataikubalia ombi lake, kila kinachopendwa na nafsi yake. Macho yake yamepowa kwa yale yatakayodumu milele, ambapo vitu vya humu duniani visivyo vya kudumu, yeye hujiweka mbali navyo. Yeye huimarisha elimu pamoja na subira, na maneno yake kwa matendo.

Wewe utayaona matamanio yake ni mepesi, kasoro zake kidogo, moyo wenye khofu, nafasi iliyotosheka, chakula chake ni kidogo na cha kawaida, Dini yake ipo salama, matamanio yake yamekufa na ghadhabu yake imezimwa. Mema tu ndiyo yanayotegemewa kutoka kwake. Hapatakuwa na khofu ya kufikiwa nauovu kutoka kwake. Yeye atakuwa akihesabiwa miongoni mwa wale wanaomkumbuka Allah swt hata kama atakutwa miongoni mwa wale wanaosahau kumkumbuka Allah swt, na anapokuwa miongoni mwa wenye kumkumbuka Allah swt, hawezi kuhesabiwa miongoni mwa wenye kumsahau Allah swt. Yeye huwesamehe wale wote wasio waadilifu kwake, na humpatia yule aliyekuwa amemnyima. Yeye huwa na tabia njema hata kwa yule asiye na tabia njema mbele yake.

Kamwe hazungumzi mazungumzo yaliyo maovu, lugha yake ni laini, maovu yake hayo tena, mema yake yapo daima mbele na mizaha imeshamwondokea kwa kumgeuzia uso. Hutukuzwa pasi na kuhangaika katika maafa, mwenye subira wakati wa dhiki, na mwenye shukuru wakati wa faraja.Yeye huwa hamchukii yule anayembughudhi, na wala hatendi madhambi kwa ajili ya yule ampendaye. Yeye anakubalia yaliyo ya haki hata kabla hajatolewa ushahidi dhidi yake.Yeye hatumii kwa ubadhilifu kile kilicho mkononi mwake, wala hasahau kile atakiwacho kukikumbuka.Yeye kamwe huwa hawaiti watu kwa majina mengine yaliyo mabaya, wala huwa hawadhuru majirani zake, na wala huwa hafurahii maafa yawapatayo watu wengine, yeye kamwe hajiingizi katika ubatilifu na wala hatoki nje ya haki.

Anapokuwa kimya, ukimya wake huwa haumsikitishi na anapocheka, hapaazi sauti yake na anapotendewa mabaya, basi yeye huketi kimya akivumilia, hadi Allah swt hulipiza kisasi kwa niaba yeke.Nafsi yake inudhika naye, na watu wamesalimika naye kwa upole wake.Yeye anajitaabisha kwa ajili ya maisha ya ahera (ya milele), na huwafikishia raha watu kutokana naye.Kujiweka kwake mbali na watu ni kwa ajili ya uchaki na kujitakasisha, na ukaribu wake kwao ni kwa ajili ya upole na rehema. Kujiweka kwake mbali si kwa ajili ya upuuzi au kujiona mwenye fahari au takabari, na ukaribu wake kwao si kwa ajili ya kuhadaa au kudanganya."

Imeripotiwa kuwa Hammam ibn Shuray alipoyasikia hayo, alizimia na kufariki papo hapo kwa kuathirika na hotuba hiyo.

Hapo Imam Ali a.s. alisema: "Kwa kiapo cha Allah swt! Hayo ndiyo niliyokuwa nikiyakhofia kwake."

Aliongezea kusema: "Mawaidha kama haya ndiyo yanavyoathiri hadi akili nzuri."

Abdullah ibn al-Kawwa (mpinzani mkuu wa Imam Ali a.s.) alisema: "Ewe Amir al-Muminiin! Je, vipi wewe hauathiriki hivyo?"

Imam Ali a.s. alimjibu: "Ole wako! Ama mauti inayo saa maalumu iliyowekewa na wala haiwezi kuzidi au kuweza kubadilishiwa. Chunga sana,usitamke tena maneno kama hayo ambayo shetani ameyaweka juu ya ulimi wako."