Sura Ya 27: Baadhi Ya Matukio Ya Mwaka Wa Kwanza Na Wa Pili Hijiriya

Hapa tunakusudia kuzieleza siri za nyororo ya kudhihiri kwa hali ya kivita kulikoendelea tangu kwenye mwezi wa nane wa mwaka wa kwanza wa Hijiriya hadi kwenye mwezi wa Ramadhani wa mwaka wa pili, na kwa hakika zilikuwa harakati na mbinu za kijeshi za kwanza za Waislamu.

Tafsiri sahihi na maelezo ya siri za matukio haya tutaweza kuyapata pale tu tutakapoweza kupata maelezo ya matukio haya kutoka kwenye vitabu vya historia1 bila ya kuongeza au kutoa chochote kile, na kuyaweka maoni ya kiuamuzi ya wanachuoni watafiti wa historia mbele ya msomaji. Haya yafuatayo hapa chini ndio kiini cha matukio haya:

1. Si zaidi ya miezi nane kupita tangu Mtume (s.a.w.w.) kuwasili Madina, ilipombidi kuitoa bendera ya kwanza kwa amir jeshi wake shujaa aliyeitwa Hamza bin Abdul Muttalib na akawapeleka, chini ya uamiri jeshi wake askari thelathini wapandao wanyama kutoka miongni mwa Muhajirina hadi kwenye pwani ya Bahari ya Sham, iliyokuwa njia iliyotumiwa na misafara ya Waquraishi. Mahali paitwapo ‘Ais’ alikutana na msafara wa Waquraishi uliokuwa na watu mia tatu, ukiongozwa na Abu Jahl. Hata hivyo, kutokana na upatanishi wa Majdi bin Amr, aliyekuwa na uhusiano mwema na pande zote mbili, waliachana na hatimaye wale askari wa Kiislamu wakarudi Madina.

2. Sambamba na kupelekwa kwa kikosi hiki cha watu, Ubaydah bin Harith bin Abdul Muttalib alipelekwa kwenye msafara wa Waquraishi pamoja na askari sitini au themanini wapandao wanyama kutoka miongoni mwa Muhajiriin. Alikwenda hadi kwenye bahari iliyoko chini ya Thaniyatul Murrah na akakutana na ule msafara wa Waquraishi wenye watu mia mbili ukiongozwa na Abu Sufyani. Hata hivyo, makundi mawili haya yaliachana bila ya kundi moja kulipiga jingine. Ni Sa’ad bin Abi Waqas pekee aliyetupa mshale. Zaidi ya hapo Waislamu wawili waliokuwamo kwenye msafara wa Abu Sufyani walijiunga na kile kikosi kilichotumwa na Mtume (s.a.w.w.).

3. Mara nyingine tena Sa’ad bin Abi Waqas alitumwa kwenda Hijaz na watu wengine nane. Vile vile alirudi bila ya kukabiliana na mtu yeyote. Katika istilahi za wanahistoria, vita ambavyo Mtume (s.a.w.w.) hakushiriki zinaitwa “sariyyah na zile alizoshiriki zinaitwa “Ghaz’wah.”

4. Kwenye mwezi wa kumi wa ‘kuhajiri’, Mtume (s.a.w.w.) alimkabidhi Sa’ad bin Ma’az mambo ya kidini ya mji wa Madina na yeye mwenyewe akaenda hadi akafika Abwa’ akifuatana na kundi la Muhajiriin na Ansar kuufuatia msafara wa Waquraishi na pia kufanya mapatano na kabila la Bani Hamza. Hakukutana na ule msafara wa Waquraishi lakini aliyafanya yale mapatano na lile kabila.

5. Kwenye mwezi wa kwanza wa mwaka wa pili alimteua Saa’ib bin Uthman au Sa’ad bin Ma’aaz kuwa mwakilishi wake mjini Madina na yeye mwenyewe akaenda hadi akafika Bawaat akifuatana na watu mia mbili kuufuata msafara wa Waquraishi. Hata hivyo hakuona msafara ule uliokuwa na watu mia moja, na uliokuwa ukiongozwa na Umayyah bin Khalaf, na akarudi Madina.

6. Katikati ya mwezi wa Jamadiul Awwal ilifika taarifa ya kwamba msa- fara wa Waquraishi ulikuwa ukitoka Makka kwenda Shamu ukiwa chini ya uongozi wa Abu Sufyani. Mtume (s.a.w.w.) alimteua Aba Salmah kuwa mwakilishi wake mjini Madina, yeye mwenyewe akaenda hadi akafika ‘Dh?tul Ashirah’ akifuatana na kikundi cha watu. Aliusubiri ule msafara pale hadi mwanzoni mwa Jamadiul Aakhir lakini hakuweza kuukamata. Wakati wa kukaa kwake pale alifanya mapatano na watu wa kabila la Bani Madlaj. Maelezo ya mapatano haya yameandikwa kwenye vitabu vya historia.
Ibn Athir anasema: “Kwenye sehemu hii, ambayo Mtume (s.a.w.w.) na masahaba wake walikuwa wakisubiri, siku moja Mtume (s.a.w.w.) alikuja kitandani pa Ali na Ammar na akawakuta wakiwa wamelala. Mtume (s.a.w.w.) aliwaamsha wote wawili. Wakati ule aliona ya kwamba chembe chembe ndogo za vumbi zilikuwamo kichwani na usoni mwa Sayyidna Ali (a.s.). Alimgeukia Sayyidna Ali (a.s.) na kumwambia: “Ewe Abu Turaab! Una nini?”

Tangu pale Sayyidna Ali (a.s.) alifahamika miongoni mwa Waislamu kwa jina la ‘Abu Turaab’ (baba wa vumbi), kisha akawageukia wote wawili na akawaambia: “Je, mnapenda nikuambieni ni nani walio waovu zaidi hapa duniani?” wakajibu wakisema: “Ndio, ewe Mjumbe wa Allah.” Akasema: “Watu waovu zaidi katika uso wa ardhi ni wawili. Wa kwanza alikuwa yule aliyekata miguu ya yule ngamia-jike wa (Mtume) Salehe. Na mwingine ni yeye yule atakayepiga dharuba ya upanga kwenye fuvu la kichwa chako (akamsoza Sayyidna Ali a.s kwa kidole) na kuzipaka rangi ndefu zako kwa damu ya kichwa chako.”2

7. Baada ya kupoteza matumaini ya kuupata msafara ule, Mtume (s.a.w.w.) alirejea Madina. Hata hivyo, ilikuwa bado hazijapita siku kumi tangu awasili mjini mle, zilipofika taarifa ya kwamba Karz bin Jaabir amewateka na kuwachukua ngamia na kondoo wa Madina. Ili kumfuatia mteka nyara huyu, Mtume (s.a.w.w.) akifuatana na kikundi cha watu, alikwenda hadi wakafika kwenye eneo la ‘Badr’ lakini ilimbidi kurudi bila ya kupata ushindi wowote. Baada ya hapo alikaa mjini Madina hadi mwishoni mwa Sha’aban.

8. Kwenye mwezi wa Rajab wa mwaka wa pili wa Hijiriya Mtume (s.a.w.w.) alipeleka watu themanini kutoka miongoni mwa Muhajiriin chini ya uamiri jeshi wa Abdallah bin Jahash. Wakati wa kuondoka kwao alimpa barua yule amiri jeshi na kusema: “Ifungue barua hii baada ya kusafiri kwa siku mbili na kisha utende kufuatana na hayo uliyoagizwa kwenye barua hii,3 na usimlazimishe mtu yeyote katika wafuasi wako kuifanya kazi fulani.” Baada ya kusafiri kwa muda wa siku mbili aliifungua ile barua na akaona ya kwamba Mtume (s.a.w.w.) alimpa amri zifuatazo: “Utakapoitazama barua yangu endelea na safari yako na ukapige kambi kwenye nchi ya ‘Nakhlah’ iliyoko baina ya Makka na Taa’if na wasubiri hapo Waquraishi na uniarifu kuhusu vitendo vyao.”

Abdullah alitenda kama alivyoagizwa kwenye barua ile na wafuasi wake wote walimfuata na wakatua kwenye sehemu ile. Wakati ule ule, kwa ghafla ulitokea msafara wa Waquraishi uliokuwa ukitoka Taa’if kwenda Makka chini ya uongozi wa ‘Amr Khazrami. Vile vile Waislamu walikuwa wamepiga kambi karibu nao. Ili kuhakikisha ya kwamba adui haitambui siri yao walinyoa nywele za vichwa vyao, ili kutoa picha ya kwamba walikuwa wakienda Makka kufanya Hija ya Nyumba ya Allah. Sura zao ziliwaridhisha Waquraishi na wakaambiana: “Waislamu hawa wanakwenda kufanya ‘Umra’ na hawana lolote lile lihusianalo nasi.”

Wakati huu Waislamu walikusanyika kwa ajili ya kushauriana juu ya vita na wakaanza kubadilishana maoni. Hatimaye walitambua ya kwamba iwapo wangesubiri siku ile, ambayo ilikuwa siku ya mwisho ya Rajab, bila shaka ule mwezi mtakatifu utamalizika na kama wakati huo huo Waquraishi wataondoka pale, wataingia kwenye eneo la ‘haram’, na kupigana kwenye eneo lile pia kulikuwa kumeharimishwa. Hivyo basi, wakaamua ya kwamba ni bora wapigane kwenye ule mwezi mtakatifu kuliko kupigana mwenye eneo la ‘Haram’. Hivyo kwa kuwashitukiza maadui walimwua ‘Amr Khazrami4 yule kiongozi wa msafara ule, kwa mshale. Kuhusu wafuasi wake, wote walikimbia ila Uthman bin Abdullah na Hakam bin Kaysaan ambao walitekwa na Waislamu. Abdullah bin Jahash akazileta bidhaa za Waquraishi na wale mateka wawili mjini Madina.

Mtume (s.a.w.w.) aliudhika alipogundua ya kwamba yule amiri jeshi wa kikundi kile alizihalifu amri zake na amepigana kwenye mwezi mtakatifu badala ya kutekeleza wajibu wake. Alisema: “Mimi sikukuamrisha hata kidogo kupigana katika mwezi mtakatifu.”

Waquraish walilitumia tukio hili kuwa ni silaha ya propaganda na wakazieneza habari kwamba Muhammad amekiuka heshima ya mwezi mtakatifu. Wayahudi walilichukulia tukio hili kuwa ni ndege mbaya na wakataka kuleta matata. Waislamu walimkemea Abdullah na wafuasi wake. Mtume (s.a.w.w.) hakuzitwaa zile ngawira za vita naye alikuwa akisubiri ufunuo wa Allah. Mara kwa ghafla Malaika Mkuu Jibriil kaileta aya ifuatayo:

Wanakuuliza kuhusu kupigana vita katika mwezi mtakatifu. Sema: kupigana vita wakati huo ni dhambi kubwa. Lakini kuzuilia watu wasende katika njia ya Mwenyezi Mungu na kumkanusha Yeye, na kuzuilia watu wasende kwenye Msikiti Mtakatifu na kuwatoa watu wake humo, ni makubwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Na fitina ni mbaya zaidi kuliko kuuwa........” (Surat al- Baqarah, 2: 217)

Kwa aya hii Waquraishi wameambiwa ya kwamba kama Waislamu wamepigana vita kwenye mwezi mtakatifu na hivyo wakafanya jambo lisilo halali, lakini wao (Waquraishi) wametenda jinai kubwa ziadi kwa kuwa wamewatoa wakazi wa Masjidul Haraam (Waislamu) kutoka maskanini mwao na wakaunda uovu kwa kuwaonea na kuwatesa. Kutokana na majinai yao haya yaliyo makuu, hawana haki ya kuikana hatua waliyoichukua Waislamu.

Kufunuliwa kwa aya hii kulitia uhai mpya kwenye kundi la Waislamu. Mtume (s.a.w.w.) akazigawa zile ngawira. Waquraishi walipendelea kuwanunua wale watu wawili waliotekwa na Waislamu. Akilijibu ombi lao, Mtume (s.a.w.w.) aliwajibu akisema: “Hamna budi kuwarudisha askari wawili wa Kiislamu mliowateka kutokana na kuwa mbali kutoka kwa wenzao ili mimi nami niwaachie mateka wenu. Na kama mkiwaua, sisi nasi tutawaua watu wenu.” Waquraishi walilazimika kuwarudisha wale mateka wa Kiislamu na kutokana na kurudi kwao vile vile zilitolewa amri za kurudishwa kwa wale mateka wa Kiquraishi. Hata hivyo, mmoja wao alisilimu na yule mwingine akarudi Makka.

Nini Lengo La Hizi Harakati Za Kijeshi?

Lengo hasa la kuvipeleka hivi vikundi na kufanya mapatano ya kijeshi na makabila yalioishi karibu na ile njia ya kibiashara ya watu wa Makka lilikuwa ni kuwajulisha Waquraishi juu ya nguvu ya kijeshi na uwezo wa Waislamu, hasa pale Mtume (s.a.w.w.) binafsi aliposhiriki kwenye harakati hizi na kukaa kwenye njia ile ya kibiashara ya Waquraishi akifuatana na kundi kubwa la watu. Huyu kiongozi maarufu wa Uislamu alitaka kuifanya serikali ya Makka itambue kwamba njia zao za kibiashara, zote zimekuwa chini ya utawala wa waislamu na wangaliweza kuisimamisha biashara yao wakati wowote watakapopenda.

Biashara ilikuwa kitu kilicho muhimu sana kwa maisha ya watu wa Makka, na zile bidhaa zilizokuwa zikisafirishwa kutoka pake kwenda Taa’if na Sham, zilijenga ule msingi wenyewe hasa wa uhai wa uchumi wao. Na kama njia hizi zikitishiwa na majeshi ya adui hodari na washirika wake kama vile Bani Zumrah na Bani Madlaj, msingi wa maisha yao ungalianguka.

Lengo la kuupeleka huu ujumbe wa kijeshi na vikundi kwenye njia za maadui lilikuwa kwamba, Waquraishi waweze kujua ya kwamba njia zao za kibiashara zimeangukia mikononi mwa Waislamu na kama waking’ang’ania kwenye ukaidi wao na wakazuia mahubiri ya Uislamu na wakawatesa Waislamu waishio mjini Makka, basi mishipa yao ya uhai itakatwa kwa nguvu ya Uislamu.

Kifupi lengo lilikuwa kwamba Waquraishi wapaswe kulitafakari jambo hili na kwa kuyatilia maanani mambo yote haya, watawaruhusu Waislamu kuuhubiri Uislamu kwa uhuru kabisa na watawafungulia njia ili wakafanye Hija ya Nyumba ya Allah na kuihubiri dini ya Allah, ili Uislamu uweze kuzivutia nyoyo kwa njia ya mafundisho yake ya kiakili na matukufu, na nuru ya dini hii iweze kuenea kila mahali katika Rasi yote ya Uarabuni chini ya himaya ya uhuru.
Mhadhiri anaweza kuwa fasaha na mwenye kuvutia sana, na mkufunzi anaweza kuwa mwaminifu na mwenye uthabiti, na isipokuwa pale wapatapo mazingira huru na hadi pale misingi ya uhuru na demokrasia itakapodumishwa, kabla ya hapo hawataweza kupata ushindi halisi katika kuwaongoza wenzao na kuyahubiri maoni yao.

Zana kuu zaidi iliyokingama kwenye njia ya maendeleo ya Uislamu ni kukosekana kwa uhuru kamili na ile hali ya mazingira ya kuhuzunisha iliyosababishwa na Waquraishi. Hivyo basi, njia pekee ya kukiondolea mbali hiki kizuizi ilikuwa kuzitishia zile njia za uchumi wao zilizokuwa mishipa ya uhai wao, na mpango huu ulipewa sura ya kivitendo kwa njia ya harakati za kivita na mikataba ya kijeshi.

Mtazamo Wa Mustashirik Kuhusu Matukio Haya

Mustashirik walikuwa wamekosea vibaya kabisa katika kuyachanganua matukio haya na wamesema mambo yaliyo kinyume na misingi ya Uislamu na malengo na shabaha za dini hii tukufu. Wanasema kwamba lengo la Mtume (s.a.w.w.) lilikuwa kuziongeza nguvu zake kwa njia ya kuteka nyara na kunyang’anya mali za Waquraishi.

Hata hivyo, maoni haya hayapatani na moyo wa hali halisi ya watu wa Yathrib, kwa sababu kuteka nyara na unyang’anyi ni matendo ya makabila ya mabedui yanayoishi majangwani, mbali kabisa na sehemu zilizostaarabika, na Waislamu wa Yathrib walikuwa na desturi ya kilimo na ambao katu hawakuwahi kushambulia msafara wowote katika maisha yao yote na hawakuwahi kuteka nyara mali za makabila yaliyokuwa yakiishi nje ya mazingira yao.

Mapigano baina ya Aws na Khazraji yalikuwa mambo ya ndani na moto wake ulikuwa unawashwa na Wayahudi ili kuyakuza maslahi yao na kuidhoofisha nguvu ya Waarabu. Sasa kuhusu Waislamu wa kundi la Muhajiriin waliohusiana na Mtume (s.a.w.w.) ingawa mali zao zimenyang’anywa na watu wa Makka, hawakuwa na mpango wa kuzifidia hasara zao. Jambo hili lathibitishwa na ukweli uliopo kwamba hawakuushambulia msafara wowote wa Waquraishi baada ya vita vya Badr. Zaidi ya hapo vingi katika vikundi hivi vilipelekwa kukusanya habari na kutoa taarifa muhimu. Vikundi vya watu thelathini au sitini na nane kwa kweli havikuwa na nguvu kiasi cha kuweza kunyang’anya, wakati idadi ya wale waliokuwa wakilinda msafara ilikuwa kubwa zaidi kuliko hii.

Wakati mwingine wanasema: “Lengo lilikuwa kulipiza kisasi kwa Waquraishi, kwa sababu Mtume na sahaba zake walipokuwa wakiyafikiria yale maonevu na mateso ambayo walikuwa wamepatishwa, hisia zao za kulipiza kisasi na heshima ya kikabila zilichochewa, nao wakadhamiria kuzichomoa panga zao ili kulipiza kisasi na kumwaga damu.”

Mtazamo huu vile vile ni dhaifu na usio na msingi kama ule wa kwanza, kwa kuwa ushahidi mwingi wa kutosha unapatikana kwenye maandishi ya historia ambayo hupinga mtazamo huu na huonyesha kwamba lengo hasa la kuvipeleka vikundi hivi halikuwa kujiingiza katika mapambano ya vita au kumwaga damu au kulipiza kisasi. Yafuatayo hapa chini ni nukta ambazo hukanusha mtazamo huu wa mustashirik:

1. Kama lengo la Mtume (s.a.w.w.) katika kuvipeleka vikundi hivi ingalikuwa ni vita na kujipatia ngawira basi ingalikuwa muhimu kwamba angaliongeza idadi yao, na kupeleka jeshi lenye silaha za kutosha kule kwenye eneo la pwani. Hata hivyo, ukweli uliopo ni kwamba alipeleka watu thelathini tu pamoja na Bwana Hamza bin Abdul Muttalib, watu sitini na Ubaydah bin Harith na idadi isiyoweza kuthaminiwa iliyokwenda pamoja na Sa’ad bin Abi Waqqas. Idadi ya waquraishi walioteuliwa kulinda msafara ule ilikuwa kubwa maradufu kuliko watu hawa.

Hamza alikabiliwa na Waquraishi mia tatu na Ubaydah alikabiliwa na Waquraishi mia mbili. Na hasa pale Waquraishi walipotambua ya kwamba Waislamu wamefanya mapatano na makabila mbalimbali waliongeza idadi ya walinzi wa misafara yao. Hivyo basi, kama wale maamiri jeshi wa Kiislamu walipelekwa kupigana, kwa nini ilitokea kwamba hakuna hata tone moja la damu lililomwagwa na katika safari moja pande zote mbili hazikutaka kupambana kutokana na kuingiliwa na Majdi bin ‘Amr?
2. Ile barua ambayo Mtume (s.a.w.w.) alimpa Abdullah bin Jahash yaonyesha dhahiri kwamba kupigana hakukuwa lengo hata kidogo, kwa sababu ndani ya barua ile alimpa maelekezo yafuatayo: “Piga kambi kwenye nchi ya Nakhlah iliyoko baina ya Makka na Taa’if na uwasubiri waquraishi hapo na uniarifu lengo lao.”

Barua hii yaonyesha dhahiri kwamba Abdullah hakupelekwa kule kupigana, kwa kuwa kazi pekee aliyopewa ilikuwa kukusanya taarifa na yale mapigano pale Nakhlah, ambayo matokeo yake ni kuuawa kwa ‘Amr bin Khazrami, yalikuwa ni matokeo ya kushauriana kwake na wafuasi wake juu ya vita. Hivyo Mtume (s.a.w.w.) alipotambua kule kumwagika kwa damu, kulikotokea, alimkaripia na kumkemea vikali Abdullah na wafuasi wake na akasema: “Sikukuamrisha hata kidogo kupigana vita.”

Ni dhahiri kwamba lengo la misafara yote hii au mingi kati yao lilikuwa ni kutafuta taarifa tu, na hata kidogo hatuwezi kusema kwamba Hamza bin Abdul Muttalib alipelekwa pamoja na watu thelathini kwenda kupigana vita. Ama kuhusu Abdullah bin Jahash alipelekwa na watu thelathini kukusanya taarifa, na hali ni kwamba kile kikundi kilichopelekwa kukusanya taarifa kilikuwa ni kikubwa mara tatu zaidi kuliko kile ambacho, kwa mujibu wa kauli za mustashirik kilipelekwa kupigana vita.

Na sababu ya kila mara kuwachagua Muhajirin katika kuunda vikundi hivi ilikuwa kwamba pale Aqabah, Ansar walifanya mapatano ya ulinzi na Mtume (s.a.w.w.) nao waliahidi kuulinda uhai wake litokeapo shambulio la adui. Hivyo basi, yeye hakutaka kuwatwika jukumu la safari zile mwanzoni kabisa, na yeye mwenyewe akabakia mjini Madina. Hata hivyo, baadae, wakati yeye mwenyewe alipotoka mjini mle Madina, vile vile aliwachukua baadhi ya Ansar pamoja naye ili kuimarisha uhusiano baina yao na Muhajirina. Ni kwa sababu hii kwamba Muhajiriin na Ansar waliipata heshima ya kufuatana naye kwa pamoja wakati wa safari zake kwenda Bawaat na Dhaatul Ashirah.

Kutokana na hoja ya mustashirik juu ya kupelekwa kwa vikundi hivi, na kwa kuchunguza yale yaliyosemwa hapo juu kwa uaminifu, mtazamo wao juu ya misafara hii aliyoshiriki Mtume (s.a.w.w.) vile vile hubatilika, kwa sababu wale waliofuatana naye kwenda Bawaat na Dhaatul Ashirah hawakuwa Muhajiriin tu lakini vile vile kikundi cha Ansar kilikwenda naye. Na pale ambapo Ansar walikuwa hawajafanya mapatano ya kijeshi naye, vipi angeliweza kuwaita kwenye vita na umwagaji wa damu?

Vita ya Badr, ambavyo maelezo yake yatatolewa baadaye vinashuhudilia kauli yetu. Mtume (s.a.w) hakuamua kupigana vita hivi mpaka Ansar waliporidhia kushiriki kwenye vita vile. Na sababu ya ‘kwa nini’ wanahistoria wa Kiislamu waliipa misafara hii jina la Ghaz’wa’ ni kwamba walitaka wakusanye matukio yote haya chini ya kichwa cha habari kimoja na si vinginevyo, basi lengo hasa la harakati hizi halikuwa utekaji nyara wala ngawira za kivita.

  • 1. Siiratu Ibn Hisham, Juzuu 2, uk. 222. na kuendelea; Biharul Anwar, Juzuu 19, uk.186- 190; Imtaa'ul Asmaa', uk. 51; Tarikhul Kamil, Juzuu 2, uk. 77-78; na Maghaazil- Waqidi, Juzuu 1, uk. 9-19.
  • 2. Tarikhul Kamil, Juzuu 3, uk. 78.
  • 3. Inasemekana kwamba hadi kwenye vita vya pili vya Dunia wanajeshi waliomaliza mafunzo yao ya kijeshi walipewa, pamoja na cheti, barua iliyofung- wa ikiwa ni amana ya kijeshi, na walielekezwa kuifungua barua ile pale tu wawapo kwenye mkusanyiko mkuu wakiwa tayari kwenda vitani na kutenda lile waliloambiwa kwenye barua ile.
  • 4. Baadhi ya wanahistoria wamelitaja jina lake kuwa ni Waaqid bin Abdullah na wengine wakasema kwamba ni 'Amr bin Abdullah.