Sura Ya 42: Matukio Ya Mwaka Wa Saba Hijiriya

Mkataba wa Amani wa Hudaybiyah ulimwondolea Mtume (s.a.w.w.) wasiwasi kutoka kwenye sehemu ya kusini mwa Makka na hivyo basi, kikundi kutoka miongoni mwa machifu wa Uarabuni kilivutiwa na Uislamu. Katika wakati ule aliitumia nafasi hii na akaanza kuwaandikia barua watawala wa zama zile, machifu wa makabila na viongozi wa kidini wa Wakristo, na kuwabalighishia dini yake watu wa mataifa yaliyokuwa yakiishi katika zama zile. Ilikuwa ni dini ambayo katika wakati ule ilikuwa imekwenda hatua moja mbele kutoka kwenye kuamini tu, na imejitwalia umbo la dini ya ulimwengu mzima na iliweza kuwaleta wanadamu wote chini ya bendera ya Upweke wa Allah na mafundisho matukufu ya kijamii na maadili.

Hii ilikuwa ni hatua ya kwanza aliyoichukua Mtume (s.a.w.w.) baada ya mgogoro wa miaka kumi na tisa na Waquraishi wakaidi. Na kama wale maadui wa ndani wasingelimshughulisha katika vita vya umwagaji damu, basi angeliyabalighishia Uislamu yale mataifa yaishio mbali na Uarabuni mapema zaidi. Hata hivyo, mashambulizi ya kutisha ya Waarabu yalimlazimisha kuitumia sehemu kubwa ya muda wake katika kuuhami Uislamu.

Barua alizoziandika Mtume (s.a.w.w.) kwa wafalme, wana wa wafalme, machifu wa makabila, viongozi mashuhuri wa kidini na kisiasa, zilitoa mwanga juu ya njia za ubalighishaji wake wa dini. Leo tunayo maandiko ya barua 185 alizoziandika Mtume (s.a.w.w.) Kwa ajili ya kuubalighisha au kuwaita watu kwenye Uislamu au kwa njia ya mapatano na mikutano.

Wanachuoni wa hadithi na wanahistoria wamezihifadhi kwenye kumbukumbu zao.1 Barua zote zaonyesha kwamba njia za kuwaita watu na kuubalighishia Uislamu alizozifanya Mtume (s.a.w.w.) ni zile za kimantiki wala si zile za vita na upanga. Mtume (s.a.w.w.) alipojihisi kuwa katika usalama kutokana na mashambulizi ya Waquraishi aliifanya sauti yake iwafikie wakazi wa ulimwenguni kote kwa kuwapelekea barua na mubalighiina.

Ujumla Wa Utume (Kwa Watu Wote)

Baadhi ya watu wajinga huutuhumu na kuutilia shaka utume wa Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) ulioletwa kwa ajili ya watu wote duniani kote, nao huziiga zile nyimbo tamu ziimbwazo na baadhi ya waandishi wa kukodiwa ambao kiongozi wao ni mtaalamu mmoja wa nchi za Mashariki aitwaye Sir William Muir, asemaye: “Wazo la ujumbe wa Muhammad kuwa dini ya ulimwengu mzima lilizuka baadae, na kuanzia kwenye mwanzo wa utume wake hadi alipokufa Muhammad aliwaita kwenye Uislamu Waarabu tu, naye hakuifahamu sehemu yoyote ile zaidi ya Uarabuni.”

Mwandishi huyu wa Kiingereza ameifuata mbinu ya ajabu iliyo ngeni kwa watu wa taifa lake. Bila kujali Aya nyingi zithibitishazo kwamba Mtume (s.a.w.w.) aliwaita kwenye itikadi ya Upweke wa Allah na Utume wake watu wote, yeye Sir William Muir anauficha mwito wa Mtume (s.a.w.w.) na anasema kwamba ulikusudiwa Waarabu tu. Hapa chini tunanukuu baadhi ya Aya za Qur’ani Tukufu zenye kuonyesha kwamba Utume wa Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) umekusudiwa kwa watu wote:

قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنِّي رَسُولُ اللَّهِ إِلَيْكُمْ{158}

Waambie: Enyi watu! Hakika mimi ni Mtume wa Allah kwenu nyote…
(Surah al A’raaf, 7:158).

Hapa hatuna budi kutambua kwamba watu wanaotajwa hapa si Waarabu tu bali ni wanadamu wote.

وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا كَافَّةً لِلنَّاسِ بَشِيرًا وَنَذِيرًا وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ {28}

“Na Hatukukutuma ila kwa watu wote uwe mtoaji wa khabari njema na mwonyaji, lakini watu wengi hawajui.” (Sura al-Saba, 34:28).

إِنْ هُوَ إِلَّا ذِكْرٌ لِلْعَالَمِينَ {27}

“Hiyo siyo ila ni ukumbusho kwa walimwengu.” (Sura al-Takwir, 81:27).

وَمَنْ يَبْتَغِ غَيْرَ الْإِسْلَامِ دِينًا فَلَنْ يُقْبَلَ مِنْهُ وَهُوَ فِي الْآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ {85}

“Na anayetaka dini isiyokuwa ya Kiislamu, basi haitakubaliwa Kwake, na yeye katika Akhera atakuwa ni miongoni mwa wenye hasara.” (Sura Al-Imran, 3:85).

Aya hii inazitangua dini zote isipokuwa Uislamu tu na inawawajibisha wanadamu wote kuufuata Uislamu tu

لِيُنْذِرَ مَنْ كَانَ حَيًّا وَيَحِقَّ الْقَوْلُ عَلَى الْكَافِرِينَ {70}

“Ili amwonye aliye hai na neno litimie juu ya makafiri.” (Sura, Yasin, 36:70)

هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَىٰ وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ وَلَوْ كَرِهَ الْمُشْرِكُونَ {33}

Yeye ndiye Aliyemtuma Mtume wake kwa mwongozo na kwa dini ya haki ili ishinde dini zote, ingawa washirikina watachukia.” (Sura Tawbah, 9:33).

Sasa tunamwuliza huyu mwandishi Mwingereza, vipi anasema kwamba wazo la Uislamu kuwa dini ya ulimwengu mzima lilikuja baadae, ingawa miito kwa watu wote inadhihirishwa kwenye aya hizi? Je, mtu anayo haki ya kutia shaka juu ya utume wa Mtume (s.a.w.w.) kuwa wa ulimwengu mzima ingawa zipo aya hizi na nyinginezo, na wapo wajumbe waliotumwa kwenye nchi za mbali na maneno ya barua za Mtume (s.a.w.w) zilizomo mwenye kumbukumbu za kurasa za historia? (baadhi ya zile barua za asilia alizozipeleka kwa watu mbalimbali wa sehemu za mbali zinapatikana na zinayapamba majumba ya kumbukumbu ya ulimwengu).

Yule mwandishi Mwingereza anasema kwa ufidhuli usio wa aibu kwamba Muhammad hakuwa na ujuzi wa sehemu yoyote ile zaidi ya Uarabuni (Hijaz) ingawa alikwenda Shamu pamoja na ami yake alipokuwa na umri wa miaka kumi na sita na wakati wa utu uzima wake alifanya biashara kwa niaba ya Bibi Khadija na alikuwa akifuatana na misafara ya biashara.

Hakuma shaka kwamba wakati tunaposoma katika vitabu vya historia kwamba, Alexander Mmakedonia alitaka kuwa mtawala wa ulimwengu, au Napoleon alikuwa na shauku ya kujenga dola ya ulimwengu mzima, hatushangazwi hata kidogo, lakini pale mustashirik wanaposikia kwamba Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) kwa amri ya Allah amewaita watawala wawili wakubwa ulimwenguni kote (ambao walikuwa na uhusiano wa kibiashara na Waarabu) wasilimu, wao pamoja na ukaidi wao wote na shaka zisizo na msingi wowote, wanasema kwamba hili ni jambo lisilowezekana.

Ujumbe Wa Utume Wapelekwa Sehemu Za Mbali

Kama yalivyo mambo yote yaliyo muhimu, suala la kuwalingania watawala wa sehemu mbalimbali kwenye Uislamu nalo liliwekwa mbele ya halmashauri kubwa ya ushauri ili lijadiliwe. Siku moja Mtume (s.a.w.w.) aliwaambia masahaba zake: “Kesho asubuhi mhudhurie nyote ili mnipe ushauri wenu juu ya jambo muhimu sana.

“Katika siku iliyofuatia aliwahutubia masahaba zake baada ya sala ya Alfajiri, alisema: “Wausieni waja wa Allah kutenda mema. Allah Ameiharimisha Pepo kwa yule aliye mlinzi wa mambo ya watu, lakini asijitahidi kuwaongoza na kuwaonyesha njia iliyonyoka. Lazima msimame na kuupeleka ujumbe wa Uislamu kwenye nchi za mbali na lazima mfanye wanadamu waisikie sauti ya Upweke wa Allah. Hata hivyo, msinipinge kama vile wanafunzi wa Nabii Isa (a.s.) walivyompinga.”

Mtume (s.a.w.w.) aliulizwa kuhusu jinsi wale wanafunzi wa Nabii Isa walivyompinga. Alijibu akisema: “Kama mimi nifanyavyo, yeye naye ali- watuma watu wakiwa wajumbe wake kwenye sehemu mbalimbali. Kutoka miongoni mwao wale waliowajibika kwenda masafa mafupi waliitii amri yake, lakini wale waliolazimika kwenda masafa marefu walimwasi.”

Baada ya hapo Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) aliwatuma watu sita walio hodari kwenda sehemu mbalimbali pamoja na barua ambazo ndani yake utume wake kwa watu wote ulidhihirishwa. Hawa mabalozi wa mwongo- zo walikwenda Iran, Byzantum (Dola ya Kikristo ya Shamu/Syria) Ethiopia, Misrii, Yamamah, Bahrain, na Hira (Jordan) katika siku ile ile.

Zile barua za Mtume (s.a.w.w.) zilipoandikwa na makatibu maalum, watu waliokuwa na ujuzi wa tabia njema za mabaraza ya kifalme ya zama zile walimshauri Mtume (s.a.w.w.) kwamba azitie muhuri, kwa sababu watawala mbalimbali hawakujisumbua kuzisoma barua zisizotiwa saini, (na katika siku zile, saini zilitiwa kwa njia ya muhuri).

Kwa lengo hili, uli- tayarishwa muhuri wa duara wa fedha, kama alivyoagiza Mtume (s.a.w.w.) mwenyewe na sentensi “Muhammad Rasulillah” Muhammad mjumbe wa Allah ilikatwa juu ya muhuri ule. Ukataji wa sentensi hii ulikuwa wa utaratibu huu kwamba neno ‘Allah’ lilikuwa juu, neno ‘Rasul’ lilikuwa katikati na neno ‘Muhammad’ lilikuwa chini. Utaratibu na uhodari huu ulitumika ili kuzuia kuiga na udanganyifu. Msomaji alitakiwa kwanza kuisoma ile saini kuanzia chini hadi alifikie neno ‘Allah’ (Muhammad Rasuli Allah). Hakutosheka na hilo tu, kila baada ya kuigandisha bahasha ya ile barua kwa nta maalumu (badala ya gundi ya ‘lac’ itumikayo siku hizi), alipiga muhuri juu yake.2

Hali Ya Dunia Wakati Wa Uwasilishaji Mwaliko Wa Jumla

Katika nyakati zile nguvu kuu ya ulimwengu ilikuwa mikononi mwa dola mbili kubwa na ushindani na vita baina yao viliendelea kwa muda mrefu. Vita baina ya Iran na Urumi zilianza katika zama za Waakimenia (Achemenias) na ziliendelea hadi katika kipindi cha Wasasani. Wakati ule upande wa Mashariki ulitawaliwa na Mtawala wa Kiirani na Iraq, Yaman na sehemu ya Asia ndogo zilihesabiwa kuwa ni sehemu za pembeni na makoloni ya Iran. Kisha ile Dola ya Kirumi iligawanyika pande mbili (ambazo ni upande wa Magharibi na Mashariki).

Kwa kuwa katika mwaka wa 395 Masihiya Theodosius The Great, yule Mtawala wa Kirumi, aliigawa dola yake baina ya wanawe wawili na hivyo akafanya kuwako kwa nchi mbili kwa majina ya dola ya Urumi ya Mashariki na Dola ya Urumi ya Magharibi; Ile dola ya Magharibi ilipinduliwa katika mwaka 476 Masihiya. Hata hivyo, ile dola ya Urumi ya Mashariki iliyokuwa na mji wake mkuu wa Constantinople na ambayo vilevile ilizitawala nchi za Shamu na Misri ilizishika hatamu za siasa za ulimwengu mikononi mwake katika wakati wa kuanza kwa Uislamu. Iliendelea kuwako hadi kwenye mwaka wa 1453 Masihiya wakati mji wa Constantinople ulipotekwa na Sultani Muhammad II Faatih. Hapo kuwako kwa dola hii kukakoma na ikavunjwa kabisa.

Arabia ilikuwa imezungukwa na hizi dola kuu mbili. Hata hivyo, kwa vile ardhi yake haikuwa na rutuba, na wakazi wake walikuwa mabedui walikuwa wametawanyika, hakuna yoyote kati ya dola hizi mbili iliyoonyesha mwelekeo wa kuliteka Bara hili.

Fahari, udhalimu wao na vita baina yao pia vilizizuia dola hizi kuyatambua maendeleo na mabadiliko ya kisiasa kwenye eneo hili, na katu hawakuona kwamba taifa lililo mbali kabisa kutoka kwenye ustaarabu lingeliweza kuzikomesha dola zao kwa nguvu ya imani yake, na kwamba yale maeneo yaliyoangukia kwenye giza kutokana na udhalimu wao yataangazwa na alfajiri angavu ya Uislamu. Kama wangeliupata utambuzi wa kuwako kwa nuru hii iangazayo, wangeliizimisha katika hatua yake ya awali kabisa.

Mjumbe Wa Uislamu Katika Nchi Ya Kirumi

Kaisari, yule Mfalme wa Kirumi, alikula kiapo kwa Mungu kwamba, kama akishinda vita dhidi ya Iran, atatoka kwenye makao yake makuu (Constantinople) na kwenda Yerusalemu kwa miguu kufanya Hija ya sehe- mu ile Takatifu, ikiwa ni ishara ya kutoa shukrani zake kwa ule ushindi mkuu. Baada ya kupata ushindi alikitekeleza kiapo chake na akaenda Yerusalem kwa miguu.

Dihyah bin Kalbi alitumwa na Mtume (s.a.w.w.) kuipeleka barua yake kwa Kaisari. Alikuwa kaishafanya safari nyingi kwenda Shamu, naye alikuwa na ujuzi kamili wa sehemu mbalimbali za ukanda ule. Sura yake ya kuvutia, na tabia tukufu vilimfanya astahiki kabisa kulibeba jukumu hili lililo muhimu zaidi.

Kabla ya kutoka Shamu kwenda Constantinople akiwa kwenye mmoja wa miji ya Shamu uliotiwa Busra3 alitambua kwamba Kaisari amekwenda Yerusalem. Hivyo basi, upesi sana akaonana na Harith bin Abi Shamir, gavana wa Busra na kumweleza kuhusu ile kazi muhimu aliyonayo.

Mwandishi wa Tabaqaatul-Kubra anaandika hivi:4 “Mtume (s.a.w.w.) alikuwa kamwelekeza Dihyah kumkabidhi barua ile yule mtawala wa Busra ili kwamba yeye ampe Kaisari. Inawezekana kwamba maelezo haya yalitolewa kwa kuzingatia kwamba yeye Mtume (s.a.w.w.) alitambua juu ya safari ya Kaisari au kwa sababu hali na uwezekano wa Dihyah ulikuwa na kikomo na safari yake ya kwenda Constantinople haikuwa huru kutokana na matatizo na shida. Hata hivyo, yule balozi wa Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) aliwasiliana na yule Mtawala wa Busra. Yule gavana alimwita mtu mmoja aliyeitwa Addi bin Haatim na kumwamrisha afuatane na yule balozi wa Mtume (s.a.w.w.) hadi Yerusalem na kumpa Kaisari ile barua ya Mtume (s.a.w.w.).

Yule balozi ilikuwa aonane na Kaisari mjini Hams. Aliomba kuzungumza na Kaisari na akaomba kwamba uwekwe muda maalum wa kuzungumza naye. Maafisa wahusika wakamwambia: “Itakubidi umsujudie Kaisari mara moja, kwa sababu kama hukufanya hivyo hatakusikiliza na hataipokea barua yako.” Dihyah, yule balozi wa Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) mwenye hekima, akasema: “Nimeichukua taabu yote hii katika kuja hapa kuzikomesha hizi desturi zisizo sahihi. Nimeelekezwa na Mtume kwamba nimwambie Kaisari kwamba kumwabudu mwanadamu hakuna budi kukoma na hakuna apasaye kuabudiwa ila Allah, Mwenye nguvu zote. Basi vipi mimi niliye na jukumu na itikadi hii nitaweza kuyakubali maoni yenu na kumsujudia mtu yeyote asiye Allah?”

Uthabiti, uimara na hoja zenye nguvu za balozi huyu zilipendwa mno na wale wafanyakazi wa baraza la mfalme. Mfuasi mmoja wa mfalme aliyekuwa mwema akamwambia Dihyah: “Iache hiyo barua kwenye meza maalum ya Mfalme kisha urejee. Hakuna aigusaye barua iliyoko juu ya meza ile ila Kaisari mwenyewe. Kaisari atakapoisoma atakuita.” Dihyah akamshukuru mtu yule kwa kumpa mwongozo ule, akaiacha ile barua kwenye ile meza na akarejea.

Kaisari akaifungua ile barua. Neno la kwanza la barua ile: Bismillah’ (kwa jina la Allah) lilimvutia na akasema: “Katu sijapata kuiona barua ya aina hii ila ya Suleimani.” Kisha akamwita mkalimani wake ili amsomee ile barua na kumtafsiria. Yule mkalimani aliitafsiri ile barua ya Mtume (s.a.w.w.) kama ifuatavyo: “Hii ni barua itokayo kwa Muhammad bin Abdullah kwenda kwa Hercules Mkuu wa Urumi. Amani na iwe juu ya wafuasi wa mwongozo. Ninakulingania kwenye dini ya Uislamu. Silimu ili usalimike. Allah Atakulipa thawabu mbili (thawabu kwa kuamini kwako wewe mwenyewe na thawabu kwa kule kuamini kwa walio chini yako). Hata hivyo, kama ukiugeuzia uso wako Uislamu, utawajibika kwa dhambi za ‘Waarisiyani’5

“Halikadhalika. Enyi watu wa Kitabu! Tunakuiteni kwenye neno lililo sawa baina yetu, yaani tusimwabudu yeyote ila Allah. Tusimfanye yeyote kuwa mshirika wake. Baadhi yetu nao wasiwafanye wengine kuwa miungu wao. Na (ewe Muhammad!) Watakapoikaidi dini ya kweli, sema: Shuhudieni ya kwamba sisi ni Waislamu.”

Kaisari Afanya Uchunguzi Juu Ya Mtume (S.A.W.W)

Yule mtawala wa Kirumi mwenye hekima alifikiria kwamba huenda mwakilishi wa barua ile alikuwa ni yule Nabii Aliyeahidiwa, Muhammad, aliyezungumziwa kwenye Injili na Taurati. Hivyo basi, aliamua kupata taarifa kamili juu ya Mtume (s.a.w.w.). hivyo alimwita mkuu wa idara ya utawala na kumwambia: “Fanya utafiti kamili kwa kupitia Shamu. Inawezekana kwamba ukaweza kupata baadhi ya jamaa au ndugu wa Muhammad au watu wengine wanaozifahamu habari zilizopita za mtu huyu ili niweze kupata taarifa kutoka kwao.”

Kwa bahati katika siku zile Abu Sufyani na watu wengine kutoka miongoni mwa Waquraishi walikuwa wamefika Shamu kwa ajili ya biashara. Yule mwakilishi wa Kaisari alionana nao na akawachukua wote hadi Yerusalemu. Walichukuliwa na kupelekwa wakaonane na Kaisari. Kaisari akawauliza: “Je, yuko yeyote miongoni mwenu aliye na uhusiano na Muhammad?” Abu Sufyani akajisoza kidole na kusema: “Yeye na mimi tunatokana na kabila moja na koo zetu zinakutana kwa jadi wetu wa nne (Abdi Munaf).”Kaisari akaamrisha kwamba Abu Sufyani asimame kwa kumwelekea na wale wengine wasimame mgongoni kwake ili kwamba kama akiwa na upendeleo katika majibu yake mara moja waeleze kosa au uwongo wake. Baada ya kuufanya mpango huu, Kaisari alimwuliza Abu Sufyani maswali yafuatayo ambayo Abu Sufyani aliyajibu kwa uhakika kama ifuatavyo:

Kaisari: Unajua nini kuhusu jadi zake Muhammad?

Abu Sufyani: Yeye anatokana na familia tukufu.

Kaisari: Je, alikuwapo yeyote kutoka miongoni mwa jadi zake aliyetawala watu?

Abu Sufyani: Hapana.

Kaisari: Je, Kabla ya kudai kwamba yu Mtume, alikuwa akijiepusha na uwongo au la?

Abu Sufyani: Hakuna shaka kwamba Muhammad alikuwa mtu mkweli.

Kaisari: Ni daraja lipi la watu wamuungao mkono na kumwamini?

Abu Sufyani: Watu watukufu wako dhidi yake na watu wa kawaida na watu daraja la chini ndio wafuasi wake waaminifu.

Kaisari: Je, wafuasi wake wanaongezeka?

Abu Sufyani: Ndio.

Kaisari: Je, mtu yeyote kutoka miongoni mwa wafuasi wake amepata kugeuka na kuwa mwenye kuikana dini yake?

Abu Sufyani: Hapana.

Kaisari: Je, alipokuwa akipigana dhidi ya maadui zake, alikuwa akishindwa?

Abu Sufyani: Katika baadhi ya nyakati alikuwa akishinda na katika nyakati nyingine alishindwa.

Kaisari akamwamrisha mkalimani amwambie Abu Sufyani na wenzie kwamba kama maelezo haya ni sahihi, yeye (Muhammad) bila shaka atakuwa ni yule Nabii wa mwisho aliyeahidiwa. Kisha akaongeza kusema: “Ninayo taarifa kwamba Nabii wa aina hii atatokea, lakini mimi sikufikiria kwamba atatokana na kabila la Waquraishi.

Hata hivyo, mimi niko tayari kutoa heshima zangu kwake na kuinawisha miguu yake ikiwa ni ishara ya heshima na hivi karibuni mamlaka na utukufu wake utazikamata nchi za Kirumi.”

Mpwawe Kaisari alisema: “Katika barua ile, Muhammad ameandika jina lake juu ya jina lako, lakini bado hajaadhibiwa kutokana na uchochezi wake huu.”

Kaisari akasema kwa ghadhabu: “Inafaa kwamba jina la mtu yule ambaye Malaika mkuu Jibriil amemshukia lilitangulie langu?”

Abu Sufyani anasema: “Upendeleo wa ndani zaidi wa Kaisari juu ya Muhammad ulizaa minong’ono mle barazani nami nikashikwa na wasiwasi kutokana na kukuwa kwa hasira zake kwamba isije ikawa kwamba cheo cha Muhammad kikawa juu zaidi kiasi kwamba taifa la kirumi likaanza kumwogopa. Ingawa pale ulipoanza uulizaji wa maswali nilijaribu kumtweza Muhammad mbele ya Kaisari na nikamwambia kwamba Muhammad alikuwa mdogo kuliko vile alivyokwisha kusikia juu yake, lakini Kaisari hakuyasikiliza maelezo yangu yenye kuvunja heshima, na akasema: “Yajibu tu yale maswali ninayokuuliza.”6

Barua Ya Mtume (S.A.W.W) Yamvutia Kaisari

Kaisari hakutosheka tu na ile taarifa aliyoipata kutoka kwa Abu Sufyani lakini aliandika barua juu ya jambo lile kwa mmoja wa wataalamu wa Urumi. Yule mtaalamu alijibu kwa kuandika hivi: “Huyo ndiye yule Nabii anayengojewa na ulimwengu.” Kaisari alitayarisha mkutano mkubwa kwenye moja ya majumba ya watawa ili ajue jinsi machifu wa Kirumi wafikiriavyo, na baada ya kuisoma ile barua ya Mtume (s.a.w.w.) mbele yao, alisema: “Je, mnakubali kwamba niiridhie dini yake?” Mara moja yakatokea machafuko makubwa mno kwenye mkutano ule kiasi kwamba upinzani wa watu ulimwogofya Kaisari kuhusu uhai wake.

Mara moja akaamka kutoka kwenye kiti chake kilichokuwa kwenye sehemu iliyoinuka na akawahutubia watu wake, akisema: “Kwa kuliweka lengo hili mbele yenu nilitaka kukujaribuni. Uthabiti na unyoofu wenu katika dini ya Nabii Isa umeuibua upendo na furaha yangu juu yenu.”

Kaisari akamwita Dihyah na akampa heshima. Aliandika jibu la Barua ya Mtume (s.a.w.w.) na vilevile akapeleka zawadi fulani fulani kupitia kwa Dihyah. Katika barua yeke ile alionyesha imani na utii wake kwake.7

Balozi Wa Mtume (S.A.W.W) Awasili Iran

Yule Balozi wa Mtume (s.a.w.w.) alipoondoka kwenda kwenye baraza la nchi ya Iran, mtawala wa nchi ile iliyo pana mno alikuwa ni Khusro Perviz. Yeye alikuwa mtawala wa pili baada ya Anushirwan ambaye alikikalia kiti cha enzi miaka thelathini na miwili kabla ya kuhajiri kwa Mtume (s.a.w.w.) na ilimbidi kuyakabili matukio mengi, machungu na matamu kwenye kipindi kile. Katika utawala wake Khusro Perviz nguvu ya Iran ilikuwa kwenye hali ya kuyumba kabisa. Kwenye wakati fulani Iran ilipenya katika Asia Ndogo na kuieneza mamlaka yake hadi karibu na Constantinople na Msalaba wa Nabii Isa (a.s.) uliokuwa kitu kitakatifu zaidi miongoni mwa Wakristo aliuchukua na kuupeleka kwenye mji wake mkuu, Taisfun (Madaa’in).

Yule mtawala wa Kirumi aliomba amani na akampeleka balozi kwenye baraza la Iran kufanya mapatano ya Amani. Sasa mipaka ya Iran ililingana na mipaka ya nchi za Waakimeni.

Kisha, hata hivyo Iran ikafika kwenye ukingo wa maanguko kutokana na sera mbaya, fahari iliyokithiri na maisha ya kibadhilifu ya mtawala. Zile nchi zilizotekwa zikaponyoka moja baada ya nyingine na majeshi ya maadui yakafika ndani zaidi ya Iran (yaani Dastgards karibu na Taisfun). Matokeo yake yakawa kwamba Khusro Perviz akalazimika kukimbia kutokana na kuwaogopa Warumi. Kitendo hiki cha aibu kwa upande wake kiliiamsha ghadhabu ya taifa na hatimaye aliuawa na mwanawe mwenyewe aliyeitwa Shirviyah.

Wanahistoria huyachukulia maanguko ya Iran kuwa ni matokeo ya fahari, kujipendelea na maisha ya anasa ya mtawala. Kama angaliukubali ujumbe ulioletwa na yule balozi wa Amani, utukufu wa Iran ungalisalia kwenye usalama na amani.

Kama ile barua ya Mtume (s.a.w.w.) haikuleta mvuto uliohitajika akilini mwa Khusro Perviz, basi hali hii haikutokana na kitu chochote kibaya katika barua ile au kwa sababu yule mtu aliyeileta alifanya kosa. Bali kusema kweli fikara zake za ajabu na kujipendelea kulikokithiri havikumruhusu kuufikiria mwito wa Mtume (s.a.w.w.) japo kwa kitambo tu. Matokeo yake ni kwamba, japo kabla ya mkalimani kuimalizia barua ile, alipiga makelele na baada ya kuinyakua barua ile, aliipasua vipande vipande. Yafuatayo hapa chini ndio maelezo kamili ya tukio lile: Mwanzoni mwa mwaka wa saba Hijiriya8 Mtume (s.a.w.w.) alimteua mmoja wa maafisa wake mashuja aliyeitwa Abdullah Huzafah Sahmi Qarashi kupeleka barua kwa Khusro Pervis akimlingania kwenye Uislamu. Hapa chini tunaona ile barua ya Mtume (s.a.w.w.):

“Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Rahim. Hii ni barua itokayo kwa Muhammad Mjumbe wa Allah, kwenda kwa Kisra Mkuu wa Iran. Amani na iwe juu yake yule autafutaye ukweli na akaidhihirisha imani yake juu ya Allah na juu ya Mtume Wake na akashuhudia ya kwamba hakuna mungu ila Allah na kwamba hana mshirika, na yule aaminiye kwamba Muhammad yu mja na Mtume wake. Kwa Amri ya Allah, ninakuita (uje) Kwake. Amenituma kwa ajili ya mwongozo wa watu wote ili kwamba niwaonye wote dhidi ya ghadhabu Yake na niwafikishie makafiri onyo la mwisho. Silimu ili kwamba uwe salama. Na kama ukikataa kusilimu, utawajibikiwa na dhambi.”9

Yule Balozi wa Mtume (s.a.w.w.) aliwasili kwenye baraza la Iran. Khusro Perviz aliamrisha kwamba ile barua ichukuliwe kutoka kwake. Lakini yule balozi akasema kwamba lilikuwa ni jambo muhimu kwamba ampe mfalme barua ile yeye mwenyewe, na kisha akaiwasilisha kwake. Khusro Perviz alimwita mkalimani naye akaitafsiri hivi:

“Hii ni barua itokayo kwa Muhammad Mjumbe wa Allah, kwenda kwa Kisra mkuu wa Iran. . . Yule mkalimani alikuwa bado hajamaliza kuisoma barua ile wakati yule mtawala wa Iran alipofadhaika mno, akapiga ukelele kwa sauti kuu, akaichukua ile barua kutoka mikononi mwa yule mkalimani akaipasua vipande vipande na akasema kwa sauti kuu: “Hebu mtazame mtu huyu! Ameliandika jina lake mwenyewe kabla ya jina langu.” Mara moja akaamrisha kwamba Abdullah atolewe nje ya Ikulu. Abdullah akatoka mle Ikulu akampanda farasi wake na akaondoka kurejea Madina. Alipofika huko alimwarifu Mtume (s.a.w.w.) jambo lile. Mtume (s.a.w.w.) alichukizwa mno kupata tarifa za utovu wa heshima aliouonyesha Khusro, na dalili za ghadhabu zilijitokeza usoni mwake. Alimlaani Khusro kwa maneno haya: “Ee Mola! Uvunje ufalme wake vipande vipande.”10

Maoni Ya Uwongo Ya Yaa’qubi

Kinyume na ukweli ukubaliwao na wanahistoria wengi, Yaa’qubi katika historia yake anasema hivi: “Khusro Perviz aliisoma ile barua ya Mtume (s.a.w.w.) na akampelekea zawadi ya manukato ya miski na nguo za hariri kupitia kwa yule balozi wake zikiwa ni ishara ya heshima kwake.
Mtume akayagawa manukato yale na akasema kwamba: “Hariri haikuwafaa wanaume.” Vile vile alisema: “Nguvu ya Uislamu itaingia katika nchi zake na amri ya Allah itatimizwa hivi karibuni.”11

Hata hivyo, hakuna yeyote miongoni mwa wanahistoria anaye kubaliana naye, ila Ahmad bin Hanbal anayeandika kwamba Khusro Perviz alipeleka zawadi kwa aijili ya Mtume (s.a.w.w.).12

Khusro Perviz Awasiliana Na Mtawala Wa Yemen

Nchi yenye rutuba ya Yaman iko upande wa Kusini mwa mji wa Makka na daima watawala wake wamekuwa wakitawala wakiwa ni vibaraka wa Wafalme wa Kisasani. Mtawala wa Yaman katika siku zile alikuwa ni Bazan na yule Mfalme wa Kisasani aliandika barua kwa jinsi ya majivuno ya majisifu hivi: “Nimearifiwa kwamba mtu mmoja kutoka miongoni mwa Waquraishi wa Makka anadai kwamba yu Mtume. Wapeleke maafisa wako wawili walio mashuja kwake ili wakamtie kizuizini na kumleta kwangu.”13

Ibn Hajr ameeleza kwenye kitabu chake al-Isabah kwamba Khusro Perviz alimwamrisha Bazan kwamba hao maafisa wawili hawana budi wamshawishi Mtume arejee kwenye dini ya jadi zake na kama akikataa kufanya hivyo, akatwe kichwa chake na kipelekwe kwake.

Barua hii yaonyesha dhahiri ujinga wa mtawala wa wakati ule, hakuweza hata kujua kwamba yule mwenye kudai utume kahajiri kutoka Makka kwenda Madina miaka sita kabla ya pale. Vilevile hakutambua kwamba haikuwezekana kumtia kizuizini kwa kuwatuma maafisa wawili, au japo kumwita aende Yaman mtu ambaye aliyedai kuwa yu Mtume kwenye nchi ambayo ushawishi wake umeenea mno kiasi kwamba alikuwa akiwatuma mabalozi kwenye mabaraza ya watawala wa ulimwengu.

Kama alivyoamrishwa na makao makuu, yule Mtawala wa Yaman aliwapeleka huko Hijaz maafisa wawili mashujaa na wenye nguvu walioitwa Firoz na Kharkhusrah. Kwanza walionana na Mquraish mmoja mjini Taa’if.

Aliwaongoza na akasema: “Mtu mnayehitaji kuonana naye, siku hizi yuko Madina.” Hapo wakaenda Madina na wakajifikisha mbele ya Mtume (s.a.w.w.) wakampa Mtume (s.a.w.w.) barua ya Bazan na kusema: “Kufuatana na amri tuliyopewa kutoka makao makuu, tumetumwa tukuchukue twende nawe Yaman, nasi tunafikiri kwamba Bazan atamwandikia barua Khusro Perviz kuhusiana nawe na atafanya yale ayasemayo, au sivyo, kwa vyovyote vile vita itaanza baina yako na sisi na nguvu ya Kisasani itazibomoa nyumba zenu na kuwauwa watu wenu.”

Mtume (s.a.w.w.) aliyasikiliza maneno yao kwa utulivu kamili. Kabla ya kuwapa jibu aliwakaribisha wasilimu. Hakuzipenda sura zao kwa vile walifuga masharubu marefu na akawaambia: “Mola wangu ameniamrisha kwamba nifuge ndevu zangu na kuyafanya masharubu yangu kuwa mafupi.”14

Maafisa hawa walitishwa mno na ukuu, haiba na utulivu wa Mtume (s.a.w.w.) kiasi kwamba alipowakaribisha wasilimu, walikuwa wakitetemeka. Kisha akawaambia: “Mnaweza kwenda leo hii. Nitakuarifuni uamuzi wangu kesho.”Wakati uleule ulikuja ufunuo na Malaika Mkuu ukimwarifu Mtume (s.a.w.w.) kuhusu kuuawa kwa Khusro Perviz.

Katika siku iliyofuatia wale maafisa wa Yaman walipokuja kwa Mtume (s.a.w.w.) aliwaambia: “Mola wa ulimwengu ameniarifu kwamba yalipopita masaa saba ya usiku uliopita, Khusro Perviz kauawa na mwanawe (Shirviyah) ambaye hivi sasa kakalia kiti cha enzi.”

Ule usiku ambao Mtume (s.a.w.w.) aliuainisha ulikuwa usiku wa kuchea Jumanne, mwezi 10, Jumadiul Awwal, 7 Hijiriya.15 Wale wawakilishi wa Bazan walishangazwa sana kusikia hivyo na wakasema: “Jukumu la yale uliyoyasema ni kubwa zaidi kuliko dai la utume lililomkasirisha yule mfalme wa Kisasani. Hatuna la kufanya ila kumtaarifu Bazan juu ya jambo hili. Atapeleka taarifa kuhusu jambo hili kwa Khusro Perviz.”

Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Mimi nitafurahi sana kama mkimweleza juu ya jambo hili na vile vile mwambieni kwamba dini na mamlaka yangu vitazifikia nchi hizo ambazo farasi waendao mbio huzifikia na kama yeye akisilimu nitamwachia nchi hizo zilizo kwenye utawala wake hivi sasa.” Kisha ili kuwashawishi wale watu wawili waliotumwa na Bazan, Mtume (s.a.w.w.) aliwapa mkanda wa bei ghali uliotariziwa kwa dhahabu na fedha na ambao alipewa zawadi na machifu fulani wa makabila. Wote wawili walitosheka kabisa na wakamwacha na wakarejea Yaman. Walipofika kule walimweleza Bazan ule ujumbe wa Mtume (s.a.w.w.).

Bazan akasema: “Kama taarifa hizi ni sahihi, bila shaka yeye yu Mtume wa Allah kweli na hana budi kutiiwa.” Wakati ule ule alipokea barua kutoka kwa Shirviyah yenye maneno haya: “Fahamu ya kwamba nimemuua Khusro Perviz. Ghadhabu ya taifa imenifanya nimuue kwa sababu amewauwa watu watukufu (wa Uajemi-Iran) na kuwatawanya wazee. Mara tu uipatapo barua yangu huna budi kupata kiapo cha utii kwa ajili yangu kutoka kwa watu, na mpaka pale upatapo amri nyingine kutoka kwangu usiwe mkali kwa yule mtu adaiye kwamba yu Mtume na ambaye baba yangu alitoa amri dhidi yake.”

Ile barua ya Shirviyah ilitoa njia ya kusilimu kwa Bazan na watumishi wa serikali wote waliokuwa Wairan. Bazan alimwandikia barua Mtume (s.a.w.w.) na kumwarifu kuhusu kusilimu kwake pamoja na wale watumishi wa serikali.

Mjumbe Wa Uislamu Awasili Misrii

Misrii ilikuwa chanzo cha ustaarabu wa kale, makao makuu ya ufalme wa Mafarao (Mafirauni) na makao makuu ya serikali ya Wakibti (Madhehebu ya Kikristo ya KiMisrii). Tangu mwanzoni mwa Uislamu huko Hijaz, Misrii ilipoteza nguvu na uhuru wake. Maqauqis ameukubali ugavana wa Misrii kutoka kwa Mfalme wa Kirumi kwa kulipwa dinar milioni kumi na tisa kwa mwaka.

Hatib bin Abi Balta’ah alikuwa mpanda wanyama shujaa na mzoefu naye alihusika na tukio maarufu la historia ya Uislamu. Yeye alikuwa mmoja wa wale watu sita waliotumwa kuzipeleka zile barua za kimialiko za Mtume (s.a.w.w.) kwenda kwa watawala wa ulimwenguni. Mtume (s.a.w.w.) alimwamrisha kuipeleka barua ifuatayo kwa Maqauqis, Mtawala wa Misri: “Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehma, Rahimu. Hii ni barua itokayo kwa Muhammad bin Abdillah kwenda kwa Maqauqis mkuu wa Wakibti. Amani na iwe juu ya wafuasi wa ukweli. Ninakulingania kwenye dini ya Uislamu. Silimu ili usalimike (kutokana na ghadhabu ya Allah). Silimu ili Allah Mwenye Nguvu zote akulipe thawabu mbili. Na kama ukiugeuzia mbali uso wako kutoka kwenye Uislamu utawajibikiwa na dhambi za Wakibti pia.

“Enyi watu wa Kitabu! Tunakuiteni kwenye neno lililo sawa baina yetu, yaani tusimwabudu yeyote ila Allah. Tusimfanye yeyote kuwa mshirika wake. Baadhi yetu wasiwafanye wengine kuwa miungu wao. Na (ewe Muhammad) Watakapoikaidi dini ya kweli, sema: “Shuhudieni ya kwamba sisi ni Waislamu.”16

Yule balozi wa Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) aliondoka kwenda Misri na akapata taarifa ya kwamba wakati ule, yule mtawala alikuwa akiishi kwenye kasri ndefu mjini Alexandria, mji ulioko kwenye ukingo wa mto. Hivyo akaenda Alexandria na akaliingia jahazi.
Habib akapokewa kwenye baraza la kifalme, mfalme akaifungua ile barua na akayafikiria maneno yaliyokuwamo katika barua ile kwa kitambo fulani. Kisha akakiinua kichwa chake na kuzungumza na yule balozi wa Uislamu kwa maneno haya: “Kama kweli Muhammad yu Mtume wa Allah kwa nini wapinzani wake waliweza kumtoa kwenye sehemu aliyozaliwa na ni kwa nini alilazimika kuishi Madina? Kwa nini asiwalaani ili kwamba waangamizwe na Allah?”

Yule balozi wa Uislamu aliye mtu mwenye akili na mjuzi wa mambo, alijibu akasema: “Nabii Isa (a.s.) alikuwa ni Mtume wa Allah nawe pia wamtambua kuwa alikuwa hivyo. Basi kwa nini hakuwalaani wana wa Israeli walipopanga kumwua ili kwamba Allah angeliwaangamiza?”

Yule Mtawala ambaye hakulitegemea jibu la haraka kiasi kile alikubaliana na hoja za kimantiki zenye nguvu za yule balozi na akamsifu akisema: “Vizuri sana! Wewe ni mtu mwenye hekima na umeuleta ujumbe utokao kwa mtu mwenye hekima na elimu nyingi.17

Yule balozi alitiwa moyo na mapokezi mazuri aliyopewa na yule Mtawala wa Misri na kwa lengo la kutaka kumkaribisha asilimu, alisema hivi: “Kabla yako, mtu mmoja (Farao) aliitawala nchi hii; aliwatesa watu kwa muda mrefu. Allah alimwangamiza ili kwamba maisha yake yawe somo kwa ajili yako. Hata hivyo, lazima ujitahidi kwamba maisha yako kama yalivyokuwa yake yasije yakawa somo kwa wengine.

“Mtume wetu anawalingania watu kwenye dini safi. Waquraishi walifanya kampeni dhidi yake na Wayahudi nao walimpinga kwa chuki isiyo kifani. Watu walio karibu yake ni Wakristo. Ninaapa kwa uhai wangu kwamba kama vile Nabii Musa bin Imran alivyowatabiria watu juu ya Nabii Isa (a.s.) naye ameutabiri Utume wa Muhammad (s.a.w).

“Ninakulingania kwenye dini ya Uislamu na kitabu chetu kilichofunuliwa (Qur’ani) kama vile ulivyowaitia watu wa Taurati kwenye Injili. Kila taifa liusikiao mwito wa Mtume ni lazima limfuate. Na sasa kwa vile niishaufanya mwito huu wa Mtume (s.a.w.w.) kufika nchini mwako, inafaa kwamba wewe na watu wa taifa la Wa-Misri muifuate dini yake. Katu mimi sikuzuieni kuifuata dini ya Nabii Isa (a.s.). Ila tu ninakuambieni kwamba ifuateni dini yake lakini muelewe kwamba utaratibu uliokamilika wa dini ya Nabii Isa (a.s.) ni huu Uislamu wenyewe.”18

Mkutano wa yule balozi na mtawala wa Misri ulimalizika, lakini yule Maqauqis hakumpa jibu la mwisho. Hivyo ilikuwa muhimu kwamba Hatib asubiri kwa muda fulani zaidi ili apate jibu la kupeleka kwa Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.). Siku moja yule Maqauqis alimwita na akafanya mkutano naye katika sehemu ya faragha ya Kasri lake, na akamwuliza kuhusu mpango na dini ya Mtume (s.a.w.w.). Yule balozi akajibu akasema: “Yeye anawalingania watu kumwabudu Allah tu.

Anaamrisha kwamba watu wasali mara tano kwenye nyakati za mchana na usiku, na pia wafunge kwenye mwezi wa Ramadhani. Pia lazima wafanye Hijja kwenye Nyumba ya Allah na watimize ahadi zao, waambae kula mfu na kunywa damu . . .” Hatib aliyamalizia maneno yake kwa kuzieleza tabia tukufu za Mtume (s.a.w.w.).

Yule mtawala wa Misri akamwambia: “Hizi ni dalili za utume. Nilijua kwamba Nabii wa mwisho bado hajaja. Hata hivyo, nilikuwa nikidhania kwamba atatokea, lakini si katika Hijaz bali nchini Shamu, nchi iliyokuwa kitovu cha kutokea kwa Mitume. Lakini, ewe balozi wa Muhammad! Huna budi kutambua kwamba kama nikisilimu Wakibti hawatashirikiana nami. Ninategemea kwamba mamlaka ya Mtume huyu yatapanuka hadi yafike Misri na masahaba zake watakuja nchini mwetu na kupata ushindi juu ya majeshi ya nchi hii na juu ya itikadi za uwongo. Na ninapendelea kwamba uyafanye mazungumzo haya kuwa siri na asiyajue Mkibti yeyote.”19

Maqauqis Amwandikia Barua Mtume (S.A.W.W)

Yule mtawala wa Misri alimwita katibu wake wa Kiarabu na kumwamrisha aandike barua iendayo kwa Mtume (s.a.w.w) kama ifuatavyo: “Hii ni barua iendayo kwa Muhammad bin Abdullah, itokayo kwa Maqauqis chifu wa Wakibti. Amani na iwe juu yako! Nimeisoma barua yako, nimeyaelewa yaliyomo humo na kuutambua ukweli wa mwito wako.

Nilijua kwamba atatokea Mtume, lakini nilifikiria kwamba atainukia katika nchi ya Shamu. Nimekukaribisha kuwasili kwa balozi wako.”

Kisha kwenye barua ile anazitaja zawadi alizompelekea Mtume (s.a.w.w.) na akaishilizia barua ile kwa maneno: “Amani naiwe juu yako.”

Heshima aliyoionyesha yule Maqauqis kwa Mtume (s.a.w.w.) kwenye barua yake na kwa kuandika jina la Muhammad mwanzoni, na zile zawadi za thamani alizompelekea Mtume (s.a.w.w.) na yale makaribisho aliyompa yule balozi wake, vyaonyesha kwamba aliukubali mwito wa Mtume (s.a.w.w.) kwa siri lakini kwa kukipenda kwake cheo chake cha utawala, kulimzuia kuidhihirisha imani yake.

Kutoka Misri, Hatib alifika Shamu akiwa chini ya ulinzi wa kikundi cha watu walioteuliwa na Maqauqis. Hapo Shamu aliwaruhusu watu wale warejee na yeye akaendelea na safari kurudi Madina pamoja na msafara. Akaifikisha ile barua ya Maqauqis kwa Mtume (s.a.w.w.) na vile vile akaufikisha ujumbe wake. Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Hakusilimu kutokana na woga kwa ajili ya utawala wake, lakini utawala wake na mamlaka vitamalizika hivi karibuni.”

Balozi Wa Uislamu Aingia Ethiopia

Ethiopia iko kwenye ncha ya mwisho ya Afrika ya Mashariki. Eneo lake ni kilometa za mraba 18,000 na mji wake mkuu wa siku hizi ni mji wa Adis Ababa. Watu wa nchi za Mashariki walifika nchini humu kwa zaidi ya karne nzima kabla ya Uislamu.

Kufika kwao huku kulianzia na mashambulizi ya jeshi la Kiirani kwenye zama za Utawala wa Anushirw?n na ukafikia ukubwa wake kwa kuhamia humo wale Waislamu waliotoka Makka kuja Ethiopia.

Wakati Mtume (s.a.w.w.) alipoamua kuwatuma wajumbe sita wenye sifa nzuri na mashujaa kwenye sehemu za mbali kuwa mabalozi kwa ajili ya kuubalighisha utume wake wa ulimwengu mzima ili ufahamike kwa watu wa ulimwenguni kote, alimteuwa ‘Amr bin Umayyah kwenda Ethiopia pamoja na barua yake na kuupeleka ujumbe wake kwa Negus, mtawala mwadilifu wa nchi ile. Hii haikuwa barua ya kwanza ambayo Mtume (s.a.w.w.) alimwandikia yule Mtawala wa Ethiopia.

Hapo awali aliandika barua pia kuhusiana na Muhajiriin akimwomba Negus kuwahurumia. Maneno ya barua ile yamehifadhiwa katika historia.20 Wakati mwingine hutokea kuchanganyikiwa baina ya hizi barua mbili (yaani baina ya ile ya kuwatambulisha wale Muhajiriin kwa Negus, na ile ya Mtume (s.a.w.w.) kuubalighisha utume wake kwa ulimwengu mzima), na maneno ya barua zote hizi yamechanganyika.

Pale Mtume (s.a.w.w.) alipompeleka balozi wake kule Ethiopia akiwa na barua, baadhi ya wahajiri wa Kiislamu walikuwa bado wakiishi pale, ambapo wengine walikuwa tayari wamesharejea na kuishi Madina, nao walikuwa wameusifu uadilifu wa yule mtawala mkuu wa nchi ile na huruma zake kwa raia zake. Hivyo basi, kama tukiona aina fulani ya mwelekeo, huruma, na upole kwenye maneno ya barua aliyoandika Mtume (s.a.w), akimwandikia mtawala yule, ni kwa sababu alizitambua fikira za Negus.
Katika barua alizowaandikia watawala wengine aliwaonya kuhusiana na wakati wa ghadhabu ya Allah na akawaambia kwamba kama hawatasilimu, basi dhambi za wale watakaoacha kusilimu kutokana na hofu vilevile zitaandikwa kwenye hesabu zao. Hata hivyo, hakuna jambo la aina hii lililosemwa kwenye barua ifuatayo, aliyoandikiwa Negus: “Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehema, Rahim. Hii ni barua itokayo kwa Muhammad Mjumbe wa Allah kwenda kwa Negus Mfalme wa Ethiopia. Amani na iwe juu yako. Ninamhimidi Allah ambaye hakuna mungu ghairi Yake. Yeye ndiye Allah aliyetakasika kutokana na kila aina ya upungufu na makosa; salama kutokana na ghadhabu Yake. Anaona na kuishuhudia hali ya waja wake.

“Ninashuhudia ya kwamba Nabii Isa Bin Maryam ni roho ya Allah na ‘neno’ (la Allah) lililokaa kwenye tumbo la uzazi la Maryam mchamungu, Allah alimuumba kwenye tumbo la uzazi la mama yake bila ya baba kwa Nguvu ile ile aliyomuumbia Adamu bila ya wazazi.

“Ninakuita kwa Allah Aliye Mmoja tu, Asiye na mshirika, na ninakutaka umtii na kuifuata dini yangu. Mwamini Allah aliyeniteuwa kuishika kazi ya utume. Mfalme wa Ethiopia, huna budi kutambua kwamba mimi ni Mtume wa Allah. Ninakuita wewe na askari zako kwa Allah, Mwenye nguvu zote, kwa kuileta barua hii na balozi wangu nitakuwa nimeshalitekeleza jukumu langu zito lililonikalia, na nimekushauri. Amani na iwe juu ya wale waufuatao mwongozo.”21

Mtume (s.a.w.w.) aliianza barua hii kwa ile salamu ya Kiislamu ya Salaamu Alayk na kutuma salaam zake binafsi kwa yule Mfalme wa Ethiopia. Hata hivyo, katika barua nyingine (zilizopelekwa kwa Kisra – Mtawala wa Iran, Kaisari-Mtawala wa Urumi na Maqauqis – mtawala wa Misri) anaanza na salaam ya ujumla (Amani naiwe juu ya wafuasi wa mwongozo). Katika barua hii alipeleka salamu za mtu binafsi kwa mtawala wa Ethiopia na hivyo akampa ubora juu ya wale watawala wengine wa ulimwenguni, katika zama zile.

Katika barua hii zimetajwa baadhi ya sifa kuu za Allah, Mwenye nguvu zote zionyeshazo Upweke na Ukuu wake. Baada ya hapo Mtume (s.a.w.w.) analizungumzia suala la ‘Uungu’ (Nabii Isa kuwa mungu), jambo ambalo ni uzushi wa fikara zilizooza za kanisa, na anaukanusha uzushi huu kwa hoja zinazotajwa kwenye Qur’ani. Ama kuhusu Nabii Isa kuzaliwa bila ya baba, analieleza tukio hili kwa kufanya ulinganisho na kuzaliwa kwa Adamu na akathibitisha kwamba kama kuzaliwa bila ya baba kutakuwa ni hoja ya mtu kuwa mwana wa Mungu, hoja hiyo hiyo haina budi kutumika kwa ajili ya Adamu, ambalo Wakristo hawana itikadi ya aina hiyo juu yake. Mwishoni mwa barua ile anatoa ushauri kumpa yeye (Negus) na kwa njia hiyo anakidhihirisha cheo chake mwenyewe.

Mazungumzo Baina Ya Yule Balozi Na Negus

Baada ya kwisha kwa taratibu zilizokuwa muhimu yule balozi wa Uislamu alipokewa kwenye baraza la kifalme la yule Mtawala wa Ethiopia. Alizungumza na mtawala yule hivi: “Ni wajibu wangu kuuwasilisha ujumbe wa Mtume (s.a.w.w.) kwako, na tabia zako zilizo safi nazo zahitaji kwamba uusikilize uwasilishaji wangu.

Ewe Mtawala mwadilifu wa Ethiopia! Huruma zako kwa wahajiri wa Kiislamu haziwezi kusahauliwa na hisia zako hizi zimetufurahisha mno kwamba tunakuhesabu kuwa u mmoja wetu. Nasi tunayo imani juu yako, kama kwamba sisi ni marafiki zako. Kitabu chako cha mbinguni ni ushahidi thabiti na usiokatalika. Kitabu hiki ni mwamuzi bora zaidi asiyefanya dhulma na huyu ni hakimu mwadilifu, anaushuhudia utume wa Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.). Kama ukimfuata huyu Mtume wa ulimwengu mzima na Mtume wa Mwisho wa Allah, utaipata baraka kubwa; au sivyo, utakuwa kama Wayahudi walioikataa dini ya Nabii Isa iliyoitangua dini ya Nabii Musa (a.s.) na wakaendelea kuifuata ile dini iliyotanguliwa. Na dini ya Uislamu inazitangua dini za awali kama vile dini ya Nabii Isa na kwa maana nyingine kwamba inazitimiza.”

Yule Mtawala wa Ethiopia alimjibu yule balozi wa Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) kwa maneno haya: “Ninamshuhudia ya kwamba yeye ndiye yule Nabii angojewaye na watu wa Kitabu na ninaamini ya kwamba, kama vile Nabii Musa alivyowaarifu watu kuhusu utume wa Isa, Nabii Isa naye alizieleza dalili za Mtume wa Mwisho. Mimi niko tayari kuutangaza utume wake mbele ya hadhara. Hata hivyo, kwa kuwa bado mazingira hayajakuwa tayari kwa tangazo hili, na vilevile nguvu zangu hazitoshelezi, ni muhimu kwamba uwanja uhitajikao hauna budi kutayarishwa ili kwamba nyoyo za watu zitumiwe kwenye Uislamu.

Kama ingaliwezekana kwangu Mimi ningaliharakisha kumfikia huyo Mtume wenu mara moja.”22 Kisha aliandika barua ya kumjulisha Mtume (s.a.w.w.).

Negus Amwandikia Barua Mtume (S.A.W.W)

“Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehema, Rahimu. “Hii ni barua iendayo kwa Muhammad, Mtume wa Allah kutoka kwa Negus. Baraka ya yule Mmoja ambaye hakuna mungu ila Yeye tu na Salaam za yule mmoja Aliyeniongoza kwenye Uislamu ziwe juu yako. Nimeisoma barua yako ihusianayo na Utume na sifa za kibinadamu za nabii Isa (a.s.). Ninaapa kwa jina la Mola wa Mbingu na ardhi kwamba kila ulilolisema ni sawa kabisa nami sina tofauti kuhusiana na itikadi hii japo iliyo ndogo. Vilevile nimeutambua ukweli wa dini yako nami nimewapa wahajiri Waislamu huduma zifaazo. Kwa njia ya barua hii ninashuhudia ya kwamba wewe ni Mtume wa Allah na mtu mkweli ambaye utume wake umethibitishwa na Vitabu vya mbinguni. Nimekwisha kuzitekeleza ibada za Kiislamu na kula kiapo cha utii kwako mbele ya binamu yako (Ja’far bin Abu Twalib).

“Ninamtuma mwanangu R?rh? mbele ya hadhara yako tukufu ili aufikishe ujumbe wangu na kusilimu kwangu. Nami ninasema dhahiri kwamba mimi siwajibikiwi na yeyote ila mimi mwenyewe. Hivyo basi, kama ukiniamuru nitafika mbele yako. Amani na iwe juu yako, Ewe Mtume wa Allah.”23

Barua Za Mtume (S.A.W.W) Kwa Watawala Wa Shamu Na Yamamah

Inawezekana kwamba kupanuka kwa matangazo ya Uislamu aliyoyafanya Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) kwa watawala mbalimbali kukafikiriwa na baadhi ya wanasiasa wa zama zile kuwa ni kitu kilicho kinyume na upole. Hata hivyo, jinsi muda upitavyo, imethibitika kwamba Mtume (s.a.w.w.) hakuwa na njia nyingine ya kufanya.

Kwanza, kule kuwapeleka wale mabalozi sita kwenye sehemu mbalimbali za ulimmwengu na pia wakiwa na barua thabiti na zenye kuvutia kuliifunga njia ya shaka kwa wapinzani wa siku zijazo. Baada ya Mtume (s.a.w.w.) kukitenda kitendo hiki kikuu, siku hizi hakuna yeyote awezaye kutia shaka juu ya mwito wake huu kuwa wa ulimwengu mzima. Aidha, ukiziachilia mbali zile aya zilizoshushwa juu ya jambo hili, kule kuwapeleka wale mabalozi ni uthibitisho mkubwa wa Uislamu kuwa dini ya ulimwengu mzima.

Pili, watawala wa zama zile ukimwachilia mbali Khusro Perviz aliyekuwa mtu mwenye kiburi na dhalimu, kwa ujumla walivutiwa na mwito ule na zile barua. Walionyesha kuwaheshimu wale wawakilishi wa Mtume (s.a.w.w.), na kule kutokea kwa Nabii wa Kiarabu kukawa jambo la kujadiliwa kwenye uwanja wa dini. Barua hizi ziliwaamsha wale waliokuwa wamelala, ziliwapa mshtuko mkali wale watu wasiosikiliza na kuzikoroga mno akili za mataifa yaliyostaarabika ili kwamba waweze tena kufanya mijadala na utafiti juu ya yule Nabii aliyeahidiwa wa Taurati na Injili, na wakuu wa dini wa wakati ule waweze kujua hii dini mpya kwa njia mbalimbali.
Kwa sababu hii, wengi wa viongozi wa dini mbalimbali za zama zile walikuja Madina, katika siku za mwishoni mwa uhai wa Mtume (s.a.w) na hata baada ya kufariki kwake dunia na wakajifunza dini hii kwa karibu zaidi.

Katika sura zilizotangulia tumeeleza kwa kirefu taswira zilizotolewa na zile barua za Mtume (s.a.w.w.) kwa watawala wa Urumi, Iran na Misri. Sasa tumeshayaona matokeo ya barua yake kwa Negus.

Baada ya mwakilishi wa Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) kumpa Negus zile zawadi ili awape wakuu wa dini wa Ethiopia, aliwapeleka makasisi thelathini wenye maarifa mengi mjini Madina ili waweze kujifunza maisha yaliyo rahisi na ya uchamungu ya Mtume (s.a.w.w.) kwa karibu zaidi, na ili wasije wakadhania kwamba yeye naye (s.a.w.w.) alikuwa na madaraka kama ya wafalme wa zama zile.

Wale watu waliotumwa na yule Mfalme wa Ethiopia walikutana na Mtume (s.a.w.w.) na wakamwuliza kuhusu itikadi yake juu ya Nabii Isa (a.s.).

Mtume (s.a.w.w.) aliwaeleza itikadi yake juu ya Nabii Isa (a.s.) kwa kuisoma Aya ifuatayo:

إِذْ قَالَ اللَّهُ يَا عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ اذْكُرْ نِعْمَتِي عَلَيْكَ وَعَلَىٰ وَالِدَتِكَ إِذْ أَيَّدْتُكَ بِرُوحِ الْقُدُسِ تُكَلِّمُ النَّاسَ فِي الْمَهْدِ وَكَهْلًا ۖ وَإِذْ عَلَّمْتُكَ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَالتَّوْرَاةَ وَالْإِنْجِيلَ ۖ وَإِذْ تَخْلُقُ مِنَ الطِّينِ كَهَيْئَةِ الطَّيْرِ بِإِذْنِي فَتَنْفُخُ فِيهَا فَتَكُونُ طَيْرًا بِإِذْنِي ۖ وَتُبْرِئُ الْأَكْمَهَ وَالْأَبْرَصَ بِإِذْنِي ۖ وَإِذْ تُخْرِجُ الْمَوْتَىٰ بِإِذْنِي ۖ وَإِذْ كَفَفْتُ بَنِي إِسْرَائِيلَ عَنْكَ إِذْ جِئْتَهُمْ بِالْبَيِّنَاتِ فَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْهُمْ إِنْ هَٰذَا إِلَّا سِحْرٌ مُبِينٌ {110}

“Allah Atakaposema: Ewe Isa mwana wa Mariam! Kumbuka neema Yangu juu yako na juu ya mama yako, pale nilipokutia nguvu kwa Roho Takatifu, ukazungumza na watu katika utoto na utu uzima. Na nilivyokufunza kuandika na hekima na Taurati na Injili. Na ulipofinyanga udongo mfano wa umbo la ndege, kwa idhini Yangu, kisha ukapuliza ndani yake, mara akawa ndege kwa idhini Yangu, na ulipowaponyesha vipofu na wakoma kwa idhini Yangu, na ulipowafufua wafu kwa idhini Yangu na nilipokukinga na wana wa Israeli ulipowajia na hoja zilizo wazi, na wakasema waliokufuru miongoni mwao: Haya si lolote ila ni uchawi mtupu.” (Surat al- Ma’ida, 5:110).

Maneno ya Aya tuliyoinukuu hapo juu yaliwatia wasiwasi mno kiasi kwamba walianza kutiririkwa na machozi machoni mwao bila ya kupenda. Watu hawa walioteuliwa na Negus wakarejea Ethiopia baada ya kujifunza kwa makini ule mwito wa Mtume (s.a.w.w.) na kumweleza mfalme yale waliyoyaona na kuyasikia. Yeye naye alijawa na machozi machoni mwake kama wale makasisi.24

Ibn Athir ameisimulia hadith ya wale makasisi waliotumwa na Negus kwa jinsi nyingine. Anasema: “Makasisi wote hawa walikufa maji baharini na Mtume (s.a.w.w.) alimpelekea mfalme barua ya rambirambi.” Hata hivyo, maneno ya barua aliyoizungumzia haionyeshi hata kidogo kwamba Negus alipatwa na msiba wowote wa aina hiyo.25

Barua Ya Mtume (S.A.W.W) Kwa Mwana Wa Mfalme Wa Waghassaani

Waghassani walikuwa ni familia ya kabila la Qaht?ni liitwalo Azd lililokuwa likiishi nchini Yeman kwa muda mrefu, na mashamba yao yalikuwa yakinyweshewa na bwawa la Ma’rib. Bwawa hili lilipoharibiwa walilazimika kuitoka sehemu ile na kuja Shamu. Nguvu na ushawishi wao uliufunika ule wa wenyeji na hatimaye walianzisha Dola iliyoitwa Ghass?niyah. Walitawala kwenye eneo hili chini ya ufalme wa Wafalme wa Urumi, na Uislamu ulipouvunja utaratibu wao, watu thelathini na wawili kutoka miongoni mwao walikuwa wametawala katika sehemu za Golan, Yarmuk na Dameski.
Miongoni mwa wale mabalozi sita waliopelekwa kwenye nchi kubwa kuubalighisha ujumbe wa utume huu wa ulimwengu mzima, wa tano wao alikuwa ni Shujaa’ bin Wahab, aliyekwenda kwenye Dola ya Ghass?niyah kuipeleka barua ya Mtume (s.a.w.w.) kwa mfalme wao, aliyeitwa Harith bin Abi Shamir mjini Ba’uzah. Yule balozi alipoingia nchi ya Harith alitambua ya kwamba yule mtawala alikuwa akijishughulisha na matayarisho ya mapokezi ya Kaisari aliyekuwa akija kutoka Constantinople kwenda Yerusalem kwa miguuu ikiwa ni ishara ya shukrani kwa kupata ushindi dhidi ya adui yake, Iran.

Katika ile hali Shujaa’ bin Wahab ilimbidi asubiri kwa muda fulani kabla ya kupata muda wa kuweza kukutana na yule mtawala. Kupatikana kwa wakati ule kulimsaidia kujenga alijenga urafiki na H?jib (Mkuu wa maazimisho), naye akamwarifu juu ya sifa za Mtume (s.a.w.w.) na juu ya Uislamu. Maneno yenye kuvutia na kupenya moyoni yalileta mabadiliko yasiyo kifani katika fikara za yule H?jib kiasi kwamba alianza kutiririkwa na machozi machoni mwake na kusema: “Nimejifunza Injili kwa makini na humo nimezisoma sifa za Mtume nami basi natamka dhahiri kwamba mimi ninamwamini. Hata hivyo, ninamwogopa Harith kwamba asije akaniuwa. Na Harith naye anamwogopa Kaisari na hata kama akiyaamini maneno yako, hataweza kuitangaza imani yake, kwa sababu yeye pamoja na jadi wa familia hii wamekuwa vibaraka wa Kaisari.”

Shujaa’ alipopata nafasi ya kufika barazani kwa mtawala alimwona akiwa ameketi kwenye kiti cha enzi na kuvaa taji. Akaitoa ile barua ya Mtume (s.a.w.w.). Barua ile iliandikwa hivi: “Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehema, Rahimu. “Hii ni barua itokayo kwa Muhammad Mtume wa Allah kwenda kwa Harith bin Shamir. Amani na iwe juu ya wafuasi wa ukweli na viongozi wa waumini wa kweli. Ewe Harith! Ninakuitia kwa Allah Aliye Mmoja tu, Asiye na mshirika. Kama ukisilimu dola yako itaendelea kuwapo.”

Maneno yaliyoko mwishoni mwa barua ile yaliyotishia kuangamia kwa ufalame wake kutokana na kushindwa kwake kuamini (Upweke wa Allah na utume wa Mtume s.a.w.w) yalimuudhi Harith naye akasema: “Hakuna awezaye kuniondolea mamlaka yangu. Ni lazima mimkamate huyu Mtume anayeamka.” Kisha ili kumvutia yule balozi aliamrisha kwamba jeshi lifanye gwaride mbele yake ili kwamba yule balozi wa Mtume (s.a.w.w.) aweze kuiona nguvu yake ya kijeshi kwa karibu zadi.

Kwa njia ya kutoa huduma iliyozidi kiasi chake kwa serikali ya Kirumi yeye naye alimwandikia barua Kaisari na akimweleza uamuzi wake wa kutaka kumkamata Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.). Kwa bahati, barua hii ilimfikia Kaisari wakati Dihyah Kalbi, yule balozi mwingine wa Mtume (s.a.w.w.) alipokuwa kwenye baraza la Kaisari na yule mtawala wa Kirumi alipokuwa akifikiria juu ya Uislamu. Yule Kaisari alikasirishwa na ile shauku kuu ya yule Mtawala wa Kighass?ni na akamjibu kwa kumwandikia hivi: “Achana na wazo lako hilo, na tuonane mjini Ailyaa.”

Hata hivyo, kufuatana na methali isemayo: “Watu huifuata njia ya mtawala wao” jibu la Kaisari liliubadilisha msimamo wa Harith na hivyo akampa yule balozi wa Mtume (s.a.w.w.) joho la heshima, na kabla ya kuondoka na kurejea Madina alimwambia: “Nitolee salaam zangu kwa Mtume wa Uislamu na mwambie kwamba mimi ni mmoja wa wafuasi wake halisi.” Hata hivyo, Mtume (s.a.w.w.) hakulipa muhimu wowote lile jibu lake la kidiplomasia, na akasema: “Hivi karibuni mamlaka yake yataporomoka.” Harith alifariki dunia kwenye mwaka wa 8 Hijiriya yaani mwaka mmoja tu baada ya tukio hili.26

Balozi Wa Sita Wa Mtume (S.A.W.W) Aenda Yamamah

Yule balozi wa sita wa Mtume (s.a.w.w.) alikwenda Yamamah, nchi iliyokuwako baina ya Najd na Bahrain, na hatimaye kuifikisha barua yake kwa mtawala wa sehemu ile aliyeitwa Hamza bin Ali Hanaf. Maneno ya barua ya Mtume yalikuwa haya yafuatayo:
“Kwa jina la Allah. Amani na iwe juu ya wafuasi wa mwongozo. Huna budi kutambua kwamba dini yangu itaenda Mashariki na Magharibi hadi kwenye pembe ya mbali zaidi ya dunia. Silimu ili kwamba ubakie kuwa salama na mamlaka na ufalme wako viendelee kuwako.”

Kwa vile yule mtawala wa Yamamah alikuwa Mkristo, balozi aliyeteuliwa kwa sehemu ile alikuwa ni mtu aliyepata kuishi nchini Ethiopia kwa muda mrefu naye alikuwa na ujuzi kamili juu ya hoja na ibada za Ukristo. Mtu huyu alikuwa ni Salit bin ‘Amr ambaye alihajiri Ethiopia chini ya amri ya Mtume (s.a.w.w.) wakati Waislamu walipokuwa wakiteswa vikali na waabudu masanamu wa Makka.

Mafundisho matukufu ya Uislamu na mawasiliano yake na watu wa matabaka mbalimbali katika safari zake vimemfanya kuwa shujaa na mwenye nguvu mno kiasi kwamba alimvutia yule mtawala wa Yamamah kwa maneno yake na akamwambia: “Yu mwenye kuheshimiwa yule aliyebarikiwa imani na uchamungu. Watu walioko chini ya uongozi wako katu hawatashindwa. Ninakuita kwenye kitu kilicho bora zaidi na ninakuzuia kutokana na matendo yaliyo maovu zaidi. Ninakuitia kwenye kumuabudu Allah na ninakuzuia kutokana na kumtii shetani na kuyafuata majaribu na tamaa mbaya. Matokeo ya kumwabudu Allah ni kuipata Pepo na yale ya kumfuata shetani ni kutiwa kwenye Moto (wa Jahanamu). Kama ukitenda kinyume na nilivyosema, basi huna budi kusubiri hadi ukweli ukudhihirikie.”

Uso wa yule Mtawala wa Yamamah ulionyesha kwamba maneno ya yule balozi yamejenga mvuto mwema akilini mwake. Aliomba muda wa kuufikiria ule utume wa Mtume (s.a.w.w.). Kwa bahati njema mmoja wa Maaskofu wakuu wa Urumi alipata kufika nchi ya Yamamah katika wakati ule naye yule mtawala wa Yamamah akalipeleka suala lile mbele yake. Yule Askofu akasema: “Kwa nini umeacha kumtambua?” Akajibu: “Ninachelea ufalme wangu na mamlaka yangu.” Yule Askofu akasema: “Ni bora kwako kumfuata huyo ndiye yule Nabii wa Kiarabu ambaye kuja kwake kumetabiriwa na Kristo na imeandikwa kwenye Injili kwamba Muhammad yu Mtume wa Allah.”

Ushauri alioutoa yule Askofu ulimshawishi yule mtawala. Alimwita yule balozi aichukue barua itokayo kwake na ampelekee Mtume (s.a.w.w.). Barua ile ilisema hivi: “Umeniita kwenye dini iliyo bora zaidi.

Mimi ni mshairi mzungumzaji fasaha na msemaji wa jumuiya yangu, nami ninacho cheo miongoni mwa Waarabu chenye kutambuliwa na watu wote. Mimi niko tayari kuifuata dini yako, kwa sharti la kwamba unaniruhusu nipate fungu katika vyeo vya juu vya kidini.”

Hakutosheka na hilo tu bali vilevile alituma ujumbe wake kwenda mjini Madina ukiongozwa na mtu aliyeitwa Muj?’ah bin Murarah ili waweze kuufikisha ujumbe wake kwa Mtume (s.a.w.w.) na kumwambia kwamba iwapo cheo hiki cha kidini atakishika yeye baada ya kufariki dunia kwa Mtume (s.a.w.w.), yuko tayari kusilimu na kumsaidia, bali iwapo sivyo hivyo, atapigana vita. Wajumbe wa ujumbe huu walifika mbele ya Mtume (s.a.w.w.) na wakasilimu bila ya masharti. Ama kuhusu yule mtawala wa Yamamah, alijibu ujumbe wake kwa kusema hivi: “Kama imani yake ina masharti, haifai kwa utawala na kuirithi nafasi yangu, na Allah Atanilinda kutokana na madhara yake.”27

Barua Nyingine Za Mtume Wa Uislamu (S.A.W.W)

Barua alizoziandika Mtume (s.a.w.w.) akiwaita wana wa wafalme, wafalme, na wakuu wa dini kwenye Uislamu ni nyingi kuliko hizi tulizozitaj hapo juu. Hata katika siku zetu hizi wanachuoni watafiti wamenukuu vitabuni mwao barua ishirini na tisa za miito aliyoipeleka. Hata hivyo, kwa ajili ya kupunguza ukubwa wa kitabu hiki, tutatosheka na hizi tulizozitaja hapo juu.

 • 1. Wanachuoni wakuu wa Uislamu wamezikusanya hizi barua za Mtume (s.a.w.w.) kwa kadiri walivyoweza. Vitabu viwili vifuatavyo ni vyenye thamani mno juu ya jambo hili:
  Al-Wasaa’iqus Siyasah’ cha Profesa Muhammad hamidullah Hyderabadi, Profesa wa chuo Kikuu cha Paris.
  Makaatibur Rasul’ cha mwanachuoni wa zama zilezile, Ali Ahmadi.
 • 2. Tabaqaatul-Kubra, Juz. 1, uk. 258; Siiratu Halabi, Juz. 3, uk. 271.
 • 3. Busra yalikuwa ni makao makuu ya Gavana wa jimbo la Haraam. Jimbo hili lilihesabiwa kuwa ni koloni la Kaisari na Harith bin Abi Shimar na watawala wa familia ya Waghassaani walilitawala jimbo hili wakiwa ni vibaraka wa Kaisari.
 • 4. Tabaqaatul- Kubra, Juz. 1, uk. 259.
 • 5. Kuna tofauti ya maoni baina ya wanachuoni kuhusu maana ya neno lihi ‘Waarisiyani’ Ibn Athiir anaandika kwenye kitabu chake ‘Nihayah,’ Juz. 1, uk. 31. ‘Lina maana ya wafanyakazi wa baraza la mfalme’. Wengine wanasema kwamba lina maana ya wakulima, kwa sababu katika siku zile watu wengi walikuwa wakulima. Maoni haya yanaungwa mkono na ukweli uliopo kwamba kwenye baadhi ya nakala za barua (Tarikhul-Kamil, Jz. 2, uk. 145) neno ‘Akaarin’ limetu- mika badala ya neno hilo hapo juu, na ‘Akar’ lina maana ya mkulima. Vile vile inafikiriwa kwamba pengine ‘Aris’ lilikuwa jina la jumuiya iliyokuwa ikiishi kati- ka Dola ya Kirumi.
 • 6. Tarikhut-Tabari, Juz. 2, uk. 290; Bihaarul-Anwwar, Juz. 20, uk. 378-380.
 • 7. Tabaqaatul-Kubra, Juz. 1, uk. 259; Siiratu Halabi, Juz. 2, uk. 277; Tarikhul- Kamil, Juz. 2, uk. 44; Bihaarul Anwwar, Juz. 20, uk. 379.
 • 8. Kufuatana na Ibn Sa’ad (Tabaqaatul- Kubra, Juz. 1, uk. 258) Mtume (s.a.w.w.) alimpeleka balozi huyu katika mwezi wa Muharam, Mwaka wa 7, Hijiriya.
 • 9. Tabaqaatul-Kubra, Juz. 1, uk. 360; Tarikhut-Tabari, Juz. 2, uk. 295 na 296; Tarikhul-Kamil, Juz. 2, uk. 81 na Bihaarul Anwwar, Juz. 20, uk. 389.
 • 10. Tarikhul-Kubra, Juz. 1, uk. 260.
 • 11. Tarikhu Ya’qubi, Juz. 2, uk. 62.
 • 12. Musnadi Ahmad, Juz. 1, uk. 96.
 • 13. Siiratu Halabi, Jz. 3, uk. 278.
 • 14. Tarikhul-Kamil, Juz. 2, uk. 106.
 • 15. Tabaqaatul-Kubra, Juz. 1, uk. 260; Bihaarul-Anwwar, Juz. 20, uk. 382.
 • 16. Siiratu Halabi, Juz. 3, uk. 280; Durrul-Mantur, Juz. 1, uk. 40 na A’ayaanis- Shi’ah, Juz. 1, uk. 142.
 • 17. Usudul Ghaba, Jz. 1, uk. 362.
 • 18. Siiratu Halabi, Juz. 3, uk. 28.
 • 19. Siiratuz-Zayni Dehlaan, Juz. 3, uk. 73.
 • 20. Tarikhut-Tabari, Juz. 2, uk. 294.
 • 21. Siiratu Halabi, Juz. 3, uk. 279; Tabaqaatul-Kubra, Juz. 1, uk. 259.
 • 22. Siiratu Halabi,
 • 23. Tarikhut-Tabari, Juz. 1; Bihaarul Anwwar, Juz. 20, uk. 392.
 • 24. A’alamal Waraa, uk. 31.
 • 25. Usudul Ghaba, Juz. 2, uk. 62.
 • 26. Siiratu Halabi, Juz. 3, uk. 286; Tabaqaati, Juz. 1, uk. 261.
 • 27. Tarikhul- Kamil, Juz. 2, uk. 83; Tabaqaat Kubra, Juz. 1, uk. 262.