Sura Ya 19: Uzushi Wa Gharaaniq

Inawezekana kwamba baadhi ya wasomaji wetu wangalipenda kuijua asili ya ngano ya ‘Gharaaniq’ iliyonukuliwa na baadhi ya wanahistoria wa Kisunni, na hivyo wakaifahamu mikono iliyokuwa ikijishughulisha katika kubuni na kutangaza uongo.

Wayahudi, na hasa viongozi wao wa Kidini wamekuwa, na bado wangali maadui wakuu wa Uislamu. Kikundi chao kama vile Ka’ab Ahbaar, ambacho kwa dhahiri walijifanya wamesilimu, walikuwa wakidumu katika kuuficha ukweli wa Uislamu kwa kuzusha uongo na kutangaza vitu visivyo na msingi kwa kuvihusisha na Mtume (s.a.w.w.), na badhi ya waandishi wa kiislamu, wakionyesha imani njema juu ya wanadini wenzao wote, waliukubali mwingi wa uzushi wao bila ya kuufanyia uchunguzi unaostahili na wakaukusanya ukiwa katika hali ya Ahadith na historia.

Hata hivyo, siku hizi fursa nyingi zaidi zinapatikana kwa upande wa wanachuoni kwa ajili ya kuchunguza mambo kama haya na hasa seti ya kanuni na mbinu zimetokea kwanye matumizi zikiwa ni matokeo ya juhudi za wanachuoni watafiti wa kiislamu katika kuzitofautisha kweli za kihistoria kutokana na ngano za uongo. Katika hali hii si sahihi hata kidogo kwa mwandishi, mwenye elimu kubwa katika mambo ya dini, kukubali kuwa ndio mwisho kwa kila alionalo kitabuni na kulinukuu pasi na kuthibitisha

Uzushi Wa Gharaaniq Ni Nini?

Inasemekana kwamba machifu wa Waquraishi kama vile Walid, Aas, Aswad na Umayyah walikutana na Mtume (s.a.w.w.) na wakapendekeza ya kwamba, ili kuziondoa tofauti zilizokuwapo baina yao, kila upande kati ya hizo mbili, uwatambue miungu wa ule mwingine. Wakati ule ule ‘Surah al- Kafirun’ ilifunuliwa kulijibu pendekezo lao na Mtume (s.a.w.w.) aliamrishwa kusema hivi: “Mimi sikiabudu kile mkiabuducho, wala ninyi hamumwabudu Yule Nimwabuduye.”

Hata hivyo, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alikuwa na shauku kuu ya kupatan- isha kati yake na watu nae alipenda kwamba iweze kufunuliwa amri itakayopunguza umbali baina yake na jamaa zake. Siku moja alikuwa ameketi karibu na Al-Ka’ba akiisoma Suratun-Najm kwa sauti ya kuvuma sana. Alipozifikia aya hizi mbili: “Je, umeyafikiria al-Lat na al-Uzza na jingine la tatu Manat?” (Surah al-Najm, 53:19-20), kwa ghafla shetani akafanya azitamke sentensi nyingine mbili ambazo ni: “Hawa ni Gharaaniq1 walio na vyeo vikuu na maombezi yao yanatakabaliwa,” na kisha akazisoma aya zilizosalia.

Alipoifikia ile aya ya Sajdah (aya ya mwisho ya Surah ile), yeye Mtume mwenyewe pamoja na wale wote waliokuwapo pale, ama Waislamu au waabudu masanamu, wote walisujudia masanamu ila Walid tu aliyekuwa mzee sana kiasi cha kutoweza kufanya hivyo.

Yalikuwapo makelele na furaha miongoni mwa wale waliokuwamo msikitini mle na wenye kuabudu masanamu wakisema kwamba, Muhammad amezungumza vema juu ya miungu wao. Taarifa juu ya maafikiano ya Muhammad na Waquraish zikawafikia wale waliohamia Ethiopia na matokeo yake yakawa kwamba baadhi yao walirudi kutoka maskanini mwao (Ethiopia). Hata hivyo, waliporudi waligundua ya kwamba hali imebadilika tena na malaika amemletea ufunuo Mtume na kumtaka tena awapinge wenye kuabudu masanamu na alimwambia kuwa Shetani amemfanya ayatamke maneno yale na yeye (malaika ) hakuyasema katu!

Hiki ndicho kiini cha uzushi huu wa ‘Gharaaniq’ ambao wataalamu wa mambo ya nchi za Mashariki (Mustashriq) wanayo shauku kuu ya kuunukuu kwa majivuno mengi.2

Kuelezeka Kwa Urahisi Kwa Uzushi Huu

Unaweza kudhania kwamba Muhammad hakuwa mmoja wa wateule wa Allah, bali hekima na akili zake haviwezi kukanwa kwa vyovyote vile. Basi sasa ni vipi mtu mwenye busara akielekee kitendo kama hiki? Je, yawezekana kwamba mtu mwenye busara zake anayeona kwamba idadi ya wafuasi wake inakuwa kubwa siku hadi siku na mpasuko kwenye safu za adui unakua, katika hali hiyo, afanye jambo liwezalo kukishusha chini cheo chake mbele ya marafiki zake pamoja na maadui zake?

Je, waweza kuamini kwamba yule mtu aliyezikataa ahadi za vyeo, na uta- jiri kutoka kwa Waquraishi, kwa ajili ya dini ya Allah aanzishe tena ushirikina na ibada ya masanamu? Achilia mbali kuzungumzia juu ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), hatuwezi kutegemea kitu cha aina hii japo kutoka kwa mwana mageuzi au mtawala wa kawaida.

Uamuzi Wa Busara Juu Ya Ngano Hii

Kwanza: Kwa mujibu wa hukmu ya busara, waalimu watakatifu daima ni wenye kinga kutokana na aina zote za makosa kutokana na nguvu ya kutokosea waliyokuwa nayo. Lakini tukikubali kwamba wao nao wana uwezekano wa kutenda makosa kwenye mambo ya kidini, ule msingi wa imani walionao watu kwenye maneno yao huvunjikia mbali.

Hivyo basi, ni muhimu kwamba hatuna budi kuyachunguza mambo ya kihistoria kwa msingi wa itikadi zetu za kiakili na tuyafumbue mafumbo haya ya historia kwa itikadi yetu iliyo madhubuti. Na haipingiki kwamba unyoofu wa Mtume Muhammad (s.a.w.w.) katika kuibalighisha dini ya Allah haungeruhusu kutokea kwa matukio ya aina hii.

Pili: Ngano hii imesimamia kwenye dhana ya kwamba Mtume (s.a.w.w.) alichoshwa na jukumu ambalo Allah ameliweka begani mwake na alihangaishwa mno na mtengano na kitendo cha watu wake kuwa mbali nae. Hivyo basi, alikuwa na shauku ya kupata njia na jinsi ya kurekebisha hali yao. Hata hivyo, ni lazima Mitume wawe na subira mno na wavumilivu, umadhubuti wao hauna budi kuwa mfano miongoni mwa watu wote na katu wasifikirie kuiacha kazi yao.

Kama ngano hii ikiwa tukio la kweli na lililothibitishwa, litakuwa na maana ya kwamba shujaa wa masimulizi yetu kapoteza umadhubuti, na subira yake na ari yake vimeshuka na amechoka. Kwa kweli hili hali- afikiani na hukmu ya hekima na vile vile haliafikiani na maisha ya Mtume (s.a.w.w.) ya kale na yaliyofuatia, kama tuyajuavyo.

Mzushi wa Hadithi hii ameukataa ukweli uliopo kwamba, Qur’ani inaushuhudia uongo wa hadithi hii, kwa sababu Allah amembashiria ya kwamba uongo hautaingia kwenye njia Yake: “. . . . Hiki ni Kitabu chenye kuheshimika. Haitakifikia batili kutoka mbele wala kutoka nyuma yake; . . . .” (Surah al-Fussilat, 41:41-42).

Vile vile Allah ame- toa ahadi nzito ya kwamba ataihami Qur’ani kutokana na kila madhara kipindi chote cha historia nzima ya mwanaadamu: “Hakika Sisi tumeit- eremsha Qur’ani na hakika Sisi ndio Wahifadhi wake.” (Surah Hijr; 15:9).

Hivyo basi, ingaliwezekana kwamba yule mlaaniwa (shetani) amshinde nguvu mteule wa Allah, achomeke uongo mwenye Qur’ani Yake na aifanye Qur’ani ambayo msingi wake hasa umesimamia kwenye kampeni dhidi ya ibada ya masanamu, kuwa mwendelezaji wa mfumo wa ibada ya ushirikina.

Inashangaza kwamba Mbunifu wa ngano hii ameimba wimbo usio na utaratibu wa sauti na ameusingizia Upweke wa Allah kwenye sehemu ile ambayo muda mfupi kabla ya hapo, Qur’ani tukufu yenyewe imepingana na masingizio haya, kwa sababu kwenye aya ya tatu, ya nne na ya tano ya Surah ile ile; Allah amesema: “. . . .Yeye (Mtume) hasemi kwa tamaa yake. Huu ni ufunuo uliofunuliwa (kwake). Amemfundisha Yule Mwenye nguvu, Mkuu.”(Surah al-Najm, 53:3-5).
Bila ya kujali bishara hii bayana, ni vipi Yeye Allah amwache Mtume wake bila ya ulinzi wowote na aruhusu kwamba Shetani aikamate akili na fikara zake?

Tunasikitika kuijadili ngano hii kwa kirefu kuliko vile inavyostahili. Lakini ukweli ni kwamba maelezo yetu yamesimamia kwenye hoja za kiakili nayo yana faida kwa wenye kuuamini Utume wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Hata hivyo, hoja hizi hazitoshi kwa wale wataalamu Mustashirki, ambao bado nyoyo zao hazijaangazwa na imani juu ya Mtume (s.a.w.w.) na ambao huzinukuu na kuzieleza ngano za aina hii ili kuthibitisha ya kwamba dini hii haina matokeo mema. Hivyo basi, hatuna budi kujadiliana nao juu ya jambo hili kwa njia nyngine.

Hitilafu Ya Hadithi Hii Kwa Njia Nyingine

Historia inatuambia kwamba pale Mtume (s.a.w.w.) alipokuwa akiisoma Sura al-Najm, machifu wa Waquraishi ambao wengi wao walikuwa ni washairi wakuu na wasomi walikuwamo msikitini mle. Mmoja wao alikuwa ni Walid aliyekuwa mtabiri na mshairi wa Uarabuni na alikuwa maarufu kwa hekima na busara zake. Nao wote waliisikia Sura ile hadi mwishoni na wakafanya Sajdah ilipomalizikia na aya iwajibishayo Sajdah.

Hivyo basi, swali liibukalo hapa ni kwa nini watu hawa, waliokuwa washairi wakuu na wanachuoni, watosheke na sentensi mbili tu zinazowasifu miungu wao, wakati aya zinazozitangulia na zinazozifuatia hizi sentensi mbili zina maonyo na lawama kwa miungu wao?

Haifahamiki ni maoni yapi anayoyajenga huyu mzushi wa uongo huu wa dhahiri juu ya watu wale ambao lugha yao ya asili ilikuwa ni kiarabu, waliokuwa wakifikiriwa kuwa ndio washindi kwenye uwanja wa ufasaha wa lugha ndani ya jamii nzima ya kiarabu, na ambao walijua vidokezo na sitiari (achilia mbali mambo ya dhahiri) za lugha yao, bora zaidi kuliko yeyote mwingine.

Je, ilikuwa sahihi kwao kutosheka na sentensi hizo mbili zinazoisifu miungu yao na kuzidharau sentesi zilizotangulia na zilizofuatia? Tukiachilia mbali watu wengine, haiwezekani kuwahadaa hata watu wa kawaida kwa sentensi zenye mvuto wa uzuri ziwekwazo kwenye maelezo yenye lawama kamili kwa itikadi na mwenendo wao.

Sasa tuziandike zile aya zihusikazo na tuweke madoa badala ya hizi sen- tensi mbili. Unaweza kuamua vizuri zaidi kama sentensi hizi mbili zaweza kuwekwa kwenye aya zilizofunuliwa juu ya lawama za masanamu haya: “Je, umeyafikiria al-Lat na al-Uzza na jingine la tatu Maanaat?3

Je, Yeye (Allah) awe na mabinti nanyi muwe na wana? Hakika huu ni ugawaji wa kidhalimu! Wao (masanamu) si chochote ila ni majina ambayo ninyi na baba zenu mmeyazusha. Allah hakuyapa mamlaka yoyote”.

Je, mtu, hata yule wa kawaida tu, aweza kuukubali msingi wa sentensi zipinganazo kama hizo, ili kuweza kuuacha uadui wake na kuja kwenye maafikiano na mtu ambaye dini yake imejitahidi kuing’oa mizizi (ya ibada ya masanamu) kwa kipindi cha miaka kumi, na ameuhatarisha uhai wake kwa ajili ya njia ile?

Hoja Dhidi Ya Ngano Hii Kwa Mtazamo Wa Lugha

Mwanachuoni maarufu wa Kimisri, Muhammad Abduh anasema: “Katu neno ‘Gharaaniq’ halikupata kutumika kwa ajili ya ‘miungu’ ndani ya lugha ya kiarabu na ushairi.
Maneno ‘Gharnuq’ na Gharniq’ yanapatikana kwenye kamusi nayo yana maana ya ndege maalumu wa majini au kijana wa kiume mwenye sura nzuri sana, kati ya maneno haya hakuna litoalo maana ya ‘miungu.’

Ushahidi Utolewao Na Baadhi Ya Mustashirki

Sir (Bwana) William Muir ameichukulia ngano hii ya Gharaaniq kuwa ni ukweli wa kihistoria uliothibitika, na ushahidi alioutegemea ni huu: “Muda wa zaidi ya miezi mitatu tangu kuhama kwa Waislamu kwenda Ethiopia ulikuwa bado kupita, nao walikuwa wakiishi maisha ya amani chini ya ulinzi wa Negus. Wasingaliweza kurudi Makkah kuwaona ndugu na jamaa zao kama wasingalipata taarifa juu ya mapatano baina ya Muhammad na Waquraishi. Hivyo basi, lilikuwa ni jambo la muhimu kwamba Muhammad atoe njia ya amani na njia ile ilikuwa ni hadithi hii hasa ya ‘Gharaaniq’ yenyewe”

Hata hivyo, mtu anaweza kumwuliza mtaalamu huyu maarufu wa mambo ya nchi za Mashariki. Kwanza: Kwamba ni kwa nini iwe muhimu kwamba kurejea kwa wahamiaji wale kule Makkahh kuwe ni matokeo ya taarifa zilizo sahihi? Katika maisha ya kila siku, watu wenye tamaa zao za kibinafsi hutawanya maelfu ya taarifa za uongo miongoni mwa watu kila mara. Hivyo basi, iliwezekana kabisa kwamba watu fulani walizizusha taarifa hizo za mapatano baina ya Mtume Muhammad na Waquraishi kwa lengo la kuwafanya Waislamu warejee nchini mwao kutoka Ethiopia, na hivyo baadhi yao waliziamini taarifa zile na wakarejea, na ambapo wengine hawakudanganyika na wakaendelea kuishi huko Ehiopia.

Pili: Japo tuchukulie kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alitaka kufanya amani na Waquraishi, ni kwa nini msingi wa amani ile usimamishiwe kwenye hizo sentensi mbili za uongo? Ukweli ni kwamba, ingalitosha kuzivutia nyoyo zao kwake kama angaliwapa ahidi ya kweli ya kunyamaza kabisa kuhusiana na itikadi zao.

Kwa ufupi ni kwamba, kurejea kwa wahamiaji hawa si ushahidi wa usahihi wa ngano hii, pia amani na mapatano navyo havitegemei kuzitamka sentensi hizi mbili.

  • 1. Gharaaniq ni wingi wa neno Gharnuq au Gharaaniq kwa maana ya aina fulani ya ndege wa majini au kijana mwenye sura nzuri sana.
  • 2. Tarikh-i Tabari, Juzuu 2, uk. 75-76.
  • 3. Kama ukiijaza ile nafasi iliyoachwa wazi kwa kuiweka tafsiri ya zile sentensi mbili tunazozizungumzia (Hawa ni gharaaniq, walio na vyeo vikuu na maombezi yao yanatakabaliwa) bila shaka utaona kwamba zinapingana na aya zinazozitan- gulia na zinazozifuatia.