Sura Ya 18: Silaha Zenye Kutu

Nguvu za kiutawala za uabudu masanamu zilikuwa kwenye hali ya ukubalikaji kila mahali kwenye Penisula ya Uarabuni. Waquraishi walikuwa wameshayatayarisha majeshi yao ili kufanya kampeni dhidi ya ibada ya Allah, Aliye Mmoja tu. Katika hatua za awali walitaka kumfanya Mtume (s.a.w.w.) aiache kazi yake kwa kumtamanisha na kumpa ahadi za utajiri na mamlaka, lakini walikabiliwa na lile jibu lake maarufu: “Naapa kwa jina la Allah! Japo muniwekee jua kwenye mkono wangu wa kulia na mwezi kwenye mkono wangu wa kushoto (yaani japo mnipe mamlaka juu ya huu ulimwengu mzima) sitaiacha kazi hii.” Kisha wakaanza kuwahofisha, kuwatweza, na kuwatesa marafiki zake na katu hawakuchoka kuwadhuru na kuwaadhibu.

Hata hivyo, ushujaa na umadhubuti wa marafiki zake hawa waaminifu viliwafanya washinde kwenye hatari hii pia, kiasi kwamba walinunua uvumilivu wao katika njia ya Uislam kwa kuyaacha makazi yao, na kujitahidi kuieneza dini hii takatifu kwa kuhamia Ethiopia.. Hata hivyo, harakati za nguvu inayotawala ya uabudu masanamu za kuung’oa ule mche mchanga wa Uislamu zilikuwa bado hazijakoma. Badala yake, sasa walitaka kuitumia silaha iliyo kali zaidi.

Silaha hii ilikuwa ni ile ya propaganda dhidi ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Kwa dhahiri mateso na maonevu yangaliweza kuwazuia kusilimu wale watu waliokuwa wakiishi mjini Makkah tu. Njia hii haikufaa kwa wale watu waliokuja Makkah kwa makundi kufanya Hija ya Nyumba ya Allah katika kipindi cha miezi mitakatifu. Hawa mahujaji walikutana na Mtume (s.a.w.w.) katika mazingira ya amani na utulivu, na ijapokuwa hawakuipokea dini yake, kwa uchechefu walitikisika kuhusiana na imani yao (ibada ya masanamu). Na wanapoondoka Makkahh baada ya siku chache na kurudi makwao, walilichukua jina la Mtume na Hadith ya hii dini mpya kwenye pembe zote za Bara Arabuni. Na jambo hili, lenyewe lilichukuliwa kuwa ni pigo kubwa kwa utawala wa uabudu masanamu na lilikuwa kisababisho cha ajabu kiongozacho kwenye uweneaji wa Uislamu.

Hivyo basi, wazee wa Waquraishi waliweka mpango mwingine wa uharib- ifu na kwa njia hii walitaka kuzuia ueneaji wa dini ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na hivyo kuyakata mawasiliano yake na jamii ya kiarabu.

Usingiziaji Uliokithiri

Tabia ya mwanaadamu yaweza kueleweka vizuri kwa kujiingiza kwenye matusi na masingizio ya maadui zake. Ili kuwapotosha watu daima adui hujitahidi kutoa shutuma za aina hii dhidi ya mpinzani wake ziwezazo kukubaliwa na jamii, kwa kiwango cha hata moja kwa elfu, ili kwamba, kwa huko kueneza uongo na mambo yasiyo na msingi, adui aweze kuvun- ja heshima na cheo chake kwa kadiri iwezekanavyo. Adui mwenye hekima hujitahidi kuzusha mambo dhidi ya adui yake yawezayo kusadikiwa na baadhi ya watu maalum au ambayo, kwa uchechefu yawezayo kutiliwa shaka na watu hao. Hata hivyo, hayaenezi mambo kuhusu adui yake yasiyoafikiana kabisa naye na yasiyo na mwelekeo kwenye fikira na matendo yake yafahamikayo mno, kwa sababu vinginevyo atapata matokeo yaliyo kinyume na yale ayapendayo.

Hivyo, mwanahistoria stadi anaweza kujifunza sura halisi ya upande wa pili nyuma ya uongo na masingizio, na anaweza kujifunza kuhusu mafanikio ya kijamii na kifikra hata kutoka nyuma ya mnara wa kuongozea wa adui. Huwa hivyo kwa sababu adui asiye na aibu na asiyeogopa haachi kutangaza shutuma za uongo zenye manufaa kwake na kujipatia faida kubwa kiasi iwezekanavyo kutokana na hiyo silaha kali ya propaganda kwa kadiri fikira, akili na ujuzi juu ya hali vitakavyomruhusu. Hivyo, kama hatalihusisha jambo lolote lisilo la haki kwa huyo mtu mwingine itakuwa ni kwa sababu mtu yule yu safi kutokana na udhaifu wowote, hivyo basi jamii haitakuwa tayari kulikubali jambo lile.

Historia ya uislamu yaonyesha kwamba ingawa Waquraishi walidumisha uadui usio na kifani na chuki dhidi ya Mtume (s.a.w.w.) na walikuwa na shauku ya kulivunjilia mbali jengo jipya la Uislamu kwa gharama zozote zile na kuivunjilia mbali hadhi na cheo cha mwasisi wake, lakini hawakuweza kuitumia kikamilifu silaha hii (ya masingizio). Walifikiria waseme nini wakati mali za baadhi ya watu wao wenyewe, zilikuwako nyumbani mwake Mtume (zikiwa ni amana) na umri wake Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) wa miaka arobaini umemthibitisha kuwa yu mtu mwaminifu.

Je, wangaliweza kumtuhumu kwa anasa? Lakini vipi wangaliweza kulileta neno hili midomoni mwao? Aliyaanza maisha yake ya utu uzima akiwa na mwanamke mtu mzima na bado angali akizipisha siku zake pamoja naye pale Waquraishi walipokutana ili kupanga propaganda zao dhidi yake! Hivyo, wakaanza kutafakari kuhusu waseme nini na hilo walisemalo liweze kurandana naye na angalau asilimia mia moja ya watu iweze kulikubali kwamba ni kweli.

Wazee wa Darun Nadwa walifadhaika kuhusu ni jinsi gani ya kuitumia silaha hii dhidi yake. Hivyo wakaamua kulifikisha jambo hili mbele ya mwenye hekima mmoja wa Kiquraishi na kuutekeleza ushauri wake. Baraza liliundwa.
Walid aliwageukia Waquraishi na kusema: “Majira ya Hajj yanakaribia, na kwenye siku hizi watu huja mjini humu kwa idadi kubwa ili kutekeleza wajibat mbalimbali na kanuni za ibada zihusianazo na Hajj. Muhammad ataitumia nafasi ipatikanayo kutokana na uhuru uliopo kwenye siku hizi na ataitangaza dini yake. Ingekuwa bora kama Waquraishi wangeelezea maamuzi yao ya mwisho juu yake na dini yake. Hivyo basi, sote tuwape Waarabu maoni ya aina moja, kwa sababu tofauti ya maoni itafanya maneno kutokuwa na athari.”

Baada ya kuyasema hayo, yule mwana hekima wa Uarabuni alilifikiria kwa makini jambo lile na akasema: “Tuseme nini” mmoja wao akashauri akisema: “Tuseme kwamba yeye yu mpiga ramli.” Walid hakulipendelea wazo hili na akasema: “Anayoyasema Muhammad sio kama ya mpigaramli.” Mwingine akasema kwamba wamwite mwendawazimu. Wazo hili nalo lilikataliwa na Walid, aliyesema: “Hakuna dalili yoyote ya uwendawazimu ionekanayo kwake.” Baada ya kulifikiria kwa kirefu waliamua hivi: “Hatuna budi kusema kwamba yu mchawi, kwa sababu jinsi yake ya kusema mambo ni ya kiuchawi na uthibitisho wa jambo hili ni kwamba, kwa kuitumia Qur’ani yake amejenga mfarakano miongoni mwa wakazi wa Makkah, ambao uhusiano wao wenye maafikiano mema ulikuwa ukitolewa mifano, na ameuvunjilia mbali umoja wao.”1

Wafasiri wa Qur’ani tukufu wanapoifasiri Suratul-Muddaththir wametoa masimulizi mengine ya jambo hili. Wanasema: “Walid alipozisikia aya fulani fulani za Sura al-Fussilat kutoka kwa Mtume (s.a.w.w.) alibutwaa na nywele zake zikamsimama. Aliondoka na kwenda nyumbani kwake nae hakutoka tena nje. Waquraishi wakaanza kumdhihaki na kusema kwamba Walid amekuwa mfuasi wa dini ya Muhammad. Walimwendea nyumbani kwake kwa kikundi na kumuuliza juu ya ukweli wa Qur’ani ya Muhammad.

Kila mmoja wa wale waliokuwapo pale alipokuwa akitoa maoni yake juu ya maelezo tuliyoyatoa hapo juu, Walid aliyakataa. Hatimaye alitoa maoni ya kwamba, wamwite Mtume (s.a.w.w.) kuwa yu mchawi, kutokana na mfarakano aliouzusha baina yao, na waseme kwamba anayo njia ya kichawi ya kusemea mambo!

Wafasiri wa Qur’ani tukufu wanaamini ya kwamba aya ya 11-26 ya Sura al-Muddath’thir zianzazo na:
Uniache Mimi na mwanaadamu Niliyemuumba peke yangu.” hadi: “Hivi karibuni Nitamwonyesha adhabu ya moto wa Jahanamu.” Zilifunuliwa kuhusiana na Walid bin Mughayrah.2

Kushikilia Kumhusisha Na Wendawazimu

Ni ukweli wa kihistoria ukubalikao kwamba tangu mwanzoni mwa utu uzima wake, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alijulikana kwa unyoofu na uaminifu wake, na hata maadui zake walimwinamishia vichwa vyao bila yakupenda mbele ya sifa zake tukufu. Moja ya sifa zake zilizojitokeza mno ni ile ya kwamba watu walimwita mno ‘Mkweli’ na ‘Mwaminifu’ kiasi kwamba wenye kuabudu masanamu walikuwa na kawaida ya kuweka vitu vyao kwake hadi miaka wa kumi baada ya ubalighishaji wa jumla wa Uislamu.

Kwa vile ulinganiaji wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) ulichukiza mno na kutoingia akilini mwa maadui zake, juhudi zao pekee zilikuwa kwamba wawageuzie mbali watu kutoka kwake kwa kutumia maneno yenye kuzi- haribu akili zao.

Kwa kuwa walijua kwamba kuuhusisha uongo na msingizio juu ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) hakutazivutia akili za wenye kuyaabubu masanamu walio wajinga na wa daraja la kawaida, walilazimika kuukana mwito wake kwa kusema kwamba chanzo cha maoni na fikara zake kilikuwa ni wendawazimu usioendana na sifa za uchamungu na unyoofu. Walifanya mifano mingi miovu na kufanya ujanja na udanganyifu katika kuifanya propaganda hii ya kinafiki.

Kutokana na unafiki wao mkali, walijifanya kuwa waaminifu mno pale walipokuwa wakizusha hivi na wakalieleza jambo hili kwa maelezo ya kutatanisha, na wakasema:

“Je, amezua uongo juu ya Allah au amepatwa na wazimu. . . ?” (Surah Saba, 34:38). Na hii ndio njia ya kishetani wanayotumia maadui wa ukweli pale wanapokuwa wanapowakataa watu mashuhuri na watengenezaji wa hali ya jamii. Qur’ani inasema kwamba hii njia yenye kuchukiza haikuwa ya kipekee tu kwa watu wa zama zake Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), kwani maadui wa mitume wa kabla yake nao waliitumia silaha hii ili kuwapinga. Qur’ani inasema:

كَذَٰلِكَ مَا أَتَى الَّذِينَ مِنْ قَبْلِهِمْ مِنْ رَسُولٍ إِلَّا قَالُوا سَاحِرٌ أَوْ مَجْنُونٌ {52}

أَتَوَاصَوْا بِهِ ۚ بَلْ هُمْ قَوْمٌ طَاغُونَ {53}

Vivyo hivyo hakuna Mtume yoyote aliyewafikia wale wa kabla yao ila walisema: “huyu ni mchawi au majinuni! Je, wameusiana jambo hili? (sivyo) bali wao wote ni watu waovu.” (Suratudh-Dhariyat, 51:52-53).

Injili ya siku hizi nayo inasema kwamba Nabii Isa (a.s.) alipowashauri Wayahudi, wakasema: “Ana pepo huyu tena ana wazimu; mbona mnamsikiliza?” (Yohana Mtakatifu, 10:20; 7:20; 8:48).

Hakuna shaka kwamba kama Waquraishi wangalikuwa na nafasi ya kumshutumu Mtume (s.a.w.w.) kwa jambo lolote jingine wasingaliacha kufanya hivyo. Hata hivyo, maisha ya Mtume (s.a.w.w.) ya heshima ya zaidi ya miaka arobaini yaliwazuia kutamka masingizio yoyote mengine dhidi ya tabia zake ingawa walikuwa tayari kukitumia kitu japo kidogo mno dhidi yake. Kwa mfano, wakati mwingine alikuwa na kawaida ya kukaa karibu na Marwah akiwa pamoja na mtumwa wa Kikristo aliyekuwa akiitwa Jabr. Mara moja maadui zake wakachukua fursa ya kitendo chake kile na wakasema: “Muhammad anajifunza Qur’ani kutoka kwa huyu mtumwa wa Kikristo.” Qur’ani tukufu inaijibu shutuma yao hii isiyo na msingi, ikisema:

وَلَقَدْ نَعْلَمُ أَنَّهُمْ يَقُولُونَ إِنَّمَا يُعَلِّمُهُ بَشَرٌ ۗ لِسَانُ الَّذِي يُلْحِدُونَ إِلَيْهِ أَعْجَمِيٌّ وَهَٰذَا لِسَانٌ عَرَبِيٌّ مُبِينٌ {103}

“Na bila shaka tunajua ya kwamba wanasema: “Hakika yuko mtu anayemfundisha.” Lugha ya yule wanayemuelekea ni ya kigeni na hii ni lugha ya kiarabu fasaha na chenye bayana” (Surah al-Nahl, 16:103).3

Hadaa Ya Nazar Bin Haarith

Ile silaha yenye kutu ya propaganda dhidi ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) haikuthubutu kuwa ni yenye kufaa hata kidogo, kwa kuwa watu kwa heki- ma na akili zao walitambua ya kwamba Qur’ani ina mvuto wa ajabu. Pia walihisi kwamba kabla ya hapo hawajawahi kusikia maneno matamu na yenye maana nzito yenye kuuliwaza moyo mno kiasi kwamba upesi sana huzivutia fikara za mtu.

Maadui waliposhindwa kutokana na kumsingizia Mtume (s.a.w.w.) waliifikiria njia nyingine ya kitoto na wakatumaini ya kwamba kwa kuitumia njia hii wangalifaulu kumkosesha usikivu na kuamini kwa watu.

Nazar bin Haatirh aliyekuwa mmoja wa Waquraishi wenye elimu na uzoefu aliyeitumia sehemu ya maisha yake nchini Hira na Iraq alikuwa na ujuzi juu ya vyeo vya wafalme na mashujaa wa Iran kama vile Rustam na Asfand Yaar na juu ya itikadi ya Wairani kuhusu wema na uovu, aliteuliwa kufanya kampeni dhidi ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Darun Nadwah liliafiki wazo la kwamba, kwa kuutangaza ustadi wake mitaani na kwenye maeneo ya maduka na masoko na kuzisimulia hadithi za Wairani na ujasiri wa wafalme wao, Nazir ataweza kuzigeuzia mbali fikara za watu kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na kuzielekeza kwake.
Ili kuishusha hadhi ya Mtume (s.a.w.w.) na kuyaonyesha kwamba maneno yake na aya za Qur’ani havina thamani alisema kwa kurudia rudia: “Enyi watu! Nini tofauti baina ya maneno yangu na yale ya Muhammad? Anakusimulieni hadithi za watu waliopatilizwa kwa ghadhabu ya Allah na adhabu kali, na anakusimulieni hadithi za wale waliobarikiwa mno na waliokuwa wakitawala usoni mwa nchi kwa miaka mingi mno.”

Njia hii ilikuwa ya kijinga mno kiasi kwamba haikudumu zaidi ya siku chache, kiasi kwamba Waquraishi wenyewe walichoshwa na maneno ya Nazar na wakamtelekeza. Zilifunuliwa aya za Qur’ani juu ya jambo hili:

وَقَالُوا أَسَاطِيرُ الْأَوَّلِينَ اكْتَتَبَهَا فَهِيَ تُمْلَىٰ عَلَيْهِ بُكْرَةً وَأَصِيلًا {5}

قُلْ أَنْزَلَهُ الَّذِي يَعْلَمُ السِّرَّ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ إِنَّهُ كَانَ غَفُورًا رَحِيمًا {6}

“Na wanasema: ‘Ni visa vya watu wa kale alivyoviandika, hivyo anavisomewa asubuhi na jioni’Sema: ‘Ameiteremsha Yule ajuaye siri za mbinguni na ardhini; bila shaka Yeye ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.” (Suratul-Furqan, 25:5-6).

Kung’ang’ania Kwa Waquraishi Kwenye Itikadi Yao

Mtukufu Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) alitambua vizuri sana kwamba watu wengi waliifuata ibada ya masanamu kwa kuiiga itikadi ya viongozi wa kabila na itikadi hii haikushika mizizi mno nyoyoni mwao. Hivyo basi, kama ikitokea akafaulu kuwabadili viongozi hao, na akafanikiwa kumuon- goza mmoja au wawili miongoni mwao, mengi ya matatizo yangalitatuliwa.

Hivyo basi alikuwa na shauku kuu ya kumvutia Walid bin Mughayrah (ambaye baadae mwanawe Khalid alipata kuwa amirijeshi wa kiislamu na mtekaji wa nchi), kwa sababu alikuwa ndiye mzee zaidi ya wote na mtu mwenye ushawishi mkubwa zaidi miongoni mwa Quraishi na alikuwa na heshima na mwenye madaraka. Alikuwa akiitwa mwenye hekima wa Uarabuni na maoni yake yaliheshimiwa zaidi katika utatuzi wa mambo mbali mbali yaliyokuwa yakileta mizozo.

Siku moja Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alipokuwa akizungumza naye (Walid), Ibn Ummi Maktum, kipofu huyu, alimjia Mtume (s.a.w.w.) na kumwomba amsomee aya fulani fulani za Qur’ani tukufu. Alilishikilia mno jambo hilo kiasi kwamba Mtume (s.a.w.w.) aliichukia tabia ile, kwa sababu haikufahamika ni lini itapatikana nafasi tena ya kuzungumza na huyu muungwana wa Uarabuni katika hali ya amani kama ile. Hivyo basi, alimgeuzia mbali uso wake yule Ibn Ummi Maktum na akiwa na paji la uso lililokunjamana, aliachana naye.

Tukio hili likakoma. Hata hivyo, Mtume (s.a.w.w.) alikuwa akiliwazia jambo lile wakati aya kumi na nne za mwanzoni za Surah ‘Abasa zilipofunuliwa:

عَبَسَ وَتَوَلَّىٰ {1}

أَنْ جَاءَهُ الْأَعْمَىٰ {2}

وَمَا يُدْرِيكَ لَعَلَّهُ يَزَّكَّىٰ {3}

أَوْ يَذَّكَّرُ فَتَنْفَعَهُ الذِّكْرَىٰ {4}

أَمَّا مَنِ اسْتَغْنَىٰ {5}

فَأَنْتَ لَهُ تَصَدَّىٰ {6}

وَمَا عَلَيْكَ أَلَّا يَزَّكَّىٰ {7}

وَأَمَّا مَنْ جَاءَكَ يَسْعَىٰ {8}

وَهُوَ يَخْشَىٰ {9}

فَأَنْتَ عَنْهُ تَلَهَّىٰ {10}

كَلَّا إِنَّهَا تَذْكِرَةٌ {11}

فَمَنْ شَاءَ ذَكَرَهُ {12}

“Alikunja uso na akageuza mgongo. Kwa sababu alimjia kipofu. Ni nini kitakujulisha huenda atajitakasa au atakumbuka na ukumbusho (wa Qur’ani) utamfaa.? Ama ajionaye hana haja, wewe ndiye unayemshughulikia. Na si juu yako kama hatajitakasa. Na ama yule anayekujia, naye yu mwenye kuogopa, wewe unampuuza. Sivyo, hakika hii (Qur’ani) ni mawaidha. Basi yule anayependa atawaidhika.” (Surah Abasa, 80:1-12).

Ulama mashuhuri na wanachuoni watafiti miongoni mwa Mashi’ah4 huichukulia sehemu hii ya Hadith kuwa si yenye msingi hata kidogo na isiyoafikiana na maadili mazuri ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na wanasema kwamba aya hizi zenyewe hazionyeshi ya kwamba ni yeye Mtume (s.a.w.w.) aliyekunja uso na kuugeuzia mbali uso wake kutoka kwa kipofu yule.

Imenukuliwa Hadith kutoka kwa Imam wetu wa sita, Jafar as-Sadiq (a.s.) isemayo kwamba mtu aliyedhamiriwa alikuwa ni mtu wa familia ya Umayyah. Wakati Ibn Ummi Maktum alipomjia Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) yule mtu alionyesha chuki juu yake na Aya hizi zilifunuliwa ili kumuonya.5

Wanapiga Marufuku Kuisikiliza Qur’ani Tukufu

Utawala wa waabudu masanamu wa mjini Makkah uliunda mpango mkubwa wa kuzuia ueneaji wa Uislamu. Wakaanza kuitekeleza mipango yao kivitendo, mmoja baada ya mwingine, lakini walishindwa kulifikia lengo lao.

Waliendesha propaganda kubwa zaidi dhidi ya Mtume (s.a.w.w.) kila mara, lakini hawakupata mafanikio yoyote. Waliona kwamba Mtume (s.a.w.w.) alikuwa imara kwenye kazi yake na mionzi ya nuru ya Upweke wa Allah ilikuwa ikipenyeza zaidi na zaidi, siku baada ya siku.

Machifu wa Waquraishi waliamua kuwazuia watu wasiisikilize Qur’ani ili kuhakikisha kupata mafanikio katika mpango wao huo, walipeleka wapelelezi kwenye sehemu zote za mji wa Makkah ili waweze kuwazuia mahujaji na wafanya biashara waliopotembelea Makkah wasiwasiliane na Muhammad na waweze kuwazuia kwa njia yoyote ile iwezekanayo wasiisikilize Qur’ani. Mzungumzaji wa kundi hili alieneza tangazo miongoni mwa wakazi wa Makkah, ambalo Qur’ani inalizungumzia ikisema:

وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لَا تَسْمَعُوا لِهَٰذَا الْقُرْآنِ وَالْغَوْا فِيهِ لَعَلَّكُمْ تَغْلِبُونَ {26}

Wanasema wale waliokufuru: ‘Msiisikilize hii Qur’ani bali ipigieni makelele pale inaposomwa, huenda mkashinda.” (Surah al-Fussilata, 41:26).

Silaha yenye athari nzuri aliyoitumia Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) iliyojenga hofu na woga wa ajabu nyoyoni mwa maadui ilikuwa ni hiyo Qur’ani yenyewe. Machifu wa Waquraishi waliweza kuona ya kwamba wengi wa maadui wa jadi wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) walikwenda kukutana nae kwa nia ya kumdhihaki au kumdhuru. Lakini mara tu walipozisikia aya chache za Kitabu hiki Kitakatifu waligeuka na kuwa wafuasi wake waaminifu. Ili kuyazuia matukio kama hayo, Waquraishi waliamua kuwazuia wa chini wao na wafuasi wao kuisikiliza Qur’ani na wakayaharamisha mazungumzo na Mtume Muhammad (s.a.w.w.).

Watunga Sheria Wenye Kuzivunja Sheria

Watu walewale waliozuia vikali kuisikiliza Qur’ani na kuwaadhibu wale wote waliolivunja tangazo lile, baada ya siku chache waliingia kwenye mkumbo wa wavunja sheria na kivitendo, walizivunja kwa siri sheria zile zile walizoziidhinisha wao wenyewe!

Siku moja Abu Sufyan, Abu Jahl, na Akhnas bin Shariq walitoka majumbani mwao na wakaelekea nyumbani kwa Mtume (s.a.w.w.) bila ya mmoja wao kutambua kuwa mwenzie nae anakwenda huko.

Kila mmoja wao alijificha kwenye kona, na lengo lao lilikuwa kuisikiliza Qur’ani ya Muhammad aliyokuwa akiisoma wakati wa usiku kwa sauti tamu, alipokuwa akisali. Wote walikaa pale hadi alfajiri, bila ya kutambua kule kuwapo kwa wale wenzie, na wakaisikia Qur’ani. Asubuhi ilibidi warudi majumbani mwao. Walikutana njiani na wakakemeana wenyewe kwa wanyewe wakisema kwamba kama watu wenye akili ndogo watavitambua vitendo vyao, watawafikiriaje?

Jambo hili hili lilirudiwa kwenye usiku uliofuata. Itaonekana kwamba shauku na mvuto wa ndani uliwavutia kwenda kule nyumbani kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Walipokuwa wakirejea, walikutana tena na wakakemeana tena na wakaamua kutokukirudia tena kitendo chao kile. Hata hivyo, mvuto wa Qur’ani ulikuwa mkali kiasi kwamba walikwenda tena nyumbani kwake bila ya kufahamiana na kukaa kandoni mwa nyum- ba ile na kuisikiliza Qur’ani hadi alfajiri. Walipozikiliza aya za Qur’ani, hofu yao ilizidi na kila mara, wakajiambia: “Kama hizi ahadi na vitisho vya Muhammad vikiwa sahihi, basi sisi tutakuwa tulioishi maisha ya dhambi!”

Kulipokucha waliondoka nyumbani pa Muhammad (s.a.w.w.) kwa kuchelea watu wenye akili finyu na vile vile wakakutana. Wote wakakiri kwamba hawakuweza kuvumilia mvuto wa ‘mwito’ na kanuni za Qur’ani. Hata hivyo, ili kuzuia tukio lolote lisilopendeza, walifunga mapatano baina yao ya kwamba hawatalirudia tendo hili tena.6

Kuwazuia Watu Wasisilimu

Baada ya kutekeleza ule mpango wa awali wa kuharamisha kuisikiliza Qur’ani, waliuanza ule mpango wa pili. Watu waliokuwa wakiishi kwenye sehemu za karibu na za mbali walipokuwa na mwelekeo wa kuelekea kwenye Uislamu walikuja Makkah. Wale wapelelezi walionana nao visin- gizio mbalmbalili. Hapa chini tunatoa mifano miwili ya dhahiri:

Mfano wa kwanza: Aa’asha alikuwa mmoja wa washairi wakuu wa Zama za Ujinga na mashairi yake yalikuwa yakinukuliwa kwenye mikusanyiko ya Waquraishi. Aa’asha alipata habari za maamrisho ya Allah na mafundisho mazuri ya Uislamu wakati alipokuwa yu mzee.

Aliishi kwenye sehemu iliyokuwa mbali na Makkah. ‘Mwito’ wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) ulikuwa bado haujaenea kwa ukamilifu hadi kuifikia sehemu ile, lakini hata yale machache aliyoyasikia kuhusu Uislam kwa maelezo machache yalijenga huba kuu moyoni mwake juu ya Uislamu. Alitunga wasifu mzuri sana akimsifu Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na hakuifikiria zawadi yoyote kuwa ni bora kuliko kuusoma wasifu ule mbele ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.).

Ingawa idadi ya mistari ya wasifu huu haikuzidi ishirini na minne, mistari hii ndiyo bora zaidi iliyowahi kusomwa katika kumsifu Mtume (s.a.w.w.) katika nyakati zile.

Wasifu huu waweza kupatikana kwenye kitabu chake cha mashairi.7 Mshairi huyu anayatukuza mafundisho bora ya Mtume (s.a.w.w.) yaliyoiangaza akili yake.

Aa’asha alikuwa bado hajapata bahati ya kuja kwa Mtume (s.a.w.w.) wakati alipokutana na wale wapelelezi wa wenye kuabudu masanamu na wakazitambua hisia zake. Walijua vema kwamba Aa’asha alikuwa mtu wa anasa na mzoefu wa mvinyo. Mara moja waliitumia fursa ya ule unyonge wake na kusema: “Ewe Abu Basir! Dini ya Muhammad haiafikiani na fikara zako na hali ya utu wako.” Akauliza; “Kwa nini?” wakamjibu: “Ameiharimisha zinaa.” Akasema: “Sina lolote nayo, na jambo hilo halinizuii kusilimu.”

Wakaendelea kusema: “Vile vile amekataza kunywa mvinyo.” Aliposikia hivyo alipatwa na hali fulani ya mashaka na akasema: “Mimi bado sijakinaiwa na mvinyo. Sasa nitarudi na kunywa mvinyo hadi nishibe kwa kipindi cha mwaka mmoja na nitakuja tena mwaka ujao na kusilimu mikononi mwake!” Kisha akarudi kwake, lakini kifo hakikumruhusu kuyatekeleza yale aliyoyasema, kwa kuwa alifariki ndani ya mwaka ule ule.8

Mfano Mwingine

Tufayl bin Amr, aliyekuwa mtu mwenye hekima na mshairi mwenye sauti nzuri na aliyeheshimiwa mno na kabila lake, alikuja Makkah. Lilikuwa ni jambo lenye kuchukiza na kusumbua kwa Waquraishi kwamba Tufayl asilimu. Hivyo basi, wale machifu wa Waquraishi na wafanya kiini macho wa diplomasia walimkusanyikia na wakagumia, wakisema: “Yule mtu anayesali kandoni mwa Al-Ka’ba ameuharibu umoja wetu na kujenga mfarakano miongoni mwetu kwa masimulizi yake ya kiuchawi, nasi twachelea ya kwamba atajenga mfarakano wa aina hiyo hiyo ndani ya kabila lako pia. Hivyo basi, ingalifaa kama usingalizungumza naye kabisa.”

Tufayl anasema: “Maneno yao yalinivutia mno kiasi kwamba hofu ya kwamba masimulizi ya kichawi ya Muhammad yangaliniathiri, niliamua nisizungumze naye au kusikiliza yale aliyosema. Hivyo basi, ili kujikinga na athari za uchawi wake, niliamua kutia pamba masikioni mwangu wakati nikifanya ‘tawaaf,’ ili sauti yake isinifikie anapoisoma Qur’ani na kusali sala zake.

Asubuhi ilipoingia niliingia msikitini baada ya kutia pamba masikioni mwangu na sikuwa na mwelekeo kabisa wa kumsikiliza hata kidogo akiongea. Hata hivyo, sijui ilitokeaje kwamba, kwa ghafla tu baadhi ya maneno yaliyo matamu mno na yenye kupendeza yalifika masikioni mwangu nami nikayafurahia mno. Kutokana na hali hii, nilisema nafsini mwangu: “Na ulaaniwe! Wewe ni mtu wenye lugha fasaha na mwenye akili sana. Kuna madhara gani kama ukiyasikia ayasemayo mtu huyu? Kama anazungumza jambo zuri, huna budi kulikubali, la sivyo, ni sawa kama utaweza kulikataa. Hata hivyo, nilingojea ili nisiwasiliane na Mtume yule hadharani.

Mwishowe, Mtume (s.a.w.w.) alitoka kurudi nyumbani kwake na akaingia humo. Mimi nami niliomba na nikaruhusiwa kuingia nyumbani mwake. Nilimwelezea kisa kizima nikisema: “Waquraishi wanahusisha nawe vitu vingi mno, na hapo mwanzoni sikuwa na dhamira yoyote ya kuonana nawe. Hata hivyo, utamu wa Qur’ani umenivuta kwako. Sasa ninakuomba tafadhali, nieleze asili ya dini yako na unisomee sehemu ya Qur’ani. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alinifahamisha dini yake na akanisomea sehemu ya Qur’ani.”

Tufayl anaendelea kusema: “Ninaapa Wallahi! Sikupata kamwe kuyasikia masimulizi yenye kuzivutia mno na sikupata kuiona sheria iliyo ya wastani!” Kisha Tufayl akamwambia Mtukufu Mtume (s.a.w.w.): “Mimi ni mtu mwenye uwezo na ushawishi katika kabila langu nami nitachukuwa hatua kwa ajili ya kuilingania dini yako.” Ibn Hisham anaandika ya kwamba9 yeye (Tufayl) alikuwa pamoja na kabila lake hadi kwenye vita vya Khaybar na alibakia katika shughuli za kuubalighisha Uislamu na alijiunga na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kwenye vita vile hasa pamoja na familia za kiislamu sabini au themanini.10 Alisalia kuwa imara kwenye Uislamu hadi alipokufa Kishahidi mwenye vita vya Yamamah.

  • 1. Siira-i Ibn Hisham, Juzuu 1, uk.270.
  • 2. Majma'ul-Bayan, Juzuu 10, uk. 387.
  • 3. Siirah-i Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 393.
  • 4. Si Mashi’ah tu, hata watafiti wa kisunni akiwemo mfasiri mwanafalsafa na mchambuzi mkubwa aliye tegemeo na dira wa madhehebu ya kisunni Al- Fakhrud-Din Razi amekanusha wazo hilo. Mchambuzi huyu katoa hoja nyingi na hatimaye akasema: “Hatukubali kuwa usemi huu ulielekezwa kwa Nabii (s.a.w.).” Akajadili tena wazo hilo na kuhitimisha kwa: “Hayo hayaendani na tabia zake nzuri.” Kwa faida zaidi rejea kitabu chetu cha Kiswahili kiitwacho Uma’asumu wa Mitume, shehemu ya tatu inayohusu Uma’asumu wa Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w.) – (Mhariri).
  • 5. Majma’ul-Bayaan, Juzuu 1, uk. 437.
  • 6. Siirah-i Ibn Hishamu, Juzuu 1, uk. 337.
  • 7. Diwaan-i Aa’asha, uk. 101-103.
  • 8. Siirah-i Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 386-388
  • 9. Siirah-i Ibn Hisham, Juzuu 1, uk.410.
  • 10. Dakta Haykal anasema: "Alijiunga na Mtume (s.a.w.w.) baada ya kutekwa kwa mji wa Makkahh lakini bado hatujapata ushahidi wowote wa kauli hii.