Mkakati Wa 18: Subira, Kukiri Makosa, Na Kulieleza Tatizo Kwa Allah (S.W.T.)

Ni lazima uwe na subira katika utekelezaji wako wa uzingativu. Hufanyi kwa ustadi kabisa ile mara ya kwanza katika mazingira yoyote yale. Ni uendelezaji wa tafakari, utulivu na uzingatiaji ndivyo vitakavyoleta manufaa. Usitegemee manufaa ya dhahiri katika muda mfupi.

Kumuomba Allah (s.w.t.) na kumueleza matatizo yako ya kutokuwa makini ni mazoea mazuri, kwani kwa hakika Yeye atakusaidia katika jambo hili.

Subira ni muhimu pale tunapotaka kufanya matendo ya utiifu kwa ajili ya mapenzi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu (s.w.t.), kama Yeye alivyosema:

“Kwa hakika hamtakipata kile Ninachokimiliki, bali kwa kuwa na subira katika mambo yale, ambayo hamyapendi (lakini bado mnayafanya) ili kuzitafuta radhi Zangu. Subira katika utii juu Yangu ni nyepesi juu yenu kuliko subira katika Moto wa Jahannam. (Hadith al-Qudsi)

Wakati wowote unaponuia kufanya tendo jema, mara moja Shetani anakuwa pale kukushawishi usilifanye. Anaweza akakufanyia vitimbi na kukushawishi usilifanye tendo hilo, lakini unapaswa kuwa makini. Lazima uweze kuvitambua vitimbi hivi na kuvitupilia mbali.

Kuyabaini maingilio yake kwenye nafsi yako ni njia inayofaa sana ya kutatulia suala hili. Na kama Shetani hatafanikiwa katika kukushawishi kutolifanya tendo fulani la utii, basi atajaribu kwa juhudi zake zote kukufanya ulitende haraka haraka na kwa umakinifu mchache sana.

Ni tofauti kubwa kiasi gani iliyopo kati yetu na wale waja watiifu wa Allah (s.w.t.) ambao wanavipokea vitendo vya ibada, na kuvishughulikia kwa furaha kabisa na kuvitimiza kwa ufanisi kabisa. Sisi tunafikiri Mwenyezi Mungu Mtukufu ametutwisha majukumu mazito, na tunayachukulia kama ni usumbuvu na tunayaona kama ni uzito. Kwa kweli hivi sivyo kabisa ilivyo.

Imam Khumeini (r.a.) anasimulia kwamba subira ipo ya namna tatu:

Subira wakati wa huzuni; Subira kuhusu utiifu; Subira kuhusu uasi. Mtu anayestahimili huzuni kwa subira, akaizuia kwa maliwazo mazuri, Allah (s.w.t.) humnyanyua yeye kwa kiwango cha nyuzi 300, mwinuko wa nyuzi moja juu ya nyingine ukiwa kama umbali kati ya ardhi na mbingu.

Na yule ambaye yu mwenye subira kuhusu utiifu, Allah (s.w.t.) humnyanyua kwa kiwango cha nyuzi 600, mwinuko wa nyuzi moja juu ya nyingine ukiwa kama umbali kati ya kina cha ardhi na Arshi.

Na yule ambaye ana subira kuhusu uasi, Allah (s.w.t.) humnyanyua kwa kiwango cha nyuzi 900, mwinuko wa nyuzi moja juu ya nyingine ukiwa kama umbali kati ya kina cha ardhi na mipaka ya mbali kabisa ya Arshi.