Sura Ya 24: Mapatano Ya ‘Aqabah

Katika nyakati zilizopita Waadiul Qura’ (bonde la Qura) lilikuwa ndio njia ya kibiashara itokayo Yemen kwenda Sham. Baada ya kupita pembeni mwa Makkah misafara ya kibiashara ya Yemen iliingia hili bonde refu, na pamoja nalo yalikuwapo maeneo ya kijani na yenye kupendeza, moja kati yao lilikuwa ni ule mji wa kale wa Yathrib, ambao baadae ulijulikana kwa jina la ‘Madinatur Rasul’ (Mji wa Rasuli). Makabila mawili maarufu yaliy- oitwa ‘Aws’ na Khazraji’ waliokuwa Waarabu wahamiaji kutoka Yemen (Qahtaani) walifanya makazi bondeni humu kwa vile makabila maarufu ya Wayahudi (ya Bani Qarayzah, Bani Nuzayr na Bani Qaynqaa) yaliyohamia kutoka upande wa kaskazini wa Penisula ya Uarabuni yalifanya maskani yao hapo pia.

Kila mwaka kikundi cha Waarabu wa Yathrib walikwenda Makkah kufanya ibada ya Hajj, na Mtume (s.a.w.w.) aliwasiliana nao. Mawasiliano haya yalitoa vitangulizi vya ‘kuhama’ na kuikusanyia nguvu iliyotawanyika ya Uislamu kwenye kituo hicho. Mengi ya mawasiliano haya hayakuwa yenye manufaa.

Hata hivyo, ingawa yalikuwako yote hayo, wale mahujaji watokao Yathrib, waliporudi makwao walitaja kule kutokea kwa Mtume mpya ikiwa ndio taarifa muhimu, na jambo hili liliwavutia watu wa eneo hili kwenye tukio hili kuu.

Hivyo basi, hapa chini tunataja baadhi ya mikutano hii iliyofanyika kwenye mwaka wa kumi na moja, kumi na mbili na kumi na tatu wa Utume wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Kwenye uchunguzi wa kina wa matukio haya, sababu ya kuhama kwa Mtume Kutoka Makkah kwenda Yathrib (Madina), na hatimaye kule kuikusanya nguvu ya Waislamu kwenye sehemu ile hudhihirika kabisa:

Pale wakati Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alitambua ya kwamba mtu maaru- fu kutoka miongoni mwa Waarabu amewasili mjini Makkah alikwenda kuonana naye upesi upesi na kumhubiria dini yake. Siku moja alisikia ya kwamba Sawayd bin Saamit amefika mjini Makkah. Alikutana naye upesi na akamweleza hali halisi kuhusu dini yake takatifu.

Suwayd akafikiria kwamba huenda kweli zile zilikuwa ni hekaya za Luqman ambazo yeye tayari aishakuwa nazo. Hata hivyo, Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Semi za Luqman ni nzuri, lakini yale aliyonifunulia Allah ni bora na matukufu zaidi kwa sababu ni taa ya mwongozo iangazayo kila mahali.

Baada ya hapo Mtume (s.a.w.w.) alimsomea aya fulani fulani za Qur’anii na akasilimu. Kisha akarejea Madina. Suwayd aliuawa na Khazraji kabla ya vita vya Bu’aath. Alifariki dunia akiwa anazitamka ‘Shahadatain’ (yaani kule kushuhuduia ya kwamba hakuna mungu ila Allah na Muhammad yu mja na Mtume wake).1

Kikundi cha watu wa kabila la Bani Aamir walikutana na Mtume (s.a.w.w.) na wakasema: “Tutauamini Utume wako kwa sharti la kwamba utatufanya kuwa makhalifa wako.” Mtume (s.a.w.w.) akawaambia: “Jambo hili lamhusu Allah, nami sina mamlaka yoyote kwenye jambo hili. Hapo wakakataa kusilimu na wakarejea kwa watu wa kabila lao wakisema kwamba hiyo ilikuwa na maana ya kwamba wao wapigane kwa ajili ya jambo lile na watu wengine waifaidi matunda yake.

Walipofika makwao walilizungumzia jambo hili kwa mmoja wa wazee wa kabila lao ambaye hakuweza kwenda Hija mwaka ule kutokana na udhaifu. Mzee yule aliyeelimika aliwalaumu na akasema: “Hii ndio ile nyota iangazayo iliyochomoza kutoka kwenye upeo wa ukweli halisi.”2

Anas bin Raafi’i alikuja Makkah pamoja na kikundi cha watu wa kabila la Abdul Ashhal na Ayaas bin Ma’aaz alikuwa pamoja nao. Lengo lao lilikuwa kuomba msaada wa kijeshi kutoka kwa Waquraishi ili wakapigane dhidi ya kabila la Khazraji. Mtume (s.a.w.w.) alijiunga na mkutano wao na akawahubiria dini yake na vile vile akawasomea aya za Qur’anii. Ayaas, aliyekuwa mtu shupavu, alisimama akasilimu na akasema: “Dini hii ni bora kuliko ule msaada wa Waquraishi mlioujia hapa.” (Ayaas alikuwa na maana ya kwamba uislamu ni uhakika wa ustawi wa kudumu kwa sababu unaung’oa mauaji na visababisho vyote vya uharibifu na udanganyifu).

Kusilimu kwa mtu huyu bila ya mwelekeo wa kiongozi wa kabila lile kulimkasirisha mno Anas. Ili kuizima ghadhabu yake alichota mchanga kwa mikono yake yote miwili, akaumwagia usoni mwa Ayaas, na kusema: “Nyamaza! Sisi tumekuja hapa kuomba msaada wa Waquraishi wala si Kusilimu.”

Hapo Mtume (s.a.w.w.) alisimama akaenda zake na baada ya hapo kikundi kile kilirejea Madina. Vita ya Bu’aath ilipiganwa baina ya Aws na Khazraji.

Ayaas aliyebaki imara kwenye imani yake hadi kwenye dakika ya mwisho ya uhai wake, aliauwa kwenye vita hivi.3

Vita Vya Bu’aath

Vita vya Bu’aath ni moja ya vita vya kihistoria vilivyopiganwa baina ya yale makabila mawili ya Aws na Khazraji. Bani Aws walishinda kweye vita hii na wakaichoma mitende ya maadui zao. Baada ya hapo, Abdullah bin Ubay aliyekuwa mmoja wa machifu wa Bani Khazraji hakushiriki kwenye vita hivi, na hivyo basi, makabila yote mawili yalimheshimu. Ilitokea kwamba zile pande zote mbili zilichoka kabisa na hivyo zikaelekea mno kwenye amani.

Makabila yote mawili yalishikilia kwamba Abdullah awe mtawala wao baada ya mapatano. Waliweza hata kumtayarishia taji ili aweze kulivaa kwenye wakati wa kutawaza kwake. Hata hivyo, mpango huu ulishindikana kutokana na mwelekeo wa kundi la kabila la Khazraji kwenye Uislamu. Na wakati ule Mtume (s.a.w.w.) alikutana na Wakhazraji sita mjini Makkah na wakaukubali mwito wake.

Maelezo Juu Ya Tukio Hili.

Kipindi cha Hija Mtume (s.a.w.w.) alikutana na watu sita wa kabila la Khazraji na akawauliza kama walifanya mapatano yoyote na Wayahudi. Walijibu, ndio. Hapo Mtume (s.a.w.w.) akawaambia: “Tafadhalini hebu ketini ili nikuambieni jambo fulani.” Walikaa na kuyasikiliza maneno yake.

Mtume (s.a.w.w.) aliwasomea aya za Qur’anii. Jambo hili lilikuwa na athari njema kwao nao wakasilimu palepale. Jambo lililowafanya wauele- kee Uislamu ni kwamba, walikuwa wamesikia kutoka kwa Wayahudi kwamba Nabii mwenye asili ya Uarabu, atakayeleta dini ya Upweke wa Allah na atakayeifutilia mbali ibada ya masanamu, hivi karibuni atateuliwa na Allah Mwenyezi, na hivyo, wao wakafikiria ya kwamba, kabla ya Wayahudi kuwatangulia wao katika jambo hili, wao wenyewe wamsaidie Mtume (s.a.w.w.) na kwa kufanya hivyo wawashinde maadui zao.

Kikundi hiki kilimgeukia Mtume (s.a.w.w.) na kusema: “Mara kwa mara moto wa vita huwaka baina yetu. Tunategemea kwamba Allah Mwenyezi atauzima moto huu kwa njia ya hii dini yako tukufu. Sasa tunarejea Yathrib na tutawafikishia watu dini yako. Kama wote wakiikubali, basi hatakuwapo mtu yeyote mwingine tutakayemheshimu zaidi yako.” Watu sita hawa walifanya juhudi za kudumu kuuhubiri Uislamu mjini Yathrib kiasi kwamba haikuwako nyumba yoyote mjini humo ambayo kwamba Mtume (s.a.w.w.) hakuzungumziwa habari zake.4

Mkataba Wa Kwanza Huko ‘Aqabah

Mahubiri yaliyoendelezwa ya wale watu sita yalizaa matunda na kikundi cha wakazi wa Yathrib
kilisilimu. Kwenye mwaka wa kumi na mbili wa kazi ya Utume kikundi kingine kilichokuwa na watu kumi na wawili kilikuja kutoka Yathrib na kukutana na Mtume (s.a.w.w.) mahali paitwapo

‘Aqabah na wakafanya mkataba wa kwanza wa kiislamu. Waliokuwa maarufu zaidi miongoni mwa watu hawa alikuwa ni As’ad bin Zuraarah, na ‘Ubadah bin Saamit. Maelezo ya mkataba wao na Mtume yalikuwa hivi: “Tumefunga mkataba na Mtukufu Mtume kwamba ‘Hatutamshirikisha yeyote na Allah. Hatutaiba wala kufanya zinaa. Hatutawaua watoto wetu. Hatutasingiziana na hatutaacha kutenda matendo mema.”

Mtume (s.a.w.w.) naye aliwaahidi ya kwamba kama wakiyatekeleza map- atano haya basi, nafasi yao itakuwa ni Peponi, lakini kama wakiasi, basi itakuwa ni juu yake Allah kuwasamehe au kuwaadhibu. Kwa mujibu wa istilahi za wanahistoria, Bay’at (kiapo cha Utii) hii inaitwa Bay’atun Nisa’ (Bay’at ya wanawake), kwa sababu wakati wa kutekwa kwa mji wa Makkah, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alifanya Bay’at ya aina hii hii na wanawake.
Watu hawa kumi na wawili walirudi Yathrib wakiwa na nyoyo zilizojaa imani na wakajishughulisha sana sana katika kuubalighisha Uislamu. Vile vile walimwandikia barua Mtume (s.a.w.w.) wakimwomba awapelekee mubalighina ili akawafundishe Qur’anii. Mtume (s.a.w.w.) alimpeleka Mus’ab bin Umayr ili akawaongoze. Chini ya mwongozo wa mubalighina huyu mwenye uwezo, Waislamu wale walikuwa wakikusanyika na kumzunguka na kuzisali sala zao za jamaa wakati Mtume (s.a.w.w.) akiwa hayupo.5

Mkataba Wa Pili Wa Aqabah

Zilikuwako ghasia nyingi miongoni mwa Waislamu wa Yathrib. Walikuwa wakisubiri kwa shauku uingie wakati wa Hija ili kwamba, ukiachilia mbali kule kuzitekeleza ibada za Hija, vilevile wataweza kumwona Mtume (s.a.w.w.) kwa karibu zaidi na kuelezea kuwa kwao tayari kuitoa kila huduma kwa ajili ya Uislamu na kuukuza upeo wa mapatano kutegemeana na wingi na ubora. Msafara wa mahujaji wa Yathrib uliokuwa na zaidi ya watu mia tano ulitoka kwenda Makkah. Msafara huo ulikuwa na waislamu sabini na watatu, ambao wawili miongoni mwao walikuwa ni wanawake, na wale waliosalia walikuwa ni watu wenye mtazamo wa kadiri au wenye nusu ya mwelekeo wa kwenye Uislamu. Kikundi hiki kilikutana na Mtume (s.a.w.w.) mjini Makkah na wakaomba wawekewe muda wa kufanyia taratibu za ‘Bay’at’. Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Tutakutana Mina usiku wa mwezi 13 Dhil-Hajj, watu watakapokuwa wamelala, kwenye Bonde la ‘Aqabah (Hii ni njia nyembamba ya mlimani iliyoko karibu na Mina).

Usiku wa mwezi 13 Dhil-Hj ukafika. Mtume (s.a.w.w.) alikuwa wa kwanza kufika ‘Aqabah pamoja na ami yake Abbas. Sehemu ya usiku ule ilipita. Washirikina wa Uarabuni wakaenda kulala Waislamu waliamka kutoka kwenye sehemu zao mmoja baada ya mwingine na wakaja pale ‘Aqabah kwa siri. Bwana Abbas, ami yake Mtume (s.a.w.w.) alikuwa ndiye wa kwanza kuzungumza, naye alisema hivi: “Enyi Bani Khazraji! Mmeonyesha kuunga mkono kwenu dini ya Muhammad! Hamna budi kufahamu ya kwamba yeye ndiye mtu mtukufu zaidi kwenye kabila hili. Bani Hashim wote, wawe wenye kuiamini dini yake au la, wanawajibikiwa na ulinzi wake.

Hata hivyo, hivi sasa Muhammad anakuelekeeni na anapenda kuwa miongoni mwenu. Kama mnao uhakika ya kwamba mtajiambatanisha na mapatano yenu nanyi mtamhami kutokana na kila dhara litokalo kwa maadui zake, basi tuko tayari kumruhusu aende nanyi. Hata hivyo, endapo hamna uwezo wa kumhami kwenye hali ngumu, mko huru kumwacha hapa aishi miongoni mwa ndugu zake kwa utukufu mwingi na heshima.”

Wakati huu Bura’a bin Ma’rur alisimama na kusema: “Ninaapa kwa jina la Allah! Kama kungalikuwa na chochote kingine nyoyoni mwetu zaidi ya yale tuliyoyasema kwa ndimi zetu, tungalisema. Hatuna nia yoyote nyingine zaidi ya kuyatimiza mapatano haya na kujitoa mhanga katika nji ya Mtume.” Baada ya hapo wale Bani Khazraji walimwelekea Mtume (s.a.w.w.) na kumwomba azungumze lolote. Mtume (s.a.w.w.) alisoma aya za Qur’anii na kuuchochea muelekeo wao wa kuelekea kwenye Uislamu. Baada ya hapo akasema: “Ninakichukulia kiapo chenu hiki ya kwamba, mtanihami kama vile mnavyowahami wana wenu wa watu wa familia zenu.”

Alipoyasikia hayo Bura’a, alisimama tena na akasema: “Sisi tu wana wa kampeni na mapambano, nasi tumefunzwa kuwa wapiganaji mashujaa. Tumezirithi sifa hizi kutoka kwa jadi zetu.” Wakati huo huo, pale mkutano mzima ulipojawa na msisimko, sauti za Bani Khazraji zili- zokuwa dalili ya hamasa zao zisizo kifani zilipaa. Bwana Abbas, huku akiwa ameushika mkono wa Mtume (s.a.w.w.) alisema: “Wamewekwa wapelelezi juu yetu na hivyo basi, ni muhimu kwamba mzungumze kwa sauti ndogo.” Hapo Bura’a bin Ma’rur, Abul Haytham bin Tayhaan na As’ad bin Zurarah waliamka kutoka kwenye sehemu zao na kuiweka mikono yao juu ya mkono wa Mtume (s.a.w.w.) kwa namna ya Bay’at.

Baada ya hapo wale wote waliokuwapo pale walifanya ‘Bay’at, mmoja baada ya mwingine.
Alipokuwa akila kiapo kile, Abul Haytham alisema: “Ewe Rasuli wa Allah! Tumefanya mapatano na Wayahudi na sasa hakuna njia yoyote nyingine ila kuipuuzilia mbali. Hivyo basi, haitafaa kwamba siku moja utuache na kuwarudia watu wako.” Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alimjibu akisema: “ Kama mmefanya mapatano ya amani na mtu yeyote yule nin- auchukulia kuwa wa kuheshimiwa.”

Kisha akaongezea kusema: “Chagueni watu kumi na wawili miongoni mwenu kama vile Mtume Musa bin Imran alivyoteua viongozi kumi na wawili miongoni mwa Bani Isra’il, ili kwamba, kwenye hali ngumu muweze kuyategemea maoni yao.” Baada ya hapo, wawakilishi kumi na wawili wa Maansari (tisa kutoka Bani Khazraji na watatu kutoka Bani Aws) walijulishwa kwa Mtume (s.a.w.w.). Majina na taarifa zao vimeandikwa kwenye vitabu vya historia. Kule kufanyika kwa

‘Bay’at kulimalizika kwenye mkutano huu na Mtume (s.a.w.w.) aliahidi ya kwamba ataondoka Makkah wakati ufaao na kwenda Yathrib. Baada ya hapo wale watu wakatawanyika.6

Hali Ya Waislamu Baada Ya Mkataba Wa ‘Aqabah’

Sasa swali linaibuka, ni kwa nini watu wa Yathrib waliokuwa mbali kuto- ka kwenye kitovu cha wahubiri wa Uislamu waliyakubali mamlaka ya Mtume (s.a.w.w.) kwa urahisi zaidi kuliko watu wa Makkah (pamoja na kuwa kwao karibu naye) na ni kwa nini mikutano mifupi na michache baina yake na watu wa Tathrib ilikuwa na uzito mkubwa kuliko yale mahubiri ya miaka kumi na mitatu mle mjini Makkah? Tunaweza kusema kwamba mambo mawili yafuatayo ndiyo yaliyokuwa sababu ya kuendelea kwa Uislamu mjini Yathrib:

“Watu wa Yathrib walikuwa majirani wa Wayahudi tangu kale na kila mara wakitaja kwenye mikutano na mikusanyiko yao kuhusu kuteuliwa kwa Nabii wa kiarabu kwenye kazi ya Utume. Nabii huyu walimtaja mno kiasi kwamba Wayahudi walikuwa wakiwaambia wenye kuyaabudu masanamu wa mle mjini Yathrib kwamba yule Nabii wa kiarabu anayengojwa ataikuza dini ya Kiyahudi na kuiharibu ibada ya masanamu. Mazungumzo haya yalizaa utayari usio wa kifani akilini mwa watu wa Yathrib katika kuikubali dini iliyokuwa ikisubiriwa na Wayahudi, kiasi kwamba wale wakhazraji sita walipokutana na Mtume (s.a.ww.) kwa mara ya kwanza walisilimu mara moja na wakaambiana: “Huyu ndiye yule Nabii anayen- gojwa na Wayahudi na hivyo basi ni muhimu kwetu sisi kwamba tuonyeshe kumwamini kwetu kabla yao.”

Hivyo basi, moja ya upinzani uliotolewa na Qur’anii Tukufu dhidi ya Wayahudi ni huu: “Mlikuwa na kawaida ya kuwaogofya wenye kuyaabudu masanamu juu ya uteuzi wa Utume kwa Nabii wa kiarabu na mkawabashiria watu ujio wake na kuzinukuu dalili zake kutoka kwenye Taurati. Basi kwa nini sasa mwazigeuzia nyuso zenu mbali naye? Inasema:

وَلَمَّا جَاءَهُمْ كِتَابٌ مِنْ عِنْدِ اللَّهِ مُصَدِّقٌ لِمَا مَعَهُمْ وَكَانُوا مِنْ قَبْلُ يَسْتَفْتِحُونَ عَلَى الَّذِينَ كَفَرُوا فَلَمَّا جَاءَهُمْ مَا عَرَفُوا كَفَرُوا بِهِ ۚ فَلَعْنَةُ اللَّهِ عَلَى الْكَافِرِينَ {89}

“Na kilipowajia kitabu kitokacho kwa Mwenyezi Mungu, chenye kuthibitisha (kile) walicho nach,o, na zamani walikuwa wakiomba ushindi dhidi ya makafiri; lakini yalipowafikia yale waliyoyajua waliyakana; basi laana ya Mwenyezi Mungu iwe juu ya makafiri.”
(Surah al-Baqarah, 2:89).

Kipengele kingine ambacho kinaweza kuwa ndicho kilichowafanya watu wa Yathrib kusilimu ni ule uchovu wao wa kiakili na kimwili. Ule usum- bufu uliosababishwa na migogoro iliyoenea kwenye kipindi cha miaka mia moja na ishirini uliimaliza subira yao. Walikaribia kuchoshwa na maisha yao na wakaona wamefungiwa milango yote ya matumaini na wokovu wao.
Uchunguzi wa vita vya Bu’aath tu, ambavyo ni moja ya vita vilivy- opiganwa na watu wa Yathrib, kabila moja dhidi ya jingine, unatoa picha ya dhahiri ya hali yao. Kwenye vita hii, Bani Aws mwanzoni walioshindwa, walikimbilia Najd.

Wale maadui walioshinda (Bani Khazraji) waliwadhihaki. Chifu wa Bani Aws (Huzayr) alijihisi vibaya mno. Alijichoma mkuki nyongani mwake, akashuka kutoka kwenye farasi wake akawaita watu wake kwa sauti kuu akisema: “Sitaamka kutoka kwenye sehemu yangu hii hadi niuawe.”

Uthabiti wa Huzayr uliibua moyo wa heshima, ushujaa na kujihami miongoni mwa wapiganaji walioshindwa. Waliamua kurudi kwa vyovyote vile itakavyokuwa na kuyatetea maslahi yao. Wakiwa wamekata tamaa kabisa juu ya maisha yao walianza mapigano makali sana. Wakati jeshi lenye kujitoa mhanga linapopigana kwa imani thabiti daima hushinda. Hivyo wale Bani Aws walioshindwa walishinda tena. Waliwashinda Bani Khazraji na wakaichoma mitende yao.

Baada ya hapo vita na amani viliendelea kwa muda mrefu na iliwabidi kuyakabili mamia ya matukio yasiyopendeza, yenye kuhuzunisha, na yenye kuchosha. Makundi yote mawili yalihuzunishwa na hali yao na wal- itaka kupata suluhisho juu yake na walitamani kupata mwanga wa matumaini.

Ni kwa sababu hii kwamba wale Wakhazraji sita walipoyasikia maneno ya Mtume (s.a.w.w.) walijihisi kwamba wamekipata kile wali- chokipoteza na wakasema: “Pengine Allah Atatuondolea huu ugomvi kupitia kwako.”

Hizi zilikuwa baadhi ya sababu zilizowashawishi watu wa Yathrib kuupokea ule mwito wa uislamu kwa mikono miwili.

Hatua Ya Quraishi Juu Ya Mapatano Ya ‘Aqabah’

Sasa Waquraishi wakauchukua msimamo wa utepetevu, na kwa vile Uislamu ulikuwa haujapata maendeleo yawezayo kutambulika mjini Makkah, walikuwa na mawazo kwamba kuanguka kwake kumeanza na kwamba jengo lake litaporomoka punde tu. Mara kwa ghafla taarifa za mapatano ya pili ya ‘Aqabah ziliangukia miongoni mwao kama bomu. Wakuu wa uongozi wa ibada ya masanamu walifahamu kwamba kwenye giza la usiku uliopita watu sabini na watatu watokao Yathrib wamefanya mkataba na Mtume (s.a.w.w.) kwamba watamlinda kama vile wawalin- davyo watoto wao. Taarifa hizi zilileta hofu isiyo na kifani nyoyoni mwao na wakajiambia wenyewe: “Sasa Waislamu wamejipatia kituo katikati mwa Penisula ya Uarabuni na kwamba ulikuwapo uwezekano kwamba wangaliweza kuyakusanya majeshi yao yaliyotawanyika na kuanza kuibalighisha dini yao ya Upweke wa Allah, na kwa njia hii wataiogofya serikali kuu ya wenye kuabudu masanamu wa Makkah kwa vita na hatari.”

Ili kulichunguza zaidi jambo hili, machifu wa Waquraishi walionana na Wakhazraji asubuhi yake na kusema: “Tumepata taarifa ya kwamba usiku uliopita mlifanya mapatano ya ulinzi na Muhammad na mmemwahidi ya kwamba mtapigana dhidi yetu!” Hata hivyo, Wakhazraji waliapa ya kwam- ba wao hawakudhamiria kupigana vita dhidi yao.

Msafara wa mahujaji wa Yathrib ulikuwa na watu wapatao 500 hivi. Miongoni mwao ni watu sabini na watatu tu waliofanya Bay’at pale ‘Aqabah kwenye ule usiku wa manane huku wengine wakiwa wamelala kwenye wakati ule na wakiwa hawajui lolote juu ya jambo lile. Hivyo basi, wale wasiokuwa waislamu waliapa ya kwamba hakuna lolote la aina ile lililotokea na ile hadithi nzima (ya yale mapatano) ilikuwa uzushi mtupu. Yule Khazraji Abdallah bin Ubay, ambaye matayarisho ya uchifu wake wa Yathrib nzima yalikuwa tayari yameshafanyika, alisema: “Hakuna jambo la aina hii lililofanyika, na watu wa kabila la Khazraji hawafanyi jambo lolote lile bila ya ushauri wangu.”

Kisha machifu wa Waquraishi waliamka wakaenda zao ili kwamba waweze kufanya uchunguzi zaidi juu ya jambo hili. Waislamu waliokuwapo mkutanoni pale, walitambua ya kwamba siri yao imefichuka. Hivyo basi, waliamua kuutumia ipasavyo muda uliopo na wakaambiana:
“Kabla ya kutambuliwa wale watu waliohusika na mapatano yale, ingalikuwa bora kama tungalirejea nyumbani na kutoka nje ya athari za Makkah.”

Haraka iliyoonekana katika baadhi ya watu wa Yathrib ilizidisha shaka za Waquraishi juu ya yale mapatano na wakahitimisha kwamba ile taarifa waliyoipata ilikuwa sahihi. Hivyo basi, waliwafuata wale watu wa Yathrib. Hata hivyo, kwa bahati walianzisha ufuatiliaji wao ule wakiwa tayari wameshachelewa na ule msafara wa mahujaji ulikuwa tayari uishafikia umbali usioweza kufikiwa na watu wa Makkah. Waliweza kumkamata Mwislamu mmoja tu naye ni Sa’ad bin Ubadah.

Kwa mujibu wa Ibn Hisham Waquraishi waliwakamata watu wawili miongoni mwao akiwemo Sa’ad na mwingine akiwa ni Manzar bin Umar. Yule wa pili aliwaponyoka. Hata hivyo, kuhusu Sa’ad, walizikamata nywele zake kwa ukali mwingi na wakamburuza chini, miongoni mwa Waquraishi yupo aliyechomwa mno moyoni kumwona Sa’ad akiwa kwenye hali hii ya kuhuzunisha na akamwuliza: “Je, una mapatano na mtu yeyote humu mjini Makkah?” Sa’ad akajibu:’ “Ndio, nina mapatano na Mut’am bin Adi, kwa kuwa niliihami biashara yake kutokana na wizi na nikampatia mahali pa usalama alipokuwa akivuka kupitia Yathrab.”

Yule Quraishi aliyetaka kumwokoa kutokana na mgogoro huu alimwendea Mut’am na kumwambia: “Khazraji mmoja amekamatwa naye anateswa vikali mno na Waquraishi. Sasa anataka msaada wako na anakusubiri ukamsaidie”. Mut’am alikuja mahali pale na akaona kuwa ni Sa’ad bin Ubadah, mtu yule ambaye kila mwaka kwa ulinzi wake misafara kule ilikokuwa ikienda ilikuwa ikifika kwa usalama. Alifanya Waquraishi wamwachie na kisha akampeleka Yathrib. Marafiki wa Sa’ad na Waislamu waliozipata taarifa za kukamatwa kwake waliamua kuchukua hatua ili afunguliwe. Walikuwa wakilifikiria jambo hili wakati Sa’ad alipotokea kwa ghafla kwa mbali. Baada ya kuwafikia aliwasimulia ile hadithi yenye kuogofya.7

Mvuto Wa Kiroho Wa Uislamu

Wataalamu wa elimu ya nchi za Mashariki wanajaribu kwa makini kunena kwa nguvu kwamba kuendelea kwa Uislamu kulifanyika kwa upanga. Kuhusiana na jambo hili husema mambo ambayo tutayajibu, moja baada ya jingine, tutakapovielezea vita vya Uislamu dhidi ya makafiri. Hata hivyo, hivi sasa tungalipenda kuzivutia fikara za wasomaji kwenye tukio lililotokea mjini Yathrib kabla ya Hijiriya. Tukio hili lathibitisha dhahiri kwamba, hapo awali, kuenea na kuendelea kwa Uislamu kulifanyika tu kwa njia ya utamu wake na uwazi wa sheria na kanuni zake zilizopendeza nyoyo za watu. Haya yafuatayo hapa chini ndio maelezo yake:

Mus’ab bin Umayr alikuwa mubalighi na msemaji mkuu wa Uislamu aliyepelekwa Yathrib na Mtume (s.a.w.w.) kwa kuombwa na As’ad bin Zurarah. Watu wawili hawa waliamua kuwabalighishia machifu wa Yathrib kwa njia ya hoja za kimantiki. Siku moja waliingia bustani walimokuwamo baadhi ya Waislamu na Sa’ad bin Ma’aaz na Usayd bin Huzayr, waliokuwa machifu wa Bani Abdu Ashhal, walikuwapo pale nao. Sa’ad alimgeukia Usayd na kumwambia: “Ufute upanga wako na uwaendee hawa watu wawili na uwaambie waache kuibalighisha dini ya Uislamu na wasiwahadae watu wetu wajinga kwa hotuba na maelezo yao. Kwa vile As’ad bin Zurarah yu binamu yangu, (mwana wa mama mdogo/mkubwa), mimi ninaona aibu kumkabili huku nikiwa na silaha iliyofutwa.” Usayd alisimama akiwakingia njia wale watu wawili kwa uso ulioghadhibika na upanga uliofutwa na akayatamka yale maneno tuliyoyataja hapo juu kwa sauti ya ukali.

Yule msemaji mkuu Mus’ab bin Umayr aliyekwisha jifunza njia ya uhubiri kutoka kwa Mtume (s.a.w.w.) alimwambia Usayd hivi: “Inawezekana kwamba uketi pamoja nasi kwa kitambo hivi ili tuweze kuzungmza. Kama yale tuyasemayo si yenye kukubalika akilini mwako, tutarudi kwa njia ile ile tuliyojia.” Usayd akasema: “Umesema jambo liingialo akilini.” Hivyo, akaketi kwa kitambo fulani na akauchomeka upan- ga wake alani mwake.
Mus’ab akazisoma aya chache za Qur’anii. Ukweli wenye kuangaza wa Qur’anii na mvuto na utamu wake vilivyoandamana na mantiki yenye nguvu ya Mus’ab vikamshinda nguvu. Alipoteza uwezo wake wa kujitawala na akauliza akisema: “Vipi mtu aweza kuwa Mwislamu?” Wakamjibu wakasema: “Ushuhudie Upweke wa Allah, uoshe mwili wako na nguo zako kwa maji na usali.” Usayd aliyekuja kwa lengo la kuimwaga damu ya hawa watu wawili, aliushuhudia kwa moyo mkunjufu upweke wa Allah na Utume wa Mtume Muhammad (s.a.w.w.).

Alioga na akafua nguo yake na kasha akarejea kwa Sa’ad huku akizikariri ‘Shahadatain’ (Kuukiri Upweke wa Allah na Utume wa Muhammad). Sa’ad bin Ma’aaz alikuwa akimsubiri kwa shauku. Mara Usayd akatokea akiwa yu mwenye uso wenye furaha na tabasamu. Sa’ad bin Ma’aaz aliwageukia wale waliokuwapo pale na akasema: “Ninaapa kwa jina la Allah! Usayd ameibadilisha imani yake na hakulifikia lile lengo aliloliendea.” Usayd akafika na akaielezea ile habari. Sa’ad bin Ma’aaz akaamka kwa ghadhabu kali mno ili aende akawazuie wale watu wawili wasihubiri Uislamu na kuimwaga damu yao. Hata hivyo, jambo lile lile lililotokea kwa Usayd, lil- imtokea yeye nae.

Ilimbidi yeye nae asalimu amri mbele ya hoja za kimantiki na zenye nguvu na maneno yenye kuvutia na matamu ya Mus’ab. Dalili za majuto zilijitokeza usoni mwake kwa lile aliloliamua, na sasa akatangaza kuunga kwake mkono Uislamu. Kisha alioga na akazitoharisha nguo zake. Baada ya hapo akarudi kwa watu na kuwaambia: “Nina cheo gani miongoni mwenu?” wakamjibu wakasema: “Wewe ni kiongozi na chifu wa kabila letu.” Kisha akasema: “Sitazungumza na mwanaume wala mwanamke yeyote wa kabila langu ila watakapokuwa wamesilimu.”

Haya maneno ya chifu yalipitishwa kinywa hadi kinywa kwa watu wote wa kabila lile na katika kipindi kifupi na hata kabla ya kumwona Mtume (s.a.w.w.) kabila zima la Bani Abdul Ashhal lilisilimu na likawa walinzi wa hii dini takatifu.8

Tunapata mifano mingi ya matukio ya aina hii kwenye kurasa za historia. Kwa dhahiri kabisa zinathibitisha kutokuwa na msingi kwa mazungumzo ya wataalamu wa elimu ya nchi za Mashariki juu ya sababu za kuendelea kwa Uislamu, kwa sababu kwenye matukio haya, nguvu au fedha havikutumika na wale watu waliohusika hawakumwona Mtume (s.a.w.w.), wala hawakuwa na mawasiliano naye. Hakikutumika kipengele chochote kingine kwenye matukio haya ila akili za Mwislamu msemaji zilizoleta mapinduzi ya kiroho ya ajabu kabisa kwenye kabila lile.

Waquraishi Wapatwa Na Hofu

Msaada uliotolewa na watu wa Yathrib kuwapa Waislamu uliwaamsha tena Waquraishi kutoka kwenye uzembe wao. Wakayaanzisha tena yale mateso na dhuluma zao na wakajitayarisha tena kuuzuia ushawishi na maendeleo ya Uislamu. Masahaba wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) walilalamika kuhusu mateso na dhuluma walizokuwa wakitendewa na makafiri na wakaomba ruhusa ya kuhajiria kwenye sehemu nyingine. Mtume (s.a.w.w.) aliwaomba wampe muda (ili aweze kuamua la kufanya). Baada ya siku chache hivi aliwaambia: “Sehemu inayokufaeni zaidi ni Yathrib. Mnaweza kuhamia kwenye sehemu ile mmoja baada ya mwingine kwa urahisi sana.”

Baada ya Waislamu kuamrishwa kuhamia, walitoka Makkah kwa kutoa sababu moja au nyingine na wakaelekea Yathrib. Hata hivyo, kwenye hatua ya kwanza kabisa ya kuhajiri kule Waquraishi walipata kuijua siri ya safari zile. Hivyo basi, wakazuia aina zote za misafara na wakaamua kuwarudisha wale wote waliokuwamo njiani (wakielekea Yathrib). Vile vile waliamua ya kwamba iwapo mtu atakuwa akihajiri na mkewe na watoto na yule mkewe yu quraishia, wasimruhusu kuondoka na mkewe huyo. Ingawa Waquraishi walizichukua hatua zote hizi, walijizuia kumwaga damu na wakaendelea kuwaonea na kuwadhulumu Waislamu. Hata hivyo, kwa bahati matendo yao hayakuzaa matunda.9

Hata hivyo, idadi kubwa ya Waislamu iliponyoka kutoka kwenye makucha ya Waquraishi na kujiunga na watu wa Yathrib.
Wote walifanya hivyo ila Mtume (s.a.w.w.) na Sayyidna Ali (a.s.), ukiachilia mbali Waislamu waliozuiwa au waliokuwa wagonjwa, hakuna Mwislamu yeyote mwingine aliyesalia mjini Makkah. Kukusanyika kwa Waislamu mjini Yathrib kuliwatahadharisha zaidi Waquraishi. Hivyo basi, ili kuuharibu Uislamu viongozi wote wa kabila lile walikusanyika kwenye Darun-Nadwah na wakashauriana juu ya hali yao. Mapendekezo yao yote yalishindikana kutokana na sera maalum za Mtume (s.a.w.w.), hatimaye yeye naye alihajiria Yathrib kwenye mwezi wa Rabiul Awwal, katika mwaka wa kumi na nne wa uteuzi wake kwenye kazi ya Utume.

  • 1. Seerah-i Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 425
  • 2. Siirah-i Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 426.
  • 3. Siirah-i Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 427.
  • 4. Tarikh-i Tabari, Juzuu 2, uk. 86.
  • 5. Siirah-i Ibn Hisham, Juzuu 1, uk.131.
  • 6. Siirah-i Ibn Hisham, Juzuu 1, uk.438-444; na Tabaqaat Ibn Sa'ad, Juzuu 1, uk. 221-223.
  • 7. Siirah-i Ibn Hisham, Juzuu 1, uk.448- 450
  • 8. A'laamul Wara', uk. 37; na Bihaarul Anwaar, Juzuu 19, uk. 10-11.
  • 9. Tabaqat-i Ibn Sa'ad, Juzuu 7, uk. 210.