read

Aya 63-66: Mtume Ndugu Yetu Pamoja Nasi

Maana

Basi waliporudi kwa baba yao, walisema: “Ewe baba yetu! Tumenyimwa chakula.”

Wakiashiria kauli ya Yusuf ‘Msiponiletea basi hampati kipimo chochote kwangu. Kisha wakamwambia baba yao:

Basi mtume ndugu yetu pamoja nasi ili tupate kupimiwa na kwa hakika sisi tutamlinda.

Walitoa ahadi ya kumlinda na kumhifadhi ili baba yao asiwanyime.

Je nikuaminini kwa huyu kama nilivyokuaminini kwa nduguye zamani? Mlivyomfanyia?

Kisha akaelekea kwa Mwenyezi Mungu na akasema:

Basi Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa kulinda na ndiye anayerehemu zaidi kuliko wanaorehemu.

Mimi namtegemea Mwenyezi Mungu katika uhifadhi na ulinzi wa mwanagu sio hifadhi yenu. Na yeye Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kuhurumia unyonge wangu na uzee wangu. Inasemekana kuwa jina la huyo mtoto wake mdogo lilikuwa ni Bin-yamin (Benjamin).

Wailpofungua mizigo yao wakakuta bidhaa zao wamerudishiwa.

Wakamkimbilia baba yao wakiwa na furaha na wakasema:

Ewe baba yetu! Tutake nini zaidi?

Yaani tutatoa sababu gani kwake kama hatukwenda na ndugu yetu na ametukirimu namna hii kama uonavyo ameturudishia mali yetu.

Hizi bidhaa zetu tumerudishiwa.

Inasemekana mali yenyewe ilikuwa ni viatu na ngozi.

Baadhi ya wafasiri wa kisasa wanasema kuwa walikuta mali yao tu, sio chakula na kwamba Yusuf alifanya hivyo ili walazimike kurudi na ndugu yao. Lakini hayo ni makosa kwa sababu yanapingana na dhahiri ya Qur’an amabayo ni: “Je hamuoni kuwa mimi ninatimiza kipimo na kwamba mimi ni mbora wa wakaribishao?”

Zaidi ya hayo kuwanyima ndugu chakula wakati wanakihitajia ni roho mbaya na ngumu sana, jambo ambalo liko mbali sana na Yusuf. Ama kauli yao “Tumenyimwa chakula” ni kunyimwa mara ya pili watakaporudi.

Na tutaleta chakula kwa ajili ya watu wetu na tutamlinda ndugu yetu na kila jambo baya.

Na tutapata ziada ya kipimo cha ngamia mmoja.

Kwa sabbu Yusuf alikuwa akimpa kila mtu kipimo cha ngamia mmoja tu, ili watu wote wapate chakula. Kwa hiyo wakienda na ndugu yao watazidisha mzigo wao.

Hicho ni kipimo kidogo.

Yaani ziada itapatikana kwa kuweko ndugu yetu; vinginevyo, hatupati. Yaqub akaona haja ya chakula imezidi na kile walichokuja nacho

kinakaribia kwisha. Hivyo akakubali kwa sababu ya haja si kwa sababu ya shinikizo la wanawe, kuongezea kumwamini waziri kutokana na sifa nzuri alizozisikia na jinsi alivyowafanyia wanawe.

Akasema: “Sitampeleka nanyi mpaka mnipe ahadi kwa Mwenyezi Mungu kwamba mtamleta kwangu ila ikiwa mmezungukwa.”
Aliwaruhusu kuondoka na Bin-yamin kwa sharti la kutoa ahadi madhubuti kuwa watamrudisha salama isipokuwa wakitokewa na sababu zisizoweza kuzuilika.

Basi walipompa ahadi yao alisema: “Mwenyezi Mungu ndiye mtegemewa kwa tuyasemayo.”

Yaani walipompa ahadi aliyoitaka, kwamba watamfidia kwa roho zao, alisema Mungu peke yake ndiye shahidi wa haya tuyasemayo. Mkitekeleza, Mungu atawalipa mema na mkihalifu atawalipa adhabu kubwa.

وَقَالَ يَا بَنِيَّ لَا تَدْخُلُوا مِنْ بَابٍ وَاحِدٍ وَادْخُلُوا مِنْ أَبْوَابٍ مُتَفَرِّقَةٍ ۖ وَمَا أُغْنِي عَنْكُمْ مِنَ اللَّهِ مِنْ شَيْءٍ ۖ إِنِ الْحُكْمُ إِلَّا لِلَّهِ ۖ عَلَيْهِ تَوَكَّلْتُ ۖ وَعَلَيْهِ فَلْيَتَوَكَّلِ الْمُتَوَكِّلُونَ {67}

Akasema: “Enyi wanangu! Msiingie mlango mmoja, bali ingieni kwa milango mbalimbali. Wala mimi siwafai na chochote mbele ya Mwenyezi Mungu; hukumu haiko ila kwa Mwnyezi Mungu tu, juu yake yeye ninategemea na juu yake yeye wategemee wanaotegemea.”

وَلَمَّا دَخَلُوا مِنْ حَيْثُ أَمَرَهُمْ أَبُوهُمْ مَا كَانَ يُغْنِي عَنْهُمْ مِنَ اللَّهِ مِنْ شَيْءٍ إِلَّا حَاجَةً فِي نَفْسِ يَعْقُوبَ قَضَاهَا ۚ وَإِنَّهُ لَذُو عِلْمٍ لِمَا عَلَّمْنَاهُ وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ {68}

Walipoingia kama alivyowaamrisha baba yao, haikuwafaa kitu kwa Mwenyezi Mungu; isipokuwa ni haja tu iliyo katika nafsi ya Ya’qub aliitimiza. Na hakika yeye ana elimu kwa tulivyomfundisha, lakini watu wengi hawajui.