Sura Ya 35: Matukio Ya Mwaka Wa Nne Hijiriya Kuharimishwa Kwa Pombe

Mvinyo na vinywaji vyenye kulevya kwa ujumla vimekuwa, na bado ni moja ya misiba yenye kuharibu jamii ya mwanadamu, na inatosha kusema kuwa, kwa ajili ya kuikemea hii sumu yenye kuua, kwamba inapigana vita dhidi ya neema ya mwanaadamu iliyo kuu zaidi inayomuainisha yeye na viumbe vingine vyenye uhai yaani akili na busara. Ustawi wa mwanaadamu unategemea hekima zake, na tafauti iliyopo baina yake na viumbe vingine vyenye uhai ni kutokana na uwezo wake wa kiakili, na pombe inatambulikana kuwa ni adui mkuu wa hekima na akili. Ni kutokana na sababu hii kwamba Mitume wote wa Allah wameharamisha matumizi ya pombe. Kusema kweli vitu hivi vimetangazwa kuwa ni hara- mu kwenye dini zote zilizofunuliwa.

Kwenye Rasi ya Uarabuni, ulevi ulikuwako kama ilivyokuwa misiba ya ujumla, ambayo kampeni thabiti dhidi yao ilihitaji muda mrefu mno, na hali ya mambo iliyokuwapo kwenye jamii ile na hali ya Waarabu kwa ujumla, nayo haikuruhusu kwamba Mtume (s.a.w.w.) aitangaze kuwa ni haramu kabla ya kuchukua hatua za awali. Vile vile alilazimika kuuta- yarisha mwenendo wa jamii ili ufae katika kukipiga vita kitendo hiki.

Hivyo basi, zile Aya nne zilizofunuliwa kuonyesha kuchukiza kwa pombe hazifanani. Mtume (s.a.w.w.) alianza kwa ushauri hadi alipofaulu kuy- atangaza matumizi yake kuwa ni haramu. Kuchunguza Aya hizi kwa makini hutufahamisha njia aliyoitumia Mtume (s.a.w.w.) kuhusu uhubiri wa sheria za Uislamu, na inafaa kwamba waandishi na wazungumzaji stadi hawana budi kuifuata njia hii ya ufundishaji na wafanye kampeni dhidi ya maovu ya kijamii kwa njia hii hii.

Sharti muhimu kwa kufanya kampeni dhidi ya kitendo kiovu katika hatua ya kwanza ni kuziamsha fikira za jamii na kuuibua usikivu wa nyoyo zao kuhusu hasara zake na athari zake zilizo mbaya. Haiwezekani kufanya kampeni dhidi ya kitendo kiovu mpaka kwanza upate kuwapo tayari kwa kiroho na uamsho wa nafsi kwenye jamii, na watu wenyewe wawe na wajibu juu ya jambo lile, vinginevyo itakuwa haiwezikani kufanya kampeini dhidi ya kitendo kiovu.

Hivyo basi, mara ya kwanza kabisa Qur’ani Tukufu iliiambia jamii, sehemu ambayo maisha yao yalikuwa ni ya ulevi, kwamba kutengeneza pombe kutokana na tende na zabibu kulikuwa kinyume na lishe nzuri, na aina hii ya mazungumzo kwa hakika ilikuwa onyo la kuziamsha fikira za watu. Inasema: “Na katika matunda ya mitende na mizabibu mnatengeneza ulevi na riziki nzuri. Hakika katika hayo mna mazingatio kwa watu wanaotumia akili.” (Surah al-Nahl, 16:67).

Kwa mara ya kwanza hiki Kitabu kitakatifu kilitamka kwamba kuten- geneza pombe kwa vitu hivi sio ‘lishe nzuri’ hasa. ‘Lishe nzuri’ ina maana ya kwamba inapasa kuliwa ikiwa kwenye hali yake ya asilia.

Aya hii iliwatia watu mshituko akilini mwao na kuufanya mwenendo wao kuwa tayari ili Mtume (s.a.w.w.) aweze kuifanya kauli yake kuwa na nguvu zaidi na kwa kupitia Aya nyingine aweze kutangaza kwamba ‘baadhi ya matumizi ya vitu’ yatokanavyo na (mapato ya) pombe na kamari ni vitu visivyo na maana, vinapolinganishwa na athari zake mbaya. Ukweli huu umetajwa kwenye Aya hii:
“Wanakuuliza kuhusu ulevi na kamari. Waambie: Katika hayo mna uovu mkubwa na manufaa (kidogo) kwa watu; na uovu wake ni mkubwa zaidi kuliko manufaa yake...” (Surat al-Baqarah; 2:219).

Hakuna shaka kwamba ulinganisho huu baina ya faida na hasara, uonye- shao kwamba kitu fulani kina madhara zaidi kuliko manufaa, unatosha kuwafanya watu wenye kuitumia akili kuonyesha kuchukizwa kwao na pombe. Hata hivyo, watu wote kwa ujumla hawaliepuki tendo baya isipokuwa kama likipigwa marufuku kabisa.

Ingawa ni kweli kwamba aya tuliyoinukuu hapo juu ilikuwa tayari ime- shafunuliwa, Abdur Rahman bin Awf alitayarisha karamu na kisha akagawa pombe kwenye kitambaa chake cha chakula. Wale waliokuwapo pale karamuni wakaanza kusali baada ya kunywa pombe. Mmoja wao aliisoma Aya fulani kwa makosa na kuibadili maana yake, yaani badala ya kusema: “Enyi waabudu masanamu! Mimi sikiabudu kile mkiabuducho” aliitamka sentensi yenye maana iliyo kinyume na hivyo, kwa kuliacha neno ‘laa’ (si) kutoka kwenye Aya ile.

Matukio haya yaliufanya mwenendo wa watu kuwa tayari, kwani hali iliruhusu ulevi kukatazwe, kwa uchechefu kwenye hali fulani fulani maalumu.

Kutokana na masharti haya, ilitangazwa dhahiri kwamba hakuna Mwislamu aliyekuwa na haki ya kusali awapo kwenye hali ya ulevi na amri hii ya Allah ilitangazwa kwa maneno haya: “Enyi mlioamini! Msikaribie swala hali ya kuwa mmelewa mpaka myajue mnayoyasema...”
(Surah al-Nisa, 4:43)1

Athari ya Aya hii ilikuwa kwamba kikundi cha watu fulani kiliacha kabisa kulewa, na hoja yao katika kufanya hivyo ilikuwa kwamba kitu chenye madhara katika sala chapasika kuachwa kabisa. Hata hivyo, wengine hawakuiacha tabia hii hata kidogo kiasi kwamba mtu mmoja kutoka mion- goni mwa Ansar alitayarisha karamu na ukiachilia mbali ukweli uliopo kwamba mtu yule alikuwa akiitambua Aya ile, aliandaa pombe pia kwenye kitambaa cha chakula.
Wale wageni baada ya kunywa pombe, walianza kugombana wakajeruhiana. Baada ya hapo walilalamika mbele ya Mtume (s.a.w.w.). Khalifa wa Pili, aliyekuwa na desturi ya kulewa pombe hadi wakati ule, akiwa na dhana ya kwamba Aya zilizotajwa hapo juu hazikuharimisha kabisa ulevi wa pombe, aliinua mikono yake alipokuwa kwenye sala na akasema: “Ewe Allah! Tufunulie amri iliyodhahiri na yenye kusadikisha.”

Ni dhahiri kwamba matukio haya yasiyopendeza yaliitayarisha hali ya hewa kuwa tayari kwa jambo hili kwamba kama matumizi ya pombe yakipigwa marufuku kabisa, Waislamu wote wangeliikubali marufuku hii kwa moyo mmoja. Hivyo basi, katika hatua ya mwisho, Aya hii ilifunuliwa: “Enyi mlioamini! Hakika pombe na kamari na kupiga ramli ni uchafu wa kazi ya shetani, basi jiepusheni nayo ili mpate kufaulu.” (Suratul-Ma’idah, 5:90).

Matokeo ya amri hii fasaha na yenye kusisitiza ni kwamba wale watu waliokuwa wakinywa pombe hadi wakati ule kwa udhuru wa kwamba amri ihusianayo na kuiacha pombe haikukamilika, sasa nao walijiepusha nayo, Khalifa wa pili alipoisikia Aya hii alisema: “Ninaikana (pombe) tangu sasa na kuendelea.”2

Vita (Ghazwah) Vya Dha Atur Riqaa

Katika lugha ya Kiarabu, neno ‘Riqaa’ lina maana ya ‘kiraka’. Hii jihadi takatifu inaitwa ‘Dhaatur Riqaa’ kwa sababu kwenye uwanja huu wa mapambano Waislamu walifika kwenye mlolongo wa sehemu zilizoinuka na za chini ambao ulionekana na viraka. Kufuatana na masimulizi mengine, iliitwa ‘Dhaatur Riqaa’ kwa sababu askari walifunga matambara miguuni mwao ili kupunguza taabu za kutembea.

Kwa vyovyote vile iwavyo, vita hivi havikuwa kampeni ya lazima hasa kwamba jeshi la Uislamu liangukie kwenye jamii kwa sababu ya kuwa kwao washirikina. Bali kusema kweli lengo lao lilikuwa ni kuizima cheche iliyokuwa karibuni kuwaka, yaani kuikomesha shauku iliyoonyeshwa na watu wa familia mbili za Ghatfan (Bani Mah?rib na Bani Sa’lahab) dhidi ya Uislamu.

Ilikuwa ni desturi ya Mtume (s.a.w.w.) kuwapeleka watu wenye busara na hekima kwenye sehemu mbalimbali ili waweze kumwarifu kuhusu hali ya ujumla ya sehemu zile. Kwa ghafla ilipokewa taarifa ya kwamba familia mbili tulizozitaja hapo juu zilikuwa zikikusanya silaha na watu ili kuja kuiteka Madina. Mtume (s.a.w.w.) alikwenda Najd akifuatana na kikosi maalumu na akapiga kambi karibu na nchi ya maadui wale. Kumbukumbu nzuri ya siku za awali za jeshi la Uislamu na kujitolea kwao mhanga na ujasiri, vitu vilivyoishangaza Rasi ya Uarabuni viliwafanya maadui kurudi nyuma na kukimbilia milimani na sehemu za juu bila ya kupigana.

Hata hivyo, kwa kuwa Mtume (s.a.w.w.) alikuwa akisali sala za wajibu kwenye vita vile pamoja na askari wa jeshi la Uislamu kama Salat-i Khawf (sala ya hofu) na aliwafundisha Waislamu jinsi ya kuisali kwa njia ya Aya ya 103 ya Suratun-Nisa, basi inaweza kudhaniwa kwamba majeshi ya maadui yalikuwa na silaha za kutosha na kwamba mapigano yaliichukua hali iliyo nyeti mno, lakini hatimaye Waislamu walishinda.

Walinzi Wavumilivu

Ingawa kwenye vita hivi jeshi la Waislamu lilirejea kutoka kwenye makao makuu ya adui na kuja Madina bila ya mapigano, walijipatia ngawira ndogo. Wakiwa njiani wakati wa kurejea, wakati wa usiku walikaa kwenye bonde pana ili wapumzike. Wakiwa hapo Mtume (s.a.w.w.) aliwateuwa askari wawili mashujaa ili wailinde njia iingiayo kwenye bonde lile.

Askari hawa wawili walioitwa ‘Abbad na ‘Ammar waliyagawa masaa ya usiku ule baina yao na walikubaliana kwamba ‘Abbad ailinde njia ile katika nusu ya kwanza ya usiku ule.

Mtu mmoja wa kabila la Ghatfan alikuwa akiwafuatilia Waislamu ili awadhuru na kisha arejee kwao upesi sana. Mtu huyu alijinufaisha kutokana na giza la usiku na akampiga mshale yule mtu aliyekuwa akilinda lile bonde wakati mlinzi yule akiwa anasali. Yule mlinzi alijishughulisha mno na du’a kiasi kwamba hakuyahisi mno maumivu yaliyosababishwa na ule mshale. Aliung’oa ule mshale kutoka mguuni mwake na akaendelea na du’a zake.

Hata hivyo, mashambulizi yale yalirudiwa kwa mara ya pili na ya tatu. Mshale wa mwisho wa adui yule uliufunua mguu wake vikali mno kiasi kwamba hakuweza kuendelea na du’a zake kama alivyotaka. Hivyo akazikomesha du’a zake upesi sana na kisha akamwamsha ‘Ammaar.

Hali ya kuhuzunisha ya Abbad ilimsikitisha mno Ammaar na akasema kwa njia ya malalamiko: “Kwa nini hukuniamsha tangu mwanzoni?” Yule mlinzi aliyejeruhiwa akajibu akasema: “Nilikuwa nikisali na nilikuwa nikisoma Sura ya Qur’ani Tukufu wakati mshale wa kwanza uliponichoma kwa ghafla. Ule utamu wa du’a na utamu wa utambuzi wa Allah Mwenye nguvu zote ulinizuia kuivunja sala yangu. Kama Mtume (s.a.w.w.) asingaliniwajibisha kuilinda sehemu hii katu nisingaliivunja sala yangu na ile Sura niliyokuwa nikiisoma. Na ningeliyatoa maisha yangu kwa Allah kabla ya kudhamiria kuivunja sala yangu.”3

Badri Ya Pili

Mwishoni mwa vita vya Uhud Abu Sufyan alitangaza akisema: “Mwaka ujao tutakutana nanyi kwenye jangwa la Badr kwenye wakati huu huu nasi tutalipiza kisasi vikali mno juu yenu.

Kwa amri ya Mtume (s.a.w.w.) Waislamu wakatangaza kuwako kwao tayari kupigana. Muda wa mwaka uliowekwa ulipita naye Abu Sufyan ambaye wakati ule alikuwa mtawala wa Waquraishi, alihusika na matatizo mbalimbali. Na’im bin Mas’ud aliyekuwa na uhusiano wa kirafiki na pande zote mbili (Waislamu na Waquraishi) aliwasili mjini Makka. Abu Sufyan alimwomba arejee Madina upesi na amshawishi Muhammad asia- mue kutoka mjini Madina.

Aliongeza kusema hivi: “Haiwezekani kwetu sisi kutoka mjini Makka mwaka huu, na maonyesho na mbinu za kivita alizozionyesha Muhammad pale Badr, ambapo ni eneo la soko la Waarabu, yatasababisha kushindwa kwetu.”

Dhamira yoyote ile aliyoweza kuwa nayo, Na’im alirejea Madina. Hata hivyo, maneno yake hayakuwa na athahri yoyote katika malengo ya Mtume (s.a.w.w.). Alipiga kambi pale Badr mwanzoni mwa mwezi wa Dhil Qaadul Haraam akiwa na askari wapiganaji 1500, na kiasi cha farasi na kiasi cha bidhaa, na akakaa hapo kwa kiasi cha siku nane zilizokwenda sawa na siku ya soko la mwaka la Waarabu, Waislamu waliziuza bidhaa zao hapo na kupata faida kubwa. Baada ya hapo watu waliokuja kutoka sehemu mbalimbali walitawanyika, lakini lile jeshi la Waislamu liliendelea kusubiri kuwasili kwa jeshi la Waquraishi.

Taarifa zilifika Makka kwamba Muhammad amefika Badr. Machifu wa Waquraishi hawakuwa na lolote jingine la kufanya kwa kujiokoa kutokana na fedheha ile isipokuwa watoke Makka na kwenda Badr. Abu Sufyan aliyekuwa na silaha za kutosha, alikuja hadi Maruz Zahraan, lakini alirejea baada ya kufika katikati ya njia akitoa udhuru wa njaa na vifo. Kurejea kwa jeshi la waabudu masanamu kulishtusha mno kiasi kwamba Safwan alimlalamikia Abu Sufyan na kusema: “Kwa kurudi nyuma huku, tumeshaipoteza heshima yote tuliyoipata, na kama isingalikuwa umeahidi pale mwaka jana kupigana vita basi tusingalikabiliwa na huku kushindwa kwa kisaikolojia.”4

  • 1. Rejea kwenye Sunan Abi Daudi, Juzuu 2, uk. 128.
  • 2. Mustadrak, juz. 4, uk. 143. na Ruhul Ma’aani, juz. 7, uk. 15.
  • 3. Siiratu Ibn Hisham, juz. 2, uk. 208-209.
  • 4. Kufuatana na ilivyoandikwa kwenye Mughaazi-i Waqidi, Juz. 1, uk. 484, tukio hili lilitokea kwenye mwezi wa 45 wa Hijiriya.