Sura Ya 39: Matukio Ya Mwaka Wa Tano Na Sita Hijiriya

Mwaka wa Tano wa hijiriya ulikuwa bado haujamalizika pale mashambu- lio ya makabila yaliporudishwa nyuma na uasi wa Bani Quraydha nao ukakomeshwa. Mji wa Madina na viunga vyake ukaja kabisa chini ya utawala wa Waislamu. Misingi ya ile Dola changa ya Uislamu iliimarika na utulivu wa kiasi fulani ulianza kuweko kwenye zile nchi za Kiislamu. Hata hivyo utulivu huu ulikuwa wa muda tu. Ilikuwa muhimu kwamba Mtume (s.a.w.w.) aendelee kuyaangalia mambo ya maadui na kukomesha mapatano yote ya kufanya mabaya dhidi ya Uislamu, tangu mwanzoni kabisa kwa msaada wa majeshi yawezayo kupatikana.

Utulivu uliokuwako kwenye mazingira ulitoa fursa ya kuwaadhibu baadhi ya wale watu waliowasha vita vya Ahzaab na kisha wakaenda nje ya mamlaka ya Waislamu baada ya yale makabila kuvunja kambi. Hay bin Akhtab aliyekuwa mmoja wa watu wale aliyefanya machocheo ya kwanza katika vita vya Bani Quraydha, alikuwa miongoni mwa Wayahudi walionyongwa kwenye ile adhabu ya Bani Quraydha, lakini rafiki yake Sall?m bin Abi Haqiq alikuwa akiishi Khaybar. Ulikuwa ni ukweli uliokubalika kwamba mtu huyu wa hatari hatatulia mpaka pale atakapoyachochea tena makabila kuamka dhidi ya Waislamu, hasa kwa sababu Waarabu waabudu masana- mu walikuwa wako tayari kupigana vita dhidi ya Uislamu na kama gharama za vita zingethibitishwa, hali ya vita vya Ahzaab ingeliweza kurudiwa tena.

Akiyazingatia mambo haya, Mtume (s.a.w.w.) aliwateua watu mashujaa wa kabila la Khazraji kuwaondoshea mbali Waislamu mtu huyu mfidhuli na mkorofi. Hata hivyo, kazi hii iliwekewa masharti ya kwamba wasiinyanyase familia yake. Wale mashujaa wa Khazraji walifika Khaybar wakati wa usiku na wakayafunga kwa nje malango ya nyumba zilizokuwa zikipakana na ya Sall?m, ili kwamba kama ikiwapo kelele yoyote ile majirani zake wasiweze kuzitoka nyumba zao. Kisha kwa kutumia ngazi waliifikia gorofa ya kwanza ya nyumba ile aliyokuwa akiishi Sall?m. Waligonga mlango, mkewe akatoka na kuwauliza walikuwa ni akina nani. Wakajibu: “Sisi ni Waarabu na tunayo shughuli fulani na chifu. Tunahitaji nafaka.”

Mkewe Sall?m alidanganyika kwa maelezo yale, akaufungua mlango bila ya kuthibitisha na akawaongoza chumbani kwa Sall?m, ambaye ndio kwamba amelala. Ili kuzuia kila aina ya makelele, walikiin- gia chumba kile upesi sana, wakaufunga mlango na kuyamalizia mbali maisha ya mtu huyu wa hatari na mfisadi aliyewanyima Waislamu amani yao ya kifikara kwa muda mrefu sana. Kisha wakashuka upesi upesi na kujificha kwenye sehemu ya kuingizia maji, nje ya ngome ile.

Vilio vya mkewe Sall?m viliwaamsha majirani na wote wakaanza kuwafuata wale mashujaa wa Khazraj wakiwa wameshika taa mikononi mwao. Hata hivyo, ingawa walitafuta sana lakini hawakuziona dalili zao zozote zile na hatimaye walirejea majumbani mwao. Ushujaa wa Waislamu wale ulikuwa mkubwa sana kiasi kwamba mmoja wao alijitolea kwenda miongoni mwa Wayahudi kwa kujificha ili akapate taarifa za matokeo ya yale waliyoyafanya (yaani wao Waislamu), kwa kuwa walikuwa wakidhania kwamba Sallaam alikuwa hado yu hai.

Alikwenda na kuingia kwenye kundi la Wayahudi wakati walipokuwa wamemzunguka Sall?m, na mkewe alikuwa akitoa taarifa kamili ya yale yaliyotokea, na kwa ghafla aliutazama uso wa Sall?m na akasema: “Kwa jina la Mola wa Wayahudi! Ameshafariki dunia!” Yule Mwislamu aliyekwenda pale kupata taarifa alirejea na kuwaambia wenzie juu ya ile hali ya mambo. Hivyo wakayatoka maficho yao na kurejea Madina. Huko wakamweleza Mtume (s.a.w.w.) yale yote yaliyotokea.1

Kikundi Cha Waquraishi Chaenda Ethiopia

Kikundi cha Waquraishi waonao mbali walitishika mno na maendeleo ya daima ya Uislamu hivyo walikwenda Ethiopia ili wakaishi huko. Walifikiria kwamba, kama mwishowe Muhammad atapata mamlaka juu ya Rasi yote ya Uarabuni, basi watakuwa tayari wameshakuwa salama kule Ethiopia na kama Waquraishi watashinda watarudi maskani mwao.

Amr bin Aas alikuwa mmoja wa watu wa kikundi hiki kilichotoka Hijaz kwenda Ethiopia kikiwa na zawadi nyingi. Kuwasili kwao kulitukia pamoja na kuwasili kwa mjumbe wa Mtume (s.a.w.w.) aliyeitwa Amr bin Umayyah aliyeleta ujumbe wa Mtume (s.a.w.w.) kuhusiana na Ja’far bin Abi Talib na Muhajiriin wengine. Ili kuupata upendeleo wa machifu wa Waquraishi, ‘Amr bin Aas aliwaambia wenzie: “Ninakwenda kuomba kukutana na Mfalme wa Ethiopia pamoja na zawadi zangu maalum nami nitaiomba idhini ya kukatwa kwa kichwa cha mjumbe wa Muhammad.”

Alifika kwenye baraza la kifalme na akakunja goti moja ili kuonyesha heshima kwa mfalme, kufuatana na desturi za kale. Mfalme alizungumza naye kwa upole na akasema: “Je, mmeniletea zawadi zozote zile kutoka nchini mwenu?” akajibu akasema: “Ndio, Jalali Mfalme.” Kisha akaziwakilisha zawadi zile na akasema: “Jalali Mfalme! Yule mtu aliyetoka hapa barazani kwako hivi karibuni yu mjumbe wa mtu aliyewauwa wazee na mashujaa wetu. Litakuwa jambo la faraja mno kwetu kama nitaruhusiwa kukikata kichwa chake ikiwa ni hatua ya kulipiza kisasi.”

Maneno ya ‘Amr bin Aas yalimkasirisha mno Negus kiasi kwamba bila ya kupenda alijipiga kofi la nguvu mno usoni mwake kiasi kwamba karibuni aivunje pua yake. Kisha kwa ghadhabu akasema: “Je, unaniomba nimsalimishe kwako mjumbe wa mtu aliyeshukiwa na Malaika Mkuu, kama alivyokuwa akimshukia Nabii Musa, ili umuue? Ninaapa kwa jina la Allah! Yeye yu mkweli na atawashinda maadui zake.” Amri bin Aas anasema: “Nilipoyasikia maneno haya nilipatwa na mwelekeo wa kwenye dini ya Mtume Muhammad lakini sikulidhihirisha jambo hili kwa wale wenzangu.”2

Kuzuia Kurudiwa Kwa Matukio Machungu

Tukio chungu na lisilopendeza la Raji’, ambalo matokeo yake ni kwamba familia za Azal na Q?rah waliotokana na kabila la Bani Lihyan waliwauwa watu wa kikundi cha wahubiri wa Uislamu kwa njia ya kikatili na ya woga kabisa, na hata kuwakamata watu wawili waliokuwa hai na kuwauza kwa Waquraishi wenye mamlaka ambao waliwanyonga, ikiwa ni hatua yao ya kulipiza kisasi, liliwahuzunisha mno Waislamu na kuisimamisha misafara ya kikundi cha wahubiri. Sasa kwa kuwa vile vizuizi vyote likuwa vimeondolewa kutoka kwenye ile njia ya Waislamu na ghasia zilizosababishwa na yale makabila ya Waarabu na Wayahudi nazo zimekomeshwa, Mtume wa Usilamu (s.a.w.w.) alifikiria kwamba sasa inafaa kuwaadhibu Bani Lihyan ili kwamba makabila mengine yazingatie wajibu wao na wasije wavisumbue vikundi vya wahubiri wa Kiislamu.

Katika mfunguo tano (Jumadiul Awwal) mwaka wa sita Mtume (s.a.w.w.) alitoka mjini Madina akamteuwa Ibn Ummi Maktum kuwa mwakilishi wake.
Hakumwarifu mtu yeyote yule juu ya lengo lake. Kwa kuwa aliche- lea kwamba Waquraishi na Bani Lihy?n watautambua mpango wake. Hivyo basi, akaishika njia ya Kaskazini iliyokuwa ikienda Shamu, na baada ya kusafiri kwa umbali fulani hivi, akabadili njia yake na akapiga kambi mahali paitwapo Ghar?n palipokuwa nchi ya Bani Lahy?n. Hata hivyo, maadui wale walilitambua lengo lake na wakakimbilia vilimani.

Shambulio hili la silaha na kufedheheshwa kwa adui lilikuwa na athari za kisaikolojia, hatimaye waliogopa mno na kufadhaika.

Ili kulifikia lengo lake, Mtume (s.a.w.w.) alifanya hila za kijeshi na yeye mwenyewe alikwenda na watu mia mbili kutoka pale Ghar?n hadi Asfaan mahali palipo karibu na Makka. Kisha akapeleka watu kumi kwenye mpaka wa Makka (Kiraa’ul Ghamim) katika wadhifa wa kikundi cha watalii katika hali ambayo mwenendo wa askari wa Uislamu na uoneshaji wa nguvu yao uweze kuonekana kwa Makureishi. Baada ya hapo alitoa amri ya kuvunja kambi na kurejea Madina.

Jabir bin Abdulah anasema kwamba baada ya kurejea kutoka kwenye vita hivi, Mtume (s.a.w.w.) alisema: “Najikinga kwa Allah kutokana na usumbufu wa safari, taabu za usafiri na matukio yasiyopendeza kwenye maisha ya kimali na kifamilia ya mwanadamu.”3

Vita Ya Ziqarad

Siku chache tu baada ya kurejea kwa Mtume (s.a.w.w.) mjini Madina, Uyainah bin Hisn Faz?ri alinyakua kundi la ngamia lililokuwa likilisha kwenye malisho ya Madina, akamuua mchungaji wao na kumteka mwanamke wa Kiislamu na akaenda naye. Salamah Aslami aliyekuwa katoka mji wa Madina kwa ajili ya kuwinda alilishuhudia tukio hili. Mara moja alikwenda kwenye kichuguu cha Sala na kuwaita Waislamu waje wasaidie na akasema: “W? Sab?h?” (Waarabu walikuwa wakiitamka sentensi hii walipokuwa wakihitaji msaada). Kisha akawafuatia wale wanyang’anyi na kwa kuwatupia mishale aliweza kuwazuia wasikimbie.

Mtume (s.a.w.w.) alikuwa mtu wa kwanza kumsikia Salamah akiomba msaada. Mara moja akawapeleka baadhi ya masahaba zake kuwafuatilia wanyang’anyi wale. Mapigano madogo yalitokea baina yao. Kwenye mapigano hayo Waislamu wawili na watu watatu wa upande wa wanyang’anyi waliuwawa. Hata hivyo, Waislamu walifaulu kurudisha sehemu kubwa ya ngamia wale kutoka kwa wale wanyang’anyi pamoja na kumpata yule mwanamke wa Kiislamu. Hata hivyo yule adui alijificha kwenye ukanda wa kabila la Ghatfaan. Mtume alikaa kwenye sehemu itwayo ‘Ziqarad’ kwa mchana mmoja na usiku. Ingawa askari wapanda wanyama wa Madina walishikilia kwamba yule adui afuatiliwe, lakini Mtume (s.a.w.w.) hakulifikiria jambo hilo kuwa ni lenye kufaa kutendwa na akarejea Madina.4

Nadhiri Isiyokubalika

Yule mwanamke aliyetetewa hadi akaachiliwa na wale wanyang’anyi alikuja mbele ya Mtume (s.a.w.w.) na kusema: “Nilipokuwa nikichukuliwa mateka pamoja na wale ngamia (alimsoza kidole ngamia mmoja wa Mtume s.a.w.w) niliweka nadhiri ya kwamba kama nikitoka mkononi mwa adui yule nitamchinja ngamia huyu.” Mtume (s.a.w.w.) akamwambia huku akitabasamu: “Umeamua kumpa malipo mabaya kiasi gani ngamia huyu! Alikupatia uhuru wako nawe unataka kumwua?” Kisha akalifafanua jambo lile na kusema: “Nadhiri yenye kuihusu dhambi au iwekwayo kuhusiana na kitu kilicho mali ya mtu mwingine hairuhusiwi. Kwa nadhiri yako hiyo ulimweka ngamia wangu. Hivyo si wajibu juu yako kuitekeleza nadhiri yako.”5

  • 1. Siiratu Ibn Hishamu, Juz. 2. uk. 274-275.
  • 2. Siiratu Ibn Hishamu, Juz. 2. uk. 276-277.
  • 3. Tarikhut-Tabari, Juz. 2, uk. 254; Maghaazil-Waaqidi Juz. 2, uk. 535.
  • 4. Tarikhut-Tabari, Juz. 2, uk. 255; Maghaazil-Waaqidi Juz. 2, uk. 255.
  • 5. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 280;