Sura Ya 34: Wayahudi Wautoka Ukanda Wa Waislamu

Wanafiki na Wayahudi wa Madina walifurahi kutokana na kushindwa kwa kikundi hicho cha wahubiri. Walikuwa wakiisubiri fursa ya kujengea ghasia mle mjini Madina na kuyafanya makabila yaishiyo nje ya Madina kutambua kwamba haukuwapo umoja mle ili kwamba ile Dola changa ya Uislamu iweze kupinduliwa kwa njia ya mashambulizi ya maadui wa nje.

Ili kupata taarifa juu ya dhamira na fikira za Wayahudi wa kabila la Bani Nuzayr, Mtume (s.a.w.w.) alizitembelea ngome zao pamoja na masahaba zake, hata hivyo lengo hasa la Mtume (s.a.w.w.) kukutana na Bani Nuzayr lilikuwa ni kupata msaada wao katika kulipa dia ya wale watu wawili waliouwawa na ‘Amr bin Umayyah, kwa kuwa kabila la Bani Nuzayr walikuwa wakiishi chini ya ulinzi wa Dola ya Kiislamu na ilikuwa sahihi tu kwamba kwenye tukio la aina hiyo, walilazimika kuichangia ile fidia iliyolazimika kulipwa.

Zaidi ya hapo, vile vile Wayahudi hawa walikuwa wamefanya mapatano baina yao kuwa daima watasaidiana kwenye matukio ya aina hiyo.

Mtume (s.a.w.w.) alishuka kutoka kwenye mnyama wake upande wa pili wa lango la kuwatembelea wale machifu wa kabila lile. Walimpokea kwa mikono miwili na wakaahidi kuchangia kwa ajili ya ile dia. Kisha walipokuwa wakizungumza na Mtume (s.a.w.w.) wakimtaja kwa jina la Abul Qaasim (babie Qassim) walimuomba aingie mle ngomeni na aitumie siku ile pamoja nao.

Hata hivyo, Mtume (s.a.w.w.) hakuliridhia ombi lao, na kulingana na ilivyonakiliwa na baadhi ya wanahistoria ni kuwa alishu- ka tu upande wa pili wa ngome na baada ya kukaa kwenye kivuli cha ukuta wa ngome ile pamoja na masahaba zake alianza kuzungumza na wale machifu wa Bani Nuzayr.1

Mtume (s.a.w.w.) alihisi ya kwamba mazungumzo yake mengi yaliandamana na matendo ya siri. Ulikuwepo mzunguko mkubwa wa watu kandokando mwa sehemu ile aliyokaa Mtume (s.a.w.w.). Walikuwa wakinong’onezana jambo lililojenga dhana kubwa ya kwamba mambo yalikuwa mabaya pale. Kwa kweli wale machifu wa Bani Nuzayr waliamua kumweka Mtume (s.a.w.w.) katika hali ya kutotambua. Wakimteuwa mmoja wa mtu wao aliyeitwa Amr Hajash kushuka kutoka kwenye paa na kumuuwa Mtume (s.a.w.w.) kwa kumtupia jiwe kubwa kichwani mwake.

Kwa bahati, mpango wao ule ulishindwa. Njama na mipango yao miovu vilifichuka kutokana na matendo yao, na kutegemeana na alivyonukuu Waaqidi, Mtume (s.a.w.w.) alitambua makri ile ya Wayahudi kupitia ufun- uo utokao kwa Allah. Aliitoka sehemu ile katika hali ambayo Wayahudi walifikiria kwamba alikuwa akienda kwa ajili ya kazi fulani na kwamba atarejea. Kwa kweli Mtume aliamua kwenda Madina moja kwa moja na hakuwaeleza hata wale masahaba zake juu ya uamuzi wake ule. Nao pia walibakia wakimsubiri pale, lakini yote yakawa hewa, patupu.

Wayahudi wa kabila la Bani Nuzayr waliingiwa na wasiwasi sana. Walidhania ya kwamba huenda Mtume (s.a.w.w.) aliitambua ile makri yao, na hivyo basi atawaadhibu vikali, vile vile walidhania nafsini mwao kuwa: “Sasa kwa vile Mtume yuko mbali hatuwezi kumfikia, tunaweza kulipiza kisasi juu ya masahaba zake.” Lakini wazo likawapitia akili mwao upesi sana kwamba katika hali ile jambo lile litakuwa kubwa mno na bila shaka Mtume (s.a.w.w.) atalipiza kisasi dhidi yao.

Kufikia hapa, wale masahaba wa Mtume (s.a.w.w.) waliamua kumfuata na kupata kujua mahali alipo. Walikuwa bado hawajafika mbali sana kutoka kwenye ile ngome, walipokutana na mtu mmoja aliyewaambia kwamba Mtume (s.a.w.w.) alikuwa tayari kaishawasili Madina. Walimtembelea na wakaigundua ile makri ya Wayahudi ambayo vile vile ilithibitishwa na wahyi.2

Jinsi Ya Kulishughulikia Jinai Hili

Sasa wajibu wa Mtume (s.a.w.w.) ungalikuwa upi kuhusiana na kundi hili? Hawa walikuwa ni wale watu waliozifaidi fursa zilizoletwa na Dola ya Kiislamu na ambao mali zao na heshima zao vilikuwa vikilindwa na askari wa Kiislamu! Wao walikuwa ni jamii iliyozishuhudia dalili za dhahiri za Utume kwa Mtume (s.a.w.w.) na waliosoma vitabuni mwao juu ya uthibitisho wa Utume wake na ushahidi wa ukweli wake.

Ni ipi njia sahihi ya kulishughulikia hili kundi la watu ambao licha ya kunufaika kutokana na aina zote za faida, lakini walipanga makri dhidi yake (Mtume s.a.w.w) na wakaamua kumwua badala ya kuonyesha ukarimu? Haki ilitakaje kuhusiana na jambo hili? Na ilitakikana kutendekaje ili kwamba matukio ya aina hii yasirudiwe tena hapo baadae?

Njia ya kulitatulia tatizo hili ilikuwa ni ileile aliyoitumia Mtume (s.a.w.w.). Aliwaamrisha askari wote kukaa tayari tayari. Kisha alimwita Muhammad bin Maslamah, mtu wa kabila la Aws, na akamwamrisha kuwapelekea machifu wa Bani Nuzayr ujumbe wake upesi iwezekanavyo. Muhammad bin Maslamah aliwasiliana na wale machifu wa Bani Nuzayr na akawaambia:

“Yule kiongozi mtukufu wa Uislamu amekuleteeni ujumbe kupitia kwangu ya kwamba mtoke mahali hapa upesi iwezekanavyo, tena ndani ya siku kumi, kwa kuwa mmetenda udanganyifu, na kama hamtaondoka kwenye ukanda huu ndani ya siku kumi, damu yenu itamwagwa!”

Bani Nuzayr walisikitika walipoupata ujumbe ule na kila mtu alimchukulia mwenzie kuwa ndiye mwenye kuhusika na hali ile ya mambo. Mmoja wa viongozi wao alishauri ya kwamba wote wasilimu. Hata hivyo ushauri huu haukukubaliwa na wengi wa watu hawa walio wakaidi. Walijihisi kuwa kwenye hali ya kutokuwa na msaada. Hatimaye walimgeukia Muhammad bin Maslamah na kumwambia: “Ewe Muhammad! Wewe ni wa kabila la Aws na kabla ya kuwasili kwa huyu Mtume wa Uislamu, sisi tulikuwa na mapatano ya ulinzi na kabila lako. Sasa vipi wewe unakuwa kwenye hali ya kivita dhidi yetu?” Akilijibu swali hili alisema kwa ujasiri kamili uliompasa kila Mwislamu. “Wakati ule ulishapita. Siku hizi nyoyo zimeshabadilika.”

Msingi wa lengo la Mtume (s.a.w.w.) ulikuwa ni yaleyale mapatano ambayo Waislamu waliyafanya baina yao na yale makabila ya Wayahudi kwenye siku za awali na yaliyosainiwa na Hay bin Akhtab kwa niaba ya Bani Nuzayr. Tayari tumeshatoa maelezo ya mapatano haya kwenye kurasa zilizotangulia na hapa tunanukuu sehemu ya maelezo hayo: “Mtume anafanya mapatano na kila moja ya yale makundi matatu (Bani Nuzayr, Bani Qaynaqaa na Bani Quraydha) kwamba hawatachukua hatua yoyote ile dhidi ya Mtume wa Allah na masahaba zake nao hawatamdhuru kwa mikono yao au ndimi zao. Na endapo lolote kati ya makabila haya litakwenda kinyume na mapatano haya, Mtume atakuwa huru kuimwaga damu yao, kuzinyakua mali zao na kuwateka wanawake na watoto wao.”

Machozi Ya Mamba

Kufikia hapa, vilevile mustashirik wameyatiririsha machozi ya mamba kwa kuwahurumia Wayahudi wadanganyifu, walioyageuka mapatano na wakasema kwamba kitendo cha Mtume (s.a.w.w.) hakikuafikiana na usawa na uadilifu. Huo ni udanganyifu na ulalamishi hafifu uliofanywa na hawa mustashirik ulikuwa ni kwa ajili ya kuuficha ukweli, kwa sababu rejea za maelezo ya mapatano zaonyesha kwamba ile adhabu aliyoitoa Mtume (s.a.w.w.) ilikuwa nyepesi mno kuliko ile iliyoelezwa kwenye ule mkataba wao.

Siku hizi mamia ya majinai na mateso hutokea kwenye nchi za Mashariki na za Magharibi mikononi mwa mabwana hawa mustashirik na hakuna yeyote miongoni mwao awakanushaye, japo kidogo tu. Hata hivyo, Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) anapoliadhibu kundi la wapanga makri japo kwa adhabu iliyo ndogo kuliko ile iliyokubaliwa hapo awali, baadhi ya waan- dishi wanaolichanganua tukio lile kwa nia zao mbalimbali za kibinfsi, hupiga makelele dhidi ya tukio lile.

Nafasi Ya Wanafiki

Maadui na hatari zaidi wa Uislamu walikuwa ni kikundi cha wanafiki waliokuwa wakivalia kinyago cha urafiki nyusoni mwao na Abdullah bin Ubayy na Malik bin Ubayy Nawfal n.k. walikuwa ndio viongozi wao.

Upesi upesi waliwapelekea machifu wa Bani Nuzayr ujumbe usemao kwamba wao (wanafiki) watawasaidia askari mashujaa elfu mbili na marafiki zao, yaani makabila ya Bani Quraydha na Ghatfan vile vile nayo hayatawaacha peke yao. Hii ahadi ya uwongo iliwashawishi Wayahudi, na ingawa hapo awali waliamua kujisalimisha na kutoka mahali pale, sasa wakaubadili uamuzi wao.

Waliyafunga malango ya ngome zao, na baada ya kujikusanyia silaha wakaona kuwa wataweza kujihami kwa gharama zozote zile kutoka kwenye minara ya ngome zile nao hawataliruhusu jeshi la Uislamu kuchukua utawala wa bustani na mashamba yao.

Mmoja wa viongozi wa Bani Nuzayr (Salaam bin Mushkam) aliifikiria ahadi ya Abdullah kuwa isiyo kuwa na maana, na akasema: “Ni bora kwetu kutoka mjini humu.” Hata hivyo, Hay bin Akhtab aliwashauri wabakie kuwa thabiti na madhubuti.

Mtume (s.a.w.w.) aliutambua ule ujumbe uliopelekwa na Abdullah akiwapelekea wale Wayahudi. Alimteua Ibn Ummi Makhtum kuwa naibu wake mle mjini Madina na kwa Takbir (Allah Yu Mkubwa) kinywani mwake alikwenda kuizingira ngome ya Bani Nuzayr. Alilifanya eneo la baina ya Bani Quraydha na Bani Nuzayr kuwa kambi yake na kwa kufanya hivyo aliyakata mawasiliano baina ya yale makabila mawili.

Kufuatana na kauli ya Ibn Hisham3 ngome ile ilizingirwa kwa mchana mmoja na usiku mmoja, na kwa mujibu wa baadhi ya waandishi, ilizingirwa kwa muda wa siku kumi na tano. Hata hivyo, wale Wayahudi wakawa madhubuti zaidi na thabiti. Mtume (s.a.w.w.) aliamrisha ya kwamba mitende iliyoizunguka ngome ile ikatwe ili kwamba ile sababu iwafanyayo wale Wayahudi waitamani sana nchi ile iondoke kabisa. Katika hali hii, vilio vya Wayahudi vilikuwa vikubwa mno kutoka mle ngomeni na wote wakasema: “Ewe Abul Qaasim! Daima umekuwa ukiwakataza askari wako kuikata miti! Basi, kwa nini sasa unalitenda jambo hili?” Hata hivyo sababu ya kufanya hivi ni kama tulivyoeleza hapo juu.

Hatimaye Wayahudi walisalimu amri na wakasema: “Tuko tayari kuwa wakimbizi, ili mradi tu turuhusiwe kuvichukua vitu vyetu.” Mtume (s.a.w.w.) alikubali kwamba wangaliweza kuvichukua vitu vyao ila silaha ambazo ni lazima wazisalimishe kwa Waislamu.

Wayahudi hawa waliojawa na choyo walijitahidi kwa kadiri ya uwezo wao wote kuzichukua mali zao, kiasi kwamba waliing’oa milango ya nyumba zao, ili waichukue na kisha wabomoe majengo. Baadhi yao walikwenda Khaybar na wengine wakaenda Shamu. Wawili miongoni mwao walisil- imu.

Ili kuficha kufunika kushindwa kwao wale Wayahudi walioshindwa na wasio na msaada wowote ule sasa, waliutoka mji wa Madina wakiwa wanapiga ngoma na kuimba nyimbo. Hivyo basi, walitaka kutoa dhana ya kwamba hawakuwa wenye huzuni hata kidogo kuitoka sehemu ile.

Mashamba Ya Bani Nuzayr Ya Gawanywa Miongoni Mwa Muhajiriin.

Kwa mujibu wa Qur’ani Tukufu (Surat Al-Hashr, 59:6) ngawira waipatayo Waislamu bila ya kupigana ni mali ya Mtume (s.a.w.w.) na anaweza kuitumia kwa ajili ya ustawi wa Uislamu na Waislamu kufuatana na aonavyo kuwa inafaa. Mtume (s.a.w.w.) aliona kuwa inafaa kuyagawa mashamba hayo, marambo ya maji na bustani (vitu vilivyoachwa na Bani Nuzayr) miongoni mwa Muhajiriin, kwa sababu tangu kuhamia kwao kutoka Makka walikuwa masikini, na kwa kweli walikuwa wakiwategemea Ansar wa Madina nao walikuwa wageni wao.

Sa’ad bin Mu’aaz na Saad bin Ubadah nao waliyaunga mkono maoni haya. Hivyo basi, mali yote iligawanywa miongoni mwa Muhajiriin na hakuna yeyote miongoni mwa Ansar aliyepata fungu lolote lile, ila Sahl bin Hunayf na Abu Dujanah, waliokuwa masikini zaidi. Kwa njia hii hali ya kiuchumi ya Waislamu ilitengenezeka kwa ujumla. Upanga wa bei ya juu ambao hapo awali ulikuwa mali ya mmoja wa machifu wa Bani Nuzayr, alipewa Sa’ad bin Mu’aaz.

Tukio hili lilitokea kwenye mwezi wa Rabi’ul Awwal (Mfunguo sita) wa mwaka wa nne hijiriya wakati Surat Al-Hashr nayo ilipofunuliwa ili kuzitaja sababu za tukio hili na kuiibua tahadhari ya Waislamu. Wengi wa wanahistoria wa Kiislamu wanaamini ya kwamba hakuna umwagaji damu uliotokea kwenye tukio hili. Hata hivyo, marehemu Shaykh Mufid4 anasema kwamba katika usiku wa kutekwa kwa ngome hii mapigano madogo yalitokea na Wayahudi kumi waliuawa na vifo vyao vilitoa msingi wa kusalimu amri kwa majeshi ya Wayahudi.

  • 1. Maghaazil anasema kwamba Mtume (s.a.w.w.) alifika kwenye mkutano wao (Juz. 1, uk. 364).
  • 2. Maghaazil- Waaqidi, juz. 1, uk. 305.
  • 3. Siiratu Ibn Hisham, juz. 2, uk. 191.
  • 4. Al -Irshaad, uk. 47-48.