Aya 77-80: Kama Ameiba Basi Nduguye Pia Aliiba Zamani
Wakasema: “Kama ameiba, basi ndugu yake pia ameiba zamani.”
Ndugu zake Yusuf ndio waliosema hivyo, wakimkusudia Bin-yamin na Yusuf. Hizo ni tuhuma walizombadika nazo Yusuf. Hakuna ishara yoyote katika Aya yoyote kwamba Yusuf kuanzia utotoni aliwahi kuiba yai au kuku au kuiba sanamu ya babu yake mzaa mama yake, au mkanda wa shangazi yake n.k.
Lakini Qur’an imesajili waziwazi uwongo wa ndugu zake Yusuf, pale waliposema kuwa ameliwa na mbwa mwitu. Kuongezea hasadi na chuki yao iliyowapelekea kufanya waliyoyafanya. Kwa hiyo basi wao ni waongo katika kumnasibishia kwao Yusuf wizi alipokuwa mtoto.
Kusema hivi, ingawaje ni natija ya uchambuzi, lakini ndio mantiki ya sawa, au angalau ndio kauli ya karibu na maana.
Wafasiri wameichukulia kauli ya nduguze Yusuf kuwa ni ya kweli, kama kwamba uwongo unastahili. Wakawa wanafanya utafiti wa hicho alichokiiba Yusuf. Kuna aliyesema kuwa aliiba yai akampa mwenye njaa; mweingine akasema ni kuku.
Wa tatu akasema aliiba sanamu la babu yake mzaa mama yake na akalivunja. Wa nne akasema kuwa alikuwa akilelewa na shangazi yake, bint wa Is-haq, alipokuwa na baba yake, akataka kumchukua, kwa hiyo akamtuhumu kuiba mkanda wa mume wa shangazi yake ili abaki naye kama mtumwa; kwa vile adhabu ya mwizi ilikuwa ni kufanywa mtumwa.
Wafasiri wengi wako juu ya kauli hii ya mwisho. Lakini jambo la ajabu ni kuwa hakuna hata mmoja wao aliyezinduka kuwa hukumu ya watoto sio ya wakubwa katika sharia zote, Ajabu zaidi ni kauli ya baadhi ya Masufi kwamba ndugu zake Yusuf walimtuhumu na wizi wa kuiba roho ya baba yake!
Yusuf aliyaweka siri moyoni mwake wala hakuwadhihirishia.
Aliapuuza maneno yao kwa upole na ukarimu; kama asemavyo mshairi: Nampitia mlaumu akinitusi Namsamehe nasema hanihusi
Akasema: “Nyinyi mko katika hali mbaya zaidi.”
Haya aliyasema kisirisiri, kwa dalili ya kauli yake: “Wala hakuwadhihirishia.”
Na Mwenyezi Mungu anajua zaidi mnayoyasema ya kuninasibishia wizi mimi na ndugu yangu, kwamba ni uwongo na uzushi.
Wakasema: “Ewe mheshimiwa! Hakika anaye baba mzee sana. Kwa hiyo mchukue mmoja wetu badala yake. Hakika sisi tunakuona wewe ni katika watu wema.”
Baada ya mambo kudhihirika na kwamba hukumu ni kuchukuliwa mtumwa ndugu yao Bin-yamin, walielekea kutaka kuhurumiwa kwa kusamehewa au kuchukuliwa fidia ya mmoja wao badala yake. Walibembeleza sana kwa kutumia wema wa Yusuf na uzee wa baba yao na cheo chake na jinsi anavyompenda sana mwanawe Bin-yamin.
Walifanya hivyo sio kwa kumpenda ndugu yao, bali ni kujitoa kwenye lawama kutokana na ahadi waliyoichukua kwa baba yao.
Akasema: “Mwenyezi Mungu apishe mbali kumchukua ila yule tuliyekuta mali yetu iko kwake. Hivyo basi tutakuwa ni wenye kudhulumu.”
Yusuf alikataa ombi lao na matarajio yao na akashikilia kumchukua ndugu yake, kwa jambo ambalo Mwenyezi Mungu alitaka kulitimiza baada ya kupita mtihani na balaa.
Yusuf alitumia ibara ya ndani sana na yenye hekima ya kumwepusha ndugu yake na wizi, alposema: “Yule tuliyekuta mali yetu iko kwake” ambapo ndugu zake walifahamu: ‘aliyeiba mali yetu.’ Na tofauti hapo ni kubwa sana.
Walipokata tamaa naye walikwenda kando kunong’ona.
Baada ya kukata tamaa watoto wa Ya’qub ya kumpata ndugu yao walijitenga ili washauriane jinsi watakavyomwambia baba yao.
Akasema mkubwa wao: “Je, hamjui kuwa baba yenu amechukua ahadi kwenu kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Baadhi ya wafasiri wanasema kuwa makusudio ya mkubwa wao ni mkubwa kiakili si kimiaka. Wengine wakasema ni kiakili na kimiaka.
Kauli hii ndiyo inayokuja haraka akilini. Vyovyote iwavyo ni kwamba mkubwa huyo aliwaambia ndugu zake mtafanyaje mtakapofika kwa baba yenu bila ya Bin-yamin nanyi mliapa kuwa mtamrudisha?
Na hapo zamani mlikosea katika Yusuf?
Anaashiria walivyomtupa shimoni na baba yao alivyokuwa mkali.
“Basi sitaondoka nchi hii mpaka baba yangu aniruhusu au Mwenyezi
Mungu anihukumie; naye ni mbora wa mahakimu.”
Mkubwa wao aliamua abakie karibu na ndugu yake kwa kumwonea haya baba yake na kwamba hataondoka kwenye nchi aliyo Bin-yamin mpaka apewe idhini na baba yake au apate faraja yoyote, kutoka kwa Mwenyezi Mungui hata kama ni mauti. Muda haukuwa mrefu ikaja faraja kwa wote; kama yatakavyokuja maelezo.
ارْجِعُوا إِلَىٰ أَبِيكُمْ فَقُولُوا يَا أَبَانَا إِنَّ ابْنَكَ سَرَقَ وَمَا شَهِدْنَا إِلَّا بِمَا عَلِمْنَا وَمَا كُنَّا لِلْغَيْبِ حَافِظِينَ {81}
وَاسْأَلِ الْقَرْيَةَ الَّتِي كُنَّا فِيهَا وَالْعِيرَ الَّتِي أَقْبَلْنَا فِيهَا ۖ وَإِنَّا لَصَادِقُونَ {82}
قَالَ بَلْ سَوَّلَتْ لَكُمْ أَنْفُسُكُمْ أَمْرًا ۖ فَصَبْرٌ جَمِيلٌ ۖ عَسَى اللَّهُ أَنْ يَأْتِيَنِي بِهِمْ جَمِيعًا ۚ إِنَّهُ هُوَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ {83}
وَتَوَلَّىٰ عَنْهُمْ وَقَالَ يَا أَسَفَىٰ عَلَىٰ يُوسُفَ وَابْيَضَّتْ عَيْنَاهُ مِنَ الْحُزْنِ فَهُوَ كَظِيمٌ {84}
قَالُوا تَاللَّهِ تَفْتَأُ تَذْكُرُ يُوسُفَ حَتَّىٰ تَكُونَ حَرَضًا أَوْ تَكُونَ مِنَ الْهَالِكِينَ {85}
قَالَ إِنَّمَا أَشْكُو بَثِّي وَحُزْنِي إِلَى اللَّهِ وَأَعْلَمُ مِنَ اللَّهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ {86}
يَا بَنِيَّ اذْهَبُوا فَتَحَسَّسُوا مِنْ يُوسُفَ وَأَخِيهِ وَلَا تَيْأَسُوا مِنْ رَوْحِ اللَّهِ ۖ إِنَّهُ لَا يَيْأَسُ مِنْ رَوْحِ اللَّهِ إِلَّا الْقَوْمُ الْكَافِرُونَ {87}