Sura Ya 48: Kutekwa Kwa Mji Wa Makka (Faatihu-Makkah)

Ukiachilia mbali kule kuwa moja ya matukio makuu ya historia ya Uislamu, kutekwa kwa mji wa Makka hutoa mwanga kwenye malengo na shabaha takatifu za Mtume na maadili yake ya hali ya juu sana.

Katika kipindi hiki cha historia, imani njema na uaminifu wa Mtume (s.a.w.w.) na masahaba zake kuhusiana na vifungu vya mkataba wa Hudaybiyah waliousaini, hudhihirika, na zaidi ya hapo ni kuwa kuvunja ahadi na uaminifu kwa Waquraishi kuhusiana na kufungamana na masharti ya mapatano yale hudhihirika pia.

Kuchunguza sehemu hii ya historia kunathibitisha ustadi na busara za Mtume (s.a.w.w.) na sera ya hekima aliyoitumia katika kuiteka ngome ya mwisho na iliyokuwa madhubuti zaidi.

Inaonyesha kwamba mtu huyu wa Allah ameitumia sehemu ya uhai wake kwenye moja ya vyuo vya kijeshi vilivyo vikuu zaidi, kwa sababu alipanga mipango ya kupatia ushindi kama vile afanyavyo kamanda mwenye uzoefu, katika hali ambayo Waislamu waliweza kuupata ushindi huu mkuu bila ya kazi ngumu wala shida.

Hata hivyo, huba ya Mtume (s.a.w.w.) kwa wanadamu na kuwajibika kwake na usalama wa maisha na mali ya maadui zake, nako kunadhihirishwa kwenye kipindi hiki cha historia. Kama tutakavyoona hivi karibuni, mtu huyu mashuhuri aliyekuwa akionyesha kuona mbele kwake, aliyatupilia mbali maovu ya Waquraishi baada ya kupata ushindi na akatangaza msamaha kwa watu wote. Yafuatayo hapa chini ni maelezo kwa urefu ya tukio hili:

Katika mwaka wa sita Hijiriya, yalifanyika mapatano baina ya machifu wa Kiquraishi na Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) na yakasainiwa na pande zote mbili. Kufuatana na kifungu cha tatu cha mapatano yale Waquraishi na Waislamu walikuwa huru kufanya mapatano na makabila mengine kwa kadiri watakavyopenda.

Kutegemeana na kifungu hiki, kabila la Bani Khuza’ah lilifanya mapatano na Waislamu na Mtume (s.a.w.w.) alichukua jukumu la kuyahami maji yao, nchi yao, uhai wao na mali zao. Kabila la Bani Kananah waliokuwa maadui wa tangu kale wa kabila la jirani yao Bani Khuz?’ah, lilifanya mapatano na Waquraishi. Jambo hili lilitekelezwa kwa mujibu ambao kwamba udumishaji wa amani wa Bara Arabuni kwa jumla utatimia. Kwa mujibu wa mapatano ya Amani ya Hudaybiyah, yale makundi mawili (la Waislamu na marafifiki zao, na Waquraishi na marafiki zao) yasiasi moja dhidi ya jingine na vile vile wasichochee marafiki wa kundi moja kuasi dhidi ya marafiki wa kundi jingine.

Ilipita miaka miwili baada ya kufanyika kwa mapatano haya, na pande zote mbili zilitumia wakati huu kwa amani, na katika miaka iliyofuatia ya mapatano yale Waislamu waliweza kwenda kufanya hija kwenye Ka’abah kwa uhuru kabisa na wakazifanya ibada zao mbele ya maelfu ya waabudu masanamu waliokuwa kwenye kambi ya adui.

Katika mwezi wa Jamadiul-Awwal wa mwaka wa nane Hijiriya Mtume (s.a.w.w.) aliwapeleka askari wenye nguvu 3000 chini ya uongozi wa maafisa watatu wa Uislamu mashujaa kuelekea kwenye mipaka ya Shamu, kwenda kuwaadhibu watawala wa Kirumi kwa kuwaua wahubiri wa Kiislamu wasiokuwa na ulizi kwa namna ya uonevu na ukatili mkubwa. Hawa mashujaa wa Uislamu waliyaokoa maisha yao kwenye msafara huu na si zaidi ya makamanda wao watatu na askari wachache waliuawa, lakini hawakurejea na ushindi uliokuwa ukitegemewa kuletwa na Mujahidiin wa Uislamu, na kazi yao haikuwa tofauti na hali yashambulia na kukimbia.

Kuenea kwa taarifa hii kuliwashawishi Waquraishi nao wakaanza kufikiria kwamba nguvu ya kijeshi ya Waislamu imedhoofika nao wamekwisha kuupoteza moyo wa ushujaa na kujitoa mhanga.

Hivyo wakaamua kuivuruga hali ya hewa ya amani na utulivu. Katika hatua yao ya kwanza waligawa silaha miongoni mwa watu wa kabila la Bani Bakr na kuwachochea kufanya mashambulizi ya usiku dhidi ya Bani Khuz?’ah waliokuwa washirika wa Waislamu, na hatimaye kuwaua baadhi yao na kuwafunga wengine. Hata hivyo, hawakutosheka na hilo tu, bali vilevile kikosi cha Waquraishi kilishiriki kwenye yale mashambulio dhidi ya Bani Khuza’ah. Hivyo waliyavunja masharti ya mapatano ya Amani ya Hudaybiyah na wakaibadili ile amani na utulivu wa miaka miwili kuwa vita na umwagaji wa damu.

Matokeo ya mashambulizi haya ya usiku ni kwamba baadhi ya watu wa kabila hili waliokuwa wamelala wakati ule na waliokuwa wakisali, waliuawa na wengine wakafanywa wafungwa. Wachache wao waliyatoka majumba yao na wakakimbilia Makka sehemu iliyokuwa ikihesabiwa kuwa sehemu ya amani miongoni mwa Waarabu.
Wale wakimbizi waliokwenda Makka walikwenda nyumbani kwa Budayl bin Warq?1 na kumhadithia kile kisa cha kuhuzunisha cha kabila lao.

Ili kwamba taarifa za msiba wao ziyafikie masikio ya Mtume (s.a.w.w.) walimtuma Amr Sal?m chifu wa kabila lao kwa Mtume (s.a.w.w.).

Alipowasili mjini Madina alikwenda moja kwa moja hadi msikitini na akasimama mbele ya watu, kwa sauti maalum alisoma beti za shairi zenye kuzipasua nyoyo zionyeshazo dhulma iliyotendewa kabila la Bani Khuz?’ah na maombi yao ya msaada, na akamkumbusha Mtume (s.a.w.w.) kuyaheshimu yale mapatano aliyoyafanya baina yake na wao. Alimwomba Mtume (s.a.w.w.) awasaidie na kuilipizia kisasi damu ya wale waliodhulumiwa. Mwishoni mwa shairi hili, alisema:

“Ewe Rasuli wa Allah! Wakati baadhi yetu walipokuwa kwenye ukingo wa maji ya Watiir na wengine walikuwa wakisali, Waquraishi waabudu masanamu, walioyatia saini yale mapatano ya kutoshambuliana kwa kipindi cha miaka kumi, waliwashambulia watu wetu wasio na ulinzi wala silaha wakati wa usiku wa manane na kuwaua ovyo”. Aliurudia ubeti huu: “Walituchanja ambapo sisi tulikuwa Waislamu.” mara nyingi kiasi cha kuibua hisia na moyo wa askari wa Waislamu wapiganaji wa panga.

Mashairi yenye kuziibua nyoyo ya chifu wa lile kabila yalikuwa na athari zake. Mtume (s.a.w.w.) alimgeukia Amr mbele ya mkusanyiko mkubwa wa Waislamu na akasema: “Ewe Amr bin Sal?m! Tukusaidieni.” Jibu hili lenye maamuzi lilileta faraja ya kiakili kubwa sana kwa Amr, kwa sababu alikuwa na uhakika kwamba karibuni tu Mtume (s.a.w.w.) atalipiza kisasi ule msiba waliotiwa Bani Khuza’ah na Waquraishi waliokuwa sababu halisi ya tukio lile la kimsiba.

Hata hivyo, hakuweza kudhania kwamba kazi hii italeta kutekwa kwa mji wa Makkh na mwishilizo wa utawala wa kidhalimu wa Waquraishi.

Mara tu baada ya hapo alifika Budayl bin Waraqa kwa Mtume (s.a.w.w.) pamoja na kikundi cha watu wa kabila la Khuza’ah ili kuomba msaada. Alimwarifu Mtume (s.a.w.w.) kuhusu ushirika wa Waquraishi na Bani Bakr katika kuwapiga na kuwaua watu wa Bani Khuz?’ah, na kisha wakarejea Makka.

Uamuzi Wa Mtume (S.A.W.W.) Wawatia Waquraishi Kiwewe

Waquraishi walijuta mno kuhusiana na yale waliyoyatenda, nao walitambua ya kwamba wamewapa Waislamu udhuru wa hatari mno na wametenda tendo lililouvunja moyo wa yale mapatano na masharti yake. Kwa lengo la kumtuliza Mtume (s.a.w.w.) na kupata uthibitisho wa kuyaimarisha mapatano ya miaka kumi (na kwa mujibu wa maelezo fulani) kwa ajili ya kuyaendeleza,2 walimtuma kiongozi wao Abu Sufyani kwenda Madina ili aweze kuyaficha makosa na uasi wao kwa njia zote ziwezekanazo. Alitoka kwenda Madina na alipokuwa njiani alikutana na Budayl, yule kiongozi wa Bani Khuz?’ah mahali paitwapo Asfan palipo karibu na Makka. Alimwuliza Badayl kama alikuwa Madina na kama amemweleza Muhammad mambo yaliyotokea karibuni.

Budayl akamweleza ya kwamba alikwenda kuwaona ndugu zake waliodhulumiwa na kuwafariji, na katu hakuwa Madina. Baada ya kuyasema hayo alirejea Makka. Hata hivyo Abu Sufyani alikivunja kinyesi cha ngamia wa Budayl na akaona humo kokwa za tende yenye sifa za tende ya Madina. Hapo akawa na uhakika kwamba Budayl alikwenda Madina kuonana na Mtume (s.a.w.w.).

Abu Sufyani akafika Madina na akaenda moja kwa moja nyumbani kwa binti yake Bibi Ummi Habibah mkewe Mtume (s.a.w.w.).
Alitaka kukaa kwenye mkeka aliokuwa akikalia Mtume (s.a.w.w.), lakini yule binti yake akaukunja. Abu Sufyani akamwambia binti yake: “Je, hukuuona mkeka huo kuwa ni wenye kunifaa au baba yako kufaa kwa mkeka huo?” Binti yake akamjibu, akasema: “Mkeka huu ni maalum kwa ajili ya Mtume, na kwa kuwa wewe ni kafiri, sipendi kwamba mtu aliye kafiri asiye tohara akae kwenye mkeka wa Mtume.”

Hivyo ndivyo hoja ya binti wa mtu aliyekwenda kinyume na Uislamu kwa kipindi kirefu cha miaka ishirini. Hata hivyo, kwa kuwa Bibi huyu mtukufu alilelewa kwenye mahadhi ya Uislamu na fundisho la Upweke wa Allah, mafungamano yao ya kiroho yalikuwa na nguvu mno kiasi kwamba aliifanya kuwa duni ile mielekeo na mivuto yote ya mtoto kwa baba yake, ikilinganishwa na nguvu yake ya kidini.

Abu Sufyani aliingiwa na wasiwasi mwingi kuhusiana na tabia za binti yake aliyekuwa kimbilio lake pekee mle mjini Madina.

Akaitoka nyumba ya binti yake na kwenda kwa Mtume (s.a.w.w.) na kuzungumza naye kuhusu kuendelezwa na kuimarishwa kwa yale mapatano ya Amani. Hata hivyo, ilimbidi kukabiliana na kimya cha Mtume (s.a.w.w.), jambo lililoonyesha kutojali kwa Mtume (s.a.w.w.) juu ya rai ile.

Abu Sufyani alionana na baadhi ya masahaba wa Mtume (s.a.w.w.) ili aweze kumwendea tena kupitia kwao, na kwa njia ile aweze kulifikia lengo lake. Lakini mawasiliano haya nayo hayakuzaa matunda. Mwishowe akaenda nyumbani kwa Sayyidna Ali (a.s.) na akazungumza naye hivi: “Wewe ndiwe mtu uliye karibu zaidi na mimi mjini humu kwa sababu u ndugu yangu. Hivyo basi, ninakuomba uniombee kwa Mtume.” Sayyidna Ali (a.s.) akamjibu akasema: “Sisi katu hatuingilii katika mambo ambayo tayari Mtume kaishafanya uamuzi.”

Baada ya kukatishwa tamaa na upande wa Sayyidna Ali (a.s.), alimgeukia Bi. Fatimah Zahra (a.s.) mkewe Sayyidna Ali na binti wa Mtume (s.a.w.w.), na akaona kwamba wanawe wawili Hasan na Husain (a.s.) walikuwa karibu naye. Ili kuuamsha mvuto wake alimwambia: “Ewe binti wa Mtume! Yawezekana kwamba unaweza ukawaeleza wanao kuwapatia watu wa Makka kimbilio na wao kuwa machifu wa Uarabuni hadi mwisho wa muda na kuwako kwa dunia.” Bibi Zahra (a.s.) aliyekuwa akiitambua nia mbaya ya Abu Sufyani, mara moja akasema: “Jambo hili liko mikononi mwa Mtume, na wanangu hivi sasa hawana cheo cha aina hiyo.”

Alirejea tena kwa Sayyidna Ali (a.s.) na kusema: “Mpendwa Ali! Hebu niongoze kwenye jambo hili.” Sayyidna Ali (a.s.) akamjibu akasema: “Hakuna njia ya kutokea kwenye tatizo hili, ila kwamba uende msikitini na kutangaza tangazo la usalama kwa Waislamu.” Akauliza: “Je, kama nikifanya hivyo, itakuwako faida yoyote ile?” Ali (a.s.) akamjibu akasema: “Si sana, lakini mimi sidhani kama kuna kitu kingine hivi sasa.”

Abu Sufyani aliyekuwa akiutambua ukweli, unyoofu na usafi wa Sayyidna Ali (a.s.) alikwenda msikitini na kuyatekeleza yale aliyokuwa akiyafikiria.

Kisha alitoka msikitini mle na akaenda Makka. Kufuatana na taarifa alizowapa wale machifu wa Waquraishi kuhusu kile alichokitenda kule Madina, vile vile aliutaja ushauri aliopewa na Ali, na akasema: “Kufuatana na ushauri niliopewa na Ali, nilikwenda msikitini na nikatangaza usalama kwa Waislamu.” Wale waliokuwapo pale wakamwambia: “Ushauri wa Ali haukuwa chochote ila ni mzaha, kwa sababu Mtume hakulisikizi tangazo lako la usalama kwa Waislamu na tangazo la upande mmoja halina faida yoyote.” Kisha wakafanya mikutano mingine zaidi ili kupata njia ya kuwatuliza Waislamu.3

Jasusi Akanaswa

Maisha yote ya Mtume (s.a.w.w.) yaonyesha kwamba daima alikuwa akijitahidi kwamba adui asalimu amri kwenye ukweli na katu hakufikiria kulipiza kisasi kwa adui au kumwangamiza. Katika vita nyingi ambazo Mtume (s.a.w.w.) alishiriki yeye mwenyewe binafsi au alituma kikosi kwenda kupigana, daima lengo lake lilikuwa kwamba mipango ya maadui iweze kushindwa, umoja wao ukome na watu wao watawanyike. Hii ni kwa sababu alitambua kuwa, vizuizi vilivyoko kwenye njia ya Utangazaji wa Uislamu vikiondolewa hoja za Uislamu zenye nguvu zitafanya mvuto wake katika mazingira huru, na kama wale watu ambao mkusanyiko wao na uundaji wa mifarakano ulizuia kupenya kwa utangazaji wa Uislamu wangelinyang’anywa silaha na kukoma kuwa katika hali ya vita na wasiweke akilini mwao matumaini ya kupata ushindi juu ya Uislamu, basi watalazimika kuvutika kuelekea kwenye Uislamu na kwa kawaida watakuwa wenye kuunga mkono Uislamu na marafiki.

Hivyo, mataifa mengi yaliyoshindwa ambayo yalizidiwa kwa nguvu za kijeshi za Uislamu, baadae yatayafikiria mafunzo yake matukufu katika mazingira ya mbali na fujo na ghasia na hatimaye yatavutika kwenye dini hii na watajishughulisha na utangazaji wa ile dini ya Upweke wa Allah.

Wakati wa kutekwa kwa mji wa Makka, jambo hili lilijitokeza katika mdhihiriko wake katika hali yake ya ukamilifu. Mtume (s.a.w.w.) alitambua kwamba, iwapo atauteka Mji wa Makka, akamnyang’anya silaha adui na akayafanya mazingira kuwa ya amani, wale watu waliokuwa maadui wake wakubwa wakati ule mara moja watakuwa waumini waaminifu wa Uislamu. Hivyo basi, ilikuwa muhimu kushinda na kumtiisha adui lakini si kumwangamiza na vile vile kuzuia umwagaji wa damu kadiri iwezekanavyo.

Ili kulifikia lengo hili takatifu (kumtisha adui bila ya umwagaji wa damu), ile kanuni ya kumshitukiza adui haina budi kufuatwa, na adui huyu hana budi kushambuliwa na kunyang’anywa silaha kabla ya kufikiria kukusanya majeshi na kujihami. Hata hivyo, kanuni ya kushitukiza dhidi ya adui inaweza kutekelezwa wakati siri zote za jeshi la Waislamu zinapobakia kuwa salama na adui asijue kama Mtume (s.a.w.w.) ameamua kushambulia au alikuwa akifikiria tu juu ya jambo lile. Vile vile ilikuwa muhimu kwamba yule adui asiyatambue matendo na mbinu za jeshi la Waislamu.

Mtume (s.a.w.w.) aliamrisha matayarisho ya watu wote kwenda kuuteka mji wa Makka na kuitiisha ngome ya ibada ya masanamu iliyokuwa madhubuti zaidi. Lengo lake lilikuwa ni kuipindua serikali ya kidhalimu ya Waquraishi iliyokuwa kizuizi kikuu katika maendeleo ya Uislamu. Vile vile alimwomba Allah kwamba majasusi wa Waquraishi wasivitambue vitendo vya Waislamu.

Ili kuidumisha siri kamili njia zote zilizokuwa zikielekea Makka zililindwa na Waislamu walioteuliwa kwa lengo hili, na utawala madhubuti ulifanyika kuhusiana na upitaji wa watu.

Ilikuwa bado askari wa Uislamu hawajaondoka pale Malaika Mkuu Jibriil alipomwarifu Mtume (s.a.w.w.) kwamba mjinga mmoja aliyeichukua nafasi yake kwenye safu za Waislamu amewaandikia barua Waquraishi na amempa mwanamke mmoja barua ile aitwaye Sarah ili awapelekee kwa malipo ya mshahara, na kwenye barua ile baadhi ya siri za kijeshi za Uislamu ikiwa ni pamoja na shambulio lao alilokusudia kulifanya hivi karibuni dhidi ya mji wa Makka, limefichuliwa ndani ya barua hiyo.

Sarah alikuwa msichana mwimbaji wa mjini Makka ambaye katika nyakati fulani fulani, vile vile aliimba nyimbo za maombolezo kwenye hafla za maombolezo za Waquraishi. Baada ya vita ya Badr, kazi yake mle mjini Makka ililegalega kwa sababu kutokana na idadi kubwa ya watu muhimu kuuawa kwenye vita vile, Makka ilizama kabisa kwenye huzuni, na haukuwepo tena wakati wa hafla za muziki na anasa. Zaidi ya hapo, ili ghadhabu na mfundo wa Waquraishi ubakie, tamaa yao ya kulipiza kisasi isife, uimbaji wa nyimbo za huzuni ulipigwa marufuku.

Kutokana na sababu tuliyoitaja hapo juu, Sarah alikuja Madina baada ya miaka miwili tangu kupiganwa kwa vita vya Badr. Mtume (s.a.w.w.) alipomwuliza kama alishasilimu, akasema: “Hapana”. Kisha Mtume (s.a.w.w.) akamwuliza ni kwa nini kaja Madina.
Kwa swali hili alisema: “Kwa upande wa asili na nasaba, ninatokana na Waquraishi. Hata hivyo, baadhi yao wameuawa na wengine wamehamia Madina. Baada ya Vita vya Badr kazi yangu ilipungua nguvu nami nimekuja hapa kutokana na shida.” Hapo Mtume (s.a.w.w.) aliamrisha kwamba upesi sana apewe chakula na nguo kwa ajili ya baridi kadiri ihitajikavyo.

Sarah alifanyiwa matendo ya huruma sana na Mtume (s.a.w.w.), lakini kwa kupata ujira wa dinari kumi kutoka kwa Hatib bin Abi Balta’ah, aliamua kufanya ujasusi dhidi ya Uislamu na kuwapelekea Waquraishi barua yake yenye taarifa zihusuzo kuwako tayari kwa Waislamu kuuteka mji wa Makka. Mtume (s.a.w.w.) aliwaita askari watatu mashuja na kuwaamrisha waende Makka kumkamata yule mwanakme popote pale watakapomwona na kuichukua ile barua.

Watu wale waliopewa jukumu lile walikuwa ni Sayyidna Ali (a.s.), Zubayr na Miqdad. Walimkamata mwanamke yule mahali paitwapo Rauzat Khakh na wakaipekua mizigo yake kwa makini lakini hawakupata kitu. Vile vile yule mwanamke alikataa kabisa kwamba alichukua barua yoyote ile kutoka kwa Hatib. Sayyidna Ali (a.s.) akasema: “Ninaapa kwa jina la Allah! Katu Mtume wetu hasemi uwongo. Huna budi kuitoa barua hiyo au la, tutaichukua kutoka kwako kwa njia zozote zile ziwezekanazo!”

Wakati ule Sarah alitambua kwamba Sayyidna Ali (a.s.) alikuwa askari asiyekata tamaa juu ya upekuzi ule hadi aitekeleze amri ya Mtume (s.a.w.w.). Hivyo basi alimwomba awe mbali naye. Kisha akaitoa barua ndogo kutoka kwenye msuko wa nywele zake na kumpa Sayyidna Ali (a.s.).

Mtume (s.a.w.w.) aliingiwa na wasiwasi kuona kwamba jambo lile limetendwa na mwislamu, mwenye rekodi ndefu ya huduma na aliyekuwa na shauku ya kuusaidia Uislamu hata kwenye hali ngumu. Hivyo basi alimwita Hatib na akamtaka aeleze msimamo wake. Aliapa kwa jina la Allah na Mtume Wake na akasema: “Hakuna kulegalega kulikotokea kwenye imani yangu. Hata hivyo, ninaishi peke yangu hapa Madina, na watoto wangu na ndugu zangu wanasumbuliwa na shinikizo la mateso huko Makka mikononi mwa Waquraishi. Hivyo basi, lengo langu katika kuipeleka taarifa hii lilikuwa kwamba Waquraishi wapunguze mateso wawatendeayo watu wangu.”

Udhuru alioutoa Haatib waonyesha kwamba, ili kupata taarifa kuhusiana na siri za Waislamu, machifu wa Waquraishi waliwatesa ndugu za Waislamu waliokuwa wakiishi mjini Makka na kuweka kuwa ni sharti la uhuru wao pindi wapatapo taarifa muhimu kutoka kwa ndugu zao walioko Madina.

Ingawa udhuru alioutoa Hatib haukuwa na msingi mzuri, Mtume (s.a.w.w.) aliukubali kutokana na sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na huduma zake za muda mrefu alizozitoa katika njia ya Uislamu, na akamwachia.

Wakati Umar alipoomba ruhusa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w.) kukidengua kichwa cha Hatib, Mtume (s.a.w.w.) alimjibu akisema: “Ninamwachia kwa sababu alishiriki kwenye Vita vya Badr na siku moja alikuwa ni sababu asili ya baraka za Allah.”

Hata hivyo, ili kuhakikisha kwamba tukio la aina hii halirudiwi tena, aya tisa za kwanza za Surat al-Mumtahinah zilifunuliwa:4 “Enyi mlioamini! Msiwafanye adui Zangu na adui zenu kuwa marafiki .....” (Sura al- Mumtahinah, 60:1).

Mtume (S.A.W.W.) Na Waislamu Waenda Makka

Katika kuzizingatia kanuni za mashambulizi ya kuotea, muda wa kuondoka, utaratibu na lengo la safari ile vilielezwa na Mtume (s.a.w.w.). Amri ile ilitolewa mnamo mwezi 10 kumi Ramadhani, mwaka wa nane Hijiriya, ingawa Waislamu wa Madina na viungani mwake walipewa maelezo yake mapema kabla ya hapo ili kujiweka tayari.
Katika siku ambayo Mtume (s.a.w.w.) aliondoka Madina, alimteua mtu mmoja aliyeitwa Abu Ruhm Ghifari kuwa kaimu wake mjini humo na akalikagua jeshi lake nje ya mji wa Madina. Alipokuwa kaishasafiri umbali fulani kutoka Madina aliomba maji mahali paitwapo Kadid na akafungua swaumu yake na kisha akawaamrisha watu wote kufanya vivyo hivyo.

Wengi wao walizivunja swaumu zao, lakini wengine wakajizuia kufanya hivyo kwa kudhania kwamba kama wakifanya Jihadi wakiwa wamefunga watapata thawabu nyingi. Watu hawa wajinga hawakutambua kwamba Mtume huyo huyo ambaye aliamrisha kufunga mwezi wa Ramadhani vilevile hivi sasa ametoa amri ya kuivunja saumu yake, na kama yeye yu kiongozi wa kuelekea kwenye ustawi na ukweli, basi amri zake zote mbili zilikuwa kwa ajili ya mema ya watu na haukuwako ubaguzi kwenye amri zake.

Mtume (s.a.w.w.) alichukia alipogundua kwamba baadhi ya watu walikataa amri yake na akasema: “Watu hawa ni wenye dhambi na waasi.”5

Kuutafuta ubora kama huo na kumtangulia Mtume (s.a.w.w.) ni aina ya upotovu kutoka kwenye ukweli na kunaonyesha utovu wa imani ya watu wale juu ya Mtume (s.a.w.w.) na dini yake. Hivyo basi, Qur’ani Tukufu imewakemea watu hawa na inasema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تُقَدِّمُوا بَيْنَ يَدَيِ اللَّهِ وَرَسُولِهِ ۖ وَاتَّقُوا اللَّهَ ۚ إِنَّ اللَّهَ سَمِيعٌ عَلِيمٌ {1}

“Enyi mlioamini! Msitangulie mbele ya Allah na Mtume Wake, na mcheni Allah. Hakika Allah ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.” (Sura al-Hujurat, 49:1).

Abbas bin Abdul Muttalib alikuwa mmoja wa wale Waislamu waliokuwa wakiishi mjini Makka. Alikuwa akiishi pale chini ya ushauri wa Mtume (s.a.w.w.), naye alikuwa akimwarifu juu ya maamuzi yaliyochukuliwa na Waquraishi. Aliudhihirisha Uislamu wake baada ya Vita ya Khaybar, lakini uhusiano wake na machifu wa Waquraishi uliendelea kudumu. Aliamua kuondoka Makka akiwa ni familia ya Kiislamu ya mwisho kwenda kuishi Madina.

Ilikuwa ni kwenye siku za Mtume (s.a.w.w.) kwenda Makka pale Abbas alipoondoka Makka kwenda Madina na akakutana na Mtume (s.a.w.w.) njiani mahali paitwapo Ju’fah. Kuwepo kwa Abbas kulithibitika kuwa ni kwenye faida kwa ajili ya kutekwa kwa mji wa Makka na hivyo kulitoa faida kwa makundi yote mawili (Waislamu na Waquraishi). Inawezekana kwamba kama asingelikuwepo yeye, basi kutekwa kwa mji wa Makka kusingelitimia bila ya upinzani wa Waquraishi. Hivyo basi, inawezekana kwamba kutoka kwake mle mjini Makka kwenda madina kulifanyika kutokana na maelezo ya Mtume (s.a.w.w.) ili kwamba aweze kulifanya jukumu la kiusuluhishi kwenye tukio hili.

Kuonyesha Huruma Uwapo Mwenye Mamlaka Na Cheo

Maisha yaliyopita ya Mtume (s.a.w.w.) yenye kung’ara, tabia zake zenye kuridhisha, na ukweli na unyoofu wake vilikuwa maarufu sana kwa watu wa familia yake na ndugu zake, kwa ujumla ni kuwa jamaa zake wote walifahamu kwamba aliishi maisha ya heshima na katu hakupata kutenda dhambi yoyote au mashambulizi au kuzungumza lolote lile lililo la uwongo. Hivyo basi, tangu siku ya kwanza ya mwito kwa watu wote, karibuni watu wote wa familia ya Bani Hashim waliuitikia mwito wake na wakajikusanya na kumzunguka kama nondo wauzungukavyo mshumaa.

Mustashrik mmoja wa Kiingereza asiye na upendeleo, ameuchukulia ukweli huu kuwa ni ishara ya usafi na uchamungu wa Mtume (s.a.w.w.) na anasema: “Kila mtu vyovyote vile awavyo mwangalifu na mwenye kujihadhari, hawezi kuwaficha watu wa familia yake na ndugu zake mambo yote ya maishani mwake.
Kama Muhammad angalikuwa na fikira na tabia mbaya, vitu hivi visingeliweza kufichikana mbele ya ndugu zake nao wasingaliweza kuvutika naye upesi sana.”6

Hata hivyo, vilevile wako watu wachache miongoni mwa Bani Hashim waliokataa kumwamini. Mbali na Abu Lahab majina ya watu wawili wa aina hiyo, Abu Sufyani bin Harith na Abdullah bin Abi Umayah, yanaweza kutajwa kuhusiana na jambo hili. Waliudhihirisha uadui na ukaidi dhidi yake na sio tu kwamba hawakumwamini lakini vilevile walikuwa kizuizi katika njia ya ukweli na kuziumiza fikara za Mtume (s.a.w.w.).

Abu Sufyani alikuwa mwana wa Harith, ami yake Mtume (s.a.w.w.) na vilevile alikuwa nduguye wa kunyonya. Kabla ya kuanza kwa Utume, Abu Sufyani alimpenda sana Mtume (s.a.w.w.) lakini akawa adui kwake baada ya hapo. Abdullah alikuwa kaka yake Ummi Salmah (aliyekuwa mke wa Mtume) na mwana wa Atik Shangazi yake Mtume (s.a.w.w.) na binti wa Abdul Muttalib.

Hata hivyo, kuenea kwa Uislamu kwenye Rasi ya Uarabuni kuliwafanya hawa watu wawili kuamua kuutoka mji wa Makka na kujiunga na Waislamu. Wakati Mtume (s.a.w.w.) alipokuwa njiani kwenda mji wa Makka, hawa wawili walikutana na jeshi la Uislamu mahali paitwapoo Thanyatul Uqaab au Nabque ‘Uqaab. Pamoja na kusisitiza kwao, lakini Mtume (s.a.w.w.) alikataa kukutana nao. Na hata pale Ummi Salmah alipowaombea kwa mapenzi, Mtume (s.a.w.w.) alikataa mapendekezo yake, na akasema: “Ni kweli kwamba Abu Sufyani yu binamu yangu, lakini amenisumbua sana. Na yule mtu wa pili ndiye mtu yule aliyeniomba mambo ya kijinga7 naye amewazuia watu kusilimu.”

Sayyidna Ali Amirul-Mu’minin (a.s.) aliyekuwa akizifahamu vizuri tabia za Mtume (s.a.w.w.) na jinsi ya kuibua mwelekeo wake, aliwaambia wale watu wawili: “Nendeni mkakae mbele ya Mtume na itamkeni ile kauli waliyoitamka nduguze (Nabii) Yusuf walipoomba msamaha (kwa ndugu yao Nabii Yusuf a.s). Nduguze Nabii Yusuf walipokuwa wakiomba radhi, walisema: “Tunaapa kwa jina la Allah! Yeye (Allah) Amekupa upendeleo juu yetu nasi tumetenda dhambi.”

Naye Nabii Yusuf alipoyasikia maneno haya, aliwasamehe akisema: “Leo hapana lawama juu yenu. Allah atakusameheni, Naye ni Mwingi wa kurehemu kuliko wote wanaorehemu.”8

Kisha Amirul-Mu’minin aliongeza kusema: “Kama mkiitamka ile kauli ya awali bila shaka atakujibuni kwa ile kauli ya pili, kwa sababu yeye yu mtu asiyekuwa tayari hata kidogo kwamba mtu awe mkunjufu zaidi yake.”

Wale watu walifanya kama walivyoshauriwa na Sayyidna Ali (a.s.) na Mtume (s.a.w.w.) naye aliwasamehe kama alivyofanya Nabii Yusuf (a.s.). Kisha wote wawili wakalivaa vazi lihitajikalo kwa ajili ya Jihad, na wakabakia kuwa imara kwenye dini yao hadi mwishoni mwa maisha yao. Ili kuweza kufanya masahihisho ya yale aliyoyatenda huko nyuma, Abu Sufyani aliimba shairi la wasifu, ambalo ubeti wake wa kwanza ulisema: “Ninaapa kwa maisha yako! Siku nilizoichukulia bendera begani mwangu ili kwamba jeshi la Laat (sanamu lililokuwako mjini Makka) liweze kushinda dhidi ya jeshi la Muhammad, nilikuwa kama msafiri wa usiku aliyetatanishwa, anayepapasa gizani, lakini huu sasa ndio wakati ninapotakikana kuwa chini ya himaya ya mwongozo wa Mtume (s.a.w.w.).”

Ibn Hisham anaandika9 kwamba binamu yake Mtume (s.a.w.w.), Abu Sufyani bin Harith alimpelekea ujumbe Mtume (s.a.w.w.) akisema: “Kama huikubali imani yangu (yaani kusilimu kwangu) nitaushika mkono wa mwanangu mdogo na kwenda jangwani.” Na ili kuuibua mwelekeo wa huruma wa Mtume (s.a.w.w.), Bibi Ummi Salamah alisema:
“Mara kwa mara nimekusikia ukisema kwamba Uislamu huyafunika matendo ya wakati uliopita.” Kwa msingi huu, Mtume (s.a.w.w.) aliweza kukaribiwa na watu hao wawili.10

Mbinu Zenye Kuvutia Za Jeshi La Waislamu

Murruz Zahran iko kilometa chache kutoka Makka. Mtume (s.a.w.w.) aliliongoza jeshi lake lenye askari elfu kumi wenye nguvu hadi kwenye mpaka wa Makka ili kwamba Waquraishi na majasusi wao na mawakala wao wasiweze kutambua kwenda kwao pale.

Ili kwamba wakazi wa Makka waweze kusalimu amri bila ya upinzani na ile ngome kubwa na kituo kitakatifu kitekwe bila ya umwagaji damu, na ili kujenga hofu nyoyoni mwa wakazi wa Makka, Mtume (s.a.w.w.) aliwaamrisha Waislamu wawashe moto kwenye sehemu za miinuko. Vilevile aliamrisha kuwaogofya zaidi watu wa Makka kwa kumfanya kila mtu akoke moto wake ili ule moto na miali iangaze vilima vya jirani na sehemu za miinuko.

Waquraishi na washiriki wao walikuwa wamelala fofofo. Hata hivyo, ile miali iliyozipa sehemu zote za miinuko umbo la moto mkubwa ambao nuru yake ilizifikia nyumba za watu wa Makka, ulijenga hofu na wasiwasi nyoyoni mwao na kuzivutia fikara zao kwenye miinuko ile. Wakati ule ule machifu wa Waqurauishi kama vile Abu Sufyani bin Harb na Hakam bin Hiz?m walitoka mji wa Makka kwa ajili ya kufanya uchunguzi na wakajishughulisha na uchunguzi na ugunduzi.

Abbas bin Abdul Muttalib aliyekuwa akifuatana na Mtume (s.a.w.w.) alifikiria kwamba, kama jeshi la Waislamu likipingwa na Waquraishi watu wengi kutoka miongoni mwa Waquraishi watauwawa. Hivyo basi, aliamua kufanya kazi fulani itakayokuwa na faida kwa pande zote mbili na kuwashawishi Waquraishi wasalimu amri.

Alimpanda nyumbu mweupe wa Mtume (s.a.w.w.) na akaenda Makka wakati wa usiku wa manane ili kupitia kwa wakata miba na watema kuni aweze kuwaarifu machifu wa Waquraishi kuhusu kuzingirwa kwa Makka na jeshi la Waislamu, na kuifanya nguvu na moyo wa upiganaji vita wa Waislamu ufahamike kwao, na watambue ya kwamba wao (Waquraishi) hawana njia nyingine ila kusalimu amri. Hata hivyo, kwa mbali aliyasikia mazungumzo yafuatayo kati ya Abu Sufyani na Budayl Warq?;

Abu Sufyan: Sijawahi kuona moto mkubwa na jeshi kubwa kama hili.

Budayl bin Warqa’: Hao ni watu wa kabila la Khuza’ah, waliojitayarisha kwa ajili ya vita.

Abu Sufyan: Khuz?’ah ni wachache mno kuliko kiasi cha kuweza kuwasha moto mkubwa kiasi hiki au kuunda jeshi kubwa kama hili!

Hapo Abbas akayaingilia mazungumzo yao na akamwita Abu Sufyani na kumwambia: “Ewe Abu Hanzalah!”11 Upesi Abu Sufyani akaitambua ile sauti ya Abbas na kujibu: “Ewe Abul Fazal12, umesema nini?” Abbas akasema: “Ninaapa kwa jina la Allah! Udhia wote huu umeletwa na mashujaa wa Mtume wa Allah. Amewajia Waquraishi na jeshi kubwa lenye nguvu na haiwezekani hata kidogo Waquraihi kuwazuwia.”

Maneno ya Abbas yalimfanya Abu Sufyani atetemeke kwa nguvu mno. Akiwa mwenye hali ya woga, alimgeukia Abbas na kusema: “Wazazi wangu wawe fidia kwako! Dawa hasa ni nini?” Abbas akamjibu akasema: “Dawa iliyopo ni kwamba, wewe ufuatane nami hadi kwa Mtume (s.a.w.w.) na uombe usalama kwake, au sivyo uhai wa Waquraishi wote utakuwa hatarini.”

Kisha akamfanya aketi kwenye kiti cha nyuma cha nyumbu wake na akaenda naye kwenye kambi ya jeshi la Uislamu. Wale watu wawili wengine (Budayl bin Warqa na Hakam bin Hizam), waliokuja na Abu Sufyani kufanya uchunguzi wakarudi Makka.

Sasa kama iwezavyo kuonekana, Abbas alifanya kazi kwa faida ya Uislamu na akamfanya Abu Sufyani kuwa na woga mno juu ya nguvu za jeshi la Waislamu kiasi kwamba hakuweza kulifikiria jambo lolote ila kusalimu amri. Na kitendo chake kilichokuwa muhimu sana kilikuwa kwamba hakumruhusu Abu Sufyani arudi Makka bali alimleta kambini kwa Waislamu wakati wa usiku wa manane na hivyo kamtenga na pande zote mbili. Angelirejea Makka, basi ingeliwezekana kwamba angeshawishiwa na watu wenye siasa kali na wangeweza kufanya upinzani wa masaa machache.

Abbas Amfanya Abu Sufyan Apite Kwenye Kambi Ya Waislamu

Yule ami yake Mtume (s.a.w.w.) alimpanda nyumbu maalum wa Mtume (s.a.w.w.) na Abu Sufyani alifuatana naye. Alimpitisha baina ya ule moto mkubwa na lile jeshi kubwa lenye askari waendao kwa miguu na wenye kuwapanda wanyama. Wale walinzi wa doria walimtambua Abbas pamoja na yule nyumbu maalum wa Mtume (s.a.w.w.), na hivyo basi wakampisha apite, macho ya Umar yalimwangukia Abu Sufyani akiwa ameketi kwenye kiti cha nyuma cha nyumbu wa Abbas, na hapo akataka kumuuwa (Abu Sufyani) mara moja. Hata hivyo, kwa vile ami yake Mtume (s.a.w.w.) amempa hifadhi, yeye (Umar) akajizuia kufanya hivyo. Hatimaye Abbas na Abu Sufyani wakalifikia hema la Mtume (s.a.w.w.). Ami yake Mtume (s.a.w.w.) alipiga hodi na kisha akaingia. Hapo yalitokea mabishano makali baina ya Abbas na Umar mbele ya Mtume (s.a.w.w.). Umar alishikilia kwamba kwa vile Abu Sufyani alikuwa adui wa Allah hana budi kuuawa mara moja, ambapo Abbas alisema kwamba amempa hifadhi. Mtume (s.a.w.w.) aliwanyamazisha kwa kumwomba Abbas amweke Abu Sufyani kwenye hema wakati wa usiku ule na kumleta mbele ya Mtume (s.a.w.w.) asubuhi yake.

Abu Sufyan Afika Mbele Ya Mtume (S.A.W.W)

Kulipokucha Abbas alimleta Abu Sufyani mbele ya Mtume (s.a.w.w.) wakati ule Muhajiriin na Ansar walikuwa karibu na Mtume (s.a.w.w.). Macho ya Mtume (s.a.w.w.) yalipomwangukia Abu Sufyani, alisema: “Je, bado haujawadia wakati wa wewe kushuhudia ya kwamba hakuna mungu ila Allah?” Abu Sufyani akajibu akasema: “Wazazi wangu wawe fidia kwako! Wewe ni mvumilivu, mkarimu, na mpole kwa ndugu zako, kiasi gani! Sasa nimetambua kwamba kama angekuwako mungu ghairi ya Allah, hadi sasa angelifanya lolote lile kwa faida yetu.” Mtume (s.a.w.w.) alipoona kwamba ameushuhudia Upweke wa Allah, aliongeza kusema: “Je, wakati bado haujawadia wa wewe kutambua kwamba mimi ni Mtume wa Allah?” Kauli ya kwanza, akasema: “Wewe ni mvumilivu, mkarimu, na mpole kwa ndugu zako, kiasi gani! Hivi sasa bado ningali ninawaza juu ya Utume wako.”

Abbas alijihisi kuudhishwa na kule kuidhihirisha shaka yake (juu ya Utume wa Muhammad) na akasema: “Kama hutasilimu uhai wako utakuwa hatarini. Hivyo basi, huna budi kuushuhudia Upweke wa Allah na Utume wa Muhammad upesi sana kwa kadiri iwezekanavyo.” Abu Sufyani aliufuata ushauri ule na akajiunga na safu za Waislamu.

Abu Sufyani alisilimu kutokana na hofu, na imani ya aina hii haikuafikiana na malengo ya Uislamu hata kidogo, lakini katika hali hii ilifaa kwamba Abu Sufyani ajiunge na Waislamu kwa vyovyote vile iwavyo, ili kwamba kile kizuizi kikuu kilichoko kwenye njia ya watu wa Makka katika kusilimu kiondoke, kwa sababu yeye na wale walio mfano wake (yaani Abu Jahl, Ikrimah, Safwaan bin Umayah n.k) walikuwa ndio watu walioijenga hofu na woga tangu zamani na hakuna yeyote aliyeweza kuwa na moyo wa kuweza kuufikiria Uislamu au kuonyesha mwelekeo kwenye dini hii. Hata kama kusilimu kwa Abu Sufyani kusiwe na faida yoyote kwake, kulikuwa na faida mno kwa Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) pamoja na wale watu waliokuwa ndugu zake.

Hata hapo Mtume (s.a.w.w.) hakumwachilia Abu Sufyani, kwa kuwa hakuwa na uhakika juu ya matendo yake hadi Makka ilipotekwa. Hivyo basi, akamuelekeza kwamba kwa sababu zitakazotajwa baadae, hana budi kumzuia ndani ya njia nyembamba ya bonde. Abbas alimgeukia Mtume (s.a.w.w.) na kumwambia: “Abu Sufyani yu mtu mwenye tamaa ya cheo katika jamii na kwamba hivi sasa mambo yamegeuka kiasi hiki, ni bora umpe cheo fulani.”
Licha ya kweli kwamba katika kipindi cha miaka ishirini Abu Sufyani ameleta madhara makubwa sana kwa Uislamu na Waislamu, Mtume (s.a.w.w.) akiyazingatia maslahi makubwa, alimpa Abu Sufyani cheo na akatamka kauli ifuatayo ionyeshayo ukuu wa roho yake (s.a.w.w.):

“Abu Sufyani anapewa mamlaka kuwathibitishia watu kwamba yeyote akimbiliaye kwenye maeneo ya Masjidul Haram au akaziweka chini silaha zake na akatangaza kusalimu amri au akajifungia nyumbani kwake au akakimbilia nyumbani kwa Abu Sufyani au nyumbani kwa Hakim bin Hiz?m, atasalimika kutokana na usumbufu wa jeshi la Uislamu.”13

Makka Yasalimu Amri Bila Ya Kumwaga Damu

Jeshi kuu la Uislamu lilikuwa limefika karibu na Makka. Hata hivyo Mtume (s.a.w.w.) alipenda kwamba auteke mji ule bila ya upinzani wowote au kumwaga damu na adui asalimu amri bila ya masharti yoyote. Miongoni mwa visababisho vya hali hiyo, ukiachilia mbali kujificha na mashambulizi ya kuotea yaliyosaidia sana katika kulifikia lengo hili, kingine kilikuwa kwamba, Abbas, ami yake Mtume (s.a.w.w.) alikwenda Makka akiwa ni ishara ya hisani kwa Waquraishi na kumleta Abu Sufyani kwenye kambi ya Kiislamu, kwani machifu wa Waquraishi hawakuweza kuchukua uamuzi wa mwisho akosekanapo Abu Sufyani.

Abu Sufyani alipojisalimisha mbele ya ukuu usio kifani wa Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.), Mtume aliamua kupata faida kubwa katika kuwaogofya waabudu masanamu kwa kadiri iwezekanavyo kutokana na Abu Sufyan kuwako kwake pale. Hivyo basi alimtaka Abbas kumtia kizuizini kweye njia nyembamba ya bonde ili kwamba vikosi vya lile jeshi la Uislamu viweze kupita karibu yake na zana zao zote, naye aweze kuiona ile nguvu ya Uislamu na kisha atakaporejea Makka, aweze kueleza kuhusu jeshi la Uislamu na awazuie wasifanye upinzani. Baadhi ya vikosi vya Uislamu vilikuwa kama ifuatavyo hapa chini:

1. Kundi la askari elfu moja wenye nguvu, wa kabila la Bani Salim chini ya uongozi wa Khalid bin Walid, lililokuwa na bendera mbili. Moja ya bendera hizi ilishikwa na Abbas bin Mird?s na nyingine ilishikwa na Miqdadi.

2. Vikosi viwili vya mashujaa mia tano vilivyokuwa chini ya uamiri jeshi wa Zubayr Aww?m aliyekuwa na bendera nyeusi mkononi mwake. Wengi wa askari wa vikosi hivi viwili walikuwa ni Muhajiriin.

3. Kikosi chenye nguvu cha askari mia tatu wa kabila la Ghif?r chini ya uamiri jeshi wa Abu Dharr Ghif?ri aliyekuwa ameishika bendera.

4. Kikosi chenye nguvu cha askari mia nne cha kabila la Bani Salim kilichokuwa chini ya uamiri jeshi wa Yazid mwana wa Khusayb, aliyekuwa ameichukua bendera.

5. Vikosi viwili vyenye askari mia tano wa kabila la Bani Kaab vilivyokuwa chini ya uamiri jeshi wa Busr bin Sufyan, ambaye naye alikuwa kaishika bendera.

6. Kundi la askari elfu moja wenye nguvu wa Bani Muzaynah lililokuwa na bendera tatu. Bendera hizi zilikuwa mikononi mwa Nu’m?n bin Maqran, Bilal bin Harith na Abdullah Amr.

7. Kundi lenye askari mia nane la kabila la Bani Juhaynah, lilikuwa na bendera nne zilizoshikwa na Ma’bad bin Khalid, Suwayd bin Sakhra, Raafi bin Makith na Abdullah Badr.

8. Makundi mawili ya askari mia mbili wa makabila ya Bani Kananh, Bani Layth na Bani Hamzah, wakiwa chini ya uamiri jeshi wa Abu W?qid Laythi aliyekuwa akiishika bendera.

9. Kikosi chenye askari mia tatu wa kabila la Bani Ashja’, kilichokuwa kikichukua bendera mbili. Moja ya bendera hizi ilishikwa na Maqal bin Sanan na nyingine ilishikwa na Na’im bin Mas’ud.

Vikosi hivi vilipokuwa vipikipita mbele ya Abu Sufyani, upesi sana akataka maelezo kutoka kwa Abbas kuhusu vikosi hivi, na Abbas akampa jibu. Kitu kilichoongeza utukufu wa jeshi hili lenye utaratibu mwema kilikuwa kwamba wale makamandda wa jeshi walipofika mbele ya Abbas na Abu Sufyaan waliitamka Takbir “Allahu Akbar” mara tatu kwa sauti kubwa na baada ya hapo askari nao waliitamka mara tatu kwa sauti kubwa kwa njia ya ibada za Kiislamu.

Hii Takbir ilipiga mwangwi kwenye mabonde ya Makka kwa jinsi ambayo marafiki walivutiwa mno na ile nidhamu ya Uislamu, na maadui walijawa na hofu na woga mwingi. Abu Sufyani alikuwa akingojea bila ya subira kukiona kikosi alichokuwamo Mtume (s.a.w.w.). Hivyo, kila kikosi kilipopita karibu naye alimwuliza Abbas kama Muhammad alikuwamo mle.

Abbas aliendelea kumwambia: “Humu hayumo” hadi pale walipovutika na jeshi kubwa lililokuwa na takriban askari elfu tano ambamo mashujaa elfu mbili walikuwa wamevaa deraya na maamiri jeshi walikuwa wamezishika bendera nyingi kwa umbali maalum. Jina la kikosi hiki lilikuwa ni ‘Katiba- i Khazraa’ – yaani ‘jeshi kijani’. Askari wale walikuwa na silaha nyingi mno.

Miili yao yote iligubikwa na silaha na hakuna kilichoweza kuonekana ila macho yao maangavu. Farasi wenye mbio na ngamia wenye manyoya mekundu waliweza kuonekana kwa wingi kwenye kikosi hiki.

Mtume (s.a.w.w.) aliweza kuonekana katikati ya kikosi hiki akiwa amempanda ngamia wake maalum. Watu mashuhuri walikuwa wamemzunguka naye alikuwa akizungumza nao.

Utukufu wa kikosi hiki ulimtishia Abu Sufyani. Bila ya kudhamiria akamwambia Abbas: “Hakuna jeshi liwezalo kulizuia jeshi hili. Ewe Abbas! Ufalme wa mwana wa nduguyo umestawi kwa kiasi kikubwa mno.” Abbas alimjibu kwa kumkemea: “Asili ya nguvu ya huyu mwana wa ndugu yangu ni Utume aliopewa na Allah, na hauna chochote kile kihusianacho na nguvu ya nje ya hapo wala ya kidunia.”

Abu Sufyan Aenda Makka

Hadi hapo Abbas alikuwa amekwishatekeleza jukumu lake vizuri mno na amemvutia Abu Sufyani kwa ile nguvu ya kijeshi ya Mtume (s.a.w.w.). Kufikia hapo Mtume (s.a.w.w.) aliona kwamba inafaa kumwachilia Abu Sufyani ili aweze kwenda Makka kabla ya kuwasili kwa vile vikosi vya jeshi la Uislamu ili awaeleze watu kuhusu ile nguvu isiyo na kifani ya Waislamu na vile vile kuwaeleza watu wa Makka kuhusu njia ya usalama wao, kwa sababu kuwatishia tu watu bila ya kuwaonyesha njia ya usalama kusingalimwezesha Mtume (s.a.w.w.) kulifikia lengo lake.

Abu Sufyani alifika mjini mle. Watu waliokuwa na wasiwasi na woga usiku wote ule nao hawakuweza kufanya uamuzi wowote ule wakati Abu Sufyani akiwa hayupo, ndipo wakamzunguka. Akiwa na uso uliojaa huzuni na mwili unaotetemeka, na akiwa anasoza kidole chake kuelekea Madina, alisema: “Vikosi vya jeshi la Waislamu, ambalo haiwezekani kwa mtu yeyote kulizuia, vimeuzingira mji na vitaingia katika muda mfupi ujao.

Kiongozi wao Muhammad, ameniahidi kwamba uhai na mali ya kila akimbiliaye msikitini au kwenye sehemu ziizungukazo Ka’abah, au akaacha kupigana na akajifungia nyumbani mwake ikiwa ni dalili ya kutounga mkono upande wowote, au akaingia nyumba yangu, au nyumba ya Hakim bin Hiz?m, atasamehemwa na atabakia kuwa salama.”
Kwa ujumbe huu wa Abu Sufyani, alizidhoofisha mno nyoyo za watu kiasi kwamba hata wale waliokuwa wakifikiria kutoa upinzani waliliacha wazo lile. Hivyo, matayarisho yote yaliyofanywa usiku uliopita kutokana na zile hatua alizozichukua Abbas, yalithibitisha kuwa ni yenye kuzaa matunda ya kutekwa kwa Makkah, na kule kutokuwepo na upinzani kutoka kwa Waquraishi, kulionekana kuwa ni jambo kuu. Wale watu walioingiwa na woga walikimbilia kwenye sehemu mbalimbali, na matokeo ya huu mpango wa Mtume (s.a.w.w.) wenye hekima ni kwamba yule adui mkuu wa Uislamu alitoa huduma kuu kwa ajili ya jeshi la Waislamu.

Wakati huohuo mkewe Abu Sufyani Hind, aliwachochea watu wapinge na akamtusi mumewe. Hata hivyo hakuna kilichoweza kutendwa sasa na vilio na malalamiko yote hayakuwa na faida yoyote. Hata hivyo, baadhi ya wale watu wenye msimamo mkali kama vile Safw?n bin Umayyah, Ikrimah (mpiganaji na mwakilishi maalum wa Waquraishi kwenye yale mapatano ya amani ya Hudaybiyah) aliapa kwamba watalizuia jeshi la Uislamu lisiuingie mji ule. Baadhi ya watu walidanganywa na kauli zao na huku wakiwa na panga zao mikononi waliifunga njia ya kile kikosi cha kwanza cha jeshi la Uislamu.

Jeshi La Waislamu Laingia Mjini

Kabla ya lile jeshi la Uislamu kuifikia barabara kuu ya mji wa Makka, Mtume (s.a.w.w.) aliwaita makamanda wa jeshi wote na kuwaambia: “Ningelipendelea kwamba Makka itekwe bila ya kumwaga damu. Hivyo basi, kuwaua watu wasiopigana hakuna budi kuepukwe. Hata hivyo, watu kumi ambao ni Ikrimah bin Abu Jahl, Habbar bin Aswad, Abdullah bin Saad Abi Sarah, Miqyas Subabah Layth, Huwairath bin Nuqayd, Abdullah Hilal na wanawake wanne waliotenda mauaji au makosa mengineyo au wameichochea vita, hawa hawana budi kuuawa upesi sana kutokana na makosa yao, wakati wowote ule watakapokamatwa.”14

Amri hii ilifahamishwa askari wote kupitia kwa makamanda wao. Ingawa hali ya kiakili ya watu wa Makka juu ya Mtume (s.a.w.w.) ilikuwa dhahiri kabisa, hivyo yeye (Mtume s.a.w.w) hakuacha kuchukua hatua za tahadhari za kijeshi wakati wa kuingia Makka. Mpango wake ulikuwa hivi:

Vikosi vyote vikiwa vimefanya mstari mmoja uliofika Zi-Tuw?15 wakati Mtume (s.a.w.w.) akiwa kazungukwa na kundi lenye askari elfu tano. Macho ya Mtume (s.a.w.w.) yalipoziangukia nyumba za Makka, machozi ya furaha yalilijikusanya machoni mwake, na ikiwa ni ishara ya kutoa shukrani kwa ajili ya ushindi ule alioupata bila ya upinzani kutoka kwa Waquraishi, yeye akiwa amempanda yule ngamia aliinama sana kiasi kwamba ndevu zake ziligusa matakia yaliyotandikwa mgongoni mwa ngamia yule. Ikiwa ni hatua ya tahadhari, aliligawa lile jeshi na akaipeleka sehemu yake kutoka upande wa juu na sehemu nyingine kutoka upande wa chini ya Makka. Hakutosheka na hilo tu, bali vilevile alivipeleka vikosi kupitia njia zote ziingiazo mjini mle.

Vikosi vyote viliingia mjini mle bila ya mapigano na malango ya mji yalifunguliwa kwa ajili yao ila kikosi kilichoongozwa na Khalid bin Walid. Kwa uchochezi wa Ikrimah, Safw?n na Suhayl, kikundi cha watu kiliamua kupigana na kikaudhihirisha upinzani wao kwa kufuma mishale na kuzitumia panga.

Hata hivyo, watu ishirini na wanane miongoni mwao walipouawa, wale wachochezi walikwenda kujificha na wengine wakakimbia.16

Kwa mara nyingine Abu Sufyani alitoa msaada kwa Uislamu kwenye tukio hili bila ya kuelewa.

Alikuwa bado kashikwa na woga mno na alijua ya kwamba upinzani haukuwa na chochote ila madhara tu. Ili kuzuia umwagaji wa damu alisema kwa sauti kuu aliwaambia watu: “Enyi Waquraishi! Msiyahatarishe maisha yenu, kwa sababu kupigana dhidi ya jeshi la Muhammad lenye utaratibu mzuri hakuna faida. Ziwekeni chini silaha zenu na kaeni majumbani mwenu au kimbilieni msikitini na maeneo yaizungukayo Ka’abah kwa kuwa kufanya hivyo maisha yenu yatasalimika!” Maneno ya Abu Sufyani yalikuwa na athari zilizohitajiwa, na hatimaye baadhi ya watu walijifungia majumbani mwao ambapo wengine walikimbilia msikitini.

Mtume (s.a.w.w.) aliona mianga ya panga za kikosi cha Khalid kutoka mahali paitwapo Az?khir, na akiwa anaitambua sababu ya ugomvi ule, alisema: “Mapenzi ya Allah yamekizidi kila kitu.”

Ngamia wa Mtume (s.a.w.w.) aliingia mji ule kwa heshima kuu na utukufu kutokea kwenye sehemu iliyoinuka ya mji wa Makkah (Az?khir). Alishukia mahali paitwapo Jahuun kandoni mwa kaburi la ami yake mpenzi Abu Twalib, na likakitwa hema maalum kwa aji yake. Ingawa watu walisisitiza kwamba akae nyumbani mwa mtu fulani, lakini yeye alikataa.

Kuyavunja Masanamu Na Kutoharisha Ka’abah

Mji wa Makka uliokuwa kitovu cha ibada ya masanamu kwa muda mrefu, ulisalimu amri kwenye jeshi la Uislamu na sehemu zote za mji ule zikawa chini ya mamlaka ya jeshi la Waislamu. Mtume (s.a.w.w.) alipumzika muda fulani hivi kwenye lile hema. Baada ya hapo alimpanda ngamia na kwenda kwenye Masjidul Haram kufanya Tawaaf (kuizunguka) ya Kaabah. Alikuwa kavaa kofia ya chuma kichwani mwake na Muhajiriin na Ansari wakiwa wamemzunguka, na hali hiyo ilionyesha ukuu wake.

Hatamu za ngamia wa Mtume (s.a.w.w.) zilikuwa zimeshikwa na Muhammad bin Maslamah, na Waislamu na baadhi ya waabudu masanamu walikuwa wamejipanga mstari kwenye njia atakayopitia. Baadhi yao walishangazwa na kutishwa ambapo wengine waliweza kuidhihirisha furaha yao. Kwa ajili ya malengo mema, Mtume (s.a.w.w.) hakushuka kwenye ngamia wake hadi akafika kwenye Masjidul Haram. Hapo alishuka na akasimama upande wa pili wa Hajarul Aswad (jiwe Jeusi). Badala ya kulibusu jiwe hili, alilisoza kwa fimbo yake maalum aliyokuwa kaishika mkononi mwake na akaitamka Takbir.

Wakimuiga Mtume (s.a.w.w.), Masahaba waliomzunguka kiongozi wao Mtukufu waliitamka Takbir kwa sauti kuu. Ile sauti ya Takbir ilifika masikioni mwa waabudu masanamu wa Makka waliokimbilia majumbani mwao au kwenye sehemu za miinuko. Ghasia zisizo za kawaida zilisikika mle msikitini na makelele ya watu waliokuwa wakimzuia Mtume (s.a.w.w.) asifanye Tawaaf kwa amani. Mtume (s.a.w.w.) aliwaashiria watu wanyamaze. Mara moja kimya kamili kilipatikana na wale wote waliokuwa ndani na walio nje ya msikiti ule walianza kumtazama Mtume (s.a.w.w.). Alianza kufanya Tawaaf na kwenye mzunguko wa kwanza wa Tawaaf aliyageukia masanamu matatu makubwa yalitoiwa Hubal, Isaaf na Naa’ilah yaliyowekwa juu ya lango la Kaabah. Aliyaangusha kwa fimbo au mkuki aliokuwa kaushika mkononi na akaisoma aya hii: “Na sema: Kweli imefika na uwongo umetoweka. Hakika uwongo lazima utoweke.” (Sura Isra, 17:81)

Kama alivyoamrisha Mtume (s.a.w.w.) Hubal lilivunjwavunjwa vipande vipande mbele ya macho ya waabudu masanamu. Hili sanamu kubwa lililozitawala fikara za watu wa Rasi ya Uarabuni kwa kipindi kirefu mno lilipoangushwa, Zubayr alimwambia Abu Sufyani kwa kumdhihaki: “Hubayl, lile sanamu kubwa limevunjwa!” Abu Sufyani akamwambia Zubayr kwa huzuni kubwa: “Jiepushe na kusema hivyo. Kama Hubal angalikuwa na uwezo wa kufanya lolote lile tusingelipatwa na hali hii.” Amekwisha kutambua kwamba mwishilizo wao haukuwa mikonini mwa sanamu hili.

Mtume (s.a.w.w.) akaimalizia Tawaaf yake na akakaa akijipumzisha kwa kiasi fulani hivi kwenye pembe ya msikiti. Kwenye siku hizo Uthman bin Talhah alikuwa mshika funguo za Ka’abah na nafasi yake hii ilikuwa ya kurithi. Mtume (s.a.w.w.) alimtuma Bilal kwenda nyumbani kwa Uthman kwenda kuileta funguo ya Ka’abah.
Bilal aliufikisha ujumbe wa Mtume (s.a.w.w.) kwa yule mtunzaji wa funguo. Hata hivyo mama yake alimkataza asiutoe ule ufunguo, akisema: “Ulinzi wa Ka’abah ni heshima yetu ya kurithiana na hivyo hatuwezi kuipoteza heshima hii.” Uthman aliushika mkono wa mama yake na akampeleka kwenye chumba cha faragha na akamwambia: “Kama hatuitoi funguo hii kwa hiari, basi uwe na uhakika kwamba wataichukua kutoka kwetu kwa nguvu!”17

Yule mtunza Ka’abah akaifungua ile Ka’abah na Mtume akaiingia. Usamah bin Zayd na Bilal na yule mwangalizi mwenyewe wakamfuatia Mtume (s.a.w.w.). Kama alivyoamrisha Mtume (s.a.w.w.), lango la Ka’abah lilifungwa, na Khalid bin Walid akasimama nje ya lango lile ili kuwazuia watu wasijazane karibu na lango lile. Kuta za ndani wa Ka’abah zilijaa picha na masanamu ya Mitume. Kama alivyoamrisha Mtume (s.a.w.w.), zile kuta zilisafishwa kwa maji ya kisima cha Zamzam na zile picha zikafutwa.

Mtume (s.a.w.w.) aliamrisha lile lango la Ka’bah lifunguliwe. Kisha akaiweka mikono yake miwili kwenye mhimili wa ubao wa lango lile na watu wakaweza kuuona uso wake mtukufu na wenye kung’aa, aliwaambia watu wale hivi: “Sifa zote zamstahiki Allah Aliyeitimiza ahadi Yake na Akamsaidia mja Wake na Akawashinda maadui.”

Allah Mwenye nguvu zote alikuwa amemuahidi Mtume (s.a.w.w.) kwa njia ya wahyi kwamba atamfanya arejee kwenye sehemu aliyozaliwa: “Hakika aliyekulazimisha kuifuata Qur’ani hapana shaka atakurudisha mahala pa marejeo (ulipozaliwa) ... ” (Surat al-Qasas, 28:85). Kwa kusema: “Allah Ameitimiza ahadi Yake.” Mtume (s.a.w.w.) aliutaja usahihi wa ile ahadi ya Allah na tena aliudhihirisha ukweli wake.

Kimya kilitawala kabisa kwenye maeneo yauzungukao msikiti na nje ya maeneo hayo. Watu wakizizuia pumzi zao, walikuwa wakiyafikiria mambo tofauti. Katika saa hii watu wa Makka walikumbushwa ule ukatili, uonevu na udhalimu waliowatendea Waislamu na mawazo mengine mbalimbali yalikuja akilini mwao. Watu walioamka mara kadhaa kupigana vita za kumwaga damu dhidi ya Mtume, wamewajeruhi na kuwauwa marafiki na masahaba, na wameamua kufanya mashambulizi ya usiku nyumbani kwake na kumkatakata vipande vipande, sasa wako chini ya mamlaka yake naye angaliweza kulipiza kisasi cha aina yoyote ile dhidi yao.

Watu hawa wakati yanatajwa makosa makubwa makubwa waliyoyatenda, walikuwa wakiambiana: “Bila shaka atatukata kwa upanga au atawauwa baadhi yetu na kuwafunga wengine na kuwafunga wanawake na watoto wetu.”

Walikuwa wamezama kwenye fikara nyingi za kishetani, mara kwa ghafla Mtume (s.a.w.w.) alikivunja kimya kile na kusema: “Mnasema nini na mnanifikiriaje?” Wale watu wenye kuogopa wakiukumbuka wema aliowatendea Mtume (s.a.w.w.) hapo zamani, walisema kwa sauti ya unyonge: “Hatuna tunachokifikiria juu yako ila upole na wema. Sisi tunakufikiria kuwa u ndugu yetu mheshimiwa na mwana wa ndugu yetu mheshimiwa.”

Wakati Mtume (s.a.w.w.) aliyekuwa na huruma mno na mwenye kusamehe akizisikia kauli hizi zenye kuzivutia hisia kutoka kwao, aliwajibu akisema: “Mimi nami ninakuambieni yaleyale ambayo ndugu yangu Yusufu aliwaambia wale nduguze wasio na huruma: “Leo hapana lawama juu yenu. Allah atakusameheni, Naye ni Mwingi wa kurehemu kuliko wote wanaorehemu.”18

Kitu kilichowafanya watu wa Makka kuwa na matumanini, ukiyaachilia mbali maneno haya, kilikuwa ni kule kwenda kinyume kwa Mtume (s.a.w.w.) na maneno ya mmoja wa maafisa wake mwenyewe, ambaye wakati wa kuwasili Makka alikuwa akiyatamka maneno ya hamasa ya: “Leo ni siku ya vita. Leo uhai wenu na mali zenu vinachukuliwa kuwa halali (kwa Waislamu).”

Mtume (s.a.w) aliudhishwa na hizi hamasa zisizo za kawaida, na ili kumwadhibu afisa aliyehusika, alitoa maelezo ya kwamba anyang’anywe bendera aliyokuwa kaishika na atolewe kwenye ukamanda. Sayyidna Ali (a.s.) aliteuliwa kuichukua ile bendera kutoka kwa afisa yule, na kwa mujibu wa masimulizi mengine mwana wa afisa yule aliteuliwa kuwa kamanda badala ya baba yake na akaichukua ile bendera kutoka kwa baba yake. Afisa huyu alikuwa ni Saad bin Ubadah, chifu wa kabila la Khazraji. Alifanya hivyo ili kuidhihirisha huruma hii (kwa watu wa Makka) mbele ya macho ya watu wale walioshindwa kuwa na matumaini fulani kwamba watapata msamaha. Na kisha msamaha wa wale waliokimbilia kwenye Ka’abah au nyumbani kwa Abu Sufyani au waliojificha majumbani wamo na wakaifunga milango yao tayari umeshatolewa kupitia kwa Abu Sufyani.

Mtume (S.A.W.W) Atoa Msamaha Kwa Watu Wote

Alipokuwa akitoa msamaha kwa watu wote, Mtume (s.a.w.w.) aliwaambia watu wa Makka hivi: “Mmekuwa ndugu zangu wa kabila moja msiotumia akili. Mliukataa utume wangu na mkanitoa nyumbani mwangu. Na nilipokimbilia kwenye sehemu ya mbali, mliamka kupigana nami. Hata hivyo, ukiyaachilia mbali makosa yenu yote haya, ninakusameheni nyote na ninakufanyeni huru na ninatangaza kwamba mnaweza kwenda kutafuta maisha.”

Bilal Atoa Adhana (Mwito Wa Swala)

Muda wa sala ya adhuhuri uliwadia, Bilal mwadhini rasmi wa Uislamu, alipanda kwenye paa la Ka’abah na kwa sauti kuu alitamka Upweke wa Allah na Utume wa Muhammad, huku akiifanya sauti hiyo kuyafikia masikio ya wale walioko kwenye mkutano mkuu. Waabudu masanamu walio wakaidi walikuwa wakisema kila aina ya mambo. Mmoja wao alisema: “Mtu fulani alikuwa na bahati njema, kwa kuwa alifariki dunia mapema na hivyo hakuisikia Adhaana.” Wakati huo huo Abu Sufyani alisema: “Sitasema lolote lile juu ya jambo hili kwa sababu idara ya habari ya Muhammad ni yenye ustadi mkubwa sana kiasi kwamba ninachelea kamba hizi na chembe chembe za mchanga zilizomo humu msikitini zitamuarifu kuhusu mazungumzo yetu.”

Mzee huyu mkaidi asiyeamini kwa uhakika juu ya Uislamu hadi mwishoni mwa maisha yake, aliichukulia elimu ya Wahyi na upatikanaji wa ukweli kutokana na wahyi wa Allah kuwa ni sawa na ujasusi na uchunguzi wa madhalimu wa ulimwengu na kuyachanganya mambo haya. Hata hivyo, ukweli ni kwamba taarifa azipatazo Mtume kupitia kwa Malaika ni tofauti kabisa na wazipatazo wanasiasa, Mtume (s.a.w.w.) alisali sala ya adhuhuri. Kisha akamwita Uthman bin Talhah na kumrudishia ile funguo ya Ka’abah, na kusema: “Cheo hiki ni chako na kitabakia katika hali ya usalama kwenye familia yako!” Na hakuna jingine liwezalo kutegemewa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w.) ambaye hupata maamrisho kutoka kwa Allah na kuwaeleza watu: “Hakina Allah anakuamrisheni mzirudishe amana kwa wenyewe, . . .” (Suratun-Nisa, 4:58).

Bila shaka angeliwapendelea watu wengine kushika amana kubwa kiasi kile. Yeye haziharibu haki za watu kwa nguvu za kijeshi. Hivyo alitangaza waziwazi akisema: “Utunzaji wa funguo za Ka’abah ni haki ikubalikayo ya mwana wa Talhah na hakuna yeyote anayeshirikiana naye kwenye haki hii.”

Hivyo basi, alizifuta kazi zote zihusianazo na Ka’abah, ila zile zilizokuwa na faida kwa watu, kwa mfano ule utunzaji wa funguo, kuifunika shuka Ka’abah na kuwapatia maji mahujaji wa Ka’abah.

Mtume (S.A.W.W) Awashauri Sana Ndugu Zake

Ili ndugu wa karibu wa Mtume (s.a.w.w.) waweze kujua kwamba uhusiano wao na yeye sio tu kwamba bado haujauondoa mzigo kutoka mabegani mwao bali umelifanya jukumu lao kuwa zito zaidi, alishauri kwamba wasiruhusiwe kuiruka mipaka ya sheria za Uislamu kwa sababu ya uhusiano wao na yeye au kujinufaisha kinyume na haki kutokana na uhusiano wao na kiongozi wa Dola.
Katika hotuba aliyoitoa kwenye mkutano waliohudhuria watu wa familia za Bani Hashim na Bani Abdul Muttalib, alishutumu kila aina ya ubaguzi na akatilia mkazo juu ya umuhimu wa uadilifu na usawa baina ya watu wa matabaka yote, na akasema: “Enyi wana wa Hashim na Muttalib! Allah amenituma kwenu ili niwe Mjumbe Wake na vifungo vya huba na huruma baina yenu na mimi vilevile si vyenye kuvunjika.

Hata hivyo, msidhanie ya kwamba uhusiano wenu na mimi tu utakuthibitishieni wokovu kwenye Siku ya Hukumu. Ninyi nyote hamna budi kutambua ya kwamba rafiki yangu kutoka miongini mwenu na wengineo ni yule aliye mchamungu na mwema, na uhusiano wangu na wale wajao mbele ya Allah na mzigo mzito wa dhambi umekatika. Sitaweza kukufanyieni lolote lile katika Siku ya Hukumu. (Katika siku hiyo) Mimi na ninyi tutawajibika kwa matendo yetu.”19

Hotuba Ya Kihistoria Ya Mtume (S.A.W.W.) Kwenye Msikiti Wa Masjidul Haram

Ulikuwako mkusanyiko mkubwa wa watu kwenye Masjidul Haram kuizunguka Ka’abah. Waislamu, waabudu masanamu, marafiki na maadui walikuwa wamekaa bega kwa bega pamoja, na hapo utukufu wa Uislamu na ukuu wa Mtume (s.a.w.w.) vilitoa tamasha kuu mle msikitini.

Utulivu ulitawala pote mjini Makka na sasa muda ukawadia kwa Mtume (s.a.w.w.) kuwaonyesha watu sifa halisi za mwito wake, na kuukamilisha ujumbe wake aliouanzisha miaka ishirini iliyopita, lakini alikuwa bado hajafaulu kuukamilisha kutokana na kuchelewa kwa waabudu masanamu.

Yeye Mtume (s.a.w.w.) mwenyewe alikuwa mkazi katika mazingira yaleyale, naye aliyatambua vizuri maradhi ya jamii ya Kiarabu na dawa yao. Aliijua sababu ya kuanguka kwa watu wa Makka. Hivyo akaamua kuyatazama maradhi ya kijamii ya jamii ya Kiarabu na kuwatibu kwa ukamilifu.

Hapa chini tunatoa baadhi ya maelekezo ya Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.). Kila moja lilidhamiriwa kuponya maradhi maalum.

Suala la mtu kujitukuza kwa sababu ya familia yake binafsi, nyumba yake au kabila lake ilikuwa moja ya maradhi yenye mizizi iliyoshamiri mno ya jamii ya Kiarabu, na fahari kuu kwa mtu ilikuwa kwamba atokane na tawi la Kabila maarufu kama vile Waquraishi.

Mtume (s.a.w.w.) aliushutumu msingi huu wa ubora wa kimawazo tu, alisema: “Enyi watu! Allah chini ya mafundisho ya Uislamu amekomesha kutoka kwenu misingi ya fahari ya zama za ujinga, na kujitukuza kwa ajili ya nasaba.

Ninyi nyote ni dhuria wa Nabii Adamu, na Adamu aliumbwa kwa udongo. Aliye bora miongoni mwenu ni yule aziambaaye dhambi na uasi.”

Ili kuwafanya watu watambue kwamba kipambanuzi cha ubora ni uchamungu tu, yeye kwenye moja ya hotuba zake aliwagawa watu wote kwenye makundi mawili, na akatangaza kwamba wale walio wachamungu ndio wastahilio kuheshimiwa kwa ubora.

Kutokana na mgao na upangaji huu wa madaraja, alibatilisha vipimo vyote vya kimawazo vya madaraja na vyeo, na akasema: “Mbele ya Allah watu wana makundi mawili tu:

Moja kati ya makundi hayo ni lile la watu wachamungu, walio waheshimiwa mbele ya Allah, na kundi la pili ni lile la waasi na wenye dhambi, ambao ni duni na waliotwezwa mbele Yale (Allah)”.

Ubora Kutokana Na Kuwa Mwarabu

Mtume (s.a.w.w.) alitambua kwamba Waarabu walichukulia kuwa kizazi cha Kiarabu ni heshima kuu kwao; walijivunia kuwa na nasaba ya Kiarabu. Ari hii ilikuwa kama maradhi ya kuambukiza kwao. Kuyatibu maradhi haya na kuiondolea mbali ile dhana ya ubora huu aliwageukia watu na kusema: “Enyi watu! Kuwa Mwarabu si kigezo cha ubora wenu au sehemu ya utu wenu, ila ni aina tu ya usemaji. Fahari ya kinasaba haina faida yoyote kwa mtu asiyeyatekeleza majukumu yake barabara, na haifanyi masahihisho kwenye mapungufu ya utendaji wake.”

Je, inawezekana kupata kauli iliyo fasaha na yenye kuelezea waziwazi kuliko hii? Yule mtangazaji halisi wa uhuru hakutosheka na kauli tulizozinukuu hapo juu, bali ili kuuthibitisha usawa wa wanadamu na jamii, aliongeza kusema: “Watu wote wamekuwa sawa hapo kale na pia wako sawa hivi sasa kama yalivyo meno ya kitana, na Mwarabu hana ubora wowote kwa asiyekuwa Mwarabu, wala mtu mwekundu si bora kuliko mweusi. Kigezo cha ubora ni uchamungu.”

Kwa kauli hii aliondoa aina zote za ubaguzi usio sahihi na vizuizi visivyo na mipaka miongini mwa mataifa ya ulimwengu, ni katika nyakati hizi za awali tu bila kuchelewa akalitekeleza jukumu lake ambalo ‘Tangazo la Haki za Binadamu’ la siku hizi au ‘Haki ya Uhuru na Usawa wa Mwanadamu’ havikuweza kulitekeleza ingawa kuna makelele yote haya juu ya hayo.

Vita Vya Miaka Mia Moja Na Mifundo Ya Tangu Kale

Kutokana na vita vya ndani na umwagaji wa damu uliokuwa ukiendelea, watu wa Uarabuni wamekuwa taifa la wenye kulipiza kisasi na daima walikuwa kwenye vita wenyewe kwa wenyewe. Baada ya kutwaa udhibiti kamili kwenye Rasi ile ya Uarabuni, Mtume (s.a.w.w.) aliliondoa tatizo hili la kijamii na ilikuwa muhimu kwamba ayatibu maradhi haya ili kuthibitisha upatikanaji wa usalama wa Dola ya Kiislamu.

Aliipata tiba ya maradhi haya kwa kuwataka watu kuacha umwagaji damu wa aina zote uliokuwa ukitendeka kwenye zama za ujinga, na kuyachukulia mambo yote kama hayo kuwa yamefutwa kabisa. Kwa njia hii alizuia umwagaji wa damu uliovuruga amani na utaratibu mwema, na akawafanya watu wayasahau maasi, utekaji nyara na mauaji, vitu vilivyozaa madai ya dia au mapambano. Ili kuifikia hatima hii, alitangaza akisema: “Ninayatupilia mbali madai yote yahusianayo na uhai na mali na heshima zote za kimawazo tu, za siku za kale, na ninazihesabu kuwa ni zisizo na msingi.”

Udugu Wa Kiislamu

Sehemu ya yale aliyoyasema Mtume (s.a.w.w.) siku ile ni kuhusiana na umoja wa Waislamu na haki alizonazo Mwislamu juu ya nduguye Mwislamu. Lengo lake katika kuzitaja faida hizi lilikuwa kwamba, kwa kuvidumisha vifungo hivi vya urafiki na umoja, pamoja na kuziheshimu haki walizonazo Waislamu juu ya wao kwa wao, wale wasiokuwa Waislamu waweze kuuelekea Uislamu na kuweza kujiunga na safu za Waislamu. Yafuatayo ni maneno ya maelezo hayo: “Mwislamu yu ndugu wa Mwislamu mwenzie na Waislamu wote ni ndugu wao kwa wao, nao huwa mkono mmoja wawapo dhidi ya wasiokuwa Waislamu.

Damu ya kila mmoja wao ni sawa na ile ya wengine na hata yule aliye mdogo zaidi miongoni mwao anaweza kuweka ahadi kwa niaba ya wenzie.”20

Wahalifu Wakamatwa

Hakuna shaka juu ya ukweli uliopo kwamba Mtume (s.a.w.w.) alikuwa kigezo kikuu cha huruma na msamaha, na ingawa ulikuwepo mwelekeo wenye nguvu wa kundi lenye msimamo mkali, alitoa msamaha kwa watu wote. Hata hivyo, walikuwepo watu wachache waliokuwa na makosa na majinai makubwa mno, na isingelifaa kwamba pamoja na maovu yote haya wapewe uhuru wa kwenda huko na huko miongoni mwa Waislamu, kwa sababu iliwezekana kabisa kwamba wakijichukulia fursa zisizostahili za ule msamaha waliopewa wangeliweza kufanya makri dhidi ya waislamu.

Baadhi yao waliuawa na Waislamu mitaani au kwenye Masjdul Haram na wawili miongoni mwao walikimbilia nyumbani kwa Ummi H?ni, dada yake Sayyidna Ali (a.s.). Ali akiwa na silaha kikamilifu aliizingira nyumba ya Ummi H?ni. Alipokabiliana uso kwa uso na afisa asiyetambulika, alijitambulisha upesi sana na akasema: “Nikiwa ni mwanamke wa Kiislamu, nimewapa kimbilio watu wawili na kimbilio alitoalo mwanamke wa kiislamu linaheshimiwa kama lile alitoalo mwanaume wa Kiislamu.” Wakati huo, ili kujitambulisha kwa Ummi Haani, Sayyidna Ali (a.s.) aliivua kofia yake. Yule bibi alimwona umbu lake ambaye mageuko ya nyakati yalimtenga kutoka kwake kwa miaka mingi. Mara macho yake yalijawa na machozi na akaikumbatia shingo ya Sayyidna Ali (a.s.). Baada ya hapo, wote wawili walikwenda mbele ya Mtume (s.a.w.w.) na yeye naye alilihesabu lile kimbilio alilolitoa Ummi Hani kuwa ni lenye kuheshimiwa.

Abdullah bin Saad bin Sarah aliyesilimu lakini baadae akaritadi, alikuwa mmoja wa wale watu kumi waliokuwa wanaume. Yeye naye alikiepuka kifo kwa uombezi wa Uthman.

Hadith Ya Ikrimah Na Safwan

Ikrimah bin Abu Jahl, aliyeviwasha vita vilivyoifuatia vile ya Badr, alikimbilia Yaman. Hata hivyo, yeye naye alisamehewa kwa mapendekezo ya mkewe. Safw?n alikuwa mwana wa Umayyah, aliyeuawa kwenye vita vya Badr. Pamoja na makosa na maovu mengine, Safw?n alimnyonga Mwislamu mjini Makka wakati wa mchana wa dhahiri ili kulipizia kisasi cha baba yake. Akiichelea adhabu, aliamua kuitoka Hijaz kwa njia ya bahari, hasa kwa sababu alitambua kwamba jina lake nalo lilikuwamo miongoni mwa wale watu kumi tuliowataja.

‘Umayr bin Wahab alimwomba Mtume (s.a.w.w.) kumsamehe Safw?n. Mtume (s.a.w.w.) aliyakubali mapendekezo yake, na ikiwa ni dalili ya hifadhi aliyopewa Safw?n alimpa ‘Umayr kilemba alichokuwa amekivaa wakati wa kuwasili kwake Makka. ‘Umayr alikwenda Jidah na kilemba kile na kumleta Safw?n mjini Makka. Macho ya Mtume (s.a.w.w.) yalipomwangukia mkosefu huyu mkuu wa zama zile, alimwambia kwa huruma nyingi: “Uhai wako na mali zako vimethibitishiwa usalama. Hata hivyo itakuwa bora kama ukisilimu.” Aliomba apewe muda wa kipindi cha miezi miwili ili kulifikiria jambo hili. Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Mimi niko tayari kukupa muda wa miezi minne badala ya hiyo miezi miwili ili kwamba uweze kuichagua dini hii kwa ufahamu kamili.” Kipindi cha miezi minne kilikuwa bado hakijamalizika wakati Safw?n aliposilimu.21

Ukiutupia jicho ule wakati ambao Mtume (s.a.w.w.) alimpa Safw?n uhuru huudhirisha ukweli ulio kinyume kabisa na fikara za mustashirik wenye ubinafsi. Ukweli uliopo ni kwamba machifu wa ushirikina walifaidi uhuru kamili katika suala la kusilimu. Si hilo tu bali vilevile hakukuwa na shurutisho lolote lililofanywa kwenye jambo hili, lakini juhudi zilifanywa kwamba waifuate hii dini ya Allah baada ya kufikiria na kujifunza kwa makini wala si kutokana na hofu na kutishiwa.

Matukio Ya Baada Ya Kutekwa Kwa Mji Wa Makka

Matukio muhimu na yenye mafunzo yahusianayo na kutekwa kwa mji wa Makka yameshasimuliwa. Hata hivyo, yako matukio mengine mawili yaliyo muhimu, ambayo ni haya tutakayoyasimulia hapa chini:

Baada ya kiapo cha utii cha Aqabah,22 Mtume (s.a.w.w.) kwanza alichukua kiapo cha utii kutoka kwa wanawake, ambacho ni kuyatekeleza majukumu haya: Kutomshirikisha Allah na yeyote yule, kutovunja ahadi, kutojishughulisha na matendo maovu, kutowauwa watoto wao, kutowahusisha na waume zao watoto ambao ukweli uliopo ni kwamba wao ni watoto wa watu wengine, kutompinga Mtume kwa jambo lolote lile.

Uendeshaji wa kiapo tulichokitaja hapo juu ulikuwa hivi: Kama alivyoamrisha Mtume (s.a.w.w.) aliletewa chombo kilichojazwa maji, naye akayachanganya maji yale na manukato. Kisha akaitumbukiza mikono yake humo na akaisoma Aya ya 12 ya Surah al-Mumtahinah. Baada ya hapo aliamka pale alipokuwa kaketi na kuwaambia wale wanawake: “Wale walio tayari kula kiapo hiki cha utii kwangu chini ya masharti niliyoyasema watumbukize mikono yao kwenye chombo hiki na watamke kwamba watayatekeleza masharti haya kwa uaminifu.”

Sababu ya kula kiapo hiki ilikuwa kwamba walikuwepo wengi miongoni mwa wanawake wa Makka waliokuwa wakiishi maisha ya upotofu, na kama haichukuliwi ahadi ya kuishi maisha ya heshima kutoka kwao, basi ulikuwapo uwezekano kwamba wangeliendelea kuyatenda matendo yao maovu kwa siri. Mmoja wa wanawake hao alikuwa ni ‘Hind’ mkewe Abu Sufyani na ambaye ni mama yake Muawiyah aliyekuwa na historia nyeusi. Akiwa fidhuli mno, Hind aliweka utashi wake juu ya mumewe Abu Sufyani; na hata katika ile siku ambayo alielekea kwenye amani, alikuwa akiwachochea watu wapigane na kumwaga damu.

Ilitokana na uchochezi wa Hind kwamba vita vilipiganwa kule Uhud na ikambidi Mtume (s.a.w.w.) kuyatoa mhanga maisha ya watu sabini akiwamo Hamza, ili kuzimisha vita ile. Na mwanamke huyu mshenzi alilipasua tumbo la mwili wa Hamza kwa ukatili usio kifani na kulitoa ini lake na kulikata mapande mawili kwa meno yake. Mtume (s.a.w.w.) hakuwa na njia nyingine ila kuchukua kiapo cha utii kutoka kwa mwanamke huyu na wengineo wa mfano wake mbele ya hadhara.

Wakati Mtume (s.a.w.w.) alipokuwa akiyasoma masharti ya mapatano yale, alikisoma kifungu ‘kutovunja ahadi’, Hind ambaye wakati ule alikuwa kakifunika gubigubi kichwa chake na uso wake, aliamka pale alipokuwa na kusema: “Ewe Mtume wa Allah! Unawaamrisha wanawake kutozivunja ahadi. Mimi nifanye nini? Mume wangu ni bahili mno na bwana mwonevu, na kwa sababu hii hapo awali nimekuwa nikiitumia bila ya haki mali yake iliyowekwa amana kwangu.” Abu Sufyani akaamka kwenye kiti chake na kusema: “Ninakihalalisha kila ulichokichukua hapo awali lakini huna budi kuahidi kwamba hutaiba tena katika siku zijazo.” Hapo Mtume (s.a.w.w.) alimtambua Hind kutokana na yale maneno ya Abu Sufyaan, na akamwambia: “Je, wewe ni binti wa Utbah?”Akajibu: “Ewe Mtume wa Allah! Ndio. Tusamehe dhambi zetu ili Allah Mwenye nguvu zote Akubariki.”

Mtume (s.a.w.w.) alipoitamka kauli isemayo: ‘Kutozini,’ Hind akaamka tena kutoka pale alipokaa na kuitamka kauli ya kujitoa katika lawama (kujibu rai), ambayo kwayo alimfunulia bila ya kupenda yale yaliyomo akilini mwake. Alisema: “Je, mwanamke muungwana anazini?” Kisaikolojia kujihami kwa aina hii kwenyewe tu kulikuwa aina fulani ya kuzifunua fikara za mtu. Kwa vile Hind alijitambua kuwa yu mwanamke wa aina ile, na alikuwa na uhakika kwamba katika kuisikia (kutoka kwa Mtume s.a.w.w) kauli tuliyoitaja hapo juu, watu watamtazama, ndipo mara moja aliuliza kwa njia ya tahadhari, kama mwanamke asiyekuwa mjakazi anaweza kuzini.

Hata hivyo, baadhi ya watu waliokuwa na uhusiano haramu na Hind katika zama za Ujinga walishangaa na wakacheka kule kukataa kwake, na vicheko vyao na kule kujihami kwake vikawa fedheha yake zaidi.23

Ukiyachunguza zaidi maneno yaliyomo kwenye kiapo hiki utayakuta yakidhihirisha jukumu la mwanamke wa Kiislamu. Vilevile kutokana na sentensi hii inadhihirika kwamba, Mtume (s.a.w.w.) hakupata ahadi yoyote kutoka kwa wanawake kuhusiana na kujihami, ambapo kwenye kiapo alichoapiwa pale Aqabah na chini ya ule mti (pale Hudaybiyah) kifungu kilichokuwa muhimu sana alichokitoa kilikuwa ni kile kihusianacho na ulinzi wa Uislamu na kumhami Mtume (s.a.w.w.).

Mahekalu Ya Masanamu Mjini Makka Na Viungani Mwake Yavunjwa

Idadi kubwa ya mahekalu ya masanamu ilijengwa kandokando ya mji wa Makka, na yalikuwa vyanzo vya heshima kwa makabila mengi. Ili kuing’oa ibada ya masanamu kutoka kwenye eneo la Makka, Mtume (s.a.w.w.) alipeleka vikundi vya askari pande mbalimbali kwenda kuyavunja mahekalu ya masanamu yaliyokuwako huko. Vilevile ilitangazwa mle mjini Makka kwamba kila aliye na sanamu nyumbani mwake alivunjevunje mara moja.24

Khalid bin Walid alikwenda akiliongoza kundi la askari hadi kwenye nchi ya kabila liitwalo Jazimah bin Aamir kuwaita kwenye Uislamu. Mtume (s.a.w.w.) alimwamrisha asiimwage damu yoyote na kutopigana vita yoyote ile, vilevile alimtuma Abdur Rahman bin Awf pamoja naye akiwa chini yake.

Katika Zama za Ujinga, kabila la Bani Jazimah lilimwua ami yake Khalid na baba yake Abdur Rahman walipokuwa wakirejea kutoka Yemen na kuziteka nyara mali zao, na Khalid bado alikuwa ana mfundo dhidi yao juu ya kisa hiki. Alipokuja uso kwa uso na watu wa kabila la Bani Jazimah, aliwaona wote wakiwa wameshika silaha na wakiwa tayari kujihami.

Yule kamanda (yaani, Khalid) akasema kwa sauti kuu: “Ziwekeni chini silaha zenu, kwa sababu kipindi cha kuyaabudu masanamu kimekwisha na Makka imeshatekwa, na watu wote wameshasalimu amri mbele ya jeshi la Uislamu.”

Machifu wa kabila waliwashauri watu wao kwamba wazitoe silaha zao na kujisalimisha mbele ya jeshi la Uislamu. Mtu mmoja miongoni mwao alikuwa na akili kiasi cha kuweza kutambua kwamba nia ya yule kamanda wa jeshi haikuwa nzuri.

Hivyo basi, akiwahutubia machifu wa kabila lile, alisema: “Matokeo ya kusalimu amri yatakuwa ni kuchukuliwa mateka na baada ya hapo ni kifo.”

Hatimaye maoni ya wale machifu yalitekelezwa na zile silaha zilitolewa na kupewa askari wa Uislamu. Wakati huo huo yule kamanda wa kundi lile la askari akiwa katika hali ya woga na kinyume na maamrisho ya Uislamu, aliamrisha kwamba mikono ya watu wa kabila lile ifungwe kinyumenyume na watiwe kizuizi. Baada ya hapo, ilipofika asubuhi baadhi yao waliuwawa kwa amri ya Khalid na wengine wakaachiliwa.

Taarifa za kosa hili la kutisha alilolitenda Khalid zilimfikia Mtume (s.a.w.w.) na akachukia mno. Upesi sana akamteua Sayyidna Ali (a.s.) kwenda kwa watu wa kabila lile na kuwalipa gharama za uharibufu wa vita vile na dia baada ya Kasma ya makini kabisa. Sayyidna Ali (a.s.) aliifanya hesabu ya hasara yao kwa makini mno kiasi kwamba alilipa hata gharama ya chombo kilichotengenezwa kwa mti ambacho mbwa wa kabila lile walikuwa wakinywea maji na kilichovunjika wakati wa mapambano ya Khalid. Kisha akawaita machifu wote waliodhulumiwa na akawauliza kama fidia yote ya vita vile na dia ya watu waliouawa kwa kuonewa imelipwa kwa ukamilifu nao, wote wakajibu:

“Ndio.” Baada ya hapo, akiuzingatia ukweli uliopo kwamba iliwezekana kwamba wamepata hasara ambayo bado hawajaitambua, Saidian Ali (a.s.) aliwapa pesa fulani kwa njia ya zawadi na kisha akarejea Makka na kutoa taarifa yake kwa Mtume (s.a.w.w.).

Mtume (s.a.w.w.) alimsifu Sayyidna Ali (a.s.) kwa kitendo chake kile na huku akiwa ameelekea Qiblah aliinua mikono yake na kuomba akisema: “Ee Mola! Unatambua kwamba mimi nimechukizwa na kosa la Khalid nami katu sikumwamrisha kupigana vita.”25

Alipokuwa Amirul-Mu’minin (a.s.) akiwalipa fidia wale watu wa Bani Jazimah, vile vile aliyazingatia madhara ya kiroho na ya kitabia waliyoyapata na akawapa pesa wale watu waliokumbwa na hofu kutokana na mashambulizi ya Khalid na akawafariji.

Mtume (s.a.w.w.) alipoitambua tabia ya unyoofu ya Amirul-Mu’minin (a.s.), alisema: “Ewe Ali! Mimi sitakibadili kitendo chako hiki na idadi kubwa ya ngamia wenye manyoya mekundu.26

Ewe Ali! Umeipata radhi yangu. Allah akuridhie! Ewe Ali! Wewe ni kiongozi wa Waislamu. Amebahatika yule akupendaye na akaifuata njia yako, na yu mwenye bahati mbaya yule akupingaye na akaifuata njia iliyo potoka.27 Cheo chako kwangu ni kama kile alichokuwa nacho Harun kwa Musa ila tu kwamba hatakuja Mtume baada yangu.”28

Kosa Jingine La Khalid

Kosa tulilolitaja hapo juu halikuwa kosa pekee la Khalid alilolitenda katika kipindi cha uhai wake wa kujifanya kuwa yu Mwislamu, kwa kuwa hivyo, katika kipindi cha Ukhalifa wa Abu Bakr alitenda kosa lililokuwa kubwa kuliko hilo la awali.

Tukieleza kwa ufupi tu ni kwamba, baada ya kufariki dunia Mtume (s.a.w.w.) baadhi ya makabila yaliritadi, au ili kueleza kwa usahihi zaidi ni kwamba, hawakuutambua Ukhalifa wa Abu Bakr na wakakataa kutoa Zaka. Khalifa alituma makundi mbalimbali ya watu kwenye sehemu mbalimbali kwenda kuwaadhibu wale walioritadi.

Khalid bin Walid alilishambulia kabila la Maalik bin Nuwayrah, kwa sababu watu hao wameritadi. Maalik na watu wote wa kabila lake walikuwa tayari kujihami, na walikuwa wakisema: “Sisi ni Waislamu na hivyo basi haistahili kwamba tushambuliwe na jeshi la Uislamu.”

Hata hivyo, Khalid aliwanyang’anya silaha kwa kufanya udanganyifu na akamwua yule chifu wa kabila lile Maalik bin Nuwayrah, aliyekuwa Mwislamu, na kisha akamnyanyasa mkewe.29

Je, hii historia nyeusi ya Khalid yathibitisha haki ya kwamba tumwite ‘Saifullah’ (Upanga wa Allah) na tumchukulie kuwa yu mmoja wa maafisa wakuu wa Uislamu?30

 • 1. Budayl alikuwa mmoja wa watu watukufu na wazee wa kabila la Khuza’ah waliokuwa wakiishi mjini Makka. Wakati ule alikuwa na umri wa miaka 97. (Amaali Tusi, uk. 239).
 • 2. Maghaazil-Waaqidi, Juz. 2, uk. 792.
 • 3. Maghaazil-Waaqidi, Juz. 2, uk. 780-794; Siiratu Ibn Hishamu, Juz. 2, uk. 389- 387; Bihaarul Anwaar,
  Juz. 21, uk. 102.
 • 4. Siiratu Ibn Hishamu, juz.2, uk.399; Majma’ul Bayaan, juz.9, uk. 269-270.
 • 5. Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 399 na Majma’ul Bayan, Jz. 9, uk. 269-270.
 • 6. Heroes an Hero Worship cha Thomas Carlyle.
 • 7. Maombi yote haya yamesimuliwa mwenye Surat al-Israa, 17:90-93.
 • 8. Sura Yusuf, 12:91-92.
 • 9. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 402.
 • 10. Bihaarul An’waar, Juz. 21, uk. 114.
 • 11. Jina la uzazi (kun'ya) la Abu Sufyani.
 • 12. Jina la uzazi (kun'ya) la Abbas
 • 13. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 400 - 404 Majmaul Bayan, Juz. 10, uk. 554- 556; Maghaazil-Waaqidi, Juz. 2, uk 816-818; Sharhu Abil Hadid, Juz. 17, uk. 268 kama alivyonuku kutoka Maghaazil-Waaqidi.
 • 14. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 409.
 • 15. Hii ni sehemu ya mwinuko ambayo mtu awapo hapo aliweza kuziona nyum- ba za Makka pamoja na Kaabah na Masjidul Haraam.
 • 16. Maghaazil-Waaqidi, Juz.2, uk. 825-826.
 • 17. Maghaazil-Waaqidi, juz. 2, uk 833.
 • 18. Maghaazil-Waaqidi, Juz. 2, uk. 835; Bihaarul Anwaar, juz. 21, uk. 107 na 133
 • 19. Bihaarul Anwaar, Juz.1, uk. 111.
 • 20. Nukuu hizi tumezitoa kwenye vitabu hivi; Rawzatul-Kafi, uk. 246; Siiratu Ibn Hisham, juz. 2, uk. 412; Maghaazil-Waaqidi, juz. 2, uk. 836; Bihaarul An’waar, juz. 21, uk. 5; Sharhu Abil Hadid, Juz. 17, uk. 281.
 • 21. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 417.
 • 22. Katika kiapo cha utii kilichofanyika pale ‘Aqabah kabla ya kuhajiri kwa Mtume (s.a.w.w.) wanawake watatu walikuwa miongoni mwa watu waliokuwa zaidi ya sabini waliokula kiapo kile.
 • 23. Majma’ul Bayaan, Juz. 5, uk. 276.
 • 24. Bihaarul Anwaar, Juz. 21, uk. 140.
 • 25. Siirah-i Hishamu, Juz. 2, uk. 430.
 • 26. Khisaal, Juz. 2, uk. 125.
 • 27. Majlis-i Ibn Shaykh, uk. 318.
 • 28. Amaali Suduq, uk. 105.
 • 29. Uhalisia wa kisa hiki ni kuwa Khalid aliyetumwa na Abu Bakr alimwingilia mke wa Malik katika usiku uleule aliomuuwa mumewe. Historia ya Uisilamu hai- jui ni Aya ipi iliyomruhusu Khalid kumwingilia mjane huyo siku ileile, na wala ni Uisilamu upi uliomruhusu kumuuwa Malik, lakini historia yajuwa kuwa Malik ni sahaba aliyeaminiwa na Mtukufu Mtume na hivyo akampa jukumu la kusimamia zaka za jamaa zake. Malik na watu wake walikataa kukabidhi zaka hizi kwa Abu Bakri kwa kuwa wao hawakumtambua kama Khalifa wa Mtume, kwani walichokijua wao kutoka kwa Mtume ni kuwa, Khalifa baada yake ni Ali (a.s.). – Mhariri.
 • 30. Hapa ndipo inapokulazimu kuelewa ni upi ukweli wa nadharia yetu isemayo “Si kila Sahaba ni mwadilifu” Mhariri