read

Aya 69-76: Mimi Ni Nduguyo, Usihuzunike

Maana

Walipoingia kwa Yusuf, alimkumbatia ndugu yake akasema: “Hakika mimi ni nduguyo. Basi usihuzunike kwa waliyokuwa wakiyafanya.”

Watu wa tafsiri akiwemo Tabari, Razi, Tabrasi na Abu Hayani al-andalusi, wametaja ufafanuzi wa Aya hii ambao hauna dalili katika Qur’an, lakini unaoana nayo na kunasibiana nayo. Kwa ajili hii tutafupiliza kauli zao, kama ifuatavyo:

Ndugu wa Yusuf walipofika Misr aliwaalika kwenye chakula na akawaweka wawili wawili, kwa lengo la kuwa yeye abakie na ndugu yake Bin-yamin akae naye kwenye meza yake ya chakula; sawa na alivyofanya Muhammad (s.a.w.) baina ya maswahaba zake wawili wawili kuwa ndugu na akambakisha Ali awe wake yeye.

Baada ya chakula, Yusuf aliwapangia vyumba vya kulala wawili wawili na ndugu yake Bin-yamini akalala naye chumba kimoja. Walipokuwa peke yao akamwambia: “Je, unapenda mimi niwe ndugu yako?” Akamjibu ni nani anaweza kuwa na ndugu mfano wako? Lakini wewe hukuzaliwa na Ya’qub wala Rahel. Basi akamkumbatia na kumwambia: “Mimi nimezaliwa na Ya’qub na Rahel. Basi mimi ni ndugu yako. Wala usuhuzunike na waliyotufanyia ndugu zetu.” Bin-Yamin akafurahi sana na akamshukuru Mwenyezi Mungu.

Alipokwisha watengenezea mahitaji yao akaweka kopo katika mzigo wa ndugu yake. Kisha mnadi akanadi: “Enyi wasafiri! Hakika nyinyi ni wezi.”

Yusuf alitaka kumtenga Bin-yamin na ndugu zake na kubaki naye, lakini hakuwa na njia ila kufanya ujanja. Katika sharia ya watu wa Ya’qub ni mwizi kufanywa mtumwa. Ndio watumishi wakaweka chombo cha kupimia kwenye mzigo wa Bin-yamin, kwa amri ya Yusuf. Akanadi mnadi kuwa nyinyi wana wa Ya’qub! Ni wezi, kwa hiyo msiendelee na msafara hadi tuangalie mambo yenu.

Wakashangaa watoto wa Ya’qub kwa mshtukizo huu.

Wakasema na hali wamewaelekea: “Mmepoteza nini?”

Walisema hivi wakiwa na yakini kuwa hawana hatia yoyote. Na hii ni mara yao ya kwanza kusikia tuhuma hii.

Wakasema watumishi wa Yusuf:

Tumepoteza kopo la mfalme na atakayelileta atapata shehena nzima ya ngamia na mimi ni mdhamini.”

Mdhamini huyu ndiye aliyewaambia nyinyi ni wezi, kama walivyosema wafasiri, na akadhamini kwa sharti ya kuwa mtu aliye na hicho chombo akirudishe yeye mwenyewe.

Aya hii inaingia kwenye milango miwili ya Fiqh: Jaala, ambayo ni kutangaza zawadi kwa atakayeleta kilichopotea na Dhamana ambayo ni kutekeleza ahadi; kama vile kauli ya alisema: ‘Na mimi ni mdhamini.’ Yaani nadhamini kutekeleza ahadi ya shehena ya ngamia. Kuna hadithi isemayo: “Mdhamini ni mwenye kugharimika.”

Wakasema watoto wa Ya’qub Wallahi mnajua vyema kwamba sisi hatukuja kufanya ufisadi katika nchi hii wala sisi sio wezi.”

Walibishana wakajadiliana na kuleta hoja za kutokuwa na hatia na usafi wao; miongoni mwa waliyoyasema ni: Vipi mnatutuhumu na mnajua nasabu yetu na sera yetu katika safari yetu ya kwanza na hii ya pili kwamba hatukuja kufanya ufisadi au hiyana; isipokuwa tumekuja kuwanunulia chakula watu wetu.

Kwenye tafsiri nyingi imeelezwa kuwa watoto wa Ya’qub, kwenye safari yao ya kwanza, walipokuta bidha zao zimerudishwa walidhani kuwa zimesahaulika, kwa hiyo hawakuzitumia, bali walizirudisha Misr. Kwa hiyo wakawa mashuhuri kwa wema na uamnifu wao.

Kauli hii ya wafasiri haiku mbali; bali inaashiria kauli ya watoto wa Ya’qub: ‘Wallah mnajua vyema kwamba sisi hatukuja kufanya uharibifu katika nchi hii’

Unaweza kuuliza: Imekuwaje kwa Yusuf kufanya njama hizi za kuwaelekezea tuhuma ndugu zake na hali anajua kuwa hawana hatia?

Jibu: Kwanza, tukio hili ni maalum, lina sababu zake, haifai kulipima na matukio mengine. Pili, aliyelengwa na tuhuma za wizi ni Bin-yamin, ndugu wa Yusuf kwa baba na mama, na hilo lilikuwa kwa makubaliano yao na kuridhika kwake, kwa hekima iliyotaka hivyo; wakati huohuo hilo halipingi msingi wowote katika misingi ya sharia; kama vile kuhalalisha haramu au kuharamisha halali.

Zaidi ya hayo, tendo la watoto wa Ya’qub la kumtoa Yusuf kwa baba yake na kumtupa kisimani kwa lengo la kumuua ni zaidi ya wizi.

Swali la pili: Vipi Yusuf kumtenganisha nduguye na baba yake na kumzidishia baba yake majonzi juu ya majonzi?

Jibu: Kila alilolifanya Yusuf lilikuwa kwa maslahi ya ndugu yake na baba yake; akiwa na uhakika kuwa baba yake atamkubalia na hata kumshukuru atakapojua uhakika wake. Na lilifanyika hilo. Kimsingi ni kuwa mambo hupimwa kwa matokeo yake sio kwa mfumo wake. Katika hali nyingine mitume hawatuhumiwi katika upande wa haki.

Wakasema: “Malipo yake yatakuwa ni nini ikiwa nyinyi ni waongo?”

Watumishi waliwaambia watoto wa Ya’qub ili waseme wenyewe kwamba mwizi atachukuliwa mateka au mtumwa, kama malipo ya tendo lake hilo. Ili iwe ni hoja juu yao pale Yusuf atakapomchukua ndugu yake.
Wakasema: “Malipo yake ni yule ambaye litaonekana katika mzigo wake, basi huyo ndiye malipo yake. Hivyo ndivyo tunavyowalipa madhalimu.

Kusema ‘basi huyo ndiye malipo yake’ ni kuzidisha ufafanuzi; sawa na kusema: malipo ya muuaji ni kuuliwa, hayo ndiyo malipo yake.

Ndugu wa Yusuf walisema hiyo ndiyo sharia yetu, ambaye mtamkuta nalo mtamchukua mtumwa au mateka. Walisema hivyo wakiwa na uhakika kuwa wao hawana hatia

Basi akaanza na mizigo yao kabla ya mzigo wa ndugu yake; kisha akalitoa katika mzigo wa ndugu yake.

Mtafutaji alianza na mizigo yao kabla ya ndugu yao madogo, ili kuificha hila. Mpaka alipoishia kwenye mzigo wa Bin-yamin akalitoa na akawaonyesha; wakapigwa na butwa na wakawa na wakati mgumu, lakini ni wapi haya na waliyomfanyia Yusuf katika giza la shimo akiwa peke yake?

Hivyo ndivyo tulivyomfanyia hila Yusuf.

Yaani tulimpa wahyi wa mpango huu, ili ndugu zake waseme wenyewe, kuwa waziri amchukue nyara au mtumwa. Imeitwa hila kwa sababu dhahiri yake sio hali halisi; na ilijuzu kisharia, kwa sababu haikuhalalisha haramu wala kuharamisha halali.

Hakuweza kumchukua ndugu yake katika sharia ya mfalme.

Yaani sharia na hukumu ya mfalme. Maana ni kuwa lau si mipango hii ingelikuwa uzito kwa Yusuf kumchukua ndugu yake, kwa sababu sharia ya mfalme wa Misr sio kuchukua mateka, bali ni kumfunga au kupigwa, na Yusuf hakutaka kumdhuru ndugu yake. Hayo ndio makusudio ya kauli yake:

Isipokuwa alivyotaka Mwenyezi Mungu.

Kwa ufupi ni kuwa hekima ilikuwa ni kutosema Yusuf kuwa yule ni ndugu yake na wakati huo huo asipatwe na sharia ya mfalme ya kufungwa au kupigwa; bali apatwe na hukumu ya watu wa Ya’qub.
Tunawatukuza kwenye vyeo tuwatakao Kwa elimu na utume kama tulivyomfanyia Yusuf juu ya ndugu zake.

Na juu ya kila mwenye elimu yuko ajuaye zaidi mpaka ishie kwa aliye juu zaidi.

Hiyo ni ishara kuwa ndugu wa Yusuf walikuwa ni maulama, lakini Yusuf alikuwa na elimu zaidi na mkamilifu zaidi.

قَالُوا إِنْ يَسْرِقْ فَقَدْ سَرَقَ أَخٌ لَهُ مِنْ قَبْلُ ۚ فَأَسَرَّهَا يُوسُفُ فِي نَفْسِهِ وَلَمْ يُبْدِهَا لَهُمْ ۚ قَالَ أَنْتُمْ شَرٌّ مَكَانًا ۖ وَاللَّهُ أَعْلَمُ بِمَا تَصِفُونَ {77}

Wakasema: “Kama ameiba, basi ndugu yake pia ameiba zamani.Yusuf aliyaweka siri moyoni mwake wala hakuwadhihirishia; akasema: “Nyinyi mko katika hali mbaya zaidi; na Mwenyezi Mungu anajua zaidi mnayoyasema.”

قَالُوا يَا أَيُّهَا الْعَزِيزُ إِنَّ لَهُ أَبًا شَيْخًا كَبِيرًا فَخُذْ أَحَدَنَا مَكَانَهُ ۖ إِنَّا نَرَاكَ مِنَ الْمُحْسِنِينَ {78}

Wakasema: “Ewe mheshimiwa! Hakika anaye baba mzee sana. Kwa hiyo mchukue mmoja wetu badala yake. Hakika sisi tunakuona wewe ni katika watu wema.”

قَالَ مَعَاذَ اللَّهِ أَنْ نَأْخُذَ إِلَّا مَنْ وَجَدْنَا مَتَاعَنَا عِنْدَهُ إِنَّا إِذًا لَظَالِمُونَ {79}

Akasema: “Mwenyezi Mungu apishe mbali kumchukua ila yule tuliyekuta mali yetu iko kwake. Hivyo basi tutakuwa ni wenye kudhulumu.”

فَلَمَّا اسْتَيْأَسُوا مِنْهُ خَلَصُوا نَجِيًّا ۖ قَالَ كَبِيرُهُمْ أَلَمْ تَعْلَمُوا أَنَّ أَبَاكُمْ قَدْ أَخَذَ عَلَيْكُمْ مَوْثِقًا مِنَ اللَّهِ وَمِنْ قَبْلُ مَا فَرَّطْتُمْ فِي يُوسُفَ ۖ فَلَنْ أَبْرَحَ الْأَرْضَ حَتَّىٰ يَأْذَنَ لِي أَبِي أَوْ يَحْكُمَ اللَّهُ لِي ۖ وَهُوَ خَيْرُ الْحَاكِمِينَ {80}

Walipokata tamaa naye walikwenda kando kunong’ona. Akasema mkubwa wao: “Je, hamjui kuwa baba yenu amechukua ahadi kwenu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Na hapo zamani mlikosea katika Yusuf? Basi sitaondoka nchi hii mpaka baba yangu aniruhusu au Mwenyezi Mungu anihukumie; naye ni mbora wa mahakimu.”