Aya 67-68: Msiingie Mlango Mmoja
Maana
Akasema: “Enyi wanangu! Msiingie mlango mmoja, bali ingieni kwa milango mbalimbali.
Baada ya kusisitiza ahadi yao kwa baba yao, aliwaruhusu kuondoka na ndugu yao mdogo na akawapa wasia huu. Inaonekana kuwa huo mji ulikuwa na milango mingi ya kuingilia. Baadhi ya tafsiri zinasema ilikuwa milango mine.
Wametofautiana wafasiri kuhusu lengo la Ya’qub kwenye wasia huu. Hakuna maelezo ya kutegemewa. Pengine inawezekana kuwa kama wataingia pamoja nao ni genge la watu 11, watu wanaweza kuanza kujiuliza uliza.
Au pengine ni kwa lengo la kuujua mji na kuchunguza habari za Yusuf. Kwa vyovyote iwavyo, sisi hatukalifiwi kutafiti lengo la wasia huo, maadamu Aya haikulidokeza.
Katika tafsir Bahrul Muhit, imeelezwa kuwa Ya’qub aliwatuma wanawe wamplekee salaam waziri kwamba baba yetu anakuombea rehema na anakushukuru ulivyotufanyia. Yusuf aliposikia ujumbe huu alilia. Hayo hayako mbali na maudhui haya.
Wala mimi siwafai na chochote mbele ya Mwenyezi Mungu. Hukumu haiko ila kwa Mwnyezi Mungu tu.
Katika kufasiri Juz.12 (12:40) kifungu ‘Hakuna hukumu sipokuwa ya Mwenyezi Mungu’ tulibainisha kwamba hukumu yake Mwenyezi Mungu inaweza kuwa ni halali na haramu, inayoitwa hukumu ya sharia.
Vile vile inaweza kuwa ni kadha yake na kadari ambayo haiepukiki. Mfumo wa Aya unafahamisha kuwa hayo ndio makusudio yake hapa. Na maana yake ni kuwa mimi ninawapa nasaha na kuwatakia mema, lakini yote hayo hayawezi kuzuia kadari na hukumu ya Mwenyezi Mungu.
Lengo lake katika hilo ni kuwabainishia wanawe kwamba mtu asitegemee vitendo peke yake wala imani peke yake; bali afanye vitendo na kujitahidi huku akimtegemea Mwenyezi Mungu na kuitakidi kuwa yeye ndiye msaidizi wake. Ndio maana akasema:
Juu yake Yeye ninategemea na juu yake Yeye wategemee wanaotegemea.
Yaani mimi ninamwamini Mwenyezi Mungu na ninamtegemea Yeye na kila anayemwamini mwenyezi Mungu anatakikana kuwa hivyo.
Walipoingia kama alivyowaamrisha baba yao, haikuwafaa kitu kwa Mwenyezi Mungu.
Yaani watoto wa Ya’qub waliingia mjini Misr kwa kupitia milango mbalimbali, kwa kufuata amri ya mzazi wao, lakini hilo halikuwafaa kitu wala kuzuia balaa, kama alivyotangulia kusema baba yao: “Wala mimi siwafai na chochote mbele ya Mwenyezi Mungu” amabapo walituhumiwa wizi na kuchukuliwa Bin-yamin wakarudi kwa baba wakiwa hoi; kama itakavyoelezwa.
Ispokuwa ni haja tu iliyo katika nafsi ya Ya’qub aliitimiza.
Wamatofautiana wafasiri kuhusu haja ya Ya’qub iliyotimizwa na Mwenyezi Mungu. Kuna aliyesema kuwa ni kuwa watoto wa Ya’qub wasipatwe na jicho watakapoingia Misr. Mwingine akasema kuwa ni waziri asiwapate na jambo baya.
Tuanavyo sisi, kulingana na hali ilivyo, na kulingana na Aya inayoonyesha kuhangaika kwa Ya’qub juu ya Yusuf na nduguye, ni kwamba haja ya kwanza na ya mwisho ya Ya’qub, katika maisha haya, ni usalama wa Yusuf na nduguye na kuwa pamoja nao ni kitulizo cha moyo wake. Na mwenyezi Mungu alimtimizia aliyoyataka kwa uzuri.
Na hakika yeye ana elimu kwa tulivyomfundisha.
Yeye ni mtume na kila mtume anafundishwa na kupata elimu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Na miongoni mwa mafunzo hayo kwa Ya’qub ni uvumilivu wake wa misukosuko na kumtegemea kwake Mwenyezi Mungu na kuacha kukata tamaa na rehema ya mwenyezi Mungu. Na miongoni mwa elimu yake ni kuwa mambo yote ya waja yako kwa Mwenyezi Mungu.
Lakini watu wengi hawajui kwamba hukumu ni ya Mwenyezi Mungu na kwamba mipango yote ya waja bila ya msaada wa Mwenyezi Mungu haina manufaa yoyote.
وَلَمَّا دَخَلُوا عَلَىٰ يُوسُفَ آوَىٰ إِلَيْهِ أَخَاهُ ۖ قَالَ إِنِّي أَنَا أَخُوكَ فَلَا تَبْتَئِسْ بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ {69}
فَلَمَّا جَهَّزَهُمْ بِجَهَازِهِمْ جَعَلَ السِّقَايَةَ فِي رَحْلِ أَخِيهِ ثُمَّ أَذَّنَ مُؤَذِّنٌ أَيَّتُهَا الْعِيرُ إِنَّكُمْ لَسَارِقُونَ {70}
قَالُوا وَأَقْبَلُوا عَلَيْهِمْ مَاذَا تَفْقِدُونَ {71}
قَالُوا نَفْقِدُ صُوَاعَ الْمَلِكِ وَلِمَنْ جَاءَ بِهِ حِمْلُ بَعِيرٍ وَأَنَا بِهِ زَعِيمٌ {72}
قَالُوا تَاللَّهِ لَقَدْ عَلِمْتُمْ مَا جِئْنَا لِنُفْسِدَ فِي الْأَرْضِ وَمَا كُنَّا سَارِقِينَ {73}
قَالُوا فَمَا جَزَاؤُهُ إِنْ كُنْتُمْ كَاذِبِينَ {74}
قَالُوا جَزَاؤُهُ مَنْ وُجِدَ فِي رَحْلِهِ فَهُوَ جَزَاؤُهُ ۚ كَذَٰلِكَ نَجْزِي الظَّالِمِينَ {75}
فَبَدَأَ بِأَوْعِيَتِهِمْ قَبْلَ وِعَاءِ أَخِيهِ ثُمَّ اسْتَخْرَجَهَا مِنْ وِعَاءِ أَخِيهِ ۚ كَذَٰلِكَ كِدْنَا لِيُوسُفَ ۖ مَا كَانَ لِيَأْخُذَ أَخَاهُ فِي دِينِ الْمَلِكِ إِلَّا أَنْ يَشَاءَ اللَّهُ ۚ نَرْفَعُ دَرَجَاتٍ مَنْ نَشَاءُ ۗ وَفَوْقَ كُلِّ ذِي عِلْمٍ عَلِيمٌ {76}