Sura Ya 13: Tabia Njema Za Husein, Mafanikio Ya Hali Ya Juu Na Semi Za Thamani

Tabia huundwa na vipengele vingi mbalimbali ambavyo kwamba vilivyo vya muhimu zaidi ni sifa za kifamilia ikiwa ni pamoja na desturi za nasa ba, mazingira, malezi, elimu na uzoefu muhimu na wa wazi katika maisha.

Tabia sharifu zilizo bainifu za familia ya Husein zilikuwa hazifanani na za familia nyingine yoyote ile nchini Arabia na hata Yazidi wakati mmoja alikubali ndani ya baraza lake kwamba mama yake Husein alikuwa bora zaidi kuliko mama yake yeye mwenyewe, na kwamba babu mzaa mama yake Husein (yaani Mtume s.a.w.w) alikuwa bora zaidi kuliko babu mzaa mama yake yeye Yazidi.1

Alama tambulishi hizi za familia yake zilidumisha yale matumaini ya ubora wa moyo wa Husein, na malezi yake yalihakikisha utukufu wa mwenendo na usafi wa tabia. Alipitia pia katika mabadiliko mengi ya maisha na alijifunza kuongozwa zaidi na mantiki ya akili kuliko hisia.

Hili lilikuwa limepatia upevu wa busara katika mtazamo wake wa maisha na pia umadhubuti imara na werevu wa haraka.

Wakati wataalamu wa wasifu (maelezo ya maisha ya mtu) walipojaribu kutoa maelezo mafupi juu ya sifa za Husein na mafanikio mengi, iliwabidi watumie maelezo ya lugha ya kushawishi (fasaha). Ibn Abi Shayba, mtaalamu juu ya hadith, katika kumuelezea Husein alisema, “Alikuwa ametaalimika vyema katika Qur’an na alitenda kwa mujibu wa hicho.

Alikuwa mchamungu, mwenye kujizuia na kujinyima, mkarimu, mzuri wa muonekano, fasaha wa maneno, mwenye utambuzi juu ya Mwenyezi Mungu, hoja ya dhati tukufu sana ya Mungu.” Akiyaona maelezo ya kawaida ya kusifia hayatoshi kutendea haki sifa nzuri sana za Husein, Ibn Abi Shayba aliongeza kifungu cha mwisho kwamba Husein alikuwa hoja ya dhati tukufu ya Mungu. Ibn al-Arabi, vile vile alisema kwamba Husein, mmoja wa wajukuu wa Mtume, alikuwa miongoni mwa alama za Mungu.

Ni kwa sababu ya Husein kwamba baadhi ya wale ambao wana mwelekeo wa Agnostiki (imani ya kusadiki kwamba hakuna habari za Mungu wala hazipatikani) wakati mwingine hujihisi kuvutika kwenye imani ya kumuamini Mungu. Kama vile Josh wa Malihabad, mtunga mashairi maarufu wa ki-Urdu, amesema hivi; “Ndiyo, yule Husein, ambaye uimara wake umeungana na umilele, mara moja moja huwaambia siri wanafalsafa ile iliyofichika katika usiri wenye rangi nyingi wa ulimwengu (kwamba) kuna Akili ambayo hufanya kazi na Dhati ambayo ina ujuzi. Huvuta uzingativu wetu kutoka kusujudu kwetu ndani ya swala kwenye lengo la kusujudu huku. Yeye pekee hutuonyesha yule Mmoja tu wa kuabudiwa.”

Hata katika akili finyu ambayo kwayo ibada kwa kawaida hushirikishwa, kumwabudu Mwenyezi Mungu kwa Husein na swala zake hudumu katika kutofikiwa. Alienda Hijja safari 25 kwa miguu.

Mtu anaweza kupata mfano wa kweli wa moyo wa ibada za Mungu wa Husein kutokana na ombi alilolitoa wakati wa mchana wa tarehe 9 Muharam pake Karbala kwa kufanya makubalianao ya kusitisha vita kwa muda ili kwamba aweze kutumia muda wa msitisho huo wa vita katika kufanya ibada za swala na du’a (maombi) kwa Mwenyezi Mungu, kusoma Qur’an na ibada nyingine kama hizo zenye maombi.
Ombi hili lilikubaliwa kwa shingo upande, na Husein na sahaba zake waliutumia usiku huo katika swala na maombi na mvumo wa sauti zao, katika ukimya ule wa usiku, ulifanana na mvumo wa nyuki. Halafu tena wakati wa mchana wa mwezi 10 Muharam, Husein alisimamisha swala zake za mchana pamoja na sahaba zake kwa nyakati zake, katikati kabisa ya uwanja wa mapigano wakati vita vilipokuwa katika hatua yake ya umwagaji damu mkubwa mno.

Wawili kati ya masahaba zake Husein walisimama mbele yake kuikinga mishale wakati yeye alipokuwa akitekeleza swala zake. Mmoja wao, Sa’id bin Abdillah al-Hanafi alianguka na kufa mara tu swala ilipofikia tamati.

Husein alikuwa mkarimu sana, na Mtume alipoitambua sifa hii ndani yake alisema: “Husein ana ukarimu na ujasiri wangu.” Katika kugawanya mis- aada yake alitofautisha kati ya waombaji kwa kutumia msingi wa daraja za mafanikio yao na sifa nzuri na utambuzi wao juu ya Mungu. Bedui mmoja wakati mmoja alifika kwa Husein kuomba msaada. Alimwambia Husein kwamba Mtume aliwahi kumshauri kuomba msaada wakati wa haja, kutoka kwa mtu ambaye alikuwa aidha Mwarabu mwenye moyo mzuri, au chifu mkarimu, au mtu anayeiunga mkono na kuitetea Qur’ani au mtu aliye muungwana.

Kisha akamwambia Husein kwamba aliziona sifa hizi zote zikiwa zimewakilishwa ndani yake yeye, na akaomba msaada wake. Husein akamwelezea (bedui huyo) vigezo ambavyo kutokana navyo hivyo aliweza kuamulia madai ya wale ambao walimjia kumtaka msaada. Kisha akamwambia yule bedui kwamba angemuuliza maswali matatu, na kwam- ba kwa kila jawabu sahihi, zawadi yake ingekuwa ni theluthi moja (1/3) ya pesa alizokuwa nazo wakati huo ndani ya mkoba wake. Mazungumzo hayo ni yenye kuvutia vya kutosha kunukuliwa:

Imam: “Ni jambo gani bora mno la kufanya?”
Bedui: “Ni kumwamini Mwenyezi Mungu.”
Imam:“Ni njia gani nzuri kabisa ya kuweza kumwokoa mtu kwenye maangamizi?”
Bedui: Ni kumtegemea Mwenyezi Mungu.”
Imam: “Ni nini pambo la mwanaadamu?”
Bedui: “Ni elimu iliyounganishwa na akili.”
Imam: “Kama hii haipatikani, ni jambo gani tena?”
Bedui: “Ni utajiri (mali) ulioambatana na ukarimu.”
Imam: “Itakuwaje basi kama hii haikupatikana?”
Bedui: “Ni umasikini ulioungana na subira (uvumilivu).”
Imam: “Je itakuwaje kama hili litakuwa pia haliwezi kutekelezeka?”
Bedui: “Basi wacha radi imtafune mtu huyo mpaka kuwa majivu.”

Husein kwa tabasamu pana kabisa aliukabidhi mkoba wake kwa Bedui huyo.2

Mkusanyiko (kitabu) wa baadhi ya du’a na maombi ya Husein kwa Mwenyezi Mungu, usiopitwa kwa maelezo ya uhusiano kati Mungu na viumbe Vyake, ufahamikao kama al-Sahifa al-Husayniyya upo mpaka leo hii. Idadi kubwa ya maelezo yake kuhusu sheria za Kiisilam, maarifa ya sheria na elimu ya dini vinapatikana katika mikusanyiko mbalimbali ya Hadith. Mbali na hizi, kiasi kidogo cha khutba zake na mashairi, akiwaagiza watu katika kupata elimu ya Mwenyezi Mungu na kuwasihi kufuata njia za uadilifu zote pia zinapatikana.

Ilikuwa ni kwa sababu ya nafasi inayowashinda wote ya Husein kuhusu elimu juu ya Mwenyezi Mungu, na uchamungu na ujuzi kwamba miongo- ni mwa masahaba zake pale Karbala, palikuwa na watu wenye uadilifu utambulikanao, na wenye mafanikio mazuri sana. Kwa kweli lilikuwa ni ua la jamii ya Kiislamu kama lilivyokuwa wakati huo na hazina ya elimu na matendo ambalo lilijitoa mhanga lenyewe pamoja na Husein. Masahaba zake walikuwa ni pamoja na watu ambao waliihifadhi Qur’ani kwa moyo, walikuwa na elimu yake ya kina na walikuwa ni wabebaji wa mwenendo wa Uislam. Watu kama hawa wangeweza kuvutwa tu na Husein ambaye ubora wake usio na upeo kwao, bila shaka kwa vyovyote vile ungeweza kukaribishwa.
Hata wale ambao walikuwa wameurithi uadui dhidi ya Husein walijua na kuikiri heshima yake kubwa na daraja lake la juu. Abdallah bin Amr al-Aas alikuwa maarufu miongoni mwa Bani Umayyah kwa kujizuia (kujinyima), uchamungu usalihina (udhari wa moyo) na kukubali kushikilia kazi za maadili mema. Alipigana akiwa upande mmoja na baba yake, Amr bin al-Aas dhidi ya Ali katika vita vya Siffin na Husein aliacha kuongea naye.

Siku moja, wakati Husein alipopita karibu na kundi la watu ambalo ndani yake Abdallah bin Amr bin al-Aas alikuwemo, yeye Abdullah aliwaambia wenzake aliokuwa nao kwamba miongoni mwa wakazi wa ardhini, aliye kipenzi kikubwa kwa wakaazi wa mbingu alikuwa Husein. Aliongeza kwa kusema kwamba kama kwa njia yoyote ile angeweza kupatanishwa na Husein, ingekuwa ni jambo lenye thamani zaidi kwake kuliko kuwa na Ngamia wekundu.3

Hata wakati wa utoto wake, Husein alikuwa na ujasiri wa kuongea ukweli. Alikatalia Khalifa wa pili, Umar, alipoivamia mimbari ya Mtume, na (Husein) akatoa amri kwa sauti akisema; “Shuka chini kutoka kwenye kiti cha baba yangu.” Khalifa alikubali, akasema, “Ni mimbari ya baba yako, kwa hakika, na siyo baba yangu mimi.”

Uthibitisho wa ukweli wa Husein mbele ya hatari kubwa sana unatolewa na ukweli kwamba hakufanya jaribio lolote kabisa la kufichua katika hatua yoyote ile ya safari yake kutoka Makka kwenda Karbala hatari zozote zile zilizokuwa zinawangoja mbele au vinavyovunja moyo na maafa (balaa) ambayo yalimpata.

Lakini kinyume chake, alirudia mara kwa mara kuwaonya masahaba zake kuhusu hatari zinazokaribia kuwazunguuka, na akawafahamisha ukweli. Kwa hiyo idadi ya watu wenye kumhurumia kwa sababu ya faida za kidunia, iliendelea kushuka. Aliendelea katika kutoa maonyo ya hatari mpaka kila uwezekano wa mtu yeyote aliyeshikamana naye kutokana na dhana potofu ukawa umetoweka.

Husein alipenda sana amani kiasi kwamba alijaribu kufanya amani na maadui zake mpaka dakika ya mwisho pale Karbala. Na bado alikuwa na ujasiri, uimara na subira na uvumilivu, kufidia kwa kichwa chake kwa ajili ya njia ya haki aliyoichagua kuiunga mkono.

Husein alikuwa mwamuzi (hakimu) wa watu asiyekosea. Ni kweli inayoshangaza kwamba hakuwa hata mmoja wa wale watu ambao alikuwa amewachagua kufuatana naye katika safari yake ya kwenda Karbala alikwepa kujitoa mhanga kwa ajli ya Husein. Alijionyesha vile vile kuwa yeye ni msimamizi wa watu mwenye kipaji sana, na alikiongoza kikundi chake kidogo cha masahaba vizuri sana kwamba, wakisaidiwa na nguvu za ajabu za moyo wa kujitoa mhanga na ujasiri, kikundi hicho kililiweka jeshi kubwa sana lililowazidi idadi la Yazid mapambano kwa sehemu kubwa zaidi ya siku hiyo ya mwezi 10 ya Muharam.

Maneno ya watu wengi walioko katika nafasi za juu mara nyingi ni yenye kuhitalifiana kwa dhahiri kabisa na vitendo vyao. Maneno yao kwa hiyo yanaelekea kuhifadhiwa vizuri kuliko kumbukumbu za matendo yao. Hivyo sivyo ilivyo kwa Husein. Tabia yake na kazi zake na mafanikio yake yalikuwa yenyewe katika mpangilio wa hali ya juu kwa kiasi kwamba ni zaidi ya kutosheleza kuikamata nathari ya waandishi na wasemaji wa ulimwengu.

Kwa hiyo, kulikuwa hakuna jitihada kubwa iliyotumika kati- ka kukusanya maneno yake ya kweli na hekima ambayo yanakutwa ndani ya vitabu mbalimbali, yote yakiwa katika nathari (insha) na beti. Baadhi yao yanafuata hapa chini:

1. Yule ambaye ni mkarimu, huwa kiongozi, yule aliye bakhili hupata fedheha.

2. Ni mkarimu mno miongoni mwa watu, yule ambaye hutoa misaada hata kwa wale ambao hawaitarajii.

3. Kuzipokea neema kutoka kwa Mungu huingiza wajibu wa kufanya fad- hila kwa wengine.

4. Kwamba watu wakujia wakati wakiwa katika haja, hilo lenyewe peke yake ni moja ya neema za Mungu.

5. Mfanye Muumba badala ya viumbe vyake kuwa kitovu (mahali pa) cha matumanini yako, na wewe utakuwa huru kutokana na mtu mwongo na yule mkweli halikadhalika.

Omba kwa ajili ya riziki yako ya kila siku ya Mungu Mwenye neema nyingi, kwani hakuna mwingine tena agawaye riziki za kila siku.

Yule ambaye hudhania kwamba watu wangeweza kumgawia mahitaji yake amepungukiwa na imani juu ya Mwenyezi Mungu.

Yule ambaye hufikiria kwamba watu wangemtoshelezea anaelekea kwenye fedheha kubwa.

6. Yeyote yule aongezaye utajiri wake hujiongezea wasiwasi wake.

7. Kujiambatisha kwa Mungu huwatenganisha watu kutokana na mwingine yeyote yule.

8. Ibn Kathir anasimulia kutoka kwa Is’hak bin Ibrahim kwamba wakati mmoja, katika kuyazuru makaburi ya mashahidi yalioko eneo la al-Baqi, Husein alisoma mashairi yakiwa na maana ya:

“Niliwaita wakazi wa makaburini na wakanyamaza kimya, lakini vumbi la makaburi yao likatoa majibu kuhusu ukimya wao.”
Likasema, “Je, unajua nimefanya nini kwa wale ambao wanakaa ndani yangu. Nimezipunguza nyama zao hadi kuwa vipande vidogo vidogo na ninezichana ngozi zao vipande vipande;
“Nimejaza macho yao kwa udongo ingawa huko nyuma kipande kidogo cha bua kiingiacho machoni mwao kiliwanyima raha ya kupumzika;
“Ama kuhusu mifupa yao, nimeipunguza na kuwa vipande vidogo vidogo kiasi kwamba maungio yao ni makano yanaonekana kwa wazi wazi kabisa;
“Nimevitenganisha viungo hivyo kimoja kutokana na kingine, ili kwamba vionyeshe alama zisizo na mashaka za kuoza na kuharibika.”

9. Ibn Sabba al-Maliki ameyahusisha kwa Husein baadhi ya mashairi kati- ka kitabu kiitwacho al-Fusul al-Muhimma, ambayo yametafsiriwa hapa chini;

“Wakati meno ya zama yanapokujeruhi, kamwe usijinyenyekeze kwa watu.
Na isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu ambaye hutoa namna ya kijikimu, kamwe usije kuomba riziki yako ya kila siku kutoka kwa yeyote yule.
Kwani hata kama utaizunguuka dunia kutoka Magharibi hadi Mashariki,
Hungekutana na mtu yeyote ambaye angeharibu au kutengeneza kile ambacho umepangiwa.”

10. Hata kama ulimwengu ungekuwa ni mahali pa kupendeza na kuvutia, thawabu na malipo ya Mwenyezi Mungu yana daraja la juu zaidi.

Na kwa vile miili imezaliwa ili ife, ni vizuri zaidi kwa mwanadamu kuuawa kwa upanga katika njia ya Mwewnyezi Mungu.

Na kwa vile ni dhahiri kwamba fungu la kila mtu katika riziki ya kila siku limekwishapangwa mtu anapaswa ajizuie na ulafi juu yake.

Na wakati inapokuwa ni hakika kwamba mali (utajiri) imehodhiwa ili ije kuachwa nyuma, je isingekuwa sio jambo la busara kuwa kama mtu bakhili?

11. Wakati mmoja mtu fulani alimwomba Husein kumpatia kipande cha ushauri kwa maneno mafupi tu. Katika kumjibu, Husein alisema:

“Yeyote yule apendaye kulipata lengo lake kwa njia ya kumwasi Mwenyezi Mungu, atafedheheshwa katika matumaini yake na atajikuta mwenyewe karibu zaidi na hatari kubwa.”

Tafsiri ya baadhi ya tungo zake za kiuchamungu ambazo alikuwa akizitumia kwa kuzikariri katika Swala zake za kila siku na dua, ni kama zinavyoandikwa hapa chini:

1.) Ee Mwenyezi Mungu! Wewe ndiye Mwanzilishi wa ukarimu na upaji, na chochote kilichopo cha uwezo na nguvu ni Chako na nguvu Zako zimeenea kila mahali. Hali ikiwa ndivyo hivi ilivyo, natafuta hifadhi kwako Wewe, na ninategemea kwenye uwezo Wako na nguvu kwa msaada. Ninatii na kujiweka chini ya kile ambacho umekiamuru kwangu mimi tangu mwanzo. Nitatembea juu ya njia ambayo Wewe umeniweka na ninadhamiria tu kwenye kile ambacho kinakubaliana na radhi Yako. Siachi kujibidisha hata kidogo wala sikubali uzembe wowote ule katika jitihada zangu za kutii amri Zako. Kinyume chake natembea kwa wepesi na hima juu ya njia ambayo Wewe umenichagulia. Napenda kutekeleza kikamilifu majukumu ambayo Wewe umeyakabidhi kwangu.

Unaweza sasa, Wewe Mwenyewe kunisaidia kwa msaada Wako, na usininyime neema Zako au uwezo Wako, wala usinitenganishe kutoka kwenye lengo ambalo kwa kupitia hilo napenda kutimiza radhi Zako. Ifanye tabia yangu itengemezwe juu ya busara na kanuni ya mwenendo Wangu (itegemezwe) juu ya mwongozo wa kweli na sahihi. Ifanye njia yangu ielekezwe kwenye makusudio sahihi ili kuweza kuniongoza kwenye ukamilishaji wa matakwa yangu, na kunifikisha mwisho wa safari ambao Wewe umeikusudia kwa ajili yangu mimi na ambao kwawo Wewe umeniumba, na ambao kwa huo Umeelekeza nia yangu.

Maneno ya du’a hii yanaashiria kwamba Husein alikuwa ameyatoa maisha yake kwa lengo fulani maalum na kwamba muda wote wa maisha yake ul tumika katika kuyatii maelekezo ya Mwenyezi Mungu. Katika mwaka wa 61 A.H maneno (semi hizi) haya yalipata sura ya kujitoa kwake mhanga kusikolinganishika huko Karbala.4

2.) Ee Mwenyezi Mungu! Kama mtu yeyote atachukua hifadhi kwa mtu mwingine zaidi mbali na kwako Wewe, basi mwache afanye hivyo. Wewe ndiyo kimbilio langu, na kimbilio langu pekee. Kama mtu ataelekea kwa mwingine yeyote mbali na Wewe kwa kutaka msaada, yuko huru kufanya hivyo, bali Wewe ndiyo msaada wangu, na msaada wangu pekee. Ufanye ukubwa Wako, ambao hauwezi kuathiriwa na tamaa potovu yoyote ile au madhara, na ambao ndani yake chuki ya kawaida haiwezi kuwa na sauti, nilinde katika mtihani wangu kutokana na kuhusishwa katika fitina yoyote ile, au kufadhaishwa na kundi lolote lile la kishetani mpaka nitakaporejea Kwako, nikiwa mtiifu kwenye utashi Wako, moyo wangu ukiwa huru kutokana na mawazo mabaya, watu wengine wakiwa hawanifikirii mawazo mabaya, wala mimi kuwatilia watu wengine mashaka, wala wengine wakiwa katika hali ya kutokuwa na yakini kuhusu mimi.5

3.) Husein alikuwa akitumia kurudia rudia kuisoma dua ifuatayo wakati wa asubuhi na jioni:
“Ewe Mwenyezi Mungu! Mimi nimenyenyekea Kwako, na nimegeukia Kwako, na nimeweka mikono yangu mkononi Mwako. Ee Mwenyezi Mungu! Wewe pekee unaweza kunilinda kutokana na fitina za kila mtu mwingine, lakini hakuna mwingine yeyote isipokuwa Wewe awezaye kuniokoa na ghadhabu Yako.”

Je, ilikuwa inawezekana kwa mtu wa namna hii, kama inavyodhihirishwa na semi na du’a za Husein kukubali kunywea kwenye nguvu za ukaidi kwa Mungu, kutoa kiapo cha utii kwa mtu muovu kama Yazid? Jibu ni lazima liwe ni hapana yenye nguvu.

Hata wakati akiwa peke yake, na akiwa amezunguukwa na jeshi kubwa pale Karbala, Husein alisimama imara katika imani yake na itikadi zake. Kweli, Husein na sahaba zake walichinjwa. Lakini wakati matokeo ya vita vya Karbala yalipoanza kujitokeza ilionekana kwamba katika hali halisi alikuwa ni Husein ambaye aliibuka kuwa mshindi.

Falsafa ya maisha ya Husein kama ilivyofundishwa na baba yake, Ali ilikuwa ‘Shikamana na haki, hata kama ikiwa chungu.”

  • 1. Tabari, juz. 6, uk. 266.
  • 2. Al-Tafsir al-Kabir, uk. 272 cha Al-Razi. (Tabari, juz. 6, uk. 266 tanbihi ya kwanza)
  • 3. Usudul-Ghaba, juz. III, uk. 235 cha Ibn al-Athir.
  • 4. Majmu Du’at, uk. 71-72.
  • 5. Ibid, uk. 73.