Sura Ya 22: Mi’iraaj - Kupaa Mbinguni

Mi’iraaj Kwa Mujibu Wa Qur’anii, Hadith Na Historia

Lilikuwa tayari giza la usiku limeshaenea kwenye upeo wa macho na kimya kilishatawala juu ya uso wa maumbili. Muda ulikuwa umekwishafika wa viumbe vyenye uhai kujipumzisha na kulala ili kwamba waweze kupata nguvu kwa ajili ya amali zao siku iliyofuata.

Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) nae hakuwa huru kutokana na kanuni hii ya maumbile (kulala) nae alitaka kujipumzisha baada ya kuzisali sala zake. Hata hivyo, mara moja aliisikia sauti. Nayo ilikuwa ni sauti ya Malaika Mkuu Jibriil (a.s.) aliyemwambia: “Usiku huu huna budi kuifanya safari isiyo kifani, nami nimeamrishwa kubakia pamoja nawe. Itakubidi kuzipitia sehemu mbalimbali za ulimwengu ukiwa umemrekebu mnyama aitwaye ‘Buraaq”.

Mtume (s.a.w.w.) aliianza safari yake kuu kutoka nyumbani mwa Bibi Ummi Haani (dada yake Amir wa waumini, Ali bin Abu Twalib a.s) na akiwa amemrekebu yule Buraaq, akaondoka kwenda Baytul Maqdis, uliokuwako nchini Jordan (Palestina ya siku hizi mjini Yerusalem) ambao vile vile huitwa Masjidul Aqsaa. Baada ya muda mfupi tu alishuka pale na kuzitembelea sehemu mbalimbali za msikiti ule na pia aliutembelea mji wa Bethlehemu ulio mahali alipozaliwa Nabii Isa (a.s.) na vile vile alizizuru sehemu mbalimbali zihusikanazo na Mitume mbalimbali. Katika baadhi ya sehemu hizi vile vile alisali rakaa mbilimbili.

Baada ya hapo aliendelea na sehemu ya pili ya safari yake na kutoka pale alipaa mbinguni. Hapo sasa akaziona nyota na utaratibu wa ulimwengu na akazungumza na nafsi za Mitume waliotangulia na vile vile alizungumza na Malaika wa mbinguni. Aliviona vituo vya mibaraka na mateso (Pepo na Moto) na akayaona makazi ya watu wa Motoni na wa Peponi1 kwa karibu zaidi, na hivyo akawa na utambuzi wa siri za maumbile, ukubwa wa ulimwengu na ishara za Allah, Mwenye nguvu zote. Kisha aliendelea na safari yake na akafika kwenye Sidratul-Muntaha2 na kuuona ukiwa umefunikwa kabisa na uzuri, utukufu na ukuu. Hapa, safari yake ikakoma na akarejea kwa njia ileile aliyoendea. Wakati safari yake ya kurejea, vile vile alifika pale Baytul Maqdis kwanza na kisha akaja Makkah.

Akiwa njiani aliukuta msafara wa kibiashara wa Waquraish uliopoteza ngamia na uliokuwa ukimtafuta. Alikunywa maji kutoka kwenye chombo chao na akayamwaga yale yaliobakia ardhini, na kwa mujibu wa wasimulizi wengine, akaweka kizibo juu yake. Huu ulikuwa ni muda kabla ya alfajiri alipofika nyumbani kwa Ummi Haani na akashuka kutoka kwenye yule mnyama aliyempaza mbinguni. Bibi huyu alikuwa mtu wa kwanza aliyesimuliwa na Mtume (s.a.w.w.) jambo hili na vile vile siku iliy- ofuatia usiku ule alilisimulia jambo hili kwenye mkutano wa Waquraishi. Hadith ya ‘kupaa’ kwake na safari yake kuu, vitu vilivyosadikiwa na Waquraishi kwamba ni vitu visivyowezekana kabisa ilienea kutoka kinywa hadi kinywa kwenye vituo vyote na ikawatatanisha zaidi machifu wa Waquraish.

Kulingana na desturi zao za tangu kale, Waquraishi waliamua kumpinga na wakasema: “Hata hivi sasa wako watu humu mjini Makkah walioiona Baytul Maqdis. Kama hayo uyasemayo ni kweli basi hebu tueleze lilivyo jengo hilo.” Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) hakuielezea tu jengo lile lilivyo, bali alieleza pia yaliyotokea baina ya Makkah na Baytul Maqdis na akase- ma: “Nilipokuwa njiani nilikutana na msafara wa kabila hili, uliokuwa umempoteza ngamia wao. Walikuwa na chombo kilichojazwa maji amba- cho kilikuwa sehemu ya masurufu yao. Nilikunywa maji kutoka kwenye chombo hiki na kisha nikakiziba.3 Kwenye sehemu nyingine nilikikuta kikundi cha watu wenye ngamia aliyewakimbia na alikuwa amevunjika mguu.”
Wale Waquraishi wakasema: “Hebu tuelezee juu ya ule msafara wa Waquraishi.” Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akawajibu akisema: “Niliwaona mahali paitwapo Tan’im (hii ni sehemu inapoanzia ‘Haram’ au mipaka mitakatifu ya mji wa Makkah).

Msafara wao uliongozwa na ngamia mwenye rangi ya kahawia nao walimwekea kitundu (cha kubebea watu juu ya mnyama) na hivi sasa wanaingia Makkah.” Wale Waquraishi wali- sisimuliwa mno na taarifa hizi za uhakika na wakasema: “Tutautambua ukweli au uongo wako sasa hivi.” Hata hivyo, haikuchukua muda mrefu kabla ya Abu Sufyani, kiongozi wa msafara ule kutokea na watu wakamweleza kwa kirefu yale aliyoyasema Mtume (s.a.w.w.). Maelezo yaliyopo hapo juu ni kiini cha yale yaliyoelezwa kwenye vitabu vya tafsiri ya Qur’anii tukufu na Hadith.4

Je, Mi’iraaj Ina Asili Ya Qur’anii?

Tukio la Mi’iraaj ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kwenda mbinguni imeta- jwa waziwazi kwenye Sura mbili za Qur’anii tukufu. Hapa chini tunatoa kwa kifupi aya zinazoitaja waziwazi Mi’iraaj.

Mwenye Surat al-Israa inasemwa hivi: “Utukufu wote wamstahiki Yeye Yule aliyempeleka mja wake wakati wa usiku kutoka Masjidul-Haraam hadi Masjidul-Aqsaa ambao tumevibariki vilivyoko pembezoni mwake, ili tumwonyeshe baadhi ya Ishara Zetu; hakika Yeye (Allah) Yu Asikiaye, Aonaye.” (Surat al-Israa 17:1).

Kwa uwazi kabisa aya hii inayataja mambo yafuatayo:-

1. Ili kutuambia ya kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alisafiri kuzipita dunia hizi kwenye kipindi tu, si kwa nguvu ya kibinadamu bali ni kwa kupitia nguvu ya ki-Ungu. Allah Mwenye nguvu zote anaianza kauli Yake kwa maneno: “Utukufu wote wamstahiki Yeye, yenye kuuonyesha ukweli ya kwamba Allah Yu safi kutokana na kila aina ya upungufu na mahitaji. Vile vile hakutosheka na hayo bali vile vile amejieleza kuwa Yeye ndiye chanzo cha safari ile kwa kusema: ‘Asra’ (Allah Amemwezesha kuifanya safari ile). Alijaalia upendeleo huu juu yake ili kwamba watu wasidhanie ya kwamba safari ile ilifanyika kwa mujibu wa kanuni za kimaumbile na kwa njia za nguvu ya kawaida, na hivyo wakaweza kuukataa uwezekano wake. Hivyo basi, imedhihirishwa ya kwamba ilifanyika kwa mapenzi ya Allah na kwa upendeleo maalumu wa Allah, Mwenyezi.

3. Safari hii ilifanyika wakati wa usiku.

4. Licha ya ukweli kwamba safari hii ilianzia nyumbani mwa Bibi Ummi Haani, binti wa Bwana Abu Twalib, Allah Mwenyezi ameitaja sehemu ya kuanzia kwa safari hii kuwa ni Masjidul-Haram, ni kwa sababu ya ukweli uliopo kwamba Waarabu wanaufikiria mji mzima kuwa ni Nyumba ya Allah, na kwa sababu hiyo, sehemu zake zote zinachukuliwa kuwa ‘Masjid’ na ‘Haraam.’

5. Hivyo, kauli ya Allah kwamba “Alimfanya asafiri kutoka Masjidul- Haraam” ni sahihi kabisa. Hata hivyo, kufuatana na baadhi ya masimulizi, safari hii ilianzia kwenye Masjidul-Haraam yenyewe.

6. Ingawa Aya hii inaitaja sehemu ya kuanzia kwa safari hii kuwa ni

7. ‘Masjidul-Haraam’ na mwishilizo wake kuwa ni ‘Masjidul-Aqsaa’ hakuna lolote ndani yake liwezalo kutoafikiana na Mtume (s.a.w.w.) kuifanya safari nyingine ya kwenda mbinguni, kwa sababu aya hii inaitaja sehemu moja tu ya safari hii na aya za Suratun-Najm zinazungumzia juu ya ile sehemu nyingine ya taarifa za safari ile.

5. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) aliifanya safari ile kwa mwili na roho yake pamoja, na wala si kwa roho tu. Maneno ‘mja wake’ yanatoa ushahidi wa jambo hili, kwa sababu neno ‘mja’ lina maana ya ‘mwili na roho’. Kama Mi’iraaj ingalifanyika kiroho tu, maneno sahihi kutumika yangalikuwa ‘roho ya mja wake.’

6. Lengo la hii safari kuu lilikuwa kumfahamisha Mtume (s.a.w.w.) hali mbalimbali za kuwako kwa Ulimwengu Mkuu. Hapo baadae tutalieleza zaidi jambo hili.

Sura nyingine inayolizungumzia tukio la Mi’iraaj waziwazi ni ‘Surah al- Najm’ na aya utakazozisoma hapa chini zilifunuliwa kuhusiana na jambo hili. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alipowaambia Waquraishi amemwona Malaika Mkuu Jibriil akiwa kwenye umbo la kimwili, pale alipouleta ufun- uo wa kwanza, walimpinga. Kuhusu upinzani wao, Qur’anii tukufu inajibu hivi:

أَفَتُمَارُونَهُ عَلَىٰ مَا يَرَىٰ {12}

وَلَقَدْ رَآهُ نَزْلَةً أُخْرَىٰ {13}

عِنْدَ سِدْرَةِ الْمُنْتَهَىٰ {14}

عِنْدَهَا جَنَّةُ الْمَأْوَىٰ {15}

إِذْ يَغْشَى السِّدْرَةَ مَا يَغْشَىٰ {16}

مَا زَاغَ الْبَصَرُ وَمَا طَغَىٰ {17}

لَقَدْ رَأَىٰ مِنْ آيَاتِ رَبِّهِ الْكُبْرَىٰ {18}

“Je, mnabishana naye juu ya yake aliyoyaona? Na bila shaka yeye amemuona (Jibril) kwa mara nyingine (katika sura ya malaika). Penye mkunazi wa mwisho (Sidratul-Muntaha). Karibu kuna pepo, iliyo makazi ya watu wema. wakati ule Mkunazi ulipofunikwa na chenye kufunika. Macho yake hayakuhangaika wala hayakugeuka, kwa hakika aliona baadhi ya Ishara za Mola wake zilizo kuu.”(Suratun-Najm, 53:12-18).

Taarifa Juu Ya Mi’iraaj

Wafasiri wa Qur’anii tukufu na waandishi wa Hadith wamenukuu mambo mengi kuhusu Mi’iraji na aliyoyaona Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), lakini taarifa zote hizo si mwishilizio na zisizokanika. Mfasiri mkuu wa Kishi’ah na stadi, Marehemu Allamah Tabrasi amezigawa taarifa hizi katika makundi manne:

1. Kundi moja la taarifa hizi ni zile zikatazo shauri na zisizopingika, kwa mfano ule ukweli wa Mi’iraaj na baadhi ya mambo yake.

2. Taarifa zilizonukuliwa kwa jinsi iliyo sahihi lakini hazikuifikia hatua ya mwishilizio, ingawa zinaafikiana na misingi na hukmu ya hekima, kwa mfano, kule kuikagua Pepo na Jahannam, safari katika anga na kule kuzungumza na roho za Mitume (a.s.).

3. Taarifa ambazo kwamba si zenye kukubalika kwa dhahiri, lakini zina uwezo wa kutafsiriwa. Kwa mfano, yale mazungumzo ya Mtume (s.a.w.w.) kwenye ule usiku wa Mi’iraaj na wale wakazi wa Peponi na Motoni ambayo yaweza kuelezwa kwa kusema kwamba aliona mizuka, maumbo na sifa zao.

4. Taarifa zilizotiwa chumvi, zilizozushwa na kuenezwa na watu waongo. Kwa mfano, wakati mwingine inasemekana kwamba kwenye usiku ule Mtume (s.a.w.w.) alikaa pamoja na Allah Mwenye nguvu zote au kwamba aliisikia sauti ya kalamu yake.5

Historia Ya Tukio Hili

Ingawa ilikuwa inafaa kwamba hili tukio kuu lingeandikwa katika hali zote zile, bado, kwa sababu fulani fulani, zimetokea tofauti juu yake, na moja miongoni mwa tofauti hizo ni kuhusu tarehe ya kutokea kwake. Wanahistoria wawili wa kiislamu (ibn Ishaq na Ibn Hisham) wanasema kwamba tukio hili lilitokea mwaka wa kumi wa Utume wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Mwanahistoria maarufu Bayhaqi anaamini ya kwamba lilitokea mwaka wa kumi na mbili wa Utume wake.

Baadhi ya watu wanasema kwamba lilitokea siku za awali za Utume wake, ambapo wengine wanasema kwamba muda wa kutokea kwake ulikuwa ni kipindi cha katikati cha Utume. Na wakati mwingine, ili kuziunganisha kauli hizi, imesemekana kwamba Mi’iraaj ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) ilitokea zaidi ya mara moja. Hata hivyo, maoni yetu ni kwamba ile Mi’iraaj ambayo sala tano za kila siku zilifaradhishwa ilitokea baada ya kifo cha Bwana Abu Twalib kilichotokea kwenye mwaka wa kumi wa Utume wa Mtume (s.a.w.w.).

Tunahitimisha hivi, kwa sababu ni moja ya mambo ya kihistoria na kiaha- dithi yaliyothubutu kwamba wakati wa usiku wa Mi’iraji Mwenyezi Mungu aliamrisha ya kwamba ni wajibu kwa wafuasi wa Mtume (s.a.w.w.) kusali sala tano kila siku na vile vile inafahamika kutokana na historia kwamba sala hazikuwajibishwa hadi alipofariki dunia Bwana Abu Twalib, kwa sababu alipokuwa kwenye kitanda cha kufia kwake, machifu wa Waquraishi walimjia ili kumaliza ugomvi baina yao na mpwa wake na kumzuia aviache vitendo vyake na kuchukua chochote kile akipendacho kiwe ni malipo yake kwa ajili ya kufanya hivyo.

Mtume (s.a.w.w.) aliyekuwepo pale aliwahutubia Machifu wale akisema: “Sitaki chochote kile kutoka kwenu ila tu kwamba muthibitishe ya kwamba hakuna mungu ila Allah na kuacha kuyaabudu masanamu!”6

Aliyatamka maneno haya na katu hakuitaja Salaat (sala) au kanuni nyingine za Imani. Jambo hili lenyewe laonyesha kwamba hadi wakati ule sala ilikuwa bado haijafanywa wajibu, kwa kuwa, kama vinginevyo, kuamini tu pasi na matendo ya wajibu, kama vile sala kusingalikuwa na faida yoyote. Na ama kuhusu lile jambo la kwamba hakutaja Utume wake, ni kwa sababu kuushuhudia upweke wa Allah kuna maana ya kuuthibitisha Utume wake moja kwa moja.

Zaidi ya hayo, vile vile wanahistoria wametaja kusilimu kwa watu kama vile Tufayl bin Amr Dosi kulikotokea mapema kidogo kabla ya kuhajiri (kwenda Madina). Wakati ule pia, Mtume (s.a.w.w.) alitosheka na kuwapa maelekezo ya kukubali upweke wa Allah na Utume wake yeye lakini hakuitaja ‘Sala.’ Matukio kama haya yaonyesha kwamba wakati wa kutokea kwa tukio hili ambalo kwalo sala ziliwajibishwa, ulikuwa ni muda mfupi tu kabla ya Hajiri.

Wale wanaofikiri kwamba Mi’iraaj ilitokea mapema kuliko mwaka wa kumi wa Utume wa Mtume (s.a.w.w.) wanakosea kabisa, kwa sababu tangu mwaka wa nane hadi wa kumi alikuwa kazingirwa kwenye ‘Bonde’ na ile hali ya kusikitisha ya Waislamu haikufaa kwamba watwishwe jukumu jingine kama vile ‘Swala.” Na ama kuhusu miaka ya kabla ya mwaka wa nane, tukiuachilia mbali ukweli uliopo kwamba shinikizo la Waquraishi lilikuwa kali mno kwa Waislamu kiasi kwamba hawakuweza kuyahimili majukumu mengine, bado idadi yao pia ilikuwa ndogo mno!

Hivyo basi, kwa wakati kama huu ambao mwanga wa dini na kanuni zake havijaingia barabara nyoyoni mwa idadi ya watu iwezayo kutambulika, yaonekana haiyumkini kwamba jukumu lisilo la kawaida kama vile sala liwajibishwe juu yao.

Ama kuhusu kauli iliyotamkwa kwenye baadhi ya masimulizi kwamba Imam Ali, Amir wa Waumini alisali pamoja na Mtume (s.a.w.w.) kwa kipindi cha miaka mitatu kabla ya uteuzi wa Mtume (s.a.w.w.) kuishika kazi ya Utume na akaendelea nazo baada ya hapo, inaweza kusema kwamba hii ilikuwa na maana ya sala maalumu na zisizo na ukomo na si zile Sala zenye ukomo na masharti na muda maalumu.7 Vile vile inawezekana kwamba sala hizo zilikuwa zilizopendekezwa ‘Sunnah’ na zisizo za wajibu.

Je, Mi’iraji Ya Mtume Ilikuwa Ya Kimwili?

Hali ya Mi’iraj ya Mtume (s.a.w.w.) imekuwa jambo la kujadiliwa kwa kipindi kirefu na mengi yamesemwa kuhusu kuwa kwake ya kimwili au ya kiroho, ingawa Qur’anii tukufu na Ahadith vinaeleza waziwazi kwamba ilikuwa ya kimwili.8 Hata hivyo baadhi ya dhana za kisayansi zimewazuia kikundi cha watu kuukubali ukweli huu. Hatimae wamekimbilia kwenye tafsiri zao wenyewe na kuichukulia Mi’raji ya Mtume kuwa ya kiroho hasa na wamesema kwamba ni roho yake tu ndio iliyosafiri katika dunia hizi na kasha ikarudi kwenye ule mwili wake mtukufu.

Wengine wameendelea zaidi hatua moja na kusema kwamba matukio yote haya yalikuwa ni ndoto na Mtume aliona aliona sehemu mbalimbali na kusafiri kupitia humo ndani ya ndoto.

Kauli ya kundi la mwisho iko mbali zaidi na mantiki na hali halisi kiasi kwamba haistahili kufikiriwa hata kidogo kwamba ni sehemu ya Ahadith na maoni yahusianayo na Mi’iraaj. Sababu yake ni kwamba Waquraish waliposikia kwamba Muhammad amedai kwamba amesafiri na kufika sehemu zote hizi ndani ya usiku mmoja tu, hapo walipatwa na wasiwasi mno na wakaamka kwa dhati kabisa kumwita mwongo, kiasi kwamba Miiraaj yake ikawa jambo lenye kujadiliwa kwenye mikusanyiko yote ya Waquraishi. Kama kule kusafiri kwake kwenye dunia hizi kungalikuwa kwa ndoto tu, kusingalikuwapo haja yoyote kwa upande wa Waquraishi kuamka na kumkanusha na kusababisha ghasia zote zile.

Hii ni kwa sababu, kama mtu akisema kwamba kwenye usiku mmoja, alipokuwa amelala, ameota hili na lile, haiwezi kuwa hoja ya malumbano, na ugomvi kwa kuwa ndoto ni ndoto tu na mambo mengi yasiyowezekana yaweza kuonekana kwenye ndoto. Hivyo basi, kwa sababu hii, maoni haya hayastahili kuchunguzwa zaidi. Hata hivyo, kwa bahati mbaya baadhi ya wanachuoni wa Kimisri kama vile Farid Wajdi wamelichukua wazo hili na kuliunga mkono kwa kauli zisizo na msingi. Hata hivyo, ingawa yamekuwako yote hayo, inafaa kuitupilia mbali.

Je, Ilikuwa Mi’iraaj Ya Kiroho?

Wale watu walioshindwa kutatua masuala madogo yahusianayo na Mi’iraaj ya kimwili wamelazimika kukimbilia kwenye tafsiri na wameichukulia Mi’iraj ya Mtume (s.a.w.w.) kuwa ilikuwa ni ya kiroho.

Mi’iraaj ya kiroho ina maana ya kutafakari juu ya vitu vilivyoumbwa na Allah Mwenyezi na kuuchunguza Utukufu na Uzuri wake na kuzama kwenye fikara juu Yake na kulisabihi jina lake na hatimaye ukapatikana uhuru kutokana na vipingamizi vya kimaada na faida za kidunia na kupitia kwenye kila uwezekano na kuingia kwenye hatua za ndani na zisizo za kimaada. Na baada ya kuupitia mpango wote huu, ukapatikana ukaribu zaidi na Allah, na haiwezekani kuieleza zaidi.

Kama Mi’iraaj ya kiroho ina maana ya kutafakari juu ya Utukufu wa Allah Mwenyezi, na kadiri ya maumbile, bila shaka Mi’iraaj ya aina hii si maalu- mu kwa Mtume wa uislam kwani Mitume (a.s.), na watu wengi walioangaziwa na wenye nyoyo safi nao wamekifikia cheo hiki, ambapo Qur’anii tukufu inaitaja Mi’iraaj yake kuwa ni jambo maalumu kwake na daraja la kipekee kwake.

Zaidi ya hapo, Mtume (s.a.w.w.) alikuwa kwenye hali tulioyoitaja hapo juu kwenye masiku mengi sana9 ambapo Mi’iraaj imethibitika kuhusika na usiku maalumu.

Jambo lililowalazimisha watu hawa kuwa na maoni tuliyoyataja hapo juu (ya kwamba Mi’iraaj ilikuwa ya kiroho tu) ni ile dhana ya yule mnajimu maarufu wa Kigiriki aitwaye Ptolemy, dhana iliyojipatia thamani kubwa kwenye duru za wanasayansi wa nchi za Mashariki na za Magharibi kwa kipindi cha miaka elfu mbili, na mamia ya vitabu yaliandikwa juu yake, na hadi kwenye miaka ya hivi karibuni, dhana hii ilichukuliwa kuwa ni moja ya kanuni zilizothibitishwa za sayansi za kimaumbile. Inaweza kuhitimishwa kama hivi:

Hapa ulimwenguni kuna aina mbili za vitu, vitu vya kimaada na vya kimbinguni. Vitu vya kimaada vina vitu vinne maarufu (maji, ardhi, hewa na moto).

Tufe la kwanza tulionalo ni tufe la dunia ambalo ndio kitovu cha ulimwengu. Kisha huja maeneo ya maji, hewa na moto na kila moja kati yao hulizunguka jingine. Matufe hayo huishia hapo na yale maumbile ya kimbinguni huanza. Maana ya maumbile ya kimbinguni ni zile anga tisa ambazo zimeungana na kila mojawapo nyingine kama matabaka ya kitun- guu na katu havina uwezo wa kupasua na kupatanisha na kutenganisha na kuungana na hakuna kiumbe awezaye kutembea moja kwa moja kupitia vitu hivi, kwa sababu hilo litalazimisha mtengano wa sehemu za mbingu, moja kutokana na nyingine.

Mi’iraaj ya Mtume (s.a.w.w.) kuwa ni ya kimwili, inalazimu kwamba apae kutoka kwenye kitovu cha ulimwengu kwa mstari ulionyooka na ayapite yale matufe manne na vile vile azipasue mbingu moja baada ya nyingine na kule kupasua na kuzipatanisha zile mbingu hakuwezekani na hakutekelezeki kulingana na elimu ya unajimu ya Kigiriki, wanafikara tuliowataja hapo juu wamelazimika kuichukulia Mi’iraaj ya Mtume (s.a.w.w.) kuwa ya Kiroho tu, kwa vile hakuwa mtu awezaye kuizuia roho kuifanya safari.

Jibu La Ukosoaji Huo Hapo Juu

Kauli hizi zilikuwa na thamani siku zile wakati elimu ya unajimu ya Ptolemy ilipokuwa bado haijapoteza thamani yake kwenye nyanja ya kisayansi na baadhi ya watu waliipenda kwa kweli na wakaielekea. Katika hali kama hii iliwezekana kwamba tungeweza kucheza na utatanishi wa Qur’anii na tungezifasiri aya za Qur’anii za waziwazi pamoja na Ahadith. Hata hivyo, dhana hizi zimezipoteza thamani zao zenye kuenea na kutokuwa kwao na msingi kumedhihirika. Ni katika baadhi ya nyakati tu kwamba unatajwa unajimu wa Ptolemy kuhusiana na historia ya sayansi.

Zaidi ya hapo, kutokana na ugunduzi wa zana mbalimbali za kinajimu na darubini zenye nguvu na kushuka kwa ‘Apollo’ na ‘Luna’ kwenye uso wa mwezi, Venus (ng’andu) na Mars na safari za wanaanga kwenye mwezi havikuacha nafasi yoyote kwa dhana hizi za kufikiria tu. Siku hizi wanasayansi huchukulia kuwako kwa zile tufe za kimaada na zile anga tisa zenye kuhusiana zenyewe kwa zenyewe kuwa ni ngano na hawajafaulu kuviona, kwa msaada wa zana za kisayansi na kinajimu na macho yaliyoandalliwa vizuri, zile dunia alizojenga Ptolemy na udhanifu wake na wanalichukulia kila wazo lililosimamia kwenye nadharia potofu za Plotemy kuwa zisizo na thamani.

Wimbo Usio Na Mahadhi

Kiongozi wa madhehebu ya Shaykhiyah (Shaykh Ahmad Ehsaai) ameim- ba wimbo mwingine kwenye jarida liitwalo ‘Qatifiyah’ na amejaribu kuyatosheleza makundi yote mawili kwa namna mpya.
Yeye anasema kwamba Mtume (s.a.w.w.) alikwenda Mi’raaj kwa njia ya barzakhi10 (mwili wenye nguvu za ajabu). Kwa mujibu wa fikira zake mwenyewe, kwa njia hii atakuwa amewatosheleza wale waaminio Mi’iraaj ya kimwili kwa vile amekubali kwamba Mi’iraaj imefanyika pamoja na mwili na vile vile atakuwa ameliondoa lile tatizo lihusianalo na mbingu au anga, kwa sababu, ilikuweza kupenya kwenye zile anga, si lazima kwa mwili wa ‘Kibarzakhi’ kuzipasua anga zile.11

Ingawa watu walioelimika, wenye kuutafuta ukweli na wasio na upendeleo huyachukulia maoni haya nayo kuwa si yenye thamani yoyote na yaliyo kinyume na Qur’anii tukufu na maelezo ya Ahadith yaliyodhihiri, kama vile yalivyo maoni ya awali

(yale ya kwamba Mi’iraaj ilikuwa ya Kiroho) kwa sababu, kama tulivyokwisha kusema, unapoiweka ile aya ya Qur’anii ihusianayo na Mi’iraj mbele ya mtaalamu wa lugha (ya kiarabu) atasema kwamba yule mzungumzaji ana maana ya mwili wa ulimwengu wa kimaada ambao kwamba neno ‘abd’ (mja) limetumika kwenye Qur’anii tukufu na wala si neno ‘herculian,’ (enye nguvu za ajabu) kwa sababu jamii ya kiarabu ilikuwa haina ufahamu wa neno hili wala maneno yafananayo na neno hili, na kwenye Surah al-Israa ni vikundi vya kawaida na watu binafsi waliozungumzishwa.

Sasa jambo lililomfanya kujichukulia hii tafsiri ya kulazimisha ni ileile ngano ya Kigiriki juu ya mpango wa maumbile ambayo, kwa mujibu wake, ngano hii ni yenye madhubuti kama vile ‘Lawh-i Mahfudh’ (ubao uliohiofadhiwa). Lakini hivi sasa kwa vile wanasayansi wote wanalikataa wazo hili haifai hata kidogo kwamba tuendelee kulifuata kama vipofu.

Kama wanachuoni wa kale wametoa kauli fulani kutokana na kuwa kwao na matarajio juu unajimu wa kizamani wanaweza kusamehewa na kwamba sio wa kulaumiwa sana, lakini si sahihi kwetu, kwenye nyakati hizi za siku hizi, kuzikataa hali halisi za Qur’anii kwa sababu ya dhana zilizokataliwa na kundi la wanasayansi.

Mi’iraaj Na Kanuni Za Kisayansi Za Kisasa

Baadhi ya wale waipendeleao sayansi ya kimaumbile wenye shauku ya kuweka chanzo asilia kwa kila tukio na kiwakilishi cha kimaada kwa kila jambo, wamechagua kuukana ule msingi wenyewe hasa wa Mi’iraaj na wanafikiria ya kwamba kanuni za kisasa za kimaumbile na za kisayansi hazithibitishi Mi’iraaj ya Mtume (s.a.w.w.). Kwa mfano, wanasema:

1. Sayansi ya kisasa inasema: ‘Ili kutoka humu duniani ni lazima kuitan- gua nguvu yake ya mvutano. Kama ukiurusha mpira hewani, nguvu ya mvutano huurudisha ardhini. Kwa kadiri nguvu yoyote ile uitumiayo, nao utarudi tena ardhini. Kama ukitaka kuitangua kabisa nguvu ya mvutano, ili ule mpira uendelee kwenda na usirudi ardhini, itakulazimu kuutupa kwa kasi isiyopungua kilomita 40,000 (au maili 25,000) kwa saa.

Hivyo basi, Mtume (s.a.w.w.) aliutoka ukanda wa nguvu ya mvutano na akakosa uzito. Lakini hapa huibuka swali la, vipi aliweza kuifanya safari ile kwa kasi hii bila ya nyenzo muhimu?

2. Hali ya hewa ambamo mtu anaweza kupumua haipatikani nje kidogo ya kilometa chache hivi kutoka ardhini. Baada ya hapo, kwa kadiri tunavyokwenda juu zaidi, hewa huwa nyepesi zaidi na kutokufaa zaidi kwa kupumua na mara moja moja tunafika mahali pasipo na hewa kabisa.

Mtume (s.a.w.w.) aliwezaje kuwa hai bila ya hewa ya Oksijeni alipokuwa akiifanya safari yake ile kwenye kanda tulizozitaja?

3. Miyonzi yenye kuua na mawe ya mbinguni huharibu kila mwili wa kidunia uguswao na vitu hivi. Hata hivyo, vitu hivi havifiki duniani kutokana na mgongano wao na zile kanda za hewa na kwa kweli kanda hizi huwa kama deraya kwa upande wa wakazi wa duniani. Kwenye hali hii, ni kwa njia ipi Mtume (s.a.w.w.) aliweza kusalia salama kutokana na hii miyonzi iuayo?

4. Maisha ya mwanadamu huharibikiwa wakati shinikizo la hewa liongezekapo au lipunguapo na mwanaadamu anaweza tu kuishi kwenye shinikizo maalumu la hewa ambalo halipatikani kwenye kanda za juu.

5. Kasi aliyoitumia Mtume (s.a.w.w.) wakati wa kuifanya safari yake ni dhahiri ilikuwa kubwa kuliko kasi ya mwanga. Mwanga husafiri kwa kasi ya kilomita 300,000 kwa sekunde na sayansi ya siku hizi imethibitisha kwamba hakuna mtu awezaye kwenda kwa kasi zaidi ya ile ya mwanga. Tukiizingatia kanuni hii ya kisayansi, vipi Mtume (s.a.w.w.) aliweza kuifanya safari yake kwa kasi iliyo kubwa kuliko ile ya mwanga na kisha akarudi akiwa salama na mwenye afya njema?

Jibu La Upingamizi Huo Hapo Juu

Tunapozinyoosha kanuni za kimaumbile hadi kukifikia kiwango hiki, idadi ya matatizo huuvuka mpaka wa hayo tuliyoyataja hapo juu. Hata hivyo, tunawauliza watu hawa lengo la kuzieleza hizi kanuni za kimaumbile. Je, wana maana ya kusema kwamba kusafiri kwenye ulimwengu wa juu hakuwezekani?

Katika kulijibu swali hili hatuna budi kusema kwamba kwa bahati nzuri utafiti wa kisayansi uliofanywa na wanajimu wa nchi za Mashariki na za Magharibi umelifanya jambo hili kuwa lenye kuwezekana na la kawaida, kwa sababu, kwa kupeleka kwao setalaiti ya kwanza ya kutengenezwa mnamo mwaka 1957, iliyopewa jina la ‘Sputnic,’ ilidhihirika ya kwamba ile nguvu ya mvutano inaweza kutanguka kwa kutumia roketi.

Halikadhalika, kwa kupeleka kwao vyombo vya angani vyenye kubeba wanajimu ‘astronatus’ kwa kutumia roketi ilidhihirika ya kwamba lile jambo ambalo hapo awali mwanaadamu alilifikiria kuwa ni kikwazo katika kusafiri kwake kwenda kwenye anga za juu kinaweza kuponywa kwa msaada wa sayansi na teknolojia, na, kwa hizi zana za kiviwanda na kisayansi alizonazo, mwanaadamu anaweza kutatua matatizo ya miyonzi yenye kuua na lile tatizo la ukosekanaji wa hewa awezayo kuivuta mtu. Na hata hivi sasa, sayansi zihusianazo na anga zimo kwenye hali ya kupanuka na wanasayansi wana uhakika kwamba baada ya muda fulani watafaulu kuendesha maisha yao kwenye moja ya matufe ya mbinguni na watasafiri kwa urahisi kwenda mwezini na kwenye Mars.12
Maendeleo haya kisayansi na ufundi yanaonyesha wazi ya kwamba kiten- do kama hiki kinawezekana kwa asilimia mia moja na si tu kilicho nje ya akili.

Inawezekana baadhi ya watu wakahoji kwamba safari ya aina hii haiwezi kufanyika bila ya vifaa vya kisayansi na kimashine, na kwa vile Mtume (s.a.w.w.) hakuwa na vifaa hivi kwenye ule usiku wa Mi’iraaj aliwezaje kusafiri kwenye malimwengu kama hayo bila ya vifaa hivi?

Jibu la kauli hii hujidhihirisha kutokana na mazungumzo tuliyoyataja hapo juu kuhusu miujiza ya Mitume (a.s.) na hasa kutokana na masimulizi marefu tuliyoyatoa hapo kabla juu ya matukio ya ule ‘Mwaka wa Ndovu’ na tukio la jeshi la Abrahah kuuawa kwa vikokoto vodogo, kwa kuwa ni ukweli uliothubutu kwamba vitu ambavyo watu wa kawaida huvitenda kwa zana na vifaa vya kisayansi, vinaweza kufanywa na Mitume (a.s.) kwa rehma za Allah, na bila ya njia za dhahiri na za nje.

Mtukufu Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) alikwenda Miiraaj kwa rehma za Allah Mwenyezi, Ambaye ulimwengu wote ni wake na ambaye ndiye Muumba wa huu mfumo wa ajabu.

Yeye ndiye Aliyeipa ardhi ule mvutano na ile miali ya ulimwengu mzima kwenye jua, na ameumba matabaka tofauti tofauti kwenye angahewa. Naye Anaweza kuvirudisha Kwake vitu hivi na kuvitawala wakati wowote ule Apendapo.

Inapokuwa kwamba mpango wa hii safari ya kihistoria ya Mtume (s.a.w.w.) ulifanyika kwa amri ya Allah, kanuni zote hizi hunyenyekea kabisa kwenye Utashi Wake Allah usiokanika na ziko kwenye mikono ya nguvu Zake kwa kila wakati.

Katika hali hiyo ni ugumu gani uwezao kuwapo iwapo kama yule Mola Aliyeipa ardhi nguvu ya mvutano na ile miali ya dunia nzima kwenye maumbo ya angani anataka amtoe mja wake mteule nje ya kile kitovu cha nguvu ya mvutano kwa uwezo Wake usizo kikomo na bila ya njia yoyote ya dhahiri? Bila shaka, Allah Aliyeumba oksijeni anaweza kuiumba hewa kwa ajili ya Mtume wake mteule kwenye yale maeneo ambamo hewa haipatikani.

Ufanisi wa muujiza kimsingi ni tofauti na ule wa visababisho vya asili na nguvu ya mwanadamu. Hatupaswi kufikiria nguvu ya Allah kuwa ni yenye kikomo kama ilivyo nguvu yetu wenyewe. Kama sisi hatuwezi kuifanya kazi fulani bila ya zana tusiseme kwamba Allah mwenye nguvu zote nae vilevile hawezi kuifanya.

Tukizungumzia matatizo na utatuzi wake, kule kuwafufua wafu, kule kuibadili fimbo na kuwa chatu na kule kumweka hai Nabii Yunus (a.s.) tumboni mwa samaki kwenye kina kirefu cha bahari, ambayo ni matukio yaliyothibitishwa na Vitabu vya Mbinguni na yaliyosimuliwa kwa ajili yetu, hayako tofauti na Mi’iraaj ya Mtume wa Uislam (s.a.w.w.).

Kifupi ni kwamba, visababisho vyote vya kimaumbile na zana za nje na za dhahiri zinadhibitiwa na kushindwa na Utashi ya Allah. Mapenzi Yake hayahusiki na kile kisicho wezekana tu, bali zaidi ya hicho Yeye anaweza kukifanya chochote kile akipendacho, iwe mwanaadamu anayo nguvu ya kukifanya au la.

Bila shaka hapa tunazungumza na wale watu wamtambuao Allah kwa Sifa na tabia zisizo kifani na wale waaminio kwamba Yu Muweza wa yote na anaweza kufanya chochote kile akipendacho.

Lengo La Mi’iraaj

Mtu mmoja alimuuliza Imam wetu wa nne Ali Zaynul Abidiin (a.s.): “Je, iko sehemu maalumu kwa ajili ya Allah?” Imam (a.s.) alijibu akisema: “Hapana.” Yule mtu akasema: “Basi ni kwa nini alimfanya Mtume Wake (s.a.w.w.) asafiri kuzipita mbingu?” Imam (a.s.) alimjibu akisema: “Alimpaisha ili aweze kuutambua upana wa Ulimwengu na kuviona na kuvisikia vitu vya ajabu, ambavyo mifano yao haikupata kuonekana au kusikika na masikio au macho hapo kabla yake.”

Bila shaka ni muhimu kwamba huyu Mtume wa mwisho (s.a.w.w.) awe na nafasi ambayo aweza kutegemea ufahamu wake mpana zaidi na awe na uwezo wa kupeleka ujumbe kwa watu wa karne ya ishirini, ambao bado wanafikiria kusafiri kwenda mwezini na kwenye Mars, kwamba alikitenda kitendo hiki bila ya zana yoyote na kwamba Muumba wake alikuwa Yu mpole kwake na amemfanya autambue kwa ukamilifu utaratibu wa maumbile yote.

 • 1. Majma’ul Bayaan, Surah Bani Isra’il, 17:1, Juzuu 3, uk. 395.
 • 2. Kwa kuielewa zaidi maana ya ‘Sidratul Muntaha’, rejea kwenye vitabu vya Tafsiri.
 • 3. Baadhi ya wasimuliaji wamenukuu hivi: “Nikamwaga yale yaliobakia.” Yawezekana kwamba tofauti iliyopo baina ya masimulizi haya mawili yatokana na kile kitendo kurudiwa tena.
 • 4. Kwa taarifa kamili, tunawashauri wasomaji wetu wazisome Sura zizungumzi- azo juu ya ‘Mi’iraj’ (kupaa) za Bihaarul Anwaar, Juzuu 18, uk. 282-410 na za Tafsir-i Burhaan, Juzuu 2, uk. 390-404.
 • 5. Majma’ul Bayaan, Juzuu3, uk. 395.
 • 6. Siirah-i Ibn Hisham, Juzuu 2, uk. 27
 • 7. Kwa taarifa zaidi kuhusu lini Wudhu, Sala, na Adhana vilifaradhidhwa rejea ‘Furu-i Kaafi’ Juzuu 1, uk. 135.
 • 8. Mwanasheria mkuu wa Kishi’ah, marehemu Tabrasi, amesema kwenye Tafsir- i Majma’ul Bayaan kwamba wanachuoni wa Kishi’ah wote wanakubaliana kwam- ba Mi’iraaj ilikuwa ya kimwili, Juzuu 3, uk. 395.
 • 9. Wasa’il, Kitabu cha Funga (saumu), Sura ya ‘Kuharimisha Funga.’
 • 10. Mwili wa Ki-barzakhi ni kama ule mwili ambao kwawo, mwanaadamu huya- tenda matendo yote awapo mwenye ndoto.
 • 11. Jarida liitwalo 'Qatifiyah' ni moja ya majarida yake 92 yaliyochapishwa kwa pamoja kwenye mwaka 1273 kwa jina la 'Jawaami'ul Kalim.' Maneno ya maelezo yake ni kama haya yafuatayo: "Kwenye tukio la kupaa kwa kadiri mwili upaavyo juu ndivyo unavyoviacha vile vitu vya kimaada vilivyoungana na kila moja ya yale matufe kwenye sehemu ile ile yenyewe na kusoga mbele. Kwa mfano, unaiacha ile maada ya hewa kwenye lile tufe la hewa na ile ya moto kwenye tufe la moto. Na kwenye wakati wa kurudi unajitwalia vile vyote ulivyoviacha."

  Hivyo basi, kwenye ule wakati wa Mi'iraaj, Mtume (s.a.w.w.) aliiacha kila moja ya zile elementi nne za mwili wake (hapo kale elementi za msingi zilifikiriwa kuwa ni nne) kwenye yale matufe yao husika na akaenda Mi'iraaj kwa mwili usiokuwa na elementi hizi. Mwili kama huo hauwezi kuwa mwili wa kimaada na hauwezi kuwa chochote kile zaidi ya 'barzakhi' (kwa mujibu wa istilahi yake 'mwili wa her- culian' - wenye nguvu za ajabu). Kwenye kitabu kiitwacho 'Sharh-i Ziarat' uk. 28-29. Sheikh huyu anasema kwamba zile anga tisa hazina uwezo wa kupasuka wala wa kujipatanisha.

 • 12. Baada ya miezi bandia ya kutengeneza kupelekwa angani, Mrusi mmoja mwenye umri wa miaka ishirini na saba aliyeitwa Major Gagarin kwanza aliianza safari yake ya kwenda angani mnamo siku ya Jumatano tarehe 12 April, 1961 ndani ya chombo cha anga. Yeye alikuwa mtu wa kwanza kufanya safari ya aina hii. Kile chombo chake cha anga kilipaa kilometa 302 juu ya ardhi na akasafiri kwa kuizunguka dunia kwa muda wa saa moja na dakika thelathini. Baada ya hapo vyombo vya angani vilipelekwa angani na Wamarikani pamoja na Umoja wa nchi za Kisovieti za Urusi. Hatimaye Apolo - 12 na abiria wake wote walitua mwezini na ilikuwa ni mara ya kwanza mwanaadamu anaubandika mguu wake juu yake.

  Mpango huu umekuwa ukifanyiwa majaribio mara kadhaa baada ya hapo na kwa kawaida yamekuwa yakifanikiwa. Shughuli zote hizi zinadhihirisha ya kwamba kutua kwa mwanaadamu usoni mwa matufe hayo kunawezekana. Na kitu aki- fanyacho mwanadamu kwa hizi njia za kisayansi kinafanywa na Muumba wake kwa njia ya Utashi Wake Mkuu.