Sura Ya 37: Vita Vya Ahzaab

Katika vita hivi majeshi ya Waarabu waabudu masanamu na Wayahudi walikusanyika dhidi ya Uislamu na, baada ya kuunda ushirikiano wa kijeshi wenye nguvu, waliuzingira mji wa Madina kwa kipindi cha mwezi mmoja hivi. Kwa kuwa makabila na makundi mbalimbali yalishiriki kwenye vita hivi na kwa kuwa Waislamu walichimba handaki kuuzunguka mji wa Madina, ili kumzuia adui asiingiye humo, vita hivi viliitwa vita vya Ahzaab, yaani vita vya makundi. Vile vile vinaitwa Vita vya Khandaq, yaani vita vya handaki.

Wale waliochochea vita hivi walikuwa ni viongozi wa kabila la kiyahudi la Bani Nuzayr na vile vile kundi la Bani Waail. Lile pigo kali walilolipata wale Wayahudi wa Bani Nuzayr kutoka kwa Waislamu na jinsi walivyoutoka mji wa Madina kwa kulazimishwa na wakaenda kuishi Khaybar, viliwafanya wapange mpango madhubuti kwa ajili ya kuupindua msingi wa Uislamu. Na kwa kweli, walipanga mpango wa hatari mno na wakawakabili Waislamu pamoja na makabila mbalimbali. Tukio hili halikuwa na kifani kwenye historia ya Waarabu.

Mpango wao ulikuwa kwamba viongozi wa kabila la Bani Nuzayr, kama vile Salam bin Abil Haqiq na Hay bin Akhtab walifika Makka pamoja na baadhi ya watu wa kabila la Waa’il na baada ya kuwasiliana na machifu wa Waquraishi, aliwaambia: “Muhammad amekufanyeni ninyi na sisi kuwa shabaha zake na amewalazimisha Wayahudi wa Bani Qaynuqa’ na Bani Nuzayr kuitoka nchi yao. Ninyi Waquraishi hamna budi kuamka na kuomba msaada kutoka kwa marafiki zenu nasi tunao wapiganaji wa panga wa kiyahudi mia saba (Bani Quraydha) watakaojitokeza upesiupesi kukusaidi- eni. Wayahudi wa Bani Quraydha wamefanya kwa dhahiri mapatano ya kiulinzi na Muhammad lakini tutawashauri kuyatupilia mbali mapatano yale na kujiunga nanyi”.1

Machifu wa Waquraishi walionyesha ukweli wao na kuchoka kupigana na Waislamu, lakini majigambo ya hawa watu wawili yaliwavutia na wakaukubali mpango wao. Hata hivyo, kabla ya kuthibitisha kukubali kwao, waliwauliza wale viongozi wa Wayahudi hivi:
“Ninyi ni watu wa Kitabu na muwafuasi wa Vitabu vilivyofunuliwa nanyi mnao uwezo wa kutosha wa kubainisha baina ya haki na batili, Mnatambua ya kwamba hatuna tofauti yoyote na Muhammad ila kwa sababu ya dini yake tu iliyotofauti na yetu. Sasa, hebu tafadhalini tuelezeni ukweli, ni ipi kati ya dini hizi mbili ambayo ni bora, dini yetu au ni ile yake iliyosimamia kwenye msingi wa Allah Aliye Mmoja tu na kuyavunja masanamu na kuyabomoa mahekalu ya masanamu?”

Hebu tuone ni jibu gani watu hawa waliojifikiria kwamba ni wenye kuliunga mkono fundisho la Upweke wa Allah na washika bendera wa itikadi ya Upweke wa Mungu walilowapa wale watu wa kundi la wajinga na wasio na walimu, waliwatambua kuwa wao ni watu walioelimika na kuliweka tatizo lao mbele yao.

Bila ya aibu waliwajibu hivi: “Ibada ya masanamu ni bora kuliko dini ya Muhammad. Hamna budi kubakia imara kwenye dini yenu na msionyeshe mwelekeo japo ulio mdogo sana kwenye dini yake.” 2

Hili lilikuwa ni doa la aibu mno kuhusiana na tabia za wayahudi, waliofanya uso wa historia ya dini ya Kiyahudi ambao tayari ulikuwa umeshafanywa kuwa mweusi na kuwa mweusi zaidi. Kosa lao hili lilikuwa lisilosameheka kabisa kiasi kwamba waandishi wa Kiyahudi walizidhihirisha huzuni zao nyingi juu ya jambo hili. Dakta Israeli anaandika kwenye kitabu chake kiitwacho History of the Jews and Arabia (Historia ya Wayahudi na Waarabu), hivi: “Haikuwa sahihi kwamba Wayahudi watende kosa la aina hii japo Waquraishi wangalikataa maombi yao. Aidha, haikuwa sahihi hata kidogo vilevile kwamba waombe ulinzi wa waabudu masanamu, kwa sababu kufanya hivyo hakuafikiani na mafundisho ya Taurati.”3

Kusema kweli hii ndio sera ya wanasiasa wa siku hizi waliojitwalia ili kuyafikia malengo na madhumuni yao. Kwa nguvu sana wanaamini kwamba ili mtu kufikia lengo lake lazima atumie njia zote zinazokubalika na zisizokubalika, na kwa kweli kwa mujibu wa fikra zao kufanikiwa kwa lengo hufanya vitu visivyo kubalika kukubalika kwao. Qur’ani Tukufu inasema hivi:

“Je, huwaoni wale waliopewa fungu katika Kitabu, wanaamini sanamu na shetani, na wakiwasema wale waliokufuru kuwa; Wao wameongoka zaidi katika njia kuliko walioamini.” (Sura al-Nisa, 4:51).

Maneno ya watu hawa waitwao wanachuoni yaliwavutia wenye kuyaabudu masananu. Kwa hiyo, wakaonesha kukubaliana kwao na ule mpango wao na vilevile wakaweka muda wa kwenda Madina.

Watu wale ambao waliokuwa na shauku ya kuanzisha vita walitoka mji wa Makka huku nyoyo zao zikiwa zimefurahi sana, na kwanza wakaenda Najd kuonana na watu wa kabila la Ghatfaan waliokuwa maadui wakuu wa Uislamu. Mbali ya kabila la Ghatfaan, koo za Bani Fazalah, Bani Murrah na Bani Asja walilikubali ombi lao chini ya sharti ya kwamba, baada ya kupata ushindi wapewe mapato ya mwaka mmoja ya Khaibar. Hata hivyo, jambo hili halikukomea hapo, kwa sababu Waquraishi waliwasiliana na marafiki zao Bani Asad na kuwaomba wajiunge na ushirika huu wa kivita. Bani Salim na Bani Asad walilikubali ombi hilo na katika siku iliyowekwa makabila yote haya yalitoka sehemu mbalimbali za Uarabuni ili kuuzingi- ra na kuuteka mji wa Madina. 4

Idara Ya Upelelezi Ya Waislamu

Kuanzia siku ile Mtume (s.a.w.w.) alipotulia mjini Madina, daima alikuwa akituma watu wajanja kwenye sehemu mbalimbali ili wapate kumwarifu kuhusu hali iliyokuwapo kwenye sehemu zile pamoja na matendo ya watu waliokiishi kwenye sehemu za nje za eneo la Waislamu. Wale watoa habari walimwarifu ya kwamba ushirikiano wa kijeshi ulio na nguvu mno umeundwa dhidi ya Uislamu na watu wale wangaliweza kuja kuuzingira mji wa Madina kwenye siku maalum. Upesi sana Mtume (s.a.w.w.) aliiarifu halmashauri ya ushauriano ili iweze kufanya uamuzi, wakiyazingatia matokeo machungu ya Vita vya Uhud.
Baadhi ya watu walipendelea kuji- hami kwa ndani ya ngome na kupigana kutoka kwenye minara na sehemu za juu badala ya kwenda nje ya mji kumkabili adui. Hata hivyo mpango huu haukutosheleza, kwa sababu kundi kubwa la mashujaa wa Uarabuni lenye maelfu ya askari, lingaliweza kuzibomoa zile ngome na minara na kuwazidi nguvu Waislamu. Hivyo basi lilikuwa jambo muhimu kuchukua hatua za kuthibitisha kwamba adui hafaulu kufikia mji wa Madina.

Salman Farsi, aliyekuwa na ujuzi kamili wa mbinu za kivita za Wairani akasema: “Huko Iran watu wanapotishiwa kushambuliwa na maadui, wanachimba handaki lenye kina kirefu kuuzunguka mji na kwa kufanya hivyo wakaweza kuwazuia maadui kuuingia mji ule.

Hivyo basi, ingelifaa kuzihami sehemu zile za Mji wa Madina ambazo zaweza kushambuliwa kwa urahisi kwa kuzichimbia handaki na kuweza kumzuia adui kwa njia hiyo kwenye maeneo hayo.

Sambamba na handaki hilo ijengwe minara na vibanda vya kungojea zamu kwenye kingo za handaki hilo kwa ajili ya ulinzi na maadui wazuiwe wasilipite handaki hilo kwa kuwatupia mishale na kuwavurumishia mawe kutoka kwenye minara na hizo ngome.”5

Ushauri alioutoa Salman ulikubaliwa na watu wengi na mpango huu wa ulinzi ulisaidia sana katika usalama wa Waislamu. Mtume (s.a.w.w.) akifuatana na baadhi ya watu, alizikagua sehemu zote zilizo rahisi kushambuli- wa na akaziwekea alama zile sehemu zilizohitaji kuchimbwa handaki.

Iliamuliwa kwamba lichimbwe handaki tangu Uhud hadi Ratij, na ili kudumisha utaratibu mwema kila watu kumi walipewa dhiraa arobaini. Mtume (s.a.w.w.) mwenyewe alipiga sururu ya kwanza kabisa ardhini na kuchim- ba, wakati Sayyidna Ali (a.s.) akijishughulisha na kuutupa udongo nje ya handaki lile. Uso na paji la uso la Mtume (s.a.w.w.) lilikuwa likitoka jasho, na alikuwa akisema: “Maisha ya kweli ni maisha ya Akhera. Ee Allah! Waghufirie Muhajiriin na Ansar!”

Kwa kujishughulisha kwake na kazi hii, Mtume (s.a.w.w.) alionyesha sehemu ya mpango wa Uislamu na kuifanya jamii ya Kiislamu kuelewa kwamba kamanda wa jeshi na kiongozi wa jamii hanabudi kuzivumilia taabu kama wengine na kuwaondolea watu mzigo wao. Kazi ya Mtume (s.a.w.w.) ilizaa shauku isiyo kifani miongoni mwa Waislamu wote, bila ya kusalia yeyote yule, walianza kufanya kazi mno kiasi kwamba Wayahudi waliofanya mapatano na Waislamu nao walitoa msaada kwa kutoa vifaa.6

Waislamu walikuwa na shida mno ya chakula katika siku zile na familia zilizokuwa na uwezo zilikuwa zikiwapa msaada wale askari wa Uislamu.

Uchimbaji wa handaki lile ulipokuwa mgumu kutokana na kutokea kwa mawe makubwa walimwendea Mtume (s.a.w.w.) ambaye yeye mwenyewe aliivunja miamba mikubwa kwa pigo kubwa.

Urefu wa handaki hili uliweza kukisiwa kwa kuichukua idadi ya wale wafanyakazi. Kwa mujibu wa kauli maarufu idadi ya Waislamu katika siku zile ilikuwa ni 3,000 na kama kuchimba dhiraa arobaini kulifanywa na watu kumi, urefu wa handaki lile utakuwa ni dhiraa 12, 000 na upana wake ulikuwa mkubwa sana kiasi kwamba wapanda wanyama werevu na wazoefu hawakuweza kulipita wakiwa kwenye migongo ya farasi.7

Maelezo Maarufu Ya Mtume (S.A.W.W.) Kuhusiana Na Salman

Wale wafanyakazi walipokuwa wakitawanywa ulizuka mzozo baina ya Muhajirina na Ansar kuhusiana na Salman. Kila mmoja wa pande hizo mbili ulidai kwamba Salman alitokana nao.

Katika hali ile Mtume (s.a.w.w.) aliumaliza mzozo ule kwa kutoa amri yenye maamuzi na kusema: “Salman yu mmoja wa watu wa nyumba yangu.”8

Mtume alitumia mchana na usiku kandoni mwa ukingo wa handaki lile hadi ile kazi ilipomalizika. Hata hivyo wanafiki hawakuifanya kazi ile kwa kutoa udhuru, nyakati fulani fulani waliondoka kwenda majumbani mwao bila hata ya kumuaga Mtume (s.a.w.w.) ambapo wale waumini wa kweli walibakia wakijishughulisha na kazi yao kwa nia madhubuti, na waliacha kufanya kazi kwa sababu njema na baada ya kupata ruhusa kutoka kwa yule kamanda, na kurejea kazini wakati udhuru ule ulipomalizika, jambo hili limesimuliwa katika Aya ya 63 ya Suratun-Nur.

Jeshi La Waarabu Na Wayahudi Lauzingira Mji Wa Madina

Jeshi la Waarabu lilipiga kambi kama kundi la wadudu na nzige kwenye ukingo wa lile handaki lenye kina kirefu lililochimbwa na Waislamu kiasi cha siku sita tu kabla ya kuwasili kwao. Walitegemea kulikabili jeshi la Uislamu chini ya mlima Uhud, lakini walipofika jangwa la Uhud hawakuona dalili yoyote ya Waislamu hapo. Hivyo waliendelea hadi walipoufikia ukingo wa handaki lile.

Walishangazwa mno kuliona lile handaki kandokando mwa zile sehemu za mji wa Madina zilizokuwa rahisi kuzishambulia na wote wakasema: “Muhammad kajifunza mbinu hizi za vita kutoka kwa Mwirani. Kwa kuwa Waarabu hawana uzoefu wa aina hii ya mbinu za kivita.”

Idadi Ya Askari Wa Hayo Majeshi Mawili

Lile jeshi la Waarabu lilikuwa na askari zaidi ya 10,000. Mwanga wa panga zao kutoka nyuma ya lile handaki uliyashangaza macho. Kufuatana na ilivyonukuliwa na Maqrizi katika ‘al-Imt?’ Waquraish peke yao walipiga kambi kwenye ukingo wa lile handaki na askari 4000, wapanda farasi mia tatu na ngamia 1500, na kabila la Salim lilijiunga nao mahali paitwapo Murruz Zahraan wakiwa na watu 700.

Kabila la Bani Fazaarah walikuwa na watu 1000 na kabila la Bani Ashja na Bani Murrah walikuwa na watu 400 kila moja, na makabila mengine ambayo idadi yao ilizidi watu 10,000 walipiga kambi kwenye sehemu nyingine.

Waislamu hawakuzidi elfu tatu na sehemu waliyopigia kambi yao ilikuwa chini ya mlima Sala’ iliyokuwa sehemu iliyoinuka. Sehemu hii ililitawala lile handaki kikamilifu pamoja na sehemu zake za nje na matendo yote na

mienendo ya jeshi viliweza kuonekana kwa dhahiri kutoka kwenye sehe- mu ile. Baadhi ya Waislamu waliwekwa kulinda ile minara na vile vibanda vya kulindia na kuitawala ile mienendo ya watu kwenye lile handaki, nao walimzuia adui asilivuke lile handaki kwa njia ya ngome za kimaumbile na za kutengeneza.

Jeshi la Waarabu lilikaa kwenye upande wa pili wa handaki kwa kipindi cha takriban mwezi mzima na katika kipindi hicho si zaidi ya watu wachache walioweza kulivuka handaki lile. Na wale waliojaribu kuvuka handaki lile walirudishwa nyuma kwa njia ya mawe maalum (kombeo au teo) yaliyokuwa yakitumika kwenye zama zile badala ya risasi za siku hizi.

Katika kipindi hiki Waislamu walipata matukio ya kijasiri ya kuvutia pamoja na Waarabu hawa wenye kuchupa mipaka kama ilivyohifadhiwa kwenye historia. 9

Ukali Wa Majira Ya Baridi Na Upungufu Wa Chakula

Vita vya Ahzaab vilitokea wakati wa majira ya kipupwe. Mji wa Madina ulikabiliwa na ukame katika mwaka ule na hali ya njaa ilikuwepo mjini mle. Kiasi cha chakula walichokuwa nacho lile jeshi la Waarabu hakikutosheleza kuwaruhusu kuendelea kukaa pale zaidi ya hapo, kwa kuwa hawakufikiria kamwe kwamba wangeliweza kuzuiwa kwenye ukingo wa lile handaki kwa kipindi cha mwezi mzima kamili. Kinyume na hivyo walikuwa na uhakika kwamba kwa shambulio moja tu wangeliweza kuwashinda wale wapiganaji wa Kiislamu na kuwaua wote kwa panga.

Wale waliowasha moto wa vita hivi (yaani Wayahudi) waliitambua hali hii mbaya, baada ya siku chache tu walielewa kwamba kwa kadiri muda ulivyoendelea kupita uamuzi wa makamanda wa jeshi utadhoofika na watapatwa na ukali wa yale majira ya baridi na upungufu wa malisho na vyakula. Hivyo basi, ikawajia fikara ya kuomba msaada wa Bani Quraydha waliokuwa wakiishi mjini Madina, ili waweze kuwasha moto wa vita ndani ya mji ule na hivyo kuifungua njia kwa jeshi la Waarabu kuingia mjini humo.

Hay Bin Akhtab Awasili Kwenye Ngome Ya Bani Quraydhah

Bani Quraydha walikuwa Wayahudi pekee waliokuwa wakiishi Mjini Madina pamoja na Waislamu kwa amani kamili na utulivu na waliyaheshimu yale mapatano waliyofanya na Mtume Muhammad (s.a.w.w.).

Hay bin Akhtab alihisi kwamba ushindi utapatikana kwa kuomba msaada kwa ajili ya jeshi la Waarabu kutoka ndani ya mji wa Madina.

Aliamua kuwachochea Bani Quraydha kuyakana yale mapatano waliyoyafanya na Waislamu ili yaanze mapigano baina yao na hizi ghasia za ndani zingaliweza kuleta ushindi kwa jeshi la Waarabu. Kwa mpango huu akilini mwake, aliiendea ngome ya Bani Quraydha na kujitambulisha. Ka’ab aliyekuwa chifu wa Bani Quraydha aliamrisha kwamba lango la ile ngome lisifunguliwe.

Hata hivyo, Hay alisisitiza na kuomba na akasema kwa sauti kuu: “Ewe Ka’ab! Je, hulifungui lango kwa sababu unachelea mkate wako na maji yako (yaani kwa sababu unachelea kwamba itakubidi kunilisha). Sentensi hii iliangaza juu ya ukarimu na utu wa chifu aliyekubaliwa na watu wote kama vile Ka’ab. Hivyo ilimhimiza kuruhusu kwamba lile lango lifunguliwe kwa ajili ya Hay.

Huyu mwanzilishi wa vita alikaa karibu na mwanadini mwenzie na akazungumza naye kwa maneno haya; “Nimekuletea neno la heshima na ukuu kwako. Machifu wa Waquraishi watukufu wa Uarabuni na wafalme wa Ghitfaan wenye silaha za kutosha, wamepiga kambi kwenye ukingo wa handaki ili kumwangamiza adui wetu sote (Mtume s.a.w.w) nao wamenipa ahadi ya kwamba hawatarejea makwao.”

Ka’ab alijibu hivi: “Ninaapa kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu zote kwamba wewe umeleta aibu na fedheha. Kwa maoni yangu, jeshi la Waarabu ni kama wingu lililo na mvua lenye kuunguruma lakini halinyeshi mvua.

Ewe mwana wa Akhtab! Ewe mwanzilishi wa vita! Iweke mikono yako mbali nasi. Sifa njema za Mtume Muhammad zinatuzuia kuyakana yale mapatano tuliyoyafanya naye. Hakuna tulichokiona kwake ila ukweli, uaminifu na unyofu. Sasa vipi tunaweza kumsaliti?”

Akiwa kama mpanda ngamia stadi amtiishaye ngamia mkaidi kwa kuikunakuna nundu yake, Hay bin Akhtab alizungumza mambo mengi mno kwa Ka’ab kiasi kwamba hatimaye alikubali kuyakana yale mapatano. Vile vile Hay alimwahidi Ka’ab kwamba kama jeshi la Waarabu halitamshinda Muhammad, yeye (Hay) mwenyewe atakuja pale ngomeni na kushiriki katika hatima ya Ka’ab.

Ka’ab aliwaita machifu wa Wayahudi mbele ya Hay na kuiarifu halmashauri ya ushauriano na akawataka watoe imani yao, wote wakasema: “Unaweza kuamua lolote lile unaloana kuwa linafaa nasi tutakutii.”10

Zubayr Bata, aliyekuwa mzee alisema: “Nimesoma kwenye Taurati kwamba katika siku za baadae, Mtume atainuka kutoka Makka. Atahajiria Madina. Dini yake itaenea ulimwenguni kote na hakuna jeshi litakalopata ushindi dhidi yake. Kama Muhammad ndiye Mtume yule jeshi hili halitamshinda.” Mara moja yule mwana wa Akhtab akasema: “Yule Nabii atatoka miongoni mwa Bani Israeli, ambapo Muhammad yu dhuria wa Isma’il; amewakusanya watu hawa karibu yake kwa njia ya udanganyifu na uchawi.”

Alizungumza mno juu ya jambo hili kiasi kwamba alifaulu kuwafanya waamue kuyaasi yale mapatano. Vile vile alitaka apewe ile karatasi yenye yale mapatano yaliyofanywa baina ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.) na Bani Quraydha na akalipasua vipande vipande machoni pao. Kisha akasema: “Sasa jambo hili limeshamalizika. Hamna budi kuwa tayari kupigana vita.”11

Mtume (S.A.W.W) Atambua Kuvunjwa Kwa Mapatano Na Bani Quraydhah

Mtume (s.a.w.w.) aliarifiwa na watumishi wake stadi kuhusu kuvunjwa kwa mapatano na Bani Quraydha katika wakati huu mgumu. Aliingiwa na wasiwasi mno kutokana na jambo hili. Mara moja akamtuma Saad bin Mu’aaz na Sa’da bin Ubadah waliokuwa askari mashujaa wa Uislamu na machifu wa makabila ya Aws na Khazraji kwenda kupata taarifa sahihi. Vile vile aliwaelekeza ya kwamba kama usaliti wa Bani Quraydha ukionekana kwamba ni kweli wamweleze jambo hilo kwa kutumia neno la siri (code-word) la ‘Azal na Qaarah’ (Majina ya makabila mawili yaliyowakaribisha wahubiri wa Kiislamu nchini mwao kisha wakavikatilia mbali vichwa vyao), na kama wakibakia kuwa madhubuti kuhusiana na yale mapatano, basi wayapinge mashtaka yale waziwazi.

Wote wawili walikwenda kwenye lango la ngome ya Bani Quraydha pamoja na watu wengine wawili. Kwenye mkutano wao wa awali na Ka’ab hakuna walichokisikia kutoka kwake ila lugha ya matusi na chafu. Mmoja wao akasema kwa msukumo wa kimuujiza; “Ninaapa kwa Jina la Allah! Jeshi la Waarabu litaondoka nchini humu na Mtume ataizingira ngome hii na atavikata vichwa vyenu na ataufanya wakati kuwa mgumu kwa kabila lenu.”

Kisha walirejea upesi upesi na wakamwambia Mtume (s.a.w.w.): “Azal na Qaarah!” Mtume (s.a.w.w.) akasema kwa sauti kuu ‘Allah Akbar’ (Allah Yu Mkubwa)! Enyi Waisilamu! Kuna biashara njema kwa ajili yenu kwamba ushindi uko karibu.” Sentensi iliyoudhihirisha ushujaa kamili na busara za huyu kiongozi mkuu wa Uislamu, ilitamkwa ili kuthibitisha kwamba moyo wa Waislamu usidhoofike kwa kusikia habari za kuvunjwa kwa mapatano na watu wa Bani Quraydha.12

Mwanzo Wa Uasi Wa Bani Quraydhah

Mpango wa awali wa Bani Quraydha ulikuwa kwamba hatua ya kwanza iwe ni kuuteka nyara mji wa Madina na kuwaogofya wanawake na watoto wa Waislamu waliojificha kwenye nyumba zao. Hivyo basi waliutekeleza mpango huu mle mjini Madina pole pole.

Kwa mfano watu mashujaa wa Bani Quraydha walianza kwenda huko na huko mjini mle kwa njia ya kisirisiri. Walifanya hivi sana kiasi kwamba Safiyah bint wa Abdul Muttalib akasema:
“Nilikuwa nikikaa nyumbani mwa Hasan bin Thabit na mwanawe Hasan na mkewe nao walikuwa wakiishi nyumbani humo. Mara kwa ghafla nilimwona Myahudi akitangatanga kuizunguka ngome yetu katika hali isiyoeleweka. Nilimwambia Hasan: “Dhamira ya mtu huyu si nzuri.

Amka umfukuze.” Hasan akasema: ‘Ewe bint wa Abdul Muttalib sina moyo wa kutosha kuweza kumwua nami nachelea kwamba kama nikitoka nje ya ngome hii nitapatwa na madhara.’ Hivyo mimi mwenyewe niliamka nikafunga kibwebwe, nikaokota kipande cha chuma na kumwua Myahudi yule kwa pigo moja tu.’”

Yule mtu aliyeteuliwa na Waislamu kukusanya taarifa alimwarifu Mtume (s.a.w.w.) kwamba Bani Quraydha wamewaomba Waquraishi na Ghatfaan kuwapatia askari elfu mbili watakaoingia Madina ndani ya ngome na kuuteka nyara mji ule. Taarifa hii ilifika wakati Waislamu walipokuwa wakiulinda ule ukingo wa lile handaki ili adui asiweze kulivuka. Mara moja Mtume (s.a.w.w.) aliwateuwa maafisa wawili ambao ni Zayd bin Harithah na Maslamah bin Aslam pamoja na askari mia tano kuulinda mji na wakiwa wanaitamka takbir’ “Allahu Akbar” (Allah ni Mkubwa) wawazuie Bani Quraydha wasitende uasi ili wanawake na watoto wakae kwa raha kwa kuisikia ile Takbir.13

Mapambano Baina Ya Imani Na Ukafiri

Wakati ule tukio la vita vya Ahzaab lilipotokea waabudu masanamu na Wayahudi walikuwa wameshapigana vita mbalimbali dhidi ya Uislamu. Hata hivyo vita vyote hivyo vilikuwa ni vita maalumu vilivyokuwa vya jamii au kundi moja tu, navyo havikuwa na sifa ya ujumla ya kuihusisha Rasi nzima ya Uarabuni kwenye vita dhidi ya Uislamu. Hata hivyo, kwa kuwa hawakufaulu kuiangusha ile dola mpya ya Uislamu, ingawa walizitumia nguvu zao zote, lakini kwenye tukio hili jeshi la mchanganyiko lenye watu wa makabila mbalimbali lilikusanyika ili kuumaliza Uislamu. Tukizungumzia kimethali, waliwatupia Waislamu mshale wao wa mwisho kwenye podo lao. Hivyo basi, baada ya kutumia fedha nyingi, na vile vile kuwaomba watu wengine wasaidie, walikusanya jeshi kubwa ili kwamba kama Waislamu wasipochukua hatua za tahadhari katika kuuhami mji wa Madina, waweze kupata ushindi wa rahisi dhidi yao, na kwa njia hiyo waweze kulifikia lengo lao. Kwa lengo hili, vile vile walikuja na mpiganaji mkuu wa Bara Arabuni (Amr bin Abdiwad) ili kuweza kuyatatua matatizo yote kupitia nguvu za mkono wake.

Katika maelezo haya, katika siku za vita vya Ahzaab na hasa wakati wa mapambano baina ya wale wapiganaji wawili wa ushirikina na Uislamu, hapo ukafiri na Uislamu vilikabiliana. Pambano hili lilikuwa ni baina ya Ukafiri na Imani (Uislamu).

Moja ya sababu za kushindwa kwa jeshi la Waarabu ni lile handaki lililochimbwa kwenye njia yao. Jeshi la adui lilijaribu usiku na mchana kulivuka handaki lile, lakini kila mara lilikabiliwa na mashambulizi makali ya wale walinzi, kama alivyopanga Mtume (s.a.w.w.).

Majira makali ya baridi ya mwaka ule na upungufu wa chakula na malisho viliutishia uhai wa jeshi la Waarabu na wanyama wao. Hay bin Akhtab (aliyeanzisha vita ile) alipata tende kiasi cha shehena ishirini za ngamia kutoka kwa Wayahudi wa Bani Quraydha lakini tende hizo zilinyakuliwa na Waislamu na kugawanywa miongoni mwa askari wa Uislamu.14

Siku moja Abu Sufyani alimuandikia Mtume (s.a.w.w.) barua ifuatayo: “Nimekuja na jeshi kubwa ili kuipindua dini yako. Lakini nifanye nini? Kwa kuwa inaonekana kwamba umekufikiria kupambana nasi kuwa ni jambo lenye kuchukiza na hivyo ukachimba handaki baina yetu na wewe.

Mimi sijui umejifunza mbinu hii ya kijeshi kutoka kwa nani, bali lazima nikueleze kwamba mpaka pale nitakapopigana vita vya kumwaga damu kama ile ye Uhud sitarejea (nyumbani).”

Mtume (s.a.w.w.) alimrudishia jibu hili: “Kutoka kwa Muhammad Mtume wa Allah kwenda kwa Abu Sufyani bin Harb ... Umejifaharisha tangu zamani na kudhania ya kwamba unaweza kuizima nuru ya Uislamu. Hata hivyo, hunabudi kutambua ya kwamba wewe ni dhaifu mno kuweza kufanya hivyo. Utarejea hivi karibuni baada ya kushindwa na hapo baadaye nitakuja kuyavunja masanamu makubwa ya Waquraishi mbele ya macho yako.”

Jibu kwa barua hii ambayo ilikuwa ishara ya uamuzi imara wa mwandishi, ilituama moyoni mwa kamanda wa jeshi la adui kama mshale. Kwa vile watu wale waliuamini ukweli wa Mtume Muhammad (s.a.w.w.) nyoyo zao zilidhoofika. Hata hivyo, ingawa hali ilikuwa hivyo, hawakukata tamaa juu ya kuziendeleza juhudi zao. Usiku mmoja Khalid bin Walid alijaribu kulivuka lile handaki akiwa na kikosi maalumu. Hata hivyo, ilimbidi kurudi nyuma kutokana na uangalifu wa askari mia mbili wa Uislamu waliokuwa wakihudumia chini ya uongozi wa Usayd Khidhr.

Mtume (s.a.w.w.) hakudharau kuziimarisha nyoyo za askari wa Uislamu japo kwa muda mfupi tu, na aliwapa moyo kwa hotuba zake zenye kuwachochea na zivutiazo ili kuulinda uhuru wa dini yao. Siku moja aliugeuza uso wake kwa wale askari na maafisa kwenye mkutano mkubwa sana na baada ya kuomba dua fupi aliwahutubia akisema: “Enyi askari wa Uislamu! Simameni imara mbele ya jeshi na kumbukeni kwamba Pepo iko chini ya kivuli cha panga zile zilizofutwa katika njia ya ukweli na haki.”15

Baadhi Ya Wapiganaji Wa Jeshi La Waarabu Wavuka Lile Handaki

Wapiganaji watano: ‘Amr bin Abdiwad, Ikrimah bin Abi Jahl, Hubayrah bin Wahab, Nawfal bin Abdullah na Ziraar bin Khatab walivalia mavazi yao ya kijeshi na wakiwa wamesimama mbele ya jeshi la Bani Kananah, walisema kwa fahari isiyo kifani; “Jitayarisheni na kupigana. Leo mtatambua ni nani walio wapiganaji wa kweli wa jeshi la Waarabu.” Kisha wakawapanda farasi wao na kuliruka lile handaki mahali fulani palipokuwa na upana mdogo kidogo. Wapiganaji hawa watano walikwenda mbali kuliko wenzao na hawakuweza kufikiwa na mishale ya askari waliokuwa wakililinda lile handaki. Hata hivyo, ile sehemu waliyovukia mara moja ilizungukwa na kuzuiwa ili askari wengine wa jeshi la Waarabu wasiweze kuvuka.

Mahali waliposimama hawa wapiganaji watano waliokuja kwa ajili ya mapigano ya mtu kwa mtu palikuwa baina ya lile handaki na mlima Sal’a (Makao makuu ya jeshi la Uislamu). Wale wapiganaji wa Kiarabu walikuwa wakicheza na farasi wao kwa fahari isiyo na kifani na majivuno, nao walikuwa wakiwaita wapinzani wao kwa njia ya vidokezo na ishara.16

Miongoni wa watu hawa watano, yule aliyekuwa maarufu zaidi kwa ushujaa na ustadi wake alijitokeza mbele, na kwanza alimwita mpinzani wake ajitokeze wapigane. Kila alipoitoa sauti yake na haja yake ya kumpata mpinzani ilipogonga kwenye uwanja ule, na kuzitetemesha nyoyo, hakupata jibu. Kimya cha Waislamu kilimchosha naye akasema: “Wako wapi wale wanaodai Pepo? Kwani ninyi Waislamu hamsemi kwamba wale wanaouwawa kutoka miongoni mwenu watakwenda Peponi na wale wanaouawa kutoka miongoni mwetu watakwenda Motoni? Hakuna hata mmoja wenu aliyeko tayari kunipeleka motoni au yeye kwenda Peponi mikononi mwangu?” Vile vile alitunga beti fulani fulani za shairi juu ya jambo hili, ambazo maana ya ule wa kwanza ni hii; “Nimechoka kupiga makelele na kumtaka mpinzani wangu ajitokeze (ili tupigane mapambano ya mtu kwa mtu) na sauti yangu imenikauka.”

Ilikuwa kimya kabisa kwenye lile jeshi la Waislamu katika kuzijibu kelele za ‘Amr ingawa kila mara Mtume (s.a.w.w.) alikuwa akitaka kwamba mtu mmoja aamke na kuwaondolea Waislamu uasi wa mtu yule, lakini hakuna aliyekuwa tayari kupigana naye ila Sayyidna Ali bin Abi Talib (a.s.).17

Hivyo basi, halikuwapo lolote jingine la kufanya ila kwamba tatizo hili litatuliwe kupitia kwa shujaa Sayyidna Ali (a.s.). Mtume (s.a.w.w.) alimpa upanga wake, akamfunga kilemba maalum kichwani mwake na akamwombea du’a kwa maneno haya: “Ee Allah! Mlinde Ali kutoka pande zote. Ewe Mola wangu! Ubaydah bin Harith alichukuliwa kutoka kwangu katika siku ya Badr na Simba wa Allah Hamza alichukuliwa kwenye vita vya Uhud. Ee Mola Wangu! Mlinde Ali kutokana na kupatwa na madhara kutoka kwa adui.” Kisha akaisoma Aya ya Qur’ani Tukufu ifuatayo: . . . Ee Mola wangu! Usiniache peke yangu Nawe ndiye mbora wa wanaorithi.”18 (Sura al-Anbiya, 21: 89).

Sayyidna Ali (a.s.) alikwenda upesi iwezekanavyo ili kufidia ule muda wa kuchelewesha kulikokwisha kufanywa. Wakati huo Mtume (s.a.w.w.) aliitamka sentensi ya kihistoria ifuatayo: “Imani kamili inaukabili ukafiri kamili.” Sayyidna Ali (a.s.) alitunga rajaz (beti za tenzi) ambazo mfuatano mzuri wa mwenendo wake na vina vyake viliafikiana na vile vya mpinzani wake, na akasema: “Usifanye haraka, kwa sababu mtu mwenye nguvu amekwishafika uwanjani ili akupe jibu.”

Mwili mzima wa Sayyidna Ali (a.s.) ulifunikwa na deraya na macho yake yalikuwa yakiangaza kupitia kwenye kofia ya chuma. Amr alitaka kumtambua yule mpinzani wake. Alimwuliza Sayyidna Ali (a.s.): “Ni nani wewe?” Sayyidna Ali (a.s.) aliyekuwa maarufu, kwa sauti ya waziwazi alimjibu hivi; “mimi ni Ali, mwana wa Abu Twalib.” Amr akasema: “Mimi sitaimwaga damu yako, kwa sababu baba yako alikuwa mmoja wa marafiki zangu wa tangu zamani. Mimi namshangaa binamu yako aliyekuleta kwenye uwanja wa vita akiwa na uhakika mwingi mno kuwa ninaweza kukuokota kwa ncha ya mkuki wangu na kukuning’iniza baina ya ardhi na mbingu ili kwamba uwe mwenye hali ya kutokufa wala kutokuwa hai.”

Ibn Abil Hadid anasema: “Kila mwalimu wangu wa historia (Abul Khayr) alipokuwa akiielezea sehemu hii alikuwa akisema: Kwa kweli Amr alikuwa akiogopa kupigana na Ali, kwa sababu alikuako kwenye Vita ya Badr na ya Uhud naye aliuona ushujaa wake. Hivyo basi, yeye alitaka kumvunja moyo Ali asipigane naye.”

Sayyidna Ali (a.s.) akasema: “Usijali kuhusu kifo changu. Katika hali zote mbili (yaani kama nikiuwa au nikiuwawa) nitabarikiwa na makazi yangu yatakuwa Peponi, lakini wewe katika hali zote hizo, moto unakusubiri.” Amr alitabasamu na akasema: “Ewe Ali! Mgawo huu si wa haki. Vyote viwili, pepo na moto ni vyako.”

Sayyidna Ali (a.s.) alimkumbusha kwamba siku moja yeye (Amr) aliubandika mkono wake juu ya kitambaa kinachoifunika Ka’aba Tukufu (kiswa) na kumwahidi Allah kwamba wakati shujaa yeyote atakapompa ushauri wa aina tatu kwenye uwanja wa vita ataukubali ushauri mmojawapo. Hivyo Sayyidna Ali (a.s.) alimshauri kwamba asilimu. Akajibu: “Ewe Ali! Liache hilo kwa kuwa haliwezekani.” Kisha Sayyidna Ali (a.s.) akasema: “Acha kupigana na umwache Muhammad peke yake.” Akajibu: “Ni aibu kwangu mimi kulikubali hilo, kwa sababu kesho washairi wa Uarabuni watanidhihaki na kudhania kwamba nilifanya hivyo kwa ajili ya hofu.” Hapo Sayyidna Ali akasema “Mpinzani wako hana mnyama wa kupanda. Hivyo wewe nawe huna budi kushuka kutoka juu ya farasi wako ili tuweze kupambana.” Akasema: “Ewe Ali! Huu ni ushauri usio na maana, nami sikufikiria kwamba Mwarabu ataniomba ombi kama hilo.”19

Mapambano Baina Ya Mabingwa Wawili Hao Yaanza

Mapambano makali yalianza baina ya wale mabingwa wawili na wote wawili walifunikwa mno na vumbi kiasi kwamba watazamaji hawakutambua ni nini kilichokuwa kikiendelea. Waliweza kuisikia migongano ya panga tu. Amr aliulenga upanga wake kichwani mwa Sayyidna Ali (a.s.) na ingawa Sayyidna Ali (a.s.) aliweza kuikinga dharuba ile kwa ngao yake maalum, hata hivyo kichwa chake kilijeruhiwa. Na hata hivyo alipata nafasi na kumpiga ‘Amri dharuba kali miguuni. Matokeo yake ni kwamba mguu mmoja au miwili yote ya ‘Amr ilikatwa naye akaanguka chini. Sauti ya Takbir ilisikika mle mwenye vumbi, jambo lililoashiria ushindi wa Sayyidna Ali (a.s.). Mandhari ya kuanguka kwa ‘Amri pale chini yalijenga hofu kuu zaidi nyoyoni kwa wale mashujaa wengine waliokuwa wamesimama nyuma yake, kiasi kwamba walianza kuwaendesha farasi wao bila ya kupenda wakielekea lile handaki, na wote isipokuwa Nawfal, walirejea kambini mwao. Ngamia wa Nawfal alitumbukia mle handakini. Wale waliowekwa kwenye ule ukingo wa handaki wakaanza kumpiga mawe, hata hivyo alisema kwa sauti kuu; “Kumwua mtu namna hii ni kinyume na kanuni za ushujaa. Hebu mmoja wenu na ashuke ili tupigane.”Sayyidna Ali (a.s.) akatumbukia kwenye lile handaki na kumuua.

Woga ukalishika jeshi zima la washirikina, na Abu Sufyani aliogopa zaidi kuliko yeyote yule mwingine. Alifikiria kwamba Waislamu watavikata kata viungo vya maiti ya Nawfal ili kulipa kisasi cha Hamza. Hivyo alimtuma mtu mmoja kwenda kuinunua maiti ya Nawfal kwa dinar elfu kumi. Hata hivyo, Mtume (s.a.w.w.) alisema: “Wapeni maiti yao na kwenye dini ya Uislamu hairuhusiwi kuchukua bei ya maiti.”

Thamani Ya Pigo Hili

Ingawa kwa madaha Sayyidna Ali (a.s.) alimuuwa adui wa Uislamu aliyetisha, lakini kwa kweli aliwahuisha wale watu waliokuwa wakitetemeka kuzisikia ngurumo za ‘Amr zenye kuzipasua pasua nyoyo, na vile vile aliliogofya lile jeshi lenye nguvu la askari elfu kumi lililodhamiria kuimalizia mbali ile Dola changa ya Uislamu. Thamani ya kujitoa mhanga huku kungelitambulika kama ushindi (angekosekana Ali) ungeangukia kwenye fungu la ‘Amr.

Wakati Sayyidna Ali (a.s.) alipopata heshima ya kujitokeza mbele ya Mtume (s.a.w.w.), Mtume (s.a.w.w.) aliitathmini ile faida ya lile pigo alilompiga nalo ‘Amr, kwa maneno haya: “Thamani ya kujitoia mhanga huku ni bora kuliko matendo mema yote ya wafuasi wangu, kwa sababu matokeo ya kushindwa kwa yule mpiganaji mkuu wa ukafiri, Waislamu wamekuwa wenye kuheshimika na jamii ya makafiri imeshuka cheo na kufedheheka na kunyongea.”20

Roho Nzuri Sana

Deraya ya ‘Amr ilikuwa na bei kubwa sana, lakini Sayyidna Ali (a.s.) alikuwa na roho nzuri mno kiasi cha kutoweza kuigusa, ingawa Khalifa wa pili alimlaumu kwa kutoivua mwilini mwa ‘Amr. Dada yake ‘Amr alipolitambua tukio lile alisema:21 “Katu mimi sihuzuniki kuuawa kwa kaka yangu, kwa sababu aliuawa mikononi mwa mtu mwenye roho nzuri sana. Kama isingalikuwa hivyo, ningalitiririkwa na machozi maishani mwangu.”22

Jeshi La Waarabu La Gawanyika

Lengo la majeshi ya Waarabu na Wayahudi katika kupigana dhidi ya Uislamu halikuwa moja. Wayahudi walikuwa wakichelea kuongezeka daima kwa kuenea kwa Uislamu, ambapo Waquraishi walisukumwa na uadui wao wa tangu kale dhidi ya Uislamu na Waislamu.

Ghatfaan na Fazarah na makabila mengineyo, walishiriki kwenye vita hivi kwa sababu ya mapatano ya Khaybar ambayo Wayahudi waliwaahidi.

Hivyo basi, lengo la hili kundi la mwisho lilikuwa la kimaada na kama lengo lao lingaliweza kufikiwa kupitia kwa Waislamu, wao wangeweza kurejea makwao kwa furaha kuu, hasa kwa vile ukali wa majira ya baridi, upungufu wa chakula na mazingira marefu ya mji wa Madina yamewasikitisha na wanyama wao walikuwa ukingoni mwa kifo.

Hivyo basi, Mtume (s.a.w.w.) alikiteua kikundi cha watu kufanya mapatano na machifu wa makabila tuliyoyataja hapo juu chini ya masharti ya kwamba Waislamu walikuwa tayari kuwapa theluthi moja ya matunda ya Madina, ili mradi tu wajitenge na majeshi ya Ahzaab (makabila) na warejee kwenye maeneo yao. Wale wawakilishi wa Mtume (s.a.w.w.) waliandika mapatano na wale machifu wa yale makabila na wakamletea ayatie saini. Hata hivyo, Mtume (s.a.w.w.) aliliweka jambo hili mbele ya maafisa wawili shujaa, ambao ni Sa’ad bin Mu’aaz na Sa’ad bin Ubadah.

Wote kwa pamoja walisema kwamba kama mapatano haya yanafanyika kwa mujibu wa amri ya Allah yatakubaliwa na Waislamu, lakini kama yanafanyika kutokana na maoni ya Mtume mwenyewe, na hivyo wanaombwa kutoa maoni yao, wao wanafikiria kwamba mpango huo ukomee hapo hapo na usisainiwe. Kuhusu sababu yao ya kutoukubali mpango ule, walisema kwamba; “Katu sisi hatukuwahi kulipa ushuru kwa makabila haya na hakuna lolote miongoni mwao lithubutilo kuchukua japo tunda moja ya tende kutoka kwetu kwa nguvu na lazima.

Na kwamba sasa tumesilimu kwa rehema za Allah na chini ya mwongozo wako na tumekuwa watukufu na wenye kuheshimiwa kwa njia ya Uislamu, suala la sisi kuwalipa wao ushuru wowote ule halipo tena. Tunaapa kwa jina la Allah! Tutayajibu madai yao yasiyo na msingi kwa panga zetu hadi jambo hili liamuliwe kwa Amri ya Allah.”

Mtume (s.a.w.w.) alisema: “Sababu ya mimi kufikiria juu ya mapatano ya aina hii ni kwamba nimeona kwamba mmekuwa shabaha (dango) ya jeshi la Waarabu nanyi mlikuwa mkishambuliwa kutoka pande zote. Hivyo basi mimi nilifikiria kwamba tatizo hili litatuliwe kwa njia ya kujenga mgawanyiko miongoni mwa maadui. Hata hivyo, sasa kwa vile msimamo wenu thabiti umedhihirika mimi ninauzuia hitimisho la mapatano haya na ninakuambieni – nayaaminini yale niyasemayo kwamba Allah hatamfedhehesha Mtume Wake na ataitimiza ahadi Yake kuhusu ushindi wa imani na Upweke wa Allah juu ya ushirikina. Hapo Sa’ad bin Mu’aaz akayafuta maneno ya mapatano yale kwa amri ya Mtume (s.a.w.w.) na akasema: “Waabudu masanamu wanaweza kufanya vyovyote vile wapendavyo. Sisi si watu wa kulipa ushuru.”23

Sababu Zilizoligawa Jeshi La Waarabu

Katika Vita vya Ahzaab, ingawa Waarabu walileta jeshi kubwa kiasi hiki, walishindwa kulifikia lengo kutokana na kugawanyika kwa jeshi. Zifuatazo hapa chini ndizo sababu zilizozaa kugawanyika kwa lile jeshi la Waarabu:

1. Sababu ya kwanza ya ushindi wa Waislamu kwenye vita hivi ilikuwa ni mazungumzo baina ya wawakilishi wa Mtume (s.a.w.w.) na wale machifu wa makabila ya Ghatfaan na Fazarah. Kwa sababu, ingawa mapatano haya hayakuthibitishwa pale mwishoni, kule kuyaasi na kuyakataa vilevile hakukutangazwa. Kwa njia hiyo, makabila yale yakashindwa kujua lipi ni lipi kuhusiana na wale marafiki zao, hivyo waliendelea kusubiri kupata taarifa za mapatano na kila walipotakiwa kufanya mashambulizi ya ujumla (ya watu wote) waliyakataa matakwa hayo kwa sababu moja au nyingine kwa tegemeo la kufikiwa kwa kamilisho la mapatano yale.

2. Watu wengi walikuwa wameweka matumaini yao juu ya kufaulu na ushindi kwa ‘Amr, yule mpiganaji mwenye nguvu nyingi wa Uarabuni. Matokeo yake ni kwamba, alipouawa, hofu kali sana iliwaingia.
Ilikuwa hivyo hasa, kwa sababu baada ya ‘Amr kuuawa wapiganaji wengine walikimbia kutoka kwenye ule uwanja wa vita.

3. Na’im bin Mas’ud aliyesilimu muda mfupi tu kabla ya vita hivi alifanya kazi kubwa sana katika kujenga mtengano baina ya makabila. Aliunda mpango bora zaidi kijasusi usio na upungufu wowote wa akili kuliko yale matendo ya majasusi wa siku hizi. Kidogo ulikuwa bora zaidi na wenye uwezo wa kutoa matokeo mazuri zaidi.

Na’im alikuja mbele ya Mtume (s.a.w.w.) na kusema: “Nimesilimu hivi karibuni nami nina uhusiano wa kirafiki na makabila yote haya, lakini wao hawajatambua kusilimu kwangu. Kama ziko amri zozote zile upendazo kunipa, nitazitekeleza.” Mtume (s.a.w.w.) akamwambia: “Fanya jambo liwezalo kuwagawa watu hawa” Yaani hakuna ubaya wowote kama ukifanywa mpango na ikapatikana dawa ya kuyasalimisha malengo yaliyo bora zaidi.

Na’im alilifikiria jambo lile kwa muda hivi. Kisha kwanza kabisa aliliendea kabila la Bani Quraydha ambao kwa kweli wao walikuwa kwenye safu ya tano ya adui, wao walikuwa wakiwatishia Waislamu kutoka kwenye mlango wa nyuma. Aliwasili kwenye ngome ya Bani Quraydha na kuilezea huba yake na urafiki wake kwao na akayatamka kila aina ya mambo yaliyoweza kumfanya wamwamini.

Kisha akaongeza kusema: “Hali yenu ni tofauti na ile ya marafiki zenu (yaani Waquraishi na Ghatfaan), kwa kuwa Madina ni maskani ya wanawake wenu na watoto wenu na mali zenu zote ziko hapa na hamwezi hata kidogo kuhamia mahali popote pale pengine, ambapo vituo vya maisha na biashara vya haya makabila yaliyojirafikisha, yaliyokuja kupigana dhidi ya Muhammad viko nje ye Madina na mbali na mji huu. Kama wakishinda vita hivi, watakuwa wamelifikia lengo lao, lakini kama wakishindwa mara moja watatoka na kuyaendea makazi yaliyopo mbali kiasi cha kutoweza kufikiwa na Muhammad. Hata hivyo, hamna budi kutambua kwamba kama makabila haya hayatashinda na wakarejea makwao wakiiacha vita, mtaachwa kwenye hali ya kutiishwa na Waislamu.

Sasa mnafikiria kwamba, kwa vile mmejishirikisha na makabila haya, ni bora kwamba muushikilie uamuzi huu. Hata hivyo, ili kuhakikisha kwamba makabila haya hayakuacheni peke yenu wakati wa vita na kurudi makwao, hamna budi kuwashika baadhi ya watu wao watukufu machifu wakawa ni dhamana ili kwamba hali itakapokuwa ngumu wasikuacheni na walimalize jambo hilo, kwa sababu, kwa njia hiyo watalazimika kupigana na Muhammad hadi mwisho ili watu wao waachiliwe.”

Maoni ya Na’im yalikubaliwa na watu wote, naye alitosheka kwamba maneno yake yalitoa athari zilizohitajika juu yao. Kisha aliiacha ngome yao na kwenda kwenye kambi ya yale makabila. Machifu wa Waquraishi walikuwa marafiki zao wa tangu kale. Hivyo basi, wakati wa mazungumzo yake na machifu wale, alisema:

“Bani Quraydha wameaibika sana nao ni wenye kujuta kwa kuyavunja kwao mapatano baina yao na Muhammad na sasa wanataka kulisahihisha jambo hilo. Hivyo basi, wameamua kuwachukua baadhi ya watu wenu ili wawe dhamana na wampe Muhammad watu hao. Kwa njia hii, watauthibitisha uaminifu wao, na Muhammad atawauwa watu wenu mara moja. Wameshalijadili jambo hilo na Muhammad nao wamemthibitishia kwamba tangu sasa hadi mwishoni mwa maisha yao watamuunga mkono na Muhammad naye ameukubali mpango wao.

Hivyo basi, kama Wayahudi wakitaka dhamana kutoka kwenu, msikubali hata kidogo. Hamna budi kutambua kwamba matokeo ya kitendo cha aina hiyo yatakuwa ya hatari. Uthibitisho wa dhahiri wa ukweli huu ni kwamba kama kesho mkiwataka washiriki kwenye vita na kumshambulia Muhammad kwa nyuma, mtawaona kwamba hawatakubali hata kidogo kufanya hivyo, na watatoa udhuru wa kila aina.”

Kisha akaiendea kambi ya Ghatfaan na kuzungumza nao kwa njia maalum. Alisema: “Ninyi watu wa kabila la Ghatfaan mu ndugu zangu. Sifikirii kwamba mtanilaumu kwa haya niyasemayo.

Nitazungumza nanyi juu ya jambo fulani bali nataka mnithibitishie kwamba hamtalizungumza kwa mtu yeyote. Wote walimthibitisha kuwa yu mtu mkweli na rafiki yao. Kisha aliwaeleza kwa kirefu yale aliyokwisha kuwaeleza Waquraishi na akawaonya juu ya matendo ya Bani Quraydha na akasema: “Msiwape jibu la kuyakubali matakwa yao kwa hali yoyote ile iwayo.”

Alitekeleza wajibu wake vizuri sana. Kisha akaja kwenye kambi ya Waislamu kwa siri na kuyaeleza mazungumzo yote haya mbele ya jeshi la Uislamu (yaani kwamba Wayahudi walitaka kuichukua dhamana kutoka kwenye majeshi ya Waarabu ili kuwapa Waislamu). Bila shaka lengo la kuyatangaza maongezi haya lilikuwa kwamba, jambo lile livuke lile handaki na kuyafikia masikio ya Waarabu.

Wawakilishi Wa Waquraishi Waitembelea Ngome Ya Bani Qurayzah

Abu Sufyani katika usiku wa kuamkia Jumamosi aliamua kumaliza jambo hili. Machifu wa Waqurashi na Ghatfaan waliwatuma wawakilishi wao kwenye ngome ya Bani Quraydha na kuwaambia: “Huu si ukanda wa makazi yetu na wanyama wetu wanakufa. Kesho hamna budi kuwashambulia Waislamu kwa mlango wa nyuma ili tuweze kulimaliza jambo hili.” Yule chifu wa Bani Quraydha akajibu akasema: “Kesho ni Jumamosi na sisi Wayahudi hatufanyi kazi yoyote katika siku hiyo kwa sababu baadhi ya jadi zetu walifanya kazi katika siku hii nao wakaangukiwa na ghadhabu ya Mungu. Zaidi ya hapo, tuko tayari kushiriki kwenye mapigano pale tu baadhi ya watu wenu watukufu watakapokuwamo kwenye ngome yetu wakiwa ni dhamana, ili kwamba muweze kupigana hadi mwisho ili kuthibitisha kuachiliwa kwao na msije kutuacha bila ya marafiki.”

Wale wawakilishi wa Waquraishi walirejea na kuwaeleza wale machifu wa makabila juu ya hali ile. Wote wakasema: “Na’im alikuwa sahihi katika kuzieleza huruma zake kwetu. Bani Quraydha wanataka kutuhadaa.” Wale wawakilishi wa Waquraishi waliwasiliana na machifu wa Bani Quraydha na kusema: “Haiwezekani kwetu sisi kuwatoa watu wetu watukufu na kukupeni ninyi ili wawe dhamana nasi hatuko tayari kukupeni japo mtu wetu mmoja tu ili awe dhamana. Kama mkielekea kuwashambulia Waislamu, fanyeni hivyo kesho nasi tutakusaidieni kwa uwezo wetu wote.”

Maneno ya wale wawakilishi wa Waquraishi na hasa kule kusema kwao kwamba hawakuwa tayari kumtoa japo mtu mmoja ili awe dhamana kuliwafanya Bani Quraydha waamini kwamba yale yote aliyoyasema Na’im yalikuwa sahihi. Yaliithibitisha hofu yao kwamba Waquraishi walikuwa wakitazama mbali na kama hawakufaulu kwenye jambo lile, watarejea nyumbani na kuwaacha watiishwe na Waislamu.”24

Sababu Ya Mwisho

Sababu nyingine ambayo kwa kweli inaweza kuitwa msaada wa Allah ilioongezwa kwenye sababu zile tulizozitaja hapo juu na kuyatawanyisha yale makabila. Sababu hii ilikuwa kwamba kwa ghafla hali ya hewa iliingiwa na dhoruba na hewa ikawa baridi mno. Badiliko la hali ya hewa lilikuwa kali mno kiasi kwamba mahema yaling’olewa, vyungu vilivyokuwa vikipikiwa chakula vilipinduliwa, taa zilizimika na moto uliokuwa ukiwaka ulitawanywa jangwani mle. Hali ilipofikia kiasi hicho, Mtume (s.a.w.w.) alimtuma Hudhayfah kulivuka lile handaki na kupata taarifa za adui.

Anasema: “Niliweza kufika karibu na Abu Sufyani na nikamwona akiwahutubia makamanda wa jeshi. Alikuwa akisema hivi: ‘Mahali hapa tulipopigia kambi si mahali pa maskani yetu. Wanyama wetu wanakufa na upepo na dhoruba havikuyabakisha mahema, vivuli na moto kwa ajili yetu. Bani Quraydha nao hawakutusaidia. Ni bora kama tukiondoka hapa.” Kisha alimpanda ngamia wake ambaye magoti yake yalikuwa yamefungwa na akaanza kumpiga kwa kurudia rudia. Maskini mtu huyu alikuwa na hofu mno ya kutatizwa kiasi kwamba hakutambua kwamba magoti ya yule ngamia yalikuwa yamefungwa.

Ilikuwa bado alfajiri haijaingia pale jeshi la Waarabu lilipoondoka kwenye sehemu ile na hakuna yeyote aliyeonekana pale tena”.25

 • 1. Maghaazil-Waaqidi, Juz. 2, uk. 441.
 • 2. Siiratu Ibn Hishamu, Juz. 2, uk. 214; Tarikhut-Tabari, Juz. 2, uk. 233.
 • 3. Hayaatu Muhammad.
 • 4. Maghaazil-Waaqidi, Juz. 2, uk. 443.
 • 5. Tarikhut-Tabari Juz. 2, uk. 224.
 • 6. Maghaazil-Waaqidi, Juz. 2, uk. 445.
 • 7. Siiratu Ibn Hishamu, Juz. 2, uk. 220. Maghaazil- Waaqidi, Juz. 2, uk. 453.
 • 8. Maghaazil- Waaqidi, Juz. 2, uk. 446; Siiratu Ibn Hishamu, Juz. 2, uk. 224.
 • 9. Siiratu Ibn Hishamu, Juzuu 1, uk. 238.
 • 10. Maghaazil-Waaqidi, Juz. 2, uk. 455-456.
 • 11. Bihaarul Anwaar, Juzuu 2, uk. 223.
 • 12. Maghaazil- Waaqidi, Juz. 2, uk. 458-459.
 • 13. Siiratul-Halabi, Juz. 2, uk. 335.
 • 14. Siiratul-Halabi, Juz. 2, uk. 345.
 • 15. Siiratu-Halabi, Juz. 2, uk. 349.
 • 16. Tarikhut-Tabari, Juz. 2, uk. 239; Tabaqaatul- Kubraa. Juz. 2, uk. 86.
 • 17. Waaqid anasema: “Kilikuwepo kimya kikali miongoni mwa Waislamu wakati Amr alipokuwa akimwita mpinzani wake wa mapambano ya mtu na mtu”. Maghaazil, Juz. 2, uk. 470.
 • 18. Sura al-Anbiya, 21: 89
 • 19. Bihaarul Anwaar, Juz. 20, uk. 227.
 • 20. Bihaar An’waar, Juz. 20, uk. 216; Mustadrik Hakim, Juz. 3, uk. 32.
 • 21. Na inasemekana kuwa dada huyu alimwomboleza kaka yake kwa beti hizi: “Laiti aliyemuuwa Amru angekuwa si huyu aliyemuuwa, basi ningelia milele maadamu bado nipo duniani. Lakini aliyemuuwa ni mtu asiyekuwa na mfano, na baba yake alikuwa akimwita: Wa pekee asiye na mfano.”
 • 22. Mustadrik Hakim, Juz. 30, uk. 33
 • 23. Siiratu Ibn Hishamu, Juzuu 1, uk. 223; Bihaar Anwaar, Juz. 20, uk. 252.
 • 24. Siiratu Ibn Hishamu, Juz. 2. uk. 229-231; Tarikhut-Tabari, Juz. 2, uk. 242- 243.
 • 25. Tarikhut-Tabari, Juz. 2, uk. 244.