Sura Ya 29: Mabadiliko La Qiblah

Ilikuwa bado haijapita miezi michache hivi tangu Mtume (s.a.w.w.) kuhajiria Madina wakati Wayahudi walipoamka kumpinga. Katika mwezi wa kumi na saba hasa tangu kuhajiri iliteremshwa amri ya Allah kwamba tangu pale na kuendelea, Qiblah cha Waislamu kiwe ni ile Ka’abah na watakaposali wazielekeze nyuso zao kwenye Masjidul Haram.

Maelezo Kamili Ya Tukio Hilo Hapo Juu:

Katika miaka kumi na tatu ya Utume wake, Mtume (s.a.w) akiwa mjini Makka, alikuwa akisali na kuuelekeza uso wake Baytul-Maqdis (Yerusalemu) na hata baada ya kuhajiri kwake kwenda Madina amri ya Allah ilikuwa ile ya kwamba Baytul-Maqdis iendelee kuwa Qiblah na Waislamu wanaposali wazielekeze nyuso zao kwenye Qiblah hicho hicho wanachozielekeza nyuso zao Wayahudi. Jambo hili, lenyewe lilikuwa aina fulani ya ushirikiano na njia ya kuzileta karibu hizi dini mbili – moja ikiwa ni ya kale na nyingine ikiwa ni mpya.
Lakini Wayahudi wakapatwa na woga kutokana na maendeleo ya Waislamu, kwa sababu ushindi wao uliokuwa ukiongezeka daima ulionyesha ya kwamba karibuni tu, dini ya Kiislamu itaenea katika Rasi zima na nguvu na ushawishi wa Wayahudi utakoma. Hivyo wakaanza kujitumbukiza katika matendo ya kuzuia ueneaji wa Uislamu na kuwadhuru Waislamu na yule kiongozi wao mtukufu kwa njia nyingi. Miongoni mwa vitu vingine waliuliza swali kuhusu kusali kwa kuelekea ‘Baytul-Maqdis’ na wakasema: “Muhammad anadai ya kwamba dini yake ni dini yenye kujitegemea na sheria yake inazipita sheria zote, lakini vivyo hana Qiblah chenye kujitegemea na anasali kwa kukielekea Qiblah cha Wayahudi.”

Habari hizi zilimuumiza Mtume (s.a.w.w.). Alitoka nyumbani mwake usiku wa manane na akatazama angani. Alikuwa akisubiri ufunuo. Wakati ule ule alifunuliwa amri kama ilivyo katika aya ifuatayo:
“Kwa yakini tukiona unavyogeuza uso wako mbinguni. Basi tutakuelekeza kwenye Kibla ukipendacho...” (Surat al-Baqarah, 2:144).

Kutokana na aya hii ya Qur’ani inaonekana kwamba kubadilika kwa Qiblah hakukufanyika tu kwa sababu za upinzani wa Mayahudi, bali kuna sababu nyingine za mabadiliko haya. Ilikuwa kwamba jambo hili lilikuwa na hali ya mtihani. Lengo lilikuwa kwamba waumini wa kweli na wale wasiokuwa waaminifu katika imani zao waweze kutambulika, na Mtume (s.a.w.w.) aweze kuwatambua vizuri watu hao, kwa sababu amri ya pili ambayo katika kuitii kwake mtu atageuza uso wake kwenye Masjidul Haraam wakati anaposali, ilikuwa ni ishara ya imani katika dini mpya, na kuiasi na kuichelewesha ni ishara ya ukigeugeu na unafiki. Qur’ani yenyewe inataja ukweli huu waziwazi kwenye aya ifuatayo: “. . . Na hatukukifanya Kibla ulichokuwa nacho ila tupate kumjua yule anayemfuata Mtume na yule anayegeuka akarejea nyuma. Na kwa yakini hilo lilikuwa jambo gumu isipokuwa kwa wale aliowaongoa Mwenyezi Mungu…” (Surat al-Baqarah, 2:143.

Hapana shaka, ziko sababu nyinginezo katika badiliko hili tunazozipata kwenye historia ya Uislamu na kutokana na kuzichunguza hali zilizokuwapo wakati ule kwenye Rasi ile, kwa mfano:

1. Ka’bah iliyokuwa imejengwa na Nabii Ibrahim (a.s.) ilikuwa ikiheshimiwa na jamii yote ya Waarabu. Kuifanya sehemu hiyo kuwa Qiblah kutazaa kuridhia kwa Waarabu kwa ujumla na kuwavutia kwenye Uislamu. Na isingelikuwako shabaha tukufu zaidi ya kwamba, washirikina wakaidi waliokuwa nyuma mno kwenye msafara wa ustaarabu, waweze kuipokea ile dini ya kweli, na Uislamu uweze kuenea kwenye sehemu zote za ulimwengu kupitia kwao.

2. Halikuwapo tegemeo kwamba Wayahudi wa siku zile wangalisilimu na hivyo basi ilionekana kwamba Waislamu wakae mbali nao kwa sababu wao walijiingiza kwenye vitendo vya kuizuia dini na waliupoteza muda wa Mtume (s.a.w.w.) kwa kuuliza maswali magumu, ambayo kwayo, kwa mujibu wa fikira zao walidhihirisha elimu na hekima zao. Badiliko la Qiblah lilikuwa moja ya midhihiriko ya kutafuta umbali na Wayahudi kama vile kufunga kulivyopigwa marufuku katika siku ya Ashurah (mwezi 10 Muharram) kwa lengo hilo. Kabla ya kuanza kwa Uislamu Wayahudi walikuwa na desturi ya kufunga kwenye siku ya Ashurah na Mtume (s.a.w.w.) na Waislamu nao waliamrishwa kufunga katika siku ile. Hata hivyo, hapo baadae amri inayohusu kufunga kwenye siku ya Ashurah iliondolewa na badala yake funga katika mwezi wa Ramadhani ikawajibishwa.

Hata hivyo, Uislamu ulio dini bora kuliko dini zote kwenye mambo yake yote, haunabudi kujidhihirisha katika njia ambayo, mambo ya ukamilifu na ubora wake viwe wazi kabisa. Kutokana na sababu hizi Malaika Mkuu Jibriil alikuja wakati Mtume (s.a.w.w.) alipokuwa tayari kaishazisali rakaa mbili za sala ya Adhuhuri na akambalighishia amri ya Allah kwamba tangu pale na kuendelea aelekee kwenye Masjidul-Haraam.

Katika baadhi ya masimulizi imesemwa kwamba, yule Malaika Mkuu aliushika mkono wa Mtume (s.a.w.w.) na akamgeuzia kwenye Masjidul Haraam. Wanaume na wanawake waliokuwamo mle msikitini walimfuata na tangu siku ile na kuendelea Ka’abah ikawa Qiblah cha kudumu cha Waislamu.

Elimu Ya Kimuujiza Ya Mtume (S.A.W.W)

Kufuatana na mahesabu ya wanajimu wa zamani, Madina iko kwenye nyuzi 25 za latitudo na nyuzi 75 za longitudo na nukta 20. Kwa mujibu wa mahesabu haya, mwelekeo wa Qiblah kama ulivyowekwa pale Madina usingalipatana na ‘Mihraab’ (mahali pa kusalia mbele ya msikiti; Kibla) ya Mtume (s.a.w.w.) ambayo bado iko kwenye sehemu yake ya awali. Tofauti hii ilikuwa yenye kushangaza kwa baadhi ya wataalamu na wakati mwingine walitoa maelezo ili kuondoa zile tofauti.

Hata hivyo, hivi karibuni Sardaar Kabuli, mwanasayansi maarufu alithibitisha, kufuatana na ukadiriaji wa siku hizi kwamba; Madina iko kwenye nyuzi 24 za latitudo na nukta 75 na nyuzi 39 za longitudo na nukta 59.1

Matokeo ya mahesabu haya hugeuka na kuwa hivi: Qiblah cha Madina huelekea nyuzi 45 kutoka ncha ya kusini na upatikanaji huu unalingana kabisa na mwelekeo wa Mihrab ya Mtume (s.a.w.w.). Jambo hili lenyewe ni muujiza wa kisayansi. Kwa sababu kwenye zama hizo, hazikuwapo zana za kisayansi na hakukuwapo kitu kama vile mahesabu ya kukokotoa.

Mtume (s.a.w.w.) alipokuwa akisali aligeuka kutoka Baytul-Maqdis na kuielekea Ka’abah katika njia ambayo haukuwapo ukoseaji japo ulio mdogo kutoka kwenye mwelekeo wa Ka’abah2 na kama tulivyoeleza hapo juu, Malaika Mkuu Jibriil alimshika mkono na kumgeuzia Ka’abah.3

  • 1. Tuhfatul Ajillah, fi Ma'rifatil Qiblah, uk. 71.
  • 2. Man la Yahzarul Faqih, Juzuu 1, uk. 88.
  • 3. Tukio la Mtume (s.a.w.w.) kugeuka kutoka Baytul Maqdis kuelekea kwenye Kaabah alipokuwa akisali, limenukuliwa na Hur Aamili katika Wasaa'il (Surah za Qiblah, Juzu 3, uk. 218).