Sura Ya 28: Matukio Ya Mwaka Wa Pili Hijiriya

NDOA: Mwelekeo wa tamaa za kujinsia hujitokeza mwilini mwa kila mtu katika hatua maalum ya maisha na wakati mwingine inatokea kwamba kutokana na kukosa mafunzo yastahiliyo, na kwa sababu ya upatikanaji wa njia za kuitoshelezea hamu ya kingono, kijana hujikuta akiwa ukingoni mwa genge. Katika hatua hii, hutokea mambo yasiyostahili kutokea.

Ndoa ndio njia bora zaidi ya kuulinda utakatifu wetu, kulingana na utaratibu wa kimaumbile Uislamu nao umemfanya mwanaume na mwanamke kuwa na wajibu wa kuoana katika hali zilizoainishwa, na umetoa maelekezo mbalimbali kuhusiana na jambo hili. Qur’ani Tukufu inasema:
“Na waozeni wajane miongoni mwenu na wema katika watumwa wenu na wajakazi wenu. Wakiwa mafakiri Mwenyezi Mungu atawatajirisha kwa fadhila Yake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa Mwenye kujua.” (Suratun-Nur, 24:32).

Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) anasema: “Yeyote yule apendaye kutokea mbele ya Allah akiwa na nafsi safi basi naaoe.” 1
Vile vile amesema: “Katika Siku ya Hukumu nitajifaharisha juu ya nyumati nyinginezo kutokana na idadi ya wafuasi wangu.”

Matatizo Ya Ndoa Katika Zama Hizi

Matatizo ya ndoa katika zama hizi si kidogo. Wanaume na wanawake wa siku hizi hawako tayari kuwa na ndoa kutokana na hali zisizofaa na mbaya. Vyombo vya habari vya kitaifa vinaonesha idadi ya matatizo katika mtandao wa familia, lakini matatizo mengi huzungukia zungukia katika nukta hii, nayo ni kwamba wanaume na wanawake wa jamii yetu hawalengi katika kuunda familia ambayo itahakikisha ustawi wao halisi.

Baadhi ya watu wanataka kuzishika nafasi kubwa katika jamii na utajiri kwa njia ya ndoa. Jambo ambalo watu hulipa mazingatio madogo mno siku hizi ni usafi (wa matendo) na adabu, na ingawa katika baadhi ya nyakati linaweza likafikiriwa, kwa kawaida huwa halipewi umuhimu. Uthibitisho wa jambo hili ni kwamba wanaume wanawapenda mno wasichana wa familia kubwa ingawa katika mtazamo wa kimaadili hawafai hata kidogo, na wengi wa wasichana wema na wachamungu wanaishi kwenye umaskini mkubwa sana katika baadhi ya sehemu za jamii na hakuna yeyote anayewajali.

Zaidi ya yote hayo, ziko zile sherehe za harusi ambazo ni chanzo kikuu cha usumbufu kwa upande wa bwana harusi na vilevile kwa upande wa wazazi wa bibi harusi. Tatizo kuu jingine ni suala la mahari. Kutokana na matatizo haya, wako watu wengi wasiopenda ndoa na huzimalizia tamaa zao za kingono kwa njia zisizo halali.

Mtume (S.A.W.W) Alifanya Kampeni Dhidi Ya Matatizo Haya

Haya ni baadhi ya matatizo ya kijamii ambayo yako kwa kiasi kikubwa katika kila jamii na hata zama za uhai wa Mtume (s.a.w.w.) nazo hazikuwa huru kutokana nayo. Watu watukufu wa Uarabuni waliwaoza mabinti zao kwa wale watu walio sawa nao katika nasaba, nguvu na utajiri, na waliwakataa wachumba wengine.

Kwa sababu ya desturi hii ya tangu kale watu wa familia tukufu, walitamani kumwoa Bibi Fatimah (a.s.) binti mpenzi wa Mtume (s.a.w.w.), wao walikuwa wakidhania kwamba Mtume (s.a.w.w.) hatakuwa mkali katika mambo ya ndoa ya binti yake, kwa sababu, kutegemeana na fikra zao walikuwa na kila kitu kiwezacho kumvutia bibi harusi na baba yake, na hata hivyo, Mtume (s.a.w.w.) hakuwa mkali kuhusiana na ndoa za mabinti zake wengine (Ruqayyah, Zainab, n.k).

Hata hivyo, wao walikuwa hawauelewi ukweli kwamba binti huyu wa Mtume (s.a.w.w.) alikuwa tofauti na wale wengine. Alikuwa ni binti aliyekuwa na cheo kikubwa mno kwa mujibu ya aya (ya Surah Aali Imran, 3:61) ihusianayo na ‘Mubahilah’ (kuapizana na Wakristo).

Wale waposaji walikosea katika fikara zao, kwa sababu hawakuelewa ya kwamba ni yule mtu aliyekuwa kama yeye katika mambo ya uchamungu na imani ndiye tu angaliweza kuwa sawa na mwenzi kwa ajili yake. Kufuatana na aya ya ‘Tatw’hir’ (Utakaso – Surah al Ahzaab 33:33).

Bibi fatimah (a.s.) ametangazwa kuwa yu safi kabisa kutokana na dhambi zote, hivyo, na mumewe naye vilevile ni lazima awe ‘Ma’asum’ (Asiye na dhambi). Kuonyesha utajiri na wa vitu vya kidunia sio kipimo cha usawa. Ingawa Uislamu unapendekeza kwamba mabinti waozwe kwa wanaume walio sawa nao, lakini vile vile imeelezwa ya kwamba huo usawa wao uwe ni katika mambo ya imani na Uislamu.

Mtume (s.a.w.w.) ameelekezwa na Allah kuwaambia hao wachumba kwamba ndoa ya Fatimah itafanyika kwa mujibu wa amri ya Allah na katika kuutoa udhuru huu, kwa kiasi fulani aliweza kuondoa kutoelewa kwao. Masahaba wa Mtume (s.a.w.w.) walitambua ya kwamba ndoa ya Bibi Fatimah (a.s.) halikuwa jambo rahisi na hakuna awezaye kumuoa kwa utajiri wake.
Vile vile walielewa kwamba mume wake anaweza tu kuwa yule mtu aliye wa pili kutoka kwa Mtume (s.a.w.w.) katika ukweli, imani, ubora wa kiroho na ubora wa tabia, na mtu wa aina hiyo hawezi kuwa yeyote mwingine ila Sayyidna Ali (a.s.). Ili kulijaribu jambo hili, walimshawishi Sayyidna Ali (a.s.) kumchumbia binti wa Mtume (s.a.w.w.). Sayyidna Ali (a.s.) naye alipenda kufanya hivyo na alikuwa akisubiri tu kuyatimiza yale masharti muhimu kabla ya kwenda kuchumbia.

Amiri wa Waumini alikwenda mbele ya Mtume (s.a.w.w.) binafsi. Utulivu na haya vilikuwa vimemzidi nguvu. Aliinamisha kichwa chake na ilielekea kwamba alitaka kusema jambo fulani lakini akiona aibu. Mtume (s.a.w.w.) alimpa moyo wa kusema na akalidhihirisha lengo lake kwa sentensi chache tu. Aina hii ya uchumba ni dalili ya uaminifu. Hata hivyo, taasisi zetu za mafunzo bado hazijafaulu kuwafunza wachumba watarajiwa uhuru huu ulioandamana na uchamungu, imani na uaminifu.

Mtume (s.a.w.w.) alikubali kulitimiza ombi la Sayyidna Ali (a.s.) na akasema: “Subiri kidogo ili nimweleze binti yangu jambo hili.” Alipomweleza Fatimah (a.s.) jambo hili (yeye Fatimah a.s) alinyamaza kimya kabisa. Hapo Mtume (s.a.w.w.) akasema: Allah Yu Mkubwa! Kimya chake kinamaana ya kukubali.” Hata hivyo, katika siku zile Sayyidna Ali (a.s.) hakuwa na chochote ila upanga na deraya.

Alishauriwa na Mtume (s.a.w.w.) kuiuza ile deraya ili aweze kuzilipa gharama za doa ile. Kwa moyo mmoja akaiuza ile deraya na akamletea Mtume (s.a.w.w.) fedha alizopata kutokana na mauzo yale. Mtume (s.a.w.w.) alimpa Bilal gao (ukofi) mmoja la pesa zile bila ya kuzihesabu aende akamnunulie bibi Zahraa (Fatimah a.s) manukato. Zile zilizosalia alizikabidhi kwa Abu Bakr (r.a) na Ammar ili waende kwenye mitaa ya maduka ya Madina wakanunue vifaa vya muhimi kwa maisha ya wanandoa wale. Mambwana hawa wawili waliamka na kama walivyoamrishwa na Mtume (s.a.w.w.) wakaenda wakanunua vitu vifuatavyo (ambavyo kwa hakika ndivyo vilivyokuwa mahari ya bibi Fatimah Zahraa (a.s.) na kuvileta kwa Mtume (s.a.w.w.).

Mahari Ya Binti Wa Mtume (S.A.W.W)

Gauni lililonunuliwa kwa dirham saba, mtandio ulionunuliwa kwa dirhamu moja; joho jeusi la kuogea, ambalo halikutosha kuufunika mwili mzima; kitanda kilichotengenezwa kwa mbao na nyuzi za mtende; magodoro mawili ya katani ya Misri, ambayo moja kati yao lilikuwa la sufi na jingine lilitengenezwa kwa nyuzi za mtende; mito minne ambayo miwili kati ya hiyo ilitengenezwa kwa sufi na ile mingine miwili ilitengenezwa kwa nyuzi za mtende; pazia, mkeka wa hajr; mawe mawili ya kusagia; kiriba kimoja cha kubebea maji; bakuli la mti la kutilia maziwa; mtungi, vibia, vyungu; bangili mbili za fedha na chombo kimoja cha shaba.

Mtume (s.a.w.w.) alipoviona vitu hivi alisema: “Ee Mola wangu! Yabariki maisha ya wale ambao vyombo vyao vingi ni vya udongo.”2

Mahari ya binti yake Mtume (s.a.w.w.) yastahili kufikiriwa. Mahari yake haikuzidi ‘Mahrus sunnah’ ambayo ni Dirham mia tano3.

Kwa kweli huu ulikuwa ni mfano kwa wengine yaani kwa wasichana na wavulana ambao wanalia kutokana na mzigo mzito wa mahari na wakati mwingine wakayaachilia mbali majukumu ya ndoa kwa sababu hiyo.

Kimsingi maisha ya ndoa hayana budi kuwa yenye kufaa na matamu kwa njia ya uaminifu na huba, kwani vinginevyo, mahari kubwa haileti nuru yoyote ile kwenye maisha.

Siku hizi walezi wa bibi harusi humtwisha mkwe wao mzigo mzito wa mahari ili kuimarisha hali ya msichana ili kwamba, yule mume siku moja asije akakimbilia kwenye talaka kutokakana na choyo chake. Hata hivyo, kitendo hiki hakitupatii uhakika kamili wa kulifikia lengo tulilolitaja, na tiba ifaayo na ya kweli ya maradhi haya ni kuyatengeneza maadili ya mwanadamu. Mazingira yetu ya kitamaduni na kijamii hayana budi kuwa katika hali ya kwamba fikara za aina hii hazitii mizizi akilini mwa wanaume. Vinginevyo, wakati mwingine hutokea kwamba msichana hukubali kuiachilia mahari yake ili kuweza kuachana na mumewe.

Sherehe Za Ndoa

Baadhi ya watu walialikwa kutoka upande wa bibi harusi na bwana harusi, na Sayyidna Ali (a.s.) alitayarisha karamu (walimah) kwa heshima ya mwenzi wake mpenzi. Baada ya karamu kwisha, Mtume (s.a.w.w.) alimwita Bibi Fatimah (a.s.). Alikuja mbele ya Mtume (s.a.w.w.) akiwa ni mwenye kuona haya mno. Alipomtazama tu, mguu wake uliteleza na karibuni aanguke. Mtume (s.a.w.w.) akamshika mkono binti yake mpenzi na akamwombea dua akisema: “Allah na Akuhifadhi kutokana na mitelezo yote.”

Usiku ule Mtume (s.a.w.w.) alidhihirisha mno upendo na uaminifu, kiasi kisichoweza kuonyeshwa katika jamii za siku hizi ingawa zina maendeleo na mabadiliko. Mtume (s.a.w.w.) aliushika mkono wa binti yake na akauweka mkononi mwa Sayyidna Ali (a.s.) na akamwelezea kuhusu wema wa mumewe. Vile vile alizitaja sifa tukufu za binti yake na akasema kwamba: “Kama Ali asingalizaliwa, asingalikuwapo mtu yeyote wa kuwa sawa na yeye (Fatimah a.s). Kisha akawagawiya kazi ya nyumbani na majukumu ya maisha. Alimpa Bibi Fatimah (a.s.) mambo ya nyumbani na akamfanya Sayyidna Ali (a.s.) kuwa mwenye madaraka ya kazi za nje ya nyumba yao. Ndoa hii ilifanyika baada ya Vita vya Badr.4

Kufuatana na baadhi ya taarifa, kisha Mtume (s.a.w.w.) aliwaomba wanawake wa Muhajirin na Ansar kumzunguka yule ngamia jike wa binti yake na kumpeleka kwa mumewe na kwa hilo sherehe za ndoa ya huyu mwanamke mashuhuri zaidi hapa duniani zilifikia mwisho.

Hapa chini tunainukuu Hadih inayotoa dokezo la daraja kuu alilokuwa nalo huyu binti wa Mtume (s.a.w):

“Kwa kipindi cha miezi sita Mtume alikuwa akitoka nyumbani mwake wakati wa sala ya Alfajiri na kwenda msikitini na wakati huo akisimama mara kwa mara mbele ya nyumba ya Fatimah na kusema: “Enyi watu wa nyumba yangu! Hudhurieni kwenye sala. Allah Anataka kukuondoleeni kila aina ya uchafu, ninyi Ahlul Beit (watu wa nyumba).5

  • 1. Man la Yahdhurul Faqih, uk. 410.
  • 2. .Biharul-Anwaar, Juzuu 43, uk. 94; na Kashful Ghumah, Juzu 1, uk. 359.
  • 3. Wasa'ilush-Shi'ah, Juzuu 15, uk. 8.
  • 4. Biharul Anwar, Juzuu 48, uk. 79 na 111.
  • 5. Musnad Ahmad Ibn Hanbal, Juzuu 2, uk. 259.