Sura Ya 36: Matukio Ya Mwaka Wa Tano Hijiriya

Matukio ya kihistoria ya mwaka wa tano hijiriya yaliyo muhimu zaidi ni Vita vya Ahzaab, hadith ya Bani Quraydha na ndoa ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na Bibi Zaynab bint Jahasha. Kufuatana na kauli ya wanahistoria, tukio la kwamza kutokea lilikuwa ni ile ndoa ya Mtume (s.a.w.w.) na Bibi Zaynab.

Qur’ani Tukufu imeihadithia hadith tuliyoitaja hapo juu kwenye Aya ya 4, 5, 36, 37 na 40 ya Sura al-Ahzaab (Sura ya 33) na haikuacha nafasi yoyote kwa uzushi wa uwongo wa mustashirik na waandishi wa hadithi za kubuni. Tutajifunza tukio hili kutoka kwenye maandishi yakubalikayo (yaani Qur’ani Tukufu) na vilevile tuta chunguza maelezo ya mustashirik kwa makini kabisa.

Zayd Bin Harith Alikuwa Ni Nani?

Zayd alikuwa ni mtu aliyetekwa wakati wa utotoni mwake kutoka kwenye msafara. Alitekwa na wanyang’anyi wa kibedui na akauzwa utumwani kwenye soko la Ukaz. Alinunuliwa na Hakim bin Hizaam kwa ajili ya shangazi yake Bibi Khadija, na Bibi huyu akampa Mtume (s.a.w.w.) kijana huyu akiwa ni zawadi, baada ya ndoa yao.

Zayd alikuwa na mapenzi makubwa mno na ule mtazamo halisi wa kiroho, hisia tukufu na tabia njema za Mtume (s.a.w.w.) kiasi kwamba, baada ya kupita kiasi fulani cha muda baba yake alikuja mjini Makka na kumwom- ba Mtume (s.a.w.w.) kumpa ungwana, ili amrejeshe kwa mama yake na watu wengine wa familia yake. Zayd alikataa kwenda na akapendelea kukaa na Mtume (s.a.w.w.). Baba yake Zayd alimpa Mtume (s.a.w.w.) mamlaka kamili ya ima Zayd abakie naye au amrejeshe makwao.

Hiki kiungo cha kiroho na hizi hisia zake za ndani zaidi kilikuwamo kwenye pande zote mbili. Kama Zayd alizipenda mno tabia za Mtume (s.a.w.w.), Mtume naye vile vile alimpenda mno Zayd kiasi kwamba alim- chagua kuwa mwanawe na watu wakaanza kumwita Zayd bin Muhammad badala ya Zayd bin Harith. Kulifanya jambo hili kuwa rasmi kama ilivyokuwa desturi ya Waarabu wa zama zile, siku moja Mtume (s.a.w.w.) aliushika mkono wa Zayd na akawaambia Waquraishi: “Huyu ni mwanangu, nasi tunarithiana.” Uhusiano huu wa wema uliendelea kuwapo hadi Zayd alipofariki dunia kwenye Vita vya Mu’ta na Mtume (s.a.w.w.) alisiki- tishwa mno na jambo hili kana kwamba alimpoteza mwanawe wa kumzaa.1

Zayd Amwoa Binamu (Binti Wa Shangazi) Yake Mtume (S.A.W. W)

Moja ya malengo matakatifu ya Mtume (s.a.w.w.) lilikuwa ni kupunguza ubaguzi wa matabaka ndani ya jamii na kuwaleta pamoja wanadamu wote chini ya bendera ya ubinadamu na uchamungu, na kuweka ubora wa tabia na sifa bora za kihulka kuwa ndio kipimo cha ubora na heshima. Hivyo basi, ilikuwa ni jambo muhimu kwamba azing’oe upesi iwezekanavyo zile desturi mbaya za Waarabu wa kale za kwamba mabinti wa watu watukufu wasiolewe na watu maskini.

Hivyo hakuna lililoweza kuwa bora zaidi ya mpango huu kuliko kuanzia kwenye familia yake mwenyewe na amwoze binamu yake Zainab mjukuu wa Abdul Muttalib kwa mtumwa wake wa zamani, ambaye tangu muda mrefu uliopita alikuwa keshapewa ungwana, ili watu watambue kwamba hivi vizuizi vya kufikiriwa tu havina budi kuondolewa upesi iwezekanavyo. Na vile vile watambue ya kwamba Mtume (s.a.w.w.) anaposema: “Kipimo cha ubora wa mtu ni uchamungu na mwanamke wa Kiislamu yu sawa na mwanaume wa Kiislamu” yeye mwenyewe alikuwa mtu wa kwanza kabisa kuitekeleza sheria hii na wa kwanza kuifanyia kazi. Ili kuing’oa desturi hii isiyo sahihi alikwenda nyumbani kwa Bibi Zaynab, yeye mwenyewe na kumwomba aolewe na Zayd.

Hapo awali yeye na kaka yake hawakuelekea kuikubali posa ile, kwa sababu fikara za siku za ujinga zilikuwa bado hazijafutika kutoka akilini mwao.

Hivyo, ingawa hili lilikuwa ni jukumu lisilopendeza, kwao wao kukataa kuitii amri ya Mtume (s.a.w.w.) walitoa udhuru wa Zayd kuwa mtumwa hapo kale.

Mara tu baadae ufunuo wa Allah ulikilaumu kitendo cha Zaynab na kaka yake kwa maneno haya: “Haiwi kwa mwanaume aliyeamini wala mwanamke aliyeamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wanapokata shauri, wawe na hiari katika shauri lao. Na Mwenye kumwasi Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, hakika amepotea upotovu ulio wazi.” (Surat al Ahzaab, 33:36).

Haraka sana Mtume (s.a.w.w.) aliwasomea Aya hii. Itikadi safi na kamili ya Bibi Zaynab na kaka yake Abdullah juu ya Mtume (s.a.w.w.) na tabia zake tukufu ilikuwa zana katika kukubali kwa yule binti Jahash tena bila ya kukawia, na matokeo yake ni kwamba yule mwanamke wa kizazi kitukufu aliolewa na mtumwa wa Mtume Muhammad (s.a.w.w.) aliyepewa uungwana. Hivyo basi, kwa njia hii, sehemu ya mpango wa Uislamu wenye kuimarisha jamii ulitimizwa na ile desturi isiyo sahihi iliondolewa kivitendo.

Zayd Atengana Na Mkewe

Hatimaye, kwa sababu fulani fulani ndoa hii iliishia kwenye talaka. Baadhi ya watu wanasema kwamba sababu ya mtengano huu ilikuwa ni fikira za mkewe Zayd, kwa kuwa alikuwa akiutaja uduni wa nasaba ya mumewe mbele yake na kujifaharisha mwenyewe kutokana na umaarufu wa familia yake na kwa kufanya hivyo akayafanya maisha ya Zayd kuwa machungu.

Hata hivyo, inawezekana kwamba Zayd mwenyewe alihusika na talaka ile, kwa sababu kumbukumbu za maisha yake zaonyesha kwamba alikuwa akiishi maisha ya kujitenga, kwa kuwa alioa wake wengi na kisha akawataliki wote (ila yule wa mwisho aliyekuwa bado yu hai wakati alipouawa kwenye vita), na talaka hizi za mfuatano zaonyesha kwamba Zayd alikuwa na moyo usiopenda kuishi na jamii.

Ushahidi wa pili juu ya maoni ya kwamba Zayd alikuwa na fungu kwenye tukio hili ni ile tabia ya ukali ambayo Mtume (s.a.w.w.) alimkanya nayo. Kwa sababu Mtume (s.a.w.w.) alipotambua ya kwamba Zayd ameamua kumwacha mkewe, aliudhika na akasema: ‘Kaa na mkeo na ichelee ghadhabu ya Allah.” Endapo kama kosa lilikuwa la mkewe hasa, kutengana kwa Zayd na yeye, hakukuwa kinyume na uchamungu na uadilifu. Hatimaye Zayd alitengana na Zaynab.

Ndoa Kwa Ajili Ya Kukomesha Desturi Nyingine Mbaya

Kabla hatujaitazama sababu ya msingi ya ndoa hii, ni muhimu kuzingatia wajibu wa nasaba ambayo ni kipengele muhimu mno kwa jamii iliyoimarika. Ikubalike kwamba uhusiano kama ule wa baba kwa mwana una msingi endelevu na kwa kweli baba yu chanzo cha kimaada cha uzazi wa mtoto na mtoto yu mrithi wa sifa za kimwili na kiakili za wazazi. Kutokana na umoja huu na damu moja, baba na mwana wanarithiana mali, na sheria makhususi zinazohusu ndoa na talaka zinakuwa ni zenye kutekelezeka kwa ajili yao.

Hivyo basi, uhusiano ambao una misingi ya kinasaba, hauwezi kuanzish- wa kwa maneno, (tazama aya 4 na ya 5 ya Surah Al-Ahzaab) na mtoto wa kulea wa mtu hawezi kuwa mtoto halisi wa mtu huyo mleaji (kama alivyo mtoto wa kuzaa). Hivyo basi, amri mbalimbali zihusianazo na mirathi, ndoa, talaka n.k. kama zitumikavyo kwa mtoto wa kuzaa, haziwezi kutumika kwa mtoto wa kulea. Kwa mfano, ingawa mtoto wa kuzaa anamrithi baba yake, na baba anamrithi mwanawe wa kuzaa, na ingawa ni haramu kwa mtu kumwoa mke aliyetalikiwa na mwanawe wa kuzaa, hata kidogo haiwezi kusemwa kwamba mtoto wa kulea vilevile anayo haki hiyo kwenye mambo haya kama alivyo huyu mtoto wa kuzaa. Bila shaka nyoro- ro ya haki hizi, zaidi ya kukosa msingi sahihi vile vile huwa aina fulani ya kichekesho kuhusiana na kisababisho kilicho muhimu (nasaba) kwenye jamii madhubuti.
Katika hali hiyo, kama ulezi wa watoto ukifanyika kwa lengo la kuzidhihirisha hisia tu hiyo inakubalika sana na ni sahihi, lakini kama itapendekezwa ili kumshirikisha mtoto wa kulea na sheria mbalimbali za kijamii ambazo zote huanzia kwenye mambo ya husikanayo na damu, basi kitendo hiki kitakuwa mbali kutoka kwenye mipaka ya kijamii.

Jamii ya kiarabu ilimchukulia mtoto wa kulea kuwa ni bora kama alivyo mtoto wa kuzaa. Kwa hiyo, Mtume (s.a.w.w.) alijulishwa ili kuifutilia mbali desturi hii isiyo sahihi kwa kumwoa Bibi Zaynab, ambaye hapo awali alikuwa mke wa mwanawe wa kulea (Zayd), na hivyo kuweza kuing’oa kivitendo tabia hii isiyofaa kutoka miongoni mwa Waarabu, kwa sababu njia hii ni yenye kufaa zaidi kuliko kuitangaza tu sheria.

Ndoa hii haikuwa na sababu yoyote nyingine zaidi ya hii, kwa sababu kwenye siku hizo hakuna aliyeweza kuwa na moyo wa kuichukua hatua hii, kwa sababu ya ukweli uliopo kwamba ilidhaniwa kuwa ni kitendo cha aibu kwa mtu kumwoa mwanamke ambaye hapo awali alikuwa mke wa mwanawe wa kulea. Hivyo basi, Allah Mwenye nguvu zote hapo awali alimjulisha Mtume (s.a.w.w.) kulitimiza jukumu hili. Anasema:“ . . .Basi Zayd alipokwisha haja naye tulikuoza wewe ili isiwe taabu kwa waumini kuwaoa wake wa watoto wao wa kulea wanapomaliza haja nao, na amri ya Mwenyezi Mungu ni yenye kutekelezwa.” (Surah al-Ahzaab, 33:37).

Tunafikiria kwamba ndoa hii ukiachilia mbali kule kuifuta desturi isiyo sahihi, vile vile imedhihirisha mno usawa, kwa sababu Mtume (s.a.w.w.) alimwoa mwanamke ambaye hapo awali alikuwa mke wa mtumwa wake aliyepewa uungwana, na katika siku hizo ndoa ya aina hiyo vilevile ili- fikiriwa kuwa kijamii si yenye utukufu.

Hatua hii ya kishujaa ya Mtume (s.a.w.w.) ilileta maneno ya lawama kuto- ka kwa wanafiki na watu wasioona mbali nao wakawa wakizieneza habari: “Muhammad amemwoa mke wa mwanawe wa kulea!”

Ili kuzivunja fikara za aina hii, Allah Mwenye nguvu zote Aliteremsha Aya hii: “Muhammad si baba wa yeyote miongoni mwa wanaume wenu, bali ni Mtume wa Allah na hitimisho la Manabii, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.” (Surah al-Ahzaab, 33:40).

Qur’ani Tukufu haikutosheka na hilo tu. Allah alimsifu Mtume Wake (s.a.w.w.) aliyeonyesha ujasiri na ushujaa mwingi katika kuzitekeleza amri Zake, yaani Aya ya 38 na ya 39 ya Surat al-Ahzaab. Kiini cha Aya mbili hizi ni hiki: “Muhammad ni kama walivyo Manabii wengine ambao waliowapelekea watu ujumbe wa Allah, naye hamwogopi yeyote yule katika kuzitekeleza amri Zake”2

Hii ndio falsafa ya ndoa ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.) na Bibi Zaynab. Sasa tutayachunguza kwa makini maoni ya mustashirik juu ya jambo hili.

Hadithi Ya Kuzusha Juu Ya Bibi Zaynab Ni Uwongo Mtupu

Ndoa ya Mtume (s.a.w.w.) na bibi Zaynab ni jambo la kawaida lililo huru kutokana na aina zote za utata. Hata hivyo, kwa vile baadhi ya wataalamu wa nchi za Mashariki wamelifanya tukio hili kuwa sababu ya kuwapotosha watu wapumbavu na wajinga, na kwa njia hii wamejaribu kuidhoofisha imani ya wale wasiokuwa na taarifa sahihi juu ya tabia ya Mtume (s.a.w.w.), inaonekana kuwa ni lazima kwamba tuyachunguze maelezo ya kundi hili la wataalamu wa mambo ya nchi za Mashariki na kuyafanya mambo kuwa ya dhahiri.

Kama ielewekavyo, wakoloni hawaitumii nguvu yao ya kijeshi na kiuchu- mi tu katika kuzitawala nchi za Mashariki, lakini wakati mwingine huingia kwa kupitia mlango wa elimu na utafiti, na kwa njia ya mipango iliyopangwa kwa uangalifu wanajaribu kuiweka aina mbaya zaidi ya ukoloni (yaani ukoloni wa kiakili) juu ya watu hawa.

Kusema kweli, mustashirik ni yule mkoloni wa kujieneza atendaye mambo katika njia maalum kwenye nyoyo za jamii na miongoni mwa watu wenye elimu na kuyafikia malengo yake ya kikoloni kwa kuzipumbaza akili za tabaka la wenye elimu.

Inawezekana kwamba wengi wa waandishi wa Magharibi na wapenzi wa elimu na hekima wasikubaliane na maelezo tuliyoyeleza hapo juu na kutulaumu kwa ugumu wa ushupavu wa moyo katika dini bila ya kutumia akili, na wakafikiria ya kwamba kiburi cha kitaifa au cha kidini kimetufanya tuyatoe maoni haya. Hata hivyo, maandishi ya mustashirik na kuuficha kwao ukweli na tabia yao ya upendeleo kwenye mambo yahusianayo na historia ya Uislamu ni ushahidi wa dhahiri na ukweli uliopo kwamba, wengi wao hawakusukumwa na kiu ya elimu na kuutafuta ukweli na hivyo maandishi yao yamechafuliwa na mlolongo wa fikira zisizo za kidini wala za kitaifa.3

Jambo tunalolijadili hapa linaudhihirisha ukweli huu. Kwa dhana maalumu na ya kipekee ya watu wa Magharibi, wameipa ndoa hii lengo pekee la ambalo lilikuwa ni kufuta desturi potovu, wameipaka ndoa hii rangi ya ‘mapenzi’, na wakaizushia kisa kama vile wafanyavyo waandishi wa hadithi za paukwa pakawa na wasimuliaji wa hekaya, wakakihusisha na mtu aliye mtakatifu zaidi wa ulimwengu wa mwanadamu.

Kwa vyovyote vile, misingi ya ngano hizi ni zile sentensi zilizonakiliwa na Tabari4 na Ibn Athir5 na baadhi ya wafasiri wa Qur’ani kwamba, siku moja Mtume (s.a.w.w.) alibahatika kumwona Bibi Zaynab mkewe Zayd.

Zayd akahisi kwamba Mtume ameangukia kumpenda Bibi Zaynab. Kutokana na heshima ya Zayd iliyokithiri juu ya Mtume (s.a.w.w.) alikuja mbele yake na kupendekeza kumtaliki Bibi Zaynab, ili kisiwepo kizuizi kwa Mtume (s.a.w.w.) kumwoa. Mtume (s.a.w.w.) alimkataza kumtaliki mkewe kwa kurudia rudia, lakini hatimaye alimtaliki na Mtume akamwoa.

Hata hivyo, mustashirik badala ya kuchunguza historia sahihi, hawaku- tosheka hata na ngano hii ya kuzushwa tu na wameipamba mno kiasi kwamba imejitwalia umbo la hadith za ‘Alfu laila u-lela,’.

Bila shaka watu wale wanaozifahamu tabia bora zaidi za Mtume (s.a.w.w.) wameichukulia hadith ya asilia na yale mapambo yaliyotiwa humo kuwa ni uzushi na ngano halisi na wazo lililo batili kwa kuwa haiafikiani na kipimo chenye kuyahusu maisha ya Mtume (s.a.waw). Aidha, wanachuoni kama vile Fakhrur-Razi na Aahisi, wameipinga hadithi hii waziwazi na wamesema kwamba imezushwa na maadui wa Uislamu na ikaenezwa miongoni mwa waandishi wa Kiislamu.6

Yawezaje kusemwa kwamba sehemu hii ya kihistoria iliaminiwa na Tabari7 na Ibn Athir ambapo dazeni ya waandishi wamenukuu kinyume chake na kumchukulia Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) kuwa safi kabisa kutokana na kila aina ya uchafu.

Hata hivyo, tungalipenda kutaja kwenye kurasa hizi dalili na ishara za hadithi hii kuwa ni nyenye kughushiwa na kuidhihirisha hali hiyo kabisa kiasi cha kutohitaji maelezo ya kuihami zaidi. Ufuatao hapa chini ndio ushahidi wetu:

Hadithi iliyotajwa hapo juu ni kinyume na kauli ikubaliwayo katika Uislamu na Waislamu wenyewe, kwa sababu kama ilivyoshuhudiwa kati- ka Aya ya 37 ya Sura al–Ahzaab, ndoa ya Mtume (s.a.w.w.) na Bibi Zaynab ni kuipinga fikara ya Waarabu isiyo sahihi, kwamba mtu hakuruhusiwa kumwoa mtalaka au mjane wa mwanawe wa kumlea, na ndoa hii ilifanyika kwa Amri ya Allah na wala haikuwa matokeo ya huba na mahaba.

Katika siku za awali za Uislamu hakuna yeyote aliyeupinga ukweli huu, na kama yale maelezo ya Qur’ani yangalipingana na ukweli, basi Wayahudi, Wakristo na Wanafiki mara moja wangalisimama na kuyalaumu na wangalilalamika, ambapo kwa kweli hawakuweza kulithibitisha jambo lolote lililo baya, ingawa daima walikuwa na shauku kubwa ya kupata makosa ya Mtume (s.a.w.w.).

Bibi Zaynab alikuwa ni mwanamke yule ambaye kabla ya kuolewea kwake na Zayd alipenda aolewe na Mtume (s.a.w.w.). Hata hivyo, ingawa alikuwa na mwelekeo huo, Mtume (s.a.w.w.) alisisitiza ya kwamba aolewe na yule mtumwa wake aliyempa uungwana, yaani Zayd. Kama kweli Mtume (s.a.w.w.) alipenda kumwoa hapakuwapo na kizuizi chochote katika kufanya hivyo. Basi ni kwa nini asimwoe? Kinyume na hivyo tunaona kwamba ingawa ulikuwako mwelekeo wote huo aliouona toka upande wa Bibi Zaynab, sio tu kwamba hakumpa jibu la kukubali, bali alimshauri aolewe na mtu mwingine.

Hivyo wakati maoni yao yanapokanushwa na historia, huwa hakuna nafasi ya yale mapambo yaliyotiwa na wanachuoni wa kikoloni. Na sisi tunayaamini maisha ya Mtume (s.a.w.w.) aliyeutumia muda wake hadi ikafikia miaka hamsini akiwa na mwanamke aliyekuwa mtu mzima kuliko yeye kwa miaka kumi na saba kuwa ni safi kabisa na bora kiasi cha kutoweza kuuthibitisha ukweli wa maelezo ya upinzani juu yake. Hivyo basi, sisi tunaacha kunukuu hapa maelezo ya hao Mustashirik.

Maelezo Ya Sehemu Mbili Za Aya Hiyo

Ili kukamilisha majadiliano haya tunatoa hapa chini Aya iliyoteremshwa juu ya jambo hili, pamoja na sehemu zake mbili, ambazo ndio sababu ya kusitasita na kuwa na mashaka miongoni mwa baadhi ya watu wasio na elimu ya kutosha, na kisha tutatoa maelezo yao. Yafuatayo ni maneno ya Aya hiyo: “Na ulipomwambia yule ambaye Allah amemneemesha na wewe (nawe) umemneemesha: Shikamana na mkeo na umche Allah . . .” (Sura al-Ahzaab, 33:37).

Hakuna fumbo lolote kwenye sehemu hii ya Aya lakini sehemu mbili zifuatazo zinahitaji ufafanuzi. “Na ukaficha nafsini mwako aliyotaka Allah kuyatoa.” Hapa swali huibuka: Mtume (s.a.w.w.) alikuwa akificha nini pale alipokuwa akimshauri Zayd, ambacho Allah Alitaka kukidhihirisha? Inawezekana kudhania kwamba kile Mtume (s.a.w.w.) alichokuwa akikifanya nafsini kilikuwa kwamba, ingawa alikuwa akimkataza Zayd kumta- liki mkewe, lakini yeye alipendelea ya kwamba amtaliki Bibi Zaynab ili yeye amwoe.

Hitimisho kama hili haliwezi kuwa sahihi kwa sababu yoyote ile, kwa kuwa kama kwa siri Mtume (s.a.w.w.) alikuwa akifikiria hivyo, kwa nini Allah asiutaje ukweli huu kwa kuzipitia Aya nyingine wakati Yeye mwenyewe Allah anasema sehemu hii kwamba: Chochote kile akifichacho, Allah atakidhihirisha? Hivyo basi, wafasiri wetu wakuu wa Qur’ani tukufu wanasema kwamba maana ya kile kitu alichokificha ni ule ufunuo alioteremshiwa na Allah.

Ili kueleza dhahiri; Allah alimfunulia ya kwamba Zayd atamtaliki mkewe, naye Mtume (s.a.w.w.) atamwoa ili kuipinga ile dhana isiyo sahihi (ya kwamba ni haramu kwa mtu kumwoa mwanamke aliyekuwa kaolewa na mwanawe wa kulea). Hivyo basi, alipokuwa akimshauri Zayd ufunuo huu ulikuwa anao akilini mwake lakini aliufanya siri kwa Zayd na wengineo. Hata hivyo, kwenye hiyo aya tuliyoitaja hapo juu, Allah anamwambia Mtume (s.a.w.w.) kwamba, Yeye atayadhihirisha yale aliyonayo akilini mwake.
Yaliyoelezwa hapo juu yanaungwa mkono na ukweli uliopo kwamba chini ya Aya hiyo hiyo Qur’ani tukufu inalitaja jambo hili kwa maneno haya:

وَإِذْ تَقُولُ لِلَّذِي أَنْعَمَ اللَّهُ عَلَيْهِ وَأَنْعَمْتَ عَلَيْهِ أَمْسِكْ عَلَيْكَ زَوْجَكَ وَاتَّقِ اللَّهَ وَتُخْفِي فِي نَفْسِكَ مَا اللَّهُ مُبْدِيهِ وَتَخْشَى النَّاسَ وَاللَّهُ أَحَقُّ أَنْ تَخْشَاهُ ۖ فَلَمَّا قَضَىٰ زَيْدٌ مِنْهَا وَطَرًا زَوَّجْنَاكَهَا لِكَيْ لَا يَكُونَ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ حَرَجٌ فِي أَزْوَاجِ أَدْعِيَائِهِمْ إِذَا قَضَوْا مِنْهُنَّ وَطَرًا ۚ وَكَانَ أَمْرُ اللَّهِ مَفْعُولًا {37}

“Basi Zayd alipokwisha haja naye tulikuoza wewe ili isiwe taabu kwa waumini kuwaoa wake wa watoto wao wa kulea wanapomaliza haja nao, na amri ya Mwenyezi Mungu ni yenye kutekelezwa.” (Surah al- Ahzaab, 33:37).

Kutoka kwenye sehemu hii ya Aya tuliyoinukuu hapo juu tunajifunza ya kwamba alichokuwa akikificha Mtume (s.a.w.w.) kilikuwa ni ule Ufunuo wa Alllah kwamba ili kuifutilia mbali desturi isiyo sahihi hana budi kum- woa mke wa mwanawe wa kulea yule mwanawe atakapomtaliki mke yule.

“. . . . . Na ukawachelea watu, hali Allah ndiye Mwenye haki zaidi ya kumchelea; . . “ Kifungu hiki ni sehemu ya pili isiyo na utata zaidi inapolinganishwa na ile ya kwanza, kwa sababu ili kuikomesha desturi iliyokuwapo kwenye mazingira yaliyochafuliwa kwa miaka kadhaa au zaidi, (yaani ndoa ya mwanamke ambaye hapo mwanzo aliolewa na mwana wa kulea) kwa kawaida kuliandamana na ugumu wa kiakili ambao uliondolewa kwenye moyo wa Mtume (s.a.w.w.) kwa mazingatio ya amri za Allah. Kama Mtume (s.a.w.w.) alihisi wasiwasi au alikuwa akihofia, ni kwa sababu alikuwa akifikiria kwamba Waarabu, waliojitenga naye, kutokana na ujinga na mawazo machafu watasema: ‘Mtume amelichagua jambo la aibu,’ ingawa kwa kweli, si aibu kitu.

  • 1. Rejea kwenye Usudul Ghabah; Al-Isti’aab na al-Isabaah chini ya neno Zayd.
  • 2. Maelezo ya hizi Aya mbili ni haya: “Si kosa kwa Nabii katika yale ambayo Mwenyezi Mungu amemlazimisha, ndiyo kawaida ya Mwenyezi Mungu kwa wale waliopita zamani, na amri ya Mwenyezi Mungu ni kipimo kilichokadiriwa. Wale wanaofikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu na kumwogopa Yeye wala hawamwogopi yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ndiye atoshaye kuhesabu.” (Surah al-Ahzaab, 33:38-39).
  • 3. Kwa maelezo zaidi rejea kitabu ‘al-Mustashriqun’
  • 4. Tarikhut-Tabari, Juz. 2.
  • 5. Tarikhul Kamil, Juz. 2, uk.121.
  • 6. Mafaatil Ghayb Razi, Juz. 15, na Ruhul Ma’aani, sura ya 22, uk. 23-24.
  • 7. Tunasikitika kusema kuwa mwanahistoria huyu wa kale amechangia sehemu kubwa kuwapa mustashrik fursa ya kumkejeli na kumshusha daraja Mtume (s.a.w.w.), hiyo ni kutokana na kitabu chake cha historia kilicho muhimu katika ulimwengu wa Kisuni kujaa ngano na uzushi usiovumilika. Ikimbukwe hata kadhia hizi za hivi punde za waandishi wa Denmaki kumchora Mtume kikatuni ni matunda ya waandishi kama hawa. Mwanahistoria huyu ndiye chimbuko la wazo la kuwepo kwa Abdallah bin Saba, mtu wa kufikirika aliyefanywa chambo cha kuwatusi na kuwadhalilisha na kuwatuhumu waisilamu halisi – Mhariri.