Sura Ya 30: Vita Vya Badr

Vita vya Badr ni mojawapo ya vita vya Kiislamu vilivyo vikubwa na maarufu, na wale walioshiriki kwenye vita hivi wana heshima maalumu miongoni mwa Waislamu. Kila mara Mujahidiin wa Badr, mmoja au zaidi, aliposhiriki au alipotoa ushahidi juu ya jambo lolote lile watu walikuwa wakisema: “Ahhil Badr (watu wa Badr) kadhaa wanakubaliana nasi” neno ‘Ahlul Badr’ linatumiwa kwenye maandiko juu ya maisha ya masahaba zake Mtume (s.a.w.w.) kwa wale watu walioshiriki kwenye vita ya Badr, na sababu ya umuhimu wao utatambulika kutokana na maelezo marefu juu ya tukio hili.

Tayari tumeshaeleza kwamba katikati ya mwezi wa Jamadul Awwal mwaka wa pili wa Hijiria ilifika taarifa mjini Madina kwamba msafara mmoja ulikuwa ukisafiri kutoka Makka kwenda Sham ukiwa chini ya uongozi wa Abu Sufyan, na Mtume (s.a.w.w.) alikwenda hadi Dhaatul Ashirah kuufuatilia msafara huu na akakaa hapo akiusubiri hadi mwanzoni mwa mwezi uliofuatia, lakini hakuweza kuukamata. Wakati wa kurejea kwa msafara ule ulikuwa ukitambulika, kwa sababu mapema kwenye wakati wa kipupwe (autumn), misafara ya Waquraishi ilikuwa ikirejea kutoka Sham kuja Makka.

Kwenye kampeni zote, kupata taarifa ndio hatua ya kwanza ya kuelekea kwenye ushindi. Ni mpaka tu hapo amiri wa jeshi lolote lile awezapo kuitambua nguvu ya maadui, mahali walipojikusanyia na moyo wa kupigana wa wanajeshi wao ndipo anapoweza kushinda, la sivyo anaweza akashindwa kwenye mapigano ya awali kabisa.

Moja ya sera zipasikazo kusifiwa alizozitumia Mtume (s.a.w.w.) kwenye vita zote (ambazo maelezo yake yataelezwa baadae) ilikuwa ile ya kwamba alikuwa akikusanya taarifa juu ya nguvu ya adui na mahali alipo. Hadi hivi leo, suala la kukusanya taarifa lina muhimu sana kwenye vita za ulimwengu mzima pamoja na zile za ndani ya nchi moja. Kufuatana na kauli ya Allamah Majlisi1 Mtume (s.a.w.w.) alimtuma Adi (na kwa mujibu wa mwandishi wa ‘Hayaatu Muhammad’ kama alivyonakili kutoka kwenye vitabu vya historia, alimpeleka Talhah bin Ubaydullah na Sa’id bin Zayd) kukusanya taarifa juu ya njia na utaratibu wa msafara ule, idadi ya walinzi wake, na hali ya bidhaa zao.
Taarifa iliyopokelewa ilikuwa hivi:Ni msafara mkubwa na watu wote wa Makka walikuwa na mafungu kwenye bidhaa zake.Kiongozi wa msafara ule alikuwa ni Abu Sufyani na walikuwako watu wapatao arobaini wanaoulinda. Bidhaa hizo zilipakiwa kwenye ngamia elfu moja na thamani yake ni kama dinari elfu hamsini.

Kwa vile Waquraishi walikuwa wametaifisha mali za Waislamu Muhajiriin waliokiishi mjini Makka, ilikuwa inafaa tu kwamba Waislamu nao wazinyakue bidhaa zao, na kama wakishikilia kuzizuia mali za Waislamu Muhajiriin kutokana na uadui na ukaidi wao, basi Waislamu nao kwa kulipiza kisasi, wazigawe bidhaa zao miongoni mwao zikiwa ni kama ngawira za Vita.

Hivyo Mtume (s.a.w.w.) aliwageukia masahaba zake na kusema: “Enyi watu! Huo ni msafara wa Waquraishi. Mnaweza kwenda nje ya mji wa Madina kuzikamata mali za Waquraishi, inawezekana kwamba hali zenu zikabadilika zikawa bora kuliko hivi sasa.”2

Kwenye hali hii, Mtume (s.a.w.w.) alitoka mjini Madina akifuatana na watu 313, kwenye mwezi wa Ramadhani wa mwaka wa pili Hijiria ili kwenda kutaifisha mali za Waquraishi na waliokuwa wamepiga kambi kandoni mwa kisima cha Badr.

Abu Sufyani alipokuwa akienda Sham alitambua ya kwamba Mtume (s.a.w.w.) alikuwa akiufuatilia msafara wake. Hivyo basi, alikuwa akitahadhari wakati wa kurejea kwake na alikuwa akiulizia misafara mingine kama Muhammad amezikalia njia za biashara. Aliarifiwa ya kwamba Mtume (s.a.w.w.) kaishaondoka Madina pamoja na masahaba zake hivyo inawezekana kwamba anaufuatilia ule msafara wa Waquraishi.

Abu Sufyan akajizuia kuendelea zaidi na safari. Hakuona njia nyingine ya kufanya ila kuwaarifu Waquraishi juu ya hatari iliyokuwa ikiusubiri msafara ule. Kwa hiyo yeye alimkodi mpanda ngamia mwenye mbio sana aliyeitwa Zamzam bin Amr Ghafari na akampa maelekezo yafuatayo: “Nenda Makka na uwaarifu watu mashujaa wa Waquraishi na wamiliki wa bidhaa hizi watoke Makka waje waulinde msafara huu dhidi ya mashambulio ya Waislamu.”

Zamzam aliharakisha kwenda Makka. Kama alivyoamrishwa na Abu Sufyan, aliyakata masikio ya ngamia wake, akamtoboa pua na akayapindua matakia yake juu chini, chini juu, na akalipasua shati lake kwa upande wa mbele na wa nyuma. Kisha alisimama juu ya ngamia wake na akapiga ukelele akisema: “Enyi watu! Ngamia waliochukua miski wako hatarini. Muhammad na marafiki zake wanadhamiria kuzinyakua bidhaa zile. Nina shaka kwamba hazitaweza kuifikia mikono yenu, saidieni saidieni!3

Hali ya kusikitisha ya yule ngamia ambaye damu ilikuwa ikimchuruzika kutoka masikioni na puani na hisia aliyoijenga Zamzam kwa maombolezo yake yaliyokuwa yakiendelea na kuomba msaada, na wale mashujaa wakawa tayari kwenda, ila Abu Lahab, ambaye hakushiriki kwenye vita ile na akamkodi Aas bin Hisham kwa dirhamu elfu nne ili aende akapigane kwa niaba yake.

Umayyah bin Khalaf, aliyekuwa mmoja wa machifu wa Waquraishi haku- penda kushiriki kwenye vita ile kwa sababu fulani fulani na aliambiwa ya kwamba Muhammad amesema: “Umayyah atauawa mikononi mwa Waislamu.” Viongozi wa jamii ile walihisi ya kwamba kutokuwapo kwa mtu yule aliye muhimu kiasi kile bila shaka kutaleta madhara katika lengo lao.

Umayyah alipokuwa ameketi ndani ya Masjidul-Haraam pamoja na watu wengine, watu wawili waliojitolea kupigana dhidi ya Muhammad walikuja na kumwekea sinia na kisanduku cha wanja mbele yake na wakasema: “Ewe Umayyah! Hivyo umejitoa katika kuihami nchi yako, utajiri wako na biashara yako na umechagua kuishi maisha ya kutawishwa kama mwanamke badala ya kupigana kwenye mstari wa mbele wa vita, inafaa kwamba uyapake wanja macho yako kama mwanamke na jina lako lifutiliwe mbali kutoka kwenye orodha ya watu mashujaa.”

Masuto haya yalikuwa na athari kubwa kwa Umayyah, kiasi kwamba upesi upesi alikusanya masurufu ya safari yake na akaenda pamoja na Waquraishi kwenda kuulinda ule msafara.4

Tatizo Lililowakabili Waquraishi

Muda wa kuondoka ulitangazwa kwa njia fulani maalumu. Hata hivyo machifu wa Waquraishi walikumbushwa ukweli uliopo kwamba vilevile walikuwa na adui mwingine aliye mbaya kama vile kabila la Bani Bakr, na ingaliwezakana kuwashambulia kwa nyuma. Uadui wa Bani Bakr na Waquraishi ulitokana na umwagaji wa damu, ambao maelezo yake kwa kirefu yametolewa na Ibn Hishamu.5 Wakati uleule Suraqah bin Malik aliyekuwa mmoja wa wazee wa Bani Kananah (sehemu ya Bani Bakr) aliwahakikishia Waquraishi ya kwamba hakuna lolote la aina ile (ya kushambuliwa na Bani Bakr kwa nyuma) liwezalo kutokea na kwamba wangali- weza kutoka Makka bila ya wasiwasi japo ulio mdogo mno.

Majeshi Ya Haki Na Ya Batili Yakabiliana

Majeshi ya haki na yale ya batili yalikabiliana kwa mara ya kwanza kwenye Bonde la Badr. Idadi ya jeshi la ukweli haikuzidi 313 ambapo jeshi la upotovu lilikuwa kubwa mara tatu ya lile la haki. Waislamu hawakuwa na silaha za kutosha, usafiri wao ulikuwa na kiasi cha ngamia sabini na kiasi cha farasi wachache, ambapo yule adui alikuja na nguvu kamili ili kuupiga Uislamu. Hata hivyo, ingawa mambo yalikuwa hivyo, uhaki ilishinda na adui akarudi Makka baada ya kupata hasara kubwa.

Mtume (s.a.w.w.) alipiga kambi kwenye njia ya kaskazini ya Badr chini ya mlima uitwao ‘Al-Udwatud Dunya’ na alikuwa akiusubiri ule msafara upite ndipo alipopata taarifa mpya. Taarifa hii iliyabadilisha mawazo ya maamiri jeshi wa jeshi la Waislamu na ikaifungua sura mpya kwenye maisha yao. Mtume (s.a.w.w.) aliarifiwa ya kwamba wale watu wa Makka waliotoka kuja kuuhami msafara ule, walikuwa wamejikusanya kwenye eneo lilelile na makabila mbali mbali yameshiriki katika kuliunda jeshi hilo.

Yule kiongozi mkuu wa Waislamu alijikuta njia panda. Yeye na masahaba zake wametoka Madina kuja kuziteka bidhaa nao hawakuwa katika hali ya kuweza kukabiliana na jeshi kubwa la watu wa Makka kiasi kile, kutokana na idadi na zana zao za kijeshi, na sasa kama wakirejea kule walikotoka, watakuwa wameupoteza utukufu walioupata kwa njia ya mikakati na utendaji wa kivita.

Kwa vile kulikuwa na uwezekano kabisa kwamba adui angeweza kuendelea mbele na kuanza kuyashambulia makao makuu ya Uislamu (Madina), Mtume (s.a.w.w.) alifikiria kwamba ni bora wasirudi nyuma bali wapigane mapigano ya makubwa kwa kuitumia nguvu iliyopo hadi dakika ya mwisho.

Jambo lipasalo kuzingatiwa hapa lilikuwa kwamba, wengi wa askari walikuwa ni Ansar na walikuwepo Muhajiriin sabini na nne tu miongoni mwao, na katika yale mapatano waliyoyafanya Ansar na Mtume (s.a.w.w.) pale ‘Aqabah’ yalikuwa ni mapatano ya ulinzi na wala hayakuwa mapatano ya vita. Kwa maneno mengine ni kwamba, Ansar walikubali kumhami Mtume (s.a.w.w.) yeye binafsi mle mjini Madina kama watakavyowalinda ndugu zao, lakini hawakujiwajibisha na kwenda naye nje ya mji wa Madina kwenda kupigana vita dhidi ya adui. Sasa swali lililoibuka pale lilikuwa yule amiri jeshi wa jesli zima angefanya nini? Hapo Mtume (s.a.w.w.) hakuliona lolote jingine la kufanya bali kushauriana na masahaba zake juu ya kupigana vita na kulitatua tatizo lile kwa njia ya mtazamo wao.

Mashauriano Ya Kijeshi

Mtume (s.a.w.w.) alisimama na akasema: “Mna maoni gani juu ya jambo hili?” Abu Bakr (r.a) alikuwa wa kwanza kusimama, naye akasema: “Machifu na wapenda vita wa Waquraishi wamejiunga na jeshi hili. Katu Waquraishi hawajaonyesha imani juu ya dini na hawajaanguka kutoka kwenye kilele cha utukufu na kuangukia kwenye shimo la fedheha. Zaidi ya hapo, hatukutoka Madina tukiwa tumejitayarisha vya kutosha.6 (Alikuwa na maana ya kusema kwamba isingalifaa kupigana nao, hivyo warudi Madina).

Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Kaa chini” Kisha Umar akasimama na akayarudia yale aliyoyasema Abu Bakr, Mtume (s.a.w.w.) alimwomba yeye naye akae.

Baada ya hapo Miqdad (Ansar) alisimama na akasema: “Ewe Mjumbe wa Allah! Nyoyo zetu ziko pamoja nawe, hivyo basi, huna budi kulitekeleza lile uamrishwalo na Allah. Ninaapa kwa jina la Allah! sisi hatutakuambia kama vile Bani Isra’il walivyomwambia Musa alipowaamrisha kwenda kupigana jihadi, wao wakasema: ‘Ewe Musa! Wewe na Mola wako nendeni mkapigane jihadi, nasi tutakaa hapa.’ Kwa vyovyote vile, sisi tunakuambia kinyume kabisa na hayo, na tunakwambia: ‘Pigana jihadi chini ya msaada wa baraka za Allah na sisi nasi tuko pamoja nawe na tutapigana.”
Mtume (s.a.w) alifurahishwa mno kuyasikia maneno ya Miqdad na akamwombea du’a.

Kuuficha Ukweli

Ingawa upendeleo, kuficha ukweli wa mambo na ushupavu wa kidini (ushabiki), ni mambo yasiyo sahihi kwa mwandishi yeyote, bali ni zaidi kwamba hayafai kabisa kwa mwanahistotia. Historia ni kioo ambacho nyuso za watu zaweza kuonekana waziwazi. Hivyo basi, kwa faida ya vizazi vijavyo, mwanahistoria hana budi kuuondoa ushupavu (ushabiki) wote wa kidini.7

Ibn Hisham,8 Miqrizi9 na Tabari10 wameyataja haya mashauriano ya kivita ya Mtume (s.a.w.w.) na vile vile wameyanukuu yale maneno ya majibu ya Sa’ad bin Ma’aaz na Miqdadi kwenye vitabu vyao vya historia, lakini wameepuka kuyanukuu kikamilifu majibu ya mabwana Abu Bakr na Umar.

Wamesema kwa kifupi tu kwamba hawa watu wawili walisimama na wakatoa maoni yao wakasema mambo mazuri. Sasa mtu anaweza kuwauliza hawa mashujaa wa historia kwamba: “Kama maoni yaliyotolewa na hawa ‘Shaykhayn’ (Mashekhe wawili – Abu Bakr na Umar) yalikuwa mazuri, kwa nini waliepuka kuyanukuu maneno yao?”

Hata hivyo, majibu yao yalikuwa ni kama tulivyoyanukuu hapo juu, na kama wanahistoria hao tuliowataja wameuficha ukweli, lakini wengine wameyanukuu maneno yao.11 Na kama uwezavyo kuona vema kabisa, hawakusema maneno mazuri. Maneno yao yanaonyesha kwamba walipatwa na hofu na waliwachukulia Waquraishi kuwa ni watukufu zaidi na wenye nguvu kiasi kwamba wao (Abu Bakr na Umar) hawakuweza japo kufikiria ya kwamba wao (Waquraishi) wangaliweza kushindwa.

Athari mbaya za maneno yao katika fikara za Mtume (s.aw.w) zinaweza kutambulika vizuri sana kutoka kwenye vipande vya historia alivyovinukuu Tabari kwenye ukurasa uleule, kwa sababu kama uonavyo, hawa Shaykhayn walikuwa watu wa kwanza kuifungua midomo na Miqdaad na Sa’ad bin Ma’aaz waliyatoa mawazo yao baadae.

Tabari anamnukuu Abdullah bin Mas’ud kwamba alisema: “Katika siku ya Badr nilitamani kwamba ningalikuwa kwenye nafasi ya Miqdaad, kwa sababu alianza kuongea na akasema: ‘Katu sisi sio kama Bani Isra’il (wana wa Isra’il) ili kwamba tukwambie kuwa wewe na Mungu Wako nendeni na kapiganeni nasi tutakaa hapa . . . . .’

Kwa muda fulani wakati uso wa Mtume (s.a.w.w.) ulipokuwa umejawa na hasira, akayasema maneno haya (na akaileta njia ya raha na furaha kwa Mtume (s.a.w.w.), na nilipenda ya kwamba ningalilipata mimi nafasi ile.”

Sasa je, hasira ya Mtume (s.a.w.w.) ilisababishwa na kitu chochote kingine badala ya maneno ya kukatisha tamaa waliyoyatamka Abu Bakr na Umar na kushikilia kwao kurejea Madina?12

Bila shaka huu ulikuwa ni mkutano wa ushauriano na kila mmoja alikuwa na haki ya kutoa maoni yake mbele ya amiri jeshi mkuu. Hata hivyo, ilithibitishwa kwamba maoni aliyoyatoa Miqdaad yalikuwa karibu zaidi na ukweli kuliko yale yaliyotolewa na wale ‘Shaykhayn’ (masheikh wawili).

Maoni yaliyotolewa yalikuwa na mwelekeo wa kibinafsi. Hata hivyo, lengo kuu la kuitisha mkutano wa ushauriano lilikuwa ni kuyapata maoni ya Ansar. Ni pale tu watakaposhiriki, ndipo itakapowezekana kutoa uamuzi wa mwisho. Hivyo, Mtume (s.a.w.w.) aliyakariri maneno yake ili kupata maoni ya Ansar na akasema: “Nifahamisheni mawazo yenu.”

Sa’ad bin Ma’az Ansar alisimama na akasema: “Je, una maana ya sisi (Ansar)?” Mtume (s.a.w.w.) akajibu akasema: “Ndio.” Baada ya hapo Sa’ad akasema: “Ewe Mtume wa Allah! Sisi tumekuamini na tumeshuhudia ya kwamba dini yako ni dini ya kweli, nasi tumekuahidi na kukubali ya kwamba tutakutii na kuyafuata maamuzi yako.

Tunaapa kwa jina la Allah Mwenye nguvu zote, Aliyekuteuwa kuishika kazi ya Utume kwamba kama ukienda baharini (yaani Bahari ya Sham) sisi tutakufuata na hakuna yeyote miongoni mwetu atakayebakia nyuma katika kukufuata. Katu sisi hatuogopi kumkabili adui. Inawezekana kwamba tutaweza kutoa huduma zetu na kutoa mihanga katika jambo hili liwezalo kuyaangaza macho yako. Katika kuitii amri ya Allah unaweza kutupeleka mahali popote uonapo kuwa panafaa.”

Maneno ya Saad yalimfanya Mtume kuwa na furaha mno na kile kivuli cha kisirani cha kukata tamaa kilipotea usoni mwake na ikadhihiri nuru ya matumaini, umadhubuti, subira na uvumilivu katika njia iendayo kwenye lengo.

Maneno ya Saad yalikuwa yenye kuvutia mno kiasi kwamba Mtume (s.a.w.w.) alitoa amri ya haraka ya kwenda mbele na akasema: “Songeni mbele nami ninakubashirieni kwamba mtakutana na msafara ule na kuzinyakua zile bidhaa au mtapigana dhidi ya majeshi yaliyokuja kuusaidia ule msafara. Hivi sasa hapa ninaweza kukuona kushindwa kwa Waquraishi na kuona kwamba wamepata hasara kubwa.”

Jeshi la Waislamu liliendelea likiwa chini ya uamiri jeshi wa Mtume (s.a.w.w.) na kupiga kambi karibu na visima vya Badr.13

Kupata Taarifa Juu Ya Adui

Kanuni za kijeshi za kisasa na mbinu za kivita zimekuwa na mabadiliko makubwa mno zinapolinganishwa na hapo kale. Muhimu wa kupata taarifa juu ya hali ya adui na ujuzi wa siri zake za kivita, na mikakati ya vita na jeshi analolileta kwenye uwanja wa vita bado upo. Hata katika siku zetu hizi, jambo hili lina mchango mkubwa kuhusiana na kushinda au kushindwa katika vita. Hakuna shaka yoyote kwamba siku hizi jambo hili limeitwaa sura ya kielimu, na madarasa na shule vimejengwa kwa ajili ya kufundisha kanuni za upelelezi.
Wakuu wa ushirika wa nchi za Masharika na za Magharibi hufikiria ya kwamba sehemu kubwa ya ushindi wao inatokana na upanuaji wa mipango yao ya upelelezi ili kwamba waweze kuzitambua mbinu za kivita za adui kabla ya kuanza kwa uadui na waweze kuwachanganya mawazo.

Majeshi ya Uislamu yalichukua nafasi yao kwenye sehemu ambayo iliafikiana na kanuni za majificho (camouflage), na kila harakati kama hiyo ambayo ingeweza kusababisha kufunuka kwa siri zao ilizuiwa. Vikundi mbalimbali vikaanza kukusanya taarifa juu ya Waquraishi na vilevile kuhusu ule msafara wao. Taarifa hizi zilikusanywa kutoka vyanzo mbalimbali katika njia zifuatazo:

1. Kwanza kabisa yeye Mtume (s.a.w.w.) mwenyewe alitoka akifuatana na askari mmoja shujaa na wakakutana na kiongozi wa kabila moja na akamwuliza, akisema: “Je, una taarifa gani kumhusu Muhammad na marafiki zake?” “Nimearifiwa ya kwamba Muhammad na masahaba zake waliondoka Madina kwenye siku kadhaa. Kama mtu huyu aliyenipa taarifa hizi yu mkweli, basi yeye (Mtume s.a.w.w na masahaba zake) watakuwa wako sehemu fulani na sehemu fulani, hivi sasa.

2. Kikundi cha doria walimokuwamo Zubayr, ‘Awaam, na Sa’ad Abi Waqqas walikwenda kwenye kisima cha Badr wakiwa chini ya Sayyidna Ali (a.s.) ili wakatafute taarifa nyingine. Hapa palikuwa ni mahali pa kukutanikia ambapo watu walipashana habari. Karibu na hicho kisima kikundi kile kiliwakuta watumwa wawili wa Waquraishi wakiwa na ngamia aliyechukua maji. Waliwakamata wote wawili na wakawaleta mbele ya Mtume (s.a.w.w.). Baada ya kuwahoji ilifahamika ya kwamba mmoja wa watumwa wale alikuwa ni wa Banil Hajjaj na mwingine alikuwa wa Banil Aas nao walitumwa kuja kuwachotea maji Waquraishi. Mtume (s.a.w) aliwauliza: “Wako wapi Waquraishi?”

Wakamjibu kwamba walikuwa upande wa pili wa mlima uliokuwako jangwani. Kisha aliwauliza kuhusu idadi yao, wakajibu ya kwamba hawakuwa na uhakika nayo. Akawauliza: “Kila siku wanachinja ngamia wangapi?” wakamjibu ya kwamba wanachinja ngamia kumi siku moja na siku nyingine wanachinja ngamia tisa. Hapo Mtume (s.a.w.w.) akasema kwamba idadi yao ilikuwa ni baina ya mia tisa na elfu moja. Baada ya hapo aliwauliza kuhusu machifu wa Waquraishi. Walijibu ya kwamba ‘Utbah bin Rabiyyah, Shaybah bin Rabiyyah, Abul Bakhtari bin Hisham, Abu Jahal bin Hisham, Hakim bin Hizaam, Umayyah bin Khalaf n.k. walikuwa miongoni mwao. Mtume (s.a.w.w.) aliwageukia masahaba zake na akasema:

“Mji wa Makka umevitoa vipande vya moyo wake (yaani wanawe walio wapenzi zaidi, kwa mji huo).14
Baada ya hapo aliamrisha kwamba wale watu wawili wazuiwe wakiwa ni mateka ili uchunguzi uendelee.

3. Watu wawili walitumwa kwenda kwenye kijiji cha Badr kwenda kukusanya taarifa juu ya ule msafara. Walishuka upande wa kilima kilichokuwa karibu na kile kisima na wakajifanya kwamba walikuwa na kiu hivyo wamekuja kunywa maji. Kwa bahati wakawaona wanawake wawili kandoni mwa kisima kile waliokuwa wakizungumza. Mmoja wao alimwambia mwenzie: “Kwa nini hunilipi deni langu? Je, hufahamu kwamba mimi nami ni mhitaji?” Yule mwenziwe alimjibu akisema: “Msafara utafika kesho au keshokutwa. Nitautumikia msafara huo na kisha nitakulipa deni lako.” Majdi bin Amr aliyepata kuwapo pale aliyathibitisha yale aliyoyasema yule mdaiwa na kisha akawaamua.

Wale wapanda ngamia wawili walifurahi sana kuzisikia habari hizi. Wakizizingatia kanuni za kujificha walifika mbele ya yule Amiri–jeshi Mkuu wa majeshi ya Waislamu na wakamwarifu yale waliyoyasikia.

Sasa kwa kuwa Mtume (s.a.w.w.) alikuwa kaishapata taarifa kamili kuhusu kuwasili kwa ule msafara na mahali walipo Waquraishi, sasa ikawa muhimu kwake kurejea kwenye matayarisho ya kazi yake.

Msafara Wa Abu Sufyani Wakimbia

Abu Sufyani kiongozi wa msafara ule aliyeshambuliwa na kikundi cha waislamu wakati wa kwenda Shamu, alijua vyema kwamba wakati wa kurejea kwake bila shaka watamshambulia tena. Hivyo, alipofika kwenye eneo lenye athari za Uislamu aliusimamisha ule msafara wake mahali fulani na akaenda kwenye kijiji cha Badr kwenda kupata taarifa. Hapo alikutana na Majdi bin ‘Amr na akamuuliza kama amewahi kumwona mtu yeyote kwenye eneo lile ambaye angaliweza kumhisi. Majdi alimjibu akisema: “Sikuona kitu chochote ambacho kingeliweza kuziamsha hisia zangu.

Niliwaona wapanda ngamia wawili tu. Waliweka ngamia wao kwenye kilima kile, wakashuka chini hapa, wakanywa maji na kisha wakaenda zao.” Abu Sufyani akakipanda kile kilima, akavunja kipande cha mavi ya ngamia wale, na alipoona kokwa za tende ndani yake, alitambua fika wale walikuwa ni watu wa Madina. Hivyo basi, aliibadili njia ya msafara ule, na kwa kwenda hatua mbili za msafara kwa wakati mmoja, aliweza kuutoa nje ya eneo la athari za Uislamu.

Vilevile alimteua mtu mmoja kwenda na kuwaarifu Waquraishi kwamba msafara wao uko salama kutokana na mashambulizi ya Waislamu, na hivyo basi, warudi Makka na wawaachie Waarabu kulimaliza jambo lile na Muhammad.

Waislamu Watambua Kutoroka Kwa Msafara

Taarifa za kutoroka kwa ule msafara zilienea miongoni mwa Waislamu. Wale waliokuwa wakizitupia jicho la ulafi bidhaa za msafara ule waliudhishwa mno na matokeo haya. Allah akazifunua Aya zifuatazo ili kuzitia nguvu nyoyo zao:

“Na Allah Alipokuahidini moja kati ya mataifa mawili ya kwamba ni lenu, nanyi mkapenda mpate lile lisilo na nguvu liwe lenu, na Allah anapenda kuitimiza haki kwa maneno Yake, na aikate mizizi ya makafiri. Ili kuthibitisha haki na kuondoa batili hata kama wakichukia wabaya” (Surah al-Anfal, 8:7-8).

Tofauti Za Maoni Miongoni Mwa Waquraishi

Abu Sufyan alipofaulu kuusalimisha msafara wake kwa kuifuata njia nyingine badala ya ile ya Badr, upesi sana aliwapelekea ujumbe wale watu waliokuja kuuokoa ule msafara akiwaarifu kuhusu usalama wa msafara na kuwaomba warejee kwa njia waliyokuja nayo, kwa kuwa lengo hasa la kukusanya jeshi lile lilikuwa ni kuuhami ule msafara na lengo hilo limeshafikiwa. Yule mjumbe wa Abu Sufyan alipoufikisha ujumbe wake kwa machifu wa Waquraishi, ulitokea mfarakano wa ajabu miongoni mwao.

Watu wa kabila la Bani Zuhrah na Akhnas Shariq na washirika wao walirejea kwa ile njia waliyokuja nayo. Wao walisema: “Lengo letu lilikuwa kuzihami bidhaa nyingi za Bani Zuhrah na lengo hilo limeshafikiwa.” Twalib bin Abu Twalib aliyelazimishwa na Waquraishi kutoka mjini Makka na kwenda kuuhami ule msafara naye alirudi baada ya ugomvi wa maneno ambao ndani yake aliambiwa: “Nyoyo zenu ninyi Bani Hashim anazo Muhammad.”

Kinyume na ushauri wa Abu Sufyani, Abu Jahl alishikilia kwamba waende kwenye ukanda wa Badr, wakakae hapo kwa muda wa siku tatu, wachinje ngamia, wanywe mvinyo, na wasikilize wasichana malenga wakiimba ili kwamba ushujaa wao ufike masikioni mwa Waarabu na wapate kuheshimiwa mno daima.

Maneno ya kupumbaza ya Abu Jahl yaliwafanya Waquraishi wasubiri katika sehemu ile, walikwenda na wakatua kwenye sehemu ya mwinuko ya jangwani, nyuma ya kilima.
Mvua kubwa iliufanya mwendo kwenye sehemu ile kuwa mgumu kwao na ikawazuia wasiendelee mbele. Hata hivyo, mvua haikuleta athari mbaya kwenye mteremko wa jangwa (al- Udwatud Dunya) ambako Mtume (s.a.w.w.) alipiga kambi. Hivyo basi, Waislamu waliweza kutembea kama walivyoamrishwa na Mtume (s.a.w.w.) wakaichukua nafasi kandoni mwa visima vya Badr.

Badr ni ukanda mpana. Upande wake wa kusini umeinuka (al-Udwatul- Qaswa) na eneo lake la kaskazini ni bonde lenye mteremko (al-Udwatul- Dunya). Maji yalipatikana kwa wingi kwenye jangwa hili kutoka kwenye visima vilivyochimbwa na wakati wote sehemu hii ilikuwa sehemu ya kupumzikia kwa misafara.

Hubaab bin Manzar, aliyekuwa mmoja wa askari wazoefu alimuuliza Mtume (s.a.w.w.): “Je umetua hapa kwa mujibu wa amri ya Allah, au umeifikiria sehemu hii kuwa ni yenye kufaa kwa kupigana vita?” Mtume (s.a.w.w.) akamjibu: “Hakuna amri maalum iliyofunuliwa kuhusiana na jambo hili na kama unafikiria sehemu ifaayo zaidi, unaweza kuitaja ili nibadili sehemu, kama masharti ya vita yanawajibisha kufanya hivyo.” Hubaab akasema: “Ni bora kwamba tukae sehemu iliyoko kandoni mwa maji ambayo iko karibu zaidi na adui. Tujenge tangi hapo, ili kwamba paweze kuwa na maji wakati wote kwa ajili ya watu na wanyama: “Mtume (s.a.w.w.) alilipendelea wazo la Hubaab na akaliamrisha jeshi kwenda mbele. Tukio hili ladhihirisha ya kwamba Mtume (s.a.w.w.) aliona umuhimu mno kufanya ushirikiano na aliyaheshimu maoni ya watu katika masuala ya kijamii.15

Mnara Wa Kuamrishia

Sa’ad bin Ma’aaz akamwambia Mtume (s.a.w.w.): “Tunakusudia kukujengea kibanda juu ya kilele cha kilima ambacho kutokea hapo uwanja mzima wa mapambano utaonekana. Kilima hicho kitalindwa na walinzi, na amri za Amir jeshi Mkuu zitatolewa kutoka hapo kwenda kwa wale maamiri jeshi wadogo. Zaidi ya mambo yote hayo, kama jeshi la Waislamu likishinda katika vita hii, itakuwa vizuri na vizuri zaidi, na kama watu wako wakishindwa na wakauawa, wewe utaweza kufika Madina kwa kumpanda ngamia mwenye mbio zaidi ukifuatana na wale walinzi wa ule Mnara wa kuamrishia baada ya kutumia mbinu za ucheleweshaji, zitakazomzuia adui kukukamata.

Wako Waislamu wengi huko ambao bado hawajaitambua hali yetu ya sasa, na kama wakijua hali hii, watakupa msaaada kamili na watafanya mambo hadi dakika ya mwisho ya uhai wao kwa mujibu wa mapatano waliyoyafanya na wewe.” Mtume (s.a.w) alimwombea du’a Sa’ad bin Ma’aaz na akaamrisha ujenzi wa kile kibanda juu ya kilima, kitakachouangalia uwanja wa vita na kituo kikuu cha kuamrishia kihamishiwe kibandani hapo.

Kulichunguza Suala La Ujenzi Wa Kibanda Cha Kivuli

Ujenzi wa kivuli kwa ajili ya Mtume (s.a.w.w.) na ulinzi wake uliofanywa na Sa’ad bin Ma’aaz na kikundi cha Ansar ni tukio lililonukuliwa na Tabari kutoka kwa Ibn Is’haaq na wengineo wamemfuata.16 Hata hivyo, kwa sababu fulani fulani hadithi hii ni yenye kutia shaka. Kwanza, kitendo cha aina hii kina athari mbaya katika nyoyo za askari. Amiri jeshi anayefanya mipango kwa ajili ya usalama wake, naye hana shauku juu ya usalama wa askari wake hawezi kuziamrisha na kuzitawala akili zao.

Pili, kitu cha aina hii hakilandani na bishara aliyoibashiri Mtume (s.a.w.w.) kwa masahaba zake, kwa msingi wa Ufunuo wa Allah. Kabla ya kukabiliana uso kwa uso na Waquraishi, aliwaambia Waislamu maneno haya: “Na Allah Alipokuahidini moja kati ya mataifa mawili (ule msafara na wale waliokuja kuulinda) ya kwamba ni lenu, nanyi mkapenda lile lisilo na nguvu liwe lenu, na Allah anapenda kuitimiza haki kwa maneno Yake, na aikate mizizi ya makafiri. Ili kuthibitisha haki na kuondoa batili hata kama wakichukia wabaya” (Surah al- Anfal, 8:7-8).

Kwa mujibu wa Tabari, wakati kile kibanda kilipokuwa kinajengwa kwa ajili ya Mtume (s.a.w), ule msafara ulikuwa umeshatoroka na walibakia tu wale watu waliokuja kutoka Makka kuuhami. Na kwa mujibu wa ahadi tuliyoitaja hapo juu, wao (Waislamu) walikuwa na uhakika kwamba ushindi ni wao. Katika hali hiyo mazungumzo yoyote yale juu ya kushindwa kwa Waislamu na ujenzi wa kibanda kwa ajili ya Mtume (s.a.w.w.) na kumweka ngamia mwenye mbio karibu na kile kibanda vingalikuwa sio mahali pake kabisa.

Ibn Sa’ad ananakili hivi, kutoka kwa Umar bin Khattab.17 “Ilipofunuliwa aya isemayo: ‘Hivi karibuni majeshi yao yatashindwa na watakimbia’ (Surah al-Qamar, 54:45), Mimi nilisema moyoni: ‘Ni jeshi lipi ambalo kushindwa kwake kumetabiriwa katika aya hii?’ Kisha niliona katika siku ya Badr kwamba Mtume (s.a.w.w.) amevaa deraya na alikuwa akiisoma aya hii kwa nguvu. Wakati ule nilielewa kwamba jeshi hili litashindwa na kuangamizwa.’” Kwa kuuzingatia ukweli huu, hivi inaweza kudhaniwa ya kwamba Mtume (s.a.w.w.) na masahaba zake watafikiria kushindwa na kukimbia kwao?”

Tatu, tabia ya Mtume (s.a.w.w.), ambaye mkao wake katika uwanja wa vita ulielezwa na Sayyidna Ali, Amiri wa Waumini (a.s.) haziafikiani hata kidogo na mbinu hii. Kumhusu Mtume (s.a.w.w.) anasema: Kila wakati mapigano yalipokuwa makali tulitafuta mahali pa kukimbilia. Hakuna hata mmoja wetu aliyekuwa karibu zaidi na adui kuliko yeye.”18

Je, inaweza kudhaniwa kwamba mtu ambaye mwanafunzi wake wa kwanza anamwelezea kwa namna hii, kwamba ajitwalie njia ya usalama wake mwenyewe na kukimbia kwenye vita ya awali kabisa waliyopigana Waislamu? Tunafikiria kwamba ujenzi wa kibanda ulikuwa ni kwa ajili ya kumpatia Mtume (s.a.w.w.) mahali palipo juu kuliko ule uwanja wa vita ili aweze kuviona vizuri vita vile, na kutoka hapo aweze kutoa maelezo sahihi kwenye jeshi lake.

Kusonga Kwa Waquraishi

Katika mwezi 17 Ramadhani ya mwaka wa pili wa Hijiriya Waquraishi walishuka alfajiri na mapema kutoka nyuma ya kilima chenye mchanga na kuja kwenye jangwa la Badr. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alipowaona aliuinua uso wake mbinguni na kuomba akisema: “Ee Allah! Waquraishi wamefika kwa kiburi na majivuno ili wapigane dhidi Yako na kumkana Mtume Wako! Basi Tuletee ule msaada uliotuahidi na uwaangamize leo (hii)!”

Kushauriana Kwa Waquraishi

Majeshi ya Waquraishi yalikusanyika mahali fulani pale Badr, lakini hawakuitambua nguvu ya Waislamu. Walimtuma Umayr bin Wahab, aliyekuwa mtu shujaa na mtaalamu wa kutathmini nguvu za majeshi, kwenda kupata idadi ya masahaba wa Muhammad. Akimpanda farasi wake aliizunguka kambi ya jeshi la Waislamu na kutoa taarifa pale aliporejea kwamba walikuwa kiasi cha mia tatu hivi. Hata hivyo, alisema kwamba atazunguuka tena ili aone kama walikuwako wengine waliojificha ili kuvizia na vilevile kama kuna majeshi ya msaada au la.

Alizunguuka huko na huko jangwani pande zote na kisha akaleta taarifa zenye kuhadharisha. Alisema: “Waislamu hawana wavamiaji wala hifadhi. Hata hivyo, nimewaona ngamia wanaokuleteeni taarifa za kifo kutoka Madina.” Kisha akaongeza kusema: “Nimekiona kikundi cha watu wasiokuwa na kimbilio lolote jingine zaidi ya panga zao.”19 Waqidi na Allamah Majlisi wameinukuu sentensi nyingineyo pia –yaani

“Je, hamwoni kwamba wako kimya na wala hawasemi japo neno moja na nyuso zao zaonyesha zile nia zao zilivyo, na wanazisogeza ndimi zao vinywani mwao kama nyoka wenye sumu kali mno?”20

Tofauti Za Maoni Miongoni Mwa Waquraishi

Maneno ya yule askari shujaa yaliibua makelele miongoni mwa Waquraishi. Jeshi zima la adui likapatwa na hofu kuu. Hakim bin Huzaam alimwendea ‘Utbah na kumwambia: “Ewe Utbah! Wewe ni chifu wa Waquraishi. Waquraishi wametokea Makka kuja kuzilinda bidhaa zao; lengo hili limeshatimia na hakuna jambo lolote lililobakia ila dia ya Hazrami na fidia ya mali iliyonyang’anywa na Waislamu hapo nyuma. Hamna budi kumlipa dia yake ninyi wenyewe na mjiepushe na kupigana na Muhammad.” Maneno ya Hakim yalikuwa na athari zenye nguvu kwa Utbah.

Aliamka na kutoa hotuba yenye kuvutia sana mbele ya watu na akasema: “Enyi watu! Waachieni Waarabu walimalize jambo hili na Muhammad. Kama Waarabu wakifaulu kuipindua dini yake na kubomoa msingi wa nguvu zake sisi nasi tutakuwa na furaha kwa jambo lile. Na kama Muhammad akishinda hatutapatwa na dhara lolote kutoka kwake kwa sababu tutakuwa tumeepuka kupigana naye ingawa sisi tuko kwenye kilele cha nguvu zetu. Hivyo basi, itakuwa bora kama tukirejea makwetu.”

Hakim alimweleza Abu Jahl maoni ya ‘Utbah na akona kwamba alikuwa akijishughulisha kuvaa deraya yake. Abu Jahl aliudhishwa mno kusikia habari za hotuba ya ‘Utbah na akamtuma mtu kwenda kwa Abu ‘Aamir Hazrami, nduguye ‘Amr Hazrami, na ujumbe huu: “Mshirika wako (yaani Utbah) anawazuia watu kuipata dia ya ndugu yako. Unaweza kuiona damu ya nduguyo kwa macho yako mwenyewe. Amka na uwakumbushe Waquraishi yale mapatano waliyoyafanya na ndugu yako na uimbe beti za huzuni kwa ajili yake”.

Abu Aamir aliamka, akaondoa kilemba chake na akasema kwa kulalamika: “Ole wako! Ewe Amr!”
Vilio na maombolezo ya Abu Aamir viliibua hisia za heshima ya Waquraishi na kuwafanya waamue kupigana. Hivyo wakayatupilia mbali maoni ya Utbah yahusuyo kutoka pale Badr. Hata hivyo, Utbah huyo huyo aliyependekeza kuondoka Badr, alishawishiwa na hisia za kidunia za wafuasi wake. Aliamka mara moja, akaivaa sare yake ya kijeshi na akawa tayari kwa ajili ya vita.

Wakati mwingine mwanadamu anaipoteza hekima yake kutokana na ushawishi wa hisia na hasira zisizo na msingi, na akashindwa kuyaangaza maisha yake. Yule mtu aliyekuwa na msimamo wa amani na akawaita wenzie kwenye maisha na kuwaacha wengine nao waishi, akawa katika hisia kali mno kiasi kwamba alikuwa wa kwanza kujitolea ili apigane.

Sababu Zilizoifanya Vita Vya Badr Kutoepukika

Aswad Makhzumi alikuwa mtu mwenye ghadhabu. Alipoliona lile tangi lililojengwa na Waislamu aliapa ya kwamba atafanya moja ya mambo matatu: Atakunywa maji kutoka kwenye tangi hili, au atalibomoa, au atauawa.

Alitoka kwenye safu za makafiri na akakutana na kamanda shujaa wa Uislamu Hamza karibu na tangi lile. Mapigano yalianza baina yao. Hamza alimpiga dhoruba mguuni mwake na kuukata. Hivyo basi, alianguka chini kandoni mwa lile tangi, huku mguu wake ukiwa unatoa damu. Ili kukitimiza kiapo chake, aliufikia ukingo wa tangi lile ili anywe maji, Hamza akampiga dhoruba jingine na akauawa.

Tukio hili lilifanya vita hiVi kuwa jambo lisiloepukika, kwa sababu hakuna jambo lenye kuibua mno hisia za kundi la watu kuliko umwagaji damu. Baadhi ya watu ambao nyoyo zao zilikuwa zikiungua kwa mfundo na chuki walikuwa makini kupata sababu ya kupigana na sasa tukio hili lilikuwa sababu iliyo bora zaidi kwao. Wakajifikiria kuwa ni wenye wajibu wa kupigana.

Mapambano Ya Mtu Na Mt

Ilikuwa ni desturi ya Waarabu ya tangu kale kwamba mwanzoni mwa vita mapigano ya watu wawili wawili huanza, na baada ya hapo ndipo ipiganwe vita ya watu wote.

Baada ya kuuawa kwa Aswad Makhazumi mashujaa watatu maarufu wa Waquraishi walitoka kutoka kwenye safu zao na wakasai (wakaalika wapinzani kutoka ili wapigane). Watu hawa walikuwa ni ndugu wawili - ‘Utbah na Shaybah, wana wa Rabiyyah, na Walid bin Utbah na wote walikuwa na silaha kikamilifu. Wakaunguruma na kuwakimbizia farasi wao kwenye uwanja wa vita na wakasai. Mashujaa watatu kutoka miongoni mwa Ansar, ambao ni Awf, Ma’uz na Abdullah bin Rawaahah walitoka kwenye safu za Waislamu. Hata hivyo, Utbah alitambua kwamba walikuwa ni watu wa Madina, akawaambia: “Hatuna la kufanya nanyi.” Kisha mtu mmoja (kutoka miongoni mwa Waquraishi) alipiga ukelele akasema: “Ewe Muhammad! Tuletee watu walio sawa yetu wapigane nasi.” Mtume (s.a.w.w.) aliugeuzia uso wake kwa Ubaydah, Hamza na Sayyidna Ali (a.s.) na akawaambia: “Simameni.” Hawa mashujaa watatu wakavifunika vichwa vyao na nyuso zao na wakatoka wakaenda kwenye uwanja wa vita. Wote watatu wakajitambulisha.

Utbah akawakubali wote kwamba wafanye nao yale mapambano ya wawili wawili, na akasema: “Ndio, ninyi ni sawa Baadhi ya watu wanasema kwamba katika mapambano haya, kila shujaa alipigana na mpinzani wake wa hirimu lake. Sayyidna Ali (a.s.) aliyekuwa kijana zaidi miongoni mwao alipambana na Walid (mjomba wake Muawiyah), na aliyekuwa na umri wa katikati miongoni mwa Waislamu (Hamzah) alimkabili Utbah (babu mzaa mama wa Mu’awiyah) na Ubaydah, aliyekuwa na umri mkubwa zaidi miongoni mwa hawa wapi- ganaji wa Kiislamu alipigana na Shaybah, aliyekuwa mtu mzima zaidi kutoka ule upande wa pili. Hata hivyo, Ibn Hisham anasema kwamba mpinzani wa Hamzah alikuwa ni Shaybah, na wa Ubaydah alikuwa ni Utbah. Sasa hebu na tutazame ni lipi kati ya haya maoni mawili lililo sahi- hi. Kwani kwa kuyachunguza maoni haya, hali halisi hudhihirika.

1. Wanahistoria wanasema kwamba Saidiana Ali (a.s.) na Hamza waliwaua wapinzani wao mwanzoni kabisa mwa mashambulio yale na kisha wakaharakisha kwenda kumsaidia Ubaydah na wakamwua yule mpinzani wake nae.21

2. Katika barua aliyoandika Sayyidna Ali (a.s.) Amiri wa Waumini, akimwandikia Mu’awiyah, anamkumbusha kwa maneno haya: “Ule upan- ga ambao kwawo niliwamaliza mababu zako walomzaa mama yako (‘Utbah, baba wa mamie Muawiyah-Hindi) na mjomba wako (Walid bin Utbah) na kaka yako (Hanzala) bado u pamoja nami (yaani bado ninazo nguvu zile zile)”22 Barua hii yaonyesha dhahiri kwamba Sayyidna Ali (a.s.) alikuwa na mkono katika kuuwawa kwa babu mzaa mama wa Mua’wiyah, na kisha vile vile tunajua ya kwamba Hamza na Sayyidna Ali (a.s.) waliwaua wapinzani wao pale pale.

Kama mpinzani wa Hamza angalikuwa ni ‘Utbah (babu mzaa mamaie Muawiyah), Sayyidna Ali (a.s.) asingaliweza kusema: “Ewe Muawiyah! Babu yako (‘Utbah) aliyapoteza maisha yake kutokana na dharuba ya upanga wangu.” Hivyo, isingaliwezekana kusema kwamba mpinzani wa Hamza alikuwa ni Shaybah na yule wa Ubaydah alikuwa ni ‘Utbah na baada ya kuwaua wapinzani wao Hamza na Sayyidna Ali (a.s.) walimwelekea ‘Utbah na wakamwua kwa dharuba za panga zao.

Mapambano Ya Wote Jumla Yaanza

Matokeo ya kuuawa kwa wale mashujaa watatu wa Waquraishi ni kuanza kwa mapambano ya watu wote. Na Waquraishi wakaanza kushambulia kwa vikundi. Mtume (s.a.w.w.) aliamrisha ya kwamba Waislamu waepuke kushambulia bali wazuie maendeleo ya uadui kwa njia ya kupigana mishale.

Kisha akashuka kutoka kwenye ule mnara wa kuamrishia na akazipanga safu za askari wake kwa fimbo. Katika wakati ule Sawaad bin Ghazbah alikuwa kasimama mbele kidogo akilinganishwa na ule mstari. Mtume (s.a.w.w.) alimpiga kwa ile fimbo tumboni mwake na akamwambia: “Usiende mbele ya hawa askari wengine,”23 Hapo Sawaad akasema: “Pigo hili nililopigwa halikuwa la haki, nami ninataka kulipiza kisasi.” Mtume (s.a.w.w.) akalivua shati lake mara moja na akasema: “Lipiza kisasi chako kwangu.” Kisha askari wote waliona ya kwamba Sawaad alikibusu kifua cha Mtume (s.a.w.w.) na akaiweka mikono yake shingoni mwake na akasema: “Nilitaka kukibusu kifua chako kwenye muda wa mwisho wa uhai wangu.”

Kisha Mtume (s.a.w.w.) alirejea pale kwenye mnara wa kuamrishia na huku moyo wake ukiwa umejawa na imani, aliugeuzia uso wake kwa Allah Mwenye nguvu zote na akaomba, akasema: “Ee Mola wangu! Kama kundi hili litaangamia hivi leo, hakuna yeyote mwingine atakayekuabudu kwenye huu uso wa ardhi.24

Maelezo kamili ya haya mashambulizi ya watu wote yamenukuliwa kwa kiasi fulani kwenye historia ya Uislamu. Hivyo ni kweli kwamba wakati Mtume (s.a.w.w.) aliposhuka pale kwenye kituo cha kuamrishia aliwahimiza Waislamu wapigane katika njia ya Allah na kumshambulia adui. Akaja tena kwa ghafla na akawaambia Waislamu kwa sauti kuu: “Ninaapa kwa jina la Allah Anayeitawala roho ya Muhammad kwamba, leo mwenye kupigana kwa umadhubuti na kupigana kwake kukawa kwa ajili ya Allah na akauawa, Allah Atamwingiza Peponi.”

Maneno ya yule Amir jeshi Mkuu yalikuwa na athari kubwa mno kiasi kwamba Waislamu walizivua deraya zao kutoka miilini mwao na wakaan- za kupigana ili kwamba waweze kupata kifo cha kishahidi mapema iwezekanavyo. Umayr Hamaam alimwuliza Mtume (s.a.w.w.): “Kuna umbali gani baina yangu na Pepo?” Mtume akamjibu hivi: “Kupigana na machifu wa kufuru.” Alizitupa tende chache alizokuwa akizishika mkononi na akaanza kupigana.

Kisha Mtume (s.a.w.w.) alichota mchanga na akautupia upande wa Waquraishi na akasema: “Nyuso zenu na ziumbuke!”25 Baada ya hapo alitoa amri ya mapigano ya watu wote. Dalili za ushindi wa Waislamu zilianza kujitokeza upesi upesi. Maadui walipigwa na hofu na wakaanza kukimbia. Waislamu, waliokuwa wakipigana kwa msaada wa imani yao, na wakajua ya kwamba vyote viwili kuua na kuuawa vilikuwa baraka za Allah, hawakuwa na shaka hata kidogo na hakuna kilichozuia kusonga mbele kwao.

Kuchunga Haki

Kuchunga haki za makundi mawili ya watu kulikuwa ni muhimu sana. Katika upande wa jeshi la watu wa Makka yalikuwamo makundi mawili: Wale waliowatendea Waislamu mambo mema kule Makaka na kuwasaidia, kwa mfano Abil Bakhtari, aliyetoa huduma kuu kwa Waislamu kwa kuviishilizia vizuizi vya kiuchumi. Wengine ni wale waliotoka Makka kuja kuuhami ule msafara kwa kulazimishwa na kwa hakika wao walikuwa wapenzi wa Uislamu na Mtume (s.a.w.w.) kwa mfano, wengi wa Bani Hashimu, kama vile Abbas, baba mkubwa wa Mtume (s.aw.w) n.k. Hivyo kuzijali haki za makundi haya mawili kulikuwa muhimu, na kwa kuwa Mtume wa Uislamu alikuwa ni Mtume wa rehma na amani, alitoa amri kali kwamba damu ya makundi haya mawili isimwagwe.

Umayyah Bin Khalaf Auwawa

Umayyah bin Khalaf na mwanawe walikamatwa kupitia kwa Abdur Rahmani bin Awf. Kwa vile ulikuwako urafiki baina ya Umayyah na Abdur Rahman, Abdur Rahman alitaka kumtoa yeye na mwanae mle kwenye uwanja wa vita wakiwa hai ili kwamba waweze kuchukuliwa mateka.
Bilal, Mhabeshi wa Ethiopia, alikuwa mtumwa wa Umayyah hapo kale. Kwa vile Bilal alisilimu akiwa yu mtumwa, Umayyah alikua akimtesa vikali mno. Ili kumfanya autoke Uislamu alikuwa akimlaza kwenye mchanga ulio moto sana kwenye majira ya kiangazi na kumbandika jiwe kubwa kifuani mwake. Hata hivyo alipokuwa kwenye hali ile Bilal alikuwa akisema: “Ahad! Ahad!” (Allah Yu Mmoja tu! Allah Yu Mmoja tu! ).

Huyu Mtumwa wa Ethiopia alipata taabu sana mpaka Mwislamu mmoja alipomnunua kumpa uungwana, (na inasemekana kwamba aliyemnunua na kumwacha huru alikuwa ni Abu Bakr).

Kwenye vita ya Badr macho ya Bilal yalimwangukia Umayyah na akatambua kwamba Abdur Rahman alitaka kumpendelea. Hivyo alipiga ukelele akisema: “Enyi Kundi la Allah! Umayyah yu mmoja wa machifu wa makafiri, asiruhusiwe kubakia hai.” Waislamu wakamzunguka Umayyah pande zote na wakamwua yeye na mwanawe. Mtume (s.a.w.w.) alikuwa ameamrisha ya kwamba Abul Bakhtari, aliye- wasaidia Bani Hashim katika siku za vizuizi vya kiuchumi, asiuawe.26

Ilitokea kwamba mtu mmoja aliyeitwa ‘Majzar alimkamata na alikuwa akijaribu kumleta mbele ya Mtume (s.a.w.w.) akiwa hai, lakini yeye naye aliuawa.

Idadi Ya Waliouawa Na Hasara

Kwenye vita hivi watu kumi na wanne kutoka miongoni mwa Waislamu waliuawa. Ama kuhusu Waquraishi, watu sabini kutoka miongoni mwao waliuawa na wengine sabini walitekwa. Wale waliotekwa ni pamoja na machifu wao waitwao Nazar Haarith, ‘Uqbah bin Mu’it, Abu Ghurrah, Suhayl Amr, Abbas na Abu Aas.27

Mashahidi wa Badr walizikwa kwenye pembe ya ule uwanja wa vita. Makaburi yao bado yapo pale na Waislamu wachamungu huyakimbilia kwenda kuyazuru na kutoa heshima zao.

Baadae Mtume (s.a.w.w.) aliamrisha ya kwamba maiti za Waquraishi zikusanywe na kutumbukizwa kisimani. Maiti ya ‘Utbah ilipokuwa ikiletwa kisimani pale, macho ya mwanawe Abu Huzayfah yalipoiangukia, naye akapauka. Mtume (s.a.w.w.) aliliona hilo akamwuliza, akisema: “Je, kuna shaka yoyote ile imekupitia akilini mwako?” Abu Huzayfah akajibu akisema: “Hapana, bali nilidhania ya kwamba baba yangu alikuwa mtu mwenye hekima, elimu na subira, nami nilidhani ya kwamba sifa hizi zingalimwongoza kwenye Uislamu. Hata hivyo, sasa nimetambua ya kwamba yale yote niliyokuwa nikiyafikiria hayakuwa sahihi.”

Kisha Mtume (s.a.w.w.) alikwenda akasimama kandoni mwa kile kisima. Alilitaja jina la kila mmoja wa machifu wa makafiri, na akasema: “Ewe Utbah, Ewe Shayb! Ewe Umayyah! Ewe Abu Jahl! Je, mmekwishakuyaona yale ambayo mungu wenu alikuahidini kuwa ni sahihi? Mimi nimeyaona yale ambayo Allah wangu Aliniahidi kuwa ni sahihi na madhubuti.”

Wale masahaba zake Mtume (s.a.w.w.) wakauliza wakisema: “Je, unazungumza na maiti?” Mtume (s.a.w.w.) akajibu, akasema: “Wanayasikia maneno yangu lakini hawana uwezo wa kujibu.”28

Baada Ya Vita Vya Badr

Wengi wa wanahistoria wa Kiislamu wanaamini kwamba kwenye Vita vya Badr, mapambano ya mtu na mtu na mapambano ya watu wote yaliendelea hadi adhuhuri na vita ilimalizika baada ya adhuhuri pale Waquraishi walipokimbia na baadhi yao kutekwa. Baada ya kuwazika mashahidi, Mtume (s.a.w.w.) alisali sala ya Alasiri kwenye sehemu ile na akalitoka jangwa la Badr kabla ya kuchwa jua.
Sasa Mtume (s.a.w.w.) kwa mara ya kwanza alikabiliwa na tofauti baina ya masahaba zake kuhusu ugawaji wa ngawira, na kila kikundi kilidai kwamba kilikua bora zaidi ya vile vingine. Wale walioulinda mnara wa kuamrishia wa Amiri jeshi mkuu walidai kwamba wao wameuhami uhai wa Mtume (s.a.w.w.) na hakuna liwezalo kuwa muhimu zaidi ya hili. Wale waliokusanya ngawira walidai ubora juu ya wengine. Na wale waliomfuatia adui hadi dakika ya mwisho kuuwezesha ukusanyaji wa ngawira walijifikiria kuwa wenye kustahili zaidi kuliko wengine.

Hakuna jambo lenye madhara zaidi kwa jeshi kuliko kuibuka tofauti miongoni mwa mtu mmoja mmoja. Ili kuzizuia tamaa za kidunia na kukomesha makelele, Mtume (s.a.w.w.) aliziweka ngawira zote chini ya Abdullah bin Kaad na akawateuwa watu fulani kumsaidia kuzisafirisha na kuzihifadhi kwa usalama hadi litakapopatikana suluhisho la tatizo lile.

Kanuni ya usawa wa haki ilihitajia kwamba jeshi zima liwe limegawana ile ngawira zile, kwa sababu wote walikuwa wamefanya kazi na kubeba majukumu na hakuna hata mtu mmoja pekee ambaye angaliweza kupata lolote lile mpaka pale wale wenzie nao walipofanya kazi pia. Mtume (s.a.w.w.) alipokuwa njiani, alizigawa zile ngawira sawa kwa sawa. Ama kuhusu Waislamu waliouawa kishahidi aliyatenga mafungu yao na kuwapa warithi wao.

Kile kitendo cha Mtume (s.a.w.w.) cha kuzigawa zile ngawira sawa kwa sawa kilikuwa kimemuudhi Sa’ad bin Waqqas aliyemwambia Mtume (s.a.w.w.): “Je, unanifikiria mimi niliye mmoja wa watu watukufu wa Bani Zuhrah, kuwa sawa na hawa wapagazi wa maji na wakulima wa Yathrib?” Mtume (s.a.w.w.) alihuzunishwa mno kuyasikia maneno haya na akasema: “Lengo langu kwenye vita hivi lilikuwa ni kuwasaidia wanyonge dhidi ya wenye nguvu nami nimeteuliwa kuishika kazi ya Utume ili kuung’oa ubaguzi na ubora wa kidhana, na kuweka usawa katika haki za wanadamu badala ya hayo.”

Kama ilivyoelezwa kwenye Aya ya Qur’ani ihusuyo Khumsi: “..... Moja ya tano ya ngawira za vita ni kwa ajili ya Allah, rasuli wake, jamaa wa karibu, yatima, masikini na msafari.” (Surah al-Anfal, 8:41). Hata hivyo kwenye tukio hili Mtume aliigawa khumsi pia miongoni mwa wanajeshi. Inawezekana kwamba aya ihusianayo na khumsi ilikuwa bado haijafunuliwa; au Mtume (s.a.w.w.) aliyatumia mamlaka aliyopewa, akaacha kuichukua Khums ili kuyazidisha mafungu ya Mujahidiin.

Mateka Wawili Waliuwawa Njiani

Kwenye kimoja cha vituo vya mapumziko wale mateka waliletwa mbele ya Mtume (s.a.w.w.). Miongoni mwao Nazar bin Haarith, aliyekuwa mmoja wa maadui wakuu wa Waislamu alinyongwa kwenye njia nyembamba ya ‘Safraa’ na Uqbah bin Abi Mu’it aliuawa kwa amri ya Mtume (s.a.w.w.) mahali paitwapo Irquz Zabiyyah. 29

Sasa swali linaibuka hapa kuhusu ni kwa nini, ingawa ulikuwako ukweli kwamba maamrisho ya Uislamu juu ya wafungwa wa vita ni yale yasemayo kwamba wao ni watumwa wa Waislamu na Mujahidiin, nao wanaweza kuuzwa kwenye soko kwa bei nafuu, Mtume (s.a.w) alikubali kunyongwa kwa watu hawa wawili, na vipi aliweza kuuchukua uamuzi huu wakati alikuwa tayari kaishawaambia Waislamu kuhusiana na mateka wa Badr: “Muwe wema kwa mateka.”30

Abu Aziz, mshika bendera wa Waquraishi kwenye vita vya Badr, anasema: “Tangu siku ambayo Mtume (s.a.w.w.) alitoa mapendekezo yake juu yetu, tulikuwa waheshimiwa mno mbele ya Waislamu kiasi kwamba hawakukigusa chakula mpaka tulipolishwa kwanza.”

Katika mazingira haya, kunyongwa kwa hawa mateka wawili kuliamrishwa kwa ajili ya ustawi wa Waislamu wote na wala hakikuwa kitendo cha kulipiza kisasi, kwa sababu hawa watu wawili walikuwa machifu wa makafiri nao walikuwa wapangaji wa makri dhidi ya Uislamu na wachocheaji wa makabila.
Inawezekana kwamba Mtume (s.a.w.w.) alikuwa na uhakika kwamba kama wakiachiwa watajitumbukiza tena katika vitendo hivyo vya hatari.

Watu Walitumwa Na Mtume (S.A.W.W) Kwenda Madina

Abdullah bin Ramahah na Zayd Harithah walitumwa na Mtume (s.a.w.w.) waende Madina na wafike huko upesi iwezekanavyo na kuwapasha habari njema Waislamu kwamba Uislamu umeshinda na viongozi wa makafiri kama vile ‘Utbah, Shaybah, Abu Jahl, Zam’ah, Abul Bakhtari, Umayyah, Nabiyyah, Manbah n.k wameuawa. Walifika wakati Waislamu walipokuwa wakirejea kutoka kwenye mazishi ya binti wa Mtume (bibi Ruqaiyah), aliyekuwa mkewe Bwana Uthman, na hivyo furaha ya ushindi katika vita hivi ilichanganyika na huzuni juu ya kifo hicho.

Wakati huo huo, washirikina na Wayahudi walishtuka mno na kufadhaika, kwa sababu katu hawakutegemea kwamba, Waislamu watabarikiwa kwa ushindi wa aina ile. Hivyo basi, walijitahidi kuwafanya watu waamini kwamba taarifa zile zilikuwa za uwongo. Hata hivyo, ukweli ulithibitika kabisa kwa kuwasili kwa lile jeshi la Uislamu pamoja na wale mateka wa Kiquraishi.

Watu Wa Makka Waja Kutambua Kuuawa Kwa Machifu Wao

Haysam?n Khaz?’i alikuwa mtu wa kwanza kuwasili Makka na kuwaarifu watu kuhusu lile tukio la kumwaga damu kule Badr, pamoja na kuuawa kwa machifu wao kwenye vita ile. Abu Raafi aliyekuwa mtumwa wa Abbas siku zile na baadaye akawa sahaba wa Mtume na wa Amiri wa Waumini (a.s.) anasema: “Katika siku hizo, Uislamu uliiangaza nyumba ya Abbas.

Yeye, mkewe Ummul Fadhl na mimi mwenyewe tulisilimu, lakini tuliificha itikadi yetu kwa kuwachelea watu. Taarifa za kuuawa kwa maadui wa Uislamu kule Badr zilipoenea tulifurahi mno. Hata hivyo, Waquraishi na wasaidizi wao walihuzunika na kushituka mno.

Abu Lahab ambaye hakushiriki kwenye vita hivi na badala yake alimpeleka mtu mwingine, alikuwa ameketi karibu na kisima cha Zamzam. Mara kwa ghafla watu wakaleta taarifa ya kwamba Abu Sufyan ibn Harb amefika. Abu Lahab akasema: “Mwambie aonane nami upesi iwezekanavyo.”

Abu Sufyani alikuja, akakaa karibu na Abu Lahab na akampa tarifa kamili ya matukio ya Badr. Abu Lahab akakumbwa na fadhaa na woga moyoni mwake kama aliyepigwa na radi. Baada ya kuunguzwa na homa kali kwa muda wa siku saba alikufa kwa maradhi yasiyoeleweka.

Hadith ya kushiriki kwenye vita vya Badr kwa baba mkubwa wa Mtume (s.a.w.w.) (aliyekuwa mmoja wa watu waliotekwa na Waislamu) ni moja ya matatizo ya historia. Yawezekanaje kwamba Abbas aliwasisitiza watu wa Madina wakati wa mapatano ya ‘Aqabah’ kumsaidia Mtume (s.a.w.w.) na kisha aambiwe kwamba alishiriki katika vita hii?

Utatuzi wa tatizo hili umo katika yale maneno aliyoyasema yule mtumwa wake Raafi. Anasema kwamba alikuwa mmoja wa watu ambao, kama alivyokuwa kaka yake Abu Twalib, aliuamini Upweke wa Allah na Utume wa mwana wa nduguye, lakini aliificha itikadi yake, akiyazingatia mahitaji ya wakati ule, ili aweze kumsaidia mwana wa nduguye na kumtaarifu juu ya mipango miovu ya Waquraishi, kama alivyofanya wakati wa Vita vya Uhud.

Kuenea kwa taarifa za kuuwawa kwa watu sabini kutoka miongoni mwa wapenzi wa Waquraishi zilizababisha wasiwasi kwenye familia nyingi na kuzifanya kuwa na huzuni na majonzi.31

Mayowe Na Maombolezo Yapigwa Marufuku

Ili kuwaweka Waquraishi katika hali ya ghadhabu na uchungu na kuhakikisha kwamba daima watu watakuwa tayari kulipiza kisasi cha damu ya mashujaa wao, Abu Sufyan ibn Harb alitoa amri ya kwamba hakuna yeyote atakayekuwa na haki ya kulia au kuomboleza wala mshairi yeyote yule asisome beti za maombolezo kwa kuwa vitu hivi hupunguza hisia za kulipiza kisasi na matwezo ya mara kwa mara ya maadui. Ili kushawishi chuki miongoni mwa watu, vile vile alitangaza ya kwamba hatalala na mwanamke yeyote mpaka atakapolipiza kisasi juu ya waislamu kwa ajili ya damu ya wale waliouawa kule Badr.

Aswad bin Muttalib alipatwa na uchungu mwingi kutokana na kuwapoteza wanawe watatu. Mara, ghafla akasikia mayowe ya kilio cha mwanamke mmoja. Alifurahi na akadhania ya kwamba kule kuwalilia wale waliouawa Badr kumeruhusiwa. Alituma mtu kwenda kuithibitisha dhana yake. Hata hivyo, matokeo ya uchunguzi huu hayakuwa sawa na alivyotaka, kwa sababu yule mwanamke alikuwa akimlilia ngamia wake aliyepotea, na kumlilia ngamia aliyepotea hakukupigwa marufuku kufuatana na ile amri ya Abu Sufyan. Aswad alilihisi mno jambo hili na akatunga beti za shairi. Hapa chini tunatoa tafsiri ya beti mbili miongoni mwazo:

“Je, anamlilia ngamia wake aliyepotea, na je anakesha katika nyakati za usiku kwa kule kumpoteza kwake? Hapana. Haistahili wakati huu kwamba amlilie ngamia wake. Bali ni muhimu kwamba alie kwa ajili ya wale waliouawa na ambao kwa kifo chao furaha, heshima na utukufu navyo vimepotea.”32

Uamuzi Wa Mwisho Juu Ya Mateka

Kwa mujibu wa sheria za Kiislamu wafungwa wa kivita huwa watumwa wa Waislamu na kila mmoja wao anahitajika kufanya kazi kwa nguvu zake zote. Watu walioelimika hutumikishwa katika kuwaelimisha wenzao na wataalamu wa viwanda hutoa elimu kwenye nyanja ya viwanda. Watumwa hawa hawawezi kuwa huru mpaka wanunuliwe kwanza na mtu fulani, hii imekuwa ni kawaida aliyokuwa akiitumia Mtume (s.a.w.w.) na Waislamu kwenye vita vilivyopiganwa na utekaji wa nchi walioufanya.

Hivyo, kuhusiana na vita hivi (vya Badr), iliamuliwa ya kwamba watu wenye elimu wangeliweza kuwa huru kama wangeliwafundisha wavulana kumi kusoma na kuandika. Wengine wangeliweza kununua uungwana wao kwa kulipa fidia ya kiasi cha kuanzia dirhamu elfu moja hadi elfu nne. Na kuhusu watu walio maskini, waliweza kuachiliwa bila ya kutozwa fidia yoyote.

Taarifa hizi zilipofika Makka zilileta furaha kuu miongoni mwa ndugu wa wale mateka na wakapeleka pesa za kulipia fidia mjini Madina ili waweze kuachiliwa. Suhayl bin Amr alipoachiliwa kwa kulipa fidia, Sahaba mmoja wa Mtume (s.a.w.w.) aliomba ruhusa kumng’oa Suhayl meno yake ya mbele ili baada ya hapo asije akausema tena Uislamu kwa ubaya. Mtume (s.a.w.w.) hakutoa ruhusa ya kufanya hivyo na akasema kwamba hiyo ilikuwa sawa na kumtia mtu kilema, jambo lisiloruhusiwa kwenye Uislamu.

Abil Aas, mkwewe Mtume (s.a.w.w.) na mume wa binti yake33 Zaynab, alikuwa mfanya biashara mwenye kuheshimika wa mjini Makka. Alimwoa Zaynab kwenye zama za Ujinga34 naye hakusilimu baada kuanza kwa kazi ya Utume. Vilevile alishiriki kwenye vita ya Badr na alitekwa wakati mkewe Zaynab alikuwa mjini Makka. Ili kumkomboa mumewe alipeleka Madina kidani alichopewa na mama yake, Bibi Khadija wakati wa ndoa yake.
Mtume (s.a.w.w.) aliwahi kukiona kile kidani alichokileta binti yake. Alilia na akaikumbuka mihanga mikubwa mikubwa aliyoitoa Bibi Khadija kwa ajili ya Uislamu na utajiri mwingi alioutumia kwa ajili ya maendeleo ya dini ya Allah. Ili kuithibitisha heshima kwa mali ya umma aliwageukia wafuasi wake na kuwaambia: “Kidani hiki ni mali yenu nanyi munayo haki kamili juu yake. Kama mtakubali kinaweza kurudishwa na Abil Aas anaweza kuachiliwa bila ya kumtoza fidia yoyote ile.” Masahaba zake walikubali maoni yake.

Kauli Ya Ibn Abil Hadid

Anasema: “Nililitaja tukio la kidani cha Zaynab mbele ya mwalimu wangu Ja’afar Basri Alawi na akaithibitisha, lakini akaongezea kusema: “Je, haikufaa kwamba makhalifa wangalimfariji Fatimah kwa kumrudishia Fadak japo idhaniwe kwamba ilikuwa ni mali ya Waislamu?” Nikasema: “Kwa mujibu wa Hadith moja, Mitume hawaachi urithi wowote na kwa sababu hiyo, Fadak ni mali ya Waislamu. Katika hali hii, vipi mali ya Waislamu apewe binti wa Mtume?” Yule mwalimu akasema: “Je, kile kidani alichokipeleka Zaynab kwa ajili ya kuachiliwa kwa Abil Aas, hakikuwa mali ya Waislamu?’

Abil Hadid anasema: “Nikasema kwamba Mtume alikuwa ndiye mtoa sheria naye alikuwa na mamlaka kwenye mambo yote, ambapo wale makhalifa hawakuwa na madaraka ya aina hiyo.35 Mwalimu akasema: Sisemi kwamba wale makhalifa waichukue Fadak kwa nguvu kutoka kwa Waislamu na kumpa Fatimah. Ninalosema mimi ni kwamba mtawala wa wakati ule hakuwataka ushauri Waislamu kuhusu kurudisha Fadak. Kwa nini hakusimama kama alivyofanya Mtume na kusema: “Enyi watu! Fatimah yu binti wa Mtume wenu. Anataka kwamba bustani ya Fadak iwe chini ya mamlaka yake kama ilivyokuwa kwenye zama za uhai wa Mtume. Je, mnakubali kwamba Fadak irudishwe kwake?”

Ibn Abil Hadid anaandika mwishoni hivi: “Sikuweza kusema lolote katika kuyajibu maelezo ya kiufasaha ya yule mwalimu na nilisema haya tu katika kuyaunga mkono: ‘Abul Hassan Abdul Jabbar naye amewalaumu makhalifa kuhusiana na jambo hili na anasema kwamba ingawa matendo yao yaliafikiana na sheria,36 hawakujali heshima na cheo alichostahiki Zahra.37

 • 1. Biharul Anwaar, Juzuu 19, uk. 217.
 • 2. Maghaazil-Waaqid, Juzuu 1, uk. 20.
 • 3. Tarikhul Kamil, Juzuu 2, uk. 81.
 • 4. Tarikhut-Tabari, Juzuu 2, uk. 138, na Tarikhul Kamil, Juzuu 2, uk. 82.
 • 5. Siiratu Ibn Hishamu, Juzuu 2, uk. 248-249.
 • 6. Maghaazil-Waaqidi, Juzuu 1, uk. 48.
 • 7. Tarikhul Kamil, Juzuu 2, uk. 82.
 • 8. Siiratu Ibn Hisham, Juzuu1, uk. 615.
 • 9. Al-Imtaa'ul Asmaa' uk. 74.
 • 10. Tarikhut-Tabari, Juzuu 2, uk. 140.
 • 11. Maghaazil-Waaqidi, Juzu 1, uk. 248; SiiratuI Halabi, Juzuu 2, uk. 160; na Bihaarul Anwaar, Juzuu 19, uk. 217.
 • 12. Tarikhut-Tabari, Juzuu 2, uk. 140.
 • 13. Maghaazil-Waaqidi, Juzuu 1, Uk. 48; Siiratu Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 615.
 • 14. Siiratu Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 617.
 • 15. Siiratu Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 620; na Tarikhut-Tabari, Juzuu 2, uk. 144.
 • 16. Tarikhut-Tabari, Juzuu 2, uk. 145. Siirah-i Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 620;
 • 17. Tabaqaat, Juzuu 2, uk. 25.
 • 18. Nahjul Balaghah, Kalimaatu Qasaar, uk. 214.
 • 19. Siiratu Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 622.
 • 20. Maghaazi, Juzuu 1, uk. 62; na Bihaarul Anwaar, Juzuu 2, uk. 234.
 • 21. Tarikhut-Tabari, Juzuu 2, uk. 148; na Siiratu Ibn Hisham, Juzuuu 1, uk. 625.
 • 22. Nahjul Balaghah, Barua 28 na 46.
 • 23. Tarikhu Ibn Hisham, Juzuu I, uk. 626.
 • 24. Tarikhut-Tabari, Juzuu 2, uk. 149.
 • 25. Siiratu Ibn Hisham, Juzuuu 1, uk. 628.
 • 26. Tabaqaatu Ibn Sa'ad, Juzuu 2, uk. 23.
 • 27. Siiratu Ibn Hisham, Juzuu 2, uk. 206-207; Maghaazi, Juzuu 1, Uk. 137-138.
 • 28. Maghaazil-Waaqidi, Juzuu 1, uk. 117.
 • 29. Siiratu Ibn Hisham, Juzuu 2, uk. 645.
 • 30. Siiratu Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 645..
 • 31. Fahristun-Najaashi, uk. 5.
 • 32. Siiratu Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 648.
 • 33. Binti wake wa kulea.
 • 34. Maelezo haya ni hoja yenye nguvu mno kuthibitisha kuwa mabinti hawa watatu, Zainab, Ruqayya na Ummu Kulthum hawakuwa mabinti wa kuzaa wa Mtume, kwani ni dhahiri isingelifikirika kwa mtu kama Mtume (s.a.w.w.) aliyekuwa na shakhsia ya tawhidi kabla ya kukabidhiwa utume, kuwaoza mabinti zake kwa mtu aliyekuwa na kila dalili ya miale ya moto wa shirk - Mhariri
 • 35. Sasa twaweza kumuuliza Abil Hadid ikiwa hivyo ndivyo, ni mantiki gani imewasukuma kuuridhia uharamisho wa Umar juu ya ndoa ya muda? Na kwa nini mwawahimiza wafuasi wenu kuiendea sala ya tarawehe iliyoasisiwa na Umar? - Mhariri.
 • 36. Kwa mtazamo wake yameafikiana na sheria, na kama hadithi za kuzushiwa Mtume ndio sheria anayoifikiria yeye, basi ajue ipo Siku ya malipo. Lakini kama Qur'ani ndio sheria, basi hamna shaka kuwa kwa mujibu wa Qur'anii kitendo hicho ni unyang'anyi na dhulma dhidi ya mali na milki ya Fatimah Zahra (a.s.) -Mhariri.
 • 37. Sharhun- Nahjul Balaghah cha Ibn Abil Hadid, Juzuu 14, uk. 191.