Sura Ya 40: Matukio Ya Mwaka Wa Sita Hijiriya

Katika mwaka wa sita hijiriya uwezo wa kijeshi wa Waislamu ulikuwa na nguvu ya kuonekana hivi, kiasi kwamba vikosi vyao maalum viliweza kuziendea sehemu zilizo karibu na Makka bila kipingamizi kisha vilirejea. Hata hivyo, nguvu hizi za kijeshi hazikukusanywa kwa lengo la kuteka nchi za makabila au kuzinyakua mali zao.

Kama washirikina wasingeliwanyima Waislamu uhuru wao, Mtume (s.a.w.w.) asingelinunua japo upanga mmoja na asingelipeleka japo askari mmoja. Hata hivyo, kwa kuwa Waislamu na vikundi vyao vya wahubiri walikuwa daima wakitishwa na maadui, Mtume (s.a.w.w.) kwa kila hali na kwa kimaadili alilazimika kuiimarisha nguvu ya kiulinzi ya Uislamu.

Sababu hasa ya vita hivi vilivyotekea hadi kwenye mwaka wa sita hijiriya, na kusema kweli, hadi dakika ya mwisho ya uhai wa Mtume (s.aw.w.) zilikuwa zifutazo:Kuyajibu mashambulizi ya kutisha yaliyofanywa na wale waabudu masanamu, (kama vile Vita vya Badr, Uhud na Vita vya Handaki).

Kuwaadhibu madhalimu waliowaua Waislamu au vikundi vya wahubiri wao katika majangwa au katika sehemu za mbali, au wale waliovunja mapatano waliyoyafanya baina yao na Waislamu. Kwenye kundi hili ni vile vita vyilivopiganwa dhidi ya makabila ya Wayahudi na ile moja iliyopiganwa dhidi ya Bani Lihy?n.

Kuyeyusha ile shauku iliyokuwa ikipikwa miongoni mwa makabila yaliyotaka kukusanya majeshi na kuushambulia mji wa Madina. Mapigano mengi madogo yalitokea kutokana na sababu hii.

Vita Vya Bani Mustaliq

Bani Mustaliq walikuwa ni tawi la Khuz?’?h waliokuwa majirani wa Waquraishi. Taarifa zilifika Madina kwamba Harith bin Abi Zir?r (chifu wa kabila lile) amedhamiria kuuzingira mji wa Madina. Kama alivyofanya katika matukio mengine, Mtume (s.a.w.w.) aliamua kuuzuia ufisadi huu, hivyo basi akaliendea kabila la Bani Mustaliq akifuatana na masahaba zake na kuwakabili karibu na kisima cha Marysi’. Mapigano yalianza baina ya pande mbili. Ushujaa wa Waislamu na woga ulioyashika makabila ya Waarabu juu ya jambo hili uliwafanya maadui kutawanyika baada ya mapigano madogo madogo ambayo ndani yake watu wao kumi na kwa makosa Mwislamu mmoja, waliuwawa. Matokeo ya vita hivi ni kwamba, ngawira nyingi ziliangukia kwenye fungu la jeshi la Uislamu na wanawake wa maadui nao walichukuliwa mateka.1

Nukta zenye mafunzo za vita hivi ni sera alizozifuata Mtume (s.a.w.w.) baada ya vita, akiyazingatia matukio ya vita hivi.

Hata hivyo, mifarakano ilizuka baina ya Muhajiriin na Ansar kwa mara ya kwanza kabisa, lakini laiti si kupatikana busara za Mtume (s.a.w.w.) umoja wao ungalivunjika kutokana na tamaa ya mali ya baadhi ya watu wasioona mbali.

Sababu ya tukio hili ilikuwa kwamba, baada ya kwisha kwa vita vile Waislamu wawili, mmoja akiitwa Jahj?h bin Mas’ud (Muhajir) na mwingine akiitwa Sin?n Juhani (Ansar) waligombana kuhusu maji. Kila mmoja aliwaita watu wake ili wamsaidie, matokeo ya miito hii ya kuomba msaada yangelikuwa kwamba Waislamu wapigane wenyewe kwa wenyewe mahali palipokuwa mbali kutoka kwenye makao yao makuu, na kwa kufanya hivyo wangeliumalizia mbali uhai wao wenyewe. Mtume (s.a.w.w.) alilitambua tukio lile na akasema: “Waacheni hawa watu wawili wenyewe. Mwito huu wa msaada wenye kuchukiza unaofanana na masazo ya kisirani cha ujinga bado haujatoka kutoka nyoyoni mwao.
Watu hawa wawili hawana ujuzi wa mpango wa Uislamu na hawajui ya kwamba Uislamu huwachukulia Waislamu wote kuwa ni ndugu wao kwa wao na kila mwito wenye kuleta mifarakano ni kinyume na dini ya Upweke wa Allah.”2

Mnafiki Mmoja Apepea Miali Ya Mfarakano

Kwa njia hii Mtume (s.a.w.w.) alizizuia tofauti na akayazuia makundi hayo mawili yasishambuliane. Hata hivyo, Abdullah bin Ubayy mmoja wa wanafiki wa Madina aliyekuwa na mfundo usio kifani dhidi ya Uislamu naye alikuwa akishiriki kwenye vita vile kwa sababu tu ya kupata fungu la ngawira, aliudhihirisha uadui na unafiki wake na akawaambia wale waliomkusanyikia hivi: “Yote haya ni matokeo ya matendo yetu wenyewe.

Tumewapa amani Muhajiriin nchini mwetu na tukawahami kutokana na maadui zao. Hali yetu inalandana na methali maarufu isemayo; ‘Mlishe mbwa wako naye atakuuma Naapa kwa jina la Allah! Tutakaporejea Madina itakuwa muhimu kwamba watu wenye nguvu na watukufu (wa Madina wawatoe wale walio dhaifu (yaani Muhajirin).”

Maneno ya Abdulah mbele ya watu ambao akilini mwao mlikuwa bado mmejibanza moyo wa kundi la Uarabu na fikara za zama za Ujinga, yalikuwa na athari zenye madhara juu yao na iliwezekana kwamba umoja wao uhatarike kabisa.

Hata hivyo, kwa bahati nzuri Mwislamu mmoja aliyekuwa na moyo aliyeitwa Zayd bin Arqam aliyekuwa pale, naye aliyajibu maneno yake ya kishetani kwa nguvu zote na akasema: “Ninaapa kwa jina la Allah! Wewe ndiwe mtu uliye duni na uliyefedheheka. Wewe ndie mtu asiyefaidi cheo chochote kile, japo kilicho kidogo sana miongoni mwa ndugu zake. Kinyume chake, Mtume Muhammad yu mwenye kuheshimika miongoni mwa Waislamu na nyoyo zao zimejawa na huba juu yeke.”

Kisha alitoka pale na kumjia Mtume (s.a.w.w.) na kumwarifu juu ya maneno ya uchochezi ya Abdullah. Ili kuonyesha kwamba maneno ya Abdullah hayakumkasirisha, Mtume (s.a.w.w.) aliyakataa maneno ya Zayd mara tatu na kusema: “Pengine wewe umekosea. Pengine hasira zimekufanya useme hivyo. Inawezekana kwamba yeye anakufikiria kuwa u duni na mjinga na wala hakuwa na maana nyingine.” Hata hivyo, Zayd aliukanusha uwezekano wa aina zote hizo na kusema: “Hapana; nia yake ilikuwa kuleta tofauti na kuwasha mifarakano.”

Khalifa wa Pili alimwomba Mtume (s.a.w.w.) amruhusu amuue Abdullah. Hata hivyo Mtume (s.a.w.w.) alimjibu hivi: “Si sahihi kufanya hivyo kwa sababu watu watasema kwamba Muhammad anawauwa marafiki zake.”3

Abdullah aliyafahamu yale mazungumzo ya Zayd bin Arqam na Mtume (s.a.w.w.). Upesi sana alikuja mbele ya Mtume (s.a.w.w.) na kusema: “Katu mimi sikuyasema maneno hayo.” Baadhi ya watu waliokuwa pale walimtakia mema nao walimuunga mkono na kusema kwamba: Zayd amekosea katika kuyanukuu maneno yake.

Hata hivyo jambo hili halikuishia pale, kwa sababu utulivu wa muda ni kama kitulizo katika dhoruba. Yule kiongozi mtukufu wa Uislamu alitaka kufanya jambo fulani litakaloweza kuyafanya yale makundi mawili husika walisahau kabisa jambo hili. Ili kufikia hatima hii, aliwaamrisha watu waondoke ingawa wakati ule haukuwa muda wa kuondokea.

Usayd alimjia Mtume (s.a.w.w.) na kusema: “Huu si muda ufaao kuondoka. Nini sababu ya amri hii?” Mtume (s.a.w.w.) alimjibu akisema: “Je, wewe huifahamu kauli ya Abdillah na kile alichokiwasha?” Usayd aliapa na kusema: “Ewe Mheshimiwa Mtume! Nguvu iko mikononi mwako. Unaweza kumtoa nje. Wewe ni kipenzi mwenye kuheshimiwa. Aliye duni na aliyefedheheshwa ni yeye. Kuwa mwenye huruma kwake kwa kuwa yeye yu mtu aliyeshindwa. Kabla ya kuhamia kwako Madina Aws na Khazraj walikubaliana kumfanya Mtawala wa Madina na walikuwa wakifikiria kukusanya vito vya thamani ili aweze kutengenezewa taji la kumtawazia. Hata hivyo, kwa kuchomoza nyota ya Uislamu cheo chake kilipatwa na mabadiliko na watu wakamwacha. Na anakufikiria kuwa ndiwe sababu ya yote haya.”

Ilitolewa amri ya kuondoka na askari wa Uislamu waliendelea kutembea kwa zaidi ya masaa ishirini na manne, nao hawakutua mahali popote pale ila kwa ajili ya kusali tu. Siku ya pili hali ya hewa ilikuwa yenye joto sana na wote walikuwa wameshapoteza nguvu yao kiasi cha kutoweza kuendelea zaidi na safari, na hapo ilitolewa amri ya kupiga kambi. Mara tu baada ya kushuka kwenye wanyama wao wa kupanda, wote walilala kwa sababu ya uchovu na kumbukumbu zote za uchungu ziliondoka akilini mwao. Hivyo basi, kwa mpango huu mifarakano yao ilipungua.4

Mgongano Baina Ya Imani Na Hisia Za Askari Mmoja

Mwana wa Abdulah bin Ubay alikuwa Mwislamu mchamungu. Kwa mujibu wa mafundisho matakatifu ya Uislamu, alikuwa na huruma zaidi kwa baba yake kuliko yeyote mwingine, ingawa yeye baba mtu alikuwa mnafiki. Alipata kutambua kuhusu yale aliyoyatenda baba yake na akafikiria ya kwamba Mtume (s.a.w.w.) atamuuwa. Hivyo akamwambia Mtume (s.a.w.w.): “Kama imeamuliwa kwamba baba yangu anyongwe, mimi mwenyewe niko tayari kuitekeleza hukumu hiyo nami naomba kazi hiyo asipewe yeyote mwingine.

Ninaomba hivi kwa sababu ninachelea kwamba, kutokana na hisia za Kiarabu na mielekeo ya mvuto wa mtoto kwa baba yake, ninaweza kuipoteza nguvu yangu ya kujitawala na nikamuuwa mtu yule amnyongae baba yangu na kwa kufanya hivyo nikaipaka mikono yangu damu ya Mwislamu na matokeo yake yakawa ni kuyaharibu maisha yangu.”

Maelezo ya mtu huyu ni midhihiriko iliyo bora zaidi ya imani. Kwa nini mtu huyu hakumwomba Mtume (s.a.w.w.) kumsamehe baba yake? Hakufanya hivyo kwa sababu alijua chochote kile alichokifanya Mtukufu Mtume kilikuwa kikiendana na amri ya Allah swt. Hata hivyo huyu mwana wa Abdullah alijikuta akiwa kwenye mashaka ya kisaikolojia. Mvuto wa huba ya mtoto kwa baba na kanuni za utu wema barani Arabia vilimhimiza kumlipiza kisasi myongaji wa baba yake, na kuwa kufanya hivyo akawa ameimwaga damu ya Mwislamu. Kwa upande mwingine, huba ya amani kwenye ukanda wa Uislamu ilimfanya afikiri kwamba ilikuwa muhimu kwamba baba yake auawe.

Ili kuushinda mgongano uliomo akilini mwake, aliichagua njia ya tatu ili kwamba yale maslahi ya Uislamu yaliyo bora zaidi yabakie katika hali ya usalama na vile vile upenzi kwa baba yake usipatwe na madhara. Na ile njia ya tatu ilikuwa iwe ya kwamba yeye mwenyewe aitekeleze amri ya kunyongwa kwa baba yake. Ingawa kitendo hiki ni chenye kuadhibu na kuupasua moyo, lakini ile nguvu ya imani na kujitolea kwa ajili ya mapenzi ya Allah hutoa faraja kwa kiasi fulani.

Hata hivyo, Mtume mwenye huruma alimwambia: “Hakuna jambo la aina hiyo linalodhamiriwa, nami nitakuwa mpole kwake.”

Maelezo hayo yalienea miongoni mwa Waislamu nao wote walishangazwa na ukuu wa kiroho wa Mtume (s.a.w.w.). Manyunyu ya mikanusho na makemeo alinyunyuziwa Abdullah. Alifedheheka mno mbele ya macho ya watu kiasi kwamba baada ya hapo hakuna tena aliyemsikiliza.

Katika matukio haya Mtume (s.a.w.w.) aliwafunza Waislamu mafunzo yenye kumbukumbu kwa daima na akazidhihirisha baadhi ya sera za kisiasa za Uislamu zenye busara. Baada ya tukio hili, yule kiongozi wa wanafiki hakuwa na mvuto tena na alichukiwa na akadharauliwa na watu kwenye mambo yote. Safari moja Mtume (s.a.w.w.) alimwambia Umar: “Uliomba ruhusa yangu umuue. Wale watu ambao katika siku ile wangelishitushwa na kuuwawa kwake na wakaamka na kumwunga mkono, leo hii wanamchukia mno kiasi kwamba kama nikitoa amri ya kumyonga, watamuuwa palepale.”

Mtume (S.A.W.W) Amuoa Juwayriyah

Mtume (s.a.w.w.) alimwoa binti wa Harith, kiongozi wa waasi. Katika vitabu mbalimbali vya maisha ya Mtume (s.a.w.w.) maelezo tofauti tofauti juu ya ndoa hii hutolewa. Hata hivyo, matokeo ya ndoa hii yalikuwa kwamba uhusiano usiovunjika ulidumishwa baina ya Mtume (s.a.w.w.) na jumuiya hii na wengi wa wanawake wa kabila hili waliokuwa wametekwa na Waislamu waliachiliwa bila ya masharti yoyote ikiwa ni ishara ya heshima kwa uhusiano baina yao na Mtume (s.a.w.w.). Ndoa hii ilikuwa ndoa iliyobarikiwa kwa sababu ilitoa matokeo ya kuachiliwa kwa wanawake mia moja.5

  • 1. Tarikhut-Tabari, Juz. 2, uk. 260.
  • 2. Maelezo ya Suhayli juu ya Siiratu Ibn Hisham.
  • 3. Kuchunguza maisha ya khalifa wa Pili kunaudhihirisha ukweli uliopo kwamba katu hakuzidhihirisha nguvu zake kwenye uwanja wa vita na daima alikuwa kwenye mistari ya nyuma. Hata hivyo, kila alipokamatwa adui, alikuwa mtu wa kwanza kumwomba Mtume (s.a.w.w.) amruhusu amwue. Ifuatayo hapa chini ni baadhi ya mifano ya aina hii: (i.) Mmoja wa mifano ya aina hii ulikuwa kwamba alitaka kumwua Abdullah Mnafiki. (ii.) Muda mfupi kabla ya kutekwa kwa mji wa Makka alimwomba Mtume (s.a.w.w.) ampe ruhusa akidengue kichwa cha Haatib bin Abi Balti'ah aliye kuwa akiwafanyia ujasusi waabudu masanamu katika jeshi la Waislamu. (iii) Wakati Abbas, ami yake Mtume (s.a.w.w.) alipomleta Abu Sufyani kwenye kambi ya Wasilamu, yeye (Khalifa wa Pili) alimwomba Mtume (s.a.w.w.) amruhusu amwue (yaani Abu Sufyani) mara moja.
  • 4. Tarikhut-Tabari, Juz. 2, uk. 261-262; Majma’ul Bayaan, Juz. 10, uk. 292-295.
  • 5. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 264.