Sura Ya 46: Matukio Ya Mwaka Wa Nane Hijiriya

Mwaka wa saba wa hijiriya ukamalizika na Waislamu walifaulu kufanya Hija ya kwenye Ka’abah kwa pamoja kwa mujibu wa masharti ya Hudaybiyah. Vile vile waliweza kuziona ibada za kupendeza na kuvutia kwa manufaa ya Upweke wa Allah zikitendwa kwenye kitovu hasa cha ibada ya masanamu, kiasi cha kuweza kuzivutia kwenye Uislamu nyoyo za baadhi ya machifu wa Kiquraishi kama vile Khalid bin Walid, Amr Aas1 na Uthman bin Talhah. Mara tu baada ya hapo hawa machifu watatu walikuja Madina kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w.) na wakaelezea mafungamano yao kwa ajili ya Mtume Muhammad na dini yake, na wakaukata uhusiano wao na Waquraishi wa Makka ambao hadi wakati ule hawakubakia kuwa chochote kile kingine isipokuwa mifupa isiyokuwa na uhai.2

Baadhi ya waandishi wa maisha ya Mtume (s.a.w.w.) wanasema kwamba Khalid na Amr bin Aas walisilimu kwenye mwaka wa 5 Hijiriya. Hata hivyo inawezekana kwa uhakika kwamba kusilimu kwao kulitokea kwenye mwaka wa 8 Hijiriya, kwa kuwa Khalid alikuwa kamanda wa kikosi cha jeshi la Waquraishi wakati wa kufanyika kwa yale mapatano ya Amani ya Hudaybiyah na wote wawili walisilimu pamoja.

Mwanzoni mwa mwaka wa 8 Hijiriya amani ilitawala katika maeneo mengi ya Hijaz na mvuto wa kuwaita watu kwenye ibada ya Mungu Mmoja ukazifikia sehemu nyingi, na ushawishi wa Wayahudi kwenye upande wa Kaskazini, na mashambulizi ya Waquraishi kutoka kwenye upande wa Kusini hayakuwatishia tena Waislamu.

Mtume (s.a.w.w.) sasa akaamua kuupanua mwito wake hadi Shamu na kufungua kituo kwa ajili ya kuupenyeza Uislamu nyoyoni mwa watu ambao wakati ule walikuwa wakiishi chini ya utawala wa mfalme wa Kirumi. Kwa ajili ya lengo hili alimtuma Harith Umayr Azd pamoja na barua kwenye baraza la mtawala wa Shamu. Katika siku zile Harith bin Shamir Ghassani alikuwa Mtawala dikteta wa Shamu, aliyetawala akiwa yu kibaraka wa Kaisari. Yule balozi wa Mtume (s.a.w.w.) aliifikia miji ya mpakani mwa Shamu na akaendelea na safari yake. Hata hivyo, Shurahbil aliyekuwa gavana wa maeneo ya mpakani alipata taarifa za kuwasili kwa yule balozi.

Alimfunga kwenye kijiji kiitwacho Muta na akafanya uchunguzi wa kina kutoka kwake. Yule balozi alikubali kwamba alikuwa na barua itokayo kwa Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) kwenda kwa Harith Ghassani mtawala dikteta wa Shamu. Akiivunja misingi yote ya ubinadamu na ikubalikayo duniani kote ambayo kwa mujibu wake (misingi hiyo) maisha na damu ya balozi huheshimiwa duniani kote, yule gavana aliamrisha kwamba afungwe mikono na miguu na kisha auwawe.

Mtume (s.a.w.w.) alipata taarifa za kitendo hiki kiovu cha Shurahbil. Alipatwa na wasiwasi mno kutokana na kuuwawa kwa yule balozi wake na akawapasha habari Waislamu kile kitendo kiovu cha Shurahbil na akawataka walipize kisasi dhidi ya yule gavana aliyetenda kitendo kile cha kinyama cha kumuuwa yule balozi hata bila ya kupata ruhusa ya wakuu wake.

Msiba Mwingine Zaidi

Sambamba na kitendo hiki msiba mwingine zaidi ulitokea, hivyo ukathibitisha zaidi ile nia ya Mtume (s.a.w.w.) kuwaadhibu watu wa Shamu ambao waliutishia uhuru wa mahubiri yao na wahubiri wake na wakamuuwa mjumbe wake na wahubiri wa Uislamu kwa njia ya ukatili mno.

Tukio tulilolizungumzia hapo juu ni hili. Katika mwaka wa 8 Hijiriya, Kaab bin Umar Ghifaari alitumwa pamoja na watu wengine kumi na watano wote wakiwa ni wahubiri stadi, waende kwenye ukanda wa Zaat Atlah ulioko kwenye upande wa pili wa Waadiul Qaraa na kuwaita watu wa sehemu ile kwenye Uislamu. Wahubiri hawa walifika kwenye eneo hili na wakaifanya ile kazi waliyopewa.

Kwa ghafla wakakumbana na upinzani mkali kutoka kwa watu wale nao wakashambuliwa wote. Kile kikundi cha wahubiri kikajikuta kikiwa kimezungukwa na kundi kubwa la watu, Walijihami kishujaa na wakapendelea kufa kishahidi kuliko kufedheheka.

Ni mmoja wao tu ambaye naye alijeruhiwa na akalala miongoni mwa maiti za wale wenziwe, aliyeweza kuamka usiku wa manane na akarejea Madina. Alipofika huko alimsimulia Mtume (s.a.w.w.) tukio zima.

Kule kuwauwa wahubiri na watu wengi mno wasio na makosa kulimfanya Mtume (s.a.w.w.) aamrishe Jihadi. Hivyo basi, jeshi la askari elfu tatu lilipelekwa huko kwenda kuwaadhibu wale waasi, na wale waliozuia kuenezwa kwa Uislamu.3

Ilitowa amri ya Jihadi. Askari elfu tatu wapiganao kwa panga wakajikusanya kwenye uwanja wa kijeshi wa Madina (uitwao Jurf). Mtume (s.a.w.w.) akaja uwanjani pale yeye mwenyewe na kuwahubiria wale askari, akasema: “Hamna budi kwenda kuwaita tena watu hao kwenye Uislamu. Kama wakisilimu basi haitahitajika kulipiza kisasi cha kule kuuwawa kwa yule mjumbe, lakini kinyume na hivyo, hamna budi kuomba msaada wa Allah na kupigana dhidi yao. Ndio! Enyi askari wa Uislamu!

Piganeni Jihadi kwa Jina la Allah! Waadhibuni maadui wa Allah na maadui wenu waishio Shamu. Msiwaingilie watawa wa kiume na wa kike (masista) wanaotumia muda wao kwenye majumba ya watawala wakiwa wamejisogeza mbali zaidi kutoka kwenye Ghasia za ulimwengu. Viangamizeni vitu vyenye asili ya kishetani kwa hizi panga zenu.

Msiwauwe wanawake, watoto na wazee. Msiikate miti wala msiyabomoe majengo.4 Ndio! Enyi Mujahidiin! Kamanda wa jeshi hili ni binamu yangu Ja’far bin Abi Twalib. Kama akijeruhiwa, Zayd bin Harith ataishika bendera na kuliongoza jeshi, na kama naye akiuawa, Abdullah bin Rawaah atachukua mkanda wa jeshi. Na kama yeye naye akijeruhiwa, mnaweza kumteua kamanda wenu mkuu ninyi wenyewe.”

Hapo ilitolewa amri ya kuanza kuondoka na yeye mwenyewe Mtume (s.a.w.w.) pamoja na baadhi ya Waislamu walilisindikiza jeshi lile hadi mahali paitwapo Thaniyatul Widaa.

Hapo wale waliowasindikiza wale askari waliwapa kwaheri na kwa mujibu wa desturi za zamani, waliwaambia: “Allah na akusaidieni mpate kurejea salama, wenye afya timamu na ngawira.”
Hata hivyo, Abdullah Rawaah aliyekuwa makamu wa pili au wa tatu wa kamanda wa jeshi lile aliusoma utenzi ufuatao: “Ninaiomba ghofira ya Allah na (kinga Yake) kutokana na mapigano makali ambayo kutokana nayo, povu la damu hububujika.”5

Kutokana na utenzi huu mtu anaweza kuitathmini vizuri sana ile nguvu ya imani na huba ya kufa kishahidi ya kamanda huyu shujaa. Wakati huo huo, watu walimwona akitokwa na machozi. Alipoulizwa ni kwa nini analia alijibu akisema: “Mimi sina haja kabisa ya huu ulimwengu, lakini nilimsikia Mtume (s.a.w.w.) akisoma ubeti huu: “Ni hukumu ya Allah isiyoepukika kwamba nyote mtawasili Motoni. Na kutoka hapo wale wachamungu waendelee na kwenda Peponi.” Hivyo basi, kuwasili kwangu Motoni ni kwenye uhakika lakini mwishilizio wa kuwasili huku sio dhahiri na haifahamiki ni kipi kitakachotokea baada ya hapo.”6

Tofauti Ya Maoni Kuhusu Kamanda Wa Kwanza

Wengi wa waandishi wa maisha ya Mtume (s.a.w.w.) wameandika kwamba yule kamanda mkuu wa jeshi lile alikuwa Zayd bin Harith mwana wa kulea wa Mtume (s.a.w.w.), na Ja’far na Abdullah walikuwa makamu wake wa pili na wa tatu, kwa utaratibu wa huku kutajwa kwa majina yao.

Hata hivyo, kinyume na maoni haya wanachuoni watafiti wa Kishia humchukulia Ja’far bin Abi Twalib kuwa ndiye kamanda mkuu wa jeshi lile na wale watu wawili wengine kuwa ni makamu wa pili na wa tatu. Sasa swali hapo ni, ni maoni yapi kati ya haya mawili yaliyo sahihi?

1. Kutokana na mtazamo wa heshima ya kijamii pamoja na uchamungu na elimu, Zayd bin Harith hakuwa sawa na Jaafar Tayyar. Ibn Athir kwenye kitabu chake Usudul Ghabah; anasema hivi kuhusiana na Jaafar: “Alifanana na Mtume katika tabia, umbile la mwili, na alimwamini Mtume muda mfupi tu baada ya Ali. Siku moja Abu Twalib alimwona Ali akiwa amesimama kuumeni kwa Mtume. Hapo akamwambia mwanawe Jaafar: “Wewe nawe huna budi kwenda na kusali ukiwa umesimama kushotoni kwa Mtume. “ Alikuwa kiongozi wa watu walioyaacha maskani yao kwa ajili ya dini na imani yao na wakatoka mji wa Makka kwa amri ya Mtume (s.a.w.w.) na kukimbilia Ethiopia. Yeye akiwa yu msemaji wa kikundi kile cha wahamiaji alimvutia Mfalme wa Ethiopia kwenye Uislamu kwa hoja zake zenye nguvu na zenye kupenya akilini na akauthibitisha uwongo wa wawakilishi wa Waquraishi waliotamani kurudishwa Hijaz kwa wale wahamiaji. Na kwa kuzisoma aya za Qur’ani zihusianazo na Nabii Isa (a.s.) na mama yake Mariam akazipata huruma na ulinzi wa Negus kwa ajili ya Waislamu wahamiaji kwa jinsi ambayo aliwatoa wale wajumbe wa Waquraishi barazani mwake.7

Jaafar alikuwa mtu yule aliyerejea kutoka Ethiopia wakati wa kutekwa kwa Khaybar, na Mtume (s.a.w.w.) aliposikia kurejea kwake, alikwenda mbele hatua kumi na sita kumlaki, akaiweka mikono yake shingoni mwake, akalibusu paji la uso wake na akatokwa na machozi kwa furaha, kisha akasema: “Sijui ni kwa tukio lipi nilifurahie zaidi imma kwa ajili ya kuonana nawe baada ya kutengana kwa miaka mingi, au kwa ajili ya Allah kutufungulia ngome za Wayahudi kwa mikono ya kaka yako Ali.”

Jaafar ndiye yule mtu maarufu aliyekumbukwa na Amirul-Mu’minin (a.s.) baada ya kifo chake kwa ushujaa na uhodari wake. Sayyidna Ali (a.s.) alipopata habari kwamba Amr bin Aas amekula kiapo cha utii kwa Muawiyah na kwamba wameafikiana kwamba kama wakipata ushindi dhidi ya Sayyidna Ali (a.s.) ugavana wa Misri utapewa Amr, basi Amirul-Mu’minin (a.s.) alikosa raha na akamkumbuka ami yake Hamza na nduguye Jaafar na akasema:
“Kama watu hawa wawili wangelikuwa hai, ushindi wetu ungalithibitika.”8

Je, inaingia akilini kwamba ingawa Jaafar alikuwa nazo zile sifa maarufu ambazo baadhi yake tumezitaja hapo juu, kisha Mtume (s.a.w.w.) amteuwe Zayd kuwa kamanda wa jeshi lile na kumfanya Jaafar kuwa msaidizi wake wa kwanza?

2. Zile tenzi walizozisoma washairi wakuu wa Uislamu wakiviomboleza vifo vya hawa makamanda watatu zaonyesha kwamba kamanda mkuu alikuwa ni Jaafar na wale watu wawili wengine walikuwa wasaidizi wake. Katika kuzisikia taarifa za vifo vya hawa makamanda, Hassan Bin Thabit, mshairi wa Mtume (s.a.w) aliusoma utenzi ulionukuliwa kwenye kitabu Siiratu Ibn Hisham. Alisema: “Allah na awabariki wale makamanda waliouawa kwenye vita vya Muta, mmoja baada ya mwingine. Wao walikuwa ni Jaafar Zayd na Abdulah, waliokikaribisha kifo mmoja baada ya mwingine.”

Neno tinaabi’u lililotumika kwenye utenzi huu linaonyesha ya kwamba hawa makamanda watatu waliuawa mmoja baada ya mwingine na wa kwanza kuuawa alikuwa ni Jaafar. Shairi lililo wazi zaidi ni ule utenzi ulioandikwa na Ka’ab bin M?lik Ansari kuomboleza vifo vya wale waliouawa huko Muta. Katika utenzi huu aliainisha kamanda wa kwanza alikuwa ni Jaafar. Mshairi huyu yeye mwenyewe alishuhudia ukweli uliopo kwamba Mtume (s.a.w.w.) alimpa Jaafar ukamanda mkuu wa jeshi lile.

Anasema: “Hebu ukumbuke ule wakati askari wa Uislamu walipowekwa chini ya bendera ya kamanda wa kwanza ambaye ni Jaafar bin Abi Twalib na akatoka kwenda kupigana Jihadi.”

Beti hizi zilizoandikwa siku zilezile na bado zimesalia kuwa salama kutokana na mageuzi ya nyakati ni muhimu sana na ni ushahidi thabiti wa ukweli kwamba kile walichokiandika waandishi wa Kisuni juu ya jambo hili hakiafikiani na habari za kihistoria, na wasimuliaji wale wameyazusha masimulizi yale kwa sababu za kisiasa, na waandishi wa maisha ya Mtume (s.a.w.w.) wameyarekodi vitabuni mwao bila ya kuyathibitisha. Hata hivyo, inashangaza kwamba ingawa upo ukweli kwamba Ibn Hisham9 amezinakili tenzi hizi lakini amemchukulia Jaafar kuwa yu kamanda msaidizi wa pili.

Utaratibu Wa Vikosi Vya Kirumi Na Kiislamu

Siku zile Urumi ilikabiliwa na ghasia zisizo kifani kutokana na vita zilizokuwa zikiendelea baina yake na Iran. Ingawa Warumi walitiwa moyo na ushindi wao juu ya Iran, vilevile waliutambua ushujaa na ujasiri wa askari wa Uislamu waliopata heshima kutokana na ushujaa wao na nguvu ya imani ya kila mmoja wao. Serikali ya kirumi ilipopata taarifa juu ya matayarisho na mwenendo wa askari wa Uislamu, Hercules na yule mtawala wa Shamu waliunda jeshi la kutisha kwenda kulikabili lile jeshi lenye nguvu la askari elfu tatu la Waislamu.

Shurahbil pekee alikusanya askari laki moja kutoka miongoni mwa makabila mbalimbali yaishiyo nchini Shamu na akaenda kule mipakani mwa nchi yake kwenda kuyazuia maendeleo ya wale mashujaa wa Kiislamu. Akiwa bado hajatosheka na hili, Kaisari naye kutokana na taarifa alizozipata kabla ya hapo, alitoka Urumi na askari laki moja na wakaenda wakapiga kambi mahali paitwapo Ma’ab ambapo ni miongoni mwa miji ya Balqaa. Walikaa hapo wakiwa ni jeshi la akiba la kuongezea nguvu.10

Ukusanyaji wa askari wote hawa ulifanywa kwenda kupigana na jeshi lililokuwa dogo sana linapolinganishwa na hilo linalokusanywa, ukusanyaji huo ulitokana na taarifa walizozipata wale makamanda wa Kirumi juu ya utekaji wa Waislamu. Isingalikuwa hivyo basi hata moja ya kumi ya jeshi hili lenye askari elfu ishirini lilitosha kabisa kuwakabili maadui wale vyovyote vile wawavyo mashujaa.

Ukweli unaopaswa kuzingatiwa hapa ni kwamba, nguvu ya haya majeshi mawili inapotathminiwa, utaona jeshi la Uislamu lilikuwa dhaifu mara nyingi sana kuliko lile la Urumi katika idadi ya askari pamoja na ujuzi wa maarifa na mbinu za kijeshi. Kutokana na kushiriki kwao kwenye vita vya muda mrefu baina ya Urumi na Iran, maafisa wa Urumi wamejipatia siri nyingi za ubora na ushindi wa kijeshi, ambapo ujuzi wa lile jeshi changa la Uislamu katika mambo haya wakati ule ulikuwa mdogo. Hivyo Waislamu hawakulingana na Warumi katika mambo ya zana na usafiri wa kijeshi.

Na jambo lililo muhimu zaidi ni kwamba lile jeshi la Waislamu lilikuwa liende kuishambulia nchi ya kigeni ambapo wale Warumi waliokuwa na zana zote hizo, walikuwa kwenye nchi yao wenyewe na walikuwa wajihami tu. Katika hali hizo, daima huwa muhimu kwamba lile jeshi lenye kushambulia liwe na zana na nguvu za kutosha kuzishinda hali zisizofaa.

Tukiyazingatia mambo haya, sasa tutaona kwamba wale makamanda wa jeshi la Waislamu walipendelea kuwa thabiti na kupigana kuliko kukimbia uwanja wa vita, na hivyo waliongeza heshima yao ya kihistoria, ingawa waliweza kukiona kifo kwa hatua chache tu.

Baada ya kuwasili mipakani mwa Shamu, Waislamu waliyatambua yale matayarisho na nguvu za kijeshi ya yule adui. Hivyo basi, upesi sana waliunda halmashauri ya ushauri ili kuweza kuamua juu ya maarifa ya kijeshi. Baadhi ya watu walikuwa na maoni kwamba jambo hilo lipelekwe kwa Mtume (s.a.w.w.) na kupata maelezo zaidi kutoka kwake. Maoni haya yalielekea kuthibitishwa, wakati uleule Abdullah Rawaahi aliyekuwa kamanda wa pili na aliyemwomba Allah kufa kishahidi katika ule wakati wa kutoka Madina aliamka na kutoa hotuba kali. Alisema: “Mmetolewa ili mlifikie lengo msilolipenda. Mmetoka Madina kukifikia kifo cha kishahidi, katika uwanja wa vita Waislamu hawategemei ubora wa idadi. Sisi tutapigana dhidi ya watu hawa katika njia ya Allah, Uislamu.

Uislamu uleule uliotufanya kuwa waheshimiwa na wastahiki. Kama tukishinda, tutaipata fahari; na kama tukifa kishahidi hilo nalo ni moja ya matakwa yetu.”

Maneno ya Abdullah yalizibadili fikara za maafisa na wale wajumbe wa halmashauri ya ushauri. Hivyo basi, iliamuliwa kwamba ili kuzitekeleza amri za Mtume (s.a.w.w.) yafanyike mapigano pale alipoamrisha Mtume (s.a.w.w.).11

Majeshi haya mawili yalikabiliana mahali paitwapo Sharaf. Hata hivyo, kutokana na kuzifikiria mbinu za kijeshi, sehemu ya jeshi la Waislamu ilirudi nyuma na kupiga kambi mahali paitwapo Muta. Jaafar bin Abu Twalib aliyekuwa kamanda mkuu wa jeshi lile, aliligawa katika sehemu tatu na akateua kamanda katika kila sehemu. Mapambano ya mtu na mtu yakaanza. Sasa ilikuwa muhimu kwa Jaafar kuishika ile bendera mikononi mwake na kuwaongoza askari wake katika mashambulizi na wakati huo huo kupigana na kujihami.

Ushujaa na uthabiti wake katika njia ya malengo yake ni dhahiri kabisa kutokana na beti za ule utenzi aliousoma pale alipokuwa akimshambulia adui. Alisema kwamba: “Ninayo furaha kwamba ile Pepo iliyoahidiwa imekuwa karibu zaidi; ile Pepo iliyo safi yenye vinwyaji baridi. Kinyume na hivyo, kuangamia kwa Urumi nako kumekaribia. Hali ya taifa kosefu kwa kufuru zake katika upande wa fundisho la Upweke wa Allah. Na ni taifa ambalo mawasiliano na uhusiano wake nasi umekatwa. Mimi ninayo dhamira ya kuwapiga pigo nitakapowakabili!” 12

Yule kamanda mkuu wa Uislamu alipigana mapigano ya kijasiri dhidi ya adui. Hata hivyo, alipojikuta akiwa amezingirwa na maadui wale, na akatambua kwamba sasa kufa kwake kishahidi kulikuwa na uhakika, ili kwamba maadui wasimtumie farasi wake na vile vile watambue kwamba sasa kaishakata uhusiano na ulimwengu, alishuka kutoka kwenye farasi wake na akampiga pigo lililomfanya yule farasi asiweze kutembea, na kisha akaendelea kupigana.
Wakati ule ule kitanga chake cha kulia kilikatwa. Ili ile bendera ya Mtume (s.a.w.w.) isianguke chini, aliishika kwa kitanga chake cha kushoto na kile kitanga chake cha kushoto nacho kilipokatwa aliishika kwa mikono yake ile isiyo na vitanga. Hatimaye,baada ya kupata majeraha themanini alianguka chini na akafariki dunia.

Sasa ikafika zamu ya Zayd bin Harith, yule kamanda wa pili. Aliichukua ile bendera begani mwake na kulitekeleza jukumu lake kwa ujasiri usio kifani na hatimaye kafariki dunia kutokana na majeraha makubwa aliyoyapata.

Kisha akafuatia Abdullah Rawaah, yule kamanda wa tatu. Akaishika ile bendera mkononi mwake. Akampanda farasi wake na akaanza kuzisoma beti za utenzi wake. Katika kipindi cha yale mapigano alijiona kuwa yu mwenye njaa sana. Alipewa tonge la chakula ili aweze kuondokwa na njaa ile kwa kiasi fulani. Alikuwa bado hajakula chochote kile kutokana na kile chakula pale aliposikia sauti ya mtiririko kama kundi la maadui. Hapo akalitupa lile tonge la chakula na akaenda mbele kumkabili adui na akaendelea kupigana hadi alipokufa kishahidi.

Jeshi La Uislamu Laelemewa

Tangu pale na kuendelea kuelemewa na kutatanishwa kwa jeshi la Uislamu kulianza. Yule kamanda mkuu na wasaidizi wake wawili wameuawa. Hata hivyo, Mtume (s.a.w.w.) aliiona hali hii kwenye fikira zake kabla ya pale na tayari amewapa mamlaka wale askari kwamba, kama mambo yakitokea hivyo wamteue kamanda wao wenyewe. Kwa wakati ule Thabit bin Arqam akaiokota ile bendera, akawageukia wale askari wa Uislamu na kuwaambia: “Jichagulieni kamanda.” Wote wakasema: “Wewe na uwe kamanda wetu.” Akajibu akasema: “Mimi siko tayari kabisa kuichukua nafasi hii. Hivyo basi, hamna budi kumchagua mtu mwingine.” Kisha Thabit pamoja na Waislamu wengine wakamchagua Khalid bin Walid aliyesilimu hivi karibuni tu, na alikuwamo kwenye jeshi lile, kuwa kamanda wao.

Khalid alipoteuliwa kuwa kamanda hali ilikuwa nyeti mno. Hofu na kitisho viliwaingia Waislamu. Yule kamanda (mpya) alipanga kuzitumia mbinu za kijeshi zisizokuwa na kifani. Aliamrisha kwamba wakati wa usiku kitakapoingia kiza kila mahali, wafanye mageuzi na mabadilishano ya farasi na kwamba pia wapige makelele. Vikosi vya kulia viende kwenye nafasi ya vikosi vya kushoto na vikosi vya kushoto vije kwenye nafasi ya vikosi vya kulia, na hali kadhalika safu ya mbele ije katikati ya jeshi na safu ya katikati iende mbele. Mabadiliko haya yaliendelea hadi asubuhi.

Kufuatana na masimulizi fulani, aliamrisha kwamba kikosi cha Waislamu kisogee kwenye sehemu ya mbali wakati wa usiku na kisha kirudi wakati wa asubuhi huku kikisoma Laailaha illallah (hakuna mungu ila Allah). Lengo la mpango wote huu lilikuwa kwamba lile jeshi la Kirumi lifikirie kwamba jeshi la msaada limefika kujiunga na Waislamu. Kwa bahati ilitokana na dhana hii kwamba hawakuwashambulia Waislamu siku iliyofuatia na wakaambiana kwamba ikiwa Waislamu wameweza kupigana kishujaa kiasi kile walipokuwa hawana jeshi la msaada sasa watapigana kishujaa zaidi baada ya kupata jeshi la msaada.

Kutulia kwa lile jeshi la Warumi kuliwapa Waislamu nafasi ya kurejea makwao. Mafanikio makubwa waliyopata Waislamu yalikuwa kwamba walipigana dhidi ya jeshi lililoandaliwa na lenye nguvu kwa muda wa siku moja au tatu hivi. Ule mpango wa kijeshi alioutumia yule kamanda mpya ulikuwa mzuri kwa sababu uliwatoa Waislamu kwenye kifo na kuwafanya warejee Madina kwa usalama. Hivyo basi anastahili kusifiwa.13

Askari Wa Uislamu Warejea Madina

Taarifa zihusianazo na mapigano na kurudi nyuma kwa askari wa Uislamu zilikuwa tayari zimeshafika Madina kabla ya kufika kwao pale. Hivyo basi, Waislamu walitoka na kwenda kuwalaki hadi wakafika Juraf kwenye uwanja wa kijeshi wa mji wa Madina.

Ile hatua iliyochukuliwa na yule kamanda mpya ilikuwa ni mbinu ya hekima, lakini kwa kuwa haikuafikiana na mwelekeo wa Waislamu na hali yao ya ushujaa halisi, na kulelewa kwenye himaya ya imani, hawakutazamia kule kurudi nyuma kwa wale askari na hawakufikiria kitendo hiki kuwa ni chenye rehema. Hivyo basi, waliwapokea kwa kauli mbiu zenye uchungu kama vile: “Enyi wakimbizi! Kwa nini mmeikimbia Jihadi?” Na kwa kuwatupia vumbi vichwani na nyusoni mwao.

Kitendo cha Waislamu hawa dhidi ya hiki kikundi kilikuwa cha jeuri mno kiasi kwamba baadhi ya watu walioshiriki mwenye vita ile walilazimika kujifungia majumbani mwao kwa kipindi hivi, nao hawakujitokeza mbele ya macho ya hadhara. Na walipotoka watu waliwasoza vidole na kusema: “Huyu ni mmoja wa wale watu walioikimbia Jihadi.”14

Hatua za Waislamu dhidi ya kurejea nyuma kwa wale askari wa Uislamu kulikofanyika kwa busara, ni dalili ya moyo wa ushujaa na ujasiri ambao itikadi juu ya Allah na Siku ya Hukumu imejenga na kukamilika nyoyoni mwao, na ambayo kutokana nayo, walikipendelea kifo katika njia ya Uislamu kuliko ile faida ndogo itokanayo na kule kurejea nyuma.

Ngano Badala Ya Historia

Kama vile Amirul-Mu’minin Sayyidna Ali bin Abi Twalib (a.s.) anavyofahamika miongoni mwa Waislamu kama Simba wa Mungu – Asadullah, baadhi ya watu waliona kuwa inafaa kuunda katika ulinganisho naye, kamanda atakayekishika cheo cha Upanga wa Allah, na mtu huyo si yeyote mwingine ila ni yule kamanda shujaa wa Uislamu, Khalid bin Walid. Hivyo basi wanasema kwamba aliporejea kutoka kwenye Vita vya Muta, Mtume (s.a.w.w.) alimpa cheo cha Upanga wa Allah.

Hakuna shaka kwamba kama Mtume (s.a.w.w.) angempa cheo hiki kwenye tukio jingine basi lisingelikuwako swali lolote juu ya jambo hili, lakini hali ya mambo ilivyo, baada ya kurejea kwa lile jeshi la Waislamu kutoka kwenye Vita vya Muuta haikufanya kuweko umuhimu wa kwamba Mtume (s.a.w.w.) ampe cheo hicho.

Je ni haki kwamba Mtume (s.a.w.w.) ampe cheo cha ‘Upanga wa Allah’ mtu anayewaongoza watu ambao Waislamu wanawaita wakimbizi na kuwapa mapokezi ya kuwamwagia vumbi vichwani na nyusoni mwao? Na hata kama akiidhihirisha sifa ya kuwa

‘Upanga wa Allah’ kwenye vita nyinginezo, lakini kwenye vita hivi hakuweza kulifikia lengo lolote zaidi ya ule mpango wake wa kijeshi ustahilio sifa, kwani vinginevyo yeye na wafuasi wake wasingalipewa sifa ya wakimbizi.

Ibn Sa’ad anaandika hivi: “Katika ule wakati wa kurudi nyuma kwa askari wa Uislamu, askari wa Kirumi waliwafuatia na kuwauwa baadhi yao.”15

Wazushi wa ngano hii ya ‘Upanga wa Allah’ vile vile wameiongeza sentensi ifuatayo ili kuiunga mkono kauli yao: “Khalid alipoushika ukamanda, aliwaamrisha askari kumshambulia adui. Yeye mwenyewe alishambulia kwa ushujaa na panga tisa zilivunjika mkononi mwake, na ikasalia ngao tu.”
Hata hivyo, wazushi wa ngano hii walisahau jambo moja nalo ni, kama Khalid na askari wake walitenda ujasiri na ushujaa wa aina ile kwenye uwanja wa vita, ni kwa nini watu wa Madina waliwaita ‘wakimbizi’ na ni kwa nini wawalaki kwa kuwamwagia vumbi vichwani mwao na nyusoni mwao, wakati wao kwa kitendo kile (yaani kama walipigana kishuja kama ilivyoelezwa hapo juu) wangewalaki kwa heshima, kwa mfano kwa kuchinja kondoo na kuwanyunyizia manukato na marashi kwenye njia yao?

Mtume Alilia Sana Kwa Kifo Cha Ja’far

Mtume (s.a.w.w.) aliangua kilio kwa kifo na shahada ya binamu yake Ja’far, alikwenda moja kwa moja kumwarifu mkewe Asmaa’ bint Umays kuhusu kifo cha mumewe na pia kumpa salamu za rambirambi. Akizungumza na Asmaa, alisema hivi: “Wako wapi wanangu?” Asmaa akawaleta wana wa Jaafar, Abdulah, Awn na Muhammad mbele ya Mtume (s.a.w.w.). Alipoona uambatanaji mkubwa sana wa Mtume (s.a.w.w.) kwa wanawe, Asmaa alitambua ya kwamba mumewe mpenzi amefariki.

Akasema: “Inaonekana kwamba wanangu wamekuwa yatima, kwa sababu ya hivyo unavyowatendea.” Mtume (s.a.w.w.) akalia sana wakati ule. Kisha akamwomba binti yake atayarishe chakula na kuifariji familia ya Jaafar kwa muda wa siku tatu. Hata baada ya hapo, Mtume (s.a.w.w.) aliendelea kumhuzunikia Jaafar bin Abi Twalib na Zayd bin Harith na alipoingia nyumbani mwake (Mtume s.a.w.w) aliwalilia mno.16

 • 1. Waaqidi ametoa masimulizi mengine ya mvuto ya chifu huyu kuelekea kwenye Uislamu (Maghaazi, Juz. 2, uk. 743-745).
 • 2. Tabaqaatu Ibn Saad, Juz. 7, uk. 394.
 • 3. Tabaqaatul Kubra, juz. 2, uk. 128.
 • 4. Maghaazil-Waaqidi, juz. 2, uk. 757.
 • 5. Na baada ya hapo, upesi sana akausoma utenzi mwingine usemao; “Wakati watu watakapoliona kaburi au maiti yangu, ikiwa imetapakaa damu, waweze kuusifu ushujaa wangu na kujitolea mhanga kwangu na kuniombea.” (Bihaarul Anwaar, juz. 21, uk. 60 na Tabaqatul Kubra, juz. 2, uk. 128).
 • 6. Siiratu Ibn Hishamu, Juz.2, uk. 374.
 • 7. Usudul Ghabah, Juz. 1, uk. 387.
 • 8. Siffin Ibn Muzaahim, uk. 47.
 • 9. Siiratu Ibn Hishamu, Juz. 2, uk. 384-387.
 • 10. Mughaazil-Waaqid, juz. 2, uk. 760; Siiratu Ibn Hishamu, Juz. 2, uk. 375.
 • 11. Maghaazil-Waaqid, Juz. 2, uk. 760; Siiratu Ibn Hishamu, Juz. 2, uk. 77.
 • 12. Siiratu Ibn Hishamu, Juz. 2, uk. 378.
 • 13. Maghaazil-Waaqid, Juz. 2, uk. 763.
 • 14. Siiratu Ibn Hishamu, Juz. 2, uk. 382-383; Siiratu Halabi, Juz. 2, uk. 79.
 • 15. Tabaqatul-Kubra, Juz.2, uk. 129.
 • 16. Bihaarul Anwaar, Juz. 21, uk. 54-55; Maghaazil-Waaqidi, Juz. 2, uk. 766.