Mkakati Wa 8: Kuendeleza Usafi

Kipengele muhimu na cha kuvutia sana cha mafunzo ya Uislamu kinahusiana na usafi. Ina maana kuwa na kawaida ya kuwa tohara wakati wote kwa kutia wudhu na kuoga majosho (ghusl) makuu kila inapokuwa lazima.

Josho kubwa (ghusl) siku ya Ijumaa, kwa mfano, limesisitizwa sana na linasafisha nafsi yako kutokana na madhambi mengi. Kwa kujiweka mwenyewe msafi na tohara, unafanya iwe vigumu kwa Shetani kuingi kwenye nafsi yako. Usafi ni kizuizi kinachozuia mawazo ya tamaa na fikira zinazovuruga kuingia kwenye akili yako wakati wa Swala. Moja ya Hadithi za Mtume (s.a.w.w.) ambayo imetufikia kama mfano halisi wa kudumu milele ni kwamba: “Unadhifu ni sehemu ya imani, na imani humuongozea mtu kwenda Peponi.”

Kwa hiyo, ni jambo zuri kupiga mswaki meno yako, kujitia manukato, na kufuata namna fulani ya sare, bora zaidi nyeupe, na kusimama mbele za Allah (s.w.t.), ukiwa mchangamfu na nadhifu. Unadhifu ni silaha ya mu’min na inaamsha hisia za ndani kabisa.

Sehemu hii ya swala yako inaweza kuhusisha chochote kati ya vipengele vifuatavyo: mara kwa mara kuvaa nguo safi nyeupe wakati wa Swala, kutumia manukato, kuchoma ubani, kutumia mkeka safi wa kuswalia na chumba nadhifu cha kuswalia, kuomba maghfira kabla ya swala, na kadhalika. Vipengele vyote vilivyotajwa hapo juu vinatengeneza mazingira mazuri na ya kiroho kwa ajili ya swala.