Sura Ya 47: Vita Vya Dhatus Salasil

Tangu siku ile Mtume (s.a.w.w.) alipohajiria Madina na kuufanya mji ule kuwa makao makuu ya Uislamu, daima alikuwa mwangalifu wa hali ya maadui na shauku yao na makri zao, na akaupa upatikanaji wa taarifa umuhimu ustahilio kuhusiana na matendo yao. Aliwapeleka Makka watu stadi na hodari na kwenye makabila mbalimbali ili waweze kumwarifu mapema juu ya maamuzi na mipango ya maadui.

Baada ya kuzitambua njama zao, mara kwa mara alikuwa akizikomesha palepale mwanzoni kabisa. Katika hali hiyo, mashujaa wa Uislamu walikuwa wakiwashambulia maadui kwa kuwasitukiza chini ya ukamanda wa Mtume (s.a.w.w.) au chini ya baadhi ya maafisa mashujaa wa Uislamu na kuwatawanya hata kabla ya kusogea kutoka kwenye sehemu zao. Matokeo yake yakawa kwamba, Uislamu ulisalimika kutokana na hatari za maadui, na umwagaji damu mwingi nao ulizuiwa.

Katika nyakati zetu hizi, taarifa za nguvu na kufaa kwa jeshi la adui na juu ya mipango yake ya siri kunafikiriwa kwamba ni moja ya visababisho vya ushindi, na mataifa makuu ya ulimwengu yanayo mipango mipana mno ya jinsi ya kuwafunza majasusi, kuwapeleka kwenye sehemu mbalimbali ulimwenguni na kuwatumia.

Katika Uislamu, mwongozo wa kuanzisha jambo la upelelezi ulichukuliwa na Mtume mwenyewe, na baada yake makhalifa wa Uislamu, na hususan yule Amirul-Mu’minin pia aliwapa majasusi kadhaa majukumu mbalimbali.

Na kila alipomteua mtu kuwa gavana wa sehemu fulani, aliwaamrisha baadhi ya watu kuiangalia tabia na mwenendo wake na kumpelekea taarifa (yaani kwake yeye Sayyidna Ali a.s). Amelitaja jambo hili kwenye barua zake kadhaa alizowaandikia magavana ambazo kwazo magavana hawa wamekemewa. (Tazama Barua Na. 33 na 35 kwenye Nahjul Balaghah).

Katika mwaka wa pili Hijiriya Mtume (s.a.w.w.) aliwapeleka watu themanini kutoka miongoni mwa Muhajiriin chini ya uongozi wa Abdullah bin Jahsh, kwa maelekezo ya kwenda kupiga kambi mahali fulani maalum na kumweleza (yeye Mtume s.a.w.w) kuhusu matendo na mipango ya Waquraishi.
Kama Mtume (s.a.w.w.) hakuweza kushambuliwa kwa kushitukizwa bila ya yeye mwenyewe kujua wakati wa vita vya Uhud, na akaweza kuyaweka majeshi yake nje ya mji wa Madina kabla ya kuwasili kwa maadui, na pia kama kwenye vita vya Ahz?b aliweza kuchimba lile handaki lenye kutisha mbele ya maadui kabla ya kufika kwao pale, ni kwa sababu tu ya zile taarifa zenye maelezo kamili ambazo Waislamu, waliotumwa kwa lengo hili waliziwasilisha kwake, na kwa njia hii wakaweza kutekeleza wajibu wao wa kidini katika kuusalimisha Uislamu kutokana na kuanguka.

Njia hii ya hekima aliyoitumia Mtume (s.a.w.w.) ni mfano wenye thamani mno kwa Waislamu kuweza kuufuata, na chini ya msingi huu ni muhimu kwamba viongozi wakuu wa Uislamu wazitambue kwa ukamilifu aina zote za makri zilizo dhidi ya Uislamu ndani ya nchi za Kiislamu na vilevile katika sehemu mbalimbali ulimwenguni. Kwa njia hii waweze kuzizima cheche kabla ya kugeuka kuwa miali na ili waweze kulifikia lengo lao. Hata hivyo, kweye zama zetu hizi jukumu hili haliwezi kutimizwa bila ya zana muhimu.

Kwenye Vita vya Dhatus-Salaasil ambavyo ndio maudhui ya mazungumzo yetu ya hivi sasa, uasi mkubwa sana ulikomeshwa kwa urahisi sana kwa kupata taarifa kamili juu ya mpango wa adui. Na kama Mtume (s.a.w.w.) asingeliitumia njia hii ya kukusanya taarifa basi angelipata hasara isiyotengezeka.Yafuatayo hapa chini ndio malezo ya tukio hili kwa urefu:

“Idara ya ujasusi ya Mtume (s.a.w.w.) ilimtaarifu kwamba kwenye Bonde la Yaabis, maelfu ya watu yalifanya mapatano ya pamoja kwamba watauangamiza Uislamu kwa nguvu zao zote na watautoa uhai wao kwa ajili ya kulifikia lengo hili au wamuue Muhammad, na afisa wake shujaa na mshindi, Ali (a.s.).” Mwanachuoni mkuu Ali bin Ibrahim Qummi anaandika hivi: “Wahyi ulimwarifu Mtume (s.a.w.w.) juu ya mpango wao huo.”1

Lakini Shaykh Mufid mwanachuoni mtafiti mkuu anasema: “Mwislamu mmoja alitoa taarifa juu ya jambo hili kwa Mtume (s.a.w.w.) na akaitaja sehemu ya njama hiyo kuwa ni bonde la Raml”2 na akaongeza kusema kwamba makabila hayo yaliamua kufanya mashambulizi ya usiku mjini Madina na kulimaliza kabisa jambo hili kwa ukamilifu.

Mtume (s.a.w.w.) alifikiria kwamba ilikuwa muhimu kuwaarifu Waislamu juu ya hatari hii kuu. Kwenye siku hizo, neno la siri lililokuwa likitumika kwa ajili ya kuwaita watu kwenye sala au kusikiliza taarifa muhimu lilikuwa ‘Assalaat Jaami’ah’ Hivyo basi, kama ilivyoamrishwa na Mtume (s.a.w.w.) mtangazaji alikwenda kwenye nafasi yake ya kutangazia iliyokuwa mahali palipoinuka kwenye paa la msikiti na kutamka ile kauli tuliyoitaja kwa sauti kuu.

Upesi sana Waislamu walikusanyika mle msikitini. Mtume (s.a.w.w.) akapanda mimbari na akazungumza mambo mengi yakiwamo haya: “Maadui wa Allah wanakuoteeni nao wameamua kukushambulieni kwa kukuvizieni wakati wa usiku. Baadhi yenu ni lazima wasimame ili kuuzuia uasi huu.”

Wakati huu, kikundi cha watu kiliteuliwa kwa lengo hili, na Bwana Abubakr aliteuliwa kuwa kamanda wake. Yeye pamoja na hicho kikundi maalum waliliendea kabila la Bani Salim. Umbali ambao hawa askari wa Uislamu walisafiri ulikuwa ni pamoja na njia yenye mawe yasio ya kawaida, na eneo lenye bonde lililokuwa likikaliwa na kabila lile lilikuwa pana sana.

Wale askari wa Uislamu walipojaribu kuliingia bonde lile iliwabidi kuwakabili Bani Salim na
yule kamanda wa jeshi la Uislamu hakuweza kuifikiria njia yoyote nyingine ila kwamba arudi kwa
njia aliyojia.3

Mwanachuoni Ali bin Ibrahim Qummi anaandika kwenye Tafsiir yake hivi: “Machifu wa kabila lile la Bani Salim walipomwuliza Abubakr: “Nini lengo la msafara huu wa kijeshi?” alijibu akisema: “Mimi nimeteuliwa na Mtume wa Allah kukubalighishieni Uislamu na kupigana dhidi yenu kama mkikataa kusilimu.” Muda uleule wale machifu wa lile kabila wakamtisha na wakamfanya aikabili idadi kubwa ya askari.

Hivyo, akawaamrisha wale askari wa Uislamu kurejea na akawarudisha Madina, licha ya ukweli kwamba walipaswa kupigana kishujaa.”

Kurejea kwa jeshi la Uislamu na pia katika hali ile inayosemekana, kulimgusa Mtume (s.a.w.w.). Sasa akakabidhi ukamanda wa jeshi hili kwa rafiki yake Abubakr, Umar. Wakati huu wale maadui walikuwa na tahadhari zaidi kuliko pale mwanzo na wakawa wamejificha kwenye mlango wa kuingilia bondeni mle nyuma ya mawe na miti. Wakati wa kuwasili kwa jeshi la Uislamu walitoka mle kwenye maficho kwa nguvu. Hivyo, yule kamanda wa jeshi alilazimika kukimbia na kurejea Madina.

Amr bin Aas, mwanasiasa mwenye hila wa Uarabuni ambaye wakati ule ndio kwanza kwamba alisilimu, alimjia Mtume (s.a.w.w.) na kusema: “Vita ni udanganyifu.” Alikuwa na maana ya kusema kwamba ushindi katika vita hautegemei ujasiri na nguvu tu, lakini vilevile unatokana na uhodari na udanganyifu ambao ni lazima utumike juu ya adui ili kupata ushindi. Aliongeza kusema: “Kama nikiruhusiwa kuwaongoza askari wa Uislamu, nitafaulu kulifikia lengo lihitajikalo.” Kwa ajili ya kulifikia lengo jema Mtume (s.a.w.w.) aliikubali rai yake lakini yeye naye kama ilivyokuwa kwa wale makamanda wa awali, alikutana na matatizo yale yale.

Sayyidna Ali (A.S.) Ateuliwa Kuwa Kamanda Wa Jeshi Lile

Kushindwa kulikoandamana kumewahuzunisha mno Waislamu. Hatimaye Mtume (s.a.w.w.) aliandaa jeshi na akamteua Sayyidna Ali (a.s.) kuwa kamanda na akampa Ali (a.s.) bendera mkononi mwake na akamwomba mkewe Bibi Fatimah (a.s.) ampe kitambaa alichokuwa akikifunga kichwani awapo kwenye hali ngumu. Yule binti yake Mtume alilia sana kumwona mumewe mpendwa akiwa anakwenda kwenye safari ya hatari mno.

Mtume (s.a.w.w.) alimfariji na akayafuta machozi machoni mwake. Kisha Mtume (s.a.w.w.) akamsindikiza Sayyidna Ali hadi kwenye Masjidul Ahzaab. Sayyidna Ali (a.s.) akampanda farasi mwenye madoa ya rangi mbili huku akiwa amevaa mavazi mawili yaliyofumwa nchini Yaman, na mkononi mwake akiuchukua mkuki uliotengenezwa Hind,4 na akatoka. Aliubadili kabisa utaratibu wa safari kiasi kwamba wale askari wakaanza kudhania kwamba alikuwa akienda Iraq. Mtume (s.a.w.w.) aliyekuwa akimtazama pale alipokuwa akiondoka, alisema: “Yeye ni kamanda mpiganaji ambaye kamwe hakimbii kutoka uwanja wa mapambano.”

Kuihusisha kauli hii makhsusia kwa Sayyidna Ali (a.s.), kunaonyesha kwamba wale makamanda wa awali sio tu kwamba wameshindwa, bali kinyume na misingi ya kijeshi ya Uislamu, kule kurudi nyuma kwao vilevile kulikuwa na maana ya kushindwa.

Siri Ya Ushindi Wa Sayyidna Ali (A.S.) Kwenye Vita Hivi

Siri ya ushindi alioupata Ali (a.s.) kwenye vita hivi inaweza kuelezwa kwa mukhtasari katika sababu tatu zifuatazo:

Hakumwezesha adui kutambua matendo yake, kwa sababu aliibadili njia yake ili kwamba, taarifa zenye kuzihusu mbinu zake zisifike kwa yule adui kupitia kwa Waarabu mabedui na makabila ya jirani.
Alitenda juu ya kanuni muhimu ya kijeshi, yaani kujificha. Alisafiri wakati wa usiku na kujificha kwenye sehemu fulani wakati wa mchana na aka- pumzika. Alikuwa bado hajaufikia ule mlango wa lile bonde pale alipowaamrisha askari wote kupumzika. Na ili adui asitambue kuwasili kwao karibu na lile bonde, vile vile aliwataka wale askari wa Uislamu kuifunga midomo ya farasi wao ili milio yao isimwamshe yule adui. Alfajiri ilipoingia alisali pamoja na wafuasi wake kisha akawaamrisha wale askari waanze kuupanda ule mlima kutoka kwenye upande wa nyuma wa mlima ule, na akawaingiza kwenye lile bonde kutoka juu ya mlima.

Chini ya uongozi wa afisa shujaa na jasiri, wale askari waliendelea mbele kama mmiminiko wa maji na kuanza kuwashambulia kama radi wale maadui wakiwa bado wamelala. Baadhi yao wakauwawa na wengine wakakimbia.

Ushujaa wa Amirul-Mu’minin usio kifani, aliyewaua wapinzani saba, ulimzidi nguvu yule adui.
Waliogopa sana kiasi kwamba walipojikuta wakiwa hawana uwezo wa upinzani zaidi, walikimbia huku wakiziacha ngawira nyingi sana nyuma yao.5

Yule kamanda shujaa alirejea madina na akavikwa taji la heshima. Mtume (s.a.w.w.) akifuatana na baadhi ya masahaba zake wakamlaki. Alipomwona Mtume (s.a.w.w.) alishuka kwenye mnyama wake upesi sana. Mtume (s.a.w.w.) alipokuwa akiupiga mgongo wa Sayyidna Ali (a.s.) ili kumpongeza, alimwambia: “Mpande farasi wako. Allah na Mtume Wake wamekuridhia.”

Hapo machozi yakaanza kumtiririka mashavuni mwake kutokana na furaha nyingi, na kisha Mtume (s.a.w.w.) aliitamka hii kauli ya kihistoria kuhusiana na Sayyidna Ali (a.s.): “Kama si kwa kuchelea kwamba kikundi cha wafuasi wangu wanaweza wakayasema kuhusiana nawe mambo kama yale wayasemayo Wakristo kuhusiana na Nabii Isa, ningalisema mambo yahusianayo nawe, ambayo watu wangaliliona vumbi lililochini ya wayo wako kuwa ni kitu cha baraka popote pale upitapo.”6

Ushujaa huu wa kujitoa mhanga ulikuwa na thamani kubwa mno kiasi kwamba Sura al-Aadiyaat ilifunuliwa kuhusiana na tukio hili na kiapo chake kisicho kifani na chenye kushtusha kinalenga katika kuuridhia moyo wa kijeshi na ujanadume wa wale askari mashujaa walioshiriki kwenye vita hii. Zifuatazo hapa chini ni baadhi ya aya za Sura hii: “Naapa kwa farasi wendao mbio wakipumua. Na wakitoa moto kwa kupiga kwato zao chini. Wakishambulia wakati wa asubuhi. Huku wakitimua vumbi. Na wakijitoma kati ya kundi..” (Sura al-Aadiyaat, 100:1-5).

Aya hizo hapo juu ni muhtasari wa tukio la vita vya Dhatus-Salasil kama lilivyoandikwa na wafasiri wa Qur’ani na wanahistoria wa Kishi’ah juu ya msingi wa wanachuoni waaminiwao. Hata hivyo, wanahistoria wa Kisunni kama vile Tabari, wametoa masimulizi mengine ya tukio hili yenye kutofautiana na yale tuliyoyaeleza hapo juu. Si jambo lisilowezekana kwamba vita mbili zote zina jina la Dhatus-Salasil na kila kundi limesimulia matukio ya moja kati ya hizo vita mbili na kuiacha ile nyingine kutokana na sababu fulani fulani.7

  • 1. Tafsirul Qummi, uk. 733.
  • 2. Inawezekana kwamba Bonde la Raml (jangwa la mchanga) na Bonde la Yaabis (jangwa kavu ) ni sehemu ile ile.
  • 3. Al-Irshaad, uk. 84.
  • 4. Hind ni jina la mji.
  • 5. Tafsirul Furaat, uk. 222-226; Majma’ul Bayaan, Juz. 1, uk. 528.
  • 6. Al-Irshaad, uk. 84-86.
  • 7. Tarikhut-Tabari, Juz. 3, uk. 30; Siiratu Halabi, Juz. 3, uk. 215; Maghaazil- Waaqidi, Juz. 2, uk. 769-774.