read

7. Fadhila Za Tawba

(a) Mwenye kufanya TAWBA ni mpenzi wa Allah swt.

Allah swt anasema katika Sura al-Baqarah, Aya 222:-

"Hakika Allah huwapenda wanaotubu........" (2:222)

Al-Imam as-Sadique (a.s.) anasema:

"Allah hufurahia mno toba zifanywazo na Muumin kama vile sisi tunavyofurahi mno wakati tunapomwona rafiki yetu mpenzi aliyekuwa amepotea."(al-Kafi)

(b) Maovu kubadilishwa kuwa mema

Kwa kufanya TAWBA, kiza cha maovu kitatoka mioyoni na nafasi yake itachukuliwa na nuru. Maovu yetu yatafanywa kuwa mema.

Allah swt anatuambia katika Sura Furqaan, aya 68-70:-

"Na wale wasiomuomba Mungu mwingine pamoja na Allah, wala hawaui nafsi aliyoiharamisha Mwenyezi Mungu (kufanya hivyo) isipokuwa kwa haki (kufanya hivyo), wala hawazini; na atakayefanya hayo atapata madhara yake.Na atazidishiwa adhabu siku ya Kiyama na atakaa humo kwa kufedheheka milele.

Ila yule atakayetubia na kuamini na kufanya vitendo vizuri; basi hao (waliotubu) ndio Mwenyezi Mungu atawabadilishia maovu yao kuwa mema; na Mwenyezi Mungu ni mwingi wa kusamehe na mwingi wa kurehemu." (25:68-70)

(c) Malaika huwaombea Dua na kuwasifu

Allah swt anatuambia katika sura Muumin, Aya ya 7-9:-

"Wale wanaokikaribia kiti cha Enzi (cha Mwenyezi Mungu) na wale wanaokizunguka, wanamtukuza Mola wao na kumsifu na wanamuamini na wanwaombea samahani walioamini, (wanasema): "Mola wetu! umekienea kila kitu kwa rehema na elimu (unakijua kila kitu). Basi wasamehe waliotubu na wakaifuata njia yako na waepushe na adhabu ya Jahannamu."

"Mola wetu! Waingize katika mabustani ya milele uliyowaahidi. Na uwape haya pia waliofanya mema miongoni mwa baba zao na wake zao na watoto wao; bila shaka wewe ndiye mweye nguvu, mwenye hekima."

"Na waepushe na maovu, kwani umuepushaye na maovu, kwani siku hiyo, hakika umemrehemu; na huko ndiko kufuzu kukubwa." (40:7-9)

(d) Mwenye kutubu ni watu wa Peponi

Allah swt anatuambia katika sura Ali-Imraan, aya 135-136:

"Na ambao wanapofanya matendo ya aibu au kudhulumu nafsi zao, hukumbuka Mwenyezi Mungu na kuomba msamaha kwa dhambi zao. Na ni nani anayeghufuria dhambi isipokuwa Mwenyezi Mungu? Na hawaendelei (kwa makusudi) yale waliyoyafanya, hali wanajua.

Hao ndio malipo yao yatakuwa msamaha kwa mola wao na Bustani (pepo) zinazopita mito mbele yake ambamo watakaa milele. Na ni wema ulioje ujira wa watendao (mema)." (3:135-136)

(e) TAWBA inarefusha maisha

Allah swt anatuelezea katika sura al-Hud, Aya ya 3:

"Na ili muombe msamaha kwa Mola wenu; kisha mtubie kwake, atakustarehesheni kwa starehe nzuri mpaka muda maalum. Na atampa kila mwenye fadhila, fadhila zake." (11:3)

Imam Jaafer as-Sadique (a.s.) amesema:
"Umri wa baadhi ya watu hupungua kwa sababu ya madhambi yao na wao hufa haraka, na baadhi ya hufariki katika wakati waliopangiwa. Yaani kwa ufupi ni kwamba,madhambi hupunguza umri wa watu wakati ambapo TAWBA huongezea umri wake."

(f) TAWBA ni sababu ya kukubaliwa kwa Duaa

Suala hili tutalizungumzia kwa undani zaidi hapo mbele na vile TAWBA inavyowezesha kukubaliwa kwa Duaa .

(g) TAWBA ni ujumbe mwema kutoka Allah swt

Allah swt anatuambia katika sura Shuraa, Aya 25:

"Naye ndiye anayepokea TAWBA za watu wake, na anasamehe makosa, na anayajua yote mnayotenda." (26:25)

Imam Jaafer as- Sadique (a.s.) amesema:
"Mwenyezi Mungu alimwambia Mtume Daudi (a.s.):"Ewe Daudi! Wabashirie habari njema watendao madhambi na waja wema uwapatie nuru ya matumaini! Hapo Mtume Daudi (a.s.) aliuliza:Ewe Mwenyezi Mungu! Je, niwabashirie vipi hao wenye madhambi na kuwapa matumaini hao wema?"

Alijibiwa:"Watendao madhambi waambie kuwa mimi nitazikubali TAWBA zao.Na hao watu walio wema waambie wawe na matumaini ya malipo yao kutoka kwangu kuliko kujionyesha na kufanya kiburi kwani kwa kufanya hivyo wao watakuwa wamejipotezea urira wao kwangu.Mimi nitachukua hisabu ya kila kitu kiwe kidogo au kikubwa."

(h) TAWBA huangamiza madhambi yote kwa pamoja

Allah swt anasema katika Sura Zumar Aya 53-54:

"Sema (Ewe Mtume wetu Muhammad!): "Enyi waja wangu! mliojidhulumu nafsi zenu, msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu; bila shaka Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote; hakika yeye ni mwingi wa kusamehe na mwingi wa kurehemu."

"Na rejeeni kwa Mola wenu na mnyenyekee kwake kabla ya kukujieni adhabu, kisha hamtanusuriwa." (39:53-54)

Katika Aya hii kuna msisitizo mkubwa juu ya kufanya TAWBA. Imam ar-Ridha (a.s.) amemsikia sahaba wake kuwa Mwenyezi Mungu anamlaani yule mtu ambaye amepigana na Ali a.s. Basi hapo Imam a.s. alimjibu: "Ila aliyetubu na amekuwa mwema." Akaendelea: "Dhambi iliyo kubwa kabisa kuliko hata kumwua Imam Ali (a.s.) ni kule kumkhilafu bila kutubu." (Wasail Shia Vol. 11, page:265, mlango wa TAWBA ya madhambi makuu).

Kwa mujibu wa riwaya hiyo tuliyoisoma, inatuelezea wazi kuwa madhambi makubwa pia yanaweza kusamehewa iwapo tutafanya TAWBA.

(i) TAWBA iliyoombwa haitobatilika iwapo itavunjwa

Iwapo tuliomba TAWBA na tukarejea kutenda dhambi kwa mara ya pili, basi ile TAWBA yetu tuliyokuwa tumetangulia kuiomba, haitavunjika au kubatilika, bali inatubidi turejee kuomba TAWBA yetu kwa upya. Tujue kuwa kila tutakavyokuwa tukiomba TAWBA basi ndivyo vivyo hivyo madhambi yetu yatakuwa yakifutwa.

Muhammad ibn Muslim anaripoti riwaya ambamo Imam Muhammad al-Baquir (a.s.) amesema:"Ewe Muhammad ibn Muslim!Muumin atakapoomba TAWBA kwa ajili ya madhambi yake, basi atasamehewa na Allah swt kwani anawapenda waja wake zaidi."Hapo mimi nilimwuliza Imam (a.s.):"Iwapo mtu atatubu na kurejea dhambi na tena akaomba TAWBA."

Imam (a.s.) alimjubu: "Ewe Muhammad ibn Muslim! Wewe waelewa vyema kuwa asikitikapo na kujutia matendo yake maovu na akaomba TAWBA, je itawezekanaje kwa Allah kutoikubalia hiyo TAWBA?

Niliuliza."Je, iwapo atakuwa akiendelea vivyo hivyo kwa mara nyingi?"

Alijibu Imam (a.s.):"Hivyo pia TAWBA yake itakubaliwa na madhambi yake yatasamehewa kwani Allah swt ni mrehemavu mno na mkubalia wa TAWBA.Kwa hivyo inambidi Muumin awe na matumani ya kusamehewa madhambi yake."

Abu Basir anasema: "Mimi nilimuuliza Imam Jaafer as-Sadique (a.s.), 'Je, nini maana halisi ya 'Tawbatan-Nasuha' ambayo Allah swt anatuamrisha?"Imam (a.s.) alijibu:"TAWBA ambayo baada yake hakutarudiwa tena kutendwa kwa madhambi."

Hapo nilimuuliza:"Je, kuna mtu yeyote miongoni mwetu ambaye harudii kutenda madhambi kwa mara ya pili au zaidi?"

Imam (a.s.) alinijibu: "Ewe Abu Basir! Mwenyezi Mungu humpenda mno yule mtu aliyepotoka mno na akaja kufanya TAWBA."

Vile vile ipo riwaya nyingineyo isemayo:"Ni jambo bora kabisa la kufanya TAWBA na kufanya juhudi za kuomba msamaha wa Allah swt kila baada ya kutenda dhambi."

(j) Milango ya TAWBA ipo wazi hadi pumzi ya mwisho

Imam Muhammad al-Baqir (a.s.) amenukuliwa riwaya isemayo:

Mtume Adam (a.s.) alimwambia Allah swt: "Ewe Mola wangu! Mimi nimeghalibiwa na Sheitani, naomba unijaalie jambo lolote lenye faida kwangu."Hapo Adam (a.s.) alijibiwa:"Ewe Adam! Ninakupatia jambo ambalo iwapo kizazi chako kitakapo kusudia kutenda dhambi, basi sitamwandikia dhambi lolote.Na iwapo atatenda dhambi moja, basi nitamwandikia dhambi moja tu.Na atakapo kusudia kufanya tendo jema, basi ataandikiwa jema moja.Na iwapo atatenda hilo jambo jema, basi ataandikiwa mema kumi badala yake."

Mtume Adam (a.s.) aliendelea, "Ewe Mola wangu:"Naomba unijalie neema zaidi.Allah swt akamjibu:"Ni neema kubwa kwake yule atakaye tenda dhambi na aniombe TAWBA, nitamsamehe."

Hapo tena Mtume Adam (a.s) akasema,"Ewe Mola wangu: "Naomba uniongezee" Allah swt akamwambia:"Ninakujaalia kwa ajili ya kizazi chako, TAWBA hadi kufikia pumzi ya mwisho.Na iwapo ataniomba TAWBA wakati huo wa mwisho wake,basi nitaikubalia na kumsamehe!"

Kwa hayo, Mtume Adam (a.s.) alisema: "Ewe Mola wangu! Haya yamenitosha."

Mtume Mtukufu (s.a.w.w.) amesema:
"Ikiwa mtu atakuwa amefanya TAWBA mwaka mmoja kabla ya kifo chake, basi Allah swt ataikubali TAWBA yake, na iwapo mwaka mmoja ulikuwa zaidi kwake, basi hata mwezi mmoja unatosha, na iwapo nayo ilikuwa mbali kwake, basi juma moja latosha, au hata siku moja pia inatosha kumfanya akubaliwe TAWBA yake kabla ya kifo chake. Na iwapo siku hiyo moja pia ilikuwa ni zaidi kwake, basi aombe TAWBA punde kabla ya kifo chake, na hata kama hivyo pia haitawezekana, basi aiombe TAWBA katika pumzi ya mwisho aipumuayo iwapo kooni mwake, basi Allah swt ataikubalia TAWBA yake." (Usuli Kaafi: Mlango wa TAWBA).

Allamah Majlisi (A.R.) anaelezea kwa kutilia mkazo Hadithi hiyo kuwa TAWBA itakubaliwa kwa kutegemea daraja za ukamilifu wake, kwa hivyo ifanywe kila jitihada ili kufikia daraja hizo na tuufanye moyo wetu uwe mweupe kwa nuru na matendo mema na vile vile nyoyo zetu ziwe nyenyekevu. Iwapo mtu hakuweza kufanya TAWBA katika kipindi cha mwaka mmoja kabla hajafariki dunia basi afanye hivyo katika kipindi cha mwezi mmoja. Na iwapo hakubahatika katika mwezi mmoja kabla ya kufariki, basi atubu kabla ya juma moja na kama hivyo pia hakuweza kubahatika, basi atubu siku moja kabla ya kifo chake au saa moja kabla ya kifo chake basi hapo Allah swt atamsamehe madhambi yake yote.

Lakini upo wakati (muayyan) ambao umezungumziwa katika Hadithi kwa ajili ya TAWBA, wakati huo TAWBA hiyo haitofaidisha chochote."

Sheikh Bahai (A.R.) anaandika katika kitabu chake 'Arbain' kuwa 'wakati muayyan' ni wakati ule ambapo mtu huwa anamwona Malaika (wa mauti).Na pia inawezekana kuwa wakati huo mtu anakuwapo katika hali ya maumivu (sakarati mauti) ya mauti na huwezekana kuwa hana fahamu timamu.Maulamaa wote wanaafikiana kuwa TAWBA ifanyiwayo wakati wa mauti ni bure na isiyoweza kumfaidisha.

Kwa hiyo ewe msomaji mtukufu, tufanye TAWBA bado tukiwa na fahamu zetu zilizotimamu, kwani isije ikatokea kuwa TAWBA yetu ingawaje tutaifanya lakini haitakuwa na faida yoyote kwetu!

Allah swt anatuelezea katika Sura an-Nissa Aya 17-18:-

"Toba inayopokelewa na Mwenyezi Mungu ni ya wale wanaofanya uovu kwa ujinga, kisha wakatubia kwa upesi. Hao ndio Mwenyezi Mungu huipokea TAWBA yao.Na Mwenyezi Mungu ni mjuzi na mwenye hekima.

Hawana TAWBA wale ambao hufanya maovu mpaka mauti yamemhudhuria mmoja wao, hapo akasema: "Hakika mimi sasa natubu." Wala hawana TAWBA wale ambao wanakufa katika hali ya ukafiri. Hao tumewaandalia adhabu iumizayo. (4:17-18)