Sura Ya 43: Ngome Ya Khaybar: Kitovu Cha Hatari

Kuanzia siku ile ambapo Uislamu ulianza kubalingiwa mjini Madina, Wayahudi walianza kuwa maadui dhidi ya Mtume (s.a.w.w.) na Waislamu hata zaidi ya Waquraishi, na wakaamka na makri na nguvu zao zote kuiangamiza dini hii.

Wayahudi waliokuwa wakiishi mjini Madina penyewe au viungani mwake walikutwa na balaa walilolistahili kutokana na matendo yao yenye madhara. Kikundi chao kimoja kilinyongwa, na wengineo kama vile kabila la Bani Qaynaqaa’ na Bani Nuzayr walipelekwa uhamishoni kutoka mjini Madina, na wakaenda kuishi Khaybar na Wadud Qaraa’.

Wanda mpana na wenye rutuba ulioko Kaskazini mwa mji wa Madina yapata masafa ya kilomita 134 unaitwa Bonde la Khaybar, kabla ya kuanza kwa utume Wayahudi walijenga hapo ngome saba madhubuti kwa ajili ya upinzani na usalama wao. Kwa kuwa sehemu hii ilifaa sana kwa malengo ya kilimo, wakazi wake walikuwa na ujuzi kamili juu ya mambo yahusianayo na kilimo, kujikusanyia utajiri, kujikusanyia silaha na misingi ya ulinzi. Idadi ya wakazi wake ilizidi elfu ishirini na watu wengi walio mashujaa na wapenda vita waliweza kuonekana miongoni mwao.1

Kosa kubwa walilotenda Wayahudi wa Khaybar ilikuwa kwamba waliyachochea makabila yote ya Kiarabu kuivunja Dola ya Kiislamu, na kwa msaada wao wa kifedha jeshi la ushirikina lilikuja kutoka sehemu mbalimbali za Uarabuni hadi kwenye kuta za Madina. Matokeo ya kitendo hiki vita vya Ahz?b vikatokea (ambavyo maelezo yake kwa kirefu tuishayaeleza). Hatua alizozichukua Mtume (s.a.w.w.) na kujitolea mhanga kwa masahaba zake vilifanya lile jeshi la washambuliaji pamoja na Wayahudi wa Khaybar kurudi nyumbani kwao baada ya kukaa kwenye upande wa pili wa handaki lile kwa kipindi cha mwezi mzima, na hapo amani na utulivu vilirudishwa tena kwenye yale makao makuu ya Uislamu.

Mchezo mbaya uliochezwa na Wayahudi ambao hapo awali waliheshimiwa na Waislamu ulimfanya Mtume (s.a.w.w.) kuamua kukiharibu hiki kituo kikuu cha hatari na kuwanyang’anya silaha wote, kwa sababu halikuwa jambo lililowezekana kwamba watu hawa wakaidi na hatari waendelee kuwepo hapo Khaybar, kwani wangeweza tena kutumia fedha nyingi katika kuwachochea Waarabu waabudu masanamu kuasi dhidi ya Waislamu, na hadithi ya vita vya Ahzaab ingelirudiwa tena, kwa kuwa utovu wao wa uvumilivu katika mambo ya dini uliizidi mno ile huba ya Waquraishi juu ya ibada ya masanamu, na ni kwa sababu ya imani hii potofu kwamba wakati maelfu ya waabudu masanamu yakisilimu, hakuna hata Myahudi mmoja aliyeonyesha kuwako kwake tayari kuiacha dini yake.

Jambo jingine lililomfanya Mtume (s.a.w.w.) kuivunja nguvu ya Wayahudi wa Khaybar, kuwanyang’anya silaha, na kuwateua maafisa wake kuiangalia mienendo yao, ni kwamba alikuwa kaishawasiliana na wana wa wafalme, wafalme na watawala wa nchi mbalimbali za ulimwengu na amewalingania wote kwenye Uislamu kwa sauti thabiti, na katika hali hiyo halikuwa jambo lisilowezekana Wayahudi kuwa silaha iliyo mkononi mwa Kisra na Kaisari na hatimaye wangaliweza kulipiza kisasi kwa Waislamu kwa msaada wa hawa wafalme wawili, na hivyo kuvunjilia mbali hili vuguvugu la kiroho la Kiislamu, au kuwachochea hawa wafalme wawili waasi dhidi ya Waislamu, kama vile walivyowachochea waabudu masanamu hapo awali, kwa kuwa katika siku zile Wayahudi walisimama pamoja na wafalme hawa, mmoja au mwingine katika vita baina ya Iran na Rumi, na hivyo Mtume (s.a.w.w.) aliona kwamba ni muhimu kuukomesha uovu huu tangu mwanzoni kabisa.

Huu ulikuwa ndio wakati ufaao zaidi wa kuchukua hatua hii, kwa sababu baada ya kuyafanya yale mapatano ya Hudaybiah, Mtume (s.a.w.w.) alikuwa salama kutokana na kila aina ya wasiwasi kutoka kwenye upande wa Kusini (wa Waquraishi) na akatambua kwamba kama akikikamata chama cha Wayahudi, hawatapata msaada wowote kutoka kwa Waquraishi. Ama kuhusu kuyazuia makabila mengine ya upande wa Kaskazini (kama vile familia ya Ghatf?n waliokuwa washirikina na marafiki wa watu wa Khaybar kwenye Vita vya Ahzaab) kutokana na kuwasaidia Wayahudi, alikuwa na mpango fulani akilini mwake ambao tutauzungumzia baadae.
Akisukumwa na mambo haya, Mtume (s.a.w.w.) aliwaamrisha Waislamu kuwa tayari kuviteka vile vituo vya mwisho vya Wayahudi Bara Arabuni. Aliongeza kusema kwamba ni watu wale tu waliokuwepo wakati wa kufanya mapatano ya Hudaybiyah ndio waruhusiwao kushiriki kwenye vita hivi. Ulikuwa ni mmojawapo wa nyakati za kuhuzunisha kwa Uislam. Kuhusu wale wengine (wasiokuwepo Hudaybiyah) wanaweza kushiriki kama askari wa kujitolea lakini hawapasiki na mgao wowote katika ngawira.

Mtume (s.a.w.w.) alimteua Ghayla Laythi kuwa mwakilishi wake mjini Madina. Mtume (s.a.w.w.) alimpa Sayyidna Ali (a.s.) bendera nyeupe mkononi mwake na akawaamrisha Waislamu waanze safari. Na ili msafara ule uweze kufika kule uendako upesi iwezekanavyo, alimruhusu kiongozi wa ngamia wake aliyeitwa ‘Aamri bin Akwa’ kusoma beti hizi za mashairi wakati wa kuwaswaga ngamia hao: “Ninaapa kwa jina la Allah! Kama Asingalitubariki tungelipotea, tusingeli- toa zaka wala tusingeliswali. Sisi ni taifa ambalo kama taifa (fulani) liki- tuonea au kutenda maovu dhidi yetu, hatungelilivumilia (taifa hilo). Ee Allah! Tujaalie uvumilivu na utuimarishe kwenye njia hii.”

Yanayonenwa kwenye beti hizi yalidhihirisha lengo na sababu za vita hivi. Hii ina maana ya kwamba, kwa vile wayahudi wametutesa na kutenda maovu kwenye kizingiti cha chini cha nyumba yetu, sisi tunaifanya safari hii kuikomesha hatari hii. Maneno ya beti hizi yalimridhisha mno Mtume (s.a.w.w.) kiasi kwamba alimwombea dua ‘Aamir. Ilitukia kwamba ‘Aamir alipata kifo cha ushahidi kwenye vita hivi.

Jeshi La Waislamu Laelekea Upande Usiojulikana

Mtume (s.a.w.w.) aliipenda mno mbinu ya kujificha2 katika kwenda kwa vikosi. Alitaka kwamba asiwepo mtu awezaye kuutambua mwelekeo wake ili awaingilie maadui kwa mshituko na kuyazingira makazi yao kabla ya wao kuweza kuzichukua hatua za lazima. Vilevile yalikuwa ni mawazo yake kwamba, kila mmoja wa wale maadui washirika afikirie kwamba yeye pekee ndiye lengo la Mtume (s.a.w.w.) na kwa njia hii basi, wajifiche majumbani mwao ikiwa ni hatua ya tahadhari na wasiungane.

Baadhi ya watu walifikiria kwamba pengine Mtume (s.a.w.w.) aliichukua safari ile kuelekea upande wa Kaskazini ili kuyakomesha makabila ya Ghatf?n na Fazarah waliokuwa washirika wa Wayahudi kwenye Vita vya Ahzaab.

Hata hivyo, baada ya kulifikia jangwa la Raji’, aliyaelekeza majeshi upande wa Khaybar na hivyo akaukata ushirikiano baina ya hawa washirika wawili na akayazuia makabila haya yasiweze kuja kuwasaidia Wayahudi wa Khaybar. Matokeo yake yakawa kwamba, ingawa mazingira ya Khaybar yaliendelea kwa kipindi cha mwezi mzima, lakini makabila tuliyoyataja hapo juu hayakuweza kuwapa washirika wao msaada wowote.3

Yule kiongozi mkuu wa Uislamu aliendelea na safari yake akielekea Khaybar akifuatana na mashujaa 1600 waliokuwa na askari wapanda wanyama mia mbili.4 Walipofika karibu na ukanda wa Khaybar, Mtume (s.a.w.a) aliiomba dua ifuatayo iliyokuwa uthibitisho wa nia yake safi: “Ee Allah! Uliye Mola wa mbingu na kila kilichoko chini yake, na Mola wa ardhi na kila chenye kuutupia uzito wake humo!... Naomba kutoka Kwako wema wa makazi haya na wema wa wakazi wake na kila kilichomo humo na ninajikinga Kwako Wewe kutokana na uovu wake na kutokana na uovu wa makazi na kila kilichomo ndani yake.”5

Dua hii iliyofanywa pia mbele ya wale mashujaa 1600 ni ushahidi wa kwamba Mtume (s.a.w.w.) hakuja kwenye nchi hii kwa ajili ya kuiteka, yaani kuitanua nchi yake au kulipiza kisasi. Kinyume na hivyo amekuja kukibomoa hiki kitovu cha hatari ambacho kingeliweza kuwa kituo kikuu cha waabudu masanamu, na lengo lake lilikuwa kwamba harakati za Uislamu zisitishwe kutoka mahali hapa. Na kama vile mheshimiwa mso- maji utakavyoona, Mtume (s.a.w.w.) baada ya kuiteka ngome hii na kuwanyang’anya silaha hawa Wayahudi, aliwarudishia mashamba yao na akatosheka na kuwapa ulinzi kamili na akawasamehe kulipa ‘Jizyah’ (ushuru).

Sehemu Muhimu Zachukuliwa Wakati Wa Usiku

Zile ngome za Khaybar zilikuwa na majina maalum; Na’im, Qamus, Katibah, Nastaat, Sahiq, Watih na Sulaalim. Miongoni mwa ngome hizi, wakati mwingine zilihusishwa na majina ya machifu wa ngome maalum. Kwa mfano, moja miongoni mwao iliitwa ngome ya Marhab. Ili kuzihami ngome hizi na kila mara kuweza kupata taarifa za hali ya mambo ya nje ya eneo lile, minara ya doria ilijengwa kwenye pembe za ngome zote, ili kwamba wale walinzi wawekwao kwenye minara ile waweze kutoa taarifa za mambo yatokeayo nje na kuwajulisha wakazi walio ndani ya ngome. Minara hiyo ilijengwa katika hali ambayo wakazi wake waliweza kulitawala barabara eneo lote la nje na waliweza kumpiga mawe adui kwa njia ya kombeo (teo), manati n.k.6

Idadi hii ya wakazi elfu ishirini inajumuisha watu mashujaa na wababe wa vita elfu mbili waliokuwa kwenye neema ya maji na akiba ya chakula. Ngome hizi zilikuwa madhubuti mno kiasi kwamba haikuwezekana hata kidogo kutoboa tundu ndani yake, na wale waliojaribu kuziendea walijeruhiwa au kuuawa kwa mawe waliyotupiwa kutoka kwenye ngome hizo. Ngome hizi zilihesabiwa kuwa ni ngome madhubuti kwa ajili ya mashujaa wa Kiyahudi.

Ilikuwa lazima kwa hawa Waislamu waliokabiliwa na adui mwenye silaha za kutosha na mwenye nguvu, kutumia ustadi wa kivita wa hali ya juu zaidi na mbinu za kivita ili kuweza kuziteka ngome hizi. Jambo la kwanza kufanywa lilikuwa kwamba zile sehemu zote zilizokuwa muhimu na njia na malango yalikaliwa na askari wa Uislamu wakati wa usiku.

Kazi hii ilifanywa kwa siri mno na upesi mno kiasi kwamba hata wale walinzi waliokuwa kwenye ile minara ya doria hawakutambua. Ilipofika asubuhi wakulima wakiwa hawana walijualo kuhusu yaliyotokea usiku, walizotoka ngome zote za Khaybar wakiwa na zana za kilimo, macho yao yaliwaangukia askari mashujaa wa Uislamu ambao wakiwa na nguvu ya imani yao na ya mikono yao na silaha kali, waliwafungia kabisa njia zote, kiasi kwamba kama wangekuja hatua moja mbele wangelikamatwa.

Mandhari hii iliwaogofya mno kiasi kwamba mara moja walianza kukimbia na kusema: “Muhammad yuko hapa na askari wake.” Upesi upesi wakayafunga malango ya ngome zao kwa nguvu kabisa, na ndani ya ngome halmashauri zao za kivita zikakutana. Macho ya Mtume (s.a.w.w.) yalipoziangukia zana haribifu kama vile mabeleshi na sululu alizifikiria kuwa ni ndege njema na akayasema maneno yafuatayo ili kuziimarisha nyoyo za askari wa Uislamu: “Allah Yu Mkubwa! Na iangamie Khaybar. Tunapolishukia taifa, utakuwa ni wakati mbaya kiasi gani kwa wale walioonywa!”

Baada ya majadiliano baina yao Wayahudi waliamua kwamba wanawake na watoto wawekwe kwenye moja ya ngome zile na maghala ya vyakula yapelekwe kwenye ngome nyingine. Kisha wale mashujaa na wababe wa vita wa kila ngome wajihami wenyewe kutoka juu ya minara kwa kutumia mawe na mishale. Katika baadhi ya matukio maalumu wapiganaji wa kila ngome watoke nje ya ngome ile na wapigane na Waislamu. Wale mashujaa wa Kiyahudi hawakuuacha mpango huu hadi mwishoni mwa uadui ule na matokeo yake ni kwamba, waliweza kulizuia lile jeshi kubwa la Waislamu kwa kipindi cha mwezi mzima. Wakati mwingine ilichukuwa siku kumi kufanya juhudi za kuiteka ngome lakini lengo halikuweza kufikiwa.

Ngome Za Wayahudi Zaanguka

Sehemu iliyochaguliwa na maafisa wa Uislamu kuwa makao makuu ya jeshi katika jihadi hii ya Kiislamu haikuwa muhimu sana kwa upande wa kijeshi. Jeshi la kiyahudi lilitawala sehemu hii kikamilifu na hakikuweko kizuizi au pingamizi yoyote katika kulenga shabaha kwenye yale makao makuu ya jeshi la Waislamu. Kwa sababu hii, mmoja wa mashujaa stadi wa Uislamu aliyeitwa Hubab bin Munzir alikuja kwa Mtume (s.a.w.w.) na kusema: “Kama umepiga kambi kwenye sehemu hii kwa amri ya Allah Mwingi wa rehema, siwezi kukataa hata kidogo kwa kuwa amri ya Allah ni nje ya hoja na tahadhari zetu zote. Hata hivyo, iwapo ni jambo la kawaida ambalo maafisa wanaweza kutoa maoni yao, ninalazimika kusema kwamba sehemu hii iko mbele ya macho ya adui na mbele ya ngome ya Nataah, na kwa kuwa hakuna miti wala nyumba hapa, wapiga mishale wa ngome hii wanaweza kulenga shabaha kwenye hiki kituo cha jeshi kwa urahisi sana.”

Mtume (s.a.w.w.) akiwa yu mwenye kuyatenda mambo kwa mujibu wa moja ya kanuni muhimu mno za Uislamu (ambayo ni kanuni ya ushauriano na kuyaheshimu maoni ya wenzie), alisema hivi: “Kama ukiitaja sehemu iliyo bora zaidi ya hii nitaisogeza hapo kambi yangu.”

Baada ya kuichunguza ardhi ya Khaybar, sahaba mmoja aliyeitwa Kubab aliipendekeza sehemu iliyokuwa nyuma ya mitende, na hivyo askari na yale makao makuu ya jeshi yalihamishiwa pale. Baada ya hapo hadi ilipotekwa Khaybar, maafisa na Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) walikuja kwenye ngome zile kila siku kutoka mahali pale, na ulipoingia usiku wakarejea kwenye kambi yao.7

Hakuna maoni yenye kukata shauri yawezayo kuelezwa kuhusiana na maelezo kamili ya Vita vya Khaybar. Hata hivyo, kutoka kwenye vitabu vyote vya historia na vya maisha ya Mtume (s.a.w.w.) tunajifunza kwamba askari wa Uislamu walizizingira ngome zile moja baada ya nyingine na wakajitahidi kuyakata mawasiliano ya ngome iliyozingirwa, na wakaendelea kuizingira nyingine baada ya kuiteka ile ya awali.

Kutekwa kwa zile ngome zilizoungana moja baada ya nyingine kulicheleweshwa kwa njia za chini ya ardhi au ambazo mashujaa wao walifanya upinzani mgumu kuliahirishwa, ambapo zile ngome ambazo makamanda wao walitishiwa mno au ambazo uhusiano wao na ngome nyingine ulikatwa kabisa, zilitekwa kwa urahisi kabisa. Katika hali hiyo, umwagaji wa damu mdogo sana ulitendeka na mambo yalimalizwa kwa haraka.

Kufuatana na kauli ya baadhi ya wanahistoria, ngome ya kwanza ya Khaybar iliyosalimu amri kwenye majeshi ya Kiislamu baada ya juhudi kubwa na taabu ilikuwa ni ngome ya Na’im. Kutekwa kwa ngome hii iligharimu kufa kishahidi kwa Muhammad bin Maslamah Ansari mmoja wa makamanda wakuu wa Uislamu. Kwenye vita hivi askari hamsini wa Uislamu walijeruhiwa. Muhammad bin Maslamah alipigwa jiwe lililovurumishwa kutoka juu na akafariki dunia papo hapo. Hata hivyo, kufuatana na kauli ya Ibn Athir8 alifariki dunia baada ya siku tatu. Ama kuhusu wale askari hamsini waliojeruhiwa, walipelekwa kwenye sehemu fulani kwenye ile kambi iliyowekwa kwa ajili ya kufunga vidonda.9

Kikundi cha wanawake wa kabila la Bani Ghif?r walikuja pale Khaybar kwa idhini ya Mtume (s.a.w.w.) kuwasaidia Waislamu kuvifunga vidonda vyao na kuwapatia huduma zote nyingine ziruhusiwazo kwa wanawake kwenye kambi ya jeshi. Walizitoa huduma hizi kwa moyo mmoja na kwa uaminifu.10

Halmashauri iliamua kwamba baada ya kuiteka ngome ya Na’im, wale askari wa Uislamu waishambulie ngome ya Qamus. Chifu wa ngome hii alikwua Ibn Abil Haqiq.
Ikiwa ni matokeo ya kujitolea mhanga kwa wale askari wa Uislamu, ngome hii ilitekwa nayo, na Bibi Safiyah binti wa Hay bin Akhtab ambaye baadae alikuwa mkewe Mtume (s.a.w.w.) alikamatwa. Kutekwa kwa ngome hizi mbili kuliziimarisha nyoyo za askari wa Uislamu na fadhaa na woga vikawapata Wayahudi. Hata hivyo, Waislamu walikuwa kwenye mashaka makubwa mno kutokana na upungufu wa chakula, kiasi kwamba walilazimika kula nyama ya baadhi ya wanyama ambao nyama yao ilichukiza (ingawa haikua haramu). Ile ngome iliyokuwa na chakula kingi ilikuwa bado haijaingia mikononi mwa Waislamu.

Uchamungu Mbele Ya Dhiki Hasa

Wakati mmoja Waislamu walipokabiliwa na njaa kubwa na wakawa wanaitosheleza njaa yao kwa kula nyama ya wanyama ambao nyama yao haikupendekezwa kwenye sheria ya vyakula, mchungaji mmoja aliyekuwa na uso mweusi na aliyekuwa akifanya kazi ya kuwachunga wanyama wa Wayahudi alikuja mbele ya Mtume (s.a.w.w.) na akaomba kwamba aelezwe ukweli juu ya Uislamu.

Baada ya kuyasikia maneno ya Mtume (s.a.w.w.) yenye kuvutia na yenye kupenya moyoni alisilimu mara moja na akasema: “Kondoo wote hawa wamewekwa dhamana kwangu na Myahudi. Niwafanye nini sasa wakati mawasiliano na wenyewe yamekatika?” Mtume (s.a.w.w.) alimweleza kwa maneno yaelewekayo, tena dhahiri mbele ya mamia ya askari wenye njaa kwamba: “Katika dini yangu, kuvunja ahadi ni moja ya dhambi zilizo kubwa zaidi. Ni muhimu kwamba uwapeleke kondoo wote hao kwenye lango la ngome.” Aliitekeleza amri ya Mtume (s.a.w.w.) na kisha yeye mwenyewe akarejea upesi na akashiriki kwenye vita ile na akafa kishahidi katika njia ya Uislamu.11

Hakuna shaka kwamba Mtume (s.a.w.w.) aliyejipatia cheo cha al-Amin (mwaninifu) kwenye zama za kabla ya Uislamu aliendelea kuwa mwaninifu na mkweli kwenye hali zote.

Upitaji wa makundi ya wanyama ulikuwa huru wakati wa asubuhi na vilevile wakati wa alasiri kwenye kipindi chote cha kuzingirwa na hakuna hata Mwislamu moja aliyefikiria kumchukua kondoo wa adui, kwa sababu Waislamu nao wamekuwa wanyoofu na waaminifu kutokana na mafundisho matukufu ya kiongozi wao.

Ni kwenye siku moja tu, wakati wote walipozidiwa nguvu kabisa na njaa, aliwaruhusu wakamate kondo wawili kutoka kwenye kundi moja na akawaacha wengine kwenye ngome yao. Hili pia lisingelitendeka kama wasingelilazimishwa na njaa kali kufanya hivyo. Hivyo basi, wale askari walipolalamika kuhusu njaa, Mtume (s.a.w.w.) aliinua mikono yake na akaomba, akisema: “Ee Mola! Wawezeshe askari hawa kuiteka ile ngome vilimohifadhiwa vyakula.” Hata hivyo, hakuwaruhusu kuitwaa mali ya watu mpaka pale ulipopatikana ushindi.12

Kwa habari zote hizi, utovu wa misingi wa kauli za baadhi ya mustashirik wa zama hizi wenye upendeleo hudhihirika, kwa sababu ili kuyatweza malengo matukufu ya Uislamu wanajitahidi kuthibitisha kwamba vita walivyopigana Waislamu vilishabahia kwenye utekaji na kukusanya ngawira, na utawala wa haki kwenye nyakati zile za kupigana vita hivi haukuzingatiwa na watu hawa.

Hata hivyo, tukio tulilolitaja hapo juu pamoja na matukio mengine ya aina hii yaliyowekwa kwenye kumbukumbu za historia huudhihirisha uwongo wa kauli hizi, kwa sababu Mtume (s.a.w.w.) hakuruhusu kwamba yule mchungaji aivunje ahadi yake na wale matajiri wake wa Kiyahudi, japo kwenye hali ngumu mno (kwa mfano pale askari wake wenye kujitoa mhanga walipokabiliwa na njaa na kifo), ingawa wakati ule angeweza kuwanyakua kondoo wote wale.

Ngome Zatekwa, Moja Baada Ya Nyingine

Baada ya kutekwa kwa zile ngome tulizozitaja, yale majeshi yenye kuzingira yalizielekeza juhudi zao kwenye ngome za Watih na Sulaalim.13

Hata hivyo, yale mashambulizi ya Waislamu yalizuiwa kwa nguvu na wale Wayahudi kwa nje ya ngome, na mashujaa wa Uislamu hawakuweza kupata ushindi ingawa walikuwa nao ushupavu wa kijasiri. Idadi ya hasara walizozipata imeandikwa na mwandishi wa historia ya Uislamu Ibn Hisham chini ya orodha maalum. Walipigana na Wayahudi kwa muda wa siku kumi lakini kila siku walirejea kule kambini kwao bila ya kupata ushindi.

Katika moja ya siku hizi kumi, Bwana Abubakr aliteuliwa aende akalete ushindi. Alikuja hadi kwenye ukingo wa ile ngome akiwa amechukua ile bendera nyeupe na wale askari mashujaa wa Uislamu walikwenda chini ya amri yake. Hata hivyo, baada ya muda fulani walirudi bila kupata matokeo yoyote yale, na yule kamanda wa kile kikosi na wapiganaji wake aalimtupiana lawama kuhusika na kule kushindwa na kukimbia kutoka kwenye uwanja wa vita.

Katika siku iliyofuatiwa uamiri jeshi aliupewa Umar. Yeye naye alirudia ile hadithi ya rafiki yake, na kwa mujibu wa kauli ya Tabari,14 aliwatishia masahaba wa Mtume (s.a.w.w.) kwa kumsifu chifu wa ngome ile aliyeitwa Marh kwa ushujaa na ujasiri wake usio kifani. Mtume (s.a.w.w.) na makamanda wa Uislamu waliudhishwa mno na jambo hili.15 Wakati huo, Mtume (s.a.w.w.) aliwakusanya maafisa na mashujaa wa jeshi pamoja akazitamka sentensi zifuatazo zenye kuamsha ushujaa wa askari ambazo zimehifadhiwa kwenye historia:

“Kesho nitampa bendera hii yule mtu ampendaye sana Allah na Mtume Wake (s.a.w.w), na apendwaye sana na Allah na Mtume Wake, na Allah atatimiza kutekwa kwa ngome hii mikononi mwake. Yu mtu ambaye katu hajawahi kumgeuzia adui mgongo wake na haukimbii uwanja wa vita.”

Na kufuatana na ilivyonukuliwa na Tabrasi na Halabi alitumia maneno ‘Karraar Ghayr-i-Farraar yenye maana ya mtu amshambuliaye adui na asiyekimbia.16 (yaani yu kinyume na wale makamanda wawili tuliwataja hapo awali)

Kauli hii, ambayo ni ushahidi wa ubora, na uwezo wa kiroho wa kamanda ambaye alikusudiwa kuwa mshindi, ilizaa hoihoi za furaha zilizoandamana na wasiwasi wa akili miongoni mwa askari na makamanda wa jeshi lile, na kila mmoja wao alikuwa akitamani17 kwamba hii medali kuu ya kijeshi imwangukie yeye.

Giza la usiku lilienea kila mahali. Wale askari wa Uislamu wakaenda kulala na walinzi wa doria wakazishika nafasi zao kwenye sehemu za miinuko ili kuiangalia mienendo ya adui.
Hatimaye kulikucha. Wale makamanda wakamzunguka Mtume (s.a.w.w.). Wale makamanda wawili walioshindwa pia nao walikuwapo pale wakizinyoosha shingo zao kwa kuwa wao nao walikuwa na shauku ya kutaka kujua upesi iwezekanavyo ni nani atakayepewa ile bendera tukufu.18

Ukimya wa watu waliokuwa wakisubiri kwa hamu na dukuduku ulivunjwa na maneno ya Mtume (s.a.w.w.): “Yuko wapi Ali?” Aliarifiwa kwamba alikuwa mgonjwa wa macho na alikuwa amepumzika pembeni hivi. Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Mleteni hapa.” Tabari anasema: “Ali alipandishwa juu ya ngamia na alisaidiwa kushuka juu ya ngamia mbele ya hema la Mtume.” Sentensi hii inaonyesha kwamba maradhi ya macho yalikuwa makubwa kiasi kwamba yalimfanya kamanda asiweze kutembea. Mtume alinyoosha mkono wake mwenyewe kwenye macho yake na akamuombea. Kitendo hiki na dua hii ilikuwa na athari kama pumzi ya Nabii Isa, kwani baada ya hapo macho ya Ali kamanda mkuu wa Uislamu, hayakuwa na matatizo maishani mwake mote.

Mtume (s.a.w.w.) alimwamrisha Sayyidna Ali (a.s.) kwenda vitani. Kuhusiana na jambo hili alimkumbusha kwamba kabla ya kuanza kupigana awapeleke wawakilishi wake kwa wale machifu wa ile ngome na wawaite kwenye Uislamu. Hata hivyo, kama watakataa kusilimu, waarifu wajibu wao wawapo chini ya bendera ya Serikali ya Uislamu, yaani kwamba watalazimika kuzitoa silaha zao na kuishi maisha yaliyo huru kabisa chini ya ulinzi wa Uislamu kwa kulipa Jizyah.19 Hata hivyo kama watakataa kuikubali, hapo apigane nao.

Na sentensi ya mwisho aliyoitamka Mtume (s.a.w.w.) ikiwa ni mwongozo kwa Sayyidna Ali (a.s.) ilikuwa hii: “Kama Allah Mwenye nguvu zote Akimwongoza japo mtu mmoja tu kupitia kwako, ni bora kuliko kwamba wewe uwe na ngamia wenye manyoya mekundu na kuwatumia (ngami hao) katika njia ya Allah.”20 Hakuna shaka kwamba Mtume (s.a.w.w.) alifikiria kuwaonyesha wanadamu njia iliyonyooka hata katika nyakati za vita, na jambo hili laonyesha kwamba vita hivi vinapiganwa kwa ajili ya mwongozo wa watu.

Ushindi Mkuu Wa Khaybar

Wanahistoria na waandishi wa wasifu wa Uislamu wameandika kwa kirefu juu ya kutekwa kwa Khaybar, na mtu anapozisoma taarifa hizi hujifunza kiasi fulani ya habari. Hapa tunayataja yale yaliyoandikwa na waandishi wa wasifu wa Mtume (s.a.w.w.) kwa njia ya kuyasimulia matukio, na hapo baadaye tutayachunguza.

Maneno na kurasa za historia ya Uislamu ihusianayo na vita hivi yaonyesha kwamba, bila ya uhodari na kujitolea mhanga kwa Amirul- Mu’minin, isingeliwezekana kuziteka zile ngome za Wayahudi wa Khaybar. Ingawa baadhi ya waandishi wamezibadili habari fulani fulani na badala yake wameweka ngano fulani fulani, lakini bado idadi kubwa kidogo ya wanachuoni watafiti wamempa Sayyidna Ali (a.s.) sifa zipasikazo. Maelezo ya mukhtasari katika jambo hili la kihistoria kama zilivyokusanywa kutoka kwenye vitabu mbalimbali vya historia tunayatoa hapa chini:

“Ali alipoteuliwa na Mtume (s.a.w.w.) kuziteka ngome za Watih na Sulaalim, zile ngome mbili ambazo wale makamanda wawili wa mwanzo walishindwa kuziteka na wakapigwa pigo lisilotengenezeka katika heshima ya jeshi la Uislamu kwa kuzionyesha jozi mbili za visigino zilizo safi (yaani kukimbia), alivaa deraya madhubuti na akaufunga upanga wake Dhulfiqar kwenye mkanda wake. Kisha akaenda kule kwenye ile ngome kwa shauku maalum imstahiliyo mpiganaji hodari awapo kwenye uwanja wa vita na akaenda akaikita ile bendera aliyopewa na Mtume (s.a.w) mahali fulani karibu na Khaybar. Wakati huo huo lile lango la Khaybar lilifunguliwa na mashujaa wa Kiyahudi wakatoka.

Kwanza kabisa Harith nduguye Marhab akaja mbele. Sauti yake yenye kuogofya, mbaya na yenye uvumi mkali iliogofya mno kiasi kwamba wale askari waliokuwa nyuma ya Ali, walisogea nyuma bila ya kupenda. Hata hivyo, Ali alisimama kwa uthabiti kwenye sehemu yake kama mlima. Mara tu baada ya hapo, Ali alimpiga dharuba Harith na akaanguka, mwili wake uliojeruhiwa ukawa umelala chini na akafa.

Kifo cha Harith kilimsikitisha mno Marhab. Akasogea mbele ili alipize kisasi cha kuuwawa kwa nduguye. Alikuja katika hali ambayo alijifunga silaha tangu miguuni hadi kwenye meno. Alivaa deraya ya Yaman mwilini mwake na alivaa kofia iliyotengenezwa kwa jiwe maalumu kichwani mwake ambayo kaifunika kwa kofia ya chuma. Kufuatana na desturi za wapiganaji wa Kiarabu wa zama zile, alizisoma beti za utenzi zifuatazo: “Milango na kuta za Khaybar zashuhudia kwamba mimi ni Marhab. Mimi ni mpiganaji mzoefu nami ninazo silaha za vita. Kama wakati ni wenye kushinda, mimi nami ni mshindi. Wapiganaji wanikabilio mimi kwenye uwanja wa vita huwapaka rangi ya damu zao”

Ali naye alisoma beti za utenzi ili kumjibu Marhab na akamweleza cheo chake yeye kama askari, na nguvu za mikono yake, na akasema: “Mimi ndiye yule mtu ambaye mama yake alimwita Haydar (Simba). Mimi ni mtu shujaa na Simba wa mapori (ya ushujaa). Nina mikono yenye nguvu na shingo yenye nguvu. (Nikiwa) kwenye uwanja wa vita huwapiga watu kwa hofu kama Simba.”

Tenzi za kujisifu toka kwenye pande zote mbili zilimalizika. Sauti za panga na mikuki ya mashujaa hawa wawili zilizovuma kama radi zilijenga hofu isiyo na kifani akilini mwa watazamaji. Mara kwa ghafla ule upanga mkali upigao dharuba wa yule shujaa wa Uislamu ulikipiga kichwa cha Marhab na kuichana ngao yake, ile kofia yake ya chuma, ile kofia ya jiwe na kich- wa chake hadi kwenye meno na hatimaye kukigawa pande mbili. Dharuba hii ilikuwa kali mno kiasi kwamba baadhi ya askari wa Kiyahudi waliokuwa wakisimama nyuma ya Marhab, walikimbia na kwenda kujificha kwenye ile ngome, na wengine waliobakia pale walipigana bega kwa bega dhidi ya Ali na wakauawa.

Ali akawafuatilia wale Wayahudi waliokimbia hadi kwenye lile lango la ngome. Katika juhudi hizi, mmoja wa askari wa Kiyahudi aliipiga ngao ya Ali kwa upanga wake nayo ikamponyoka ikaanguka chini. Upesi sana Ali akaigeukia ile ngome akalikwanyua lango lake na kulifanya ngao hadi mwishoni mwa vita vile. Na alipoitupa chini, askari kumi wa Uislamu wenye nguvu, ikiwa ni pamoja na Abu Raf’i walijaribu kuipindua chini juu, juu chini lakini walishindwa kufanya hivyo.21 Matokeo yake ni kwamba, ile ngome ambayo Waislamu walikuwa wakiisubiri kutekwa kwake kwa muda wa siku kumi, ilitekwa kwa muda mfupi. Yaa’qubi anasema:22”Lile lango la ngome ile lilitengenezwa kwa jiwe na lilikuwa na urefu wa dhiraa23 nne na upana wa dhiraa mbili.

Sheikh Mufid ameinukuu ile Hadith ya kulikwanyua lile lango la Khaybar kutoka kwa Amirul-Mu’minin, kutoka kwa watu maalum wenye kuamini- ka ya kwamba: “Nililing’oa lile lango la Khaybar na nikalifanya ngao. Baada ya kwisha mapambano yale nililiweka mithili ya daraja penye han- daki lililochimbwa na Wayahudi. Kisha nililitumbukiza ndani ya handaki.” Mtu mmoja alimwuliza: “Je, uliliona zito?” Ali alijibu: “Nililiona kuwa ni zito kama ile ngao yangu.”24

Wanahistorisa wamenukuu mambo yenye kushangaza sana juu ya lile lango la ile ngome ya Khaybar na maajabu yake na ule ushujaa alioudhihirisha Sayyidna Ali (a.s.) katika kuiteka ngome ile. Ukweli ni kwamba ujasiri kama huu hauwezi kutendwa kwa nguvu ya binadamu wa kawaida. Hata hivyo, Sayyidna Ali (a.s.) amelieleza jambo hili yeye mwenyewe na hivyo basi ameziondoa shaka zote na dhana mbaya. Kwa sababu, akilijibu swali lililoulizwa na mtu mmoja, alisema: “Sikuling’oa lango lile kwa nguvu za kibinadamu. Nilifanya vile kwa nguvu niliyojaaliwa na Allah, na kutokana na imani yangu thabiti juu ya siku ya Hukumu.”25

Kuugeuza Ukweli Wa Mambo

Haki inahitaji kwamba tusiwe na budi kukubali kwamba Ibn Hisham na Abu Ja’afar Tabari wametoa taarifa ndefu vya kutosha juu ya mapigano ya Sayyidna Ali (a.s.) pale Khaybar na wameeleza mambo hata yale yaliyo madogo mno juu ya tukio lile. Hata hivyo, mwishoni wameutaja uwezekano wa kimawazo tu juu ya Marhab kwamba aliuwawa mikononi mwa Muhammad bin Maslamah na wanasema: “Baadhi ya watu wanaamini kwamba Marhab aliuwawa mikononi mwa Muhammd bin Maslamah kwa sababu aliteuliwa kwa lengo lile na Mtume (s.a.w.w.) ili alipizie kisasi cha kuuwawa kwa nduguye kulikofanywa na Wayahudi wakati wa kutekwa kwa ngome ya Na’im na inawezekana kwamba alifaulu kulitimiza jukumu hili.”

Uwezekano huo ni usiothibitishwa kabisa kiasi kwamba hauwezi kulinganishwa na yale maelezo sahihi na yenye kufululiza yasimuliwayo kwenye historia ya Uislamu. Aidha, matatizo fulani fulani hujitokeza kwenye ngano hii kama tutakavyoeleza hapa chini: Tabari na Ibn Hisham wameinukuu ngano hii kutoka kwa sahaba maarufu wa Mtume (s.a.w.w.) Jabir bin Abdullah, na msimuliaji wa hadith hii amelinukuu jambo hili geni kutoka kwa mtu huyu mkubwa, ambapo ukweli ni kwamba Jabir alipata heshima ya kufuatana na Mtume (s.a.w.w.) kwenye vita vyote, lakini hakuweza kushiriki kwenye vita hivi.

Muhammad bin Maslamah hakuwa shujaa vya kutosha kiasi kwamba aweze kuwa mtekaji wa Khaybar na hakupata kuonyesha uthibitisho wowote wa ushujaa maishani mwake. Kwenye mwaka wa pili wa Hijiriya aliteuliwa na Mtume (s.a.w.w.) kumwua Myahudi Ka’ab bin Ashraf, aliyekuwa akiwachochea waabudu masanamu waamke dhidi ya Uislamu baada ya vita vya Badr na kupigana tena na Waislamu.

Hata hivyo, aliogopa mno kiasi kwamba hakula wala kunywa kitu chochote kwa siku tatu mchana na usiku, na Mtume (s.a.w) akamlaumu kwa woga wake huu.

Akajibu, akisema: “Sijui kama nitafaulu katika jukumu hili au la.” Mtume (s.a.w.w.) alipoona hali hii ya mambo, aliwatuma watu wanne pamoja na yeye ili wakaumalizie mbali uasi wa Ka’ab bin Ashraf, aliyekuwa akijaribu kuufufua uadui baina ya waabudu masanamu na Waislamu. Wakaunga makri maalum kwa lengo hili na wakamwua yule adui wa Allah wakati wa usiku wa manane. Hata hivyo, kutokana na woga uliokithiri, na hofu, Muhammad alimjeruhi mmoja wa wale wenzie.”26 Hakika mtu mwenye moyo wa aina hii, hangeliweza kumsukumizia nyuma yule shujaa wa Khaybar.

Yule Mtekaji wa Khaybar hakupambana na Marhab pekee na kumwua, bali baada ya kuuawa kwa Marhab, baadhi ya watu walikimbia na wengine waliingia uwanjani mmoja baada ya mwingine na kupambana naye katika mapambano ya wawili wawili. Wale mashuja wa Kiyahudi waliopigana na Sayyidna Ali (a.s.) baada ya Marhab na kuuawa ni hawa:

(i) Dawudi bin Qubus

(ii) Abil Haqia,

(iii) Abul Ba’ith

(iv) Marrah bin Marwaan

(v) Yasir Khaybari

(vi) Zajih Khaybari.

Watu sita hawa ndio waliokuwa mashujaa wa Wayahudi nje ya Khaybari nao walihesabiwa kuwa walikuwa kizuizi kikuu katika kuziteka zile ngome za Khaybar. Na wote hawa walipokuwa wakiziimba beti za tenzi na kumwita mpinzani ili aje kupigana, waliuawa mikononi mwa Amirul-Mu’minin (a.s.). Katika hali hii, hatuna budi kuamua ni nani awezaye kuwa mtekaji wa Khaybar.

Hii ni kwa sababu kama Muhammad bin Maslamah angelikuwa muuwaji wa Marhab asingelirejea kwenye ile kambi ya Waislamu baada ya kumuuwa Marhab na kuwaacha wale mashujaa waliokuwako mgongoni kwa Marhab, kwa sababu angelilazimika kupigana na watu wale pia, ambapo wanahistoria wote wanakubaliana kwamba watu hawa walipigana na Sayyidna Ali (a.s.) na waliuawa mikononi mwake.

Ngano hii ya historia ni kinyume na hadith zenye kurudiwa rudiwa zilizonukuliwa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w.), kwa sababu alisema kuhusiana na Sayyidna Ali (a.s.) kwamba: “Nitampa bendera hii yule mtu ambaye mikononi mwake ushindi utakamilika,” na katika siku iliyofuatia alimpa (yeye Sayyidna Ali - a.s) ile bendera ya ushindi. Na moja ya vizuizi vikuu katika kuupata ushindi kilikuwa ni Marhab wa Khaybar, ambaye uhodari wake umewafanya makamanda wawili wa Uislamu kuukimbia uwanja wa Vita. Sasa kama muuwaji wa Marhab angelikuwa Muhammad bin Maslamah ingelifaa tu kwamba Mtume (s.a.w.w.) angeliitamka juu yake sentensi tuliyoitaja hapo juu, na wala si juu ya saidina Ali (a.s.).

Mwanahistoria maarufu Halabi anasema: “Hakuna shaka juu ya ukweli uliopo kwamba Marhab aliuawa mikononi mwa Ali.”27 Ibn Athir anasema kwamba waandishi wa wasifu wa Mtume (s.a.w.w.) na wanahadithi wanamhesabu Sayyidna Ali (a.s.) kuwa ndiye muuwaji wa Marhab na masimulizi yenye kurudiwa rudiwa yamenukuliwa kuthibitisha ukweli huu.

Tabari na Ibn Hisham kwa kiasi fulani walisumbuliwa kimawazo na wakalitaja lile tukio la kushindwa na kurejea kwa wale makamanda wawili walioteuliwa kuiteka ngome ile kabla ya Sayyidna Ali (a.s.) kwa jinsi isiyoafikiana na maana ya ile sentensi aliyoitamka Mtume (s.a.w.w.) juu ya Sayyidna Ali (a.s.): “Yule asiyekimbia,” yaani yu kamanda asiyekimbia, ambapo wale makamanda wawili wa awali, kwa hakika walikimbia na wamepaacha pale mahali pa vita. Hata hivyo, hawa waandishi wawili tuliowataja hapo juu hawakulitaja jambo hili nao wamelisimulia tukio hili kwa njia ambayo kana kwamba walilitekeleza jukumu lao kikamilifu. Lakini hawakufaulu katika kuiteka ngome ile.

Nukta Tatu Zenye Kung’ara Katika Maisha Ya Ali (A.S)

Sasa tunaimalizia maudhui hii hapa baada ya kutaja nemsi tatu za yule mtekaji wa Khaybar. Siku moja Muawiyah alimlaumu Sa’ad bin Waqqas kwa kutokumlaani Ali (a.s.), yeye alimjibu akisema: “Kila ninapozikumbuka nemsi tatu za Ali, ninatamani kwamba angalau ningekuwa na mojawapo ya hizo:

1. Siku moja Mtume (s.a.w.w.) alimteua kuwa mwakilishi wake mjini Madina na yeye mwenyewe akatoka na kwenda kwenye Vita vya Tabuk, alimwambia Ali: “Wewe kwangu unacho cheo kama kile alichokuwa nacho Harun kwa Musa ila tu kwamba hatakuwepo Mtume baada yangu.”

2. Katika siku ya Khaybar Mtume alisema: “Kesho nitampa bendera yule mtu apendwaye na Allah na Mtume.” Maafisa na makamanda wa Uislamu wakuu wote walikuwa na tamaa ya kuipata heshima ile. Hata hivyo, siku iliyofuatia Mtume alimwita Ali na akampa ile bendera na Allah akatujaalia ushindi ambao hasa ulitokana na kujitolea mhanga kwa Ali.

3. Ilipoamualiwa kwamba Mtume aingie kwenye Mubahilah (kulaaniana) na viongozi wa Najr?n, aliishika mikono ya Ali, Fatmah, Hassan na Hussein, na akasema: “Ee Allah! Hawa ndio watu wa Nyumba yangu.”28

Mambo Yaliyoleta Ushindi

Malango ya ngome za Khaybar yalifunguliwa na Wayahudi wakasalimu amri mbele ya jeshi la Uislamu chini ya masharti maalum. Hata hivyo, hatuna budi kujua ni mambo gani yaliouleta ushindi huu, na bila shaka mambo haya yatakuwa ndiyo yaliyo makuu zaidi kwenye kisa hiki. Ushindi huu mkuu wa Waislamu ulikuwa ni matokeo ya mambo yafuatayo: Mipango na mbinu za Kijeshi.

Kujipatia taarifa na kuwa macho juu ya siri za adui. Ushujaa kamili na kujitoa mhanga kwa Sayyidna Ali, Amirul-Mu’minin (a.s.)

2. Mipango Na Mbinu Za Kijeshi

Jeshi la Uislamu lilipiga kambi mahali palipowawezesha kuyakata mawasiliano baina ya Wayahudi na marafiki zao (yale makabila ya Ghatf?n). Kwa ujumla ilikuweko idadi kubwa ya askari wapiganao kwa panga na watu wasiotishika kwenye familia za Ghatf?n, na kama wangelikuja kuwasaidia Wayahudi na wakapigana bega kwa bega pamoja nao basi kutekwa kwa ngome ya Khaybar kusingeliwezekana. Watu wa kabila la Ghatf?n walipopata taarifa juu ya jeshi la Waislamu kwenda Khaybar walikwenda upesi sana wakiwa na zana za kutosha ili wakawasaidie washirika wao.

Hata hivyo, walipokuwa njiani ziliwafikia fununu miongoni mwao kwamba wapiganaji wa Muhammad walikuwa wakija nchini mwao kwa kupitia njia isiyokuwa ile ya kawaida. Fununu hizi zilipata nguvu mno kiasi kwamba walirejea kwao walipokuwa katikati ya njia na hawakutoka tena nchini mwao mpaka ilipotekwa Khaybar na Waislamu.

Wanahistoria huihesabu fununu hii kuwa ni matokeo ya sauti ya siri. Hata hivyo, si jambo lisiliwezekana kwamba uvumi huu ulienezwa na Waislamu wa kabila la Ghatf?n, na waundaji wa uvumi huu walikuwa ni wale watu ambao kusema kweli walikuwa ni Waislamu nao walikuwa wakiishi miongoni mwa watu wa kabila lao katika vazi la makafiri na walikuwa wastadi mno katika kuibuni mbinu hii kiasi kwamba waliweza kufaulu kuyazuia majeshi ya Ghatf?n kwenda kuwasaidia washirika wao. Na kitendo hiki kilikuwa ni mfano wa vita vya Ahzaab, kwa sababu kwa matokeo ya upelezi wa Mwislamu mmoja wa kabila la Ghatf?n aliyeitwa Na’im bin Mas’ud, jeshi la makafiri lilitawanyika na akauzuia msaada wao kutoka kwa Wayahudi.

Kujipatia Taarifa

Mtume (s.a.w.w.) aliweka muhimu mkubwa sana katika kupata taarifa kuhusiana na vita. Hivyo basi, kabla ya kuizingira Khaybar alipeleka watu ishirini kwenye sehemu ile ili wawe watangulizi wakiwa chini ya uongozi wa ’Abbad bin Bashir. Watu hawa walikutana na mkazi mmoja wa Khaybar karibu na sehemu ile. Baada ya kuzungumza naye, ‘Abbad alitambua kwamba alikuwa mmoja wa watu wenye taarifa kamili juu ya Wayahudi.

Hivyo akaamrisha akamatwe upesi sana na akampelekwa kwa Mtume (s.a.w.w.). Alipotishiwa kifo alizivujisha siri zote za Wayahudi. Kutokana naye ilifahamika kwamba Wayahudi wamekuwa na woga mno baada ya kupata taarifa kutoka kwa yule chifu wa wanafiki, (yaani Abdulah bin Sullul) na vile vile kwa kuwa bado hawajapata msaada kutoka kwa watu wa kabila la Ghatfan.

Katika usiku wa sita wa vita vile, kikosi cha doria cha Waislamu kilimkamata Myahudi na wakamleta mbele ya Mtume (s.a.w.w.) aliyemuuliza kuhusu hali na mambo ya Wayahudi. Alisema: “Nitakuambieni mradi tu nithibitishieni uhai wangu.” Alipothibitishiwa alisema: “Usiku huu askari wa Khaybar watahama kutoka kwenye Ngome ya Nastaat kwenda kwenye Ngome ya Shiq ili wajihami kutoka pale.

Ewe Abul Qaasim! Kesho utaiteka ngome ya Nastaat.” Mtume akasema: “Kama Allah Akipenda.” Yule Myahudi akaendelea kusema: “Kwenye ngome hiyo utapata idadi kubwa ya teo, zana za kijeshi, deraya, na panga, vikiwa vimefichwa ardhini, na kwa silaha hizi utaweza kuipiga mawe ngome ya Shiq.”29

Yule kiongozi mkuu wa Uislamu hakuzitumia silaha hizi zenye uwezo wa kuleta uharibifu mkubwa, lakini zile taarifa zilizotolewa na yule mfungwa zilikuwa muhimu kwa kuwa zilieleza waziwazi kwamba ni ngome ipi ipasikayo kushambuliwa siku iliyofuatia, na ilifahamika kwamba kutekwa kwa Ngome ya Nastaat hakungalihitaji nguvu kubwa na kwamba tahadhari ilihitajika ili kuiteka ngome ya Shiq.

Baada ya kucheleweshwa kwa kutekwa kwa moja ya ngome zile kwa muda wa siku tatu Myahudi mmoja alimjia Mtume (s.a.w.w.), pengine kwa lengo la kutaka kuyaokoa maisha yake, na kusema: “Japo ukae mahali hapa kwa muda wa mwezi mzima hutaweza kuwazidi nguvu. Hata hivyo, ninaweza kukuonyesha chanzo cha maji cha ngome hii na kama ukipenda unaweza kuwakatia maji.”

Mtume (s.a.w.w.) hakuikubali rai hii, na akasema: “Hatumkatii maji mtu yeyote ili asije akafa kwa kiu.” Hata hivyo, ili kuweza kuzidhoofisha nyoyo za maadui aliamrisha kwamba upatikanaji wa maji kwa ajili yao uzuiwe kwa muda. Jambo hili liliwaogofya mno kiasi kwamba mara tu baada ya mapigano madogo walisalimu amri kwenye jeshi la Uislamu.30

3. Kujitoa Mhanga Kwa Ali (A.S)

Tumetaja kwa kifupi hapo awali kujitoa mhanga kwa Ali (a.s.) na sasa tunayanakili maneno yake mwenyewe: “Tulisimama upande wa pili wa jeshi kubwa na ngome imara za Wayahudi. Mashuja wao walitoka nje ya ngome zile na kuwaita wapinzani ili waje kupambana nao na kila siku waliua baadhi ya watu. Wakati huo Mtume (s.a.w.w.) aliniamrisha nisimame na niende kwenye ile ngome. Niliwakabili wapiganaji wao na kuwaua baadhi yao na kuwarudisha nyuma wengine. Walikimbilia kwenye ngome ile na kujificha, kisha wakalifunga lango lake. Nililing’oa lile lango kisha nikaingia ile ngome peke yangu. Hakuna aliyeweza kunipinga na kwenye jambo hili, hakuna yeyote aliyenisaidia ila Allah.”31

Hisia Za Huruma Mwenye Uwanja Wa Vita

Ilipotekwa ngome ya Qamus Bibi Safiah binti Hay bin Akhtab na mwanamke mwingine walitekwa. Bilal aliwapitisha hawa wanawake wawili karibu na maiti za Wayahudi waliouawa kwenye vita vile na akawaleta mbele ya Mtume (s.a.w.w.). Mtume (s.a.w.w.) alipopata taarifa za jambo lile aliamka akaliweka joho lake kichwani kwa Bibi Safiyah na akamtendea mambo yaonyeshayo heshima kwake na akampa mahali maalum pa kupumzikia kule kambini.

Kisha akamwambia Bilal kwa ukali: “Je, umepotewa na hisia za huruma kabisa kiasi kwamba umethubutu kuwapitisha hawa wanawake karibu na maiti za watu wao wapendwa?” Mtume (s.a.w.w.) hakutosheka na hilo tu bali alimchagua Bibi Safiyah kuwa mkewe na kumtendea hivyo akamfidia kwa kuvunjika kwake moyo.

Kutendewa wema alikotendewa Bibi huyu na Mtume (s.a.w.w.) na hisia zake Mtume (s.a.w.w.) za huruma zilikuwa na athari njema mno kwa Bibi huyu kiasi kwamba baadaye alihesabiwa kwamba alikuwa moja wa wakeze wapenzi zaidi na waaminifu, naye alilia zaidi ya watu wengine pale Mtume (s.a.w.w.) alipokaribia kufariki dunia.32

Kananah Bin Rabi’ Auwawa

Tangu pale Wayahudi wa kabila la Bani Nuzayr walipofukuzwa kutoka Madina na wakaenda kuishi Khaybar walianzisha kisanduku cha watu wote kwa ajili ya mambo ya ustawi wa jamii na gharama za vita na kwa ajili ya kulipa dia kwa ajili ya wale waliouawa mikononi kwa Bani Nuzayr. Taarifa alizozipata Mtume (s.a.w.w.) zilionyesha kwamba pesa hizi zilikuwa zikitawaliwa na Kananah, mumewe Bibi Safiyah. Mtume (s.a.w.w.) alimwita Kananah na akamwuliza kuhusu kisanduku kile.

Hata hivyo, yeye alikataa kuwa na taarifa juu ya kitu kile. Hivyo, Mtume (s.a.w.w.) akatoa amri ya kwamba Kananah abakie mpaka pale zitakapopatikana taarifa zaidi juu ya kisanduku kile. Wale walioteuliwa kuzitafuta fedha zile waliendelea kufanya uchunguzi. Hatimaye mtu mmoja akasema: “Ninadhani hazina hii itakuwa imefichwa mahali pale (kwenye gofu), kwa sababu nimemwona Kananah akiitembelea sehemu ile mara kwa mara wakati ule wa vita na baada ya hapo.” Mtume (s.a.w.w.) akamwita tena Kananah na akamwambia: “Inasemekana kwamba kile kisanduku kiko mahali pale (Akapataja). Kama hazina ile ikipatikana hapo utauawa.” Kananah akakana tena kwamba hana taarifa yoyote juu ya jambo lile. Mtume akaamrisha sehemu ile ichimbuliwe na ile hazina ya Bani Nuzayr ikaangukia mikononi mwa askari wa Uislamu.

Sasa ikawa muhimu kumwadhibu Kananah kwa vitendo vyake. Ukiachilia mbali kuficha taarifa juu ya jambo hili (yaani kule kuelewa ilipokuwa ile hazina) vile vile Kananah alimuua afisa mmoja wa Uislamu kwa jinsi ya kiwoga (yaani alimtupia jiwe kubwa kwa ghafla kichwani mwa Mahmud bin Maslamah, aliyefariki dunia palepale). Ili kulipiza kisasi na vilevile kuwaadhibu Wayahudi ili kwamba wasije tena wakafanya hadaa na uwongo kwa serikali ya Uislamu hapo baadaye, Mtume (s.a.w.w.) alimkabidhi yule Kananah kwa ndugu wa yule afisa wa Kiislamu, na nduguye marehemu akamuua. Kananah alikuwa mtu wa mwisho kuuawa kwa kumuua afisa maafuru wa Uislamu.

Nyara Za Vita Zagawanywa

Baada ya kuziteka ngome za adui na kuwanyang’anya Wayahudi silaha na kukusanya nyara, Mtume (s.a.w.w.) aliamrisha ya kwamba nyara zote ziletwe mbele yake katika sehemu fulani maalum. Kama ilivyoamrishwa na Mtume (s.a.w.w.) mtu mmoja alitangaza miongoni mwa askari wa Uislamu: “Ni wajibu juu ya kila Mwislamu kurudisha kwenye hazina ya Umma kila nyara aliyonayo japo iwe ni uzi na sindano, kwa sababu kuvunja uaminifu ni jambo la aibu na itakuwa moto kwa upande wa roho yake katika Siku ya Hukumu.”

Wale viongozi halisi wa Uislamu wamekuwa wakali mno katika mambo ya amana kiasi kwamba wamekuhesabu kurudisha amana kuwa ni moja ya ishara ya imani, na kuvunja ahadi kuwa ni moja ya dalili za unafiki.33

Hivyo basi pale mali iliyoibiwa ilipopatikana kwenye mali zilizoachwa na askari mmoja aliyefariki dunia, Mtume (s.a.w.w.) hakumsalia askari yule sala ya maiti. Maelezo marefu ya tukio hili yako kama ifuatavyo: “Siku ya kuondoka pale Khaybar, mshale wa ghafla ulimpiga mtumwa mmoja aliyekuwa akifunga kitundu anachokalia Mtume (s.a.w.w.) juu ya mgongo wa ngamia anaposafiri, na mtumwa yule akafa palepale.

Waliteuliwa watu wa kulichunguza jambo lile. Watu wale waliifanya kazi ile lakini hawakupata jibu. Watu wote wakasema: “Na abarikiwe kupata Pepo.” Hata hivyo, Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Mimi siafikiani nanyi juu ya jambo hili, kwa kuwa joho lililoko mwilini mwake ni sehemu ya hizi nyara za vita naye alivunja uaminifu, na litamzunguka likiwa katika hali ya moto katika Siku ya Hukumu.” Wakati ule ule mmoja wa masahaba wa Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Nimechukua jozi moja ya vigwe vya viatu kutoka kwenye nyara bila ya ruhusa.”
Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Virudishwe au sivyo vitafungwa miguuni mwako katika Siku ya Hukumu vikiwa katika umbo la moto!”34

Ni mahali hapa ambapo malengo ya siri ya mustashirik wenye upendeleo hudhihirika, kwa sababu, wanazisimulia vita za Uislamu kuwa ni utekaji nyara, lakini huyafumbia macho yale malengo ya kiroho, kwa kuwa aina hii ya nidhamu haiwezi kuelezeka kutoka kwenye kundi lenye kuteka nyara. Haiwezekani kwa kiongozi wa jumuia ya wateka nyara kuufanya uaminifu kuwa ni dalili ya imani imara na kuwafundisha askari wake katika hali ambayo aweze kuwazuia kuchukua japo ugwe wa kiatu kutoka kwenye mali ya umma.

Msafara Utokao Ethiopia; Nchi Ya Kumbukumbu

Kabla ya kwenda Khaybar, Mtume (s.a.w.w.) alimtuma ‘Amr bin Umayyah kwenye baraza la Negus. Lengo la kumpeleka mjumbe wake kwenye lile baraza kule Ethiopia lilikuwa kwamba aufikishe ujumbe wa Mtume (s.a.w.w.) kwa yule Mfalme wa Ethiopia na kumwomba awapatie masurufu ya safari ya Waislamu wote ili watoke Ethiopia na kurudi nyumbani. Yule Negus aliwatayarishia jahazi mbili. Zile jahazi za Muhajiriin zilitia nanga kwenye pwani ya Madina. Waislamu wakapata habari kwamba Mtume (s.a.w.w.) amekwenda Khaybar hivyo nao wakaja Khaybar bila ya kuchelewa. Wale wasafiri watokao Ethiopia walifika Khaybar wakati zile ngome zilipokuwa tayari zimeshatekwa.

Mtume (s.a.w.w.) akaenda mbele hatua kumi na sita kumlaki Ja’far bin Abu Twalib, akalibusu paji la uso wake na akasema: “Sijui ni kipi nikifurahie zaidi kukutana nawe tena baada ya kuachana kwa miaka mingi au kwa Allah kutufungulia ngome za Wayahudi kupitia kwenye mikono ya kaka yako Ali?” Kisha akaongezea kusema: “Leo ninataka kukupa zawadi” Watu wakafikiria kwamba zawadi ile itakuwa zawadi ya kimaada ya kawaida kama vile dhahabu au fedha.

Mara kwa ghafla Mtume (s.a.w.w.) akakivunja kimya kilichotanda pale na akafundisha dua ambayo hapo baadae ilifahamika kwa jina la ‘Dua ya Ja’far Tayyaar.’35

Idadi Ya Waliouwawa

Waliouawa kwa upande wa Waislamu katika vita hivi hawakuzidi watu ishirini. Waliouwawa katika upande wa Wayahudi walikuwa ni watu tisini na watatu kufuatana na ilivyoandikwa kwenye vitabu vya historia.36

Msamaha Wakati Wa Ushindi

Wakati watu wakubwa na wachamungu wanaposhinda huonyesha huba na huruma kwa wale maadui zao waliowashinda na wasio na msaada. Mara tu baada ya adui kusalimu amri wao huonyesha huruma na huepuka kumlipizia kisasi na kutokuwa na mfundo dhidi yake.

Baada ya kutekwa kwa Khaybar yule kiongozi mkuu wa Waislamu alionyesha hisia za huruma kwa watu wa sehemu ile (bila kujali ukweli wa kwamba walikitumia kiasi kikubwa cha fedha katika kuwachochea Waarabu waabudu masanamu kupigana dhidi yake na kuuweka mji wa Madina kwenye mashambulizi na uwezekano wa kuanguka), na akakubali matakwa yao kwamba wangeliweza kubakia Khaybar na wakaendelea kuyamiliki mashamba na miti ya eneo lile kwa masharti ya kwamba watalipa nusu ya mazao kwa Waislamu.37
Si hilo tu, bali kufuatana na nukuu ya Ibn Hisham mwenyewe,38 Mtume (s.a.w.w.) aliitoa rai hii mwenyewe na kwa rai hii akawapa Wayahudi uhuru wa kuendelea na kilimo, kupanda na kukuza miti.

Mtume (s.a.w.w.) angeliweza kuwakata vichwa wote au kuwatoa pale Khaybar au kuwalazimisha kusilimu. Hata hivyo, kinyume na fikira za mustashirik wenye upendeleo walio watumishi na askari wa kinadharia ya ukoloni, ambao hudhania kwamba Uislamu ulienezwa kwa ncha ya upanga, yeye Mtume (s.a.w.w.) hakutenda mambo ya aina hii bali aliwapa hifadhi na akawaruhusu kuifuata misingi, kanuni, taratibu na ibada za dini yao.

Kama Mtume (s.a.w.w.) alipigana vita dhidi ya Wayahudi wa Khaybar, hii ilitokana na ukweli uliopo kwamba Khaybar na wakazi wake ilikuwa kitovu cha hatari kwa Uislamu na daima ilishirikiana na waabudu masanamu ili kuipindua ile serikali mpya ya Waislamu.

Hivyo basi, Mtume (s.a.w.w.) alilazimika kupigana nao na kuwanyang’anya silaha ili kwamba waweze kujishughulisha na kilimo kwa uhuru kabisa na kuweza kuzitekeleza ibada zao chini ya utawala wa serikali ya Kiislamu. Au la, maisha yangalikuwa magumu mno kwa Waislamu na kuenea kwa Uislamu kungelisimama.

Kama alitwaa Jizyah kutoka kwao, ni kwa sababu ya kwamba walipatiwa ulinzi chini ya serikali ya Kiislamu na ilikuwa wajibu juu ya Waislamu kuuhami uhai na mali zao. Na kufuatana na kasma iliyokasimiwa kwa makini, kodi iliyo wajibu kwa Mwislamu iliizidi Jizyah ambayo Wayahudi na Wakristo walitakiwa kulipa. Waislamu waliwajibika kulipa Zaka na Khumsi, na katika nyakati nyingine vilevile walitakiwa kulipa malipo kutokana na mali zao ili kutimiza mahitaji ya serikali.

Kwa kulinganishwa na hilo, Wayahudi na Wakristo ambao waliishi chini ya bendera ya Uislamu na wakazifaidi haki za pamoja na za mtu binafsi, iliwabidi walipe kwa njia ya Jazyah kama walivyofanya Waislamu kwa usalama wa bendera hii.

Utozaji wa Jizyah ya Kiislamu ni jambo lililo tofauti na kutoa ushuru. Mwakilishi wa Mtume (s.a.w.w.) aliyekuwa akiteuliwa kila mwaka kukasimia na kugawa (katika nusu mbili) mazao ya Khaybar, alikuwa mtu mchamungu na mwadilifu, aliyepata kupendwa na Wayahudi kwa kutopendelea kwake na uadilifu wake. Mtu huyu alikuwa ni Abdullah Rawaha, ambaye baadaye aliuwawa katika Vita vya Muta. Alikuwa akiyakasmia mafungu ya Waislamu kutokana na mazao ya Khaybar na wakati mwingine Wayahudi walifikiria kwamba alikuwa akikosea katika kukasimia, na akawa anatia alama ya kujulisha kwenye (lile fungu la Waislamu) zaidi (ya vile ipasikavyo kuwa). Alikuwa kila mara akisema: “Niko tayari kukirudisha kwenu kile kiasi kilichokasimiwa, na kile kilichobakia kiwe ndio mali ya Waislamu.”

Wayahudi waliusifu uadilifu wake kwa kusema: “Mbingu na nchi hutulia chini ya kivuli cha usawa na uadilifu wa aina hii.”39

Zile nyara za vita zilipokusanywa kipande cha Taurat kiliangukia mikononi mwa Waislamu. Wayahudi wakamwomba Mtume (s.a.w.w.) kwamba warudishiwe kipande kile. Mtume (s.a.w.w.) alimwelekeza yule mtu aliyekuwa akiingoza hazina ya umma kuirudisha ile sehemu ya Taurati kwa Wayahudi.

Tabia Ya Ukaidi Ya Wayahudi

Bila kujali upole huu wa hali ya juu, Wayahudi hawakuuacha ukaidi na makri zao. Waliweka mitego kwa ajili ya kumvamia Mtume (s.a.w.w.) na masahaba zake na wakapanga makri dhidi yao. Hapa tunanukuu mifano miwili ya uvunjaji wao wa ahadi:

1. Watu fulani walimchochea mwanamke mmoja aliyeitwa Zaynab, aliyekuwa mke wa mmoja wa watu watukufu miongoni mwa Wayahudi, kukitia sumu chakula cha Mtume (s.a.w.w.). Yule mwanamke akamtuma mtu aende kwa mmoja wa masahaba wa Mtume (s.a.w.w.) na kumwuliza ni sehemu gani ya nyama ya kondoo aipendayo sana? Mtume (s.a.w.w.) akamjibu kwamba chakula chake akipendacho sana ni mkono wa kondoo. Zaynab akambanika yule kondoo na nyama yote akaitia sumu, Kisha akaipeleka kwa Mtume (s.a.w.w.) ikiwa ni zawadi. Mtume (s.a.w.w.) alipoweka kinywani finyango ya kwanza alihisi kwamba ilitiwa sumu. Hivyo upesi sana akaitema.

Hata hivyo, Bishr bin Baraa’ Ma’rur, aliyekuwa akila nyama ile na Mtume (s.a.w.w.) alikula finyango nyingine zaidi. Bila ya kujua akafariki dunia baada ya muda fulani. Mtume (s.a.w.w.) aliamrisha kwamba aitwe Zaynab mbele yake. Alitoa sababu za kitoto na kusema: “Umeichafua hali ya kabila letu. Nilifikiria kwamba kama wewe ni mtawala utakufa kwa sumu ile na kama u mtume wa Allah kweli, bila shaka utaitambua na utaacha kuila nyama ile.” Mtume (s.a.w.w.) alimsamehe vile vile hakuwatolea madai wale watu waliomchochea Zaynab kulitenda kosa lile.

Hata hivyo, kama kitu cha aina hii kingalitokea kwa mtawala mwingine asiyekuwa Mtume, angaliwaua bila ya huruma wale wakosefu au angaliwahukumu vifungo virefu.40

Kutokana na malengo haya maovu ya yule mwanamke wa Kiyahudi wengi wa masahaba wa Mtume (s.a.w.w.) nao hawakumwamini yule mwanamke wa Kiyahudi Bibi Swafiyah ambaye sasa amekuwa mkewe (s.a.w.w.), na wakafikiria ya kwamba inawezekana kwamba atajaribu kuudhuru uhai wake wakati wa usiku.

Hivyo, Abu Ayub Ansari alichukua jukumu la kulilinda hema la Mtume (s.a.w.w.) kule Khaybar pamoja na siku ya kurejea Madina, ingawa Mtume (s.a.w.w.) hakutambua ya kwamba masahaba wanamhurumia. Hivyo, Mtume (s.a.w.w.) alipotoka mle hemani asubuhi alimwona Abu Ayub akilizunguka zunguka huku akiwa ameufuta upanga mkononi mwake. Mtume (s.a.w.w.) alipouliza sababu ya kufanya vile ndipo alipomjibu: “Dalili za ushupavu wa kidini na ukafiri bado hazijafutika kutoka moyoni mwa mwanamke huyu (Swafiyah) ambaye hivi sasa yu mmoja wa wakezo, nami nina imani ndogo katika nia yake. Hivyo nilikuwa nikilizunguka zunguka hema lako tangu usiku hadi asubuhi ili kulinda uhai wako.” Mtume (s.a.w.w.) alimshukuru kwa zile hisia za huruma za huyu rafiki wake wa tangu kale na akamwombea dua.41

2. Safari moja Abdullah bin Sahl aliteuliwa na Mtume (s.a.w.w.) kuyasafirisha mapato ya Khaybar kutoka pale na kuyapeleka Madina. Alipokuwa akiifanya kazi hii alishambuliwa na kikundi cha Wayahudi ambacho hakikutambulika. Matokeo ya shambulizi hili ni kwamba shingo yake ilijeruhiwa vibaya sana. Alianguka chini na akafariki dunia. Kile kikundi cha washambuliaji kikaitupa maiti yake kwenye bwawa.

Wazee wa Kiyahudi waliwatuma watu kwa Mtume (s.a.w.w.) ili kumpasha habari za kifo kile kisichoeleweka cha wakala wake, wasichojua kimesababishwa na nani. Ndugu wa yule aliyeuwawa aliyeitwa Abdur Rahman bin Sahl alimjia Mtume (s.a.w.w.) pamoja na binamu yake na kumwarifu juu ya tukio lile. Yule ndugu wa yule marehemu alitaka kufanya mazungumzo juu ya jambo lile, lakini kwa vile alikuwa ndiye mdogo zaidi miongoni mwa wale waliokuwapo, Mtume (s.a.w.w.) aliidokeza moja ya desturi za kijamii za Uislamu na akasema: “Kabir, KabirYaani aache watu wakubwa wazungumze kwanza.

“Kama mnaweza kumuainisha muuwaji wa Abdullah na mkaapa kwamba yeye ndiye muuwaji, mimi nitamkamata na kumweka mikononi mwenu.” Hata hivyo wao walionyesha uchamungu na unyoofu na ingawa walishikwa na ghadhabu lakini hawakuuficha ukweli na wakasema:
“Hatuwezi kumtambua yule muuwaji.” Hapo Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Je, mnakubali kwamba Wayahudi waeleze kwa kiapo kwamba wao hawakumuuwa na kwa msingi wa kiapo hicho waachiwe huru kutokana na kifo cha Abdullah?” Hata hivyo, walijibu kwamba mapatano na viapo vya Wayahudi haviwezi kuaminika. Katika mazingira haya Mtume (s.a.w.w.) aliamrisha iandikwe barua kwenda kwa wazee wa Wayahudi ikiwaambia kwamba maiti ya Mwislamu imepatikana kwenye eneo lao na hivyo basi wao hawana budi kulipa dia kutokana na sababu hii.

Katika jibu lao, Wayahudi waliapa kwamba katu wao hawakumuuwa Abdullah na vile vile kwamba hawamtambui yule muuwaji. Mtume (s.a.w.w.) alitambua ya kwamba jambo lile limeifikia hatua ya kukwama. Hivyo basi, ili kuzuia kurudia umwagaji damu, yeye mwenyewe alilipa dia kwa ajili ya Abdullah.42 Kwa kitendo hiki aliwaonyesha tena Wayahudi kwamba hakuwa mpenda vita na kama angelikuwa mtawala wa kawaida angelifanya tukio la Abdullah kama shati la Uthman na kuuwa idadi fulani ya Wayahudi.

Hata hivyo, kama vile Qur’ani imwitavyo, yeye alikuwa ni Mtume wa rahma na mdhihiriko wa huruma ya Allah, naye hakuuchomoa upanga wake mpaka pale alazimikapo kufanya hivyo.

Wayahudi Watolewa Khaybar

Kukithiri kwa Wayahudi hakukukomea kwenye matukio haya tu bali vilevile waliendelea kuwasumbua Waislamu kila mara kwa makri zao mbalimbali.

Mwishowe kwenye zama za Ukhalifa wa Umar mwanawe Abdullah aliyekwenda Khaybar akifuatana na watu wengine, ili kwenda kufanya mapatano, aliteswa na Wayahudi. Khalifa alipata taarifa za tukio lile na akawaza jinsi ya kulitatua tatizo lile. Hivyo, akiitegemea hadith moja ya Mtume (s.a.w.w.) iliyonukuliwa na baadhi ya watu, aliwaambia masahaba wa Mtume (s.a.w.w.): “Yeyote yule ambaye anataka kulipwa deni lake kutoka kwa watu wa Khaybar basi na afanye hivyo, kwani nitatoa amri ya kwamba watoke sehemu ile.”

Mara tu baada ya hapo Wayahudi wa Khaybar walipigwa marufuku kukaa pale kutokana na kukithiri kwa matendo yao maovu waliyokuwa wakiyatenda mara kwa mara, nao wakaitoka Rasi ya Uarabuni.43

Uongo Uliothibitishwa Na Nia Yake

Mfanyabiashara mmoja aliyeitwa Hajjaj bin Il?t alikuwako pale Khaybar. Alikuwa kafanya biashara na watu wa Makka. Utukufu wa Uislamu na mapenzi na huruma alizozionyesha Mtume (s.a.w.w.) kwa taifa lake kaidi (yaani Wayahudi) viliuangaza moyo wake na akamjia Mtume (s.a.w.w.) na akasilimu. Kisha akapanga mpango ili kulipwa deni lake kutoka kwa watu wa Makka. Aliuingia mji wa Makka kupitia kwenye lango moja na akaona kwamba machifu wa Waquraishi walikuwa wakisubiri taarifa na walikuwa na shauku kuu juu ya matokeo ya Khaybar.

Wote wakamzunguka ngamia wake na wakaulizia hata bila ya subira kuhusu hali ya Muhammad, aliwajibu akisema: “Muhammad ameshindwa vibaya sana na masahaba zake wameuwawa au kutekwa. Yeye mwenyewe (Mtume) ametekwa na machifu wa Wayahudi na wameamua kumleta Makka na kumnyonga mbele ya macho ya Waquraishi.” Taarifa hii ya uwongo iliwaridhisha sana sana.

Kisha alirejea kwa watu na kusema: “Kutokana na taarifa hii njema, ninakuombeni mnilipe deni langu mapema iwezekanavyo ili kwamba niende Khaybar mapema kuliko wafanyabiashara wengine ili niweze kununua watumwa.” Wale watu waliodanganyika wakamlipa deni lake katika muda mfupi sana.

Kuenea kwa taarifa ile kulimkera sana Abbas ami yake Mtume (s.a.w.w.) na akataka kukutana na Hajjaj. Hata hivyo, alimpiga ukope Abbas, kwa maana ya kwamba atamweleza hali halisi baadae. Muda mfupi kabla ya Hajjaj kutoka, alikutana na huyu ami yake Mtume (s.a.w.w.) kwa siri na akasema: “Nimesilimu na mimi nilipanga mpango huu ili niweze kulipwa madeni yangu tu. Taarifa zilizo sahihi ni kwamba siku niliyotoka Khaybar ngome zote zilikuwa zimeshatekwa na Waislamu na binti wa kiongozi wao aliyeitwa Hay bin Akhtab (Swafiyah) amekamatwa na amekuwa mkewe Mtume. Tafadhali ufanye ukweli huu ufahamiwe na watu baada ya siku tatu za kuondoka kwangu hapa.”

Baada ya siku tatu Abbas alivaa nguo zake nzuri zaidi, akajipaka manukato ya bei ghali zaidi na akauingia msikiti akiwa ameshika fimbo mkononi mwake na akaanza kufanya Tawaaf ya Kaabah. Waquraishi walishangazwa kuliona vazi la Abbas lililoonyesha shangwe na furaha kwa kuwa walifikiria kwamba kutokana na msiba uliomwangukia mwana wa kaka yake angalivaa nguo ya msiba. Hata hivyo, aliwaondolea ule mshangao wao kwa kusema: “Ile taarifa aliyokupeni Hajjaj ilikuwa ni ujanja wa kupata kulipwa madeni yake. Yeye amesilimu na ametoka Khaybar wakati Muhammad akiwa tayari kaishapata ushindi mkubwa, na Wayahudi wameshanyang’anywa silaha, na baadhi yao wameuwawa na wengine wamefanywa mateka.” Machifu wa Waquraishi wakasikitika sana walipoisikia taarifa hii na mara tu baada ya hapo walizipata taarifa zile zile (kutoka kwa watu wengine vilevile).44

 • 1. Siiratu Halabi, Juz 3, uk. 36; Tarikhu Yaa’qubi, Juz. 2, uk. 46.
 • 2. Wakati mwingine inasemekana kwamba, ingawa Mtume (s.a.w.w.) aliitumia mbinu hii ya kujificha kwa ukamilifu wake, yule chifu wa Wanafiki (Abdullah Sallul) aliwaarifu Wayahudi wa Khaybar juu ya mpango ule na akawashauri kwamba, zaidi ya kujihami kutoka juu ya ngome zao zile, vile vile wapigane na Waislamu nje ya ngome zao.
 • 3. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 330.
 • 4. Amaalit-Tusi, uk. 164.
 • 5. Tarikhul Kamil, Juz. 2, uk. 147.
 • 6. Siraatu Halabi, uk. 38.
 • 7. Siiratu Halabi, Juz. 3, uk. 39.
 • 8. Usudul Ghabah, Juz. 4, uk. 334.
 • 9. Siiratu Halabi, Juz. 3, uk. 40.
 • 10. Siiratu Ibn Hishamu, Juz. 3, uk. 342.
 • 11. Siiratu Ibn Hishamu, Juz. 3, uk. 344.
 • 12. Siiratu Ibn Hishamu, Juz. 2, uk. 335.
 • 13. Badhi ya wanahistoria wanaamini kwamba ngome hizi zilichukuliwa kwa amani kwa njia ya mapatano na tukio linalosimuliwa hivi sasa, linahusiana na ngome ya Qamus au Nastat.
 • 14. Tarikhut-Tabari, Juz. 2, uk. 300.
 • 15. Majma’ul Bayaan, Juz. 9, uk. 120 Siiratu Halabi, Juz. 2, uk. 43.
 • 16. Hadithi ya kukimbia kwa wale makamanda wawili ilimhuzunisha sana Ibn Abil Hadid, mwanahistoria mkuu wa Uislamu. Anasema mwenye Qaswida yake maarufu: “Japo nisahau kila kitu, siwezi kuisahau hadithi ya hawa makamanda wawili, kwa sababu walimwendea adui kwa panga mikononi mwao, lakini walimgeuzia adui migongo yao na wakakimbia, ingawa walijua kwamba ni haramu kuikimbia Jihadi. Waliichukua ile bendera kuu ya Uislamu na kuipeleka kwa adui yule, ingawa, kwa kweli fungu lao lilikuwa fedheha na uduni. Mtu mwepesi kutoka miongoni mwa dhuria wa Nabii Musa aliwarudisha nyuma. Yeye alikuwa yu mtu mrefu aliyekuwa akimrekebu farasi mwenye mbio.
 • 17. Sayidna Ali (a.s.) aliopoyasikia haya maneno ya Mtume (s.a.w.w.) mle hemani, alisema kwa tamaa yenye nguvu zaidi akilini mwake: “Ee Mola! Kama ukimpa mtu hakuna wa kumnyima; na kama ukimnyima mtu yeyote hakuna wa kumpa.” (Siiratu Halabi, Juz. 3, uk. 41)
 • 18. Maneno yaliyotumiwa kwenye Tarikhut-Tabari kwa jambo hili ni Fa tataawala Abu Bakr wa Umar.
 • 19. Bihaarul Anwwaar, Juz. 21, uk. 28.
 • 20. Sahih Muslim, Juz. 5, uk. 195; Sahih Bukhari, Juz. 5, uk. 22-23.
 • 21. Tarikhut-Tabari, Juz. 2, uk. 94.
 • 22. Tarikhu Yaaqubi, Juz. 2, uk. 46.
 • 23. Dhiraa moja ni kama sentimita 37 hivi.
 • 24. Al-Irshaad, uk. 59.
 • 25. Bihaarul Anwwar, Juz.21, uk. 21.
 • 26. Siiratu Ibn Hisham, Juz.2, uk. 65.
 • 27. Siiratu Halabi, Juz. 3, uk. 44.
 • 28. Sahih Muslim, juz. 7, uk. 120.
 • 29. Siiratu Halabi, Juz. 3, uk. 41.
 • 30. Siiratu Halabi, Juz. 3, uk. 47.
 • 31. Khisaal, Juz. 2, uk. 16.
 • 32. Tarikhut-Tabari, Juz. 3, uk. 302.
 • 33. Wasaa’ilus- Shi’ah, Sura ya Jihad bin-Nafs, Hadith ya 4.
 • 34. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 3, uk. 339.
 • 35. Khisaal, Juz. 2, uk. 86; Furuul Kafi, juz. 1, uk. 129.
 • 36. Bihaarul Anwaar, Juz. 21, uk. 32.
 • 37. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 1, uk. 327.
 • 38. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 1, uk. 356
 • 39. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 354; Furu’i Kaafi, Juz. 1, uk. 405.
 • 40. Inafahamika vema kwamba kwenye ugonjwa wa Mtume (s.a.w.w.) uliomal- izikia kwenye kifo chake, alisema: “Maradhi haya wametokana na athari za chakula kilichotiwa sumu ambacho yule mwanamke wa kiyahudi aliniletea baada ya kutekwa kwa Khaybar” Ingawa Mtume (s.a.w.w.) aliitema finyango ya kwan- za, ile sumu ya hatari ilichanganyika mno na mate yake kiasi kwamba iliidhuru afya yake.
 • 41. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 339-340; Bihaarul Anwwar, Juz. 21, uk. 6.
 • 42. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 356.
 • 43. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 3, uk. 356.
 • 44. Bihaarul An’war, Juzuu 21, uk. 34.