Sura Ya 33: Matukio Ya Mwaka Wa Tatu Na Wa Nne Hijiriya

Athari za kisiasa za kushindwa walizozipata Waislamu kwenye vita ya Uhud zilidhihirika kabisa mwishoni mwa vita vile. Ingawa walionyesha uthabiti mbele ya yule adui mwovu, na wakayazuia marejeo yake (mjini Madina), lakini baada ya tukio la Uhud fitina za ndani na za nje na kujaribu kupindua Uislamu viliongezeka.

Wanafiki na Wayahudi wa Madina na washirikina waishio nje ya mji pamoja na makabila yanayoabudu masanamu waishio mbali nao walipata shauku isiyo ya kawaida, nao hawakuacha kupanga makri na kukusanya askari na silaha dhidi ya Uislamu.

Mtume (s.a.w.w.) alizinyamazisha fitina za ndani kwa ustadi mkuu, na akakomesha kwa kuyapelekea vikosi yale makabila yaishio nje, yaliyotaka kuushambulia mji wa Madina. Wakati huo huo ilipokewa taarifa ya kwam- ba kabila la Bani Asad lilijaribu kuuteka mji wa Madina na kuwaua Waislamu na kuziteka nyara mali zao.

Upesi sana Mtume (s.a.w.w.) alipeleka kikosi cha askari 150 chini ya uongozi wa Abu Salman kwenye makao makuu ya wahaini. Alimwamrisha yule kamanda wa kikosi hiki alifiche lengo lake, asafiri kwa njia iliyopindapinda na kupumzika wakati wa mchana na kusafiri wakati wa usiku. Alifanya kama alivyoagizwa na Mtume (s.a.w.w.) na wakalizingira kabila la Bani Asad wakati wa usiku, wakaikomesha makri ile tangu mwanzoni kabisa, na wakarejea Madina wakiwa ni washindi wakiwa na ngawira za vita. Tukio hili lilitokea katika mwezi wa 35 wa Hijiriya.

Mpango Wa Kistadi Wa Kuwauwa Wahubiri

Mtume (s.a.w.w.) aliivuruga mipango ya wahaini kwa kupeleka vikosi, na akayavutia makabila adilifu kwenye Uislamu kwa kuvipeleka vikundi vya wahubiri kwenye makabila mbalimbali na vituo vya maeneo yenye watu wengi.

Wahubiri waliofunzwa na walioihifadhi Qur’ani Tukufu pamoja na amri na Hadith za Mtume (s.a.w.w.) walitayarishwa kwa moyo na nafsi kwenda kuwabalighishia mafunzo ya Uislamu wakazi wa yale maeneo ya mbali, kwa ufafanuzi na adabu njema, kwa gharama ya maisha yao wenyewe.

Kwa kuvipeleka vikosi vya kijeshi na vikundi vya wahubiri Mtume (s.a.w.w.) aliyatekeleza majukumu mawili makuu yahusianayo na cheo kikuu cha Utume. Kwa hakika lengo la kuvipeleka vikosi vya kijeshi lilikuwa ni kudumisha amani na kufutilia mbali hali ya hatari na vurugu ili kwamba lile kundi la wahubiri liweze kulitekeleza jukumu lake la kuzitawala nyoyo na kuziongoza fikara za watu kwenye hali ya hewa ya amani na uhuru.

Hata hivyo, baadhi ya makabila ya kishenzi na duni yalifanya udanganyifu dhidi ya lile kundi la wahubiri, lililokuwa la jeshi la kiroho la Uislamu na ambao hawakuwa na lengo lolote jingine ila maendeleo ya haki na uhuru na kuondoa ukafiri na ibada ya masanamu. Waliwauwa katika hali ya kuhuzunisha mno. Hapo chini tunatoa maelezo ya kile kilichotokea kwa baadhi ya hawa wahubiri wa Kiislamu waliofunzwa, ambao idadi yao kwa mujibu wa Ibn Hisham walikuwa sita, na kwa mujibu wa Ibn Sa’ad walikwua kumi.

Mauwaji Ya Kikatili Ya Wahubiri Wa Uislamu

Kikundi cha wawakilishi wa makabila yaliyokuwa yakiishi kwenye mae- neo ya jirani yalifanya udanganyifu ili kuidhoofisha nguvu ya Uislamu na kulipiza kisasi. Walimjia Mtume (s.a.w.w.) na kusema: “Ewe Mtume wa Allah! Nyoyo zetu zinauelekea Uislamu na mazingira yetu yako tayari kwa kuupokea. Ni muhimu kwamba uwatoe baadhi ya masahaba zako twende nao ili wakauhubiri Uislamu miongoni mwa kabila letu na kutufundisha Qur’ani Tukufu na kutueleza mambo yaliyohalalishwa na yaliyoharimishwa na Allah.”1

Ulikuwa ni wajibu wa Mtume (s.a.w.w.) kulikubalia kundi hili la wawak- ilishi wa makabila makuu, na Waislamu wanao wajibu wa kuitumia fursa ya aina hiyo kwa vyovyote vile.
Hivyo Mtume (s.a.w.w.) aliamrisha kikundi cha wahubiri waende kwenye maeneo hayo chini ya uongozi wa Marsab, pamoja na wale wawakilishi wa yale makabila.

Kikundi hiki kilifuatana na wale wawakilishi wa yale makabila, waliutoka mji wa Madina na wakaenda hadi wakalitoka eneo lililoko chini ya mamlaka ya Waislamu hata wakafika mahali paitwapo Raji. Hapo wale wawakilishi wa yale makabila walionyesha nia yao mbaya na kwa msaada wa kabila moja lililoitwa Huzayl, waliamua kuwafunga na kuwaua wale watu waliotumwa na Mtume (s.a.w.w.). Wakati ule Waislamu wakiwa wamezungukwa pande zote na kikundi chenye silaha hawakuwa na njia yoyote ya kujihami. Hawakuwa na chochote cha kufanya bila ya kufuta panga zao.

Hivyo basi, wakazifuta panga zao na wakawa tayari kujitetea. Hata hivyo, maadui zao waliapa kwamba hawakuwa na lengo lolote ila kwamba wawafunge ili kwamba wawapeleke kwa wakuu wa Waquraishi wakiwa hai na waweze kupata pesa, ikiwa ni zawadi yao.

Waislamu walitazamana na wakaamua kupigana. Hivyo, walijibu kwamba hawazitegemei ahadi za washirikina na waabudu masanamu, na kisha wakaamua kushika silaha na wakayatoa maisha yao kishujaa katika njia ya mahubiri na ulinzi wa Uislamu. Hata hivyo watu watatu, Zayd bin Dasinah, Khubayb Adiy na Taarah, walizichomeka silaha zao alani na wakajisalimisha. Walipokuwa njiani Taarah alijuta na akaona aibu kwa kujisalimisha kwake. Hivyo alifaulu kuutoa mkono wake kwenye nyororo, akaushika upanga mkononi mwake na kuanza kuwashambulia wale maadui. Wale maadui walianza kurudi nyuma na wakamfanya ashindwe kwa kumvurumishia mawe. Walimpiga mno mawe kiasi kwamba alianguka chini na akafariki dunia kutokana na majeraha. Alizikwa kwenye sehe- mu hiyo hiyo.

Hata hivyo, wale wafungwa wengine wawili walifikishwa kwa maafisa wa Kiquraishi wenye mamlaka nao kama fidia, wafungwa wawili wa kabila lile lililokuwa limewafunga wale waislamu waliachiwa huru.

Safwan bin Umayyah, ambaye baba yake aliuawa kwenye Vita vya Badr alimnunua Zayd ili alipize kisasi cha baba yake. Iliamuliwa kwamba Zayd anyongwe mbele ya mkutano mkuu wa watu. Miti ya kunyongea ikawek- wa mahali paitwapo Tan’im2

Waquraish na marafiki zao walikusanyika mahali hapo katika siku maalumu. Yule mtu aliyehukumiwa kunyongwa alisimama kandoni mwa ile miti ya kunyongea na dakika chache tu za uhai wake zilimbakia, wakati Abu Sufyan, aliyekuwa Firauni wa Makka na ambaye mkono wake ulikuwa ukifanya kazi nyuma ya pazia kwenye matukio yote haya alimgeukia Zayd na akasema: “Ninakutaka uniapie kwa jina la yule Mola unayemwamini kama unapenda kwamba Muhammad angaliuawa badala yako nawe ukaachiliwa huru na ukarudi nyumbani.” Zayd alijibu kwa ushujaa akisema: “Sitaki japo kwamba mwiba uchome mguu wa Mtume, ingawa ningaliweza kuachiliwa kwa hilo.” Jibu la Zayd lilikuwa na athari kubwa kwa Abu Sufyan. Alishangazwa na kujitolea kusiko kifani kwa masahaba wa Mtume (s.a.w.w.) na akasema: “Maishani mwangu mwote sijapata kuwaona marafiki wa mtu yeyote walio waaminifu na wenye kujitoa mhanga kama wale wa Muhammad!’

Mara tu baada ya hapo Zayd alinyongwa kwenye ile miti ya kunyongea na roho yake ikatoka kuuendea ulimwengu wa Akhera. Aliyatoa mhanga maisha yake kwa ajili ya Uislamu.

Yule mtu wa pili Khubayb aliwekwa kifungoni kwa muda fulani. Baadaye Halmashauri ya Makka iliamua kwamba yeye naye anyongwe pale Tan’im.3 Matayarisho yalifanywa kuiweka tayari ile miti ya kunyongea. Akiwa amesimama karibu na miti ile, Khubayl aliomba ruhusa kutoka kwa wale maafisa wenye mamlaka ili asali rakaa mbili. Baada ya kuruhusiwa alisali ile sala ya rakaa mbili kwa ushujaa mkubwa na kamilifu.

Kisha akarejea kwa wale machifu wa Waquraishi na kusema: “Kama isingalikuwa kwamba mnanifikiria kwamba nilikuwa nikukiogopa kifo, ningalisali zaidi4 na ningalizirefusha rukuu na sujuud (kurukuu na kusujudu) za sala hizo.” Kisha aliuinua mbinguni uso wake na akasema: “Ee Allah! Tumefanya wajibu tuliyopewa na Mtume.” Ilitolewa amri na Khubay akanyongwa hadi akafa. Alipokuwa kwenye ile miti ya kunyongea alisema: “Ee Allah! Unaweza kuona kwamba hayupo hata rafiki mmoja karibu yangu awezaye kuzifikisha salamu zangu kwa Mtume. Ee Mola wangu! Nifikishie salam zangu kwake.” Itaweza kuonekana kwamba hisia za kidi- ni za mtu huyu mchamungu, zilimuudhi Abu Uqbah. Aliamka na kumwua kwa kumpiga pigo mwilini mwake.

Ibn Hishamu5 amenakili ya kwamba Khubayb alizisoma beti fulani za shairi kabla ya kufa kwake pale kwenye ile miti ya kunyongea: “Ninaapa kwa jina la Allah. Kama nikifa hali ya kuwa ni Mwislamu, sitakuwa na wasiwasi wowote juu ya sehemu nitakayozikiwa. Kifo changu hiki chenye kuhuzunisha kimo kwenye njia ya Allah, na kama Akipenda anaweza kukifanya kifo hiki cha kishahidi kuwa heri kwa ajili ya kuvunjwa vunjwa kwa viungo vyangu.”

Tukio hili lenye kuupasua moyo lilimghadhibisha mno Mtume (s.a.w.w.) na kuliwafanya Waisalamu wote washikwe na huzuni.

Hassan bin Thabit, mshairi mkuu wa Waislamu alizisoma beti za huzuni zilizonakiliwa na Ibn Hisham kwenye Siirah yake. Mtume (s.a.w.w.) alichelea kwamba tukio hili litarudiwa tena na kikundi cha wahubiri kilichofunzwa kwa taabu kubwa, kwa njia hii kinaweza kupata pigo lisilotengenezeka. Vile vile alichelea kwamba kikundi hiki kitakatifu kilichokuwa bora kilichokuwa kikipigana kwenye mstari wa mbele kinaweza kikakumbwa na makri za maadui wa Uislamu.

Maiti ya Khubayb ilibakia kwenye miti ile ya kunyongea kwa kipindi kirefu na kikundi cha watu kilikuwa kikiilinda. Hata hivyo, hatimaye kutokana na amri ya Mtume (s.a.w.w.) watu wawili mashujaa walikwenda usiku na wakaizika.6

Masaibu Ya Bi’r Ma’unah

Mwaka wa tatu Hijiriya, pamoja na matukio yake yote machungu na yenye mafunzo ulimalizika, na mwaka wa nne ukaanza kwa kuandama kwa mwezi wa Muharram. Kwenye mwezi wa Safar wa mwaka ule ule, Abu Baraa’a alikuja Madina na Mtume (s.a.w.w.) alimkaribisha asilimu. Hakulikubali hilo lakini vile vile hakutaka kujitenga.

Alimwambia Mtume (s.a.w.w.) kama ukiwapelekea watu wa Najd kikundi chenye nguvu cha wahubiri inaweza kutegemewa kwamba watasilimu kwa vile wao wanaelekea mno kwenye Uislamu.” Mtume (s.a.w.w.) akamjibu akasema: “Mimi nachelea udanganyifu na uadui wa watu wa Najd. Ninatambua kwamba mhanga wa Raji’, uliozaa kuuawa kwa idadi fulani ya watu waso- mi na wahubiri, unaweza kurudiwa.” Abu Baraa’a akasema:

“Hicho kikundi utakachokipeleka kitakuwa chini ya ulinzi wangu nami ninakuthibitishia kwamba mimi nitawahami kutokana na kila dhara.”

Waislamu arobaini walio wasomi waliohifadhi Qur’ani na mafunzo mbalimbali ya Uislamu walitoka kwenda Najd chini ya uongozi wa Munzir na wakaenda wakapiga kambi karibu na Bi’r Ma’unah. Mtume (s.a.w.w.) aliandika barua yenye kuwaita watu kwenye dini ya Uislamu kwa chifu mmoja wa Najd aliyeitwa Aamr. Sio tu kwamba Aamr hakuisoma barua ile bali vilevile aliwauwa wale watu waliokuja na barua ile. Vile vile aliomba msaada wa makabila jirani na lile eneo kilipopigia kambi kile kikundi cha wahubiri lilizungukwa na watu wake.
Wale watu waliounda kile kikundi cha wahubiri hawakuwa wahubiri wakuu na hodari tu, bali vile vile walikuwa wakifikiriwa kuwa mashujaa na watu wafaao kwa vita. Hivyo, walifikiria kwamba ni aibu kwao kujisalimisha. Hivyo walichukua silaha na wote, isipokuwa mmoja tu, walikufa kishahidi baada ya kupigana mapigano makali. Yule aliyebakia hai alikuwa Ka’ab bin Zayd ambaye alifika Madina akiwa na mwili uliojeruhiwa na akatoa taarifa za kile kilichotokea.7

Haya matukio mawili ya kimsiba yalikuwa matokeo maovu ya kule kushindwa kwa Waislamu pale Uhud, kulikoyashawishi makabila jirani kukimbilia kuwauwa Waislamu.

Tabia Ya Upendeleo Ya Mustashirik

Mustashirik wapendao kulikuza donda lililoko usoni mwa waabudu masanamu na kuutupia Uislamu na Waislamu masingizio ili kuthibitisha kwamba Uislamu ulienea kwa nguvu ya upanga, wameifunga midomo yao kuhusiana na hii misiba miwili na hawatamki japo neno moja juu ya misiba hii. Ni wapi ulimwenguni ambako wanachuoni na watu watakatifu wamekatwa panga? Kama Uislamu umestawi chini ya kivuli cha upanga, basi ni kwa nini wahubiri hawa wayatoe mhanga maisha yao?

Haya matukio mawili yana mambo makuu ya mafunzo fulani fulani. Nguvu ya imani, kujitolea mhanga, ushujaa na ujasiri wa roho hizi mashuhuri ndio msingi yalimosimamia mafanikio ya Waislamu. Inastahili wao kuvutiwa nayo na haina budi kuwa mfano kwa ajili yao.

Muumini Wa Kweli Kamwe Hang’atwi Kutokea Kwenye Tundu Lilelile

Matukio ya masaibu ya Raji’ na Bi’r Ma’unah yaliyoishilizia kwenye mauaji ya wahubiri wa Uislamu yaliwasikitisha mno Waislamu. Kufikia hapa bila shaka wengi wa wasomaji watapatwa na mwelekeo wa kuuliza ni kwa nini Mtume (s.a.w.w.) alikifanya kitendo hiki? Alipokuwa tayari kaishapatwa na tukio chungu la (Raji) ni kwa nini aliwapeleka wale watu arobaini kule Bi’r Ma’unah? Je, yeye Mtume (s.a.w.w.) mwenyewe hakusema: “Katu Muumini wa kweli hang’atwi mara mbili kutokea kwenye tundu lile lile?”

Jibu la swali hili hudhihirika tunapoyarejea maelezo ya kihistoria, kwa sababu usalama wa hiki kikundi cha pili ulihakikishwa na Abu Bara’a Aamr bin Malik bin Ja’afar, aliyekuwa chifu wa kabila la Bani Aamr, na kamwe kabila (la Kiarabu la zama zile) halikwenda kinyume na shabaha za chifu wake. Zaidi ya hapo, ili kutoa uhakikisho zaidi, yeye mwenyewe aliamua kubakia mjini Madina hadi kile kikundi cha wahubiri kirejee.

Mpango uliopangwa na Mtume (s.a.w.w.) ulikuwa sahihi na ulikuwa na uwezo wa kutoa matokeo. Ukweli uliopo ni kwamba wale watu wa kile kikundi hawakuuawa na watu wa kabila la Abu Bara’a. Hakuna shaka kwamba mwana wa nduguye, yaani Aamr bin Tufayl alilichochea kabila la Abu Bara’a dhidi ya kile kikundi cha wahubiuri lakini hakuna yeyote aliyemsikiliza na wote wakasema: “Ami yako amewathibitishia usalama wao.” Hatimaye Aamr bin Tufayl alipata msaada kutoka kwenye makabila mengine kama vile Salim na Zakwaan na wakawauwa wale watu wa kikundi cha wahubiri wa Kiislamu.

Kile kikundi cha wahubiri wa Kiislamu kilipokuwa kikienda kwenye jimbo lile la Abu Bara’a, kiliwateuwa watu wawili kutoka miongoni mwao ambao ni ‘Amr bin Umayyah na Hirith bin Simmah8 ili waweze kuwapeleka ngamia wao malishoni na kuwachunga. Watu hawa wawili walitekeleza jukumu lao walilolibeba, nao hawakuitambua hali ya baadae ya wale wenzao.
Mara kwa ghafla, Aamir bin Tufayl aliwaotea. Matokeo yake ni kwamba Harith bin Simah aliuwawa, na Amr bin Umayyah aliponyoka.

Alipokuwa njiani akirejea Madina Amr Bin Umayyah alikutana na watu wawili na alikuwa na uhakika kwamba walikuwa watu wa yale makabila ambayo watu wao walikiuwa kile kikundi cha wahubiri wa Kiislamu. hivyo basi, aliwauwa wote wawili walipokuwa wamelala na kisha akarejea Madina.

Amr alifanya uamuzi wenye makosa. Watu wale walikuwa wa kabila la Abu Bara’a (kabila la Bani Aamir) lililoiheshimu damu ya wahubiri wa Kiisilamu kutokana na ile heshima waliyo nayo kwa ajili ya chifu wao. Tukio hili nalo liliongeza ile huzuni ya Mtume (s.a.w.w.) na akaanza kuli- pa dia kwa ajili ya wale watu wawili.

  • 1. Maghaazil Waaqidi, Juz. 1, uk. 354.
  • 2. Tan’im ni mahali panapochukuliwa kuwa ndio mwanzo wa Haraam na mwishilizio wa ‘Hil’ na ‘Ihraam’ inavaliwa hapo kwa ajili ya ‘Uimratul- Mufradah’
  • 3. Waaqid anasema kwamba mateka wote wawili walinyongwa kwenye siku ile moja. (Mughaazi, Juz. 1, uk. 358).
  • 4. Maghaazil Waaqidi, Juz. 1, uk. 359.
  • 5. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 170.
  • 6. Safinatul Bihaar, Juz. 1, uk. 382.
  • 7. Maghaazil Waaqidi, Juz. 1, uk. 349-364.
  • 8. Kutegemeana na ilivyonukuliwa na Ibn Hisham kwenye Siira yake, Juz. 2, uk. 186, Mtu yule alikuwa ni Munzir bin Muhammad