Aya 94 – 96: Hakuna Kuwinda Katika Haram Wala Pamoja Na Ihram
Maana
Enyi Mlioamini! Hakika Mwenyezi Mungu atawajaribu kwa baadhi ya mawindo yanayofikiwa na mikono yenu na mikuki yenu.
Makusudio ya baadhi ni mawindo ya bara tu. Kauli yake Mwenyezi Mungu yanayoafikiwa na mikono yenu na mikuki” ni fumbo la kuwinda, bila ya shaka. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameharamisha kuwinda bara katika Haram1 na katika hali ya Ihram2 jambo ambalo ni jepesi; sawa na alivyowaharimishia Wana wa Israil kuvua samaki siku ya Jumamosi (sabato).
Ili Mwenyezi Mungu amjue ni nani anayemwogopa kwa ghaibu,
Yaani Mwenyezi Mungu amewajaribu kwa kuharamisha kuwinda katika hali hii ili ampambanue yule anayemwogopa katika siri kama yule anayemtii katika dhahiri na yule anayejionyesha kwa kumtii na kum- wogopa mbele ya watu na kumwasi katika uficho.
Basi atakayeruka mipaka baada ya hayo, atapata adhabu iumizayo.
Yaani mwenye kuhalifu amri ya Mwenyezi Mungu kwa kuwinda baada ya ubainifu huu na hoja, basi atastahiki adhabu ya Mwenyezi Mungu na mateso.
Maana Ya Kujaribu Kwa Mwenyezi Mungu
Unaweza kuuliza kuwa kwa Mwenyezi Mungu halifichiki lolote lilo katika ardhi wala katika mbingu; sasa kuna wajihi gani wa kauli yake Mwenyezi Mungu:
"Hakika Mwenyezi Mungu atawajaribu, na kauli yake: "Ili Mwenyezi Mungu amjue anayemwogopa."
Jibu: Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t) hamjaribu mja wake ili ajue ambayo hakuwa akijua, hapana! Kwani yeye anamjua zaidi kuliko yeye mwenyewe. Isipokuwa anamtia mtihani kwa mambo mengi; kama haya yafuatayo:-
Kuyafasiri yale yalioko katika nafsi ya mja yajitokeze. Ambapo hekima imepitishwa kutowahisabu watu kwa yale anayoyajua kwao wala yale yanayokuwa katika nafsi zao katika silika. Isipokuwa atawahisabu na matukio ya matendo. Silika ya kinafsi peke yake haina haja ya kuhisabiwa wala kupewa adhabu, maadam iko ndani tu ya binadamu na athari yake haionekani kwa macho au kusikiwa kwa masikio.
Imam Ali anasema: "Mwenyezi Mungu anasema: Jueni kuwa mali zenu na watoto wenu ni fitna. Maana yake ni kuwa anawajaribu kwa mali na watoto ili abainike mwenye kuichukia riziki yake na mwenye kuridhia ugawanyo wake, ingawaje Mwenyezi Mungu (s.w.t) ni mjuzi zaidi kuliko nafsi zao, lakini ni kudhihirisha vitendo ambavyo vinastahiki thawabu na adhabu.
Kumpambanua mwovu na mwema na kuidhihirisha hakika yake mbele ya watu na kumchukulia vile anavyostahiki.
Na hayo, mara nyingi sana, hutokea katika maisha ya watu. Kwa mfano wewe unajua Zedi ni katika watu wa elimu na maarifa. Ikawa yeye yuko baina ya watu wasiojua ujuzi wake, nawe ukataka wajue mwamko wake na elimu yake. Kwa hiyo ukamuuliza mbele ya watu, ili aseme na ajulikane.
Au pengine unajua kwamba yeye ni duni mjinga, na watu wanamdhania kuwa ni mjuzi mwenye hekima. Kwa hiyo ukafanya hivyo hivyo udhihirishe ujinga wake na uduni wake.
Watu wengi wao wenyewe hawajijui na wanasema : lau tungelikuwa na hali fulani, basi tungefanya kadha wa kadha. Kwa hiyo Mwenyezi Mungu huwapa uwezo na fursa ili awe na hoja juu yao na ijulikane hakika yao na hali yao. Mwenyezi Mungu anasema: "Na miongoni mwao wako waliomwahidi Mwenyezi Mungu kuwa: Akitupa katika fadhila zake, kwa hakika tutatoa sadaka na kwa hakika tutakuwa katika wanaotenda mema. Alipowapa katika fadhila yake wakaifanyia ubakhili na wakageuka na huku wao wanapuuza" (9:75-76)
Wana wa Israil walimtaka Musa awafanyie siku ya kupumzika na kufanya ibada. Mwenyezi Mungu akawajaalia siku ya Jumamosi (sabato). Wakaahidi kutofanya chochote siku hiyo; kama walivyotaka, lakini ikawa samaki wanawajia sana siku hii na inapokwisha Jumamosi na samaki nao hupotea. Wana wa Israil wakafanya hila ya kuwavua na wakavunja ahadi.
Kwa hiyo kwenye wajihi wa kwanza tulioueleza - kudhihiri vitendo vinavyostahiki thawabu na adhabu, ndiyo yamechukuliwa maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu "Hakika atawajaribu Mwenyezi Mungu, ili amjue Mwenyezi Mungu anayemwogopa. Na ili awajue Mwenyezi Mungu wale walioamini" na mfano wa Aya hii.
Enyi mlioamini! Msiue windo na hali mko katika Ihram.
Wameafikiana Mafakihi kwamba kuwinda ndani ya Haram haijuzu kwa aliye katika Ihram na asiye katika Ihram. Ama nje ya Haram inajuzu kuwinda kwa asiyekuwa katika Ihram. Lau atachinja aliye katika Ihram windo basi litakuwa ni mfu ulio haramu kuliwa na watu wote.
Imeelezwa katika Kitab Fiqhu Sunna cha Sayyid Sabiq kwamba mpaka wa Haram ya Makka kwa upande wa Kaskazini ni sehemu inayaoitwa Tani'm, kilomita 6 kutoka Makka. Upande wa kusini ni mahali panapoitwa Ardhah, kilomita 12. Upande wa Mashariki ni Ja'rana kilomita 15.
Na miongoni mwenu atakayemua kwa kusudi, basi malipo (yake) yatakuwa ni mfano wa aliyemuua katika wanyama wa kufugwa, kama watakavyo hukumu waadilifu wawili miongoni mwenu. Mnyama apelekwe Al-K'aaba (kama sadaka); au kutoa kafara kwa kuwalisha masikini au badala ya hayo ni kufunga.
Mwenye kuwa katika Ihram akiuwa, au akiwa hayuko katika Ihram, laki- ni ameuwa ndani ya haramu, basi ikiwa mnyama aliyemuuwa ana mfano katika aina tatu za wanyama wa kufugwa - Ngamia, Ngombe, Kondo au Mbuzi, basi atakuwa na hiyari ya kuchinja mfano wa mnyama aliyeuliwa na mtoe sadaka; au kutoa thamani ya mnyama anyefanana na aliyemuua. Anunue chakula na kukitoa sadaka kwa masikini kila masikini vibaba viwili, kilogram 1.6 takriba. Wengine wamesema kuwa atatoa kibaba kimoja, au afunge kwa kila vibaba viwili siku moja, au kwa kila kibaba kimoja kulingana na kauli nyingine.
Maana ya "Kama watakavyohukumu waadiifu wawili" ni kushuhudia watu wawili waadilifu, kuwa mnyama huyu wa kufuga ni sawa na mnyama aliyeuawa.
Maana ya "Mnyama apelekwe Al-Kaaba" ni kuchinjwa huyo mnyama jirani ya Al-Kaaba na kutolewa nyama yake kwa masikini.
Ikiwa hakupata mfano katika aina zile tatu za wanyama wa kufugwa, basi atatoa kima cha mnyama mwingine wa kufugwa na anunue chakula na kukitoa sadaka; au kufunga, kwa ufafanuzi uliotangulia.
Ili aonaje ubaya wa jambo lake.
Kuwinda katika Haram au katika hali ya Ihram ni kuvunja mwiko wa Mwenyezi Mungu, kwa hiyo ndio akaadhibiwa mwindaji kwa kafara hiyo iliyotajwa. Maana ya ubaya wa jambo lake, ni mwisho wa kitendo chake kibaya.
Mwenyezi Mungu amekwishayasamehe yaliyopita; ya kuwinda kabla ya kuharamishwa. Na atakayerudia kuwinda, Mwenyezi Mungu atampa adhabu kwa kung'ang'ania kwake dhambi.
Mmehalalishiwa kuvua baharini na chakula chake, kwa manufaa yenu na kwa wasafiri.
Dhamiri katika chakula chake inarudia bahari, kwa sababu mna vinavyoliwa visivyo vuliwa. Inawezekana kuwa dhamiri inarudia kinachovuliwa; na maana yawe Mwenyezi Mungu (s.w.t) amehalalisha kuvua na kula vilevile. Makusudio ya wasafiri ni wale wasiokuwa katika Ihram.
Na mmeharamishiwa kuwinda bara maadamu mko katika Ihram.
Yaani kuvua baharini ni halali kwa hali yoyote. Imam Jafar Assadiq anasema. Usihalalishe chochote katika mawindo - ya bara - ukiwa katika Ihram. Wala usipokuwa katika Ihram pia usimfahamishe aliye katika Ihram au asiye katika Ihram, akawinda na wala usimwonyeshe kwani katika hayo kuna fidia kwa mwenye kufanya makusudi.
Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye kwake mtakusanywa.
Yaani jitahidi ni katika kumtii na kutafuta radhi zake, ili awalipe wema siku ya ufufuo.
جَعَلَ اللَّهُ الْكَعْبَةَ الْبَيْتَ الْحَرَامَ قِيَامًا لِلنَّاسِ وَالشَّهْرَ الْحَرَامَ وَالْهَدْيَ وَالْقَلَائِدَ ۚ ذَٰلِكَ لِتَعْلَمُوا أَنَّ اللَّهَ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ وَأَنَّ اللَّهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ {97}
اعْلَمُوا أَنَّ اللَّهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ وَأَنَّ اللَّهَ غَفُورٌ رَحِيمٌ {98}
مَا عَلَى الرَّسُولِ إِلَّا الْبَلَاغُ ۗ وَاللَّهُ يَعْلَمُ مَا تُبْدُونَ وَمَا تَكْتُمُونَ {99}