Mkakati Wa 2: Kujikumbusha Juu Ya Allah (S.W.T.)

Moja ya sababu za kwa nini Adhana na Iqama zimesisitizwa sana kabla ya Swala ni kusimamisha kiungo imara kati ya mwenye kuabudu na Muumba wake, kabla hajajasiri kwenye safari hii takatifu Swala na kuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na Mwenyezi Mungu. Kwa njia hii, unaanza kujikumbusha na kujihakikishia wewe mwenyewe juu ya kuwepo kwa Allah (s.w.t.) kabla hujaianza Swala:

إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ لَآيَاتٍ لِأُولِي الْأَلْبَابِ {190}

الَّذِينَ يَذْكُرُونَ اللَّهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىٰ جُنُوبِهِمْ وَيَتَفَكَّرُونَ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ رَبَّنَا مَا خَلَقْتَ هَٰذَا بَاطِلًا سُبْحَانَكَ فَقِنَا عَذَابَ النَّارِ {191}

Hakika katika kuumba mbingu na ardhi, na kutofautiana kwa usiku na mchana, ni dalili kwa watu wenye akili. Ambao humkumbuka Mwenyezi Mungu wakiwa wamesimama wima, na wakiwa wamekaa, na wakilala, na wanatafakari juu ya kuumbwa kwa mbingu na ardhi, (wakisema) Mola wetu! Hukuviumba hivi bure tu, utukufu ni Wako, basi tuepushe na adhabu ya Moto. (3:190-191)

Mwanachuoni mkubwa, al-Mutahhari (r.a.) ananukuu Hadithi, ambayo imerejewa ndani ya kitabu kiitwacho The Light Within Me:

“Madhumuni ya Dhikr – kumkumbuka Allah (s.w.t.) ni kwamba moyo wakati wote uwe unalitambua al-Haqq, Jina la Mwenyezi Mungu (s.w.t.), yaani, Mkweli Zaidi, kwani kulitumia kwake kunaondosha ile hali ya kutokuwa makini.”
Dhikr zina umuhimu kama ule wa maji yalivyo kwa chembe hai ndani ya mwili wako.

Chukulia kwa mfano, ile hewa unayovuta mchana na usiku, ambayo kwayo uhai wako na vilevile ule wa viumbe hai vingine unategemea, hakuna kinachoweza kubakia hai bila hiyo hewa. Ni zawadi nzuri ya ajabu iliyoje. Kama viumbe vyote vingepanga kitu kama hicho, haviwezi kulifanya hilo.

Na hilo linaingia hata kwenye zawadi nyingine ambazo tumezawadiwa bila wasiwasi wowote, kutoka kwa Mwenyezi Mungu (kama vile kuona, kusikia, kuonja na kadhalika), kila mojawapo ikiwa na faida zisizo na ukomo.

Anakutimizia mahitaji yako katika dunia hii na ya akhera, bila kuhitajia kuabudu kwako. Kuzishika amri Zake au kuzivunja hakuleti tofauti yoyote Kwake. Ni kwa ajili ya faida yako mwenyewe kwamba Yeye ameamrisha mema na kukataza maovu.

Imam al-Khumeini (r.a.) anaelezea kwamba ‘unapoyakumbuka yote haya, je, huoni kwamba kumheshimu na kumtii Mfadhili kama huyu ni muhimu juu yako? Yeye ndiye Muumba na Mfalme wa ulimwengu huu mkubwa, ambao kutokuwa na kikomo kwake hakuwezi kupimwa au kufikiwa na akili ya mwanadamu.

Sisi wanadamu, viumbe tunaotambaa juu ya moja ya sayari ndogo, kwa huzuni sana tunashindwa kufahamu eneo la udogo wa dunia yetu wenyewe, ambayo jua lake haliwezi kulinganishwa na majua ya makundi ya nyota yasiyo na idadi.

Mfumo wetu wa jua na sayari zake si chochote ukilinganishwa na mifumo midogo mingine ya jua, ambayo bado inayatatiza macho makini ya wavumbuzi wakubwa na wachunguzi wa dunia.’

Tumeshauriwa na wanavyuoni wa kiislamu kujaribu kumkumbuka Allah (s.w.t.) wakati wote unaowezekana. Hii ni pamoja na kukariri baadhi ya nyiradi za ibada na kujifunga, au inaweza kuwa namna ya tafakari, kuthamini dunia hii na ile ya akhera.

At-Tabatabai (r.a.) katika kitabu chake, al-Mizan, Juzuu ya Pili, anaelezea namna ya kuishi ambayo ni furaha zaidi na maisha ambayo ni yenye kudumu zaidi. Katika simulizi hii, ad-Daylami anasimulia katika al-Irshad yake kwamba Allah (s.w.t.) katika hatua moja wakati wa Mi’raj, alimwambia Mtume (s.a.w.w.):

“Na kwa njia ya furaha ya namna ya kuishi, ni ile ambayo ndani yake mtu hachoki kunikumbuka Mimi, hasahau neema Zangu, na hapuuzi haki Zangu (juu yake). Anazitafuta radhi Zangu mchana na usiku.

Uhai wa milele unatambulika pale mtu anapotumikia manufaa yake ya kiroho mpaka dunia ikapoteza umuhimu kwake yeye, na ikaonekana ni ndogo machoni mwake. Akhera inakuwa ndio kubwa kwake.

“Anatoa kipaumbele kwenye radhi Zangu kuliko kwenye matamanio yake; anazitafuta radhi Zangu; anaifikiria haki ya neema Yangu kuwa ni kubwa; anakumbuka akilini mwake yale Niliyomfanyia yeye (yaani, kwa manufaa yake); ananikumbuka Mimi mchana na usiku kila anaposhawishika kutenda ovu lolote lile au dhambi; anauweka moyo wake safi kutokana na yale ninayoyachukia Mimi; anamlaani shetani na minong’ono yake, na hamruhusu shetani kuanzisha ushikiliajia,au njia ya kuingilia kwenye moyo wake.

“Anapofanya namna hii, basi Mimi huweka mapenzi Yangu kwenye moyo wake, mpaka Ninaufanya moyo wake na vilevile mapumziko na kushughulika kwake, na mawazo na kauli zake, kuwa sehemu ya fadhila Zangu ambazo Nimezishusha juu ya wale miongoni mwa viumbe Wangu wanaonipenda; na Ninalifungua jicho na sikio la moyo wake, ili awe anasikia kwa moyo wake na anaangalia kwa moyo wake kwenye Utukufu na Ukuu Wangu; na Ninaifanya dunia kuwa nyembamba juu yake na kumfanya aichukie pamoja na starehe zake zote; na Ninamtahadharisha juu ya dunia na vyote ilivyonavyo, kama mchungaji anavyowazuia kondoo wake kwenye ardhi ya malisho yenye hatari.

“Hili linapotokea, anawakimbia watu na anahama kutoka kwenye nyumba ya kumalizia na kwenda kwenye makazi ya milele, na kutoka kwenye nyumba ya shetani kwenda kwenye Makao ya Allah (s.w.t.), Mkarimu. Ewe Ahmad! Mimi ninampamba na heshima na utukufu. Hivyo, hii ndio njia nzuri ya kuishi na ya maisha ya milele, na ndio hali ya wale ambao wameridhika (Nami).

“Kwa hiyo, yeyote atakayetenda kwa ajili ya radhi Zangu, Mimi humpa sifa tatu: Ninamfundisha shukrani, ambayo haikuchafuliwa na ujinga, ukumbusho, ambao haukuchanganyika na usahaulifu, na upendo ambao unachukua kipaumbele juu ya mapenzi ya viumbe. Kisha pale anaponipenda Mimi, Nami ninampenda na kulifungua jicho la moyo wake kwenye Utukufu Wangu. Sivifichi viumbe (Vyangu) maalum kwake yeye. Ninazungumza naye sirini katika giza la usiku na mwanga wa mchana, mpaka anakoma kuongea na kukaa na viumbe.

“Ninamfanya ayasikie maongezi Yangu na maneno ya Malaika Wangu. Ninaifanya siri Yangu ijulikane kwake, ambayo Nimeifanya ifichikane kwa viumbe (Wangu) wote. Ninamvalisha kwa kadiri, mpaka viumbe wote wawe na staha juu yake.

Anatembea katika ardhi (na madhambi yake yote yakiwa) yamesamehewa. Ninaufanya moyo wake kuwa wenye kusikia na kuona, na simfichi kitu chochote cha Peponi au Motoni. Ninayafanya yajulikani kwake, hofu na mateso yanayowangojea watu hiyo Siku ya Kiyama, na kuhusu mambo ambayo Nitawauliza matajiri na masikini, vilevile wasomi na wajinga.

“Nitamfanya alale (kwa amani) ndani ya kaburi lake, na Nitawatuma Munkar na Nakir (a.s.) kwenda kumuuliza maswali. Hatapatwa na huzuni ya kifo au tishio la utangulizi (la dunia ijayo). Kisha nitaisimamisha mizani yake ya vipimo kwa ajili yake, na nitakikunjua kitabu chake (cha matendo). Halafu nitakiweka kitabu chake kwenye mkono wake wa kulia na atakisoma kikiwa kimekunjuliwa. Tena Sitaweka mkalimani yoyote kati Yangu na yeye.

“Hivyo hizi ndio sifa za wapenzi. Ewe Ahmad! Fanya shughuli yako kuwa shughuli moja, fanya ulimi wako kuwa ulimi mmoja, na ufanye mwili wako (yaani, nafsi yako) kuwa hai ambayo kamwe haiwi yenye kutokunikumbuka (Mimi). Yeyote ambaye hanikumbuki Mimi, Sitajali ni kwenye bonde gani anakopotelea.”