Sura Ya 26: Matukio Ya Mwaka Wa Kwanza Wa Hijiriya

Nyuso za Ansar zenye furaha na shauku, na makaribisho ya moyo mkunjuvu ambayo watu wa makabila ya Aws na Khazraji walikuwa wamempa Mtume (s.a.w.w.) yalimshawishi kujenga kituo cha ustawi wa jamii kwa ajili ya Waislamu kabla ya kufanya jambo lolote jingine, kituo hiki kiliitwa ‘Masjid’ (Msikiti) ili kitumike kwa kufanyia mambo ya maelekezo, maendeleo, siasa na haki.

Na kwa vile kuwaita watu kwenye ibada ya Mungu Mmoja tu na Mlezi, lilikuwa ndilo jambo la kwanza kwenye mpango huu, alifikiria kwamba lilikuwa ni jambo muhimu kwanza kabisa, kujenga maabadi ambamo Waislamu wangeliweza kujishughulisha humo katika kumdhukuru Allah na kulisabihi Jina Lake wakati wa kusali. Vile vile ilikuwa muhimu kwamba aunde kituo ambamo watu wa kawaida wa kundi la Kiislamu (kundi la Allah) waweze kukutana humo kila juma katika siku maalum iliyowekwa na kufanya mijadala na mashauriano juu ya maslahi ya Uislamu na Waislamu, na zaidi ya kukutana kila siku waweze kusali sala za Idi humo mara mbili kwa mwaka.

Msikiti haukuwa tu kituo cha ibada bali vile vile ulikuwa ndiyo sehemu ambamo kila aina ya maelekezo ya Kiislamu na amri ziliweza kutolewa, na kila aina ya elimu ya kidini na kisayansi iliweza kufundishwa, ikiwa ni pamoja na kusoma na kuandika. Hadi mwanzoni mwa karne ya nne ya Kiislamu misikiti ilitumika kama shule zilizokuwa zikifanya kazi nyakati zote, ila ile iliyotengwa kwa sala tu. Baada ya hapo taasisi za kielemu zilichukua sura maalum. Wengi wa wanachuoni wakuu walihitimu kutoka kwenye vituo vya elimu vilivyojengwa kwenye misikiti.

Kwa kipindi fulani Msikiti wa Madina ulichukua sura ya kituo cha masomo pia. Washairi wakuu wa Uarabuni ambao tungo zao zililandana na mafundisho ya maadili na kielemu ya Uislamu waliweza kuzisoma beti zao mbele ya Mtume (s.a.w.w.). Ka’ab bin Zuhayr alilisoma shairi lake maarufu la kumsifu Mtume (s.a.w.w.) mbele ya Mtume (s.a.w.w.) mwenyewe msikitini na akapata zawadi kubwa na joho la heshima kutoka kwake. Hassan bin Thabit, aliyeihami heshima ya Uislamu kwa njia ya beti za mashairi yake alikuwa na kawaida ya kuyasoma mashairi yake kwenye Msikiti wa Mtume (s.a.w.w.).

Mikutano ya kielimu kwenye Msikiti wa Madina, katika zama za Mtume (s.a.w.w.), ilivutia mno kiasi kwamba wawakilishi wa kabila la Saqaf walivutiwa mno na mandhari ile; walishangazwa na shauku waliyokuwa nayo Waislamu katika kuitafuta elimu. Mambo ya kisheria na daawa yaliamuliwa, na humo msikitini adhabu zilitolewa kwa wale waliokosa, nao ulitumika kwa nia na makusudio maalum na baraza la kisheria ambamo malalamiko ya watu yalitatuliwa.

Zaidi ya hapo, Mtume (s.a.w.w.) alikuwa akitoa hotuba zenye kuamsha hisia za watu msikitini humo ili kuwafanya watu wafanye jitihada na kampeni dhidi ya ukafiri. Inawezekana kwamba moja ya siri za kuunganisha mambo ya kidini na kielimu msikitini ilikuwa kwamba yule kiongozi wa Kiislamu alitaka kuonyesha kivitendo kwamba elimu na dini, kila kimoja kinakamilisha kingine, na kama sehemu fulani ni kituo cha kidini, basi ni lazima vile vile iwe kituo cha elimu na hekima.

Na kama mambo ya kisheria na mengineyo, yakiwemo mambo yahusianayo na jihadi yaliweza kuamuliwa katika msikiti, hiyo ilikuwa ni kwa sababu ya kwamba alitaka kudhihirisha ya kwamba dini yake si dini ya kiroho tu isiyokuwa na uhusiano wowote na mambo ya kidunia, bali ni dini ambayo inapowatia watu kwenye uchamungu na dini, vile vile haiyadharau mambo ya kidunia na ustawi wa jamii.

Upatanifu huu (baina ya elimu na dini) ni hamasa ya Waislamu hata katika siku zetu hizi. Wakati vituo vya kielimu vyenye sura maalum vilipojengwa daima shule na vyuo vikuu viliasisiwa kando kandoni mwa Msikiti mkuu ili kuuthibitishia ulimwengu kwamba vitu hivyo viwili vya ustawi wa jamii havitengani.

Kisa Cha Ammaar

Pale mahali ambapo ngamia wa Mtume (s.a.w.w.) alipopiga magoti palinunuliwa kwa dinari kumi kwa ajili ya ujenzi wa msikiti. Waislamu wote walishiriki katika ujenzi wa msikiti huo na katika ukusanyaji wa vifaa vya ujenzi, na hata Mtume (s.a.w.w.) alikusanya mawe pamoja na masahaba wake. Usayd bin Huzayr alikwenda mbele ya Mtume (s.a.w.w.) na kusema: “Ewe Mtume wa Allah! Niruhusu nilinyanyue mimi (hilo jiwe).” Mtume (s.a.w.w.) akamjibu akasema: “Nenda ukalete jingine.” Kwa jinsi hii alionyesha kidokezo cha tabia yake tukufu. Alisema: “Mimi ni mtu nifanyaye mambo kwa vitendo. Mimi ni mtu wa vitendo wala si wa maneno tu.” Katika tukio hilo, Muslim alisoma beti fulani za shairi zenye maana ya: “Kama tukikaa chini, na Mtume akafanya kazi, itakuwa ni chanzo cha upotofu na uovu kwa upande wetu.”

Mtume (s.a.w) na Waislamu walipokuwa wakiifanya kazi hii walikuwa wakitamka maneno haya: “Maisha ya kweli ni maisha ya Akhera. Ewe Allah! Wahurumie Ansar na Muhajiriin.”

Uthman bin Maz’un alikuwa mchungu sana kuhusu unadhifu wa nguo zake na alitaka kuiweka nguo yake katika hali ya usafi. Hivyo basi, yeye hakushiriki katika ujenzi wa msikiti, ili nguo yake isije ikaingia mavumbi. Sayyidna Ali (a.s.) alimlaumu kwa maneno haya: “Mtu ajengaye msikiti, akiwa amekaa au amesimama, daima yu mwenye kujitahidi kwa ajili ya maendeleo yake si kama yule ajitengaye na vumbi naye hayuko tayari kuzitia doa nguo zake katika kujenga Msikiti.1

‘Ammar Yasir, ambaye alikuwa mtu mwenye nguvu, alikusanya mawe kwa ajili ya ujenzi wa msikiti na kuyapeleka kule ufanyikapo ujenzi. Baadhi ya watu walijinufaisha visivyostahili kutokana na upole wake na kumtwisha mawe yaliyokuwa mazito mno kwake. Alisikika akisema: “Na nyanyua jiwe moja kwa ajili yangu mwenyewe na jingine kwa ajili ya Mtume (s.a.w.w.).” Siku moja Mtume alimwona akibeba mzigo mzito, wakati alipokuwa katwishwa mawe matatu. ‘Ammaar alilalamika akisema: “Masahaba zako wana nia mbaya dhidi yangu na wanataka kuniua.

Wao wenyewe wanaleta jiwe moja moja lakini mimi wananitwisha mawe matatu.” Mtume (s.a.w.w.) alimshika mkono, akamfuta vumbi mgongoni mwake, na akatamka maneno haya ya kihistoria: “Wao sio wauwaji wako. Utauawa na kundi la madhalimu utakapokuwa ukiwaita kwenye haki na ukweli.”2

Utabiri huu ni moja ya thibitisho za Utume na ukweli wa Mtume (s.a.w.w.). Hatimaye jambo hilo alilolitabiri Mtume lilitimia kweli, kwa sababu ‘Ammar, aliyekuwa pamoja na Imamu Ali (a.s.) Amiri wa Waumini kwenye vita vya Siffin na wakati ule alikuwa na umri wa miaka 90 aliuawa mikononi mwa wafuasi wa Mu’awiyah. Taarifa hii ya fumbo iliendelea kuwa na athari za ajabu kwa ‘Ammar katika kipindi chote cha uhai wake. Baada ya tukio hili Waislamu walimfikiria ‘Ammar kuwa yu kiini cha ukweli na kila ukweli ulikuwa ukipimwa kwa uhusiano wake na ‘Ammar.

Alipouawa ‘Ammar kwenye vita vile, makelele ya kushangaza yalitokea miongoni mwa watu wa Sham. Watu waliokuwa na shaka juu ya ukweli wa Sayyidna Ali (a.s.) kutokana na propaganda yenye sumu ya Mu’awiyah na Amr bin Aas, walipata mwanga. Huzaymah bin Thabit Ansar alikwenda kwenye vita vile pamoja na Imamu Ali (a.s.), lakini alichanganyikiwa kuhusu kushiriki kwake katika vita vile. Hata hivyo, aliposikia ya kwamba ‘Ammar ameuawa aliuchomoa upanga wake na kuanza kuwashambulia watu wa Shamu.

Dhul Kulaa’ Himyari akifuatana na watu ishirini elfu wa kabila lake walikuja kupigana dhidi ya Sayyidna Ali (a.s.). Mtu huyu alikuwa na msaada alioutegemea sana Mu’awiyah, naye Mu’awiyah hakuamua kupigana vita hadi alipopata uhakika wa kushirikkiana naye.
Chifu huyu aliyepotoshwa alipotambua ya kwamba ‘Ammar bin Yasir alikuwa pamoja na Sayyidna Ali (a.s.) alichanganikiwa mno. Makachero wa Mu’awiyah walijaribu kuyafanya mambo kuwa yenye kutia shaka kwa chifu huyu, na wakasema: “Hakuna suala lolote kuhusu ‘Ammar kuwapo Siffin.

Watu wa Iraq hawajali kuhusu kuzusha uwongo kama huo.” Hata hivyo Dhul Kalaa’ hakushawishika. Alimgeukia Amr Aas na kumwuliza “Je, Mtume hakusema maneno haya na haya kuhusu Ammar?” Ibn Aas akamjibu akasema: “Ndio, alisema hivyo, lakini kwa hakika ‘Amar hayuko kwenye jeshi la Ali.” Akasema: “Nitalichunguza jambo hili mimi mwenyewe.” Kisha aliwatuma watu fulani kuithibitisha hali hiyo. Mu’awiyah na ‘Amr bin Aas walitambua katika hali hii ngumu kuwa kama Dhul Kalaa atagundua kuwako kwa Ammar kwenye jeshi la Ali au juu ya kuuawa kwake kishahidi akiwa kwenye huduma ya Ali, waweza kutokea mgawanyiko kwenye jeshi la watu wa Shamu. Hivyo basi, kwa kulizuia hili, huyu chifu maarufu wa Syria aliuawa kwa njia isiyoeleweka.3

Hadithi hii ni maarufu mno miongoni mwa wanachuoni wa Hadithi wa kawaida na wale walio maarufu zaidi kiasi kwamba haihitaji kunukuliwa hapa taarifa yoyote ya kulithibitisha jambo hili. Ahmad bin Hanbal amenakili hivi: “Alipouawa ‘Ammar katika vita vya Siffin, Amr bin Hazm alimjia ‘Amr bin Aas na kumwambia: “Ammar ameuawa, na Mtume alisema kuhusiana naye kwamba kikundi cha madhalimu kitamwua.” Amr bin Aas alilia na akaisoma aya isemayo: “Sisi tunatoka kwa Allah na Kwake tutarejea.(2:156) na akampasha Mu’awiyah taarifa hii. Mu’awiyah akasema: “Sisi si wauaji wa ‘Ammar. Yeye ameuawa na Ali na marafiki zake, waliokuja pamoja naye na wakamweka mbele ya panga zetu.”4

Hata hivyo, ni dhahiri kwamba tafsiri hii ya uwongo iliyotolewa na Mu’awiyah, mwana wa Abu Sufyani ili kuzipumbaza akili za askari wa Shamu haiwezi kukubalika hata kidogo katika baraza la Allah Mwenye nguvu zote, na kila mtu mwenye hekima anaweza kuelewa vizuri ya kwamba hoja yake haina msingi hata kidogo.

Yaya Mwenye Huruma Zaidi Kwa Mtoto Kuliko Mama Yake.

Hatukuweza kupata sentensi iliyo bora zaidi ya hii ili kuionyesha tabia ya mwanahistoria5 wa karne ya nane Hijiriya aliyechagua kumuunga mkono Mu’awiyah na kuandika hivi:

“Si muhimu kwamba, kwa sababu Mtume (s.a.w.w.) amewataja wauaji wa ‘Ammar kuwa madhaalimu, basi wawe ni makafiri kweli, kwa sababu ingawa wameichagua njia isiyo sahihi na wakapigana dhidi ya Ali, lakini kwa vile waliichukua hatua hii kuhusiana na dini yao katika usahihi wa kitendo chao (Ijtihaad), hivyo haiwezekani kuibatilisha au kuwaita makafiri.”

Anaongezea kusema hivi: “Alichomaanisha Mtume kwa yale maneno yasemayo: “Ammaar anawaita Peponi, lakini wale wauaji wa ‘Ammar wanamwitia Motoni ni kwamba, Ammar anawaita kwenye kuushuhudia Upweke wa Allah na kuungana (na hii ndio hiyo pepo yenyewe), lakini wauaji wa ‘Ammar wanajitahidi kumpa Mu’awiyah ubora kuliko Ali, ambaye anastahili zaidi kuwa khalifa, na hivyo basi wanaunda utawala kwenye kila moja ya mikoa ya Kiislamu na matokeo yake ni kwamba unakuwapo ufa mpana mno miongoni mwa Waislamu, ingawa wao wenyewe wanaweza kuwa hawakutambua ya matokeo kama hayo (na huo ndio Moto wenyewe).”

Kwa kadiri tutakavyofikiria kuhusu ni jina gani tuipe tafsiri hii, hatuwezi kulipata jina lolote lile lifaalo ila lile la kuzibatilisha mambo. Licha ya ujuzi kiasi hiki waliokuwanao kikundi hiki cha watu wenye kuasi katika kubatilisha na kugeuza mambo na kuyafanya yawe uwongo, hawakuweza kuukana utabiri uliotabiriwa juu yao na Mtume (s.a.w.w.), na wanahistoria kama Ibn Kathir wameifanya kazi ya yaya aliye na huruma zaidi kwa mtoto kuliko mama wa mtoto yule, na wakakimbilia kwenye kuubadili ukweli ambao wao wenyewe hawakuwa wakiutambua.
Ahmad bin Hanbal anasema: “Watu wawili walimjia Mu’awiyah na kila mmoja wao alidai kwamba amemua ‘Ammar. Mwana wa Amr bin Aas (Abdullah) akasema: “Mmoja wenu ambakishe mwenziwe kwa kuwa nilimsikia Mtume akisema kwamba ‘Ammar atauawa na kikundi cha madhalimu.”

Mu’awiyah akamwambia Abdullah: “Kama sisi ni kikundi cha madhalimu, basi ni kwa nini umejiunga nasi?” Akamjibu akisema: “Siku moja baba yangu ‘Amr alilalamika dhidi yangu kwa Mtume (s.a.w.w.) na Mtume akaamrisha nimtii baba yangu. Hivyo basi, mimi niko pamoja nawe lakini sipigani.6

Udhuru wa Abdullah ni kama tafsiri ya Ibn Kathir asemaye kwamba Mu’awiyah alipigana vita vile kwa msingi wa ijtihad na imani, ingawa upo ukweli kwamba alikosea katika (kuifanya) ijtihad yake hii,7 kwa sababu mtu kumtii baba yake ni muhimu pale tu inapokuwa matokeo yake sio ya kuiasi sheria ya dini. Qur’ani Tukufu inasema: “. . .Na ikiwa watakushikilia unishirikishe Mimi na usiyokuwa na ujuzi nayo, basi usiwatii.......” (Sura al-Ankabut, 29:8).

Hali kadhalika ijtihad (kutoa maoni yake mtu) ni sahihi pale tu yanapokosekana masimulizi ya dhahiri ya Mtume (s.a.w.w.), vinginevyo ijtihad ya watu kama vile Mu’awiyah na ‘Amr bin Aas, yenye kuipinga Hadith ya dhahiri ya Mtume (s.a.w.w.) si sahihi na ni batili. Na kama mlango wa ijtihad uko wazi katika hali hiyo, itakuwa muhimu kwetu kuwasamehe washirikina na wanafiki wote kwa kufanya kampeni dhidi ya Mtume (s.a.w.w.) na Uislamu, na vile vile hatuna budi kusema kwamba watu kama vile Yazid na Hajjaj walikuwa na haki katika kuimwaga damu ya watu wachamungu na wasio na makosa wa taifa hili, na vile vile walikuwa na haki ya kupata malipo mazuri kwa kitendo chao hicho.Ujenzi wa msikiti ulimalizika na kila mwaka eneo lake lilipanuliwa. Vile vile palitengenezwa mahali penye mwinuko kandoni mwa msikiti ule kwa ajili ya Muhajiriin wasio na msaada na masikini, ili kwamba waweze kuishi hapo, na Ubadah bin Saamit aliamrishwa kuwafundisha kusoma na kuandika Qur’ani.

Udugu – Dalili Kuu Kabisa Ya Imani

Kukusanyika kwa Waislamu mjini Madina kuliifungua sura mpya kwenye maisha ya Mtume (s.a.w.w.). Kabla ya kuwasili kwake pale, alikuwa akijishughulisha katika kuzivutia nyoyo na katika kuibalighisha dini yake, lakini tangu siku ile na baadae, ilikuwa muhimu kwamba auhami uhai wake pamoja na ule wa wafuasi wake kama mtawala mwenye uzoefu na asiwaruhusu maadui wa ndani na wa nje kuingia kwenye jamii ya Waislamu. Kwenye kiungo hiki, alikabiliwa na matatizo makuu matatu:

1. Hatari kutoka kwa Waquraishi na wenye kuabudu masanamu wengine wa Rasi ya Uarabuni.

2. Wayahudi wa Yathrib walioishi mjini mle na nje yake, na waliokuwa na utajiri na mali nyingi sana.

3. Tofauti zilizokuwapo baina ya wale wafuasi wake.

Kwa vile Muhajiriin na Ansar wamekulia kwenye mazingira mawili tofau- ti, ilikuwapo tofauti kubwa sana baina ya njia zao za kufikiria na utamaduni. Kisha yalikuwamo yale makundi mawili ya Ansar (yaani Bani Aws na Bani Khazraji) yaliyokuwa yakigombana kwa kipindi cha miaka mia, wakiwa maadui wakuu wao kwa wao. Kutokana na hatari na tofauti zote hizi haukuwepo uwezekano wowote ule wa kuishi maisha ya amani ya kidini na kisiasa.

Hata hivyo, Mtume (s.a.w.w.) aliyashinda matatizo yote haya katika hali ya hekima kamili; kuhusu yale matatizo mawili ya kwanza alichukua hatua ambazo maelezo yake kwa kirefu tutayaeleza baadae, na kuhusu zile tofauti baina ya wafuasi wake aliziondoa kwa hekima kamili na unyofu.

Aliamrishwa na Allah kujenga udugu baina ya Muhajiriin na Ansar. Siku moja akiwa kwenye mkutano mkuu aliwageukia wafuasi wake na akasema: “Sasa hamna budi kuwa ndugu katika dini kwa jozi.” Maelezo kamili juu ya watu waliokuwa ndugu wao kwa wao yameandikwa na wanahisto- ria wa Kiislamu akiwamo Ibn Hisham.8

Hivyo basi, kwa njia hii, Mtume (s.a.w.w.) aliweza kudumisha umoja wa Waislamu kisiasa na kiroho na umoja huu ulimwezesha kufikiria jinsi ya kuyatatua yale matatizo mawili mengine.

Tofauti Kubwa Mbili Za Sayyidna Ali (A.S.)

Wengi wa wanahistoria na wanahadithi wa Kishia na Kisunni wamezitaja sifa tofauti kuu mbili za Sayyidna Ali (a.s.) ambazo tutaziandika hapa kwa ufupi. Mtume (s.a.w.w.) alijenga udugu baina ya jozi ya wawili miongoni mwa masahaba zake mia tatu kutokana na Muhajiriin na Ansar, na kumwambia kila mmoja wao kwamba alikuwa ni ndugu wa mtu huyu. Alipomaliza kuujenga udugu ule, Sayyidna Ali (a.s.) akiwa anatokwa na machozi alimwambia Mtume (s.a.w.w.): “Umejenga udugu baina ya masa- haba zako lakini mimi hukunifanya ndugu wa yeyote yule.” Kusikia hivyo Mtume (s.a.w.w.) alimgeukia Sayyidna Ali (a.s.) na kumwambia: “Wewe u ndugu yangu mimi, hapa duniani na kesho Akhera.”

Qanduzi amelinukuu tukio hili kwa kirefu zaidi na anasema kwamba Mtume (s.a.w.w.) alimjibu Sayyidna Ali (a.s.) akisema: “Ninaapa kwa jina la Allah Mwenye nguvu zote (Aliyeniteuwa niwaongoze watu) nilili- ahirisha suala la udugu wako kwa sababu ya kwamba mimi nilitaka niwe ndugu yako wakati nilipokwisha kujenga udugu baina ya wale wote. Daraja lako kwangu ni kama lile la Harun na Musa, ila tu kwamba hapatakuwapo Mtume mwingine baada yangu. Wewe ni ndugu yangu na mrithi wangu.”9

Hata hivyo, Ibn Kathir aliutilia shaka usahihi wa tukio hili.10 Lakini kwa vile shaka yake ni matokeo ya fikira zake maalum na si tofauti na udhuru ambao alioutoa kwa niaba ya Mu’awiyah na wasaidizi wake, tunaacha kuyanakili maelezo yake na kuyakanusha.

Sifa Nyingine Ya Saidina Al I (A.S)

Ujenzi wa msikiti ulimalizika. Zilikuwako nyumba za Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na za masahaba kuuzunguka msikiti ule. Vile vile zilikuwako nyumba ambazo milango yao ilielekea msikitini, na ambazo wakazi wake waliingia msikitini kupitia milango ile. Mara kwa ghafla ilikuja amri kutoka kwa Allah kwamba milango yote inayoelekea msikitini ifungwe ila ule wa nyumba ya Sayyidna Ali (a.s.). Baadhi ya watu walikuwa wenye wasiwasi juu ya jambo hili na wakadhania ya kwamba kule kuubakisha mlango wa Sayyidna Ali (a.s.) kulifanyika kwa misingi ya hisia.

Ili kuwaelimisha watu wale juu ya jambo hili Mtume (s.a.w.w.) alitoa hotuba, pamoja na mambo mengine alisema: “Sikutoa amri ya kuifunga wala kuifungua milango kwa kupenda kwangu mwenyewe. Kwa kweli jambo hili lilikuwa ni amri itokayo kwa Allah nami sina lolote jingine ila kuitimiza amri hiyo.”

Kwa kifupi ni kwamba, kwa kuudumisha udugu wa Kiislamu, Mtume (s.a.w.w.) aliziondoa tofauti baina ya wafuasi wake zilizokuwepo kwa miaka mingi na matokeo yake ni kwamba moja ya matatizo hayo lilitatuliwa.

Tatizo la pili lilikuwa lile la Wayahudi wa Madina. Waliishi mjini na nje ya mji wa Madina nao walikuwa wameshachukua udhibiti wa uchumi na biashara za mji ule.
Mtume (s.a.w.w.) alitambua kabisa kwamba mpaka pale matatizo ya ndani yatakapotatuliwa na kuupata ushirikiano wa Wayahudi wale ndipo ataweza kujenga umoja wa kisiasa kwenye makao makuu ya serikali yake, na kama si hivyo basi mche mchanga wa Uislamu hautakuwa, naye hataweza kufikiria juu ya hatua zozote zile kuhusu wenye kuabudu masanamu wa rasi ile, hasa wale Waquraishi (yaani lile tatizo la kwanza). Vile vile alitambua kwamba ni mpaka pale tu amani na utulivu vitakapotawala ndani ya serikali, itakuwa haiwezikani kuihami serikali ile kutokana na maadui wa nje.

Katika siku za mwanzo za kuwasili kwa Mtume (s.a.w.w.) mjini Madina maelewano yalikuwapo baina ya Waislamu na Wayahudi katika hali fulani, kwa sababu jamii zote mbili zilimwabudu Allah na ziliipinga ibada ya masanamu na Wayahudi walifikiria kwamba kama Uislamu ungalipata nguvu wao wangalikuwa salama kutokana na mashambulio ya Wakristo wa Kirumi. Zaidi ya hapo ni kuwa, uhusiano na mapatano ya tangu kale yalikuwapo baina yao kwa upande mmoja, na Bani Aus na Bami Khazraj kwa upande mwingine.

Kuhusiana na mambo haya Mtume (s.a.w.w.) aliandika mkataba kwa ajili ya kusimamisha umoja baina ya Wahajirina na Ansar, (wa kabila la Aws na Khazraji) na Wayahudi wa Madina nao pia walisaini mkataba huo na Mtume (s.a.w.w.) alikubali kuiheshimu dini yao na mali zao katika hali walizokubaliana. Waandshi wa wasifu wa Mtume (s.a.w.w.) wameandika maelezo kamili ya mkataba huo.11

Kwa vile mapatano haya ni maandiko ya kihistoria yaliyo hai na yenye kuonyesha wazi wazi jinsi Mtume (s.a.w.w.) alivyoiheshimu misingi ya uhuru, utaratibu na haki katika maisha, basi kwa njia ya mapatano haya akajenga umoja ulioungana dhidi ya mashambulizi ya nje, hapa chini tunayataja baadhi ya mambo yake yaliyo muhimu ikiwa ni ushahidi wa ushindi wa kisiasa katika zama zile za serikali mpya ya Uislamu.

Mkataba Mkuu Wa Kimaandishi Katika Historia

Kwa Jina la Allah, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu. Huu ni mkataba uliofikiwa na Muhammad, Mtume wa Allah baina ya Waislamu Waquraishi na wa Yathrib na wale watu waliowafuata na kusimama pamoja nao kwa ajili ya jihadi.

Sehemu Ya Kwanza

1. Wanaosaini mkataba huu wanaunda taifa moja. Kuhusiana na dia (malipo ya damu). Muhajiriin wa kikuraishi wanaruhusiwa kuifuata desturi yao ya tangu kale iliyokuwapo kabla ya Uislamu. Kama yeyote miongoni mwao atamuua mtu mwingine au akiwa mateka watalipa dia kwa kusaidiana na kumnunua yule mateka.

2. Bani Awf (kabila la Ansar) wanaweza pia kuzihami njia zao za maisha kama watakavyofanya Muhajirin wa kiquraishi na kwa pamoja wanaweza kulipa fidia kwa ajili ya kuachiwa kwa watu wao waliotekwa. Baada ya hapo makabila mengine ya Ansar ambayo ni Bani Sa’idah, Bani Harith, Bani Jasham, Bani Najjar, Bani ‘Amr bin Awf, Bani Nabit na Bani Aws, wamekumbushwa na kuwajibishwa kwa kila mmoja wao kwamba kwa pamoja watalipa dia na kuwakomboa mateka wao kwa kuwalipa fidia.

3. Waislamu watawajibika kuwasaidia maskini na kumsaidia muumini kuhusiana na gharama kubwa awajibikazo kuzilipa katika kulipa dia au fidia ya mateka.

4. Waislamu wachamungu watapaswa kuungana dhidi ya mtu mwenye kuasi au atendaye ukatili na dhuluma, japo mkosefu huyo awe mwana wa mmoja wao.

5. Hakuna yeyote mwenye madaraka ya kufanya mapatano na mtumwa wa Kiislamu au mtoto wa kiislamu bila ya ruhusa ya bwana wake au baba yake mtoto.

6. Muumini hatakuwa na haki ya kumuua muumini mwingine aliyemwua kafiri. Vile vile hana haki ya kumsaidia kafiri dhidi ya Mwislamu.

7. Mkataba wa Allah na ahadi yake kwa Waislamu wote ni moja. Kwa sababu hiyo, hatimaye aliye mdogo zaidi miongoni mwao anayo haki ya kulichukua jukumu kwa ajili ya mapatano na makafiri.

8. Waislamu ni marafiki na wasaidizi wa wao kwa wao.

9. Kila mmoja miongoni mwa Wayahudi wenye kutufuata sisi na akasilimu, atakuwa na haki ya kuupata msaada wetu na haitakuwapo tofauti baina yake na Waislamu wengine, na hakuna yeyote atakayekuwa na haki ya kumwonea au kumchochea yeyote mwingine kumwonea au kusaidia adui yake.

10. Waislamu hawana budi kuungana wakati wa kufanya mkataba wa amani na hakuna Mwislamu yeyote awezaye kufanya mapatano ya amani bila ya kushauriana na Mwislamu mwingine ila kwa misingi ya haki na usawa.

11. Vikundi vya Waislamu vitawajibika kwenda kupigana jihadi kwa zamu ili kwamba damu yao inayomwagika kwa ajili ya Allah igawanywe kwa usawa.

12. Waislamu wanayo dini bora zaidi na sheria madhubuti.

13. Hakuna yeyote miongoni mwa washirikina (wa Madina) aliye na haki ya kuyahami maisha na mali za washirikina wa kiquraishi au kufanya mapatano nao au kumzuia Mwislamu katika kuwazidi nguvu.

14. Kama Mwislamu akimwua Mwislamu mwingine, bila ya sababu ya haki, na kosa lake hilo likithibitika kisheria, atauawa, isipokuwa kama warithi wa yule aliyeuawa wakisamehe, na kwenye hali yoyote kati ya hizo mbili ni wajibu wa Waislamu kuungana dhidi ya muuwaji yule.

15. Yeyote yule ayatambuaye haya yaliyomo kwenye mkataba huu na akamwamini Allah na Mtume wake, hataruhusiwa kumsaidia mzushi au mkosefu au kumpa hifadhi, na mwenye kumsaidia yeye, ataipata ghadhabu ya Allah, na fidia na gharama havitakubalika kutoka kwake.

16. Mamlaka ya kumaliza tofauti zozote zile zitokeazo, daima yatakuwa na Allah na Mtume Wake Muhammad (s.a.w.w.).

Sehemu Ya Pili

17. Wakati Waislamu watakapokuwa wakipigana kwa ajili ya ulinzi wa mji wa Madina, Wayahudi watalipa fungu la gharama za vita kwa Waislamu.

18. Wayahudi wa kabila la Bani ‘Awf, (kabila moja la Ansar) ni washirika wa Waislamu, nao ni sawa na taifa moja. Waislamu na Wayahudi wako huru katika masuala ya sheria na dini zao. Watumwa wao hawaachwi kwenye kifungu hiki, yaani wao nao wako huru katika mambo ya sheria yao, isipokuwa wale wahalifu na madhalimu ambao ambao wanajiangamiza wao wenyewe na familia zao (kwa sababu kwa kawaida watu wa familia ya dhalimu humfuata yeye). (Lengo la kutoachwa huku ni kwamba uhusiano na umoja viweze kudumu baina ya Wayahudi hao na Waislamu wasio waonevu na wadhalimu).

19. Wayahudi wa makabila ya Bani Najjar, Bani Harith, Bani Sa’adah, Bani Jasham, Bani Aws, Bani Tha’labah na Bani Shatibah ni kama Wayahudi wa kabila la Bani Awf na hakuna tofauti baina yao katika mambo ya haki na fursa. Kabila la Jafnah ni tawi la kabila la Tha’labah na taratibu zitumikazo kwa Wayahudi wa kabila la Bani Awf vile vile hutumika kwa hili tawi la Bani Shatibah.

20. Watiaji saini wa mapatano haya hawana budi kuyafanya maadili yao kushinda dhidi ya dhambi zao.

22. .Wale ambao wamefanya mapatano na kabila la Bani Tha’alabah watakuwa wako sawa nao.

23. Wale walio kwenye hali ya urafiki na Wayahudi, na wasiri wao, watabakia kuwa kwenye hali ile.

24. Hakuna mwenye haki ya kuuacha mkataba huu bila ya ruhusa ya Muhamad.

25. Kutoka miongoni mwa watu hawa damu yoyote ya mtu aliyejeruhiwa (achilia mbali yule aliyeuawa) ni yenye kuheshimika. Yeyote yule auwaye mtu atawajibika kulipa dia na hatimaye kujiangamiza mwenyewe na watu wa familia yake, isipokuwa pale tu yule muuwaji awapo ni mtu aliyeonewa.

26. Gharama za vita zitakazopiganwa na Wayahudi na Waislamu kwa pamoja ni wajibu wa kila mmoja wao, na wakati mtu yeyote mwingine apiganapo dhidi ya kundi lililo kwenye mkataba huu ni jukumu lao kupigana naye kwa pamoja.

27. Uhusiano wa pande zihusikazo na mapatano haya unategemeana na wema na ni muhimu kwamba wajiepushe na maovu.

28. Hakuna mtu atakayemuonea mwenziwe aliyefanya mapatano naye, vinginevyo, yule aliyeonewa italazimu kusaidiwa.

29. Sehemu ya ndani ya mji wa Madina panatangazwa kuwa ‘Haram’ kwa wale waliousaini mkataba huu.

30. Uhai wa majirani na wa wale waliopewa kimbilio ni kama uhai wetu wenyewe, na wasinyanyaswe.

31. Hakuna mwanamke atakayepewa kimbilio bila ya idhini ya watu wake.

32. Muhammad ndiye msuluhishi wa kuamua tofauti zitakazotokea baina ya watiaji saini wa mapatano haya wawe ni Waislamu au wasio Waislamu. Allah Yu pamoja naye yule ayaheshimuye zaidi mapatano haya.

33. Waquraishi na wale wafanyao mapatano nao hawatapewa kimbilio (hifadhi).

Sehemu Ya Tatu

34. Watiaji saini wa mapatano haya watabeba jukumu la pamoja kwa ajili ya ulinzi wa Yathrib.

35. Pale Waislamu wanapowaomba Wayahudi kufanya amani na adui; hawana budi kuukubali mpango huo, na Waislamu nao hawana budi kuukubali mpango wa aina hiyo ufanywao na Wayahudi, ila tu pale uwapo ukweli wa kwamba adui yule anaipinga dini ya Uislamu na uhubiri wake.

36. Wayahudi wa kabila la Aws, wawe ni watumwa au mabwana, wao nao wamo kwenye mapatano haya.

Sehemu Ya Nne

37. Mapatano haya hayamwungi mkono mwonevu au mtenda majinai.

38. Yeyote yule asaliaye mjini Madina atahifadhiwa humo, na yeyote atakayeondoka humo anahifadhiwa ili mradi tu si mwonevu na mtenda majinai.

Mkataba huu ulihitimishwa kwa sentensi ifuatayo: “Allah ndiye Mlinzi wa walio wema na wachamungu na Muhammad ni Mtume wa Allah.”12
Mapatano haya ya kisiasa na Sheria ya msingi ya Uislamu ya wakati ule, vilivyoelezwa kwa kifupi hapo juu, ni mfano halisi wa mtazamo wa uhuru wa imani, ustawi wa jamii na umuhimu wa ushirikiano katika mambo ya pamoja katika Uislamu, na zaidi ya yote umeifafanua mipaka na mamlaka ya kiongozi na wajibu wa watia saini wote.

Wayahudi wa kabila la Bani Quraydha, Bani Nuzayr na Bani Qaynqaa hawakushiriki kwenye maamuzi ya mkataba huu, na ni Wayahudi wa mak- abila ya Aws na Khazraji tu waliokuwa washirika wa mapatano haya. Hata hivyo, baadae watu hawa walifikia mapatano na Mtume (s.a.w.w.) na sentensi zifuatazo zimechukuliwa kutoka kwenye yaliyomo ndani ya map- atano hayo:

“Mtume (s.a.w.w.) anayafanya mapatano haya na makundi matatu kwa matokeo kwamba hawatamdhuru yeye na marafiki zake kwa ndimi na kwa mikono yao, na kwamba hawatatoa silaha na wanyama wa kupanda kwa maadui wake. Iwapo watakwenda kinyume na yaliyomo katika mkataba huu, basi Mtume (s.a.w.w.) atakuwa na haki ya kumwaga damu yao, kuzichukua mali zao na kuwateka wanawake na watoto wao”. Kisha Hay bin Akhtab alisaini kwa niaba ya Bani Nuzayr, Ka’ab bin Asad kwa niaba ya Bani Quraydha na Mukhayriq kwa niaba ya Qaynaqaa.13

Kwa njia hii Yathrib na maeneo tegemezi yaliyokuwa karibu ya mji ule yalitangazwa kuwa eneo la amani na usalama na ‘Haram.’ Sasa ulikuwa umefika muda ambapo kwamba Mtume (s.a.w.w.) afikirie njia na jinsi ya kulitatua lile tatizo la kwanza, yaani lile la Waquraishi, kwa sababu kwa kadiri adui huyu asimamavyo kwenye njia yake, basi Mtume (s.a.w.w.) hataweza kufaulu katika kuubalighisha Uislamu na kuzisimamia sheria zake.

Vizuizi Vya Wayahudi

Mafundisho matukufu ya Uislamu na maadili mema na tabia za Mtume (s.a.w.w.) vikawa sababu vya kuongezeka kila siku kwa idadi ya Waislamu. Hali yao ya kijeshi, kiuchumi na kisiasa pia viliongezeka kwa kiasi fulani. Haya maendeleo ya mfululizo ya Uislamu, yalizua fadhaa ya ajabu na kutokutulia katika duru za kidini za Wayahudi, kwa sababu walifikiria kwamba kwa nguvu zao wangaliweza kumvutia kwao Mtume (s.a.w.w.) na katu hawakudhania ya kwamba siku moja, nguvu zake mwenyewe zitazipita hata zile za Wayahudi na za Wakristo.

Kwenye hali ile walianza kujitia kwenye matendo yanayofarakisha watu. Kwa kuuliza maswali ya kidini yaliyo magumu walijitahidi kuitikisa itikadi ya Waislamu juu ya Mtume (s.a.w.w.), lakini silaha hizi zilizo butu hazikuwa na athari yoyote juu ya safu madhubuti za Waislamu. Sehemu kubwa ya midahalo hii imesimuliwa kwenye Qur’ani Tukufu kwenye Sura Al-Baqarah na Suratun- Nisa.

Kwa kuzichunguza hizi Sura mbili zilizotajwa, wasomaji wapenzi wanaweza kuuelewa vizuri uadui na ukaidi wa Wayahudi.

Walipewa jibu la waziwazi kwa kila swali waliloliuliza lakini ili kuepuka kuubeba mzigo wa Uislamu, waliujibu kwa ukaidi ule mwito wa Mtume (s.a.w.w.) wa kuwaita kwenye Uislamu: “Nyoyo zetu zimezibwa wala hatuyafikirii yale uyasemayo kuwa ni sahihi.”

Abdullah Bin Salaam Asilimu

Midahalo hii ilizidisha uadui na mfundo wa Wayahudi, lakini katika muda fulani midahalo hii ikawa chanzo cha kusilimu kwa baadhi ya watu. Abdullah bin Salaam alikuwa mmoja wa makasisi na wanachuoni wa Wayahudi. Alisilimu baada ya kufanya majadiliano marefu na Mtume (s.a.w.w.).14 Mara baada ya hapo mwanachuoni wao mwingine aliyeitwa Makhyriq naye alijiunga naye.

Abdullah alifikiria ya kwamba kama jamaa zake wakifahamu kusilimu kwake, watamtusi na kumkashifu. Hivyo basi, alimwomba Mtume (s.a.w.w.) kwamba asitangaze kusilimu kwake mpaka watu wa kabila lake waithibitishe elimu na uchamungu wake. Hivyo basi, Mtume (s.a.w.w.) aliwauliza Wayahudi: “Nini maoni yenu juu ya Abdullah?” Wote wakajibu wakasema: “Yeye yu kiongozi wetu wa dini na mwana wa kiongozi wetu wa dini na mwanachuoni mkuu.” Kisha Abdullah akaenda kwenye eneo lake na kuwaarifu watu wa kabila lake kuhusu kusilimu kwake. Mara tu baada ya taarifa za kusilimu kwake kuenea miongoni mwa Wayahudi, walisisimka kwa hasira. Ingawa kwa pamoja waliithibitisha elimu na uchamungu wake masaa machache tu yaliyopita, vivyo, sasa wote wakaanza kumwita mtu asiye na tabia njema na mjinga.15

Mpango Mwingine Wa Kuipindua Serikali Ya Kiislamu

Mdahalo na maswali magumu ya Wayahudi hayakuiimarisha tu itikadi ya Waislamu juu ya Mtume (s.a.w.w.), lakini vile vile yalikuwa sababu ya sifa zake tukufu na elimu ya dini kueleweka kwa kila mtu. Matokeo ya mijadala hii ni kwamba makundi mbalimbali ya wenye kuabudu masanamu na Wayahudi walimwelekea Mtume (s.a.w.w.). Hivyo basi, ili kulifikia lengo lao, Wayahudi waliunda mpango mwingine na wakarejea kwenye mpango wao wa “wagawe ili uwatawale”.

Walifikiria kuuhuisha ule uadui wa kale wa miaka 120 wa Bani Aws na Bani Khazraji uliotoweka chini ya msaada wa imani, Uislamu, udugu na usawa. Walitaka kwamba mapigano na kumwaga damu vianze miongoni mwa safu za Waislamu nao. Kwa njia hii wangaliweza kuliwa na miali ya migongano ya ndani.

Siku moja baadhi ya watu wa kabila la Bani Aws na Bani Khazraji walikuwa wamekaa pamoja. Umoja na udugu wa watu wa kundi hili, ambao hadi siku chache zilizopita walikuwa maadui wenye kiu ya damu dhidi ya wao kwa wao, ulichukiwa mno na Myahudi mfitini ambaye alijiunga nao kwa nia ya kuanza hila ya uovu ya kujenga mfarakano na ugomvi miongoni mwa Waislamu. Aliwakumbusha watu wa makabila ya Bani Aws na Bani Khazraji zile kumbukumbu chungu za vita za zamani baina ya hayo makabila mawili na akasimulia kwa kirefu matukio ya vita ya Bua’ath, ambavyo hatimaye Bani Aws waliibuka kuwa washindi. Aliyatanua mno haya matukio ya tangu kale na yaliyosahaulika kiasi kwamba ugomvi na majisifu yakaanza baina ya yale makundi mawili ya Waislamu (Aws na Khazraji).

Kulikuwa na uwezekano kabisa kwamba vita vya mara kwa mara vingeweza kuanza, lakini wakati ule taarifa zilimfikia Mtume (s.a.w.w.) naye akautambua ule mpango mwovu wa Wayahudi. Hivyo akafika mahali pale akiwa pamoja na baadhi ya masahaba wake na akayakumbusha yale makundi mawili kuhusu lengo la Uislamu na ule mpango wake mtukufu, alisema: “Uislamu umekufanyeni ndugu wa kila mmoja wenu na umeufanya uadui wote na mifundo kuwa vitu vya kale vilivyosahauliwa.” Aliwashauri kwa muda fulani hivi na akawakumbusha matokeo ya ugomvi wao. Mara wote wakaanza kulia na kutokwa na machozi na wakakumbatiana ili kuuimarisha tena udugu wao na wakamwomba Allah awaghufirie.

Hila za Wayahudi hazikuishia hapo, bali walikikuza kiwango cha makri, majinai na kuvunja ahadi, na wakadumisha mawasiliano maalum na makafiri wa makabila ya Bani Aws na Bani Khazraji, na pia wakawasiliana na wale watu wenye akili ya kigeugeu kwenye mambo ya Uislamu na dini yao. Kwa dhahiri wakaingilia kwenye vita walizopigana Waislamu dhidi ya Waquraishi, na walijishughulisha mno katika kuyakuza maslahi ya waabudu masanamu.

Kushirikiana kwa dhahiri na kwa siri kwa Wayahudi na washirikina wa Kiquraishi, kulizaa vita vya kumwaga damu baina ya Waislamu na Wayahudi ambavyo hatimaye viliishia kwa kuwang’oa Wayahudi kutoka Madina. Maelezo kwa urefu ya matukio haya yatatolewa baadae pamoja na matukio ya mwaka wa tatu na wa nne wa Hijiriya, na itadhihirika jinsi gani Wayahudi walivyomlipa Mtume (s.a.w.w.) kwa matendo yake mema yaonekanayo dhahiri kwenye ile mikataba miwili aliyofanya nao, kwa wao kuvunja ahadi, matendo yao ya dhahiri dhidi ya Uislamu na Waislamu wenyewe, makri zao dhidi ya Mtume (s.a.w.w.) na kuwapa msaada maadui zake, na hivyo wakamlazimisha Mtume (s.a.w.w.) kwa matendo yao, kuipuuza ile mikataba tuliyoitaja hapo juu.

 • 1. Siiratu Halabi, Juzuu 2, uk. 76-77.
 • 2. Siiratu Halabi, Juzuu 2, uk. 76-77
 • 3. Mustadrakul Haakim, Juzu 3, uk. 385.
 • 4. Musnad Ibn Hanbal, Juzu 2, uk. 199.
 • 5. Al-Badaayah wan Nihaayah, Juzuu 3, uk. 218.
 • 6. Musnad Ibn Hanbal, Juzuu 2, uk. 162.
 • 7. Hapa hakuna suala la kupatia au kukosea (katika muktadha wa ijtihad) kwa sababu hii ni ijithad ya makosa kuanzia mwanzo, tena kwa makusudi - Mhariri.
 • 8. Siiratu Ibn Hisham, Juzuu 1, uk.25- 126.
 • 9. Yanabi'ul Mawaddah, Juzuu 1, uk. 55.
 • 10. Al-Bidayah wan-Nih?yah, Juzuu 2, uk. 226.
 • 11. Siiratu Ibn Hisham, Juzuu 2, uk. 501.
 • 12. Siiratu Ibn Hisham, Juzuu1, uk. 503 -504; na Al-Ammaal, uk. 125 na 202.
 • 13. Bihaarul-Anwaar, Juzuu 19, uk. 110-111.
 • 14. Maelezo juu ya majadiliano haya na Mtume (s.a.w) tazama Biharul Anwwar, Juzuu 19, uk. 131.
 • 15. Siirah-i Ibn Hisham, Juzuu1, uk 516.