Sura Ya 14: Msisitizo Wa Yazid Juu Ya Kiapo Cha Utii Cha Husein Na Kukataa Kwa Husein.

Kwa kuwa mfalme, Yazid alijikuta katika kumiliki utajiri mwingi usioelezeka madaraka yasiyo na mipaka. Kitu kimoja ambacho baba yake alimwonya nacho akiwa kwenye kitanda chake alichofia, hata hivyo kilimweka na wasiwasi uliomhuzunisha sana. Lilikuwa kwamba watu wachache maarufu miongoni mwa Maquraishi wamekaidi kutoa viapo vyao vya utii kwake. Muhimu miongoni mwa waliopinga ambao idadi yao iliwajumlisha Abdalla bin Zubairi, Abdillahi bin Umar na Husein bin Ali.

Yazid hakupoteza muda katika kumwandikia barua binamu yake, al-Walid bin Utbah bin Abi Sufyani, gavana wa Madina, kuhusu kifo cha Mu’awiyah na kumwelekeza kuwalazimisha Husein bin Ali na Abdullah bin al-Zubeir kutoa kiapo cha utii kwake, na asiwaachie kabla hawajafanya hivyo.

Mbali ya kuwa na uhusiano wa karibu sana na Yazid, al-Walid alikuwa na hisia za heshima kubwa kwa Husein kutokana na kunyanyuka kwa daraja lake tukufu. Maelekezo yaliyopokelewa toka kwa Yazid, kwa hiyo yalimtingisha na kumtia wasiwasi sana. Ingawaje hakuwa katika hali ya mahusianao mazuri sana na Marwan kwa wakati fulani, alimtaka ushauri Marwan kuhusiana na jambo hili ili kujizoesha na mwelekeo wa sasa wa fikra za Bani Umayyah. Inaweza pia kutajwa kwamba Marwan aliishi kwa kufanya hizaya na dharau wakati wa uhai wa Mtume kwa kiasi kwamba alifukuzwa pamoja na baba yake kutoka Madina na Mtume mwenyewe.

Marwan alimwambia al-Walid ondoa wasiwasi wote kuhusu Abdallah bin Umar kwani yeye hataudai Ukhalifa. Alisisitiza sana kwamba kiapo cha utii kwa Yazid kichukuliwe kutoka kwa Husein bin Ali na Abdullah bin Zubeir, na kwamba endapo wataweka vipingamizi, basi wauawe kabla taarifa za kifo cha Mu’awiyah hazijatangazwa, kwani kama itakuwa hivyo, yeye alidhani, wote wawili wangejitahidi kukusanya waunga mkono kuhusu madai yao, na kwa wazi wangemkataa Yazid.1

Al-Walid aliwaita Husein na Abdillaha bin Zubeir ambao wote wawili walikuwa katika msikiti wa Mtume. Ilikuwa ni saa zisizokuwa za kawaida kwa Al-Walid kuwaita watu katika wakati kama huo na wangeweza kudhania kwamba Mu’awiyah amekufa na kwamba walikuwa wameitwa kutoa kiapo cha utii kwa Yazid. Husein aliwakusanya ndugu na marafiki zake na kwenda nao kwenye jumba la gavana. Aliwaambia wamngojee mlangoni kwa al-Walid wakati yeye alipokwenda ndani kumwona gavana, lakini waingie ndani ya nyumba hiyo endapo angewaita au al-Walid atakapopandisha juu sauti yake.

Al-Walid alizitangaza habari za kifo cha Mu’awiyah na baada ya taratibu za kawaida za rambirambi zilipokwishafanyika, alimtaka Husein kutoa kiapo cha utii kwa Yazid. Husein alijibu kwamba labda ingefikiriwa haitoshi kwamba mtu kama yeye angetoa kiapo cha utii kwa siri badala ya kufanya hivyo mbele ya halaiki ya watu.

Al-Walid alikubali kuchukua kiapo cha utii cha Husein wakati atapokuja kutangaza hadharani kuhusu kifo cha Mu’awiyah, na akawataka wengine wote kutoa kiapo cha utii kwa Yazid, kwani huo ndio ungekuwa wakati mwafaka kwa suala hili kuweza kupatiwa ufumbuzi wa mwisho kabisa.

Marwan, ambaye alikuwa anaangalia maendeleo ya shughuli zote hizi hakuupendelea mwelekeo wa hisani wa al-Walid juu ya Husein, akiipandisha juu sauti yake alisema, “Kama Husein ataondoka sasa, bila kutoa kiapo, kamwe hutaweza tena kupata nafasi kama hii, labda iwe hivyo baada ya kumwagika damu nyingi. Ni bora zaidi kumkamata hapa na sasa hivi, na kumzuia kurudi nyumbani kwake mpaka labda atoe kiapo cha utii au vinginevyo kumuua.”

Hili lilimkasirisha sana Husein ambaye alisimama na kusema; “Marwan, vipi unaweza kuthubutu kuniua? Wallahi umetamka kimakosa na umetenda dhambi.” Husein kisha akaondoka kwenda nyumbani kwake (Tabarim uk.218)

Kwa nini Yazid awe alisisitiza sana kwa jitihada zisizokuwa na mwisho juu ya kupata kiapo cha utii cha Husein juu yake yeye? Inapaswa iwe dhahiri kwamba hata liwe kundi la watu kubwa namna gani ambalo Mu’awiyah angeweza kulikusanya Makka na Madina ili waape kumuunga mkono Yazid, lazima kutakuwepo mamia ya watu katika sehemu zote mbili ambao wanaweza kuwa walibakia majumbani mwao na hawakutoa kiapo.

Tena, hakuna mtu mwingine zaidi ya Husein, ambaye alitokana na familia ya Mtume, au aliyetokana na kizazi cha Ali, aliyetakiwa kuchukua kiapo cha utii kwa Yazid, hata ingawaje Muhammad ibn al-Hanafiyya Abdallah bin Ja’afar na Abbas ibn Ali walikuwepo hapo.

Katika demokrasia kukubalika na watu wengi juu ya uhalali wa serikali kunatosha, na maoni ya wachache wasiokubaliana hutupiliwa mbali kabisa. Kundi hilo dogo halilazimishwi kuacha maoni yao, wala yeyote kati ya watu wake kutishiwa kwa kufanyiwa vurugu, au kuteswa kwa hilo.

Katika vipindi vyote vya ukhalifa vilivyopita kulikuwepo na watu ambao hawakutoa viapo vya utii kwa khalifa. Wakati wa Ukhalifa wa Ali mwenyewe, Hassan bin Thabit, Ka’b bin Malik na Zayd bin Thabit, miongoni mwa wengine wengi, hawakutoa kiapo cha utii kwake, bila ya kufikwa na matokeo yoyote yale mabaya, yasiyopendeza. Kwa nini, basi utaratibu mzima wa serikali ya Syria utake kwa nguvu kiapo cha utii kutoka kwa Husein pekee?

Ilikuwa hivyo kwa sababu Yazid alitaka akubalike kama Khalifa wa Uislam, licha ya ukiukaji mwingi wa amri za sheria za Qur’an na Sunna za Mtume, siyo na watu wa kawaida, bali akubaliwe na Husein ambaye juu yake yeye, akiwa kama mkubwa kabisa wa familia ya Mtume, na mrithi wake wa haki kabisa, alikuwa ndiyo mwenye wajibu pekee wa kuusaidia Uislamu na kuitetea haki.

Yazid angeweza kufanya hivyo bila ya kiapo cha Husein kama masingizio yake yangevutika kwenye madaraka ya kidunia tu, bali kwa vile alipenda kuidhibiti dini pia, na kuifanya iwe ya kutumikia utashi wake na matakwa yake, ilibidi apate kiapo cha utii cha Husein. Hata hivyo Husein aliuzuia mkono wake (kwa kutokutoa kiapo cha utii) na akakitoa kichwa chake katika muhanga kwa ajili ya Uislamu.

  • 1. Tabari, uk. 217.