Sura Ya 38: Hatua Ya Mwisho Ya Madhara

Katika mwaka wa kwanza wa kuwasili kwa Mtume (s.a.w.w.) mjini Madina aliandika mkataba muhimu na sheria za msingi kwa ajili ya mji wa Madina na vitongoji vyake ili kukomesha mifarakano na tofauti za ndani, na Wayahudi na makabila ya Aws na Khazraji wote kwa ujumla walikubali kulihami eneo hili. Tayari wasomaji wameshasoma vifungu vya sheria na maelezo kamili ya mkataba huu. Aidha, vile vile alifanya mapatano mengine na Wayahudi wa Madina. Mapatano haya yalitiwa saini na makundi yote ya Wayahudi kwa ujumla.

Ilikubaliwa kwamba kama wakimfanyia Mtume (s.a.w.w.) madhara yoyote, au masahaba zake au wakawapa silaha au wanyama wa kupanda maadui zao, Mtume (s.a.w.w.) atakuwa huru kisheria kuwauwa, kuzichukuwa mali zao na kuwateka wanawake na watoto wao.

Hata hivyo mapatano haya yalivunjwa na kutupiliwa mbali na makundi yote ya Wayahudi katika njia tofauti. Bani Qaynaqaa’ walimuuwa Mwislamu, Bani Nuzayr walipanga mpango wa kumuuwa Mtume (s.a.w.w.) na hivyo basi, akawalazimisha kuihama nchi yao na kwenda kuishi nje ya eneo la Waislamu. Ama kuhusu wale Bani Quraydha, wao walishirikiana kwa moyo mmoja na jeshi la Waarabu katika kuudhuru Uislamu. Sasa hebu na tutazame jinsi Mtume (s.a.w.w.) alivyowaadhibu Bani Quraydha.

Kabla ya kucha kwa siku ile, kikosi cha mwisho cha jeshi la makabila kiliitoka nchi ya Madina wakiwa wenye hofu mno. Ingawa dalili za uchovu na ulegevu zilijidhihirisha nyusoni mwa Waislamu, Mtume (s.a.w.w.) aliamrishwa na Allah kulimaliza jambo la Bani Quraydha. Mwadhini aliadhini na Mtume (s.a.w.w.) akasali sala ya adhuhuri pamoja na Waislamu.

Kisha kwa amri ya Mtume (s.a.w.w.) yule mwadhini alitangaza akisema: “Waislamu lazima wakaisali sala yao ya alasiri kwenye eneo la Bani Quraydha.” Kisha Mtume (s.a.w.w.) alimpa Sayyidna Ali (a.s.) bendera.

Askari mashujaa wakatoka wakiwa chini ya uamiri jeshi wake na wakaizingira ngome ya Bani Quraydha. Mlinzi wa ngome ile akatoa taarifa ya matendo ya jeshi la Waislamu kwa wakazi wa ngome ile. Milango ya ngome ile ikafungwa mara moja, lakini ikaanza vita baridi kwa kule kuwasili kwa jeshi la Waislamu.

Wayahudi wa Bani Quraydha walimtusi Mtume (s.a.w.w.) kupitia madirishani na minarani mwa ngome ile. Yule mshika bendera wa jeshi, Sayyidna Ali (a.s.) alikuwa Madina kumzuia Mtume (s.a.w.w.) asiikaribie ngome ile ili asiyasikie yale maneno machafu ya Wayahudi.

Hivyo Mtume (s.a.w.w.) alimwambia Sayyidna Ali (a.s.) kwamba, wao Wayahudi wakimwona wataacha kuyatumia maneno ya matusi. Hivyo, Mtume (s.a.w.w.) akaikaribia ngome ile na akazungumza nao kwa ukali kidogo na akasema: “Je Mwenyezi Mungu hakukufedhehesheni ninyi?”

Aina hii ya ukali na hasira za Mtume (s.a.w.w.) vilikuwa ni vitu visivyo kifani kwa Wayahudi. Hivyo basi ili kumtuliza Mtume (s.a.w.w.) walisema upesi upesi: “Ewe Abul Qaasim! Wewe hukuwa mwepesi wa kughadhibika kiasi hicho!” Maneno haya yalizituliza mno hasira za Mtume (s.a.w.w.) kiasi kwamba aligeuka nyuma bila ya kukusudia na joho lake likaanguka chini kutoka mabegani mwake.1

Mashauriano Ya Mayahudi Ndani Ya Ile Ngome

Hay bin Akhtab Nuzayri, aliyeViwasha vita Vya Ahzaab alishiriki kwenye majadiliano haya, kwa sababu kufuatana na ahadi aliyomuahidi Ka’ab, yule chifu wa Bani Quraydha, yeye hakwenda Khaybar baada ya kutawanyika kwa makabila na badala yake alikuwa kwenye ile ngome ya Bani Quraydha. Yule chifu wa jamii ile alitoa maazimio matatu na kuwataka watu kuchagua lolote lile miongoni mwao. Alisema:

1. Sisi sote tusilimu, kwa sababu utume wa Muhammad ni ukweli uliodumishwa na kuthibitishwa na watu wote, na Taurat nayo inauthibitisha.

2. Tuwauwe wanawake na watoto wetu na kisha tutoke humu kwenye ngome na kupigana na Waislamu kwa mkono ulio huru. Kama tukiuawa hatutakuwa na chochote cha kututia wasiwasi na kama tukishinda tunaweza kujipatia tena wanawake na watoto.

3. Usiku huu ni usiku wa kuchea Jumamosi, Muhammad na masahaba zake watafikiria kwamba Wayahudi hawafanyi jambo lolote kwenye usiku wa kuchea Jumamosi na katika siku ya Jumamosi. Hivyo tujinufaishe na utovu wao wa tahadhari na tuwashambulie wakati wa usiku.”

Ile kamati ya ushauri iliyakataa maazimio yote matatu na kusema: “Hatutaikana dini yetu na Taurati, na maisha yetu nayo hayatakuwa na raha baada ya wanawake na watoto wetu (kuuawa).

Ama kuhusu azimio la tatu haliwezi kutekelezeka kutokana na itikadi za dini yetu kwa sababu, iwapo tutafanya hivyo, tunaweza kupasika na ghadhabu ya Mungu kama vile ilivyotokea kwa nyumati zilizopita kutokana na kutoipa heshima ipasikayo siku ya Jumamosi.”2

Hotuba za wanakamati ni mwongozo wetu katika kuzielewa fikara zao. Kulikataa kwao azimio
la kwanza kwaonyesha kwamba walikuwa watu wakaidi na wenye uadui, kwa sababu kama
kweli waliuamini utume (kama ilivyoelezwa na chifu wao) kumpinga kwao hakukuwa na
maana yoyote ila ukaidi.

Ama kuhusu lile azimio la pili, mazungumzo yaliyofanyika miongoni mwao yaonyesha kwamba walikuwa watu wakatili na wenye nyoyo ngumu kwa sababu kuwauwa wanawake na watoto wasio na kosa, hakuwezekani bila ya kuwa na moyo mgumu mno.

Inapasa kuzingatia kwamba wajumbe wa kamati ya ushauri walilikataa azimio hili kutokana na ukweli uliopo kwamba, maisha yao hayatakuwa yenye furaha bila ya wanawake na watoto. Hakuna hata mtu mmoja aliyeuliza ni kosa gani walilolitenda watu hawa wasio na msaada ambalo kutokana nalo wanauawa, na vipi wao mababa wenye huruma na wakarimu, waweze kulitenda tendo hili wakati katu Mtume (s.a.w.w.) asingaliwauwa kama angalipata mamlaka juu yao?

Azimio la tatu laonyesha kwamba hawakuitathmini barabara nguvu ya kiroho ya Mtume (s.a.w.w.) na ujuzi wake wa mbinu za vita na kanuni za ulinzi, na wakafikiria ya kwamba Mtume wa Uislamu hatachukua tahadhari ya lazima kwenye usiku na siku ya Jumamosi – na kwamba vile vile hata kuhusu adui kama wale Wayahudi, watu walio maarufu kwa hadaa zao na hila.

Kuchunguza tukio la Ahzaab kunathibitisha kwamba walikuwa wako watu wachache tu waliokuwa werevu na wenye busara miongoni mwa jamii hii, au sivyo wangaliuhami uhai wao kwa njia ya kidiplomasia bila ya kujishirikisha na kundi lolote lile (yaani la Uislamu au la ukafiri). Kusema kweli wangalibakia kuwa watazamaji tu wa mapigano yale baina ya Mtume (s.a.w.w.) na jeshi la Waarabu, na upande wowote ule ushindao, uhai wao na nguvu zao vingelibakia.

Hata hivyo, kwa bahati mbaya walidanganywa na wepesi wa kuzungumza wa Hay bin Akhtab na wakajiunga na jeshi la Waarabu, na mkosi wao ukawa mkali mno pale ambapo baada ya kushirikiana na jeshi la Waarabu kwa kipindi cha mwezi mmoja, wakakataa kuwasaidia Waquraishi, na waliponaswa kwenye ule mpango wa Na’im bin Mas’ud waliwapelekea ujumbe Waquraishi ya kwamba hawatawasaidia kupigana dhidi ya Mtume (s.a.w.w.) mpaka Waquraishi wawape baadhi ya watu wao watukufu wawe dhamana.

Kufikia hapa, watu hawa wapumbavu walizipoteza kabisa fahamu zao njema. Hawakutambua kwamba, upande mmoja wameshamwasi Mtume (s.a.w.w.), na hivyo kama upande mwingine wakikataa uhusiano na Waquraishi na ikatokea jeshi la Waarabu likajihisi kuwa ni dhaifu na kurejea makwao na kuacha vita, basi wao (Bani Quraydha) watatiishwa na Waislamu.

Kama wangalipanga mpango sahihi wa kisiasa, mara moja wangalivunja uhusiano wao na jeshi la Waarabu na moja kwa moja wakadhihirisha majuto yao kwa kuyaasi yale mapatano baina yao na Waislamu, ili waweze kubakia salama kutokana na hatari ya uwezekano wa kushinda kwao (wao Waislamu). Hata hivyo, waliangukia kwenye windo la bahati mbaya kwa vile walikataa uhusiano wao na Waquraishi na vile vile hawakujiunga na Waislamu.

Baada ya kuondoka kwa jeshi la Waarabu, Mtume (s.a.w.w.) hakuweza kuwaacha Bani Quraydha kwa sababu wao (jeshi la Waarabu) katika wakati utakaowafaa wangelirejea tena wakiwa na zana zitoshelezazo na hatimaye kuuteka mji wa Madina na kuuhatarisha uhai wa Uislamu kwa ushirikiano na Bani Quraydha watakaokuwa ufunguo wa ushindi na kushindwa kwa Waislam, na kwa sababu hii walichukuliwa kuwa ni maadui wa ndani. Kwa sababu hii utatuzi wa suala hili la Bani Quraydha na kumalizika kwa jambo lao kulikuwa jambo lihusulo uhai wa Waislam.

Usaliti Wa Abu Lubabah

Baada ya kuzingirwa, Wayahudi wa Bani Quraydha walimwomba Mtume (s.a.w.w.) awapelekee Abu Lubabah wa kabila la Aws ili waweze kumtaka ushauri.

Abu Lubabah alikuwa tayari kaishafanya mapatano ya urafiki na Bani Quraydha. Alipowasili kwenye ngome ile wanaume na wanawake walimkusanyikia huku wakilia na kusema; “Je, ni sahihi kwamba tusalimu amri bila ya masharti yoyote?” Abu Lubabah akawajibu akasema: “Ndio.” Hata hivyo alifanya ishara kwa mkono wake kuelekea kwenye koo lake iliyokuwa na maana ya kwamba kama wakifanya hivyo, watakatwa vichwa vyao.

Abu Lubabah alitambua ya kwamba Mtume hatavumilia kuwapo hai kwa jamii ile iliyokuwa adui hatari zaidi kwa Uislam. Hata hivyo, alijuta mno kuyasaliti maslahi makubwa ya Uislamu na Waislamu na kuzifunua siri zao. Hivyo aliitoka ngome ile akiwa anatetemeka na mwenye wasiwasi na akaenda moja kwa moja hadi msikitini. Pale akajifunga kwenye moja ya nguzo za msikiti na akaweka nadhiri ya kwamba kama Allah asipomghufiria, atautumia muda wa maisha yake uliosalia katika hali ile. Wafasiri wa Qur’ani Tukufu wanasema kwamba Aya ifuatayo hapa chini ilifunuliwa kuhusiana na usaliti wa Abu Lubabah: “Enyi mlioamnini! Msimfanyie khiyana Mwenyezi Mungu na Mtume na msikhini amana zenu na hali mnajua.” (Sura al-Anfal, 8:27).

Taarifa juu ya Abu Lubabah zilimfikia Mtume (s.a.w.w.). Akasema: “Kama angalinijia kabla ya kuweka nadhiri, ningalimwombea msamaha na Allah angalimsamehe, lakini sasa hana budi kusubiri hadi ataposamehewa na Allah.”

Mkewe alikuwa akija wakati wa sala na kufungua zile kamba alizojifungia kwenye ile nguzo. Na baada ya kusali alimfunga tena kwenye nguzo ile. Baada ya siku sita Malaika Mkuu Jibril alikuja mapema wakati wa asubuhi na Aya ifuatayo, wakati Mtume (s.a.w.w.) alipokuwa nyumbani kwa Bibi Ummu Salamah:

وَآخَرُونَ اعْتَرَفُوا بِذُنُوبِهِمْ خَلَطُوا عَمَلًا صَالِحًا وَآخَرَ سَيِّئًا عَسَى اللَّهُ أَنْ يَتُوبَ عَلَيْهِمْ ۚ إِنَّ اللَّهَ غَفُورٌ رَحِيمٌ {102}

“Na wengine waliokiri dhambi zao na wakachanganya vitendo vizuri na vingine vibaya, huenda Allah akapokea toba zao, hakika Allah ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.” (Sura al-Taubah, 9:102).

Macho ya Bibi Ummu Salamah yaliuangukia uso wa Mtume (s.a.w.w.) wakati akiwa na tabasamu midomoni mwake. Mtume (s.a.w.w.) alimwambia Bibi huyu: “Allah Amesamehe dhambi ya Abu Lubabah. Amka na uwafikishie watu habari hii njema.” Mkewe Mtume (s.a.w.w.) alipowapasha habari watu juu ya habari hizi njema walikimbilia kwenda kumfungua, lakini Abu Lubabah akasema: “Ingalifaa kama yeye Mtume mwenyewe angalifungua kamba zangu.” Baadae Mtume (s.a.w.w.) alifika mle msikitini kusali sala ya Alfajiri na akamfungua kamba zile na kumwacha huru.3

Hadithi ya Abu Lubabah ni yenye mafundisho. Kosa lake lilitokana na hisia zake zisizo za busara. Kulia kwa wanaume na wanawake walio wahaini kulimnyima uwezo wake wa kujitawala na hivyo akazifunua siri za Waislamu. Hata hivyo, nguvu za imani yake na kumcha Allah zilikuwa kubwa zaidi kuliko vile na hivyo akatubia mno kwa yale aliyoyatenda kiasi kwamba lile wazo la kuzisaliti siri zile lisipite tena akilini mwake.

Hatima Ya Kundi La Tano

Siku moja Shaas bin Qays alishuka kutoka kwenye ngome akiwa yu mwakilishi wa Wayahudi na akaonana na Mtume (s.a.w.w.). Alimwomba Mtume (s.a.w.w.) aliruhusu kabila la Bani Quraydha lichukue vitu vyao kama walivyofanya Wayahudi wengine na watoke Madina. Hata hivyo, Mtume (s.a.w.w.) hakuikubali rai yake na akasema: “Wasalimu amri bila ya masharti yoyote.” Shaas akaisahihisha rai yake na akasema: “Bani Quraydha wako tayari kuwapa Waislamu mali zao na kutoka Madina.” Mtume (s.a.w.w.) alikataa kuikubali rai ile pia. 4

Sababu ya Mtume (s.a.w.w.) kutoikubali rai ile ilikuwa dhahiri kabisa, kwa sababu ulikuwako uwezekano wa kwamba, kama lilivyofanya kabila la Bani Nuzayr, watu hawa nao watakapokuwa mbali na Waislamu wangaliweza kuwakabili Waislamu katika njia ya hatari kwa kushirikiana na jeshi la Waarabu wenye kuyabudu masanamu na wangaliweza kuwa sababu ya mauaji zaidi. Hata hivyo, kwa sababu hii Mtume (s.a.w.w.) hakukubaliana na Shaas, aliyerejea kule ngomeni na kuilezea hali ya mambo kwa wakuu wa kabila lile.

Hatimaye Bani Quraydha waliamua kusalimu amri kwa Waislamu bila ya masharti yoyote, au kufuatana na ilivyoelezwa na baadhi ya wanahistoria, wakauukubali uamuzi wa Sa’ad bin Muaaz, waliyekuwa tayari wameshafanya mapatano naye kwa lengo hili, malango ya ngome ile yakafunguliwa. Hivyo Amir wa Waumini akaingia ngome ile akifuatana na kikosi maalum na kuwanyang’anya silaha Wayahudi wote. Kisha akawaweka kizuizini ndani ya nyumba moja ya Bani Najjar hadi baadae hatima yao ilipoamuliwa.

Kama walivyotendewa Wayahudi wa Bani Qaynaqaa’ waliotiwa kizuizini na jeshi la Waislamu hapo awali, walivyosamehewa kwa maombezi ya Bani Khazraj na hasa Abdullah Ubayy, na Mtume (s.a.w.w.) akajiepusha kuimwaga damu yao, watu wa Bani Aws nao walimshikilia Mtume (s.a.w.w.) kwa lengo la kushindana na Bani Khazraji, kwamba kwa vile Bani Quraydha walifanya mapatano nao, angaliweza kuwasamehe.

Hata hivyo, Mtume (s.a.w.w.) hakulikubali ombi lao na akasema: “Ninamwachia Sa’ad bin Mu’aaz mzee na chifu wenu wa Bani Aws atoe uamuzi. Lolote alisemalo nitalikubali.” Wale wote waliokuwapo pale waliukubali kwa moyo mmoja upendeleo ule wa Mtume (s.a.w.w.).
Zaidi ya hapo Bani Quraydha wenyewe vile vile walikubali kukubaliana na uamuzi wa Sa’ad Mu’aaz. Kutegemeana na ilivyonukuliwa na Ibn Hishamu na Shaykh Mufid, ni kuwa Wayahudi wa Bani Quraydha walimpelekea ujumbe Mtume (s.a.w.w.) kwamba Sa’ad bin Mu’aaz aliamue jambo lao. 5

Katika siku zile mkono wa Mu’aaz ulikuwa umejeruhiwa kwa kupigwa mshale, naye alikuwa kalazwa kitandani kwa ajili ya matibabu kwenye hema la mwanamke mmoja aliyeitwa Zamidah aliyekuwa stadi wa upasuaji. Mtume (s.a.w.w.) alikuwa akienda pale mara kwa mara kumtazama.

Vijana wa Bani Aws walikwenda na kumleta yule chifu wa kabila lao mbele ya Mtume (s.a.w.w.) kwa taratibu maalum. Sa’ad alipofika, Mtume (s.a.w) alisema: “Ninyi nyote hamna budi kutoa heshima zenu kwa chifu wenu.” Wale wote waliokuwapo pale walisimama ili kuonyesha heshima yao kwa Sa’ad. Wale waliofuatana na Sa’ad nao walirudia mle njiani kumwomba kwamba awatendee wema Bani Quraydha na awaokoe kutokana na kifo.

Hata hivyo, kinyume na tukio lote hili, alitoa uamuzi wake kwamba askari wao wote wauwawe, mali zao zigawanywe miongoni mwa Waislamu na wanawake na watoto wao wafanywe kuwa mateka.6

Uchunguzi Juu Ya Uamuzi Wa Busara Wa Sa’ad Bin Mu’aaz

Hakuna shaka juu ya ukweli kwamba kama mapenzi ya hakimu yatazishinda fikira na akili zake, kile chombo cha kisheria huvurugika na utaratibu mzima katika jamii hupatwa na mvurugiko.

Mapenzi ni kama njaa ya uwongo ambayo huonesha madhara na vitu vibaya kuwa vyenye manufaa na faida, wakati ambapo, kwa kutenda juu ya mapenzi hayo masilahi ya maelfu ya watu pamoja na ustawi wa jamii nzima utakuwa umevunjwa.

Mapenzi na hisia za Sa’d bin Mu’z, hali ya kuhuzunisha ya wanawake na watoto wa Bani Quraiyza, hali ya masaibu ya wanaume wao ambao walikuwa kizuizini na fikira ya jumla ya Bani Awsi ambao kwa umakini walisisitiza kwamba hakimu apuuze kosa lao, mambo yote haya yalihitaji kwamba hakimu aliyeteuliwa na pande zote angetoa hukumu yake juu ya masilashi ya wachache (Bani Quraydha) badala ya upendeleo kwa masilahi ya wengi (Waislamu kwa ujumla), na angewaachia huru wahalifu wa Bani Quraydha kwa kisingizio fulani, au angalau kuwapunguzia adhabu kwa kadiri iwezekanavyo au kutenda juu ya moja ya ushauri uliotajwa hapo juu.

Hata hivyo, mantiki, akili, uhuru na kujitegemea kwa hakimu, na kuyaheshimu maslahi ya watu wote, vyote hivi vilimuongoza kwenye njia ambayo hatimaye aliitumia na akautoa uamuzi wake kwa kuwakata vichwa askari, kuzinyakua mali zao na kuwateka wanawake na watoto wao. Aliufikia uamuzi wake huo kwa kuzizingatia hoja zifuatazo:

Kipindi fulani hapo awali Wayahudi wa bani Quraydha walifanya mapatano na Mtume (s.a.w.w.) chini ya masharti ya kwamba kama wakipigana dhidi ya maslahi ya Uislamu na Waislamu au wakiwasaidia maadui wa Uislamu na kufanya ghasia au kuwachochea watu kupigana dhidi ya Waislamu, wao (Waislamu) watakuwa na haki ya kuwauwa. Hakimu huyu alikuwa na maoni ya kwamba kama akiwaadhibu kwa mujibu wa masharti ya mapatano yale hatakuwa ametenda kinyume na misingi ya haki.

Watu hawa kwa kuyavunja yale mapatano waliuweka mji wa Madina kwenye hali ya hatari kwa muda fulani hivi ukiwa chini ya kivuli cha mikuki ya kijeshi ya Waarabu na wameingia kwenye nyumba za Waislamu na kuwatisha.

Na kama Mtume (s.a.w.w.) asingalichukua hatua ya tahadhari ya kabla na asingalipeleka kikosi kutoka kwenye makao makuu ya jeshi kwenda kwenye sehemu ya ndani zaidi ya mji ili kudumisha amani na utulivu, kulikuwa na uwezekano mkubwa kwamba Bani Quraydha wangalifaulu kuutekeleza mpango wao. Katika tukio lile wangaliwauwa Waislamu, kuzinyakua mali zao na kuwachukua mateka wanawake na watoto wao. Sa’ad bin Mu’aaz alifikiria kwamba kama akitoa hukumu hiyo dhidi yao, hatakuwa ametenda kinyume na ukweli na haki.

Sa’ad bin Mu’aaz aliyekuwa chifu wa kabila la Aws, alikuwa kafanya mapatano na Bani Quraydha nao walikuwa na uhusiano mwema wa kirafiki baina yao. Hivyo basi inawezekana kwamba alikuwa akiitambua sheria ya adhabu ya Wayahudi. Maelezo ya Taurati ya Wayahudi ni haya: “Utakaposongea karibu ya mji kwenda kupigana juu yake, ndipo utakapowapigia ukelele wa amani.

Itakuwa utakapokujibu kwa amani na kukufungulia, ndipo watu wote watakapoonekana humo watakufanyia kazi ya shokoa na kukutumikia. Na kwamba hautaki kufanya amani nawe, laki- ni utafanya vita juu yako, ndipo uuhusuru; na Bwana Mungu wako autiapo mkononi mwako, mpige kila mume aliyemo kwa makali ya upanga; lakini wanawake na watoto, na wanyama wa miji, na vilivyo mjini, vyote navyo ni nyara zake zote, uvitwae viwe mateka kwako; nawe utakula nyara za adui zako alizokupa Bwana Mungu wako. (Kumbukumbu la Torati, 20:10-14.

Inawezekana Sa’d alifikiria kwamba kama yeye aliyeteuliwa kuwa hakimu na pande zote mbili, angaliwaadhibu waasi kwa mujibu wa sheria ya dini yao wenyewe, angekuwa hakutenda jambo lolote jingine zaidi ya utekelezaji wa haki.

Tunafikiria kwamba sababu kuu iliyomfanya Sa’d bin Mu’aaz atoe uamuzi wake huu, ni kwamba ameona kwa macho yake kwamba Mtume (s.a.w.w.) amewasamehe watu wa Bani Qaynaqaa’ kwa maombezi ya Bani Khazraji na ametosheka na kuwapeleka uhamishoni tu nje ya mazingira ya Madina. Watu hawa walikuwa bado hawajaitoka ile nchi ya Kiislamu kabisa pale Ka’ab Ashraf alipokwenda Makka na kutoa yale machozi ya mamba kwa ajili ya wale waliouawa kwenye Vita vya Badr na hakupumzika hadi alipowatayarisha Waquraishi kwa ajili ya vita. Kwa matokeo ya jambo hili vita vya Uhud vilipiganwa. Kwenye vita vile askari sabini wa Uislamu walikufa kishahidi. Hali kadhalika Bani Nuzayr walisamehewa na Mtume (s.a.w.w.).

Hata hivyo, katika kuitikia ishara hii ya huruma waliunda urafiki wa kijeshi na Waarabu na wakaleta vita vya Ahzaab. Na laiti si ule ustadi wa Mtume (s.a.w.w.) na mpango wa kuchimba handaki, Uislamu ungaliangamizwa na maelfu ya Waislamu wangaliuawa.

Sa’ad bin Mu’aaz aliyaona matendo yote haya. Uzoefu wa siku zilizopita haukumruhusu azidiwe nguvu na mapenzi, kwa sababu kulikuwa hakuna shaka kuhusu ukweli kwamba wakati huu wangaliunda ushirikiano wenye nguvu zaidi na wangaliuhatarisha usalama wa kile kituo kikuu cha Uislamu kwa kuyachochea majeshi ya Waarabu kuamka dhidi ya Waislamu pamoja na kuunda mipango mingine. Hivyo basi, aliuchukulia uhai wa kundi hili kuwa ni wenye madhara kabisa kwa jamii ya Waislamu.

Kama sababu hizi zisingelikuwako ingalikuwa muhimu mno kwa Sa’ad bin Mu’aaz kuyaheshimu maoni ya watu wote juu ya jambo hili, kwa sababu chifu wa kabila huhitaji sana kuungwa mkono na watu wake, na kuwaudhi na kuyakataa mapendekezo na maombi yao ni jambo lenye madhara mno kwake. Hata hivyo, aliyafikiria maombi yote haya kuwa kinyume na maslahi ya Waisalamu, na matokeo yake ni kwamba, alizitii kanuni za matumizi ya akili na hoja.

Uthibitisho wa kuona kwake mbele kwa ndani zaidi na hukumu yake ikubalikayo kuwa ya kiakili, ni kwamba wakati wao (Wayahudi) walipokuwa wakichukuliwa kwenda kunyongwa, waliyasema yale yaliyokuwa nyoyoni mwao. Macho ya yule aliyeviwasha vita vile, Hay bin Akhtab yalimwangukia Mtume (s.a.w.w.) wakati ule na akasema: “Mimi sijutii kuwa kwangu adui kwako. Hata hivyo, yeye ambaye Allah anataka amfedheheshe, amefedheheka”.7
Kisha aliwageukia watu na kusema: “Msiwe na wasiwasi kutokana na Amri ya Allah. Hatimaye Allah amehukumu mateso na fedheha kwa ajili ya Bani Israeli.”

Kutoka miongoni mwa wanawake, mmoja wao aliuawa kwa sababu alimuuwa Mwislamu kwa kumvurumishia jiwe la kijaa mwilini mwake. Na miongoni mwa wale waliohukumiwa kifo, mtu mmoja ambaye ni Zubayr Bata alisamehewa kwa mapendekezo ya Mwislamu mmoja aliyeit- wa Thabit bin Qays, hata wanawake wake na watoto waliachiwa huru na mali yake ilirejeshwa kwake. Watu wanne kutoka miongoni mwa Bani Quraydha walisilimu. Nyara za vita ziligawanywa miongoni mwa Waislamu baada ya kutoa katika hiyo, sehemu moja ya tano (Khums) iliyoangukia kwenye fungu la Idara ya fedha ya Waislamu. Askari wapanda wanyama walipewa mafungu matatu kila mmoja na wale watembeao kwa miguu walipewa fungu moja kila mmoja. Mtume (s.a.w.w.) alimpa khumsi ya nyara zile Zayd kwa maelekezo ya kwamba aende Najd na kupata farasi, silaha na masrufu ya vita kutokana na bei ya fungu lile.

  • 1. Siiratu Ibn Hishamu, Juz. 2. uk. 234; Tarikhut-Tabari, Juz. 2, uk. 245-246.
  • 2. Siiratu Ibn Hishamu, Juz. 2. uk 235.
  • 3. Siiratu Ibn Hishamu, Juz. 2. uk. 237.
  • 4. Maghaazil- Waaqidi, Juz. 2, uk. 501.
  • 5. Irshad Mufid, uk. 50.
  • 6. Siiratu Ibn Hishamu, Juz. 2. Uk. 240, Maghaazil- Waaqidi, Juz. 2, uk. 510.
  • 7. Tarikhut-Tabari, Juz. 2, uk.250.