read

Utangulizi

“Uislamu ni dini ya Uovu” “Inatangaza vurugu” Hizi ni nembo za kawaida zinazotumiwa dhidi ya Uislam na vyombo vya habari vya Ukristo wa mrengo wa kulia. Chuki kama hiyo imeegemea kwenye taarifa zisizo na asili, za kihistoria zilizo rudiwa rudiwa, kwa Waarabu waliwaagiza kwa nguvu katika imani ya Uislam wale watu ambao hawakuwa Waarabu. Katika zama zilizopita hivi karibuni halikuwa ni jambo la ajabu kuona vitabu vyenye picha au michoro ya Mwarabu aliyepanda farasi akiwa na upanga katika mkono mmoja na Qur’an katika mkono mwingine.

Hivyo basi hebu tuutazame Uislam jinsi ulivyoenea katika dunia: Ni kwa upanga au kwa mazungumzo?

Mtazamo Wa Qur’ an Tukufu

Hebu kwanza tuangalie suala hili la “ubadilishaji kwa nguvu” kutoka kwenye mtazamo wa Qur’an Tukufu.

1. Qur’an Iko Wazi Kabisa Katika Suala Hili La Kuingia Kwenye Kundi La Kiislam:

“Hakuna kulazimishana katika dini; hakika uongofu umekwisha pambanuka kutoka kwenye upotovu. Basi yule anayemkataa shetani na kumwamini Mwenyezi Mungu, bila shaka yeye ameshika kishikio kigumu kisichovunjika, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mjuzi.” (2:256)

Hapawezi kuwa na kutumia nguvu katika kuukubali Uislam. Wenyewe Uislam unataka waumini waaminifu, sio wanafiki. Kwa kuingizwa kinguvu, wewe utakuwa unaongeza tu idadi ya wanafiki, sio idadi ya waumini wakweli hasa.

2. Mtume Wa Kiislam Ameitwa Vilevile Kama Mkumbushaji, Sio Kama Mtu Ambaye Anaulazimisha Uislam Juu Ya Wengine:

“Basi kumbusha, hakika wewe ni mkumbushaji tu. Wewe si mwenye kuwatawalia wao” (88:21-22)

Katika aya nyingine nyingi, Mtume anaelezewa kama “Mwenye kubeba habari njema” na pia kama “Muonyaji wa adhabu ya Mwenyezi Mungu” (2:119; 34:28) Jukumu lake lilikuwa ni kuwakumbusha tu watu juu ya silika yao ya asili ya kumuamini Mwenyezi Mungu. Kama aya ile ya kwanza ilivyoeleza, nguvu haihitajiki kwa sababu ile njia iliyonyooka iko tofauti kabisa na ile njia iliyopotoka.

Mfano Wa Mtume

Maisha ya Mtume Muhammad (s.a.w.) yanaweza hasa yakagawanywa katika sehemu mbili: (a) Ile miaka kumi na tatu ya mwanzo ya ujumbe wa Mtume kule Makkah, na (b) ile miaka kumi na moja ya mwisho ya maisha yake huko Madina.

Huko Makkah:

Miaka kumi na tatu ya mwanzo ya ujumbe au kazi ya Mtume ilipita akiwa Makkah. Yeye pamoja na Waislam walikuwa na idadi ndogo hapo Makkah; na hivyo matumizi ya nguvu yalikuwa hayawaziki na ni jambo lisilowezekana kihistoria. Yalikuwa ni mateso yaliyomlazimisha yeye kuhama kutoka Makkah kwenda Madina.

Huko Madina:

Ile miaka kumi na moja ya mwisho, Mtume aliishi Madina.

3. Uislamu Ulienea Vipi?

Wengi wa watu wa Madina – waliotokana na makabila ya Aus na Khazraji – walikuwa wameukubali Uislam kabla ya Mtume kuhamia kwake kuja mjini hapo. Ni dhahiri kabisa, kukubali huku au kubadili imani huku kwa watu wa Madina kusingeweza kupatikana kwa nguvu! Mtume na wafuasi wake huko Makkah walikuwa hawana njia ya kuwabadili kinguvu watu wa Madina. Uislam ulienea hapo Madina kupitia kutangazwa kiulinganiaji tu.

Mara alipokuwa amekwishafanya makazi yake hapo Madina, Mtume alitambua kwamba kulikuwa na jamii ndogo ya Kiyahudi katika mji ule ambayo ilikuwa haina mwelekeo wa kuukubali Uislam. Alikutana nao na akawakaribisha kufanya makubaliano na Waislam ili kwamba kila kikundi cha kidini hapo Madina kijue haki zake na wajibu wake. Sehemu husika ya mkataba huo inasomeka kama ifuatavyo:

Wayahudi ambao wanaingia kwenye makubaliano haya watalindwa kutokana na fedheha za aina zote na uchokozi wowote; watakuwa na haki sawa kama za watu wetu wenyewe kwenye misaada yetu na ofisi zetu nzuri. Wale Wayahudi wa makabila mbali mbali ya Aus, Najjar, Harith, Jashim, Tha’labah, Aws, na yote mengine yanayoishi Yathrib (Madina) yataunda pamoja na Waislamu taifa moja mchanganyiko.

Watashughulika katika dini yao kwa uhuru kabisa kama Waislam wafanyavyo. Wateja na washirika wa Wayahudi hao watanufaika na usalama na uhuru ule ule. Wenye hatia watafuatiliwa na kuadhibiwa. Wayahudi wataungana na Waislam katika kuilinda Yathrib (yaani Madina) dhidi ya maadui wa aina zote. Ndani ya Yathrib itakuwa ni sehemu ya heshima kuu kwa wale wote watakaokubali Mkataba huu. Wale wateja na washirika wa Waislam na wale wa Wayahudi watakuwa wenye kuhishimiwa kama wakazi……….

Hii inaonyesha wazi kwamba Mtume hakuwalazimisha watu kuukubali Uislam, bali alieneza kuishi pamoja kwa amani pamoja na wafuasi wa dini nyingine.

Vita Za Wakati Wa Uhai Wa Mtume

Ni vipi Kuhusu vile vita ambavyo Mtume Muhammad (s.a.w.) alivyopigana baada ya kuanzisha mamlaka yake ya kisiasa pale Madina? Je hilo lilikuwa ni kwa lengo la kuulazimisha Uislam juu ya wengine?
Hebu kwa kifupi tutupie macho vile vita muhimu vya zama zile:

Mwaka Wa 2 Hijiria: Vita Vya Badr:

Waislam walikabiliana na majeshi ya Makkah mahali paitwapo Badr, maili 80 kutoka Madina, na maili 200 kutoka Makkah. Mahali penyewe na mazingira yake viko wazi kabisa kwamba wale makafiri wa Makkah walikuwa ndio wachokozi.

Mwaka Wa 3 Hijiria: Vita Vya Uhud:

Vita hivi vimeitwa hivyo kwa jina la mlima nje kidogo tu ya mji wa madina.
Watu wa Makkah walikuja kutoa kisasi kwa ajili ya kule kushindwa kwao kule Badr.

Mwaka 5 Hijiria: Vita Vya Ahzab (Au Khandaq):

Wale makafiri wa Makkah, wakiwa na ushirikiano na Wayahudi wa Arabia ya kaskazini, walikuja kuwashambulia Waislam wa Madina.

Mwaka Wa 6 Hijiria: Mkataba Wa Amani Wa Hudaybiyya:

Mnamo mwaka wa sita baada ya kuhama kwa Mtume, akifuatana na Waislam, yeye aliamua kwenda kuhiji Makkah. Makafiri waliwazuia Waislam kuingia mji wa Makkah. Baada ya mazungumzo marefu, pande zote mbili zilitia saini mkataba wa amani kwa kipindi cha miaka kumi.

Vidokezo vya mkataba huu wa amani vilikuwa na athari pana sana:

Kwanza kabisa, mpaka kusainiwa kwa mkataba huu, Waislam walikuwa wakishughulika zaidi na kujilinda wenyewe dhidi ya watu wa makkah (maadui zao wa nje) na Wayahudi (maadui zao wa ndani).

Pili, ni baada tu ya kusainiwa kwa mkataba huu, ndipo Waislam walipojihisi kuwa salama na bila hofu vya kutosha kuweza kusafiri kwenda mikoani na nchi nyingine nje ya Madina. Mkataba huu wa amani uliwapa Waislamu fursa ya kuanza harakati zilizoandaliwa za kulingania Uislam miongoni mwa makabila na nchi za jirani.

Tatu, kuanzia mwaka ule wa sita wa kuhama kwa Mtume, hadi mwaka wa tisa, kazi kubwa ya ulinganiaji na tablighi ulionekana kiasi kwamba takriban Peninsula yote ya Arabia ikawa imeingia kwenye himaya ya Uislam – bila ya matumizi ya nguvu ya upanga! Matokeo yake, ule mwaka wa tisa ukawa unajulikana kama Amul Wufud – Mwaka wa uwakilishi mwingi: kwa sababu wajumbe wengi wa makabila ya Waarabu walikuwa wakija Madina kutangaza kuukubali kwao Uislam.

Mwaka Wa 9 Hijiria: Kutekwa Kwa Makkah

Ni wakati ule tu watu wa Makkah walipovunja masharti ya mkataba huu wa amani , ndipo Waislam wakautwaa mji wa Makkah bila ya umwagaji wa damu, baada ya hapo, mnamo mwaka wa tisa hijiria mji wa Makkah ukatangazwa kama mji mtakatifu ambamo uabudu masanamu ulipigwa marufuku na kukataliwa kabisa.

Hata hivyo wale waabudu masanamu wa Makkah bado walipewa miezi minne ya muda wa nyongeza wa kukaa na kuuchunguza Uislam. Kama wakiwa bado hawajavutiwa na ujumbe wa Uislam, basi walikuwa waambiwe waondoke kwenye nchi takatifu ya Makkah. (Tazama Qur’an 9:3)

Awamu Mbili Za Maisha Ya Mtume Muhammad

Awamu ya Kwanza
Enzi ya Makkah ya miaka 13 ya mwanzo.
Alikuwa katika idadi ndogo ya watu, hivyo nguvu haiwezekani
Awamu ya Pili
Enzi ya Madina ya miaka 11 ya mwisho ya maisha yake.
Mwaka wa 1 hadi wa 6:
Kujihami na kujilinda dhidi ya uchokozi wa majeshi ya
Makkah na washirika wao.
Mwaka wa 7 hadi wa 9:
Ulinganiaji na kuwafikia wengine kulikoishia katika kusilimisha takriban Peninsula yote ya Bara Arabu.

Katika hali zote kama hizi, tunaona kwamba sio upanga wala nguvu, iliyotumika katika kuwabadili watu kuingia kwenye Uislam. Hususan kwa wale Wayahudi na Wakristo - ambao Uislam unawatambua kama Ahlul-Kitab – watu wa Kitabu, - Uislam uliwahakikishia uhuru wa imani zao na ibada ya kidini chini ya utawala wa Kiislam.

Mapambano Ya Baada Ya Mtume

Baada ya kifo cha Mtume Muhammad, Waislam kidogo kidogo wakazishinda na kuziteka nchi za Iraq, Syria, Palestina, Misri na Iran.
Katika utawala wa Abu Bakr, Iraqi ilitekwa mnamo mwaka 633 Miladia. Wakati wa utawala wa Umar ibn al-Khattab, Syria ilitekwa mnamo mwaka 635 Miladia, Palestina mnamo mwaka 637 Miladia, Misri mnamo mwaka 642 Miladia na vilevile theluthi mbili za Uajemi (Persia) zilitekwa. Sehemu ya Uajemi iliyobakia ilitekwa katika wakati wa utawala wa Uthman bin Affan.

Wanahistoria wengi wanayaangalia mapambano haya ya watawala hawa waliokuja baada ya Mtume kama ushahidi na uthibitisho wa “uingizwaji kwa nguvu kwenye Uislam.” Hata hivyo, sisi tuna mtazamo tofauti juu ya mapambano haya yaliyofanywa na Waislam baada ya kifo cha Mtume. Ni kweli kwamba Waislam waliziteka hizi ardhi na nchi za jirani LAKINI je hii inamaanisha ya kwamba Uislam, dini hii, ilienezwa kwa nguvu?

Utatanishi unaibuka na kujitokeza wakati waandhishi na wanahistoria wanapoutafsiri upanukaji wa Himaya ya Kiislam/ Kiarabu kama upanuzi wa Uislam kama dini.

Ni jambo ambalo halipingiki kwamba ile dola ya Kiislam/ Kiarabu ilipanuka kwa nguvu za kijeshi kote katika Masharikiya Kati; lakini hili halikutafsirika moja kwa moja kwenye kuenea kwa Uislam kama dini.

Ira M. Lapidus katika Kitabu chake “A History of Islamic So- cieties” – Historia ya Jamii za Kiislam – anaandika: “Swali la kwa nini watu wanaingia kwenye Uislam wakati wote limezua hisia kali. Kizazi cha hapo mapema cha wasomi wa ulaya kiliamini kwamba kujiunga kwenye Uislam kulifanyika kwa nguvu kwa ncha ya upanga na kwamba wale watu waliokuwa wametekwa walipewa fursa ya kuchagua kuingia Uislam au kifo.

Sasa hivi ni dhahiri kwamba kusilimu kwa nguvu, sio kwamba hakujulikani ndani ya nchi za Kiislam, kulikuwa ni kwa nadra sana kwa kweli. Watekaji wa Kiislam kwa kawaida walipenda kutawala badala ya kuingiza au kusilimisha watu kwenye Uislam, na uingiaji mwingi kwenye Uislam ulikuwa ni wa hiyari.”1

Katika wingi wa miji, wakazi wake waliendelea kufuata dini zao wenyewe. Wale wateka nchi wa Kiislam walitia saini mikataba ya kuwahakikishia wale watu walioshindwa na kutekwa, uhuru wa kuendesha dini yao madhali tu wakiwa wanatoa au kulipa ile kodi inayotakiwa kwenye hazina ya Khalifa.

Hayati Marshall Hodgson, katika Kitabu chake maarufu kiitwacho “The venture of Islam” – “Ujasiri wa Uislam,” anasema: “Hakukuwa na jaribio la kuwaingiza watu wa nchi za Kifalme kwenye Uislam, ambao karibuni wote walikuwa wafuasi kwenye namna fulani ya dini ya maungamo tayari…….. Katika zile ardhi za kilimo ambazo hazikuwa za kiarabu hasa, lengo halikuwa ni kuwasilimisha watu bali lilikuwa ni utawala…… Ubora wa Uislam kama dini, na kwa hiyo katika kuleta utangamano wa jamii, kungehalalisha utawala wa Kiislam: Kungehalalisha wale Waislam sahihi, waungwana katika kuchukua nafasi ya wale wawakilishi wa wenye wajibu wa siku nyingi matajiri na waonevu.”2

Ira M. Lapidus, anaandika haya yafuatayo katika kitabu kile tulichokitaja mwanzoni, A History of Islamic Societies: Kanuni ya pili…........ilikuwa kwamba wale watu wengi waliotekwa wasumbuliwe kwa kiasi kidogo sana iwezekanavyo. Hii ina maana kwamba wale Waarabu Waislam, kinyume na sifa inayovuma, hawakujaribu kuingiza watu kwenye Uislam.

Muhammad alikuwa ameweka mfano wa kuwaruhusu hao Wayahudi na Wakristo waliokuwa Arabuni kushika dini zao, kama wamelipa kodi, Khalifa; alisogeza haki zile zile huko kwa Wayahudi, Wakristo na zoroasti wa mashariki ya kati ambao walichukuliwa kama “Watu wa Kitabu” wafuasi wa funuo zilizoandikwa zamani……..”3

Upanuzi wa himaya ya waislam/ waarabu dhidi ya upanuzi wa dini ya Kiislam

Sina wasi wasi katika kusema kwamba baadhi ya watawala wa Kiislam (kwa kweli) walipendelea kwamba wale wananchi walioshindwa wafuate dini zao za zamani ili kuhakikisha uingiaji wa mapato yaliyohitajika kwenye hazina zao! Hawakuwa katika shughuli ya kuinua na kuendeleza Uislam; au kuueneza zaidi.

Mifano Kutoka Kwenye Historia Ya Uislam

Historia inatoa uthibitisho wa kutosha kwamba dola za Kiislam zilienezwa kwa nguvu ya kijeshi, lakini hilo halina maana kwamba lazima itafsirike kwamba Uislam ulienea kwa nguvu pia.

1. Angalia Mfano Wa India Waislam waliitawala India kwa takriban miaka 800, lakini kamwe hakukuwa na idadi kubwa ya Waislam katika nchi hiyo. Idadi zenyewe zinaonyesha kwamba nguvu haikutumika kwa upande wa kueneza Uislam katika eneo hilo.

Mwanahistoria maarufu wa India na ambaye ni mwandishi wa habari, Dr. Khuswant Singh, katika Kitabu chake ‘A History of the Sikhs’ – Historia ya Masingasinga amejadili kuusu siku za mwanzo za Uislam huko India. Yeye anaelezea wazi kwamba Uislam ulienezwa huko India sio na watawala wa kiislamu bali na Mabwana wa Kiroho na Mubalighina (wahubiri)4

2. Ichunguze historia ya Mashariki ya mbali (Far East), na utaona kwamba jeshi la Waislam ama kikosii cha wanamaji cha kiislam hakijawahi kutua kamwe huko Malaysia au Indonesia. Hata hivyo ki-idadi ya watu Indonesia ndio nchi yenye idadi kubwa zaidi ya Waislam duniani. Uislam ulienea kule kupitia kwa wafanyabiashara wa kiislam tu, na mubalighina. Lapidus anataja mbinu tatu kuelezea ukubalikaji wa Uislam huko Mashariki ya Mbali: Lile jukumu la wafanyabiashara, umuhimu wa wahubiri (Mubalighina) na thamani ya Uislam kwa watu wa kawaida kuliko kwa lile tabaka la watawala.5Ilikuwa ni kupitia tabia na mwenendo wa wale wafanyabiashara wa Kiislam ambapo watu wa Indonesia walivutiwa kwanza na Uislam.
Hali kama hizo hizo katika kuenea kwa Uislam zimearifiwa kwa ajili ya bara la Afrika.

3.Angalia ile dola ya mwisho ya Kiislam, Himaya ya Othumania “Ottoman Empire.” Ilitawaliwa na khalifa wa Kituruki na ilidhibitiwa na mfumo ulioitwa mfumo wa Millet, jamii ya dini mchanganyiko na utamaduni wa namna nyingi mchanganyiko. Dola ya Othumainia ilimiliki eneo kubwa la ardhi ya Wakristo ndani ya Ulaya Mashariki lakini haukuwalazimisha kamwe raia wa Kikristo kuingia kwenye Uislam; walipewa haki ya kuendesha maisha yao kulingana na desturi zao za kidini. Hebu iangalie Greece (Ugiriki), jirani na Uturuki, ambayo ilitawaliwa na Waislam wa Uturuki kwa takriban miaka 500, lakini husikii kamwe au kuona idadi kubwa kiasi ya Waislam wachache miongoni mwa Wagiriki, hata leo hii.

Kama ingekuwa tulinganishe mwenendo wa watawala wa Kiislam kwa wale watu wachache waliokuwa wanaishi chini ya utawala wao katika kipindi hicho cha karne ya kumi na tisa – pamoja na mwenendo wa Wazungu wa Ulaya na Wamarekani kwa watu wao wachache, nathubutu kusema kwamba ile rekodi ya Waislam itakuwa bora zaidi. Profesa Davison, mwanahistoria maarufu wa utawala wa Othumainiya anaandika hivi:- “Kwa kweli ingeweza kutolewa hoja kuthibitisha kwamba Waturuki walikuwa na uonevu kidogo sana kwa watu wao walio watawala kuliko walivyokuwa wale wa – Prussia wa kule Poles, Waingereza kwa watu wa Ireland, au Wamarekani kwa Wanegro (Wamarekani weusi)…….. Upo ushahidi wa kuonyesha kwamba katika kipindi hiki (yaani mwishoni mwa karne ya 19), walikuwepo wahamaji kutoka Ugiriki huru kwenda kwenye dola ya Othmaniya, kwa vile baadhi ya Wagiriki waliiona ile serikali ya Othmaniya kuwa mmiliki au bwana mwema zaidi (kuliko serikali yao wenyewe ya Kigiriki)”6

4. Uislam unakabiliwa na adui wa kutisha sana katika muundo wa vyombo vya habari vyenye upendeleo wa kibaguzi huko Ulaya na Marekani. Lakini hebu tazama kule kukua na kuenea kwa Uislam huko Magharibi. Licha ya vikwazo vyote, ni mojawapo ya dini zinazokua kwa kasi huko Marekani. Ipo kwa nguvu sana ndani ya Uingereza, Ufaransa na Ujerumani. Hii inatoa ushahidi wa kutosha kuhusu jinsi dini hii ilivyoenea na inaenea hata hivi sasa.

Njia Ya Baadae

Waislam huko Magharibi lazima watambue kwamba majibu ya nguvu sana kwa vyombo vya habari vyenye upendeleo ni tabia yao wenyewe na mwenendo wao. Kama wanatoa taswira ya mwenendo wa Uislam sahihi katika maisha yao ya kila siku, basi hao majirani zao, wafanyakazi wenzao, na wale wanaowafahamu hawataamini simulizi zenye taswira hasi ya Uislam katika vyombo vya habari.

Imam Ja’far as-Saiq (a.s.), Imam wa sita kutoka Ahlul-Bayt amesema: “Waiteni watu kwenye Uislam bila ya kutumia ndimi zenu.” Hii ina maana kwamba, sio kwa maneno bali kwa vitendo – tabia yako ukiwa nyumbani, sehemu ya kazi na miongoni mwa jamii inapaswa kuwa ni njia ya kuulinda na kuonyesha picha ya kweli ya Uislam.

  • 1. Ira M. Lapidus, A History of Islamic Sicieties (Cambridge: CUV, 1988) ukurasa wa 243 – 244.
  • 2. M.Hodgson, “The venture of Islam” Juz. 1, uk. 199
  • 3. A History of Islamic Societies, uk. 43
  • 4. Khushwant Sing, A History of the Sikhs, Juz.1 (N.J: Princeton University Press, 1963) uk. 20-28
  • 5. A History of Islamic Societies, uk. 469
  • 6. Roderic H. Davison, Reform in the Ottoman Empire 1856 – 1876 (New Jersey: Princeton University Press, 1963) uk. 116