Sura Ya 31: Mipango Ya Hatari Ya Wayahudi

Vita vya Badr vilikuwa dhoruba ya kuogofya iliyovuma katikati ya Rasi ya Uarabuni. Hii ni dhoruba iliyong’oa mizizi mingi ya kale ya ushirikina na ibada za masanamu. Baadhi ya mashujaa na watetezi wa Waquraishi waliuwawa au kutekwa na wengine walikimbia katika hali ya kufedhehesha mno. Taarifa za kutimuliwa kwa Waquraishi zilienea kila mahali Uarabuni. Hata hivyo, baada ya dhoruba hii, ilikuwapo aina fulani ya utulivu kwa kitambo hivi ulioandamana na hofu na mshtuko wa fikara, utulivu huu wa kitambo fulani ulipitwa mara kwa mara na taswira ya hali ya ujumla ya siku zijazo ya Rasi ile.

Makabila yaliyokuwa yakiabudu masanamu, Wayahudi matajiri wa Madina na Wayahudi wa Khaybar na Wadiul Quraa walikuwa wakiyaogopa sana maendeleo endelevu ya ile serikali mpya, na waliyaona maisha yao kuwa yako kwenye hatari kwa sababu hawakuamini ya kwamba Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) atakuwa na nguvu kiasi kwamba atawaangamiza Waquraishi waliokuwa na nguvu zenye umri wa karne nzima.
Wayahudi wa kabila la Bani Qaynaq? waliokuwa wakiishi mjini Madina nao waliutawala uchumi wa mji ule, waliogopa zaidi kuliko wengine, kwa sababu maisha yao yalichanganyika kabisa na yale ya Waislamu na ilikuwako tofauti baina yao na wale Wayahudi wa Khaybar na Wadiul Quraa walioishi nje ya mji wa Madina na mbali kutoka kwenye ukanda ulio chini ya mamlaka ya Waislamu. Hivyo basi, kwa sababu hii, kabila la Qaynaq? likajishughulisha zaidi kuliko wale wengine na wakaanzisha vita baridi vya propaganda kwa kueneza maneno yenye kuchochea na mashairi ya uchochezi. Hivyo, kivitendo wakayakataa yale mapatano yaliyofanywa katika mwaka wa kwanza wa Hijiriya.

Hata hivyo, vita hivi baridi havikuhalalisha kwamba majeshi ya Uislamu yajibu kwa silaha kali, kwa sababu, kama fundo laweza kufunduliwa kwa vidole, basi si lazima kulifundua kwa meno. Zaidi ya hapo Mtume (s.a.w.w.) aliweka mbele umuhimu wa kudumisha umoja wa kisiasa na sheria na kanuni njema.

Akitoa onyo lake la mwisho kwa Wayahudi, Mtume (s.a.w.w.) alitoa hotuba kali kwenye soko la Bani Qaynaq?’. Katika hotuba hii aliwaeleza Wayahudi mambo mengi likiwamo hili: “Majaaliwa ya Waquraishi yamewatendea haki. Ni fundisho kwenu ninyi vile vile. Ninachelea ya kwamba msiba huu huu unaweza kukukamateni. Wako wasomi na wanachuoni wa kidini miongoni mwenu. Hamna budi kuthibitisha kutoka kwao ili kwamba waweze kukuelezeni wazi wazi kwamba mimi ni Rasuli wa Allah na kwamba ukweli huu umeandikwa kwenye kitabu chenu (Taurati).”

Wayahudi hao wakaidi na wenye kiburi, sio tu kwamba hawakunyamaza baada ya kuyasikia maneno ya Mtume (s.a.w.w.), bali walimjibu kwa kauli yenye kukasirisha, wakasema: “Je, unafikifi sisi ni wanyonge na tusiozijua mbinu za kivita kama Waquraishi? Mlilikabili kundi lisilokuwa na ujuzi wa kanuni na mbinu za mapigano. basi nguvu ya wana wa Qaynaq? itakudhihirikieni mtakapokutana nao kwenye uwanja wa vita.”1

Maneno machungu na ya dharau ya Bani Qaynaq?’ na kule kuimba yale maneno ya uchochezi wa vita na tenzi za watetezi wao havikuwa hata na athari zozote mbaya katika tabia za Waislamu. Hata hivyo, walipewa onyo la mwisho kwa mujibu wa kanuni ya siasa za Kiislamu na ilidhihirika ya kwamba wakati ule, lile fundo lilibidi kufunguliwa kwa njia nyingine au sivyo ujasiri, uasi, na udhalimu vitaongezeka siku hadi siku. Hivyo basi, Mtume (s.a.w.w.) alisubiri apate fursa ya kuwapa Wayahudi wale adhabu kali.

Cheche Yawasha Moto Wa Vita

Wakati mwingine inatokea kwamba jambo dogo hupelekea kwenye mapinduzi makubwa na mabadiliko ya kijamii, yaani tukio dogo hupelekea kwenye tukio kuu na makundi husika huchukua njia ya kumaliza matukio mengi mengineyo pia (ukiachilia mbali tukio lile).

Sababu ya kuanza kwa vita vya kwanza vya dunia, ambavyo ni moja ya tukio kuu la historia ya mwanadamu, ilikuwa ni tukio dogo tu, lililotoa sababu kwa mataifa makuu kujitumbukiza kwenye vita. Tukio lililokuwa sababu ya kuanza kwa vita hivyo lilikuwa ni kuuawa kwa mwana wa Mfalme Fransis Ferdinand aliyetegemewa kuwa mrithi wa kiti cha enzi cha Austria. Tukio hili lilitokea mnamo tarehe 28 Juni 1914 na baada ya mwezi mmoja na siku chache, Vita vya kwanza vya Dunia vilianza kwa Ujerumani kuishambulia Ubelgiji. Matokeo ya vita hivi ni kwamba watu milioni kumi waliuawa na wengine milioni ishirini walijeruhiwa.

Waislamu waliudhishwa mno na ukaidi na kiburi cha Wayahudi na walikuwa wakisubiri watende tukio baya ili Waislamu waamke dhidi yao. Siku moja ilitokea kwamba mwanamke mmoja wa kiarabu alikwenda kwenye mtaa wa masoko wa Bani Qaynaq? kuuza kitu fulani karibu na duka la sonara wa kiyahudi. Yule mwanamke alijihadhari kwamba mtu yeyote asiuone uso wake (yaani alivaa Hijab). Hata hivyo, Wayahudi wa Bani Qaynaq? walishikilia ya kwamba afunuliwe uso wake. Kwa kuwa alikataa kufanya vile, yule mwuza duka alitoka dukani mwake na kuushona ukaya wa vazi lake mgongoni mwake.
Matokeo yake ni kwamba yule mwanamke alipoamka baada ya kitambo kidogo, sehemu ya mwili wake ikawa wazi. Baada ya hapo wale wanaume (wa Bani Qaynaq?) wakamdhihaki.

Suala la sifa na heshima, jambo lililo muhimu kwenye kila jamii, lilipewa muhimu sana miongoni mwa Waarabu, na hasa miongoni mwa makabila ya kibedui ambao walikimbilia umwagaji damu kutokana na shutuma ndogo mno juu ya heshima yao. Hivyo basi, hali ya kusikitisha ya yule mwanamke mgeni, iliibua hisia za Mwislamu, naye akamuua yule sonara.

Kwa kawaida kitendo hiki kilichotendwa kwenye eneo la Wayahudi wenyewe kisingeliweza kuachwa bila ya kuchukuliwa hatua kutoka upande wao. Hivyo, wakamshambulia yule mwislamu kwa pamoja na wakamwua.

Hatuhusiki juu ya ukweli ya kwamba mauji ya yule Myahudi yaliyotokana na kumtusi yule mwanamke yaliafikiana na kanuni na sababu za kiakili au la. Hivyo, Mwislamu mmoja tu kushambuliwa na mamia ya Wayahudi kwa pamoja, kulikuwa jambo la kuudhi mno.

Hivyo, taarifa za mauaji ya kimsiba na kusikitisha ya yule mwislamu zilizikoroga hisia za kiutu za Waislamu waliodhamiria kuliweka sawa jambo lile na kukiharibu kabisa kituo cha ufisadi.

Wasomaji wa tenzi wa Bani Qaynaq? walitambua kwamba jambo lile limekuwa gumu nalo halikuwezekana tena kwao kushauriana na kuendelea na biashara zao kwenye masoko na mitaa ya Madina. Hivyo, upesi sana wakakimbilia kwenye nyumba zao zilizo kwenye ngome ndefu na madhubuti na kuingia humo ingawa walikuwa wakizisoma zile tenzi zao kwa ushujaa mkuu.

Pia walifanya kosa kwa kupanga kufanya hivi. Kama wangalijuta kwa yale waliyoyatenda na wakaomba msamaha bila shaka wangaliweza kusuluhisha mambo na Waislamu kutokana na tabia ya msamaha ya Mtume (s.a.w.w.). Hata hivyo, kule kujifungia kwenye ngome zao kulikuwa ni dalili ya upinzani na uadui unaoendelea. Mtume (s.a.w.w.) aliamrisha ile ngome ya adui izingirwe.

Majeshi ya Waislamu yaliizunguka ngome yote tangu kwenye mwishilizio mmoja hadi ule mwingine. Kuzingirwa huku kulidumu kwa siku kumi na tano na kuingia kwa mahitaji ya maisha kwenye ngome hiyo kulizuiwa. Mawasiliano yoyote na watu hawa yalipigwa marufuku pia.

Wayahudi walipiga magoti ikiwa ni matokeo ya vizuizi vya kiuchumi. Walilifungua lango la ngome ile, baada ya kutoa ishara za masharti yaliyotakiwa wakajisalimisha kwa Waislamu. Vile vile waliamua ya kwamba uamuzi wa Mtume (s.a.w.w.) vyovyote vile iwavyo, wataufuata.

Mtume (s.a.w.w) alidhamiria kutoa adhabu kali kwa wakaidi na wapinzani wa umoja wa kisiasa mjini mle Madina.

Hata hivyo, aliepuka kuchukua hatua kutokana na msisitizo wa Abdullah bin Ubay aliyekuwa mmoja wa wanafiki wa Madina na akasilimu kwa dhahiri. Hivyo basi, iliamuliwa kwamba Wayahudi wasalimishe silaha na utajiri wao na wautoke mji wa Madina upesi iwezekanavyo na jukumu hili litimizwe chini ya ukaguzi wa afisa mmoja aliyeitwa Ubadah bin Saamit.

Wayahudi hawakupata njia yoyote nyingine ila kuutoka mji wa Madina na wakaenda Wadiul Qara na baada ya hapo kwenda Azra’aat kwenye ukanda wa Shamu.

Umoja wa kisiasa wa Madina ulirudi tena kwa kutolewa kwa Wayahudi wa Qaynaq?’. Wakati huu umoja wa kisiasa uliungwa na umoja wa kidini pia, kwa sababu tukiwaachilia mbali Waislamu, hakukuwepo watu wengine walio wengi mjini Madina, na idadi ya Waarabu wenye kuabudu masanamu na wanafiki ilikuwa ndogo mno ikilinganishwa na ile ya waumini.2

Taarifa Mpya Zafika Madina

Katika maeneo madogo, kwa kawaida tarifa huenea upesi kama radi, kutoka mtu hadi mtu. Kwa sababu hii, taarifa zenye kuhusu njama za kufanya mabaya na mikutano dhidi ya Waislamu kwenye kila mkoa zilifika makao makuu ya Uislamu upesi sana kupitia kwa wasafiri waadilifu na marafiki walio macho. Zaidi ya hapo Mtume (s.a.w.w.) mwenyewe binafsi alikuwa mfahamivu mno na alizikomesha njama za kufanya ubaya tangu mwanzoni kabisa. Mara tu baada ya taarifa kupokewa kwamba kabila fulani lilikuwa likipanga kukusanya silaha na watu, upesi sana alipeleka kikosi kulizuia lile lengo la yule adui, au yeye mwenyewe alikwenda upesi sana akifuatana na jeshi litoshelezalo, na kulizingira lile eneo la adui na kuushinda mpango wake. Zifuatazo hapa chini ni mukhtasari wa baadhi ya Ghazwaah (vita ambazo Mtume s.aw.w alishiriki) zilizopiganwa katika mwaka wa pili wa Hijiriya.

Ghazwatul Kadar

Jimbo la ukanda wa kati wa kabila la Bani Salim uliitwa Kadar. Ilipokewa taarifa mjini Madina kwamba watu wa kabila lile walikuwa wakipanga kukusanya silaha na kuja kuyashambulia makao makuu ya Uislamu. Mtume (s.a.w.w.) alipotoka mji wa Madina alimteuwa mtu mwingine kuwa mwakilishi wake na kuyaweka mambo ya serikali mikononi kwake.

Safari hii alimteuwa Ibn Ummi Makhtum kuwa naibu wake mjini Madina, na yeye akatoka pamoja na kikosi kwenda kwenye mkoa wa katikati wa Kadar.

Hata hivyo, wale maadui walikuwa wametawanyika kabla ya kuwasili kwa Waislamu. Hivyo, Mtume (s.a.w.w.) alirejea Madina bila ya mapigano yoyote yale, lakini kwa kujiridhisha kwake alipeleka tena jeshi mahali pale pale chini ya uongozi wa afisa mmoja aliyeitwa Ghalib Abdullah. Jeshi hili lilirudi na ushindi baada ya mapigano madogo ambayo ndani yake watu wao watatu waliuawa.3

Ghazwatus-Sawiiq

Waarabu wa zama za ujahilia walikuwa wakifanya viapo vya ajabu. Kwa mfano, baada ya vita vya Badr Abu Sufyan aliapa kwamba hatamkaribia mkewe mpaka alipize kisasi juu ya Waislamu kwa kuuawa kwa Waquraishi. Ili kukitimiza kiapo chake hiki alilazimika kuendesha mashambulizi. Alisafiri na watu mia mbili na kwa msisitizo wa Salam bin Mushkam, chifu wa kabila la Kiyahudi la Bani al-Nuzayr, waliokiishi nje ya Madina, Abu Sufyan alimuuwa mwislamu mmoja na akachoma bustani ya mitende kwenye jimbo la Arz. Upesi sana mtu mmoja akatoa taarifa ya tukio lile mjini Madina. Mtume (s.a.w.w.) alitoka mjini Madina na kumfuatilia yule adui kiasi cha umbali fulani. Hata hivyo, Abu Sufyan na wapiganaji wake walikuwa wameshakimbia. Yule adui akiwa njiani aliacha mifuko ya ‘Sawiiq’ (chakula kilichotayarishwa kwa unga na tende). Waislamu waliichukua mifuko ile na wakavipa vita hivi jina la ‘Ghazwatus Sawiiq.’4

Ghazwah Zil Amr

Taarifa zilifika mjini Madina kwamba watu wa kabila lililokuwa likiitwa ‘Ghatfan’ wamekusanyika pamoja na walidhamiria kuuteka mji wa Madina. Mtume (s.a.w.w.) alitoka na watu mia nne na hamsini kwenda kuwakabili maadui hawa. Maadui wakawa na woga na wakakimbilia kwenye milima. Wakati ule ule ilinyesha mvua kubwa na nguo za Mtume (s.a.w.w.) zililowa. Hivyo, alikwenda umbali fulani kutoka pale lilipokuwa jeshi lake. Hapo akazivua nguo zake akakaa chini ya kivuli. Wale maadui walikuwa wakimwona Mtume (s.a.w.w.) pale.
Shujaa mmoja kutoka miongoni mwao akajinufaisha na hali ile. Alishuka kutoka kule mlimani akiwa kashika upanga uliofutwa na akiwa amesimama karibu na Mtume (s.a.w.w.) alisema kwa sauti ya ukali: “Ni nani awezaye kukuokoa wewe leo hii kutokana na upanga wangu mkali?”

Mtume (s.a.w.w.) akamjibu kwa sauti kuu: “Allah.” Neno hili lilikuwa na athari kubwa mno juu ya mtu huyu kiasi kwamba alianza kutetemeka kwa woga, na ule upanga ukamponyoka ukaanguka. Mtume (s.a.w.w.) akasimama upesi, akauokota, akaanza kumkabili na kumwambia: “Ni nani sasa awezaye kukuokoa kutokana nami?” Kwa kuwa yule mtu alikuwa muabudu masanamu na alijua ya kwamba miungu wake wa miti hawakuwa na uwezo wa kumhami kwenye ule wakati mgumu, alijibu akisema: “Hakuna.”

Wanahistoria wanasema kwamba yule mtu alisilimu pale pale lakini kitendo hiki hakikutokana na woga kwa sababu alibakia kuwa madhubuti kwenye imani yake. Sababu ya kusilimu kwake ni mwamko wa tabia yake, kwa sababu kushindwa kwake asikotegemea na kwa kimiujiza kulizigeuzia fikara zake kwenye ulimwengu mwingine na akatambua kwamba Mtume (s.a.w.w.) anao uhusiano na ulimwengu ule. Mtume (s.a.w.w.) alimpeleka kwenye ulimwengu wake (uhusianao na kusilimu kwake) na akamrudishia upanga wake. Baada ya mtu yule kwenda mbele kidogo akampa Mtume (s.a.w.w.) ule upanga wake, na akasema: “Kwa vile wewe u kiongozi wa hili jeshi la kuongoza watu waliopotea, unayo haki zaidi ya kuimiliki silaha hii.”5

Waquraishi Wabadili Njia Yao Ya Msafara Wa Kibiashara

Pwani ya Bahari ya Shamu imekuwa na hatari kwa Waquraishi kutokana na jeshi la Kiislamu na watu waliofanya mapatano na Waislamu. Hivyo basi, walifanya mkutano wa ushauriano na kuisoma ile hali. Wakaambiana: “Kama biashara yetu ikiahirishwa, pole pole tutaipoteza mitaji yetu na matokeo yake yatakuwa ni kusalimu amri kwa Waislamu. Na kama tukiendelea na biashara, hatuna tegemeo la kufaulu, kwa sababu kwa kawaida Waislamu huzinyakua bidhaa zetu tunapokuwa njiani.”

Mmoja wao alishauri kwamba waende Shamu kupitia Iraq na ushauri huu ulikubaliwa na watu wengi kwa pamoja. Hivyo matayarisho yakafanywa kupeleka msafara pamoja na bidhaa. Abu Sufyan na Safwaan bin Umayyah binafsi walisimamia msafara ule na mtu mmoja aliyeitwa Furaat Hayyaan, wa kabila la Bani Bakr, alikuwa mwongozaji wao.

Maqrizi anaandika hivi: “Mtu mmoja wa Madina aliangalia mwenendo wa msafara ule. Aliporejea Madina alilieleza jambo lile kwa rafiki yake. Mtume (s.a.w.w.) alilitambua upesi sana na akapeleka jeshi kuelekea kwenye njia ya msafara ule chini ya uongozi wa afisa mmoja aliyeitwa Zayd bin Haarith. Kwa kuwakamata watu wawili na kuzikamata bidhaa zao waliwazuiya maadui kuendelea na safari yao.” 6

  • 1. Maghaazil-Waaqidi, Juzuu 1, uk. 176.
  • 2. Maghaazil-Waaaqidi, Juzuu 1, uk. 177-179; na Tabaqaatul-Kubra, Juzuu 2, uk. 27-38.
  • 3. Maghaazil-Waaqidi, Juzuu 1, uk. 182; na Tabaqaatul Kubra; Juzuu 2, uk.30.
  • 4. Maghaazil-Waqidi, Juzuu 1, uk. 181.
  • 5. Manaqib, Juzuu 1, uk. 164; na Maghaazil-Waaqidi, Juzuu 1, uk. 194-196.
  • 6. Al-Imtaa', uk. 112.