Sura Ya 21: Bwana Abu Twalib Afariki Dunia

Kizuizi kilichowekwa na Waquraishi dhidi ya Waislamu kilimalizikia kwenye kushindwa kutokana na kuingiliwa na watu wenye nyoyo njema. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na wasaidizi wake walilitoka lile “Bonde la Abu Twalib” na kurudi majumbani mwao baada ya miaka mitatu ya ukim- bizi, kuzuiliwa na shida. Kazi na biashara zao na Waislamu zikafufuliwa na iliweza kutegemewa ya kwamba hali yao ingalitengenezeka. Hata hivyo, mara kwa ghafla, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akakabiliwa na tukio liumalo mno lililoacha athari mbaya mno kwenye hamasa za Waislamu wasiokuwa na msaada wowote.

Kadiri ya athari za tukio hili kwenye hali ile mbaya haiwezi kupimwa kwa kipimo au mizani yoyote ile, kwa sababu kukua kwa wazo au fikra hutegemea visababisho viwili, navyo ni uhuru wa kuzungumza na uwezo uhitajikao kwa mtu kuweza kujitetea dhidi ya mashambulio maovu ya adui. Hivyo basi, ilitokea kwamba pale Waislamu walipojaaliwa uhuru wa itikadi, walikipoteza kile kisababisho cha pili kwa sababu yule msaidizi na mlinzi mkuu wa Uislamu alifariki dunia.

Siku ile Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alimpoteza msaidizi na mlinzi aliyekuwa anahusika juu ya ulinzi na usalama wake tangu pale Mtume (s.a.w.w.) alipokuwa na umri wa miaka minane hadi mwishoni, alipokuwa akipita kwenye mwaka wake wa hamsini. Ni yeye aliyekuwa akimzunguka zunguka mwilini mwake kama vile afanyavyo kipepeo kandokando ya mshumaa. Ni yeye aliyempatia Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) mahitaji ya maishani mwake hadi yeye mwenyewe alipopata uwezo wa kujipatia vitu hivyo na akampendelea zaidi kuliko yeye mwenyewe pamoja na wanawe.

Mtume (s.a.w.w.) alimpoteza mtu ambaye Bwana Abdul-Muttalib (babu yake Mtume s.a.w.w) alipofariki dunia alimfanya mlezi wake kwa maneno yafuatayo:

“Ewe Abdi Munaf!1 Ninakufanya kuwa mwenye kuwajibika juu ya ulinzi wa yule anayemwabudu Mungu Mmoja tu, kama alivyokuwa baba yake.” Abu Twalib akasema: “Ewe baba yangu mpenzi! Muhammad hahitaji usia wowote kwa kuwa yu mwanangu mwenyewe na vile vile yu mpwa wangu.”

Mifano Ya Huba Na Huruma Za Bwana Abu Twalib

Mifano ya huba na huruma za watu mbali mbali imeandikwa kwenye kurasa za historia. Hata hivyo, kwa kawaida imesimama kwenye msingi wa fikara za kidunia na kidesturi. Nayo huzunguka kwenye mhimili wa utajiri, na uzuri na ule mwali wa huba hutosheleza nafsini mwao katika kipindi kifupi sana na kisha hufutika. Hata hivyo, hisia zilizo kwenye msingi wa uhusiano wa udugu au itikadi kwenye ubora wa kiroho wa yule apendwaye haupotei upesi mno.

Ilitokea kwamba upendo wa Bwana Abu Twalib kwa Mtume (s.a.w.w.) ulikuwa kwenye msingi wa hali zote mbili, yaani alimwamini na akamkubali kuwa yu mtu mkamilifu na kigezo kisicho kifani cha utu wema, na vile vile alikuwa yu mpwa wake hasa ambaye alimpa hadhi ya ndugu na mwana moyoni mwake.

Bwana Abu Twalib aliuamini mno ukamilifu wake wa kiroho na utakatifu kiasi kwamba wakati wa ukame alikwenda naye kwenye ‘musallah’ (zulia la kusalia) na kumwomba Allah kwa ‘wasila’ wake na akaomba mvua kwa ajili ya watu waliokumbwa na ukame ule, na dua yake ilitakabaliwa na Allah Mwenyezi. Wanahistoria wamelinukuu tukio lifuatalo:

“Wakati mmoja Waquraishi walikabiliwa na ukame mkubwa mno na ardhi na mbingu zilizuia baraka zao juu yao. Walimjia Bwana Abu Twalib huku wakitiririkwa na machozi machoni mwao na wakamwomba kwa uaminifu aende kwenye musallah na amwombe Allah kwa ajili ya mvua. Bwana Abu Twalib alimshika mkono Mtume (s.a.w.w.), ambaye wakati ule alikuwa kijana mdogo, na akaegemea ukutani mwa Al-Ka’ba na akainua kichwa chake kuelekea mbinguni na akasema: “Ee Mola! Tunyeshee mvua kwa ajili ya mtoto huyu (akimsoza kwa kidole Mtume s.a.w.w) na utubariki kwa baraka Zako zisizo na kikomo.”

Wanahistoria kwa pamoja wameandika hivi: “Alimwomba Allah kwa ajili ya mvua kulipokuwa hakuna hata wingu moja mbinguni, lakini baada ya hapo lilitokea wingu upesi sana kutoka kwenye upeo wa macho. Sehemu ya wingu lile ilienea kwenye anga juu ya mji wa Makkah na viungani mwake. Ngurumo na radi vilitoa sauti kuu. Sehemu zote zikafurika maji na kila mtu akafurahi.”2

Mabadiliko Kwenye Mpango Wa Safari

Mtume (s.a.w.w.) alikuwa bado hajaufikia umri wa miaka kumi na miwili wakati Bwana Abu Twalib alipoamua kwenda Sham pamoja na msafara wa kibiashara wa Waquraishi. Wakati ngamia walipokuwa wameshasheheni na walikuwa karibuni kuanza safari, na tayari kengele ya kuondokea ishagongwa, mpwa wake Bwana Abu Twalib, kwa ghafla akaishika hatamu ya ngamia na akasema huku akitokwa na machozi machoni mwake: “Mpenzi ami yangu! Unaniacha katika dhamana ya nani? Ni lazima niende pamoja nawe.”

Hapo chozi lililokuwapo jichoni mwa Mtume Muhammad (s.a.w.w.) lilileta mafuriko ya machozi machoni mwa Bwana Abu Twalib.

Kwenye wakati huu mgumu, aliamua bila ya matayarisho ya kabla yake, kwenda na yule mpwa wake. Ingawa nafasi ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.) kwenye msafara ule haikujadiliwa, Bwana Abu Twalib aliamua kuzibeba taabu zihusikanazo na kule kufuatana naye, yeye mwenyewe. Alimpakiza kwenye ngamia wake na alichukua tahadhari iliyolazimika kwenye safari nzima kuhusiana naye. Kwenye msafara ule aliona mambo yasiyo na kifani ndani ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.) na akatunga beti za mashairi juu ya mambo hayo. Beti hizo zimenukuliwa mwenye vitabu vyake vya ushairi.3

Ulinzi Wa Itikadi Zake Takatifu

Kwa upande wa kuwa madhubuti, hakuna nguvu iliyo sawa na ile ya imani. Nguvu ya imani kwenye lengo lake mtu ndicho kipengele chenye nguvu zaidi kwa maendeleo ya mwanadamu katika daraja zote za maisha. Inamtayarisha kuuhimili usumbufu na taabu zote na kumfanya ayatoe mhanga maisha yake yenyewe kwa ajili ya kulifikia wazo lake takatifu.

Askari mwenye silaha ya nguvu ya imani yu mwenye kushinda kabisa. Anapoamini kwamba kuua au kuuwawa kwenye njia hii ni rehma, ushindi na kufaulu kwake vinathibiti. Kabla ya askari kupewa silaha za kisasa za kimaada hana budi kupata silaha ya nguvu ya imani, na ni lazima moyo wake ujazwe huba ya ukweli. Harakati zake wakati wa vita na wa amani hazinabudi kuongozwa na imani. Kwenda kwake vitani au kufanya kwake amani ni kwa ajili ya ulinzi wa itikadi yake tu.

Fikara na itikadi ni matunda ya mwelekeo na busara za mtu. Kama vile mtu awapendavyo watoto wake, vile vile anayapenda maoni yake yatokanayo na busara na moyo wake. Bali, huba yake kwa dini huwa kubwa hata kuliko ile ya wanawe. Hivyo basi, yuko tayari hata kukikumbatia kifo kwa ajili ya kuihami dini yake, lakini haendi umbali ule kuhusiana na kuwahami watoto wake.

Huba ya mwanaadamu juu ya utajiri na hadhi ina ukomo maalumu. Anaviendea vitu hivi kwa kiasi kile ambacho hahofishwi na kifo cha uhaki- ka. Hata hivyo, kuhusiana na dini yake, mtu yuko tayari kukitafuta kifo na akapendelea kifo cha heshima kuliko maisha ambayo ndani yake hataruhusiwa uhuru wa dini. Anaona kwamba maisha halisi ni yale ya ‘mujahidah’ (mwenye kujitahidi) na husema kwa kukariri: “Maisha ya kweli yanaandamana na imani na jihadi.”

Hebu yatupie jicho maisha ya Bwana Abu Twalib, muunga mkono mashuhuri na mlinzi wa Uislamu na Mtume Muhammad (s.a.w.w.). Alikuwa na kichocheo gani kwenye njia hii na ni kipengele kipi kili- chomshawishi hadi kufikia kiwango cha kujihatarisha na maangamizi, kuutelekeza uhai wake, utajiri wake, cheo chake na kabila lake, na kuvitoa mhanga vitu vyote hivi kwa ajili ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.)? Ni ukweli ukubalikao kwamba hakuwa na hamasa ya kidunia na katu hakuwa na shauku ya kuipata faida yoyote ya kidunia kutoka kwa yule mpwa wake, kwa sababu kwenye siku zile, Mtume (s.a.w.w.) mwenyewe hakuwa na utajiri wowote. Hakutaka kukipata cheo au nafasi yoyote ile, kwa sababu, tayari yeye alikuwa ameishika nafasi kuu zaidi kwenye jamii ya wakati ule na alikuwa ndiye chifu wa Makkah na Batha. Na kusema kweli, angaliweza kukipoteza hata kile cheo na daraja lake kuu kutokana na kumhami Mtume (s.a.w.w.), kwa kuwa ulinzi wake ndio sababu ya machifu wa Makkah kuupinga ukoo wa Hashim na wa Abu Twalib.

Dhana Potovu

Inawezekana kwamba baadhi ya watu wenye uoni mfupi wa mambo wakadhania kwamba sababu ya kujitoa mhanga kwa Bwana Abu Twalib ni ule uhusiano wa kijamaa wa karibu zaidi uliokuwapo baina yake na Mtume Muhammad (s.a.w.w.) na ni kwamba ni kwa sababu hii kwamba alikuwa tayari kuyatoa mhanga maisha yake hasa kwa ajili yake. Hata hivyo, dhana hii haina msingi kiasi kwamba tafakari ndogo tu huudhihirisha upumbavu wake, kwa sababu kifungo cha udugu wa damu hakina nguvu kiasi cha mtu kuweza kuitoa nafsi yake yote kwa ajili ya mmoja wa ndugu zake na amtoe mhanga mwanawe mwenyewe (Saidina Ali a.s) kwa ajili ya mpwa wake, na kuwa tayari kumwona mmoja wao akikatwa vipande vipande kwa ajili ya mwenziwe.

Wakati mwingine hisia za kiudugu humvutia mtu kwenye kiwango cha maangamizi, lakini hakuna maana katika hisia hizi kuwa kali hivyo kwa ajili ya mtu maalum tu, ambapo Bwana Abu Twalib aliitoa mihanga yote hii kwa ajili ya mtu maalum miongoni mwa nduguze (yaani Mtume s.a.w.w) na hakufanya hivyo kuhusu dhuria wengine wa Abdul-Muttalib na Hashim.

Kichocheo Halisi Cha Bwana Abu Twalib

Kutokana na hayo tuliyoyaeleza hapo juu tunaweza kusema kwamba kichocheo halisi cha mihanga hii ya Bwana Abu Twalib kilikuwa cha kiro- ho na wala si cha kimaada, naye alikuwa tayari kulikabili shinikizo lolote lile la adui kwa ajili ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.). Ilikuwa hivyo kwa sababu, alimwamini kwamba yu kigezo halisi cha ubora na utu wema na ameiona dini yake kuwa ni mpango ulio bora zaidi kwa mtu kuweza kujipatia ustawi na furaha. Kwa vile alikuwa mpenzi wa ukweli, bila shaka alikuwa akiuhami ukweli.

Ukweli huu hudhihiri kutokana na beti za mashairi ya Bwana Abu Twalib, akizionesha hisia zake anasema kwamba Muhammad yu Mtume mithili ya Mitume Musa na Isa. Hii ifuatayo hapa chini ni tafsiri ya mashairi yake: “Watu mashuhuri hawana budi kutambua kwamba Muhammad yu Mtume na Kiongozi kama Mitume Isa na Musa na kila Mtume hulibeba jukumu la mwongozo wa wanadamu kwa amri ya Allah. Unaweza kuzisoma sifa zake kwenye Vitabu vya Mbinguni kwa usahihi kamili na haya ni maneno ya kweli na wala si masingizio juu ya ghaibu.”4

Kwenye shairi lake jingine lenye kusifia aliloliandika juu ya huyu mpwa wake, anasema hivi: “Je, hamjui ya kwamba sisi tunamwona Muhammad kama yu Mtume wa Allah kama Musa bin Imraan na tunazisoma habari zake kwenye Vitabu vilivyopita.”5

Beti tulizozitaja hapo juu pamoja na nyingine nyingi zinazopatikana kwenye kitabu cha ushairi cha Abu Twalib na vile vile kwenye vitabu vya Ahadith na vya tafsiri ya Qur’ani zinadhihirisha ya kwamba kichocheo halisi cha Bwana Abu Twalib katika kumhami Mtume (s.a.w.w.) kilikuwa ni ulinzi wa dini ya kweli ya Uislamu. Hapa chini tutaitaja baadhi ya mihanga aliyoitoa, nawe unaweza kuamua vizuri, baada ya kufanya uchunguzi muhimu, kama ingaliweza kuhamasishwa na kitu chochote kile kisi- chokuwa imani ya kweli.

Mukhtasari Wa Mihanga Aliyoitoa Bwana Abu Twalib

Machifu wa Waquraishi walifanya mkutano nyumbani mwa Bwana Abu Twalib wakati Mtume (s.a.w.w.) akiwepo pia. Walizungumza wenyewe kwa wenyewe. Wale machifu waliamka kwenda zao bila ya kupata majibu ya mkutano ule, na ‘Uqbah bin Abi Mu’it akaanza kusema kwa sauti kuu: “Mwacheni. Ushauri hauna faida yoyote. Ni lazima auawe; ni lazima amaliziwe mbali!”

Bwana Abu Twalib aliudhika sana alipoyasikia maneno haya lakini hakuweza kufanya lolote, kwa kuwa walikuja nyumbani kwake wakiwa ni wageni wake. Ilitokea kwamba Mtume (s.a.w.w.) alitoka nje ya nyumba yake siku ile na hakurudi hadi jioni.

Ami zake walikwenda nyumbani kwake lakini hawakumkuta huko. Kwa ghafla Bwana Abu Twalib aliyakumbuka yale maneno ya ‘Uqbah aliyoyatamka masaa machahce yaliyopita na akasema moyoni: “Bila shaka wameshamwua mpwana wangu na waishayamaliza maisha yake!”

Alifikiria kwamba uamuzi umekwishafanyika na kwamba ilikuwa muhimu kumhami Muhammad na kulipiza kisasi kwa wale Mafirauni wa Makkah. Aliwaita dhuria wa Hashim na Abdul-Muttalib na akatoa maelezo kwam- ba wote wafiche silaha kali ndani ya mavazi yao na wafike kwenye Masjidul Haraam kwa pamoja. Zaidi ya hapo, kwamba kila mmoja wao akae karibu na chifu mmoja wa Waquraishi na yeye Bwana Abu Twalib atakaposema kwa sauti kuu: “Enyi machifu wa Waquraishi! Ninamtaka Muhammad kutoka kwenu.” Waamke mara moja na kila mmoja wao amuue yule chifu aliyekaa karibu naye, na hivyo machifu wote wawe wamekutana na hatima yao.

Bwana Abu Twalib alipokuwa karibu kuondoka, Zayd bin Harith aliingia nyumbani mle kwa ghafla na akawaona kwenye hali ya kuwa tayari tayari. Alishikwa na bumbuwazi alipoona hivyo na akasema: “Hakuna madhara yoyote yaliyompata Mtume. Yuko nyumbani kwa Mwislamu na sasa anajishughulisha na kuubalighisha Uislamu.” Baada ya kuyasema hayo alitoka upesi upesi na kumwendea Mtume (s.a.w.w.) na kumwarifu ule uamuzi wa hatari aliochukua bwana Abu Twalib.

Hapo Mtume (s.a.w.w.) alikwenda nyumbani kwake. Baada ya Bwana Abu Twalib kuuona uso wa yule mpwa wake alitokwa na machozi machoni mwake na akasema: “Ewe mpwa wangu! Ulikuwa wapi? Je ulikuwa kwenye furaha huko na salama kutokana na kila dhara wakati huo?” Mtume (s.a.w.w.) alimthibitishia ami yake kwamba hakuna dhara lililojitokeza kutoka upande wowote ule.

Usiku wote ule Bwana Abu Twalib alikuwa akiwaza. Alitafakari juu ya jambo lile na akasema moyoni: “Leo mpwa wangu hakuwa shabaha ya adui, lakini hawa Waquraishi hawatakaa kimya mpaka wamwue.” Aliona kwamba ni bora aende kule msikitini pamoja na dhuria wa Hashim na Abdul-Muttalib baada ya kuchomoza jua, wakati Waquraishi walipokuwa wamekusanyika pale, na kuwaarifu juu ya uamuzi wake ule ili kwamba, pengine huenda wakaogopa na wakaacha kupanga kumwua Muhammad. Jua lilipochomoza na muda ukafika kwa Waquraishi kutoka majumbani mwao na kwenda kujiunga na mikutano yao.

Walikuwa bado hawajaanza kuzungumza pale alipotokea Bwana Abu Twalib kwa mbali, nao wakaona ya kwamba mashujaa kadhaa wamefuatana naye. Wote wakawa makini na wakasubiri wasikie yale Bwana Abu Twalib aliyotaka kuyasema na ni kwa lengo gani kaja kule msikitini na watu wote wale.

Bwana Abu Twalib alisimama mbele ya mkutano wao na akasema: “Jana Muhammad alitoweka machoni petu kwa kitambo hivi. Nilidhani ya kwamba mmelitekeleza lile alilosema ‘Uqbah na kwamba mmemwua. Hivyo, nikaamua kuja hapa Masjidul Haraam pamoja na watu hawa. Pia niliwaagiza kwamba wawe nyuma ya kila mmoja wenu na mara tu wanisikiapo nikisema kwa sauti kuu waamke na kukushambulieni kwa silaha zao walizokuwa wakizificha. Hata hivyo, kwa bahati nimempata Muhammad akiwa hai na salama kutokana na madhara yoyote yale kutoka kwenu.” Kisha akawataka wale watu wake wazitoe silaha zao walizozi- ficha na akaiishilizia hotuba yake kwa maneno haya: “Wallahi! Kama mngalimwua, nisingalimwacha hata mmoja wenu na ningalipigana nanyi hadi mwishoni.”6

Kama ukitazama ndani ya wasifu wa maisha ya Bwana Abu Twalib utaona ya kwamba alimsaidia Mtume (s.a.w.w.) kwa miaka arobaini na miwili kamili na ameudhihirisha ushujaa mkubwa ajabu na kujitoa mhanga kwenye miaka kumi ya mwisho ya uhai wake iliyokuwa muhimu mno kwa sababu ya kule kuteuliwa kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kuishika kazi ya Utume na kwa ‘mwito’ wake wakati ule. Kipengele pekee kilichomfanya aendelee kuwa madhubuti, kilikuwa ni imani yake yenye nguvu ya itikadi yake halisi na safi juu ya ile kazi takatifu ya Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.). Na kama tukiongezea ile mihanga ya mwanawe, Imam Ali (a.s.) maana ya beti za Ibn Abil Hadid, kama zilivyotafsiriwa hapa chini, hudhihirika kabisa:

“Kama Abu Twalib na mwanawe wasingalikuwako dini isingalifaulu. Alimsaidia na kumhami yeye (Mtume s.a.w.w) pale mjini Makkah, na mwanawe alipiga mbizi kwenye dimbwi la kifo mjini Yathrib kwa ajili yake.”

Wasia Wa Bwana Abu Twalib Wakati Wa Kufariki Kwake Dunia

Wakati wa kufariki kwake dunia Bwana Abu Twalib aliwaambia watoto wake: “Ninakuusieni juu ya Muhammad, kwa kuwa yu mtu mwaminifu wa Waquraishi na mtu mkweli wa Arabia na anayo maadili yote.
Ameileta dini iliyokubaliwa na nyoyo, lakini ndimi zimechagua kuikana kwa kuhofia kuchekwa na kudhihakiwa. Ninaweza kuona kwamba watu wanyonge na wasiokuwa na msaada wa Uarabuni wameamka kumsaidia Muhammad na wakamwamini, naye vile vile ameamka kuwasaidia katika kuzivunja safu za Waquraishi. Amewafedhehesha wakuu wa Quraishi na ameyaharibu makazi yao na kuwaimarisha wasiokuwa na msaada na kuwapa hadhi.” Aliyamalizia mazungumzo yake kwa maneno haya: “Enyi ndugu zangu! kuweni marafiki na wafuasi wa dini yake (Uislamu). Yeyote yule amfu- ataye atakuwa amestawi. Kama kifo kingalinipa muda zaidi, ningalizikinga hatari zote zimjiazo.”7

Hatuna shaka juu ya hilo kwamba alikuwa mkweli kabisa katika kuyaelezea matakwa yake, kwa sababu huduma zake na mihanga yake, hasa kwenye kile kipindi cha miaka kumi ya mwishoni mwa uhai wake, vinaushuhudia ukweli wake. Ushahidi mwingine wa ukweli wake ni ile ahadi aliyomwahidi Muhammad mwanzoni mwa Utume wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), kwa sababu yeye Mtume alipowakusanya ami na ndugu zake wote, na kuwabalighishia Uislamu, Bwana Abu Twalib alimwambia Mtume (s.a.w.w.): “Amka, ewe mpwa wangu! Wewe unacho cheo kikuu. Dini yako ndio dini tukufu zaidi miongoni mwa dini zote. Wewe u mwana wa mtu mkuu. Kama ulimi ukikudhuru, ndimi kali zaidi zitajitokeza kukuhami na panga zilizo kali zitazikata ndimi za maadui zako. Ninaapa kwa jina la Allah! Waarabu watakuwa watiifu mbele yako kama mtoto wa mnyama alivyo mbele ya mama yake.”

Safari Ya Mwisho

Ingalikuwa bora kama tungaliulizia kuhusu ukweli wa itikadi ya Bwana Abu Twalib kutoka kwa akraba zake walio waaminifu, kwa kuwa mwenye nyumba ndiye mwenye kujua vizuri zaidi vilivyomo nyumbani mle.

1. Wakati Sayyidna Ali (a.s.) alipomwarifu Mtume (s.a.w.w.) kuhusu kifo cha Bwana Abu Twalib, Mtume (s.a.w.w.) alilia sana. Alimwagiza Sayyidna Ali (a.s.) atayarishe josho lake, na kisha akamwomba Allah kwa ajili ya wokovu wa roho ile iliyotoka.8

2. Alitajwa Bwana Abu Twalib mbele ya Imam wetu wa nne, Ali Zaynul Aabidin (a.s.). Yeye Imam akasema: “Nashangaa kwa nini watu wanatia shaka juu ya imani ya Abu Twalib, wakati mwanamke hawezi kuendeleza muungano wake ki-ndoa na mume asiye Mwislamu baada ya mwanamke yule kusilimu, na Fatimah binti Asad alikuwa miongoni ma wale wanawake waliosilimu kwenye siku za mwanzoni kabisa na bado akasalia kuwa mkewe Abu Twalib hadi pale alipofariki dunia

3. Imam wetu wa Tano, Muhammad Baqir (a.s.) anasema: “Imani ya Abu Twalib ilikuwa bora kuliko ile ya watu wengi, na Amir wa Waumini Ali bin Abi Twalib (a.s.) aliamrisha ya kwamba ifanyike Hajj kwa niaba yake.”9

4. Imam wetu wa Sita, Jafar As-Sadiq (a.s.) amesema: “Abu Twalib alikuwa mithili ya watu wa pango. Walikuwa na imani nyoyoni mwao laki- ni wakajifanya kuwa washirikina. Kutokana na sababu hii watalipwa maradufu.”10

Maoni Ya Wanachuoni Wa Kishi’ah

Wakiwafuata watu wa Nyumba ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), Ulamaa wa Imamiyah, kwa pamoja wanaafikiana juu ya ukweli kwamba Bwana Abu Twalib alikuwa mmoja wa Waislamu mashuhuri kabisa na alipofariki dunia alikuwa na moyo uliokuwa na imani iliyokamilika juu ya Uislamu na alikuwa mwaminifu sana kwa Waislamu. Wanachuoni hawa wameandika vitabu na makala nyingi juu ya jambo hili.

  • 1. Wakati mwingine inasemekana kwamba jina halisi la Abu Twalib lilikuwa ni Imraan. Baadhi ya wanachuoni wanaona kwamba Abu Twalib lilikuwa ndio jina lake hasa na si "Kuniyat” (jina la ubaba) yake.
  • 2. Siirah-i Halabi, Juzuu 1, uk. 125.
  • 3. Diwaan-i Abu Twalib, uk. 33.
  • 4. Majma'ul Bayaan, Juzuu 7, uk. 37; na al-Hujjah, uk. 56-57.
  • 5. Majma'ul Bayaan, Juzuu 7, uk. 36; Ibn Hisham amenukuu beti kumi na tano za shairi hili kwenye Siirah yake, Juzu 1, uk. 352-353.
  • 6. Taraa'if, uk. 85; na al-Hujjah, uk. 61.
  • 7. Siirah-i Halabi, Juzuu 1, uk. 390
  • 8. Sharh-i Nahjul Balagha, cha Abil Hadid, Juzuu 14, uk. 76.
  • 9. Sharh-i Nahju Balagha, Juzuu 14, Uk. 68
  • 10. Usul al-Kaafi, uk. 244.