read

Aya 54-57: Yusuf Ni Muheshimiwa Misr

Akasema mfalme: “Mleteni awe wangu mwenyewe.Basi alipozungumza naye alisema: “Hakika wewe leo kwetu ni mwenye heshima, mwenye kuaminika.”

Baada ya mke wa waziri na wale wanawake wengine kukiri na watu wote kujua kuwa Yusuf hana hatia, Yusuf alikubali kutoka gerezani na mfalme alipokutana naye na kumsikiza, alimpenda na akamtaka awe kiongozi katika serikali yake aweze kumsaidia kuendesha serikali, akamwambia: “Wewe ni mwenye heshima na mtu mwenye kuaminiwa kwenye kila kitu katika serikali.“

Mfalme hakuyasema haya ila baada ya kuwa na uhakika wa uwezo wake, ujuzi wake na hekima yake. Inasemekana umri wa Yusuf wakati huo ulikuwa ni miaka 30. Katika Majmaul bayan imeelezwa kuwa Yusuf alimsalimia mfalme kwa lugha ya kiarabu.

Mfalme alipomuuliza umeipata wapi lugha hii, alisema ni lugha ya ami yangu Ismail. Katika tafsir Al-manar imeelezwa kwamba mfalme aliyekuweko wakati wa Yusuf alikuwa ni katika wafalme wa kiarabu walio maarufu kwa jina la Hyksos.

Tabari anasema alikuwa akiitwa Walid bin Rayyan.

Akasema(Yusuf): “Nifanye mweka hazina wa nchi, hakika mimi ni mlinzi, mjuzi.”

Baada ya mfalme kumwachia Yusuf afanye atakavyo na achague cheo, basi alichagua cheo cha wizara ya hazina na uchumi.
Alichagua cheo baada ya kuhiyarishwa na wala hakuanza yeye, isije ikaonekana kuwa anataka cheo. Hata kama tukisema ameanza yeye, basi itakuwa sio kwa maslahi yake bali ni kwa maslahi ya umma na kulinda haki za wanyonge; hasa kwenye mwaka wa kahati na njaa.

Yusuf alijua kuwa nchi inakabiliwa na janga; ikiwa mweka hazina si mjuzi na asiyekuwa mlinzi imara, basi watu hawatapata haki yao; hasa mafukara na maskini.

Zaidi ya hayo ni kuwa wizara hiyo ni nyeti sana; ikishikwa na watu wasio na ujuzi na uamnifu, umma utaangamia tu; hata ikiwa sio wakati wa shida. Lakini ikiwa mikononi mwa wajuzi na walio na uaminifu, umma utaongoka kidunia na kiakhera.

Wengi wamenukuu kuwa Yusuf aliposhikilia hazina, na watu kuona uamnifu wake na kumpa kila mtu haki yake, waliamini utume wake; hata mfalme pia alishahadia kuwa hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu na kwamba Yusuf ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu.

Ismail Haqqiy, anasema katik Rawhul bayan:

“Amesema Mujahid: Mfalme alisilimu kupitia kwa Yusuf, pamoja na watu wengi.” Mwenye Tafsir al-bayan, aliongezea juu ya kauli hii ya Mujahid kwa kusema: Ikiwa hisani na ukarimu wa Yusuf ni sababu ya imani, basi unaonaje yule aliyemsaidia mtume (s.a.w.) na akamkinga na kumhami muda wa uhai wake. ambaye ni ami yake, Abu Twalib? Kwa hiyo ukweli hasa, yeye ni katika wale ambao Mwenyezi Mungu amewahuyisha kwa imani, kama ilivyotangulia kuelezwa.”

Yametangulia maelezo ya kusilimu Abu Twalib katika Juz. 11 (9:113).

Hakika mimi ni mlinzi, mjuzi.

Nitailinda mali isipotee bure na kufanyiwa israf, na ninajua wale wanaostahiki kupewa na kila kitu nitakiweka mahali pake panapostahiki.

ImepokewakutokakwaImamJafarAs-Sadiq,amesema:“Inajuzukwamtu kujisifu ikibidi kufanya hivyo, kwani Yusuf alisema: “Nifanye mweka haz- ina wa nchi; hakika mimi ni mlinzi, mjuzi.”

Katika baadhi ya Tafsiri imeelezwa kuwa Yusuf hakuwahi kumnyenyekea Mfalme kwa kumwambia: uishi ewe mfalme! Mimi ni mtumwa wako mnyenyekevu; kama wafanyavyo leo wale wanaojipendekeza kwa wakubwa; isipokuwa alitaka yale ambayo anaamini kuwa anayamudu; kama maandalizi ya kukabiliana na majanga na kulinda nchi kutokana na uharibifu. Laiti wale wanaojipendekeza kwa wakubwa wangelisoma Qur’an wakajua kuwa heshima haiji kwa kujipendekeza

Razi anasema: Yamepokewa masimulizi kuwa Mfalme alimwambia Yusuf: “Napenda kukushirikisha kwenye kila kitu isipokuwa katika watu wangu wa nyumbani na kula na mimi.” Yusuf akamwambia: “Siwezi kula pamoja nawe na mimi ni Yusuf bin Ya’qub bin Is-haq bin Ibrahim kipenzi cha Mungu!”

Na hivyo ndivyo tulivyompa cheo Yusuf katika nchi akae humo popote apendapo. Tunamfikishia rehema zetu tumtakaye, wala hatupotezi ujira wa wafanyao mema.

Yusuf alivumilia kutupwa kisimani, kuuzwa utumwani, kutumikia nyumba ya waziri, kutuhumiwa na kufungwa gerezani. Aliyavumilia yote hayo na mengine kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu na kutosheka naye. Je, natija yake ilikuwa ni nini? Alitoka gerezani kishujaa akiwa ni mshindi wa vita vya uvumilivu; ni mtu huru na akawa mmoja wa viongozi wa nchi. Hivi ndivyo wanavyolipwa wavumilivu ujira wao katika dunia.

Na ujira wa akhera ni bora kwa wale walioamini na wakawa ni wenye kumcha (Mungu).

Malipo ya akhera ni Pepo ambayo “Haikatiki neema yake, haondoki mkazi wake, hazeeki anayedumu, wala kukata tamaaa anayekaa humo” kama alivyosema Imam Ali.
Sasa iko wapi neema hii na ile ambayo mfalme anazeeka kwa taabu na maumivu. Baadhi ya mapokezi yanasema kuwa mke wa mheshimiwa alimjia Yusuf siku za kahati akitafuta chakula, mumewe akiwa amekufa na yeye dunia imemwinamia, yakawa yamempata yaliyompata.

Yusuf alipomuona alimwambia imekuwaje kuwa katika hali hii, naye akasema:

Ametakataka na maovu ambaye anawafanya wafalme kuwa watumwa kwa kwa sababu ya kumwasi na anayewafanya watumwa kuwa wafalme kwa sababu ya kumtii.

وَجَاءَ إِخْوَةُ يُوسُفَ فَدَخَلُوا عَلَيْهِ فَعَرَفَهُمْ وَهُمْ لَهُ مُنْكِرُونَ {58}

Wakaja ndugu zake Yusuf wakaingia kwake. Yeye akawajua na wao hawakumjua.

وَلَمَّا جَهَّزَهُمْ بِجَهَازِهِمْ قَالَ ائْتُونِي بِأَخٍ لَكُمْ مِنْ أَبِيكُمْ ۚ أَلَا تَرَوْنَ أَنِّي أُوفِي الْكَيْلَ وَأَنَا خَيْرُ الْمُنْزِلِينَ {59}

Alipowatengenezea mahitaji yao aliwaambia: “Nileteeni ndugu yenu kwa baba. Je hamuoni kuwa mimi ninatimiza kipimo na kwamba mimi ni mbora wa wakaribishao?

فَإِنْ لَمْ تَأْتُونِي بِهِ فَلَا كَيْلَ لَكُمْ عِنْدِي وَلَا تَقْرَبُونِ {60}

Msiponiletea basi hampati kipimo chochote kwangu wala msinikurubie.”

قَالُوا سَنُرَاوِدُ عَنْهُ أَبَاهُ وَإِنَّا لَفَاعِلُونَ {61}

Wakasema: Tutamrairai baba yake, na hakika sisi tutafanya.”

وَقَالَ لِفِتْيَانِهِ اجْعَلُوا بِضَاعَتَهُمْ فِي رِحَالِهِمْ لَعَلَّهُمْ يَعْرِفُونَهَا إِذَا انْقَلَبُوا إِلَىٰ أَهْلِهِمْ لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ {62}

Akawaambia watumishi wake: Tieni bidhaa zao katika mizigo yao ili wazione watakaporudi kwa watu wao ili wapate kurejea.”