Sura Ya 23: Safari Ya Kwenda Taif

Mwaka wa kumi tangu kuanza kwa Utume ukamalizika kwa matukio yake yote, mazuri na mabaya. Kwenye mwaka huu Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) aliwapoteza watetezi na wafuasi wake wakuu wawili. Kwanza kabisa yule chifu wa familia ya Abdul-Muttalib, mtetezi maarufu wa Mtume (s.a.w.w.) na mtu mashuhuri zaidi miongoni mwa Waquraishi – yaani Bwana Abu Twalib alifariki dunia. Ilikuwa bado maumivu ya msiba huu yangalimo moyoni mwa Mtume (s.a.w.w.) wakati kifo cha mpenzi mkewe Bibi Khadija1 kiliongezea ukali wa maumivu yake. Bwana Abu Twalib alikuwa mlinzi wa uhai na heshima ya Mtume (s.a.w.w.) na Bibi Khadija aliuhudumia Uislamu kwa utajiri wake mkubwa.

Tangu mwanzoni mwa mwaka wa kumi na moja wa Utume wa Mtume (s.a.w.w.), Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alikuwa akiutumia muda wake kwenye mazingira yaliyojaa uadui na mfundo dhidi yake. Uhai wake ulikuwa kwenye hatari endelevu na alinyimwa uwezo wote wa kuubalighisha Uislamu.

Ibn Hisham anaandika2 kuwa siku chache tu baada ya kifo cha Bwana Abu Twalib Quraishi mmoja alimwagia vumbi Mtume (s.a.w.w.) kichwani mwake na akaingia nyumbani mwake akiwa kwenye hali ile. Macho ya mmoja wa mabinti zake yaliangukia kwenye hali ile ya kusikitisha. Binti yule3 akilia kwa sauti kuu na huku machozi yakitiririka kutoka machoni mwake, aliamka akaleta maji na kukiosha kichwa na uso wa baba yake mpenzi. Mtume (s.a.w.w.) alimfajiri binti yake yule na akasema: “Usilie. Allah ndiye Mlinzi wa baba yako.” Kisha akasema: “Abu Twalib alipokuwa hai Waquraishi hawakufaulu kutenda kitu chochote kibaya dhidhi yangu.”

Kutokana na hali chungu ya Makkah Mtume (s.a.w.w.) aliamua kwenda kwenye mazingira mengine. Katika zama zile mji wa Taa’if ulikuwa kituo kinachosisimua na kuvutia. Hivyo, aliamua kwenda huko akiwa peke yake na kuwasiliana na machifu wa kabila la Thaqif na kuwaita kwenye Uislamu, huenda akapata kufaulu kwa kuitumia njia hii. Baada ya kufika Taa’if alikutana na machifu na wazee wa kabila lile na akawaelezea dini ya kuabudu mungu mmoja, na akaomba msaada wao. Hata hivyo, maneno yake hayakuwa na athari zozote zile kwao na wakasema:

“Kama wewe ndiy yule mteule wa Allah itakuwa ni kuyakaribisha mateso kukukataa, na kama dai lako ni la uongo, basi haistahili kuzungumza nawe.”
Mtume (s.a.w.w.) alielewa kutokana na hoja yao hii dhaifu na ya kitoto kwamba walidhamiria kujiepusha naye. Hivyo, aliamka na kuchukua ahadi kutoka kwao ya kwamba wasiwaambie watu lolote lile lihusulo jambo lile, kwa sababu ingaliwezekana kwamba jamii ya watu wa daraja la chini na duni wa kabila la Thaif wangalilifanya jambo hili kuwa ni sababu ya kumdhuru na wangaliweza kutumia fursa ya kuwa kwake peke yake na mbali kutoka mjini kwao.

Hata hivyo, wazee wa kabila lile hawakuitimiza ahadi yao na wakawachochea wahuni na wajinga dhidi yake, mara kwa ghafla Mtume (s.a.w.w.) alijikuta akizingirwa na kundi la watu waliotaka kuzitumia njia zote kumsumbua. Hakuiona njia yoyote ile nyingine ila kukimbilia kwenye bustani moja iliyokuwa mali ya watu wawili waitwao ‘Atbah na Shibah’. Mtume (s.a.w.w.) aliingia bustani ile kwa taabu sana na hapo wale watu wakaacha kumfukuza. ‘Atbah na Shibah walikuwa ni Waquraishi matajiri ambao pia walikuwa na bustani mjini Taif.

Mtume (s.a.w.w.) alipoingia bustani ile jasho lilikuwa likimmiminika kutoka kichwani usoni, na baadhi ya viungo vya mwili wake mtakatifu navyo vilikuwa vimejeruhiwa. Bila ya kupenda alikaa chini ya mzabibu uliopandishwa kwenye kichanja na akaomba dua ifuatayo: “Ewe Mola wangu! Ninauweka unyonge na utovu wangu wa nguvu mbele Yako. Wewe ndiye Mtunzaji Mwenye huruma. Wewe Msaidizi wa wanyonge. Unaniacha kwenye hifadhi ya nani?”

Hii na dua nyingi nyinginezo tulizozinukuu kwa ufupi, huzivutia mno nyoyo, kwa kuwa ni dua za mtu aliyeitumia miaka hamsini ya uhai wake kwa heshima kuu na utukufu akiwa chini ya ulinzi wa wafuasi waliojitolea mhanga, lakini sasa hali yake imebadilika mno kiasi kwamba imembidi kukimbilia kwenye bustani ya adui na anayasubiri majaaliwa yake huku mwili wake ukiwa umechoka na umejeruhiwa.

Wana wa Rabiyyah, ambao, ingawa walikuwa wenye kuabudu masanamu na maadui wa Uislamu walihuzunika sana walipoiona ile hali ya kusiki- tisha ya Mtume (s.a.w.w.). hivyo, wakamwamrisha mtumwa wao wa Kikristo aliyeitwa Adas, kumpelekea chombo kilichojazwa zabibu.

Adas alimpelekea Mtume (s.a.w.w.) zabibu zile na akaziweka mbele yake na akamtazama usoni mwake kwa kumkazia macho kidogo. Wakati ule lilitokea tukio lenye kuvutia. Yule mtumwa wa Kikristo aliona kwamba Mtume (s.a.w.w.) alipokuwa akizila zabibu zile, alianza kwa kusema: “Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehema, Rahim.” Yule mtumwa alishangaa sana kuyasikia hayo na akikivunja kimya kilichokuwapo pale akasema: “Watu wa Penisula hii (ya uarabuni) hawakuyazoea maneno haya na sikupata kumsikia mtu yeyote miongoni mwao akiyatamka. Watu wa sehemu hii huzianza kazi zao kwa majina ya ‘Laat na Uzza.”

Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alimuuliza kijana yule sehemu aliyozaliwa na dini yake. Yule kijana akajibu ya kwamba anatoka Naynawah na kwamba alikuwa Mkiristo. Hapo Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Unatoka mahali alipotoka yule mchamungu Yunus (Yona) mwana wa Mata (Mathew)?” Yule kijana akashangazwa zaidi kuyasikia haya na akauliza tena: “Ulimjuaje Yunus mwana wa Mata?” Mtume (s.a.w.w.) akamjibu akasema: “Ndugu yangu Yunus alikuwa yu Mtume wa Allah kama nilivyo.” Maneno ya Mtume (s.a.w.w.) yaliyozionesha dalili za ukweli yalijenga hisia za ajabu kwenye nafsi ya Adas na akavutiwa naye bila ya kupenda. Akasujudu, akaibusu mikono na miguu ya Mtume (s.a.w.w.) na akadhi- hirisha kuiamini dini yake. Baada ya hapo alimwacha na akawarudia wale wenye bustani ile.

Wale wana wa Rabiyyah walishangazwa mno kuyaona yale mapinduzi ya kiroho yaliyomtokea yule mtumwa wao wa Kikristo. Walimwuliza: “Ulizungumza nini na mgeni huyu na kwa nini ulionyesha unyenyekevu mwingi kiasi kile mbele yake?” yule mtumwa akasema: “Mtu huyu ambaye hivi sasa amekimbilia bustanini mwenu yu Sayyidi wa wanaadamu wote. Ameniambia mambo yafahamiwayo na Mitume tu, naye ndiye yule Nabii wa Ahadi hasa.” Wale wana wa Rabiyyah walichukizwa mno walipoyasikia maneno ya yule mtumwa. Hata hivyo, kwa ukarimu wao wakasema waziwazi: “Na asikugeuze mtu huyu kutoka kwenye dini yako ya awali. Na dini ya ‘Isa (Yesu Kristo) unayoifuata hivi sasa ni bora kuliko yake.”

Mtume (S.A.W.W.) Arudi Makkah

Ukali ambao kwawo watu wa Taa’if walimwindia Mtume (s.a.w.w.) ulimalizikia kwenye ile bustani ya wana wa Rabiyyah. Hata hivyo, sasa ilimbidi kurudi Makkah, na hata huku kurejea kwake hakukuwa huru kutokana na matatizo, kwa sababu, mlinzi wake pekee alikuwa ameshafariki dunia, hivyo ulikuwapo uwezekano wa kwamba wakati wa kuwasili kule Makkah angaliweza kukamatwa na kuuawa.

Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) aliamua kubakia kidogo mahali paitwapo Nakhlah (palipo baina ya Makkah na Taif) kwa siku chache hivi. Wazo lake lilikuwa ni kumtuma mtu kutoka hapo kwenda kwa mmoja wa machifu wa Waquraishi ili ampatie ulinzi na kisha aingie mjini mle alimozaliwa akiwa chini ya ulinzi wa mtu kama yule. Hata hivyo, pale Nakhlah hakumpata mtu yeyote wa kwenda Makkahh kwa niaba yake. Baadaye aliondoka Nakhlah na kwenda kwenye mlima Hira.

Huko alikutana na mwarabu wa kabila la Khazaa’i na akamwomba aende Makkah na akazungumze na Mut’am bin Adi aliyekuwa mmoja wa watu wa Makkah walio maarufu, kuhusiana na usalama wake (yeye Mtume s.a.w.w) yule mtu alikwenda Makkah na kuufikisha ujumbe wa Mtume (s.a.w.w.) kwa Mut’am. Ingawa Mut’am alikuwa mwenye kuyaabudu masanamu, alikubali ombi la Mtume (s.a.w.w.) na akasema: “Na aje Muhammad moja kwa moja nyumbani kwangu. Wanangu na mimi mwenyewe tutauhami uhai wake.” Mtume (s.a.w.w.) aliingia Makkah wakati wa usiku na akaenda moja kwa moja nyumbani kwa Mut’am na akalala humo usiku ule.

Asubuhi iliyofuatia Mut’am alimwambia Mtume (s.a.w.w.): “Hivyo hivi sasa uko chini ya ulinzi wangu itakuwa bora kwamba Waquraishi nao walijue jambao hili. Hivyo, kulitangaza jambo hili ni muhimu kwamba ufuatane nami hadi kwenye Masjidul-Haram.” Mtume (s.a.w.w.) alilikubali wazo hili na akajitayarisha kwenda huko. Mut’am aliwaamrisha wanawe washike silaha na wamzunguke Mtume (s.a.w.w.), kisha wakaingia msikitini mle. Kuwasili kwao Masjidul-Haraam kulivutia mno. Abu Sufyani aliyekuwa akimvizia Mtume (s.a.w.w.) kwa muda mrefu alikerwa mno kuyaona mandhari haya na akaliacha lile wazo la kumnyanyasa Mtume (s.a.w.w.). Mut’am na wanawe wakakaa chini na Mtume akaanza kufanya ibada ya ‘Tawaaf’. Baada ya kuifanya ibada hiyo aliondoka na kurudi nyumbani kwake.4

Muda mfupi baada ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kuondoka Makkah na kwenda Madina na mwanzoni mwa mwaka wa Hijiria, Mut’am alifariki dunia mjini Makkah. Taarifa za kifo chake zikafika Madina na Mtume (s.a.w.w.) alimkumbuka kwa wema wake. Mshairi wa kiislamu, Hassan bin Thabit alisoma beti fulani fulani kwa kuikumbuka huduma yake.

Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alimkumbuka mno Mut’am kwenye matukio mbalimbali kiasi kwamba baada ya vita vya Badr, Waquraishi walipokuwa wakirejea Makkah baada ya kupata hasara kubwa na kuiacha idadi ya watu waliotekwa na waislamu, Mtume (s.a.w.w.) alimkumbuka Mut’am na akasema: “Kama Mut’am angalikuwa hai akanitaka niwaachie mateka wote au niwatoe zawadi kumpa yeye nisingalilikataa ombi lake.”

Jambo Linalostahili Kuzingatiwa

Ile safari yenye kutaabisha ya kwenda Ta’if aliyoichukua Mtume (s.a.w.w.) inaudhihirisha umadhubuti na uvumilivu wake na ule ukweli uliopo kwamba katu hakuzisahau huduma alizozitoa Mut’am katika muda maalum, hutudhihirishia tabia zake tukufu na maadili ya hali ya juu. Hata hivyo, zaidi ya sifa hizi mbili za Mtume (s.a.w.w.) tunaweza kuona jinsi alivyokuwa na shukurani kwa huduma zenye thamani alizozipata kutoka kwa Bwana Abu Twalib. Mut’am alimsaidia Mtume (s.a.w.w.) kwa kipin- di cha masaa machache au siku chache hivi, lakini yule ami yake mtukufu alimhami kwenye kipindi chote cha uhai wake. Mut’am hakupata hata moja ya elfu ya taabu na mateso aliyoyapata Bwana Abu Twalib.
Na wakati Mtume (s.a.w.w.) alipokuwa tayari kuwaachia mateka wote wa Badri au kumpa zawadi Mut’am kwa ajili ya huduma alizozitoa, kwa masaaa machache, je Mtume (s.a.w.w.) angalifanya nini badala ya zile huduma ali- zozitoa yule kipenzi ami yake?

Ni muhimu kwamba, yule mtu aliyemsaidia Mtume (s.a.w.w.) kwa kipindi cha miaka arobaini na miwili kamili na akayahatarisha maisha yake mwenyewe kwenye kipindi cha miaka kumi ya mwisho, kwa ajili ya kumhami, bila shaka atakuwa yu mwenye kukistahili cheo kikubwa zaidi mbele ya Mtume Muhamad (s.a.w.w.) yule kiongozi wa wanaadamu. Na halafu basi, kuna tofauti ya dhahiri baina ya watu wawili hawa. Mut’am alikuwa mshirikina na mwenye kuabudu masanamu, ambapo Abu Twalib alichukuliwa kuwa mmoja wa watu mashuhuri wa ulimwengu wa kiisla- mu.

Hotuba Alizozitoa Kwenye Mitaa Maarufu Ya Biashara Ya Arabuni

Kwenye majira ya Hajj, Waarabu walikusanyika sehemu mbalimbali kama vile ‘Ukaz’, Majannah’ na ‘Dhil-Majaaz’. Washairi na wazungumzaji maarufu walikaa kwenye sehemu zilizoinuka na kuwaburudisha watu kwa beti na hotuba zao zenye kuelezea ushujaa, majisifu ya mtu na mapenzi. Mtume (s.a.w.w.) aliitumia fursa hii kama walivyofanya Mitume wa kale. Na kutokana na kuwa salama kutokana na kero za wenye kuabudu masana- mu kufuatia kuharamishwa kwa mapigano kwenye ile miezi mitakatifu, alipanda kwenye sehemu iliyoinuka, akawageukia watu na akawahutubia akisema:

“Ushuhudieni Upweke wa Allah ili mpate kuokoka. Kwa nguvu ya imani mnaweza kuudhibiti ulimwengu mzima, mnaweza kuwafanya watu wazitii amri zenu na mnaweza kujipatia nafasi Peponi kesho Akhera.”

Mualiko Kwa Viongozi Wa Makabila Wakati Wa Hajj

Wakati wa Hajj Mtume (s.a.w.w.) aliwasiliana na machifu wa Uarabuni na kuonana nao wote kwenye makazi yao husika ya muda na kuwafikishia ukweli wa dini yake. Nyakati fulani, pale Mtume (s.a.w.w.) alipokuwa aki- jishughulisha na kuzungumza na machifu hawa alitokea pale Abu Lahab na akasema: “Enyi watu! Msiyaamini yale ayasemayo, kwa sababu yeye anafanya kampeni dhidi ya dini ya jadi zenu na maneno yake hayana msingi.” Upinzani wa huyu ami yake Mtume (s.a.w.w.) ulizipunguza athari za hotuba zake miongoni mwa hawa viongozi wa makabila na wakaambiana: “Kama dini yake ni ya kweli na yenye faida, basi watu wa familia yake wasingalimpinga.”5

  • 1. Ibn Sa'ad anasema kwamba kifo cha Bibi Khadija kilitokea mwezi mmoja na siku tano baada ya kile cha Bwana Abu Twalib (Tabaqaat, Juzuu 1, uk. 106). Hata hivyo, wengine kama vile Ibn Athir, wanaamini ya kwamba alifariki kabla ya Bwana Abu Twalib (Tarikh-i Kamil, Juzuu 2, uk. 63).
  • 2. Siirah-i Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 25.
  • 3. Binti huyu ni Bi Fatimah Az-Zahra ambaye alikuwa kama mama yake mpend- wa kiasi kwamba Mtume akampa jina la "Ummu Abiha" yaani Mama wa baba yake. Ukizama ndani ya kina cha bahari ya historia sahihi, basi utachota mchango wake katika Uislamu na jinsi alivyomuhami baba yake kwa mapenzi yake kwa Allah. Na hatimaye utakunywa utukufu wa hali ya juu wa binti huyu - Mhariri.
  • 4. Tabaqaat Ibn Sa'ad , juzuu 1, uk. 210-212 na al- Bidaayah wan-Nihaayah, Juzuu 3, uk. 137.
  • 5. Tabaqaat Ibn Sa'ad, Juzuu 1, uk. 216 na Siirah-i Ibn Hisham, Juz. 1, uk. 422-442.