Sura Ya 44: Hadith Ya Fadak

Nchi iliyoendelea na yenye rutuba ambayo ilikuwa karibu na Khaybar na umbali wa kilometa 140 kutoka Madina na iliyokuwa ikifikiriwa kuwa ngome yenye nguvu ya Wayahudi wa Hijaz, baada ya zile ngome za Khaybar, ilikuwa ikiitwa kijiji cha Fadak. Baada ya kuivunja nguvu ya Wayahudi wa Khaybar, Wadi’ul Qurra’ na Taym?’, na kuzijaza sehemu hizo kwa majeshi ya Uislamu, pengo pekee lililoachwa kwenye upande wa Kaskazini wa Madina lilikuwa ni Fadak.

Sasa Mtume (s.a.w.w.) aliona kwamba aivunje nguvu ya Wayahudi wa eneo la Fadak waliokuwa wakifikiriwa kwamba ni hatari kwa Uislamu na Waislamu. Hivyo akampeleka balozi aliyeitwa Muhit kwa wazee wa Fadak. Yush’a bin Nun aliyekuwa chifu wa kijiji kile aliipendelea amani na kusalimu amri kuliko kupigana, na hatimaye wakazi wa sehemu ile walikubali kumpelekea Mtume (s.a.w.w.) mapato ya kila mwaka na kuishi chini ya ulinzi wa Uislamu na kutofanya makri dhidi ya Waislamu. Serikali ya Uislamu kwa upande wake, ilithibitisha usalama wa eneo lao.

Kwa mujibu wa Uislamu zile sehemu zitekwazo kwa njia ya vita na nguvu za kijeshi ni mali ya Waislamu wote na utawala wake unakuwa mikononi mwa mtawala wa Kiislamu. Hata hivyo, nchi ziangukiazo mikononi mwa Waislamu bila ya kuzitumia nguvu za kijeshi huwa mali ya Mtume (s.a.w.w.) na baada ya kuondoka kwake huwa mali ya Imam (a.s.). Yeye (Mtume s.a.w au Imamu a.s) huwa na mamlaka kamili juu ya nchi hizi na anao uwezo wa kuzitoa zawadi au kuzikodisha. Na moja ya sababu zimfanyazo aweze kuzitumia mali hizi ni kwamba, aweze kuzikabili gharama za halali za jamaa zake kutokana na mali hii kwa njia ya heshima.1

Chini ya msingi huu, Mtume (s.a.w.w.) aliitoa zawadi Fadak kwa binti yake mpenzi, Bibi Fatimah Zahrah (a.s.). Kama vile ambavyo hali ya baadae itakavyoonyesha. Mtume (s.a.w.w.) alikuwa akifikiria mambo mawili pale alipoitoa mali yake hii kuwa zawadi:

1. Kama vile ambavyo mara kwa mara Mtume (s.a.w.w.) alikuwa akieleza, utawala wa Waislamu baada ya kufariki dunia kwa Mtume (s.a.w) ulikuwa ushikwe na Sayyidna Ali Amirul-Mu’minin (a.s.), na kukishika cheo hiki kunamfanya alazimike kuzikabili gharama kubwa. Hivyo basi, Sayyidna Ali (a.s.) angaliweza kuyatumia mapato ya Fadak kwa kadiri iwezekanavyo katika kukihami cheo chake.
Inaweza kuonekana kwamba wale walioshika madaraka ya Ukhalifa walizitambua hatua hizi za tahadhari na hivyo basi wakawanyang’anya watu wa Nyumba ya Mtume (s.a.w.w.) ile Fadak katika siku za awali kabisa za kuyatwaa mamlaka.

2. Lilikuwa ni jambo muhimu kwamba baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.w.) familia yake iliyokuwa na binti yake mpenzi Fatimah Zahrah (a.s.) na wanawe Hasan (a.s.) na Husain (a.s.), ingeliweza kuishi maisha ya heshima na heshima ya Mtume (s.a.w.w.) ikasalimika. Mtume (s.a.w.w.) aliitoa zawadi Fadak kwa binti yake ili kulifikia lengo hili. Wanahadithi na wafasiri wa Qur’ani wa Kishia na baadhi ya wanachuoni wa Sunni wanasema hivi:

“Ilipoteremshwa aya isemayo: “Na mpe aliye jamaa yako haki yake, na masikini na msafiri wala usitumie ovyo kwa fujo” (Sura Israa, 17:26), Mtume (s.aw.w) alimwita binti yake Fatimah na akampa Fadak.”2 Na msimuliaji wa tukio hili ni Abu Saidi Khudri aliyekuwa mmoja wa masahaba zake Mtume (s.a.w.w.) walio maruufu sana.

Wafasiri wote wa Qur’ani wa Kishia na Kisunni wanakubaliana kwamba aya hii iliteremshwa kwa ajili ya jamaa wa karibu zaidi wa Mtume (s.a.w.w.) na maneno ‘aliye jamaa’ yanamhusu zaidi binti yake. Zaidi sana kiasi kwamba mtu mmoja aliye mwenyeji wa Shamu alimtaka Imam wetu wa Nne, Imamu Sajjad (a.s.) ajitambulishe mwenyewe. Imamu (a.s.) alisoma aya tuliyoitaja hapo juu ili kujitambulisha kwa mtu yule. Na ukweli huu ulifahamika vizuri mno kwa Waislamu kiasi kwamba yule mtu wa Shamu alipokuwa akikitikisa kichwa chake katika hali ya kukubali alimwambia Imamu: “Kwa uhusiano maalum ulionao kwa Mtume (s.a.w.w.), aliamrishwa na Allah kukupeni haki yenu.”3

Kifupi ni kwamba wanachuoni wote wa Kiislamu wanaamini kwamba aya hii iliteremshwa kwa heshima ya Bibi Fatimah Zahraa (a.s.) na wanawe. Hata hivyo, swali ni je, wakati wa kuteremshwa kwa aya hii, Mtume (s.a.w.w.) aliitoa Fadak na kumpa binti yake? Wanachuoni wote wa Kishia wanakubaliana kwamba kwa kweli alifanya hivyo, na baadhi ya wanachuoni wa Kisuni pia wanakubaliana nao.

Wakati mfalme Maamun (wa ukoo wa Bani Abbas) alipotaka kuirudisha Fadak kwenye kizazi cha Zahra alimwandikia barua mmoja wa wanahadithi maarufu (aliyeitwa Abdullah bin Musa) ili ampe mwanga juu ya jambo lile. Yeye (Abdullah) aliiandika hadith tuliyoitaja hapo juu (ambayo kwa kweli inalielezea tukio la kuteremshwa kwa aya hii) na akampelekea. Matokeo yake yakawa kwamba yeye, yaani Mamun aliirudisha Fadak kwenye kizazi cha Fatimah.4 Na akamwandikia gavana wake wa Madina, akisema: “Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) aliitoa zawadi Fadak na kumpa binti yake Fatimah. Huu ni ukweli unaokubalika na hakuna tofauti kwayo miongoni mwa kizazi cha Fatimah.”5

Maamun alipokikalia kiti maalum ili kusikiliza malalamiko ya watu, ombi la kwanza lilikuwa ni lalamiko moja ambalo mwandishi wake alijitambulisha kwa jina la mtetezi wa Bibi Fatimah (a.s.), Maamum alilisoma ombi lile akalia kidogo na akasema: “Ni nani huyu mtetezi wake?” Mzee mmoja alisimama na kujitambulisha kuwa ndiye huyo mtetezi. Kisha lile baraza la kisheria liligeuka na kuwa kikao cha mdahalo baina ya mzee yule na Maamun. Hatimaye Maamun alitambua kwamba ameshindwa. Hivyo alimwamrisha Jaji mkuu kuandika mkataba wenye kichwa cha habari: “Kuirudisha Fadak kwenye kizazi cha Zahra.” Mkataba ule uliandikwa na ukapata idhini ya Maamun.

Katika wakati huo Da’bal Khuzaa’i aliyekuwepo pale wakati wa mdahalo ule alisimama na akazisoma beti fulani za utenzi.6

Ili kuthibitisha kwamba Fadak ilikwua ni mali ya Bibi Fatimah Zahra (a.s.) Mashia hawahitaji ushahidi ulioelezwa hapo juu, kwa sababu mtu aliye mkweli zaidi katika Uislamu, Sayyidna Ali Amirul-Mu’minin (a.s.) ameutaja ukweli huu waziwazi kwenye barua aliyomwandikia Uthman bin Hunayf, Gavana wa Basra. Anaandika hivi: “Ndio! Miongoni mwa vile vilivyoko chini ya mbingu mali ihusianayo nasi na tuliyonayo ni Fadak. Watu fulani waliona kijicho. Baadhi ya watu wakuu hawakulikataza jambo hili (la kuinyakua Fadak kutoka kwetu) kutokana na maslahi yao. Na Allah ndiye Hakim bora zaidi.” Je inawezekana kutia shaka yoyote ile juu ya jambo hili baada ya kauli hii ya dhahiri?

Hadith Ya Fadak Baada Ya Mtume (S.A.W.W)

Baada ya kufariki dunia kwa Mtume (s.a.w.w.) binti yake mpenzi alizuiwa umiliki wake wa Fadak kutokana na matilaba ya kisiasa, na watendaji na wafanyakazi wa serikali walimtoa kwenye baraza la Khalifa alilokwenda kupeleka dai la Fadak. Hivyo basi aliamua kuichukua haki yake kutoka kwa Khalifa yule kwa kutumia hatua za kisheria.

Kwanza kabisa kijiji cha Fadak kilikuwa katika umiliki wake, na umiliki huu haswa ulikuwa ni dalili ya kuwa yeye ndiye mwenye mali ile. Hata hivyo, kinyume kabisa na vipimo vyote vya sheria ya Kiislamu, Khalifa yule alimuomba atoe ushahidi wakati wote ilihali tunajua kwamba mwenye kumiliki kitu hatakiwi kutoa ushahidi.

Hapo alilazimika kuwapeleka mashahidi mbele ya Khalifa ambao ni Sayyidna Ali (a.s.) na mwanamke mmoja aliyeitwa Ummi Ayman (ambaye kuhusiana naye Mtume (s.a.w.w.) alithibitisha kwamba atakwenda Peponi) na (kama ilivyonukuliwa na Bal?dhuri kwenye kitabu chake kiitwacho Futuhul Buladn, uk. 43), na Rabah mtumwa wa Mtume (s.a.w.w.) aliyepewa uungwana.

Hata hivyo, kutokana na maslahi fulani, yule Khalifa hakuukubali ushahidi wao na hatimaye yule binti wa Mtume (s.a.w.w.) alinyimwa mali ile ambayo baba yake alimpa ikiwa ni zawadi yake. Kwa mujibu wa Aya ya Tohara (Sura al-Ahzab, 33:33), Bibi Zahrah, Sayyidna Ali, na wana wao Hasan na Husein wamesafika kutokana na aina yote ya uchafu (ikiwemo kusema uongo), na kama aya hii itachukuliwa na kuhusishwa vilevile wake wa Mtume (s.a.w.w.) utumikaji wake (aya hii) kwa binti wake ni wa uhakika kabisa. Hata hivyo, kwa bahati mbaya hali hii ya mambo nayo ilikataliwa, na Khalifa wa wakati ule hakulikubali dai lake.7

Hata hivyo, wanachuoni wa Kishia wanaamini kwamba hatimaye Khalifa aliyakubali maoni ya yule binti wa Mtume (s.a.w.w.) na akaandika hati ionyeshayo kwamba Fadak ilikuwa ni mali yake na akairudisha kwake. Lakini alipokuwa njiani rafiki wa tangu kale wa Khalifa yule alibahatika kukutana naye na akapata kuyatambua yaliyokuwamo kwenye hati ile.

Aliichukua hati ile kutoka kwake na kuileta kwa Khalifa na kumwambia: “Kwa kuwa Ali ndiye mnufaika katika kesi hii, ushahidi wake haukubaliki, na Ummi Ayman kwa vile ni mwanamke, ushahidi wake naye hauna thamani.” Kisha akaipasua hati ile mbele ya Khalifa.8

Halabi, mwandihsi wa Kisuni wa maisha ya Mtume (s.a.w.w.) aliye maarufu sana anatoa maelezo mengine ya tukio hili, na anasema: “Khalifa alikubali umiliki wa Fatima (a.s.).

Mara kwa ghafla Umar alitokea pale na akauliza: “Hati hii ni ya nini?” Yule Khalifa akajibu akasema: “Nimethibitisha umiliki wa Fadak kwa Fatimah katika hati hii.” Umar akasema: “Wewe unahitaji mapato yatokanayo na Fadak. Kama kesho waabudu masanamu wa Uarabuni wakiamka dhidi ya Waislamu, utazikabili gharama za vita kutoka wapi?” Kisha akaishika hati ile mkononi mwake na akaipasua pasua.”9

Hapa ndipo mahali ambapo mtu huukubali ukweli uliotajwa na mwanatheolojia mmoja wa Kishia, ambaye alisimulia kwamba Ibn Abil Hadid alisema: “Nilimwambia mwanatheolojia mmoja wa Kishia aliyeitwa Ali bin Naqi: Kijiji cha Fadak hakikuwa kikubwa sana, na sehemu ndogo kama hiyo iliyokuwa na mitende michache tu hivi, hakikuwa muhimu mno kiasi kwamba wapinzani wa Fatimah wakitamani.” Alisema katika jibu lake: “Hapa umekosea. Idadi ya mitende ya sehemu ile haikuwa kidogo kama miti iliyoko Kufah hivi sasa.

Hakika familia ya Mtume (s.a.w.w.) ilinyang’anywa ardhi hii yenye rutuba ili Ali Amirul-Mu’minin asije akayatumia mapato ya ardhi hii katika kufanya kampeni dhidi ya Khalifa; hivyo basi, sio tu kwamba walimnyima Fatimah Fadak, bali vilevile waliinyima familia nzima ya Bani Hashim na kizazi cha Abdul Muttalib haki zao za kisheria (khums; yaani 1/5 ya ngawira) kwa sababu watu ambao maisha yao wanaishi katika hali ya matatizo ya kiuchumi hawafikirii kuzibadili hali zilizopo.”10

Na kisha mwandishi huyo anainukuu sentensi tunayoinukuu hapa chini, itokayo kwa mmoja wa waalimu maarufu wa Madrasatul Gharbi Baghdad Iraq, aliyeitwa Ali bin F?ruqi. Anasema: “Nilimwambia: Je yule bintiye Mtume (s.a.w.w.) alikuwa mkweli katika kulifanya dai hilo?” Akasema: “Ndio.” Nikasema: “Je Khalifa alitambua kwamba yeye alikuwa ni mwanamke mkweli?” Akasema: “Ndio.”

Nikasema: “Kwa nini Khalifa hakumpa kile chenye kukubalika kwamba ni haki yake?” Wakati huu yule mwalimu alitabasamu na akasema kwa heshima kuu: “Kama angeliyakubali maneno yake katika siku ile, na akairudisha Fadak kwake kwa sababu ya yeye kuwa yu mwanamke mkweli, na bila ya kumtaka alete mashahidi, kesho angaliweza kabisa kukitumia cheo hiki kwa faida ya mumewe, na kusema: ‘Mume wangu Ali ana haki ya kuushika ukhalifa,’ na hapo Khalifa atalazimika kuutoa ukhalifa na kumpa Ali kutokama na kule kumtambua kwake kwamba yu mwanamke mwaminifu. Hata hivyo, ili kulikatisha dai au ugomvi wowote wa aina hii, ilimbidi amnyang’anye haki yake ikubalikayo.”11

Msingi wa kunyimwa kwa kizazi cha Bibi Fatimah (a.s.) lile dai lao la Fadak ulijengwa kwenye zama za Khalifa wa kwanza. Baada ya kufa kishahidi kwa Sayyidna Ali (a.s.) Muawiyah akazishika hatamu za serikali na akaigawa Fadak miongoni mwa watu watatu (Marw?n, Amr bin Uthman na mwanawe Yazid). Katika kipindi cha ukhalifa wa Marw?n mafungu yote matatu aliyachukua yeye na akampa zawadi mwanawe, aliyeitwa Abdul Aziz. Na yeye Abdul Aziz alimpa mwanawe aliyeitwa Umar.

Kutokana na ukweli uliopo kwamba Umar bin Abdul Aziz alikuwa mtu mnyoofu kutoka miongoni mwa Bani Umayyah uasi wa kwanza aliouondoa ulikuwa ni kurudisha Fadak kwenye kizazi cha Bibi Fatimah (a.s.). Hata hivyo, baada ya kifo chake makhalifa wa Bani Umayyah waliofuatia waliichukua tena Fadak kutoka kwa Bani Hashim na iliendelea kumilikiwa na wao hadi ulipokoma utawala wao.

Katika ukhalifa wa Bani Abbas, suala la Fadak lilitangatanga katika hali ya ajabu. Kwa mfano, Saffah alimpa Abdulah bin Hassan na baada yake Mansur Daw?niqi aliichukua, lakini mwanawe Mahdi aliirudisha kwenye kizazi cha Bibi Zahra (a.s.).

Baada yake, Musa na Harun waliitwaa kutoka kizazi cha Bibi Zahra (a.s.) kutokana na sababu za kisiasa. Maamun alipokikalia kiti cha Ukhalifa kwanza aliitoa na kuwapa wale wamiliki wa awali. Baada ya kifo chake hali ya Fadak ilisitasita tena na wakati mmoja ilirudishwa kwenye kizazi cha Bibi Fatimah (a.s.) na kisha ikachukuliwa tena kutoka kwao.

Katika kipindi cha ukhalifa wa Bani Abbas, Fadak ilijitwalia mwelekeo wa kisiasa mkubwa zaidi ikilinganishwa na mwelekeo wake usiyo na kifani. Na hata kama wale makhalifa wa kwanza walikuwa wahitaji wa mapato kutoka Fadak, makhalifa na waungwana wa baadae walikuwa matajiri sana kiasi kwamba hawakuwa wahitaji wa haja yoyote ya mapato yake.

Hivyo basi, wakati Umar bin Abdul Aziz alipoirudisha Fadak kwenye kizazi cha Bibi Fatimah (a.s.), Bani Umayah walimkemea na wakasema: “Kwa kitendo chako hicho, umewaona wale watu wawili walio watukufu (yaani Abu Bakr na Umar) kuwa wana makosa.” Hivyo basi, walimshauri kuyagawa mapato ya Fadak miongoni mwa kizazi cha Bibi Fatimah (a.s.), lakini kuubakisha umiliki wake mikononi mwake mwenyewe.12

 • 1. Sura al-Hashir; 59:6,8; na kwenye vitabu vya Fiqhi (sheria za Kiislamu) jambo hili limejadiliwa kwenye sura ihusuyo Jihadi chini ya kichwa cha habari ‘Fay’.
 • 2. Majma’ul Bayaan, Juz. 3, uk. 411; Sharh Ibn Abil Hadid, Juz. 16, uk. 248.
 • 3. Durrul-Manthur, Juz. 4, uk. 176.
 • 4. Majma’ul Bayaan, juz. 2, uk. 211; Futuhul Buldaan, uk. 45.
 • 5. Sharh Nahjul Balagha cha Ibn Abil Hadid, Juz. 15, uk. 217.
 • 6. Sharhu Nahjul Balagha cha Ibn Abil Hadid, Juz. 16.
 • 7. Hii ina maana kwamba Qur’ani inasema Fatimah ni Mkweli asiyesema uongo - Mhariri.
 • 8. Sharhu Ibn Abil Hadid, Juz. 16, uk. 274.
 • 9. Siiratu Halabi, juz. 3, uk. 400.
 • 10. Sharhu Ibn Abil Hadid, Juz. 16, uk. 236.
 • 11. Sharhu Nahjul Balagh cha Ibn Abil Hadid, uk. 284.
 • 12. Sharhu Ibn Abil Hadid, Juz. 16, uk. 278.